Monday, 20 May 2013

Gari la polisi lakamatwa na bangi

GARI la polisi wa usalama barabarani Mkoa wa Arusha pamoja na askari polisi, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, kwa kukutwa wakisafirisha magunia 18 ya bangi. Polisi hao wakiwa na gari hilo, walikamatwa juzi katika maeneo ya Kilema Pofu, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani hapa. Askari hao walikamatwa Mei 18 mwaka huu na katika kusafirisha bangi hiyo, walikuwa wakishirikiana na mfanyabiashara mmoja aliyejulikana kwa jina la Livingstone Urassa (35).
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema askari hao walikamatwa kutokana na mtego uliokuwa umewekwa na askari polisi mkoani Kilimanjaro, baada ya kupata taarifa kuwa kuna mfanyabiashara anasafirisha bangi kwa kutumia gari ambayo haisimamishwi njiani.

Kamanda Boaz alisema kwamba, baada ya kuwakamata askari hao, walikwenda hadi nyumbani kwa mfanyabiashara huyo na kukuta magunia mengine 16 yakiwa yamefichwa kwenye migomba.

Kwa mujibu wa Kamanda Boaz gari hilo la polisi lilikuwa likiendeshwa na mmoja wa askari hao, ambaye ni koplo Edward na Pc George na kwamba namba za gari hazijafahamika.

Hata hivyo, taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema gari hilo la polisi linashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro.

No comments: