Dar/Dodoma. Serikali imeumbuliwa bungeni
ikidaiwa kuwasilisha taarifa za uongo kupitia Hotuba ya Ofisi ya Waziri
Mkuu kuhusu ugawaji wa madawati yaliyonunuliwa kwa ‘chenji ya rada’.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu
alitoa tuhuma hizo jana, wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya
Serikali ya mwaka 2013/2014, akisema Serikali imewadanganya wabunge kwa
kuwa hakuna kitu kilichofanyika.
Alisema katika majibu ya Serikali kumekuwa na
mkanganyiko mkubwa kwa kuwa imetangaza kununua madawati 93,740 na
kuyagawa katika halmashauri mbalimbali nchini wakati siyo kweli.
Alisema kwa mtindo huo, Serikali imelidanganya Bunge pamoja na Watanzania kwa kuwa imetangaza madawati hewa ambayo hayapo.
“Wabunge kama kweli mnatimiza majukumu yenu na
hampo hapa kwa masilahi yenu tu, hebu hojini halmashauri zetu
zimepelekewa haya madawati 93,000 yanayozungumzwa humu au mnapiga makofi
tu? Serikali inadanganya tunatakiwa tuihoji tuiwajibishe,” alisema.
Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, alitoa mfano wa mgawo huo kwenye Halmashauri ya Ikungi, Singida
kwamba ilitangazwa kupelekewa madawati 508 lakini amekwenda jimboni na
hakukuta dawati hata moja.
Alisema uchunguzi wake umebaini kuwa hata katika wilaya mbalimbali ikiwamo ya Iringa, hakuna kitu kama hicho.
“Jana sikuwa hapa bungeni nilikwenda kwenye
halmashauri yangu, hakuna dawati hata moja. Hata Halmashauri ya Iringa
kwa Mchungaji Msigwa (Peter) hapa ananiambia hakuna dawati hata moja,
mnatudanganya ili iweje?” Aliwashauri wabunge wengine kufanya utafiti
katika maeneo yao iwapo kuna madawati ambayo yamepelekwa kutokana na
fedha zilizorejeshwa na Serikali kama chenji ya rada.
Lissu alisema ni maneno matupu ambayo yamekuwa
yakiwahadaa wabunge na kuwafanya wasahau wajibu wao wa kuisimamia
Serikali na kujikuta ni washangiliaji wakati wote. Lissu alisema kinyume
na taarifa hizo za Waziri Mkuu, Bunge jana lilikuwa limeelezwa na Naibu
Waziri (hakumtaja) kuwa madawati hayo hayajagawanywa.
Katika kipindi cha maswali na majibu, Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Kassim Majaliwa akijibu swali
la nyongeza la Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe - CUF), kuhusu madawati hayo,
alisema kwa kuwa madawati hayo bado yanagawanywa, watakaa na kuangalia
utaratibu mzuri wa kuyafikisha Zanzibar.
Lissu pia alisema fedha ambazo zilitajwa na Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo kuwa ni pato la
Watanzania ni uongo kwa kuwa ni mali ya wamiliki wa migodi.
Alisema takwimu za waziri zimesababisha Watanzania
kuamini kuwa wameingiza fedha nyingi ilihali kiasi kilichoingia
hakifikii hata asilimia 10 ya pato la wawekezaji.
Awali, akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhanga
Mpina alielezea hofu yake kuhusu maendeleo ya mifuko ya hifadhi ya jamii
kwamba inaweza kufa kutokana na Serikali kutokuilipa madeni yake.
“Mifuko ya hifadhi ya jamii itakufa kutokana na
kuidai Serikali madeni mengi makubwa. Kuna haja ya kuangalia jinsi
ambavyo tunaweza kuishauri Serikali kwa suala hili,” alisema Mpina.
Mbunge huyo alielezea kukerwa kwake na matumizi ya
Dola ya Marekani badala ya Shilingi katika malipo mbalimbali, jambo
ambalo linazidi kushusha thamani ya Shilingi.
“Watu wanakuja na Dola wanatumia na wanaondoka
nazo bila hata kuzibadilisha, basi ni vyema kama tunaona fedha yetu
haifai tuiondoe tutumie hizo Dola,” alisema Mpina.
Aliikosoa Serikali akisema haijawahi kufanya
mdahalo wa kina kujadili jinsi matumizi ya Dola yanavyoiathiri Shilingi
ya Tanzania.
Majaliwa
Hata hivyo, Majaliwa akizungumza na gazeti hili
jana jioni alisema inawezekana Lissu hakumwelewa au amefanya makusudi
kupotosha kile ambacho yeye alikizungumza ili kujipatia sifa kwa umma.
“Nilichokisema hakitofautiani na kile kilichomo
kwenye jedwali la hotuba ya Waziri Mkuu, nimesema kwamba hadi sasa
tunaendelea kugawa madawati ya plastiki katika halmashauri za wilaya 41
na hivi ninavyozungumza halmashauri ya mwisho inayopelekewa madawati leo
(jana) ni Temeke,” alisema Majaliwa na kuongeza:
“Kwa upande wa madawati ya mbao, ambayo yeye
(Lissu) ameyaita ya chuma, nayo yanaanza kusambazwa katika halmashauri
zilizobaki 123, na kazi hiyo itaendelea na ifikapo Agosti 15 mwaka huu
kila halmashauri itakuwa imepata mgawo wake.”
Alisema tayari Serikali imetangaza zabuni ya
utengenezaji wa madawati awamu ya pili ambayo itafunguliwa Jumatatu
ijayo na kwamba baada ya taratibu kukamilika utengenezaji huo utaanza na
kukamilika katika muda wa miezi miwili.
Alisema katika awamu ya kwanza, kila halmashauri inatarajiwa kupata madawati 756, sawa na madawati 123, 984.
“Kama unakumbuka awali tulipanga madawati haya
yapelekwe kwenye wilaya kama sita nadhani, lakini wabunge walishauri
kwamba kila wilaya inufaike na ndicho tulichokifanya,” alisema.