Wednesday, 11 March 2015

Waziri Samuel Sitta azuia mabehewa 124 akihofia ufisadi

Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amezuia uingizaji wa mabehewa 124 ya mizigo yaliyobaki katika zabuni iliyofanywa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), hadi pale uchunguzi wa tuhuma za ufisadi katika manunuzi hayo utakapokamilika.
Pamoja na hayo, Sitta alisema kuna hisia zimejitokeza kuwa huenda mabehewa hayo ni mitumba siyo mapya kama inavyodhaniwa.
Sitta aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa zabuni ilihusisha ununuzi wa mabehewa 274 na kwamba 150 tayari yalishaingia nchini, huku kukiwa na harufu ya ufisadi kuwa yalitengenezwa chini ya kiwango.
Mapema Aprili 2013, TRL iliipatia kampuni ya India iitwayo M/S Hindustan Engineering & Industrial Limited zabuni ya kutengenezea mabehewa ya mizigo kwa ajili ya Reli ya Kati. Serikali iliilipa kampuni hiyo Sh45.5 bilioni sawa na Sh166 milioni kwa kila behewa.
Hata hivyo, Sitta alisema kuwa Serikali ililipa asilimia 50 ya gharama zote za manunuzi na kwamba iwapo ikibainika udanganyifu wowote kampuni hiyo itawajibika.
“Nimekataza kabisa yale 124 yaliyobaki kule yasije. Nimeshawaagiza Reli kuwa yaliyopo kiwandani yanaendelea kutengenezwa au safarini hayaruhusiwi kuja kwa sasa mpaka tuweze kukwamua sakata hili.”
“Haiwezekani wakati tunachunguza 150 yaliyoingia tukayaruhusu yale 124 yaingie. Je, yakiwa na ubovu ule ule itakuwaje?” alihoji Sitta.
Alisema anaungana na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe kuwa mabehewa hayo ya mizigo yapo chini ya kiwango kutokana na kupinduka na kuacha reli mara kwa mara.
Alisema kiwango cha kuacha reli kwa mabehewa hayo siyo cha kawaida na ripoti ya Desemba mwaka jana ilionyesha kulikuwa na wastani wa upindukaji kila siku.
Kutokana na suala hilo kuwa kikwazo cha ufanisi kwa TRL, Sitta aliiagiza kamati ya uchunguzi wa sakata hilo (iliyoundwa na Dk Mwakyembe) kupitia Bodi ya Wakurugenzi ya TRL kukamilisha ripoti ifikapo Ijumaa wiki hii ili Serikali ijue la kufanya.
“Kuna mambo mengi tu ya kufanya kama kuvunja mkataba na mkandarasi, kumshtaki mhusika, kuangalia nani walienda kukagua na bado tukapata vibovu.
“Hii itatusaidia kujua hatua za kuchukua kiuwajibikaji kwa kuwa hivi sasa ni lazima mtu awajibike aidha kwa kufanya jambo kwa makusudi au kwa uzembe,”alisema Sitta. Alisema Idara ya Uhandisi katika wizara yake itasaidia kubaini nini kilitokea kiasi cha kuingiza nchini mabehewa yanayoleta hasara kubwa kwa taifa.
Kuhusu utendaji wa jumla wa TRL, Sitta alisema kwa sasa hali inaridhisha katika kampuni hiyo kiasi cha kuongeza mapato maradufu hadi kufikia Dola za Marekani 140 milioni (Sh252 bil) Desemba, 2014 kutoka Dola 38 milioni (Sh68.4 bil) Januari mwaka huo.
Alisema mabehewa mapya ya abiria yanatarajia kuanza kufanya kazi Aprili baada ya kukamilisha taratibu za Sumatra huku akibainisha kuwa hadi Julai mwaka huu watakuwa na vichwa 60 dhidi ya 107 vinavyohitajika.

Tuesday, 10 March 2015

Mtoto mwingine akatwa kiganja Sumbawanga

Sumbawanga. Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ‘albino’ Baraka Cosmas (6) anayeishi na wazazi wake kijijini Kipeta, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga ameshambuliwa na kujeruhiwa vibaya kwa kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana kisha kutokomea nacho kusikojulikana.
Tukio hilo limetokea wakati Serikali ikiwa katika mkakati kabambe wa kupambana na mauaji ya albino na ikiwa ni wiki chache tu tangu mtoto mwingine Yohana Bahati aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja kutekwa Februari 15, mwaka huu na kukutwa ameuawa katika eneo la Shilabela.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema tukio hilo la kikatili lilitokea saa saba usiku wa kuamkia juzi.
Alisema wakati hayo yakitokea baba mzazi wa mtoto huyo inadaiwa alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo.
Kamanda Mwaruanda alisema mtoto huyo amelazwa katika Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya kwa matibabu akiwa pamoja na mama mzazi.
Mwaruanda alisema, “Watu watatu majina yao yamehifadhiwa wanashikiliwa na polisi na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea ili kuwasaka wahusika na kiungo cha mtoto huyo.”
Mama mzazi Prisca Shaaban (28), alisema tukio hilo lilimkutana saa saba usiku, wakati akitaka kutoka nje kujisaidia.
“Nilikutana na mtu akifungua mlango, akanipiga ni kitu kichwani kisha nikazimia, nilipozinduka nikapiga kelele na majirani wakafika ndipo nilipogundua mtoto wangu amekatwa kiganja cha mkono wa kulia,” alisema mama mzazi.

Dk Slaa: Nalindwa na Mungu

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema analindwa na Mungu na ndiyo maana chama hicho kimegundua mpango wa mlinzi wake kushawishiwa na maofisa usalama wa taifa ili kumwekea sumu katika chakula au maji.
Mlinzi huyo (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay juzi, pia anadaiwa kutumiwa na kigogo mmoja wa CCM kuiba siri za chama hicho.
Tayari polisi imeanza kuchunguza taarifa hizo na jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura aliliambia gazeti hili kuwa mtuhumiwa huyo ana haki kama watuhumiwa wengine wanaofikishwa polisi wakikabiliwa na kesi za jinai na kusisitiza kuwa; “Tuhuma zinazomkabili ni za kawaida na tunazichunguza.”
Akieleza alivyopokea taarifa hizo Dk Slaa alisema, “Ninalindwa na Mungu ndivyo ninavyoweza kusema. Chadema sisi huwa tunaanza na Mungu na kumaliza na Mungu. Ushahidi umewekwa wazi na hili ni jambo la kweli na limenigusa kwa kiasi kikubwa.”
Alisema baadhi ya mambo yaliyofanywa na mlinzi wake ameyaona kwa macho na kusisitiza kuwa njama zinazofanywa na wanaomtumia haziwezi kukiondoa chama hicho katika harakati zake za kila siku.
“Tupo makini ndiyo maana tumebaini yote. Tunawajua waliohusika na tupo makini katika kuwafuatilia. Kama Mungu yupo upande wetu tumuogope nani zaidi,” alisema.
Alisema Chadema ina safari ndefu hivyo ni lazima wana-Chadema kuvaa viatu ili kujikinga na vumbi na uchafu wa kila aina, akimaanisha kuwa chama hicho kinakumbana na vikwazo vingi.
Tuhuma dhidi ya mlinzi huyo zilitolewa juzi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando kuwa wamebaini nyendo za mlinzi huyo na kuzifuatilia kwa ukaribu hadi kupata taarifa hizo alizosema ni ukweli mtupu.
Hili ni tukio la tatu kwa Chadema kudai kuna mipango ya kumfuatilia Dk Slaa, mara ya kwanza ilikuwa Februari 2009 alipobaini kutegewa vinasa sauti hotelini mkoani Dodoma na mkakati uliotajwa kuwa wa kuwaua yeye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Akieleza jinsi walivyombaini mlinzi huyo, Marando alisema pamoja na ushahidi wa mawasiliano ya simu, lakini pia mlinzi huyo alikiri kwa kinywa chake kutumiwa na maofisa hao ambao hakuwataja majina lakini alisema wako 22.
“Mlinzi alitueleza kwamba alikuwa akipewa fedha kwa ajili ya kutoa siri za vikao vya chama kupitia simu yake…kwa kuwa anaruhusiwa kuingia kwenye vikao vya chama hicho kama mlinzi amekuwa akitegesha simu yake ili kuwapa taarifa watu wa CCM `live’ ili wasikie kila kinachojadiliwa,” alidai Marando.
Marando aliyewahi kuwa ofisa wa usalama wa taifa na kuongeza kuwa wako mbioni kufikisha suala hilo polisi.
Mipango yenyewe
Akifafanua namna mipango hiyo ilivyofanywa, Marando alidai walibaini mlinzi huyo kutumiwa muda wa maongezi kwa nyakati tofauti wa jumla ya Sh7 milioni kwenye simu zake.
Marando alisema, “Kilichokuwa kinatokea ni kwamba kigogo wa CCM (anamtaja) na wenzake walikuwa wanasikia kila kinachozungumzwa kutoka kwenye vikao vya ndani vya Chadema kwa sababu ya mlinzi huyo.”
Kigogo huyo wa CCM hakupatikana juzi na jana kujibu tuhuma dhidi yake, lakini ofisa mmoja wa makao makuu alisema taarifa hizo zimewafikia na zitajibiwa kwa njia rasmi.
Kadhalika, Marando alisema walibaini kuwa mlinzi huyo amekuwa akizungumza kwa simu kwa saa mbili hadi tatu na maofisa usalama hao ili kuwapa taarifa mbalimbali za chama.
Marando alisema kwa miaka miwili mfululizo mlinzi huyo amekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na ofisa mmoja usalama wilayani Kinondoni ambaye ana uhusiano wa karibu na kigogo huyo wa CCM.

Wakulima wa kahawa kunufaika


Dar es Salaam. Wakulima wa kahawa nchini wataendelea kunufaika na zao hilo baada ya kuanzishwa kwa viwanda vya usindikaji.
Mkurugenzi Mtendaji Kampuni ya Chai Bora Kapila Ariyatilaka alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa bidhaa zitokanazo na kahawa.
Alisema wameingiza bidhaa mpya sokoni zitakazopanua wigo wa soko la kahawa na kuwanufaisha zaidi wakulima.
“Tumekuja kupanua wigo wa soko la kahawa, tuna mahitaji ya wastani wa tani 500 kwa mwezi, kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa zetu hususan ile ya Cafe Bora,” alisema na kuongeza:
“Lengo la kampuni ni kutosheleza mahitaji ya ndani pamoja na nchi za Afrika Mashariki.
Ariyatilaka alisema wakulima wa nyanya, pilipili na bidhaa nyingine pia wana fursa nzuri ya soko baada ya kampuni hiyo kuingia makubaliano ya kibiashara na Kampuni ya Dabaga iliyopo Iringa.
“Tunaangalia zaidi fursa ya masoko kwa bidhaa za mashambani kutokana na changamoto zinazowakabili wakulima, ndiyo maana tunashirikiana na Dabaga,” alisema.
Alisema iwapo bidhaa za Dabaga zitauzwa zaidi, mahitaji yataongezeka kwa wakulima wa nyanya Iringa na kwingineko.
“Tutakuwa tumewawezesha wakulima kuongeza kipato na pia Serikali itapata kodi zaidi kutokana na mauzo ,” alisema
Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Kampuni ya Chai Bora, Martin Ng’ethe alisema Tanzania inajivunia kuwa na aina zote za kahawa.
Alizitaja kuwa ni Arabika na Robusta tofauti na nchi nyingine zenye aina mmoja ya kahawa.

Zitto Kabwe avuliwa rasmi uanachama Chadema

Baada ya Mahakama Kuu Tanzania kanda ya Dar es Salaam leo kutupilia mbali kesi iliyokuwa imefunguliwa na Zito Kabwe dhidi ya Chama Cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) ya kuhoji uhalali wa uanachama wake ndani ya chama hicho…
Habari zilizotufikia hivi punde zinaeleza kuwa Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo Tundu Lissu ametangaza kuvuliwa rasmi uanachama wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe.
Akitangaza hatua hiyo ya kumvua uanachama,Lissu amesema kanuni na sharia za chama hicho ziko wazi na zinaelekeza kuwa endapo mwanachama yeyote atakishtaki chama hicho mahakamani na iwapo atashindwa atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye chama

Friday, 6 March 2015

Viongozi kujiuzulu pekee haitoshi

Jana Profesa Sosperter Muhongo alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Nishati na Madini, akieleza kuwa anataka nchi isonge mbele kwa kuwa suala la kumtaka Rais amwondoe kutokana na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, limesababisha mambo mengi kukwama.
Profesa Muhongo amekuwa waziri wa pili kuondoka baada ya Profesa Anna Tibaijuka kuvuliwa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na kuingiziwa kwenye akaunti yake Sh1.6 bilioni na mmiliki wa zamani wa IPTL, fedha ambazo zinahusishwa na sakata la escrow.
Mbali na mawaziri hao, tayari Jaji Fredrick Werema amejiuzulu kazi yake ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akieleza kuwa ushauri wake kuhusu fedha za escrow haukueleweka na kusababisha tafrani.
Pia, katibu mkuu wa wizara hiyo, Eliackim Maswi amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa sakata hilo, wakati watumishi watano wa Tanesco, Benki Kuu (BoT) na Mamlaka ya Mapato (TRA) wamefikishwa mahakamani wakishtakiwa kwa kupokea rushwa inayohusu sakata hilo. Kashfa hii ni moja ya matukio mengi makubwa yaliyosababisha Rais kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri. Baadhi ya matukio hayo ni kashfa ya Richmond, CAG na Operesheni Tokomeza ambazo zilisababisha Rais kupangua baraza lake.
Ni jambo la kupongeza kwamba angalau hatua zimechukuliwa kwa kiwango fulani katika kushughulikia tatizo hilo lililohusu uchotwaji wa takriban Sh306 bilioni kutoka kwenye akaunti hiyo iliyokuwa BoT.
Kitu cha ajabu ni hii tabia inayoendelea kujengeka ya kuibuka kwa kashfa, mawaziri kujiuzulu, kuundwa kwa baraza jipya na baadaye mambo kuendelea kama kawaida kusubiri kashfa nyingine kuibuka bila ya hatu za dhati kuchukuliwa kudhibiti matukio kama hayo.
Jambo la ajabu ni kwamba kila kashfa inapoibuka, hutumika nguvu nyingi kuizua au kutetea viongozi wa Serikali hadi mambo yanapoonekana kuwa yamekuwa makubwa ndipo hatua zichukuliwe.
Tumeona katika kashfa ya escrow zilitumika nguvu nyingi kutetea wahusika hadi maji yalipozidi unga ndipo hatua zilipochukuliwa na kushughulikia wahusika. Kitu kibaya ni kwamba hadi wakati hatua zinaanza kuchukuliwa, tayari Serikali inakuwa imeshafuka na wananchi wameshaumia.
Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri sasa yamekuwa ya kawaida kwa kuwa kila yanapofanyika hazichukuliwi hatua thabiti kuzuia kashfa zisitokee. Suala la fedha kuchotwa kwa fedha zinazokuwa BoT sasa linaonekana kuwa la kawaida kwa kuwa kashfa ya Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje lilipotokea, hakukuchukuliwa hatua madhubuti kuziba mianya kama hiyo kwenye taasisi hiyo nyeti ya fedha.
Tunadhani ni wakati mwafaka sasa kwa Serikali kuweka misingi imara ya uongozi itakayowabana viongozi wetu kujiingiza kwenye kashfa kama hizo. Misingi hiyo pia ihusishe hatua kali ambazo zinaweza kuchukuliwa kwa viongozi ambao wataingia kwenye kashfa hizo kwa makusudi au uzembe ili kuzuia wengine kufanya mambo ya aibu na yanayoumiza wananchi.
Pia, siyo ufahari kuwawajibisha viongozi wakati ufisadi umeshafanyika kama ilivyokuwa kwenye sakata la EPA na sasa escrow kwa kuwa fedha za walipa kodi zinakuwa zimeshachotwa. Ufisadi unatakiwa uzuiwe mapema kuliepusha Taifa kupoteza mabilioni ya fedha na wanaowajibishwa wachukuliwe hatua kwa kujaribu kula njama za ufisadi na siyo kuadhibiwa kwa kufanya ufisadi.
Kadri Serikali inavyoonekana kuweka mikakati ya kuwakingia kifua watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, ndivyo vitendo hivyo vinavyozidi. Serikali inatakiwa ionyeshe kuchukia ufisadi kwanzaNa ikichukia ufisadi, basi kujiuzulu wa kuwavua madaraka wahusika kutakuwa ni moja ya hatua za kuwashughulikia wahusika wote nah ii itasaidia kupunguza vitendo hivyo..

Magufuli: Mbowe kama malaika

Hai. Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli jana aliungana na viongozi wenzake wa Serikali kuwamwagia sifa viongozi wa vyama vya upinzani baada ya kumwelezea Mbunge wa Hai na Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe kuwa ni mpigania maendeleo ya wananchi na kwamba alitakiwa awe malaika.
Dk Magufuli alimuelezea kiongozi huyo wa upinzani bungeni kuwa ni mtu ambaye anafuatilia maendeleo ya watu bila ya kujali itikadi zao.
Waziri huyo ameungana na Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kusifu utendaji wa viongozi wa upinzani.
Februari 10, Rais Kikwete alisifu utendaji wa meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael wa kuwaletea maendeleo wananchi, na siku 12 baadaye Waziri Pinda alimsifu mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kwa kuwa kiongozi wa kwanza kuchangia vitanda 30 kwenye Hospitali ya Frelimo.
Jana, Dk Magufuli alimmwagia Mbowe sifa hizo katika mkutano wa hadhara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Kwasadala-Masama-Machame katika Jimbo la Hai inayojengwa kwa kiwango cha lami.
“(Mbowe)Unadhihirisha kwamba maendeleo hayana chama na kwa kweli tukienda hivi Tanzania itakuwa ni nchi ya kutolewa mfano. Sincerely (kwa dhati) nakupongeza Mbowe na Mungu akubariki,” alisema.
Kabla ya Dk Magufuli kutoa pongezi hizo, Mbowe aliwataka wanasiasa kutekeleza ahadi zao kwa vitendo kwa kuwa maendeleo hayana itikadi.
“Mimi naamini maendeleo hayana itikadi. Jambo jema likifanywa na chama chochote cha siasa ama kiongozi wa chama chochote au Mtanzania, kama ni jema anastahili kupongezwa,” alisema Mbowe.
“Hakuna aibu ya kukiri pale jambo jema linapofanyika. Ujenzi wa Barabara ya Kwasadala-Mula-Machame ni jambo jema,” alisisitiza Mbowe.
Hata hivyo, alitumia mkutano huo wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Masama kumuomba Dk Magufuli atoe maagizo ya kiserikali baada ya viongozi wawili wa CCM kutishia kuchoma moto greda lake.
“Nimenunua greda ili tusaidiane na Serikali, lakini juzi diwani na mwenyekiti wa kijiji walitishia kuchoma moto greda eti kwa sababu mbunge hajapewa kibali cha kuchimba barabara,” alilalamika.
Mbowe alisema vyama vya siasa ni lazima vifanye pamoja kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Akihutubia mkutano huo, Dk Magufuli alisema Mbowe ni kiongozi mpole na mstaarabu na ndiyo maana kila ombi lake analoliwasilisha serikalini kwa ajili ya wananchi wake haligongi mwamba.
“Utapata wapi mtu mpole kama huyu? Alimuomba Rais pale kwamba niongezee kilometa tatu, (Rais) akatoa siku ile ile,” alisema.
“Rais Kikwete ni mwenyekiti wa CCM, lakini ameleta barabara hapa kwa mwenyekiti wa Chadema. Huo ndiyo utanzania na haya ndiyo tunatakiwa viongozi tuige mfano.”
Waziri Dk Magufuli alisema Mbowe ni miongoni mwa wabunge wachache wa upinzani ambao hawamsumbui bungeni na anapokuwa na jambo, huwa wanatoka nje na kuteta.
“Wako wengine wanapigaga kelele, lakini wewe unakuja tunazungumza. Unasema ndugu yangu, brother (kaka). Mbowe weweee! Ulitakiwa uwe malaika,” alisema Dk Magufuli katika mkutano huo.
Hata hivyo, Dk Magufuli aligeukia siasa na kusema ustaarabu na upole alio nao Mbowe unatokana na malezi mazuri ya CCM kwa vile wazazi wake walikuwa wana-CCM na kwamba pongezi anazitoa kwa dhati. Alimpongeza Mbowe kwa kununua greda, akisema fedha hizo angeweza kuzitumia kwa shughuli nyingine lakini akaamua kulinunua ili kusaidia wananchi wak

Makongoro Nyerere afunguka urais

Dar es Salaam. Wakati CCM ikielekea katika kipindi kigumu cha kuamua mgombea wake wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, Makongoro Nyerere, ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, amezungumzia taarifa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii zikimtaja kuwa na mpango wa kuwania nafasi hiyo ya juu nchini.
CCM, ambayo imeshika nchi tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi, hujikuta katika wakati mgumu kila wakati inapotakiwa kutoa mgombea wa kurithi nafasi ya Rais aliye madarakani baada ya kuongoza vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja.
Tayari wanachama wanne wa chama hicho tawala wameshatangaza rasmi kuwania urais huku wengine sita wakifungiwa kwa makosa ya kudaiwa kuanza kampeni mapema, huku kukiwa na mlolongo wa watu wanaotajwa kuwa na mpango wa kujitokeza kuwania nafasi hiyo, akiwamo Makongoro, ambaye imeelezwa kuwa ameshauriwa kuchukua uamuzi huo kujaribu kukinusuru chama kutokana na makundi yanayoonekana kujitokeza katika mbio hizo.
“Mimi si mtabiri, siwezi kukwambia nitagombea au la, lakini uamuzi wangu utajulikana mara kipenga kitakapopulizwa na CCM,” alisema Makongoro ambaye ni ofisa wa zamani wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) na mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).
Vyanzo hivyo vya habari vimeeleza kuwa mkakati wa kuhakikisha Makongoro anakuwa rais, unaratibiwa na baadhi ya makada waliowahi kufanya kazi na Mwalimu Nyerere.
Mkakati huo pia unatajwa kuwa ulianza pale alipochaguliwa kuwa mbunge wa Eala. Tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda, January Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Lazaro Nyalandu ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii na Hamisi Kigwangala (mbunge) wametangaza nia ya kuomba ridhaa ya CCM kuwapitisha kuwania urais.
Hata hivyo, upinzani mkubwa unaonekana kuwa kwa vigogo ambao hawajatangaza nia hiyo na ambao wanatumikia adhabu ya kufungiwa kwa zaidi ya miezi 12 kutokana na kikiuka taratibu za chama hicho.
Miongoni mwa ambao hawajajitokeza ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye wafuasi wake wamekuwa wakijitokeza katika siku za karibuni kueleza wazi msimamo wao kuwa ndio chaguo sahihi, na Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Pia yumo Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, Spika wa zamani wa Bunge, Samuel Sitta, Waziri wa Kilimo na Chakula, Steven Wasira na Naibu Waziri wa Fedha-Sera, Mwigulu Nchemba, ambaye alionywa na chama hicho dhidi ya safari zake mikoani zilizodaiwa kuwa na dalili za kampeni.
Kauli ya Makongoro
Akizungumza na gazeti hili, Makongoro hakuonyesha kukataa wala kukubali kuhusu uamuzi wa kugombea nafasi hiyo iliyoshikwa na baba yake kwa takribani miaka 25.
“Ninachoweza kutabiri kwa sasa ni iwapo nina njaa basi lazima nitakula au simba akitokea lazima nikimbie. Kama nina usingizi na kuna kitanda karibu lazima nitalala lakini mambo mengine siwezi kuyasemea,” alisema Makongoro ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya chama cha NCCR-Mageuzi. Alisema anasubiri siku ambayo CCM itatangaza mchakato wa kuchukua fomu ndipo hatma yake itajulikana.
Makongoro ni nani
Makongoro ni mtoto wa tatu wa familia ya Hayati Nyerere na Januari 30 mwaka huu alitimiza miaka 56 tangu azaliwe. Alipata mafunzo ya uongozi wa kijeshi Monduli kati ya mwaka 1980 na 1982.
Luteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi alipata elimu ya sekondari ya juu na ya kawaida kwenye Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora wakati elimu ya msingi alisomea katika shule tatu tofauti za Arusha, Bunge na Isike kati ya mwaka 1971 na 1978.
Mwaka 1995 Makongoro alihama CCM na kujiunga na NCCR Mageuzi na katika uchaguzi wa kwanza tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi, Makongoro alishinda ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, lakini hakumaliza kipindi chake kutokana na ubunge huo kupingwa mahakamani na hatimaye kutenguliwa.
Aprili 7, 2012 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilimchagua kuingia kwenye Bunge la Afrika Mashariki.
Maoni ya wachambuzi
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema masuala ya urais wa Makongoro aulizwe mwenyewe.
“Sitaki kuulizwa kuhusu hilo, mimi si meneja wa kampeni wa hao watu. Nitoe kabisa katika hilo,” alisema Butiku, ambaye ni miongoni mwa watu waliofanya kazi na Mwalimu Nyerere wakati wa utawala wa awamu ya Kwanza.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru alisema hawezi kutoa maoni yoyote hadi pale Makongoro atakapoamua kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema iwapo Makongoro anahitaji kuwa rais, basi angepata kwanza ushauri wa wazee kutoka Butiama.
“Kwangu mimi Makongoro hana sifa ya kuwa rais, kwani kuna vigezo gani vinavyoangaliwa? Angeomba ushauri kwanza hata kwa kina Butiku,” alisema Dk Bana.
Alisema kwa anavyofahamu, CCM huchagua viongozi wazalendo, wenye maadili na historia za kupendeza wala si viongozi kutokana na koo zao au umaarufu tu. Kadhalika Dk Bana alisema mchakato wa kumpata rais ajaye ni mgumu hivyo akaitaka CCM isikurupuke.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Gaudence Mpangala alisema haoni tatizo kwa mtoto huyo wa muasisi wa Taifa kwa kuwa ana sifa zote za uongozi na hana sifa ya ‘uchafu.’
“Ukizungumzia usafi wa viongozi, hana neno. Anaweza kuwa kiongozi mzuri tu na pia ana haki kikatiba,” alisema.
Profesa Mpangala alisema licha ya watu kukosoa kuwa watoto wa viongozi wa zamani wanatengenezwa kuwa viongozi, lakini kama mtu ana sifa basi hana budi kugombea.

Albino wapambana wakienda kwa Rais Kikwete

Dar es Salaam. Hali ya sintofahamu ilitokea jana baada ya wanachama wa Chama cha Albino Tanzania (Tas) kumshambulia kiongozi wao, Ernest Kimaya wakati wakiwa njiani kuelekea Ikulu ambako Rais Jakaya Kikwete aliwaita kwa mazungumzo.
Pembeni ya barabara inayopakana na Ikulu, karibu na jengo la Wizara ya Elimu wakati wakielekea kumuona Rais Kikwete, wanachama hao walianza kumshambulia Kimaya wakidai kuwa si kiongozi halali, lakini aliokolewa na maofisa usalama waliokuwapo katika tukio hilo.
Wanachama hao walitaka kushinikiza na wao kumwona Rais Jakaya Kikwete badala ya viongozi 15 ambao ndiyo waliotakiwa wamwone Rais na kuzungumza naye. Saa moja baadaye, viongozi hao wa Tas waliingia Ikulu kuonana na Rais Kikwete.
Wanachama hao walikuwa wakimtaka Kimaya aachie wadhifa wake kwa kuwa si kiongozi.
Kimaya alizomewa muda wote na kumvuta nguo na baadhi ya wanachama hao ambao walimtuhumu kuwa anajinufaisha na vifo vya albino vinavyozidi kutokea nchini.
Hata hivyo, Kimaya alishindwa kujizuia na kutaka kupigana na baadhi watu waliokuwa wakimzonga na kumtukana. Maofisa usalama walimchukua na kumwondoa eneo la tukio ili vurugu zisiendelee.
Baadhi ya wanachama wa Tas walisema viongozi wao wamejikusanya wenyewe kwenda Ikulu bila kuwashirikisha na kuwa hawafanyi mikutano ya mara kwa mara zaidi ya kuwaita kwenye maandamano.
Mmoja wa albino hao, Nuru Iddi alisema hawana imani na viongozi wao kwa sababu muda wao wa kuwepo madarakani uliisha tangu mwaka jana.
Alisisitiza kuwa tangu wakati huo hawajafanya uchaguzi wowote na viongozi wametulia ili waendelee kujinufaisha.
“Albino akiuawa kule Mwanza mimi ndiyo napata uchungu, siyo hawa viongozi... wao wanapokea michango mingi kutokana na vifo vya wenzetu lakini hawafanyi jambo lolote la maana kulinda maisha yetu,” alisema mwanachama huyo.
Iddi aliongeza kuwa wao ndiyo walitakiwa kuonana na Rais Kikwete ili wamueleze hali halisi na nini cha kufanya ili kulinda maisha yao.
Aliulaumu uongozi wa Tas kwa kutowashirikisha wao kama wanachama kutoa maoni ambayo yangewasilishwa kwa Rais.
Naye Mwalimu Matimbwa alisisitiza kuwa viongozi wao wako nje ya muda kikatiba. Alisema mwaka 2006 kulikuwa na kisa kimoja tu cha mauaji ya albino lakini mpaka sasa idadi imefikia 78. Aliushutumu uongozi wa Tas kutodhibiti ongezeko hilo la mauaji ya albino.
“Nasikia uchungu sana ninapoona wenzangu wanauawa lakini baadhi yetu wanajinufaisha na mauaji hayo. Hatuwezi kushinda vita hivi kama hatuna uongozi thabiti. Tunataka uchaguzi ufanyike haraka sana,” alisisitiza Matimbwa.
Matimbwa aliongeza kuwa katiba yao inataka uchaguzi ufanyike kila baada ya miaka mitano lakini uchaguzi huo haukufanyika mwaka jana.
Kimaya alikiri kuwa walitakiwa kufanya uchaguzi mwaka 2014, lakini walikubaliana na wanachama kuwa uongozi uliokuwepo madarakani kwa ngazi ya wilaya, mikoa na taifa uendelee na kazi.
“Sisi tupo madarakani kihalali kwa sababu wanachama wenyewe ndiyo walipendekeza kuwa tuendelee kuongoza. Hili ni kundi la wahuni tu, siyo wanachama wetu,” alisema kiongozi huyo kabla ya kushambuliwa na wanachama waliokuwa wakipiga kelele wakisema “hatumtambui, aachie kiti huyo”.
Kimaya alifafanua kuwa mara ya mwisho walifanya uchaguzi mwaka 2009, lakini mwaka jana walishindwa kufanya uchaguzi kwa sababu kulikuwa na mwingiliano wa mambo.
Rais Kikwete aliandaa chakula cha mchana na viongozi wa Tas, Ikulu jijini Dar es Salaam. viongozi wa Tas walipata nafasi ya kuongea naye juu ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yanayoshika kasi nchini kwa sasa.

Sunday, 25 January 2015

Ukawa waivuruga Serikali, hawatashiriki kura ya maoni

Dar es Salaam. Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimeeleza kuwa kuna matatizo mengi kwenye mchakato wa Kura ya Maoni na kutangaza rasmi kutoshiriki, vikidai vitahamasisha wananchi kuwaunga mkono.
Tamko hilo limekuja siku chache baada ya mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kueleza kuwa uwezekano wa Kura ya Maoni kupigwa Aprili 30 ni mdogo na kwamba juhudi za kutaka azma hiyo itimie zinaweza kusababisha sheria kupindishwa.
Kauli yake iliungwa mkono na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye alisema uwezekano wa kupiga Kura ya Maoni siku hiyo ni mdogo na kwamba Serikali inahitaji kuwa makini ili kuhakikisha inapigwa Aprili 30.
Jana, vyama hivyo viliongeza uzito kwenye hoja hiyo ya kutaka mchakato huo usimamishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu vilipotoa tamko la pamoja la kususia mchakato huo, vikieleza kuwa muda uliosalia kukamilisha mchakato wa Kura ya Maoni ni mfupi, ikilinganishwa na maandalizi hafifu yanayofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ambayo imetangaza uandikishaji katika Daftari la Wapigakura utaanza Februari 16.
Wenyeviti wa vyama vinavyounda Ukawa, Freeman Mbowe wa Chadema, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzina na Emmanuel Makaidi wa NLD, walitangaza msimamo huo jana baada ya kumalizika kwa kikao chao kwenye ofisi za makao makuu ya CUF Buguruni jijini Dar es Salaam.
Profesa Lipumba ambaye alitoa tamko la Ukawa kujiondoa kwenye Bunge Maalumu la Katiba Aprili mwaka jana, alisema wamefikia uamuzi wa kutoshiriki katika Kura ya Maoni kwa sababu mchakato mzima haukuwa na maridhiano ya kitaifa.
“Vyama vya siasa, ikiwemo CCM vilikubaliana mwaka jana kwamba Kura za Maoni ifanyike mwaka 2016 baada ya Uchaguzi Mkuu, tulisaini wote na Rais Jakaya Kikwete alikubali,” alisema Lipumba.
Alisema jambo la kushangaza, Rais Kikwete aliwageuka na kutangaza kwamba Aprili 30, mwaka huu kuwa siku ya kupiga kura ya maoni.
“Tukashangaa Rais anatupiga chenga kwenye jambo kubwa kama hili ambalo tulishakubaliana naye kuwa lifanyike baada ya uchaguzi,” alisema.
Alisema pamoja na kutangaza siku ya kupiga kura, bado uandikishaji katika Daftari la Wapigakura haujaanza kwa sababu wanasubiri vifaa.
“Hadi sasa vifaa vya Biometric Voter Registration (BVR) vilivyopo ni seti 250 wakati vinavyohitajika ni seti 7,500, Tume inasubiri hadi sasa, zoezi hili litafanyika?” alihoji Lipumba.
Hata hivyo, juzi uongozi wa Nec ulisema Kura ya Maoni itafanyika kama ilivyopangwa licha ya vifaa hivyo kuchelewa kufika.
Ulisema muda uliobaki utatosha kwa asasi za kiraia kutoa elimu na vyama vya siasa kufanya kampeni.
Lipumba alisema historia ya mchakato huo imekuwa haishirikisha maoni ya watu na matatizo yanayojitokeza katika maandalizi ya Kura ya Maoni, wameamua kujitoa na hawatashiriki kutengeneza Katiba ambayo ni batili.
Naye Mbowe aliwaomba Watanzania wote kujitoa kwenye mchakato wa kura za maoni kwa sababu unalazimishwa na unafanyika bila ya kuwa na uhakika.
“Tumeamua kwamba hatuwezi kukengeuka na kushiriki kupigia kura kwenye mchakato ambao ni haramu. Tumeona tuwaachie CCM wenyewe wamalizie mchakato wao haramu,” alisema Mbowe.
Akifafanua zaidi Mbowe alisema Sheria ya Kura ya Maoni inataka Jaji wa Tanzania na Jaji wa Zanzibar kutengeneza kanuni ambazo wasioridhika kwenye kura ya maoni wanaweza kushtaki.
“Lakini hadi leo majaji hao hawajakaa kutengeneza kanuni hizo jambo ambalo tunaona mchakato huu hauna masilahi ya wananchi bali ya watu,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema mchakato mzima wa Katiba sasa `umeporwa’ na Ikulu kwa sababu hata kutangaza siku ya kupiga Kura ya Maoni kulitakiwa kufanywe na mwenyekiti wa Nec, lakini cha kushangaza Rais ndiye aliyetangaza.
Naye Mbatia alisema Katiba haitakuwa na maridhiano ya kitaifa.
“Hatuwezi kushiriki kwenye Kura ya Maoni kwa sababu muda uliobaki hauruhusu, tunawaachia wenyewe CCM waendelee kuchakachua, sisi tunaona tusijihusishe kuleta Katiba haramu,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa NLD, Makaidi alisema amegundua mbinu za kuanza kuwasafirisha wananchi wa Bara kwenda kuishi Zanzibar kwa lengo la kupiga kura za ndiyo kwenye Katiba Inayopendekezwa.
Maoni ya wadau
Baadhi ya wasomi walioongea na gazeti hili jana, walikuwa na mawazo tofauti kuhusu tamko hilo.
Profesa Aidan Msafiri wa Chuo Kikuu cha Mtwara, alisema Serikali ni lazima izungumze na Ukawa ili kueleza kuhusu mchakato huo.
“Tunajenga nyumba moja kwa nini tugombanie fito, Serikali ni lazima iangalie hoja za Ukawa kama ni za msingi na ichukue hatua.”
Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema Ukawa wameshaandaa ajenda yao ya kutokea katika Uchaguzi Mkuu.
Alisema Ukawa hawana hoja na hawana huruma na mamilioni ya fedha zilizotumika katika mchakato wa Katiba mpya.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) wameshasema kwamba muda uliobaki unatosha kufanya kampeni na kutoa elimu lakini wao wanajitoa,” alisema Bashiru.
Alisema siasa za Tanzania hivi sasa zimekuwa za vituko na matukio kwa sababu walitakiwa kusubiri ili kuona Nec wameshindwa kutekeleza zoezi hilo ndipo waamue kususia.