*Awataka wafanye mchakato wao bila kuvuruga chama
*Awashushua wanaokacha majimbo na kuwanunia wenzao
*Wabunge wamtaka awang’oe mawaziri watatu ‘mizigo’MWENYEKITI
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amefungua milango kwa
kuwataka baadhi ya watu ndani ya chama hicho wanaowania urais mwaka
2015 kuendelea na mchakato huo.
Rais Kikwete amewatahadharisha
watu hao kuendesha kampeni zao kwa ustaarabu pasipo kuibua chuki wala
kujenga makundi ambayo alisema ni hatari kwa kuwa yanaweza kukipasua
chama. Rais Kikwete aliyasema hayo katika mkutano ndani wa wabunge wa
chama hicho uliofanyika jana katika ukumbi wa CCM (white house) mkoani
hapa.
Mkutano huo ambao ulianza saa 3.00 asubuhi ulilenga
kujadili masuala mbalimbali ya taifa ikiwamo utekelezaki wa ilani ya
uchaguzi ya chama hicho katika majimbo na ahadi mbalimbali za viongozi
wa taifa.
Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya ukumbi huo kilieleza kuwa Rais
Kikwete aliwataka wanachama wenye nia ya kugombea urais kuwa na
tahadhari na watu aliowaita vishoka wa siasa.
Kwa mujibu wa
chanzo hicho, Rais Kikwete alisema watu wa aina hiyo wana tabia ya kula
huku na huku kwa kujiingiza katika kambi zaidi ya moja.
“Tuangalie
makundi ya urais 2015 yasishambuliane kwa kuvunja chama, wenye nia hiyo
ya kugombea waendelee na mikakati yao kujenga chuki kwa makundi
mengine.
“Katika hatua hiyo, pia mkumbuke kuwa katika kambi hizo
za urais zinatakiwa kujitizama wao na wafuasi wao maana wafuasi wengine
hawaaminiki, ” alisema Rais Kikwete.
Kwa mujibu wa chanzo hicho,
miongoni mwa ajenda alizokuwa nazo Rais Kikwete ni pamoja na suala la
urais na utendaji wa wabunge majimboni.
Rais Kikwete aliwataka
wabunge wa chama hicho kubadili mwenendo wa kuyatelekeza majimbo yao na
badala yake akawahimiza kujenga tabia ya kutembelea majimbo yao mara kwa
mara.
“Hili JK amelisemea kwa ukali kwamba tabia ya baadhi ya
wabunge kuhamia mijini na kutelekeza majimbo yao ni hatari kwani mwisho
wa siku wananchi watawanyima kura na kuzipeleka upinzani.
“Pia
alikemea tabia ya baadhi ya wabunge kununa na kuwachukia watu wengine
wenye nia ya kugombea katika majimbo yao. Akasema mbunge asiyetimiza
wajibu wake kwa wananchi wake na bungeni ni vigumu kubaki.
“Wanatakiwa
kurudi majimboni kwao kusimamia ilani ya chama pamoja na ahadi zao
walizoahidi na zile za viongozi wa chama na Serikali ikiwamo ahadi zake
kama rais,” alisema.
Kuhusu suala la ukosoaji, Rais Kikwete
alisema wabunge wa chama hicho wana wajibu wa kuikosoa Serikali yao
lakini akaonya aina ya ukosoaji wenye lengo la kuibomoa Serikali.
“Mnatakiwa
kuisimamia Serikali na kuikosoa bila kuibomoa, lakini kuna baadhi yenu
mmekuwa mkiibomoa Serikali kwa jinsi mnavyochangia huko bungeni… hilo si
jambo jema hata kidogo, waachieni wale wenzetu,”alisema Kikwete.
Chanzo
hicho kilieleza kuwa wabunge wamekuwa hawaridhishwi na utendaji wa
baadhi ya mawaziri ambao walisema ni mizigo na kutaka waondolewe katika
nafasi zao.
Chanzo hicho kilitaja majina ya mawaziri hao
wanaodaiwa kuwa ni mizigo kuwa ni Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya
Uvuvi, Dk. David David Mathayo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Dk. Shukuru Kawambwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Dk. Fenera Mkangara.
Baadhi ya wabunge walimtaka Rais Kikwete
kudhibiti ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watendaji wa halmashauri
mbalimbali nchini, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa.
“Rais
anatakiwa kukunjua makucha yake kuondokana na uozo huu katika
halmashauri zetu. Haiwezekani waendelee kunyamaziwa, tunatakiwa
kuimarisha chama kwa kuangalia namna Serikali inavyoweza kutimiza ahadi
kwa wananchi,” kilisema.
Kiliendelea kusema. “Serikali iweze
kusaidia katika kutimiza ahadi kwa kutelekeza ilani ya chama, viongozi
wa vijiji, kata na vitongoji kuanza kulipwa mshahara maana wamejitolea
kwa muda mrefu hivyo huwalazimu kupata ushawishi kutokana na njaa,”
kilisema.
Imeelezwa kuwa katika kikao hicho kinachoendelea kitakuwa na ajenda nyingi ambazo zitaibuliwa na wabunge.
Hizo
ni pamoja na maslahi ya wabunge, utendaji kwa baadi ya mawaziri na aina
ya ukosoaji inayofanywa na baadhi ya wabunge wa chama hicho.
Baada
ya mapumziko ya mchana, kikao hicho kiliendelea kwa wabunge kupata
nafasi ya kujadili hoja mbalimbali kutokana na hotuba ya Rais Kikwete
aliyoitoa asubuhi.
Rais Kikwete anakutana na wabunge hao wakati
wenyewe wanaonekana kugawanyika kutokana na kuwapo kundi la wabunge
wanaoitetea Serikali na wengine wanaoikosoa.
Miongoni mwa wabunge
wanaoikosoa Serikali ya chama hicho waziwazi ni Mbunge wa Mwibara,
Kangi Lugola, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, Mbunge wa Kisesa,
Luhaga Mpina na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy.
Hata
hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa wabunge hao machachari walichanwa
hadharani na baadhi ya wabunge wanaoiunga mkono Serikali hali
inayoonyesha kuwa wabunge hao si wamoja.
Mbunge wa Sikonge, Said
Nkumba alisimama na kueleza kuwa anashangazwa na aina ya ukosoaji
unaofanywa na wabunge hao na kusema. “Kama hawataki kufuata maelekezo ya
chama wahame,” alisema.