Waandamanaji nchini wanaopinga ndoa za jinsia moja na na haki ya kurithi watoto nchini ufaransa
SKOFU Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa amesema kuwa mpango wa ndoa za jinsia moja ulioruhusiwa na baadhi ya matifa duniani si mpango wa Mungu, bali ni wa shetani. Askofu Nzigilwa alibainisha hayo hivi karibuni alipokuwa akitoa mahubiri kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Maurus Kurasini jimboni humo, kwenye hafla iliyokwenda sambamba na kufungisha Ndoa takatifu kwa Waamini wa Parokia hiyo.
Askofu Nzigilwa alisema katika dunia ya sasa kumeibuka ndoa ambazo ziko kinyume na mpango wa Mungu kwa Wanadamu na hivyo nafasi ya mwanamke kuchukuliwa na mwanaume na nafasi ya mwanaume kuchukuliwa na mwanamke. “Sakramenti ya ndoa ina tabia moja ya mke na mume yaani mwanaume mmoja na mwanamke mmoja maana zipo ndoa za siku hizi ambazo mwanaume anachukua nafasi ya mwanamke halafu anaolewa na mwanaume mwenzake halafu mwanamke anachukua nafasi ya mwanaume halafu anamuoa mwanamke mwenzake hii ni kinyume kabisa na mpango wa Mungu kwa wanamdamu”,alisema Askofu Nzigilwa. Alisema ndoa ya Kisakramenti ya Kanisa Katoliki ni ya mume na mke wa jinsia tofauti ambayo hudumu daima haitenganishwi na kitu chochote mara baada ya kufungwa kihalali.
Aidha Askofu huyo, aliwaambia wanandoa hao kuwa wanaingia katika mpango wa Mungu ambao aliuratibu tangu mwanzo wa uumbaji na kuwataka iwe ya mume mmoja na mke mmoja. Askofu Nzigilwa alisema katika kitabu cha mwanzo sura ya pili inaeleza kwamba hapo mwanzo Mungu aliumba vitu ili Adamu avitawale na hiyo ilikuwa ishara ya mamlaka ya Adamu ya kuvipa hata majina ndiyo maana kuna alivyoviita mimea, samaki na wanyama kitendo ambacho kinaendelea hadi leo kwa wazazi kuwapa majina Watoto wao. Alisema pamoja na Adamu kupewa vitu hivyo vyote hakuwa na furaha hadi pale Mwenyezi Mungu alipompa mwenza Eva ambapo alikuwa na furaha na kusema kuwa huyo ndiye mnyama katika nyama na kila kitu katika maisha yake ambapo aliwataka wanandoa hao kuacha kuwakimbia wenzao kwa ajili ya mali.
“Katika ulimwengu huu wa leo tumekuwa tukishuhudia watu wakiwakimbia waume au wake zao ili waweze kumiliki mali jamani nguvu na furaha zenu mnazipoteza kwa sababu ya mali hakuna mwanaume aliyepewa mali hapa duniani kuliko Adamu lakini bado alionekana hana furaha hadi pale Mungu alipompatia mke:
Hebu muulizeni kwanza Adamu kwa nini hakuwa na furaha hadi alipopewa mwenza yaani Eva sasa nyinyi akina baba mkianza kuwakimbia wake zenu mkidhani mtapata furaha shauri zenu”,alisema Askofu Nzigilwa. Askofu Nzigilwa alisema furaha katika familia inakamilishwa kwa mume na mke kukaa pamoja na kutawala ulimwengu kwa kuwa huo ni mpango wa Mungu alipomuumba Eva na kumwambia Adamu kuwa huyo ndiye mke wake kwa kuwa angetaka ndoa ya mme mmoja na wanawake wengi angempatia adamu wake wengi na si Eva peke yake. Aliwataka wanandoa hao kila mmoja kuwa msaada kwa mwenzake katika safari ya kuelekea mbinguni huku wakizifanya familia zao kuwa Kanisa dogo la nyumbani kwa kuwalea katika imani na kwa njia ya sala kwa kuwa kanisa ni mahala ambapo Mungu anaabudiwa na kuheshimiwa na neema za zake zinapatikana mahala hapo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Waziri mkuu aliyehudhuria hafla hiyo ambaye ni Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji Dk.Mary Nagu alisema uaminifu na uadilifu kwa watu unatokana na uwepo wa Makanisa ambapo Viongozi wa dini wamekuwa wakitoa mafundisho mbalimbali ya kumcha Mungu. Alisema mauaji ya Vikongwe yanatokana na kutokuwepo kwa madhehebu ya dini sehemu wanazoishi na hivyo kukosa mafundisho ya dini kitendo kinachosababisha watu kukosa uadilifu. Alisema vitendo vya ongezeko la matukio ya wizi, ukahaba, uzinzi, rushwa, ufisadi, dawa za kulevya, uchochezi, udanganyifu, ulevi, uasherati na ulevi ni baadhi ya viashiria vya watu kupungukiwa na uchaji wa Mungu. Dk. Nagu alisema ili kuondokana na rushwa Waamini hawana budi kwenda katika nyumba za ibada kumuomba Mungu na kupata mafundisho stahiki husani kanisani kwa sababu Mungu huangalia wanaofanya vitendo hivyo viovu na kuwa wawapo Ofisini hujiona kuwa wapo salama kwa kutokukamatwa hasa pale ushahidi unapokosekana.
Kanisa la Mtakatifu Maurus lilijengwa mwaka 1894 na Padri Maurus Hagman na kuwekwa wakfu Februari 20, mwaka 1898 na hivyo kuwa makao makuu ya Vikariat ambapo mwaka 1965 ilifanywa kuwa kigango na mwaka 1970 ilifanywa kuwa Parokia. Mwaka 1988 ilikabidhiwa kwa Shirika la Wasalvatoriani na hivyo kufanya kuwa na Jumuiya ndogondogo 27 kitendo kilichoongeza Waamini na kusababisha kanisa kuwa dogo baada ya kukosekana kwa hewa ya kutosha wakati wa ibada ya misa na hivyo waamini wengine kusali nje.








