Friday, 20 March 2015

Nini kimejificha kuhusu Muswada wa Sheria ya Habari?

Tunawaunga mkono wabunge waliojitokeza kupinga kuwasilishwa kwa hati ya dharura muswada wa Sheria ya Kupata Habari wa mwaka 2015.
Wakizungumza bungeni juzi, baadhi ya wabunge waliihoji Serikali sababu ya kuharakisha kuwasilisha muswada huo kwa ajili ya kupitishwa kama sheria.
Si wabunge pekee, wadau wa sekta ya habari wanajiuliza kuhusu uharaka wa muswada huo ambao kimsingi si suala la jana au juzi. Ni suala la muda mrefu ambalo wadau wa habari wamekuwa wakilipigania.
Ikiwa muswada huu utawasilishwa kwa njia ya hati ya dharura, ina maana utasomwa kwa mara ya kwanza na kupitishwa vipengele vyote kwa siku moja. Hii ina maana kuwa si wadau wa habari wala watunga sheria wetu, watakaopata muda wa kutosha wa kuupitia muswada na kujiridhisha kuwa una kila sababu ya kuwa sheria kwa maendeleo ya sekta ya habari na wanahabari.
Aidha, wadau wa habari kama wataalamu wa sekta hiyo, watakosa fursa ya kuwaelewesha wabunge masuala mbalimbali yaliyomo katika muswada, ili hata wanapoupitia wawe na weledi wa kutosha wa kitu wanachotaka kukipitisha kuwa sheria rasmi.
Mchakato mzima wa suala hili umegubikwa na usiri ambao sisi tukiwa wadau wa habari, unatupa wasiwasi na hata kujiuliza una maana gani? Nini kimejificha nyuma ya usiri huu?
Tumesema hapo awali hili si suala la jana wala juzi, tumekuwa tukilipigania kwa muda mrefu. Kwa nini taratibu za kawaida za uwasilishaji wa miswada zisifuatwe ili wadau wote wajiridhishe kuwa sheria itakayotungwa itakuwa na tija na maendeleo kwa sekta yenyewe, wanahabari na Taifa kwa jumla?
Kinachotokea sasa kuhusu haraka na usiri ulioligubika suala hili, wadau wa habari hasa wanahabari wanaweza kusukumwa kuamini kuwa kuna dhamira isiyo njema kwao.
Hofu hii ya wanahabari imeshaanza kujidhihirisha katika mjadala bungeni, baada ya baadhi ya wabunge kufikia hatua ya kuinyooshea kidole Serikali kuwa pengine ina dhamira ya kutaka kuvikandamiza vyombo vya habari kupitia muswada huo.
Hatutaki kuamini kuwa Serikali yetu sikivu na inayoongoza kwa misingi ya kidemokrasia, inaweza kutunga kwa makusudi sheria inayolenga kuvibana vyombo vya habari. Na kama itakuwa hivyo, tunauliza ni kwa masilahi ya nani?
Tunawakumbusha viongozi na watendaji serikalini kuwa Tanzania ni nchi yetu sote, hakuna mtu mwenye haki ya kujiona yeye ni Mtanzania zaidi kuliko wengine au mzalendo kuliko wengine.
Tunatoa tanbihi hii kwa kuwa umejengeka utamaduni wa viongozi serikalini na hata wanasiasa kufikiri kuwa wao ni weledi wa kila kitu kuhusu maendeleo na ustawi wa Taifa hili.
Watu hawa wachache siku zote wanalazimisha maoni, mitazamo na fikra zao vitamalaki hata katika mazingira ambayo umma mpana unaona siyo sahihi tena kwa kuegemea katika hoja zenye mashiko.
Matokeo ya utamaduni huu wa wachache kujiona ndiyo wenye uwezo wa kufikiria kwa niaba ya wengine, tuliyaona wakati wa mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba wakati wanasiasa walinyofoa mambo mengi yaliyopendekezwa na wananchi, wakapendekeza wanayoyataka wao. Mwishowe mchakato huo umegawanya nchi.
Na ndio maana tunasema muswada huu hauna udharura wowote, kwanini uwe siri? Urudishwe kwa wadau wauone ili kuzuia mgawanyiko mwingine.

Thursday, 12 March 2015

Kiswahili dhidi ya Kiingereza au Kiswahili pamoja na Kiingereza?

Suala la matumizi ya lugha Tanzania limeleta ushindani mzito kati ya Kiswahili na Kiingereza.
Hoja ya watetezi wa Kiingereza inajumuisha pia madai kuwa kuendelea kutumia Kiswahili, ni kuwafanya Watanzania washindwe kushindana kiuchumi katika dunia ya leo.
Dunia ya leo ni dunia ya utandawazi ambapo mipaka baina ya mataifa inapuuzwa na watu wanaweza kuwekeza, kuajiriwa na kufanya biashara karibu popote duniani.
Kwa sababu hiyo Kiingereza kinawafungulia milango katika dunia ya utandawazi. Lakini tusije kusahau watu wengi kutoka nchi nyingi wanakitumia Kiingereza kama lugha ya kibiashara na mawasiliano na watu ambao hawajui lugha yao ya kitaifa. Watu hawa wakiwa katika nchi zao wanatumia lugha zao za taifa.
Mifano ni pamoja na Wajerumani, Wajapani, Wafaransa, Waitalia, Wachina, Warusi na wengineo.
Ninavyoona mimi ni kwamba uzito wa hoja ya wale wanaopendekeza Kiingereza iwe lugha ya kufundishia Tanzania, unatokana na hoja ya umuhimu wa lugha hiyo katika uchumi wa viwanda.
Msingi wa lugha ni fikra zinazoelezwa katika maneno ambayo yanadhihirisha mkakati wa mpango fulani. Endapo mchakato wa mpango hauridhiki katika kasi ya mwenendo wake, lugha inaweza kurekebisha na kuongoza kutokana na msingi wa lugha husika kuwa desturi za wote wanaohusika ambao wamekipa kipaumbele matumizi yake.
Changamoto iliyopo katika maendeleo ya matumizi ya Kiswahili ni kuendeleza fikra za Watanzania. Fikra zitakazoeleza vitendo endelevu ambavyo vitasukuma mbele uchumi wa Tanzania na kuboresha maisha ya Watanzania.
Tukumbuke moja ya maneno maridhawa ya Mwalimu Julius Nyerere aliyeahi kuandika kitabu akakipa jina la “We Must Run While They Walk. Alimaanisha Tukimbie wakati wenzetu wakitembea.
Hoja yangu ni lugha ipi inawasukuma Watanzania kukimbia kati ya Kiswahili na Kiingereza? Jibu la kimsingi ni zote hizo mbili. Uchaguzi uliopo ni wa njia. Kila lugha husika ina njia inayoweza kutumika kufikia malengo ya matumizi yake kwa ufanisi. Lakini pia tujiulize kama njia hiyo inajenga maadili ya kudumu nchini Tanzania?
Nashauri iwe njia ya kufuata au njia ya kuongoza ambayo itajenga utaifa Tanzania. Kiswahili kikiwa lugha ya chimbuko la Utanzania kinaweza kuongoza.
Kiingereza ni lugha ya uvamizi wa ardhi ya Afrika, haina budi iwe ya lugha ya pili. Wasichoelewa watu wengi ni kuwa Kiingereza kinaweza kusaidia katika dunia ya utandawazi, lakini hakina uwezo wa kujenga Utanzania.
Msingi wa uthibitisho wa hoja yangu nautolea mfano nchini Uingereza. Kwa nini Mfalme Henry VIII alikifanya Kiingereza kuwa lugha rasmi ya Uingereza akiipinga lugha ya Kilatini iliyotumiwa na jamaa wa mfalme, watu wa tabaka ya juu, matajiri, wasomi na wataalamu?
Kiingereza kilikuwa lugha ya sokoni, lugha ya kina yakhe, Ilikuwa lugha ya kuongea na watumishi na wahudumu nyumbani.
Kiswahili hata katika taaluma kinawezekana na kwa mfano, hakuna haja ya kutafsiri istilahi za sayansi, tiba au hesabu. Tukumbuke hata Kiingereza bado kinatumia istilahi za Kilatini katika fani hizi.
Wataalamu Waingereza waliendelea kutumia Kilatini katika fani hizo hata baada ya mapinduzi ya kilugha Uingereza.
Aidha, sioni haja kwa mfano tutohoe neno pressure na kuita presha, ilhali tunaweza kusema shinikizo
Pete Mhunzi ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika na mpenzi wa Lugha ya Kiswahili

Mbatia aitupia lawama Serikali ajali ya Iringa

Dar es salaam. Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi taifa ,James Mbatia amesema kwamba  ajali  iliyotokea eneo la Mafinga Changalawe mkoani Iringa ilikuwa imepangwa na binadamu na wala sio mipango ya Mungu.
Akizungumza jijini leo Mbatia amesema ajali hiyo ilipangwa na watendaji wa serikali  kwa sababu ajali hiyo ilisababishwa na shimo kubwa ambalo limekaa kwa muda mrefu eneo hilo pasipo juhudi zozote za Serikali kulikarabati.
Mbatia amesema hawezi kukaa kimya ni lazima awasilishe suala hili  bungeni ili wahusika wachukuliwe hatua kwa kuacha shimo kubwa barabarani kwa muda mrefu bila kuliziba.
Amesema shimo hilo ambalo ndio hasa lilikuwa chanzo cha ajali hiyo ni la muda mrefu lakini viongozi wa serikali wanaliangalia tu bila kuchukua hatua ya kuliziba.
 ‘’Jamani  watanzania waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo ni wengi na  ni aibu kwa taifa, ukizingatia chanzo cha ajali hiyo ni shimo la muda mrefu ambalo linaangaliwa na viongozi wetu kila siku bila kuliziba’’alisema Mbatia
Amesema ajali hudokeza kwa ujumla matokeo mabaya ambayo labda yangeweza kuepukwa au kukingwa ikiwa matukio yaliyosababisha ajali hiyo yangetambuliwa na kurekebishwa kabla ya tukio.
Amesema madereva wanaoendesha magari ya abiria wanatakiwa kupelekwa shule angalau kwa miezi sita ikiwa ni pamoja na kupimwa afya mara kwa mara.
Aidha ameitaka serikali kutoa tamko kuhusu ajali hiyo na sio kukaa kimya mpaka waanze kupigiwa makelele na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Watu  zaidi ya 40  waliokuwa kwenye basi  la kampuni ya Majinjah Express lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam, walifariki papo hapo katika ajali hiyo iliyotokea jana wengine 23 wakijeruhiwa.

Wednesday, 11 March 2015

Waziri Samuel Sitta azuia mabehewa 124 akihofia ufisadi

Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amezuia uingizaji wa mabehewa 124 ya mizigo yaliyobaki katika zabuni iliyofanywa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), hadi pale uchunguzi wa tuhuma za ufisadi katika manunuzi hayo utakapokamilika.
Pamoja na hayo, Sitta alisema kuna hisia zimejitokeza kuwa huenda mabehewa hayo ni mitumba siyo mapya kama inavyodhaniwa.
Sitta aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa zabuni ilihusisha ununuzi wa mabehewa 274 na kwamba 150 tayari yalishaingia nchini, huku kukiwa na harufu ya ufisadi kuwa yalitengenezwa chini ya kiwango.
Mapema Aprili 2013, TRL iliipatia kampuni ya India iitwayo M/S Hindustan Engineering & Industrial Limited zabuni ya kutengenezea mabehewa ya mizigo kwa ajili ya Reli ya Kati. Serikali iliilipa kampuni hiyo Sh45.5 bilioni sawa na Sh166 milioni kwa kila behewa.
Hata hivyo, Sitta alisema kuwa Serikali ililipa asilimia 50 ya gharama zote za manunuzi na kwamba iwapo ikibainika udanganyifu wowote kampuni hiyo itawajibika.
“Nimekataza kabisa yale 124 yaliyobaki kule yasije. Nimeshawaagiza Reli kuwa yaliyopo kiwandani yanaendelea kutengenezwa au safarini hayaruhusiwi kuja kwa sasa mpaka tuweze kukwamua sakata hili.”
“Haiwezekani wakati tunachunguza 150 yaliyoingia tukayaruhusu yale 124 yaingie. Je, yakiwa na ubovu ule ule itakuwaje?” alihoji Sitta.
Alisema anaungana na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe kuwa mabehewa hayo ya mizigo yapo chini ya kiwango kutokana na kupinduka na kuacha reli mara kwa mara.
Alisema kiwango cha kuacha reli kwa mabehewa hayo siyo cha kawaida na ripoti ya Desemba mwaka jana ilionyesha kulikuwa na wastani wa upindukaji kila siku.
Kutokana na suala hilo kuwa kikwazo cha ufanisi kwa TRL, Sitta aliiagiza kamati ya uchunguzi wa sakata hilo (iliyoundwa na Dk Mwakyembe) kupitia Bodi ya Wakurugenzi ya TRL kukamilisha ripoti ifikapo Ijumaa wiki hii ili Serikali ijue la kufanya.
“Kuna mambo mengi tu ya kufanya kama kuvunja mkataba na mkandarasi, kumshtaki mhusika, kuangalia nani walienda kukagua na bado tukapata vibovu.
“Hii itatusaidia kujua hatua za kuchukua kiuwajibikaji kwa kuwa hivi sasa ni lazima mtu awajibike aidha kwa kufanya jambo kwa makusudi au kwa uzembe,”alisema Sitta. Alisema Idara ya Uhandisi katika wizara yake itasaidia kubaini nini kilitokea kiasi cha kuingiza nchini mabehewa yanayoleta hasara kubwa kwa taifa.
Kuhusu utendaji wa jumla wa TRL, Sitta alisema kwa sasa hali inaridhisha katika kampuni hiyo kiasi cha kuongeza mapato maradufu hadi kufikia Dola za Marekani 140 milioni (Sh252 bil) Desemba, 2014 kutoka Dola 38 milioni (Sh68.4 bil) Januari mwaka huo.
Alisema mabehewa mapya ya abiria yanatarajia kuanza kufanya kazi Aprili baada ya kukamilisha taratibu za Sumatra huku akibainisha kuwa hadi Julai mwaka huu watakuwa na vichwa 60 dhidi ya 107 vinavyohitajika.

Tuesday, 10 March 2015

Mtoto mwingine akatwa kiganja Sumbawanga

Sumbawanga. Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ‘albino’ Baraka Cosmas (6) anayeishi na wazazi wake kijijini Kipeta, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga ameshambuliwa na kujeruhiwa vibaya kwa kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana kisha kutokomea nacho kusikojulikana.
Tukio hilo limetokea wakati Serikali ikiwa katika mkakati kabambe wa kupambana na mauaji ya albino na ikiwa ni wiki chache tu tangu mtoto mwingine Yohana Bahati aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja kutekwa Februari 15, mwaka huu na kukutwa ameuawa katika eneo la Shilabela.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema tukio hilo la kikatili lilitokea saa saba usiku wa kuamkia juzi.
Alisema wakati hayo yakitokea baba mzazi wa mtoto huyo inadaiwa alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo.
Kamanda Mwaruanda alisema mtoto huyo amelazwa katika Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya kwa matibabu akiwa pamoja na mama mzazi.
Mwaruanda alisema, “Watu watatu majina yao yamehifadhiwa wanashikiliwa na polisi na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea ili kuwasaka wahusika na kiungo cha mtoto huyo.”
Mama mzazi Prisca Shaaban (28), alisema tukio hilo lilimkutana saa saba usiku, wakati akitaka kutoka nje kujisaidia.
“Nilikutana na mtu akifungua mlango, akanipiga ni kitu kichwani kisha nikazimia, nilipozinduka nikapiga kelele na majirani wakafika ndipo nilipogundua mtoto wangu amekatwa kiganja cha mkono wa kulia,” alisema mama mzazi.

Dk Slaa: Nalindwa na Mungu

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema analindwa na Mungu na ndiyo maana chama hicho kimegundua mpango wa mlinzi wake kushawishiwa na maofisa usalama wa taifa ili kumwekea sumu katika chakula au maji.
Mlinzi huyo (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay juzi, pia anadaiwa kutumiwa na kigogo mmoja wa CCM kuiba siri za chama hicho.
Tayari polisi imeanza kuchunguza taarifa hizo na jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura aliliambia gazeti hili kuwa mtuhumiwa huyo ana haki kama watuhumiwa wengine wanaofikishwa polisi wakikabiliwa na kesi za jinai na kusisitiza kuwa; “Tuhuma zinazomkabili ni za kawaida na tunazichunguza.”
Akieleza alivyopokea taarifa hizo Dk Slaa alisema, “Ninalindwa na Mungu ndivyo ninavyoweza kusema. Chadema sisi huwa tunaanza na Mungu na kumaliza na Mungu. Ushahidi umewekwa wazi na hili ni jambo la kweli na limenigusa kwa kiasi kikubwa.”
Alisema baadhi ya mambo yaliyofanywa na mlinzi wake ameyaona kwa macho na kusisitiza kuwa njama zinazofanywa na wanaomtumia haziwezi kukiondoa chama hicho katika harakati zake za kila siku.
“Tupo makini ndiyo maana tumebaini yote. Tunawajua waliohusika na tupo makini katika kuwafuatilia. Kama Mungu yupo upande wetu tumuogope nani zaidi,” alisema.
Alisema Chadema ina safari ndefu hivyo ni lazima wana-Chadema kuvaa viatu ili kujikinga na vumbi na uchafu wa kila aina, akimaanisha kuwa chama hicho kinakumbana na vikwazo vingi.
Tuhuma dhidi ya mlinzi huyo zilitolewa juzi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando kuwa wamebaini nyendo za mlinzi huyo na kuzifuatilia kwa ukaribu hadi kupata taarifa hizo alizosema ni ukweli mtupu.
Hili ni tukio la tatu kwa Chadema kudai kuna mipango ya kumfuatilia Dk Slaa, mara ya kwanza ilikuwa Februari 2009 alipobaini kutegewa vinasa sauti hotelini mkoani Dodoma na mkakati uliotajwa kuwa wa kuwaua yeye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Akieleza jinsi walivyombaini mlinzi huyo, Marando alisema pamoja na ushahidi wa mawasiliano ya simu, lakini pia mlinzi huyo alikiri kwa kinywa chake kutumiwa na maofisa hao ambao hakuwataja majina lakini alisema wako 22.
“Mlinzi alitueleza kwamba alikuwa akipewa fedha kwa ajili ya kutoa siri za vikao vya chama kupitia simu yake…kwa kuwa anaruhusiwa kuingia kwenye vikao vya chama hicho kama mlinzi amekuwa akitegesha simu yake ili kuwapa taarifa watu wa CCM `live’ ili wasikie kila kinachojadiliwa,” alidai Marando.
Marando aliyewahi kuwa ofisa wa usalama wa taifa na kuongeza kuwa wako mbioni kufikisha suala hilo polisi.
Mipango yenyewe
Akifafanua namna mipango hiyo ilivyofanywa, Marando alidai walibaini mlinzi huyo kutumiwa muda wa maongezi kwa nyakati tofauti wa jumla ya Sh7 milioni kwenye simu zake.
Marando alisema, “Kilichokuwa kinatokea ni kwamba kigogo wa CCM (anamtaja) na wenzake walikuwa wanasikia kila kinachozungumzwa kutoka kwenye vikao vya ndani vya Chadema kwa sababu ya mlinzi huyo.”
Kigogo huyo wa CCM hakupatikana juzi na jana kujibu tuhuma dhidi yake, lakini ofisa mmoja wa makao makuu alisema taarifa hizo zimewafikia na zitajibiwa kwa njia rasmi.
Kadhalika, Marando alisema walibaini kuwa mlinzi huyo amekuwa akizungumza kwa simu kwa saa mbili hadi tatu na maofisa usalama hao ili kuwapa taarifa mbalimbali za chama.
Marando alisema kwa miaka miwili mfululizo mlinzi huyo amekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na ofisa mmoja usalama wilayani Kinondoni ambaye ana uhusiano wa karibu na kigogo huyo wa CCM.

Wakulima wa kahawa kunufaika


Dar es Salaam. Wakulima wa kahawa nchini wataendelea kunufaika na zao hilo baada ya kuanzishwa kwa viwanda vya usindikaji.
Mkurugenzi Mtendaji Kampuni ya Chai Bora Kapila Ariyatilaka alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa bidhaa zitokanazo na kahawa.
Alisema wameingiza bidhaa mpya sokoni zitakazopanua wigo wa soko la kahawa na kuwanufaisha zaidi wakulima.
“Tumekuja kupanua wigo wa soko la kahawa, tuna mahitaji ya wastani wa tani 500 kwa mwezi, kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa zetu hususan ile ya Cafe Bora,” alisema na kuongeza:
“Lengo la kampuni ni kutosheleza mahitaji ya ndani pamoja na nchi za Afrika Mashariki.
Ariyatilaka alisema wakulima wa nyanya, pilipili na bidhaa nyingine pia wana fursa nzuri ya soko baada ya kampuni hiyo kuingia makubaliano ya kibiashara na Kampuni ya Dabaga iliyopo Iringa.
“Tunaangalia zaidi fursa ya masoko kwa bidhaa za mashambani kutokana na changamoto zinazowakabili wakulima, ndiyo maana tunashirikiana na Dabaga,” alisema.
Alisema iwapo bidhaa za Dabaga zitauzwa zaidi, mahitaji yataongezeka kwa wakulima wa nyanya Iringa na kwingineko.
“Tutakuwa tumewawezesha wakulima kuongeza kipato na pia Serikali itapata kodi zaidi kutokana na mauzo ,” alisema
Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Kampuni ya Chai Bora, Martin Ng’ethe alisema Tanzania inajivunia kuwa na aina zote za kahawa.
Alizitaja kuwa ni Arabika na Robusta tofauti na nchi nyingine zenye aina mmoja ya kahawa.

Zitto Kabwe avuliwa rasmi uanachama Chadema

Baada ya Mahakama Kuu Tanzania kanda ya Dar es Salaam leo kutupilia mbali kesi iliyokuwa imefunguliwa na Zito Kabwe dhidi ya Chama Cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) ya kuhoji uhalali wa uanachama wake ndani ya chama hicho…
Habari zilizotufikia hivi punde zinaeleza kuwa Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo Tundu Lissu ametangaza kuvuliwa rasmi uanachama wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe.
Akitangaza hatua hiyo ya kumvua uanachama,Lissu amesema kanuni na sharia za chama hicho ziko wazi na zinaelekeza kuwa endapo mwanachama yeyote atakishtaki chama hicho mahakamani na iwapo atashindwa atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye chama

Friday, 6 March 2015

Viongozi kujiuzulu pekee haitoshi

Jana Profesa Sosperter Muhongo alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Nishati na Madini, akieleza kuwa anataka nchi isonge mbele kwa kuwa suala la kumtaka Rais amwondoe kutokana na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, limesababisha mambo mengi kukwama.
Profesa Muhongo amekuwa waziri wa pili kuondoka baada ya Profesa Anna Tibaijuka kuvuliwa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na kuingiziwa kwenye akaunti yake Sh1.6 bilioni na mmiliki wa zamani wa IPTL, fedha ambazo zinahusishwa na sakata la escrow.
Mbali na mawaziri hao, tayari Jaji Fredrick Werema amejiuzulu kazi yake ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akieleza kuwa ushauri wake kuhusu fedha za escrow haukueleweka na kusababisha tafrani.
Pia, katibu mkuu wa wizara hiyo, Eliackim Maswi amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa sakata hilo, wakati watumishi watano wa Tanesco, Benki Kuu (BoT) na Mamlaka ya Mapato (TRA) wamefikishwa mahakamani wakishtakiwa kwa kupokea rushwa inayohusu sakata hilo. Kashfa hii ni moja ya matukio mengi makubwa yaliyosababisha Rais kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri. Baadhi ya matukio hayo ni kashfa ya Richmond, CAG na Operesheni Tokomeza ambazo zilisababisha Rais kupangua baraza lake.
Ni jambo la kupongeza kwamba angalau hatua zimechukuliwa kwa kiwango fulani katika kushughulikia tatizo hilo lililohusu uchotwaji wa takriban Sh306 bilioni kutoka kwenye akaunti hiyo iliyokuwa BoT.
Kitu cha ajabu ni hii tabia inayoendelea kujengeka ya kuibuka kwa kashfa, mawaziri kujiuzulu, kuundwa kwa baraza jipya na baadaye mambo kuendelea kama kawaida kusubiri kashfa nyingine kuibuka bila ya hatu za dhati kuchukuliwa kudhibiti matukio kama hayo.
Jambo la ajabu ni kwamba kila kashfa inapoibuka, hutumika nguvu nyingi kuizua au kutetea viongozi wa Serikali hadi mambo yanapoonekana kuwa yamekuwa makubwa ndipo hatua zichukuliwe.
Tumeona katika kashfa ya escrow zilitumika nguvu nyingi kutetea wahusika hadi maji yalipozidi unga ndipo hatua zilipochukuliwa na kushughulikia wahusika. Kitu kibaya ni kwamba hadi wakati hatua zinaanza kuchukuliwa, tayari Serikali inakuwa imeshafuka na wananchi wameshaumia.
Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri sasa yamekuwa ya kawaida kwa kuwa kila yanapofanyika hazichukuliwi hatua thabiti kuzuia kashfa zisitokee. Suala la fedha kuchotwa kwa fedha zinazokuwa BoT sasa linaonekana kuwa la kawaida kwa kuwa kashfa ya Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje lilipotokea, hakukuchukuliwa hatua madhubuti kuziba mianya kama hiyo kwenye taasisi hiyo nyeti ya fedha.
Tunadhani ni wakati mwafaka sasa kwa Serikali kuweka misingi imara ya uongozi itakayowabana viongozi wetu kujiingiza kwenye kashfa kama hizo. Misingi hiyo pia ihusishe hatua kali ambazo zinaweza kuchukuliwa kwa viongozi ambao wataingia kwenye kashfa hizo kwa makusudi au uzembe ili kuzuia wengine kufanya mambo ya aibu na yanayoumiza wananchi.
Pia, siyo ufahari kuwawajibisha viongozi wakati ufisadi umeshafanyika kama ilivyokuwa kwenye sakata la EPA na sasa escrow kwa kuwa fedha za walipa kodi zinakuwa zimeshachotwa. Ufisadi unatakiwa uzuiwe mapema kuliepusha Taifa kupoteza mabilioni ya fedha na wanaowajibishwa wachukuliwe hatua kwa kujaribu kula njama za ufisadi na siyo kuadhibiwa kwa kufanya ufisadi.
Kadri Serikali inavyoonekana kuweka mikakati ya kuwakingia kifua watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, ndivyo vitendo hivyo vinavyozidi. Serikali inatakiwa ionyeshe kuchukia ufisadi kwanzaNa ikichukia ufisadi, basi kujiuzulu wa kuwavua madaraka wahusika kutakuwa ni moja ya hatua za kuwashughulikia wahusika wote nah ii itasaidia kupunguza vitendo hivyo..

Magufuli: Mbowe kama malaika

Hai. Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli jana aliungana na viongozi wenzake wa Serikali kuwamwagia sifa viongozi wa vyama vya upinzani baada ya kumwelezea Mbunge wa Hai na Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe kuwa ni mpigania maendeleo ya wananchi na kwamba alitakiwa awe malaika.
Dk Magufuli alimuelezea kiongozi huyo wa upinzani bungeni kuwa ni mtu ambaye anafuatilia maendeleo ya watu bila ya kujali itikadi zao.
Waziri huyo ameungana na Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kusifu utendaji wa viongozi wa upinzani.
Februari 10, Rais Kikwete alisifu utendaji wa meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael wa kuwaletea maendeleo wananchi, na siku 12 baadaye Waziri Pinda alimsifu mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kwa kuwa kiongozi wa kwanza kuchangia vitanda 30 kwenye Hospitali ya Frelimo.
Jana, Dk Magufuli alimmwagia Mbowe sifa hizo katika mkutano wa hadhara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Kwasadala-Masama-Machame katika Jimbo la Hai inayojengwa kwa kiwango cha lami.
“(Mbowe)Unadhihirisha kwamba maendeleo hayana chama na kwa kweli tukienda hivi Tanzania itakuwa ni nchi ya kutolewa mfano. Sincerely (kwa dhati) nakupongeza Mbowe na Mungu akubariki,” alisema.
Kabla ya Dk Magufuli kutoa pongezi hizo, Mbowe aliwataka wanasiasa kutekeleza ahadi zao kwa vitendo kwa kuwa maendeleo hayana itikadi.
“Mimi naamini maendeleo hayana itikadi. Jambo jema likifanywa na chama chochote cha siasa ama kiongozi wa chama chochote au Mtanzania, kama ni jema anastahili kupongezwa,” alisema Mbowe.
“Hakuna aibu ya kukiri pale jambo jema linapofanyika. Ujenzi wa Barabara ya Kwasadala-Mula-Machame ni jambo jema,” alisisitiza Mbowe.
Hata hivyo, alitumia mkutano huo wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Masama kumuomba Dk Magufuli atoe maagizo ya kiserikali baada ya viongozi wawili wa CCM kutishia kuchoma moto greda lake.
“Nimenunua greda ili tusaidiane na Serikali, lakini juzi diwani na mwenyekiti wa kijiji walitishia kuchoma moto greda eti kwa sababu mbunge hajapewa kibali cha kuchimba barabara,” alilalamika.
Mbowe alisema vyama vya siasa ni lazima vifanye pamoja kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Akihutubia mkutano huo, Dk Magufuli alisema Mbowe ni kiongozi mpole na mstaarabu na ndiyo maana kila ombi lake analoliwasilisha serikalini kwa ajili ya wananchi wake haligongi mwamba.
“Utapata wapi mtu mpole kama huyu? Alimuomba Rais pale kwamba niongezee kilometa tatu, (Rais) akatoa siku ile ile,” alisema.
“Rais Kikwete ni mwenyekiti wa CCM, lakini ameleta barabara hapa kwa mwenyekiti wa Chadema. Huo ndiyo utanzania na haya ndiyo tunatakiwa viongozi tuige mfano.”
Waziri Dk Magufuli alisema Mbowe ni miongoni mwa wabunge wachache wa upinzani ambao hawamsumbui bungeni na anapokuwa na jambo, huwa wanatoka nje na kuteta.
“Wako wengine wanapigaga kelele, lakini wewe unakuja tunazungumza. Unasema ndugu yangu, brother (kaka). Mbowe weweee! Ulitakiwa uwe malaika,” alisema Dk Magufuli katika mkutano huo.
Hata hivyo, Dk Magufuli aligeukia siasa na kusema ustaarabu na upole alio nao Mbowe unatokana na malezi mazuri ya CCM kwa vile wazazi wake walikuwa wana-CCM na kwamba pongezi anazitoa kwa dhati. Alimpongeza Mbowe kwa kununua greda, akisema fedha hizo angeweza kuzitumia kwa shughuli nyingine lakini akaamua kulinunua ili kusaidia wananchi wak