Sumbawanga. Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ‘albino’ Baraka Cosmas
(6) anayeishi na wazazi wake kijijini Kipeta, Bonde la Ziwa Rukwa
wilayani Sumbawanga ameshambuliwa na kujeruhiwa vibaya kwa kukatwa
kiganja cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana kisha kutokomea
nacho kusikojulikana.
Tukio hilo limetokea wakati Serikali ikiwa katika
mkakati kabambe wa kupambana na mauaji ya albino na ikiwa ni wiki chache
tu tangu mtoto mwingine Yohana Bahati aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja
kutekwa Februari 15, mwaka huu na kukutwa ameuawa katika eneo la
Shilabela.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema tukio hilo la kikatili lilitokea saa saba usiku wa kuamkia juzi.
Alisema wakati hayo yakitokea baba mzazi wa mtoto huyo inadaiwa alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo.
Kamanda Mwaruanda alisema mtoto huyo amelazwa
katika Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya kwa
matibabu akiwa pamoja na mama mzazi.
Mwaruanda alisema, “Watu watatu majina yao
yamehifadhiwa wanashikiliwa na polisi na uchunguzi zaidi kuhusiana na
tukio hilo unaendelea ili kuwasaka wahusika na kiungo cha mtoto huyo.”
Mama mzazi Prisca Shaaban (28), alisema tukio hilo lilimkutana saa saba usiku, wakati akitaka kutoka nje kujisaidia.
“Nilikutana na mtu akifungua mlango, akanipiga ni
kitu kichwani kisha nikazimia, nilipozinduka nikapiga kelele na majirani
wakafika ndipo nilipogundua mtoto wangu amekatwa kiganja cha mkono wa
kulia,” alisema mama mzazi.

No comments:
Post a Comment