Suala la matumizi ya lugha Tanzania limeleta ushindani mzito kati ya Kiswahili na Kiingereza.
Hoja ya watetezi wa Kiingereza inajumuisha pia
madai kuwa kuendelea kutumia Kiswahili, ni kuwafanya Watanzania
washindwe kushindana kiuchumi katika dunia ya leo.
Dunia ya leo ni dunia ya utandawazi ambapo mipaka
baina ya mataifa inapuuzwa na watu wanaweza kuwekeza, kuajiriwa na
kufanya biashara karibu popote duniani.
Kwa sababu hiyo Kiingereza kinawafungulia milango
katika dunia ya utandawazi. Lakini tusije kusahau watu wengi kutoka nchi
nyingi wanakitumia Kiingereza kama lugha ya kibiashara na mawasiliano
na watu ambao hawajui lugha yao ya kitaifa. Watu hawa wakiwa katika nchi
zao wanatumia lugha zao za taifa.
Mifano ni pamoja na Wajerumani, Wajapani, Wafaransa, Waitalia, Wachina, Warusi na wengineo.
Ninavyoona mimi ni kwamba uzito wa hoja ya wale
wanaopendekeza Kiingereza iwe lugha ya kufundishia Tanzania, unatokana
na hoja ya umuhimu wa lugha hiyo katika uchumi wa viwanda.
Msingi wa lugha ni fikra zinazoelezwa katika
maneno ambayo yanadhihirisha mkakati wa mpango fulani. Endapo mchakato
wa mpango hauridhiki katika kasi ya mwenendo wake, lugha inaweza
kurekebisha na kuongoza kutokana na msingi wa lugha husika kuwa desturi
za wote wanaohusika ambao wamekipa kipaumbele matumizi yake.
Changamoto iliyopo katika maendeleo ya matumizi ya
Kiswahili ni kuendeleza fikra za Watanzania. Fikra zitakazoeleza
vitendo endelevu ambavyo vitasukuma mbele uchumi wa Tanzania na
kuboresha maisha ya Watanzania.
Tukumbuke moja ya maneno maridhawa ya Mwalimu
Julius Nyerere aliyeahi kuandika kitabu akakipa jina la “We Must Run
While They Walk. Alimaanisha Tukimbie wakati wenzetu wakitembea.
Hoja yangu ni lugha ipi inawasukuma Watanzania
kukimbia kati ya Kiswahili na Kiingereza? Jibu la kimsingi ni zote hizo
mbili. Uchaguzi uliopo ni wa njia. Kila lugha husika ina njia inayoweza
kutumika kufikia malengo ya matumizi yake kwa ufanisi. Lakini pia
tujiulize kama njia hiyo inajenga maadili ya kudumu nchini Tanzania?
Nashauri iwe njia ya kufuata au njia ya kuongoza
ambayo itajenga utaifa Tanzania. Kiswahili kikiwa lugha ya chimbuko la
Utanzania kinaweza kuongoza.
Kiingereza ni lugha ya uvamizi wa ardhi ya Afrika,
haina budi iwe ya lugha ya pili. Wasichoelewa watu wengi ni kuwa
Kiingereza kinaweza kusaidia katika dunia ya utandawazi, lakini hakina
uwezo wa kujenga Utanzania.
Msingi wa uthibitisho wa hoja yangu nautolea mfano nchini
Uingereza. Kwa nini Mfalme Henry VIII alikifanya Kiingereza kuwa lugha
rasmi ya Uingereza akiipinga lugha ya Kilatini iliyotumiwa na jamaa wa
mfalme, watu wa tabaka ya juu, matajiri, wasomi na wataalamu?
Kiingereza kilikuwa lugha ya sokoni, lugha ya kina yakhe, Ilikuwa lugha ya kuongea na watumishi na wahudumu nyumbani.
Kiswahili hata katika taaluma kinawezekana na kwa
mfano, hakuna haja ya kutafsiri istilahi za sayansi, tiba au hesabu.
Tukumbuke hata Kiingereza bado kinatumia istilahi za Kilatini katika
fani hizi.
Wataalamu Waingereza waliendelea kutumia Kilatini katika fani hizo hata baada ya mapinduzi ya kilugha Uingereza.
Aidha, sioni haja kwa mfano tutohoe neno pressure na kuita presha, ilhali tunaweza kusema shinikizo
Pete Mhunzi ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika na mpenzi wa Lugha ya Kiswahili

No comments:
Post a Comment