Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu imeandika historia katika
nchi yetu, baada ya kutoa hukumu iliyohitimisha safari ndefu ya
wananchi kutaka wagombea binafsi waruhusiwe katika chaguzi za serikali
za mitaa, ubunge na urais. Tunasema mahakama hiyo imeandika historia
kutokana na suala hilo kukataliwa na Serikali yapata zaidi ya miongo
minne sasa, hata pale mahakama za juu nchini zilipotamka kwamba kuwapo
kwa mgombea binafsi ni haki ya kila raia kikatiba.
Pengine wananchi wengi hawajui kwamba nchi yetu
iliwahi kuwa na wagombea binafsi. Katika Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi wa
mwaka 1960, chama tawala cha TANU kilipoteza kiti cha ubunge katika
Jimbo la Mbulu, baada ya Herman Elias Sarwatt aliyegombea kiti hicho
kama mgombea binafsi kushinda.
Ushindi huo na mwingine wa baadhi ya wagombea wa
vyama vya upinzani ulikishtua chama hicho tawala na ndipo kilipotumia
wingi wa wabunge wake bungeni kubadilisha Katiba na kufuta vyama vya
upinzani na wagombea binafsi, hivyo kuifanya Tanganyika nchi ya utawala
wa chama kimoja.
Hivyo kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka
1992 kuliibua suala la mgombea binafsi. Serikali iliendelea kumkataa
mgombea binafsi, ikisema lazima kila mgombea awe mwanachama wa chama cha
siasa. Ndipo mwaka 1993 Mchungaji Christopher Mtikila alipofungua kesi
ya kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma iliyosikilizwa na Jaji
Kawha Lugakingira ambaye alikubaliana na hoja zake, kwamba kugombea kama
mtu binafsi ni haki ya kila raia kwa mujibu wa Katiba, kwa maana ya
haki ya kuchagua viongozi na haki ya kugombea uongozi.
Lakini katika hali ya kushangaza mwaka 1994,
Serikali kwa kutumia wingi wa wabunge wake bungeni ilihakikisha chombo
hicho kinafanya mabadiliko ya 11 ya Katiba katika Ibara ya 34 kwa kuzuia
wagombea binafsi. Ndipo mwaka 2005, Mchungaji Mtikila alifungua kesi
Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam akipinga marekebisho hayo ya
Katiba. Hatimaye, jopo la majaji watatu chini ya Jaji Kiongozi, Amiri
Manento lilikubali hoja za Mchungaji Mtikila na kuruhusu mgombea
binafsi.
Iliwashangaza wengi mwaka 2010 kuona Serikali
ikikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa. Majaji saba wa mahakama hiyo
walisikiliza kesi hiyo chini ya aliyekuwa Jaji Mkuu Augustino Ramadhani.
Serikali ilidai katika rufaa yake kwamba hakuna mahakama yoyote nchini
yenye uwezo kisheria kusikiliza kesi inayotaka mgombea binafsi na kwamba
mahakama za chini zilijipachika madaraka ya kibunge ya kutunga sheria
badala ya kuzitafsiri. Katika hukumu iliyokosolewa na wengi, mahakama
hiyo, pamoja na kukubaliana na hoja ya haki ya kila raia kuchagua au
kuchaguliwa bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa, ilisema siyo jukumu
la mahakama kujielekeza katika masuala ya kisiasa.
Ndipo Mchungaji Mtikila alikata rufaa katika
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu iliyoko Arusha na Juni mwaka
jana, mahakama hiyo ilitoa ushindi kwa mrufani na kuitaka Serikali ya
Tanzania kutoa taarifa ndani ya miezi sita kuhusu namna inavyotekeleza
hukumu hiyo.
Ni jambo jema sasa kwamba Serikali imesema imo
katika mchakato wa kisheria utakaoruhusu mgombea binafsi. Sisi tumetiwa
moyo na hali hiyo na tunaitaka Serikali itambue kwamba suala hilo halina
mjadala tena.








