Sunday, 30 November 2014

IPTL yazamisha mawaziri, AG, wabunge

Dodoma. Bunge limehitimisha mjadala wa Kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kwa kupitisha maazimio manane, likiwamo la kuwawajibisha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine waliowajibishwa pamoja na mawaziri hao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na kuwavua nyazifa zao wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge.
Wenyeviti waliovuliwa nyadhifa zao ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge. Viongozi hao wamevuliwa nyadhifa zao chini ya azimio la Bunge namba mbili.
Maazimio hayo mapya manane yalisomwa bungeni jana jioni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
Akizungumza bungeni Zitto alisema, mabilioni ya fedha yaliyotolewa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow yametumika kuwapa kile kinachoonekana kuwa ni rushwa.
Zitto alisema baadhi ya watu waliochukua fedha hizo ni viongozi wa umma na maofisa wa Serikali kama mawaziri, majaji, wabunge, wenyeviti wa kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi.
“Vitendo vilivyofanywa na watu hawa vinaashiria uzembe na makosa mbalimbali ya jinai kama vile wizi, ubadhilifu kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kupokea mali ya wizi,” alisema.
Alitaja azimio la kwanza la Bunge ni kulitaka Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
Zitto alisema watu wote waliotajwa na taarifa maalumu ya kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai, watachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Azimio la tatu ni kuzitaka Kamati husika za kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya mkutano wa 18 wa Bunge kuwavua nyazifa zao za wenyeviti wa kamati husika za Bunge. Zitto alitaja azimio la nne ni la kumuomba Rais auende Tume ya kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Alisema utaratibu wa kushughulikia nidhamu za majaji kwa mujibu wa Katiba unamtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji, kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji.
Pia azimio la tano ni mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Benki ya Stanbic na benki nyingine yoyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
Azimio la sita alilitaja Zitto kuwa ni kuiomba Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisasa.
Alisema azimio la saba la Bunge ni kuitaka Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.
Katika azimio lake la nane Bunge liliazimia kwamba Serikali itekeleze azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme.
Mbowe, Filikunjombe, Wassira
Wakichangia mapendekezo hayo mapya yaliyosomwa na Zitto, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe alisema wamekubaliana na mapendekezo hayo mapya manane yanayotosha kufikisha ujumbe.
Alisema ni muhimu viongozi wa Serikali wakalinda rasilimali za nchi kwa kutekeleza wajibu wao wakijua Watanzania wengi masikini wanawategemea wao kuwatoa kwenye umaskini.
“Niombe tu Waziri Mkuu awe mkali ili tusifike kwenye mshike mshike kama huu tuliofikia kwa sasa,” alisema Mbowe na kuongeza: “Waziri Mkuu uwe mkali kwa kweli.”
Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) alilishukuru Bunge kwa kufanya kazi yake akieleza kuwa limeweka maslahi ya nchi kwa kushikana pamoja.
“Kumekuwa na makosa yamefanyika kwenye baadhi ya maeneo, hivyo hatua zimechukuliwa,” alisema Filikunjombe.
Alisema anafurahi kwamba hatua stahiki zimechukuliwa kwa waliohusika.
“Sasa hatua stahiki zitachukuliwa kwa kila mmoja kwa nafasi yake,” alisema.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira alisema juzi hali ilikuwa mbaya, lakini wameweza kuridhiana kwa kuwa wote ni binadamu.
Alisema mtafaruku uliotokea umewafundisha kwamba wanaweza kukubaliana wakijadiliana.
“Kazi haikuwa rahisi, lakini tumeelewana na aliyosema Zitto ndiyo tuliyokubaliana kwa kuwa CCM haina sera ya kukubali jambo lolote ambalo linaminya maendeleo ya wananchi,” alisema.
Alisema Serikali ina wajibu wa kutekeleza maazimio ya Bunge hivyo yanayowagusa wenzao ndani ya Serikali watawajibika kwa kuwa ndiyo wajibu.
“Sasa hivi kila mhimili umeguswa hivyo tutatekeleza,” alisema Wasira.
Spika Anne Makinda aliwaonya wabunge kuachana na watu wenye fedha wanaotoa kwa lengo la kuwahonga, kwani zitawaweke pabaya kwa kuwa hawana kinga za makosa ya jinai.
Bunge laendelea jana asubuhi
Baada ya juzi Spika Makinda kuahirisha Bunge kwa kushindwa kufikia mwafaka, jana Bunge liliendelea asubuhi, lakini baada ya wabunge kuingia Spika alitangaza kuahirisha Bunge hadi saa tano asubuhi ili vyama vikafanye vikao kwa ajili ya kutafuta suluhu ni maneno gani yatumike katika mapendekezo ya Kamati ya PAC yanayotaka kuwang’oa vigogo wote wa Serikali wanaotuhumiwa kuhusika na sakata hilo.
Wakati Spika akitoa maelekezo hayo tayari asubuhi na mapema wabunge wa Kambi ya Upinzani walioungana wote walikuwa wameshakutana kwenye Ukumbi wa Msekwa kuweka msimamo kuhusu mapendekezo hayo.
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) Mchungaji Peter Msigwa walisema kuwa kikao chao kiliamua kuwa wasimamie mapendekezo yote yaliyopendekezwa na kamati kama yalivyo na lisibadilishwe hata moja.
Selasini alisema wabunge wa CCM wanachotaka kufanya ni kuwaokoa watuhumiwa, lakini wao wanaingia bungeni na msimamo mmoja wa kutaka mapendekezo yote ya PAC yapite kama yalivyo.
“Wakikataa tutamalizana pale ndani,” alisema Selasini huku Msigwa akisema, “Wanataka kutufanyia uhuni, sisi tunataka mapendekezo yote ya kamati yapite kama yalivyo.”
Wakati upinzani ukiwa na msimamo huo na kuendelea na shughuli zao Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alionekana akizunguka kuwaomba wabunge wa CCM waelekee White House (Makao Makuu ya CCM Dodoma) kwa ajili ya kikao chao.
Hata hivyo, wabunge wengine wa CCM walionekana kutojali kikao hicho huku wakiendelea mazungumzo na wabunge wa upinzani huku wakipongezana na wengine wakikandiana kutokana na jambo lililotokea juzi.
Bunge larejea saa tano na kuahirishwa
Kikao cha Bunge kilirejea jana saa tano baada ya kuahirishwa asubuhi na Spika alimpa nafasi Lukuvi ambaye alitoa hoja ya kuomba Bunge liridhie kuongeza muda wa saa moja kwa ajili ya pande zote mbili kufanya mashauriano na kurudi na kauli moja kama Bunge. “Nilikuwa naomba tuahirishe Bunge kwa saa moja ili tuendelee na mashauriano na kuja na kauli moja,” alisema Lukuvi.
Hoja hiyo ilipingwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliyesema kuwa haiwezekani wakatoka nje kwenda kwenye mashauriano ya kukubaliana na msimamo wa CCM na kusema ni kauli moja ya Bunge. “Haiwezekani tukatoka na kauli moja kwa kuweka msimamo wa misimamo ya kichama,” alisema Mnyika.
Lukuvi alisimama tena na kusema; “Tumeomba saa moja tuendelee na mashauriano ili tutoke pamoja na siyo suala la vyama hapa. Tunataka tushauriane kama Bunge.”
Baada ya Lukuvi kumaliza, Spika Makinda alisema anatoa muda hadi saa kumi jioni ili viongozi wa upinzani na CCM wakakae ili kushauriana jinsi gani ya kuweza kuja na maneno yanayofaa kwenye mapendekezo yanayofuatia.
Hoja hiyo ilionekana kupingwa na wabunge wakieleza kwamba saa kumi jioni ni mbali hivyo Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alisimama na kusema kuwa masaa mawili yanatosha kwa mashauriano lakini siyo saa moja kama Serikali ilivyoomba.
Spika alimpa nafasi Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia ambaye yeye alipendekeza masaa matatu ili kamati ikae na kuona jinsi gani wataweza kufikia mashauriano yao.
Spika Makinda alisema ni lazima wabunge waelewe kwamba mabunge ya kisasa yakifikia katika hali kama ya jana na juzi, lazima wakutane pande zote na kufanya mashauriano.
“Tuwe Bunge la kisasa lazima tushauriane tunapofika kwenye suala kama hili na hivyo mkutane wote na kukubaliana. Hivyo tukubaliane wakija na kauli moja tunapitisha,” alisema Spika Makinda.
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka aligomea kauli hiyo ya Spika na kueleza kuwa anakubali pande zote kutoa watu, lakini hakubaliani kwamba wakija na kauli moja ndiyo ipitishwe.
Kabla Ole Sendeka hajakaa Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiel Wenje alisimama na kusema watu wapewe muda wa kushauriana, hivyo timu iundwe na ikae kwa muda mrefu ili wengine ambao hawatakuwa kwenye kamati hiyo wapate nafasi ya kutaarifiwa juu ya nini kinachoendelea
“Kwa hiyo Spika mimi nakubali turudi saa kumi ili hiyo timu ikakae na sisi kwenye vikao vyetu tupewe taarifa tukifika hapa baadaye tumalizane tu,” alisema Wenje na hoja yake iliungwa mkono na wabunge hivyo Spika Makinda akasema viongozi wote wakae na kuja na kauli moja.
Pia, akitaka Zitto awe na wawakilishi kwa kuwa ndiye mwenye hoja, lakini wale wanaotuhumiwa wasiingie kwenye kamati hiyo. Hivyo akaahirisha Bunge.
Bunge laahirishwa tena saa kumi
Bunge lilirejea tena saa kumi jioni na kuahirishwa baada ya Spika kupewa taarifa kwamba kamati iliyoteuliwa kwa ajili ya mashauriano haijamaliza kazi.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Muhagama alisimama kwa upande wa CCM na kumweleza Spika kuwa corcus yao imeambiwa kwamba bado majadiliano yanaendelea.
“Spika sisi tulituma wawakilishi sita na mpaka sasa tumeambiwa kazi inaendelea lakini sijui kwa wenzetu imekuwaje lakini hadi sasa bado,” alisema Muhagama.
Spika Makinda alipokea taarifa hiyo na kuhoji upande wa upinzani una taarifa gani ambapo Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisimama na kusema, “Na sisi tumeelezwa kwamba bado.”
Kwa kauli hiyo Spika Makinda aliamua kuahirisha Bunge hadi saa moja jioni na kuwaeleza wabunge kwamba suala hilo lazima limalizike ifikapo saa mbili na robo usiku.
Wabunge walitoka nje na kuendelea na shughuli zao huku wengine wakijikusanya vikundi vikundi wakijadiliana. Wengine waliamua kukaa Kanteen ya Bunge kusikiliza hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye amerejea nchini jana akitokea nchini Marekani alikokuwa kwa matibabu ya tezi dume.
Kilichotokea juzi usiku
Juzi Spika Makinda alilazimika kuahirisha Bunge kutokana na wabunge wa Kambi ya Upinzani kugoma kukubali marekebisho ya Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge kwamba uamuzi wa kumng’oa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo uachiwe mamlaka iliyomteua.
Chenge alifanya marekebisho akieleza pendekezo la kumng’oa Profesa Muhongo lisomeke kama lile la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi ambalo Bunge lilipitisha kwamba: “Bunge linaazimia kulifikisha suala hili kwa mamlaka ya uteuzi kwa hatua zaidi.”
Kipengele hicho kilikataliwa na upinzani na kuamua kusimama wakitaka Profesa Muhongo achukuliwe hatua lakini CCM waligoma ndipo Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliposimama na kusema kuwa haiwezekani kamati imependekeza mambo halafu Bunge linataka kuwalinda watuhumiwa.
Mbowe alisema kama Bunge linaamua hivyo wao hawawezi kuwa upande wa uamuzi huo kauli iliyowanyanyua wabunge wote wa upinzani vitini kutaka waondoke, ingawa Spika alimsihi Mbowe kuwatuliza, ilishindikana na Spika kuamua kisitisha Bunge hadi jana.
Jitihada kubwa zilifanyika kuwasihi wabunge wa upinzani kutulia lakini walianza kupiga kelele wakieleza kuwa hawawezi kulinda wezi.
Spika Makinda kabla ya kuahirisha aliwaeleza wabunge kuwa anapata wakati mgumu kwa kuwa Bunge limekuwa likiingilia shughuli za mihimili mingine na kwamba tayari ana kesi mahakamani kutokana na kuelezwa kuingilia shughuli za mahakama hivyo aliwaomba wabunge waache kutoa maamuzi ambayo yanaingilia mhimili wa Serikali.
“Tayari mimi nina kesi huko katika mhimili mwingine sasa mnataka nigombane tena na Executive (Serikali) itakuwaje jamani naomba tutafute maneno ya kutokuingilia mhimili mwingine,” alisema Spika Makinda.
Maneno yake hayo yalionekana kupuuzwa na wabunge wa upinzani na wengine wa CCM huku wakipiga kelele kuwa ni lazima watuhumiwa waliohusika kwenye sakata la escrow washughulikiwe kama ilivyokuwa kwenye sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili.

Wednesday, 26 November 2014

Majina Ya Waliokula Fedha Za Akaunti Ya Escrow Katika Ripoti Ya PAC Iliyosomwa Sasa Bungeni





Zitto: Upande wa viongozi wa kisiasa ambao waliingiziwa fedha katika akaunti zao binafsi ni; Mhe.
Andrew Chenge (Mb)
Zitto: Andrew Chenge aliingiziwa shilingi bilioni 1.6.
Zitto: Mhe. Anna Tibaijuka (Mb) na Waziri wa 62
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi shilingi bilioni 1.6.
Zitto: Mhe.William Ngeleja (Mb) na ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini alipewa shilingi milioni 40.4
Zitto: Ndg. Daniel N. Yona ambaye alikuwa pia Waziri wa Nishati na Madini alipewa shilingi milioni 40.4.
Zitto: Ndg. Paul Kimiti ambaye ni Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Sumbawanga
alipewa shilingi milioni 40.4
Zitto: Dr. Enos S. Bukuku ambaye alikuwa Mjumbe wa Bodi ya TANESCO aliingiziwa shilingi milioni 161.7.
Zitto: Upande wa Majaji Prof. Eudes Ruhangisa, aliingiziwa milioni 404.25 na J.A.K Mujulizi aliingiziwa shilingi milioni 40.4
Zitto: kwa upande wa Watumishi wa umma,Ndg. Philip Saliboko ambaye alikuwa mtumishi wa RITA aliingiziwa
shilingi milioni 40.4
Zitto: Ndg. Emmanuel Daniel Ole Naiko ambaye
alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa (TIC) aliingiziwa shilingi milioni 40.4
Zitto: Ndg. Lucy L. Appollo ambaye ni Mtumishi wa TRA aliingiziwa shilingi milioni 80.8.
Zitto: Viongozi wa Madhehebu ya
Dini walioingiziwa fedha na Benki ya Mkombozi ni Askofu 63
Methodius Kilaini shilingi 80.9
Zitto: Askofu Eusebius Nzigirwa shilingi milioni 40.4 na Mchungaji Alphonce Twimann Ye Simon shilingi milioni 40.4.
Zitto: Watu walienda kugawana fedha kwenye Benki tajwa wakiwa na mifuko ya rambo, sandarusi,
mabox, magunia na lumbesa TegetaEscrow
Zitto: Bilioni 73.5
zilitolewa na kugawanywa kwa watu mbalimbali kinyume cha
Sheria ya Benki Kuu na Taasisi za Fedha ya 2006
Zitto: Taarifa
ya benki (bank statements) yenye majina na akaunti zote
zilizoingiziwa fedha zimeambatishwa.
Zitto: Kamati imebaini mawasiliano kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha

Friday, 14 November 2014

Bunge likatae miswada inayominya uhuru wa habari

Dar es Salaam Muungano wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) huenda ukapata nafasi kubwa katika Uchaguzi Mkuu 2015, utafiti mpya wa Taasisi ya Twaweza umebanisha.
Utafiti huo umebainisha kuwa kuungana kwa vyama hivyo kutaongeza ushindani na kukitisha Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kina ngome imara. Ukawa inaundwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD.
Hata hivyo, takriban nusu ya Watanzania waliohojiwa katika utafiti huo uliowataka kubainisha iwapo upinzani ungesimamisha mgombea mmoja wangemchagua nani, walisema wangeichagua CCM na karibu theluthi moja wangemchagua mgombea wa upinzani iwapo watasimamisha mmoja.
Utafiti huo wa awamu ya 24 ulibainisha kuwa watu wawili kati ya 10 walikuwa tayari kumpigia mgombea badala ya chama wakati mmoja kati ya 10 akisema hajui angempigia nani iwapo upinzani ungemsimamisha mgombea mmoja 2015.
“Kundi lililosema kuwa wangemchagua mgombea wa upinzani lilipoulizwa kuwa nani anapaswa kuwa mgombea urais, watu wanne kati ya 10 (asilimia 41) walimtaja Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.
“Majina mengine ya viongozi wa upinzani yaliyopata zaidi ya asilimia 10 ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kwa asilimia 14 na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akipata asilimia kumi na moja.
Viongozi wengine wa upinzani waliotajwa kuwa wangefaa kugombea urais ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe kwa asilimia sita huku Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, wakiambulia asilimia moja kila mmoja.
Pamoja na mapendekezo hayo, bado karibu kila watu wawili kati ya 10 (asilimia 21) walioulizwa swali hilo walisema hawajui ni nani anafaa kugombea urais kupitia upinzani, jambo ambalo linaweza kubadili matokeo hayo kwa urais katika dakika za mwisho.

Bunge likatae miswada inayominya uhuru wa habari

Serikali juzi iliwasilisha bungeni Muswada wa Sheria unaotishia uhuru wa vyombo vya habari, lakini ikauchomoa baadaye jioni baada ya kugundua kwamba umestukiwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Hatua hiyo ya Serikali ya kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Takwimu unaoonekana kulenga kukwamisha vyombo vya habari katika kupata takwimu na kuzitumia katika habari na taarifa zinazotolewa kwa wananchi, imeonekana kwa wengi katika tasnia ya habari kama uthibitisho kwamba pengine Serikali haina dhamira ya kuona wananchi wanapata haki ya kupata habari.
Moja ya kifungu cha muswada huo kilicholalamikiwa na wabunge wengi ni Ibara ya 37 (4), ambacho kinaeleza kwamba wadau na vyombo vya habari vitakavyotoa takwimu bila kibali cha Ofisi ya Takwimu watakwenda jela miaka mitatu pamoja na faini ya Sh10 milioni au vyote kwa pamoja.
Inasikitisha kuona kwamba adhabu hiyo kubwa kupita kiasi imeungwa mkono na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, ambayo iliwasilisha maoni yake bungeni juzi.
Adhabu ya kosa hilo awali ilikuwa kifungo cha mwaka mmoja, lakini katika hali ya kushangaza Kamati hiyo ilipendekeza iongezwe hadi miaka mitatu eti kuzuia tabia ya baadhi ya watu kutoa takwimu za uongo na kwa makusudi ili kupotosha jamii.
Hakuna anayepinga kuwapo umuhimu wa kuipa mamlaka zaidi na kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu kutekeleza majukumu yake ya kitakwimu kwa ufanisi, wala hakuna anayepinga uanzishwaji wa mfumo thabiti wa utoaji wa takwimu unaokusudia kuboresha na kuimarisha takwimu rasmi nchini.
Jambo hilo tumekuwa tukilisisitiza mara kwa mara na kwa kweli tunadhani Serikali imechelewa sana kuanza kuchukua hatua.
Hata hivyo, tunadhani Serikali inafanya makosa kudhani kwamba uchapishaji wa takwimu zisizo sahihi unatokana na watu kutaka kupotosha jamii na kuleta machafuko.
Ni kweli kwamba katika mazingira fulani takwimu zisizo sahihi zinaweza kusababisha vurugu, lakini pia lazima tukubali kwamba Serikali yenyewe ndiyo inapaswa kubeba lawama kwa uzagaaji wa takwimu zinazokinzana na zisizo sahihi.
Tangu tupate uhuru Serikali haijawahi siyo tu kuwa na utamaduni wa kuheshimu na kutunza takwimu, bali pia kuweka mazingira ya kuboresha ukusanyaji wa takwimu kwa kuweka mfumo thabiti na kuboresha Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Hivyo kama ni kupotosha takwimu, Serikali ndiyo imekuwa mpotoshaji namba moja. Hii imetokana na kutokuwapo mfumo wa kuainisha takwimu kutoka katika wizara, taasisi za Serikali, sekta ya umma na sekta binafsi kama inavyofanyika katika nchi nyingi duniani. Kwa mfano, hatudhani kama Serikali inazo takwimu sahihi kuhusu Deni la Taifa hivi sasa.
Tunachotaka kusema hapa ni kwamba muswada huo wa Sheria ya Takwimu uliochomolewa bungeni juzi ulilenga kuvibana vyombo vya habari na kuminya uhuru na haki ya wananchi kupata habari.
Kwa miaka minane sasa, Serikali imekuwa ikisuasua kupeleka bungeni Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Habari na Vyombo vya Habari, hata baada ya kuihakikishia jumuiya ya kimataifa mara kwa mara kwamba muswada huo ungepelekwa bungeni.
Tunadhani Muswada wa Sheria wa Takwimu ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali wa kuvibana vyombo vya habari. Bunge litafanya vyema kuukataa iwapo Serikali itaurudisha ukiwa na maudhui yaleyale yaliyoufanya uchomolewe bungeni juzi.

Mbowe amtaka Kikwete avunje Baraza la Mawaziri

Kigoma. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemtaka Rais Jakaya Kikwete kulivunja Baraza la Mawaziri na kuunda jipya kutokana na tuhuma za ufisadi.
Katika taarifa yake aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari baada ya mikutano yake katika mikoa ya Magharibi alisema ni lazima hatua hiyo kuchukuliwa ili kukabiliana na mafisadi ambao hakuwataja, vinginevyo alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni anayoiongoza, itaanza maandalizi ya kuwasilisha bungeni, hoja ya kutokuwa na imani naye.
Alisema Serikali imekuwa ikishindwa kuchukua hatua za ufisadi ambazo zinawakabili watendaji wake: “Kambi ya Upinzani Bungeni inamtaka Rais Kikwete kumfukuza kazi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mawaziri wake na kuunda Serikali mpya.”
Hivi karibuni, Mbowe alitoa tuhuma nzito kuhusu ufisadi katika ujenzi na bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam akisema kuna ufisadi umefanywa na vigogo wa Serikali wakiwamo baadhi ya mawaziri.
Alisema mradi huo ulitakiwa kugharimu Sh1.2 trilioni lakini vigogo hao wakaongeza kiasi kama hicho na sasa unagharimu Sh2.4 trilioni. Alitaka kuteuliwa kwa taasisi ya kimataifa ya ukaguzi ili kufahamu thamani halisi ya ujenzi wa bomba hilo.
Alisema kutokana na ufisadi huo na mwingine katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ni dhahiri kuwa Baraza la Mawaziri limeshindwa kazi ya kumsaidia Rais.
Mbowe amnanga Zitto
Katika mkutano wa juzi mjini Kigoma, Mbowe alimzungumzia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe akisema alimsaidia kuhakikisha anashinda ubunge wa Kigoma Kaskazini mwaka 2005 lakini akakosa shukrani.
Akihutubia mamia ya wakazi wa Kata ya Kalinzi iliyopo katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, Mbowe alisema hamchukii Zitto kama baadhi ya watu wanavyofikiri, bali mbunge huyo alikiuka maadili ya chama hicho akavuliwa uongozi.
“Nilimshauri Zitto Kabwe akagombee katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, lakini akaniambia kwamba hawezi kufanya hivyo kwa sababu hana fedha, nikampa fedha za kutosha, nikampa gari Toyota Hilux la kuzungukia katika jimbo na akawa mbunge.
Alisema gari hilo hajawahi kulirudisha hadi leo na yeye hakumuuliza kwa sababu alimchukulia kama ndugu yake... “Zitto ni kama mdogo wangu, amelala na kula nyumbani kwangu, nyumba yangu ilikuwa kama yake, nashangaa anakosa shukrani.”
Alisema kabla ya kugombea alimlipia nauli kutoka Ujerumani kurudi nchini kwa ajili ya kutafuta nafasi hiyo ya ubunge, hivyo anashangaa mtu wa aina hiyo amchukie kwa lipi.
Mbowe alisema Mkoa wa Kigoma umebahatika kuwa viongozi wa upinzani wenye uwezo lakini wamekuwa wakiwasaliti wananchi wa mkoa huo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema uchaguzi wa serikali ya vijiji, mitaa na vitongoji kiwe kipimo cha kuing’oa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Aliwataka vijana kufanya uamuzi sahihi kwenye uchaguzi huo kwa kuvichagua vyama vinavyounda Ukawa kwa kuwa CCM imewatelekeza.
Zitto ajibu
Akizungumzia madai ya Mbowe, Zitto alisema ni utoto kwenda kumtangaza kwamba alimsaidia... “Yeye Mbowe anajua nilivyomsaidia pia lakini kwa kuwa nimelelewa kwa maadili mema na wazazi wangu siwezi kumtangaza. Ila muulizeni alikuwa na hali gani baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 na nilimsaidia nini?
“Nimeshangazwa na tabia hiyo ya kusimanga tena kunisimanga kwetu, nyumbani kwetu. Hata hivyo, nimepuuza maana kwa vyovyote vile aliongea bila kufikiri.
“Anasema nilitaka kusaliti chama, aseme kwa ushahidi maana kutamka tu hakuna maana kitu hata kidogo.”
Alisema kiongozi mkubwa kama Mbowe anapaswa kujadili masuala ya Taifa na namna ya kutatua changamoto si, kusema watu na kuwasimanga.
“Nimeibadilisha Kigoma na kusimamia ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege. Yeye kafanya nini Hai? Nimewezesha wakulima wangu kuwa na hifadhi ya jamii, bima ya afya na kukuza uzalishaji, yeye kafanya nini Hai?
Nimeibua hoja bungeni za maana ikiwamo kubadili sheria kwa manufaa ya nchi. Yeye kafanya nini bungeni tangu aingie, ametoa hoja gani binafsi, ametunga sheria gani binafsi?

Friday, 31 October 2014

Mkapa atoa ya moyoni rais 2015

Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, amezungumzia mbio za kuwania urais wa 2015 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), akitaja sifa za mtu anayepaswa kuteuliwa kuwa mgombea wake, ikiwamo ya kukubalika na kuuzika kwa jamii.

Amesema kukubalika na kuuzika kwa mtu katika siasa kunatokana na utendaji, haiba, wasifu na ushawishi wa mtu huyo ndani ya chama na serikalini na kwamba, umri siyo kigezo cha kuangaliwa ingawa siyo dhambi vijana wakajitokeza kujitosa katika kinyang’anyiro hicho.

Mkapa, ambaye anasifika kwa kuwa kiongozi jasiri na asiyemung’unya maneno, alisema hayo wakati akihojiwa na televisheni ya Citizen ya nchini Kenya, kwa njia ya simu.

Alikuwa akihojiwa juu ya kifo cha Rais wa Zambia, hayati Michael Satta, aliyefariki dunia, jijini London, nchini Uingereza Jumanne wiki hii.

Katika mahojiano hayo, Mkapa pia aliulizwa na mwandishi kuhusu Tanzania kutazamiwa kufanya uchaguzi mkuu mwakani huku mambo mengi yakisikika, hasa kwa wanaojitokeza kupitia CCM kutaka kuwania urais katika uchaguzi huo hadi wengine kufikia kuadhibiwa na chama.

Kabla ya kujibu, Mkapa alianza kwa kucheka na kisha akasema anachelea kupata jibu sahihi kuhusiana na swali aliloulizwa na mwandishi.


“…Ila niseme CCM ni chama kikongwe na kina hazina kubwa ya kutosha. Na Katiba ya chama chetu inaelezea kuhusu dhumuni la chama chetu, kubwa ikiwa ni kuhakikisha tunakamata dola, kuanzia serikali za mitaa mpaka serikali kuu. Sasa swali ni kwamba, dola inakamatwaje?” alihoji Mkapa.

Aliongeza: “Chama kama chama lazima muwe na mtu anayeuzika na kukubalika katika jamii kwa utendaji wake, haiba yake, wasifu wake (ndani ya chama na serikali).

“Lakini vile vile, ushawishi wake...Haya mambo ya umri na kadhalika, sisi hatukutazama wakati huo. Ila siyo dhambi vijana wakijitokeza. Maana yake hata wakati wangu, Rais wa sasa Mheshimiwa Kikwete na kina Lowassa walijitokeza. Na leo unaona Kikwete ndiye Rais.”


Alisema wakati wa utawala wake, viongozi wenzake wengi walihisi na kuamini kuwa hakuwa akimuunga mkono Rais Kikwete.

“Lakini mwandishi, nataka nikuhakikishie, hata kama mimi Ben Mkapa siko na Kikwete, mwisho wa siku wanachama ndiyo watakaosema wewe humtaki ila sisi tuachie huyo huyo...,” alisema Mkapa. 

Aliongeza: “Na hayo yalijitokeza mwaka 2005. Watu walimtaka Mheshimiwa Kikwete. Sasa mimi kuwa mwenyekiti wa chama hakunipi Mandate (mamlaka) ya kushindana na walio wengi. Na mliona (Kikwete) alishinda kwa asilimia kubwa kweli kweli”.

“Hivyo CCM ina taratibu zake na wanajua nani anafaa. Maana yake siasa hizi, tuhuma zingine za kipuuzi kweli kweli. Sasa mkiendekeza tuhuma, mwishowe mnakuta mnabaki bila chama. Na kwenye siasa mkianza kutuhumiana, hakuna wa kusimama...”

Alisema yeye binafsi, anaamini chama kitapata mtu safi, mwenye nguvu ya kukisaidia chama na serikali na kuendeleza yatakayoachwa na Rais Kikwete.

Mkapa alisema hakuna chama duniani kinachoona fulani atakivusha halafu kimwache na kusema kufanya hivyo, maana yake ni kukiua chama.

“Hivyo, hata sisi vyombo vyetu vya ndani vilikuwa vinatueleza kabisa kwamba, fulani yuko vizuri sana. Ila labda kuna aka katatizo. Sasa ako katatizo tunakafanyia kazi kwa maslahi ya chama na kwa maslahi ya huyo ajaye,” alisema Mkapa na kuongeza kuwa ana amini ndivyo ilivyo mpaka sasa.

Alisema tafiti zimefanyika na kwamba, anaamini wamesikika watu wakisema wanamtaka nani.

“Na wakati wangu mimi mgombea alikuwa ameshatungiwa nyimbo na watu mbalimbali wenye mapenzi naye. Hivyo, labda hata sasa yaweza kuwa hivyo...Waswahili walisema nyota njema huonekana asubuhi,” alisema Mkapa.

Aliongeza: “Nimalizie kama nilivyosema, ukongwe wa CCM na viongozi wake, naamini watapata mtu bora na mwenye nia njema na Taifa hili...”

Akijibu kuhusu wana CCM waliotajwa kwamba, anaamini yupo mmoja au wawili, ambao ameona wanaweza ama kufuata nyayo zake au za Mwinyi au za Mwalimu Nyerere au za Rais Kikwete, kwanza alianza kwa kucheka.

Baada ya kicheko, Mkapa alisema Tanzania kuna Kamati ya Maadili na kwamba, yeye na wenzake hivi sasa kikatiba ni wazee washauri, hivyo akasema vikao vya chama ndivyo vitakavyowaongoza na baada ya hapo, nao wanaenda na mtu huyo huyo.

Makada wa CCM waliowahi kutuhumiwa kuanza kampeni za kuwania urais mwaka 2015 kabla ya kuzuiwa na chama kupitia Kamati yake Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu kujihusisha na suala hilo kwa miezi 12, huku mienendo yao ya kisiasa ikifuatiliwa, ni pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

Wengine ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira.

Yumo pia aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pia hivi karibuni alikaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akitangaza nia yake ya kuwania urais 2015. Mwingine aliyekwisha kutangaza nia ya kuwania urais mwakani ni Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla.

KUHUSU USHIRIKIANO WA VYAMA VYA UPINZANI (UKAWA)

Akijibu swali kuhusu ushirikiano uliosainiwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD wa kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi, kuanzia ngazi ya serikali ya mtaa hadi urais kama ilivyokuwa kwa Kenya, Mkapa alisema bado hajajua
sera za vyama hivyo na namna makubaliano yao yalivyo.

Alisema pia bado hajaelewa kama inawezekana kuufananisha ushirikiano wa vyama hivyo na muungano wa Coard na Jubilee uliokuwapo nchini Kenya.

“Otherwise I'd like to wish them all the best (vinginevyo ningependa kuwatakia kila kheri),” alisema Mkapa na kumfanya mwandishi aangue kicheko.

KIFO CHA RAIS SATTA

Akimzungumzia hayati Rais Satta, Mkapa alisema hakuitwa “King Cobra” kimakosa, bali alistahili kutokana na uwezo aliokuwa nao ama wa kimaamuzi au wa kimsimamo.

“Nina hakika sana kwamba Wazambia na sisi kama Mataifa ya Afrika tutamkumbuka daima ndugu Satta. Satta daima alikuwa kwa ajili ya watu wake na Bara letu kwa jumla. Alisema na kusimamia kile alichokiamini kuwa ni cha kweli na chenye mafanikio, Satta ataendelea kuwa kiongozi mzuri daima,” alisema Mkapa.

Aliongeza: “Hivyo, maumivu yanayotukabili kwa kumpoteza Mzee Nyerere, Mzee Nkrumah, Mzee Mandela, Mzee Kenyatta ni sawa na yale yanayotukabili leo tunapomjadili Mheshimiwa Satta (Inatosha kusema kwamba tumempoteza shujaa mwingine katika Bara letu) Naitakia roho yake mapumziko ...”

Akijibu swali namna anavyoziona siasa za Afrika akiwa Rais mstaafu, Mkapa alisema ni kawaida na hana jambo kubwa la kusema japo kuna mengi yanatokea, ambayo mengine ni ya hovyo.

“Mathalan, Waafrika wazee wetu, walipigania sana ukombozi wetu. Ila nadhani wengi bado kuna watu wana matatizo na wanahitaji kukombolewa kifikra,” alisema Mkapa.

Aliongeza: “Maana yake kuna wenzetu wanatumika pasipo kujua na kusababishia nchi zao kuingia katika matatizo, kama vita na wengi wao wameanza kujuta”.
“Hivyo, ni lazma ifikie mahali watu waweze kujitambua na kujua ni yepi malengo mema kwa Bara letu ni yepi tunashinikizwa...” aliongeza kusema Mkapa.

Lowassa amuombea radhi Sitta kwa Kanisa

Wakati Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba (MBK) ikitarajia kuingia katika hatua ya kura ya maoni mwakani, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, ameibuka na kuliomba radhi Kanisa Katoliki kufuatia mgongano iliyojitokeza kati ya kanisa hilo na baadhi ya viongozi serikali na wa Bunge hilo.

Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, aliomba msamaha huo wakati akitoa salamu zake katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa Katoliki Jimbo la Mahenge, mkoani Morogoro.

Alisema Kanisa Katoliki lina mchango mkubwa katika kudumisha amani na mshikamano nchini, hivyo mambo yaliyojitokeza yanapaswa kusamehewa.

“Najua hivi karibuni tumewaudhi, lakini mimi naomba mtusamehe bure tu, kama vile mzazi anavyomsamehe mtoto wake anapokosea,” alisema Lowassa na kuongeza kuwa Kanisa Katoliki ni muhimu katika maendeleo ya nchi.

Ingawa Lowassa hakueleza kwa undani tofauti zilizojitokeza kati ya Kanisa hilo na baadhi ya viongozi wa serikali, lakini  wakati BMK likiendelea, taasisi za dini zilisambaza waraka uliosainiwa na viongozi wake ukilikosoa Bunge hilo kwa mambo mbalimbali ikiwamo kuendelea kujadili rasimu bila maridhiano kutokana na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia.

Kadhalika, viongozi wa madhahebu hayo ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Baraza la Kikiristo Tanzania (CCT) na Makanisa ya Pentekoste Tanzania (PCT), walilikosoa BMK kwa kupuuza maoni ya wananchi yaliyokuwa katika Rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Waraka huo ulisababisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kujiweka katika wakati mgumu kwa kuzua mgogoro dhidi ya viongozi wa dini ya Kikristo, baada ya kuita waraka huo kuwa ni wa kipuuzi na wa hovyo hovyo.

Sitta ambaye alitoa kauli hiyo Oktoba Mosi mwaka huu, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa waraka wa maaskofu una lugha ya Ukawa, ingawa maaskofu kwa upande wao waliueleza kuwa ni waraka wa kinabii, kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi.

Sitta alitoa kauli ya kuuponda waraka huo bungeni alipokuwa akielezea mwenendo wa upigaji kura za kupitisha ibara na sura za rasimu ya katiba iliyopendekezwa kabla ya upigaji wa kura na wakati wa kutangaza matokeo, akisema watu wa Mungu kama maaskofu hawawezi kutoa waraka kama huo na kudai kuwa amekuwa akituhumiwa kwenye mitandao kwamba anadharau maaskofu.

“Nimalizie na viongozi wangu wa kiroho…mababa zangu maaskofu, natuhumiwa sana kwenye mablog kwamba nadharau maaskofu. Wakiwa na matendo kama hayo hao baadhi ya maaskofu itabidi tuendelee kuwadharau,” alisema na kuongeza:

“Ninao waraka huu ambao umelazimishwa kutumwa katika makanisa. Sioni utukufu wa Ukristo katika waraka huo. Huu waraka unamwamuru Rais airudishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba.”

 Kuna Ukristo hapa?” alihoji na kuendelea: “Waraka huu unamlazimisha Rais asitishe mchakato wa Bunge Maalum…tangu lini watu wa kiroho wanatoa maagizo ya kisiasa? Hii sio haki hata kidogo…kuna Ukristo hapa? Waraka una lugha za wale Ukawa tuliowazoea.”

“Hivi kweli maaskofu wa Kikristo wanaweza kusema kwamba Wizara ya Katiba na Sheria irudishe tovuti ya Tume ya Jaji Warioba na kuirejeshea nyaraka zake zote ili wananchi wasome na kujifunza?” alihoji Sitta.

“Kwamba maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauriwa na chama tawala, hivyo basi Bunge la Katiba lijadili na kuboresha tu rasimu ya katiba na si kubadilisha,” alisema Sitta.

“Waraka huu kwa shinikizo la maaskofu umesambazwa kwenye makanisa na kusomwa. Mimi nasema kama Mkristo, tukianza kuruhusu nchi yetu kutoa nyaraka hizi za kisiasa zisomwe makanisani kwa kudai huo ni msimamo wa maaskofu, basi nchi hii tutaipeleka kubaya.

“Na mini kama mtu mzima lazima nionye kuhusu tabia hii, ukizingatia nchi hii haina dini, hawa baadhi ya maaskofu ambao walikusanywa Dar es Salaam na makundi yale yale yanayohusishwa na Ukawa, kama wao ni wanachama wa siri wa vyama vya siasa vinavyochukia CCM wajitokeze waziwazi,” alisema Sitta.

Sitta aliendelea kunukuu waraka huo kwamba kuna askofu mmoja ameapa kwamba atawaelimisha waumini wake ili siku za usoni wawashughulikie viongozi kama mimi (Sitta). Nasema aendelee, lakini Mungu anaona yote yaliyo moyoni mwetu.”

Baada ya Sitta kutoa kauli hiyo, Askofu wa Jimbo la Katoliki la Bunda, Mhashamu Renatus Nkwande, alisema matamshi ya Sitta yanaonyesha anavyohangaika kualalisha kilicho haramu.

Alisema kitendo cha Sitta kuendesha BMK kwa kukejeli wajumbe wenzake walioondoka bungeni (Ukawa) na wajumbe walioandaa rasimu ya pili kwenye Tume ya Katiba Mpya chini ya Jaji Joseph Warioba, ni jambo la aibu ambalo halivumiliki, na ndiyo maana walitoa waraka wa kutokubaliana nacho.

“Kwa kweli Sitta ametutukana, ametafuta ubaya kwa viongozi wa dini, kwa kuwa tumesema ukweli ? Sisi tulikuwa tunatimiza wajibu wetu kwa Wakristo …tulizungumza kutokana na hitaji la wakati, na ulikuwa waraka wa unabii,” alisema.

Viongozi wengine wa kanisa Katoliki waliojibu kauli za Sitta ni Makamu Mwenyekiti wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi na Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini, ambaye alinukuliwa akisema kuwa Sitta amelewa madaraka.

JK: Watendaji wakuu wananikwamisha

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amewatuhumu baadhi ya watendaji wa serikali yake kuwa ni kikwazo katika kufanikisha masuala mbalimbali ya maendeleo kutokana na urasimu usiokuwa wa lazima katika kutoa huduma kwa wananchi.
Akifungua kongamano la miaka 10 ya Tume ya Utumishi wa Umma Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alikemea na kulaumu tabia ya baadhi ya watendaji hao wa Serikali ambao wamekuwa wakikwamisha kwa makusudi kasi ya viongozi wa kisiasa ya kuleta maendeleo.
“Katika utendaji wa baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali limekuwa ni tatizo na wamekuwa wakikwamisha sana kasi ya utekelezaji wa haraka wa malengo ya kisiasa,” alisema.
“Mara nyingine, viongozi wa kisiasa wamekuwa mbele kimtazamo kuliko watumishi wa umma, hili limekuwa tatizo sana katika utekelezaji wa malengo kwa haraka,” alisema Kikwete.
Alisema kumekuwa na malalamiko kwa makatibu wakuu wa wizara kutoka kwa wawekezaji ambao huwachelewesha kwa makusudi kwa visingizio vya kufuata utaratibu.
Alisema katika kufuatilia, amekuwa akilazimika kuingilia utendaji wa baadhi ya wizara ili kuhakikisha mambo yanakwenda na mara nyingine urasimu huo umekuwa ukifanywa kwa makusudi ili kuwachosha wawekezaji na ‘kuwatoa upepo’ kwa manufaa binafsi.
“Haya ni malalamiko makubwa sana na yanatoa picha mbaya kwa nchi yetu…watendaji wa namna hii ni lazima wabadilike, ninahitaji kuona mabadiliko makubwa kwa kupitia Tume ya Utumishi ambayo inatakiwa kukaa na hawa watumishi na kuwapa mafunzo ya kiutendaji yanayoendana na mahitaji ya sasa,” alisema.
Abeza zawadi ya uprofesa
Akizungumzia utaratibu wa upandishwaji vyeo, Rais Kikwete alisema ni muhimu weledi ukazingatiwa na utaratibu uliowekwa ukaheshimiwa, kwamba lazima wafanyakazi wapandishwe vyeo na madaraja ndani ya kipindi kilichowekwa, ambacho ni miaka mitatu.
Alisema kumekuwa na malalamiko kwa wafanyakazi wengi wa Serikali kutopandishwa vyeo kwa muda mrefu na hata wanapopandishwa vyeo mabadiliko ya mishahara kuendana na vyeo na madaraja mapya hayafanyiki kwa wakati.
Alieleza kwamba utaratibu unaotumika katika vyuo vikuu wa namna ya kuwapata wahadhiri wasaidizi, wahadhiri, maprofesa ni wa wazi na ni mfano wa kuigwa kutokana na namna unavyofanyika, kwa kutoa mafunzo kisha kuyathibitisha na kumpandisha mhusika daraja.
“Vyuo vikuu wana ngazi wanazotakiwa kuzipitia na mafunzo maalumu hadi mtu anakuwa profesa. Siyo honorary professor (uprofesa wa heshima) niliopewa mimi nilipokwenda China…walinishtukiza. Nilifika pale wakanipiga na uprofesa, nikasema haya sasa makubwa! (kicheko),” alisema.
Alisema matatizo ya upandishwaji vyeo yasipotatuliwa kwa wakati ni tatizo kubwa kwa Serikali hasa unapokutana na vyama vya wafanyakazi vyenye nguvu kama Chama cha Walimu na wanapofikia hatua ya kusema wanagoma, unalazimika kuwaangukia.
Alisema suala la mtumishi kupandishwa cheo ni haki yake ya msingi kazini hivyo hatarajii kusikia matatizo ya malalamiko ya watumishi kutopanda vyeo kwa wakati.

Ukawa na dhana ya nguvu ya mnyonge au ‘zamu yetu kula’

Dar es Salaam. Kwa jumla, kuungana ni jambo jema kwani muungano huongeza nguvu. Muungano ni silaha ya mnyonge dhidi ya mwenye nguvu.
Ni kwa sababu hii, tumekuwa tukipigania umoja wa Afrika ili kujenga nguvu ya pamoja dhidi ya mabeberu wa mataifa ya Magharibi tukiamini kwamba bila nguvu moja mataifa ya Afrika hayataweza kuukabili ubeberu wa mataifa haya.
Tunao msemo maarufu usemao nguvu ya mnyonge ni umoja na hivi ndivyo waasisi wa mataifa ya Afrika walivyofanya katika kumfukuza mkoloni.
Bila kujali tofauti zao za kikabila na vinginevyo, wananchi wa Afrika waliunganisha nguvu na hatimaye pamoja na silaha zao duni, wakafanikiwa kumfukuza mkoloni katika ardhi ya Afrika.
Katika uwanja wa siasa, vyama vya siasa huungana kwa sababu mbalimbali lakini sababu tatu ni za msingi zaidi. Mosi, huungana pale ambako hakuna chama kinaibuka na ushindi wa moja kwa moja katika uchaguzi ulio na ushindani mkali.
Katika mazingira haya, inakuwa hakuna chama kinachoweza kuunda serikali imara peke yake bila kushirikisha kingine kwa sababu hakitaweza kupitisha sera au sheria yoyote bungeni.
Hivi ndivyo vyama vya Conservatives na Liberal Democrats vilivyoungana huko Uingereza baada ya vyama vikuu nchini humo vya Labour na Conservatives kushindwa kupata ushindi ambao ungekiwezesha chama kimojawapo kuunda serikali na kupitisha sera bungeni bila msukosuko mkubwa.
Hivi ni vyama ambavyo vina itikadi na msimamo tofauti kabisa kifalsafa na ilibidi viongozi wake wakae saa nyingi kukubaliana programu ya kutekeleza kabla hawajakubaliana kugawana nafasi za uongozi.
Kiongozi wa Liberal Democrats, Nick Cleggy alimshinikiza David Cameroon akubaliane na masharti ya kulegeza misimamo mikali ya chama chake kuhusu sera ya uhamiaji na hifadhi ya jamii kabla hajakubali kuingia naye ubia kuunda serikali.
Cameron amekiri mara kadhaa kwamba alilazimika kulegeza msimamo kuhusu sera mama za Conservatives ili kufanikisha kuwashawishi Liberal Democrats kuunda nao serikali vinginevyo Nick Cleggy angeunda serikali na Gordon Brown wa chama cha Labour.
Ni katika mazingira ya chama kimoja kushindwa kupata ushindi wa wazi ambayo yalivilazimisha vyama hasimu vya CUF na CCM kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar.
Pamoja na kwamba SUK iliundwa kama njia sahihi ya kuepusha shari na vita visiwani, msingi wa serikali hiyo ni ukweli kwamba hakuna chama chochote kati ya hivi viwili chenye uwezo wa kuunda serikali imara kwa sababu ushindi wa chama chochote huwa ni mwembamba. Hata hivyo, hatujui ni kwa kiwango gani vyama vya CUF na CCM huko Zanzibar vilikubaliana kutekeleza programu ya pamoja inayotokana na sera za vyama hivyo viwili.
Sababu ya pili ya vyama kuungana ni kuunganisha nguvu katika jitihada za kumwondoa adui anayefanana.
Kwa mfano, huko Zanzibar kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964, vyama kadhaa viliungana katika jitihada za kuuondoa utawala wa Sultani uliokuwa unaendeshwa kibaguzi. Kwa hiyo, adui hapa alikuwa Sultani na ubaguzi wake wa rangi.
Sababu ya tatu ni pale vyama vinapounganisha nguvu ili kushinda uchaguzi kwa kutambua kwamba vikiingia kwenye uchaguzi kimoja, kimoja havitaweza kushinda kutokana na nguvu kubwa aliyonayo mshindani wao.
Hata hivyo, kushinda uchaguzi hakuwezi kutokana na kuunganisha nguvu ya kiuongozi pekee. Ni lazima kuunganisha pia nguvu ya kiitikadi, kifalsafa na kisera ili kuweza kujipambanua kwa wananchi.
Muungano wa kisera ni muhimu ili kuweza kutabirika tabia za wagombea watakapokuwa madarakani. Aidha, ni programu ya kisera inayoweza kuongoza kuchagua mgombea anayefaa zaidi kushika usukani wa utekelezaji wake baadaye.
Muungano wa vyama vinavyounda Ukawa umepokewa kwa shangwe kubwa. Furaha hii inatokana na msingi nilioueleza hapo awali kwamba wanyonge wakiungana hupata nguvu ya ajabu hata ya kuweza kuangusha milima.
Kwa hiyo, watu ambao wamekuwa wakisubiri utawala wa CCM kuanguka wanaamini kwamba kwa muungano huu angalau vyama vya upinzani vitafuta unyonge.
Nami naungana na Watanzania wengine kuwapongeza viongozi wa vyama ya Chadema, CUF, NCCR na NLD kwa ujasiri na uthubutu waliouchukua katika kujaribu kushirikiana katika chaguzi mbalimbali zijazo.
Lakini tunapowapongeza Ukawa, ni vizuri kutambua kwamba kuunganisha nguvu kama walivyofanya ni hatua moja tu inayopaswa kuanzisha hatua nyingi huko mbele. Hatua muhimu inayofuata sasa ni kujipambanua kwa wananchi kiitikadi, kifalsafa na kisera.
Kwa bahati viongozi wa sasa wa vyama vilivyoungana siyo watu wanaoamini katika mambo ya itikadi na falsafa.
Hawa ni viongozi ambao huitwa ‘wayakinifu’ (pragamatists). Myakinifu ni kiongozi anayeamini katika kinachowezekana leo na haongozwi na falsafa bayana ya kisiasa.
Kwa hiyo kiongozi yakinifu atambeba yeyote anayeona anafaa na huwezi kumuweka katika mrengo wowote kiitikadi. Kimsingi, hii ndiyo aina ya viongozi tulionao sasa tangu Mwalimu Julius Nyerere alipoondoka.
Ndiyo maana tumekuwa Taifa ambalo si la kijamaa, wala kiliberali wala kibepari. Tupotupo tu maadamu siku zinakwenda.
Pamoja na uyakinifu wao, bado naamini kwamba Ukawa watahitaji programu ya pamoja ya kisera. Hii ni hatua muhimu ili kutoa nafasi kwa wananchi kupima aina ya serikali watakayounda kama watashinda katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Bila msimamo yakinifu wa kisera, ni rahisi kutofautiana kwa sababu ya kukosa msingi wa kugawana madaraka. Bila sera yakinifu, utakapofika wakati wa kugawana nafasi za kugombea na hatimaye katika kuunda Serikali watalazimika kuzingatia sifa za kuchagulika na umaarufu badala ya sifa za kiuwezo.
Nakumbuka mwaka 2005 palipokuwa na jitihada za kuunda ushirikiano kama huu wa sasa, nilipewa jukumu la kufanya utafiti kujua nani alikuwa anakubalika zaidi katika Jimbo la Ubungo kati ya mgombea wa Chadema (John Mnyika) na mgombea wa CUF (marehemu mama Minja).
Niliandaa hojaji na nikaligawa katika kata zote za Jimbo la Ubungo kwa kutumia sampuli iliyopatikana kwa njia ya bahati nasibu. Matokeo yalionyesha kwamba Mnyika alikuwa anakubalika kwa mbali dhidi ya wagombea wengine wa upinzani.
Hata hivyo, katika kikao cha kujadili matokeo hayo, wawakilishi wa CUF waliyakataa na kunituhumu kwamba nilikuwa napendelea chama changu na huo ndiyo ukawa mwanzo wa ushirikiano kusuasua na hatimaye kusambaratika kabisa kabla ya kampeni kuanza.
Yote hii ni kwa sababu tuliwekeza zaidi kwenye kugawana wagombea lakini hatukuwekeza kabisa katika ushirikiano wa kisera.
Ninachojaribu kusema hapa ni kwamba, muungano wowote endelevu wa vyama vya siasa Tanzania, lazima uwe wa kuunganisha nguvu za wanyonge dhidi ya mabavu ya chama dola cha CCM.
Muungano wa namna hii lazima uwaunganishe kisera Watanzania na ndiyo unaopaswa kuwa msingi wa kugawana vyeo.

Lipumba: Kwanza CCM ing’oke, ruzuku baadaye

Dar es Salaam. Wakati Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi akisema suala la ruzuku na viti maalumu ni changamoto kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema hicho si kipaumbele.
“Tunachokitaka ni kuunganisha nguvu zetu ili kuhakikisha tunaing’oa CCM madarakani kwanza, masuala mengine kuhusu ruzuku tutaweka utaratibu maalumu baadaye,” alisema.
Profesa Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alisema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akiwaeleza waandishi wa habari maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lililokutana Jumatatu na Jumanne iliyopita.
“Wenzetu Kenya waliweza kuungana na kuhakikisha wanaking’oa chama tawala madarakani, lakini sasa kwa hapa mkiungana na kuwa chama kimoja ni lazima msajili chama chenu, sasa tunachokitaka ni kushirikiana tu kwanza,’’ alisema.
Alisema suala la ruzuku na uteuzi wa viti maalumu siyo lengo kuu la Ukawa inayoundwa na vyama vinne; CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD kwa kuwa linajadilika. Alisema jambo la msingi hivi sasa ni ushirikiano wa amani.
Alisema kinachotakiwa kwa viongozi wa Ukawa ni kuaminiana kwanza ili kulinda muungano huo ambao alisema umeshaanza kukitikisa chama tawala, CCM.
Maazimio ya Baraza Kuu
Alisema Baraza hilo lilisisitiza umuhimu wa kuaminiana miongoni mwa vyama washirika katika ngazi zote ili kudumisha umoja huo na kufikia lengo la kuitoa CCM madarakani.
“Baraza limetaka uwepo utaratibu mzuri na wa wazi utakaoonyesha mambo ya msingi ambayo vyama vinavyounda Ukawa vimekubaliana. Utaratibu huu uwafikie viongozi wa ngazi zote za chama ili kuhakikisha jukwaa la Ukawa linatumika kwa lengo na dhamira iliyopo ndani ya hati ya makubaliano ambayo ni kuing’oa CCM madarakani,” alisema.
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa Profesa Lipumba alisema Baraza limetaka sheria irekebishwe ili uchaguzi wa diwani ufanyike pamoja na wa viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji kwa wakati mmoja, kwa vile diwani ndiye kiongozi mkuu wa kuchaguliwa wa kata.
Baraza hilo pia limetaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iratibu na kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na utengenezwe utaratibu ambao utaifanya Tume hiyo kuwa huru kuwezesha chaguzi zote zijazo kufanyika kwa uhuru na haki.
“Taarifa za Tume zilieleza kuwa itaandikisha wapigakura mpaka kwenye ngazi ya vijiji na vitongoji, kwa hiyo uchaguzi wa Serikali za Mitaa usubiri mpaka daftari la kudumu la wapigakura likamilike na ndilo litumiwe kwenye uchaguzi huo,” alisema.
Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa, Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu la CUF, limesikitishwa kwa kiasi kikubwa na kitendo cha kupitishwa na kutangazwa kwa katiba hiyo na Bunge la Katiba lililoongozwa na Samuel Sitta akisema halikuzingatia sheria na taratibu za mabunge ya Jumuiya ya Madola.
“Ni ukweli usiofichika kwamba mchakato mzima wa kupitisha katiba haukuwa na mwafaka wa kisiasa, kanuni za uendeshaji wa bunge hilo zilikiukwa na Katiba yote inayopendekezwa haikupigiwa kura ya mwisho,” alisema
Profesa Lipumba alisema, katika vikao vya ushauriano na viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Rais Jakaya Kikwete alikubaliana na viongozi hao kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya, hususan kura ya maoni uahirishwe mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu 2015.
“Mwanasheria wa Serikali alitangaza kura ya maoni Machi 30, Rais akiwa China alisema Aprili, yaani tayari tarehe imeshatangazwa kabla hata ya daftari la wapigakura kukamilishwa,” alisema.
Alisema baraza hilo pia limesikitishwa na utaratibu unaofanywa na NEC juu ya uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapigakura akisema hadi sasa hatua za uandikishaji hazipo wazi na wadau wengi hawana taarifa za kutosha juu ya nini kinaendelea.
Alisema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2012, zinaonyesha kuwa kuna vijana zaidi ya milioni 4.6 ambao watafikisha umri wa kuwa wapigakura kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 lakini bado hawajapewa fursa ya kuandikishwa huku wananchi wengi wakiwa wameshapoteza vitambulisho vya kupigia kura.
Alisema Juni, 19 mwaka huu, Nec, ilitangaza kufuta matumizi ya vitambulisho vya kupigia kura vya sasa na badala yake itatumia teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR), ikiwa ni maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura na kwamba Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva alinukuliwa akisema katika Kura ya Maoni ya Katiba na Uchaguzi Mkuu, mpigakura atatumia kitambulisho kipya baada ya kuandikishwa upya katika mfumo huo na si vinginevyo.
Pia alisema Baraza Kuu linalaani vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na sheria vinavyoendelea kufanywa na Serikali kwa kulitumia Jeshi la Polisi.
Alitoa mfano wa masheikh waliokamatwa Zanzibar na kuhamishiwa Dar es Salaam na kufunguliwa kesi akisema walijitokeza mbele ya Mahakama na kusema waziwazi kwamba wamefanyiwa mateso na vitendo vya kinyama lakini hakuna hatua zilizochukuliwa ikiwamo kupelekwa hospitali.
Kadhalika, alisema baraza hilo limepokea kwa mshangao taarifa za utoaji wa uraia unaofanywa na Serikali kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi. Alisema uamuzi wa kuwapa uraia wakimbizi katika majimbo yanayoongozwa na wabunge wa vyama vya upinzani ni mbinu ya kudhoofisha upinzani kwa kuwa wakimbizi wanaopewa uraia wanahamasishwa kuwa wachague chama tawala.
Kuhusu ardhi alisema: “Pamoja na Tanzania kuwa na ardhi ya kutosha kwa raia wake, ugawaji wa mapande makubwa ya ardhi kwa wawekezaji yataleta mtafaruku wa uvunjifu wa amani na kuwafanya raia wazawa kuwa maskini wa kudumu,’’ alisema Profesa Lipumba.
Kuhusu maradhi hatari ya ebola, Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu limeitaka Serikali kuwa makini ili usiingie nchini akisema limesikitishwa na taarifa ya kwamba mpaka sasa nchi haina vifaa vya kuthibitisha kuwapo kwa vimelea vya ebola.