Imetaja sababu hizo kuwa ni ushiriki mdogo wa jamii kwenye shughuli za jamii na maendeleo, mahudhurio hafifu ya wananchi katika vikao vya uamuzi, ukusanyaji na usimamizi dhaifu wa mapato yake.
Dodoma.
Serikali imekiri kukabiliwa na changamoto kubwa zinazoikabili katika
kutekeleza sera ya ugatuaji madaraka kwa wananchi wake.
Imetaja sababu hizo kuwa ni ushiriki mdogo wa
jamii kwenye shughuli za jamii na maendeleo, mahudhurio hafifu ya
wananchi katika vikao vya uamuzi, ukusanyaji na usimamizi dhaifu wa
mapato yake.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri alisema ngazi
ya mitaa na vijiji kumekuwa na tatizo kubwa la utunzaji wa vitabu vya
hesabu, uandaaji taarifa za mapato na matumizi na taarifa za utekelezaji
majukumu ya mitaa na vijiji.
Alikuwa akijibu swali la mbunge Viti Maalumu,
Anastazia Wambura (CCM) ambaye alihoji Serikali inawezaje kuwahakikishia
wananchi kwamba wenyeviti wa mtaa na vijiji wanajua wajibu wao
kulingana na nafasi walizonazo.
Pia, mbunge huyo alitaka kujua Serikali jinsi
inavyofuatilia fedha za uwezeshwaji na kujengewa uwezo, ambazo hutengwa
kwa ajili ya kuwapa mafunzo viongozi hao ambazo hazifiki kwa wakati
unaotakiwa.
Naibu Waziri alisema wenyeviti wa vijiji na mitaa
wana wajibu wa kusimamia ulinzi na usalama maeneo yao, kuwakilisha
wananchi katika vikao vya Kamati za Maendeleo ya Kata, wilaya na
kuitisha na kuongoza mikutano.
“Kutokana na changamoto hizi, ni wazi kuwa upo
umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwajengea uwezo wenyeviti wa vijiji na
mitaa na watendaji wao ili kuhakikisha wanajua majukumu yao ipasavyo,”
alisisitiza Mwanri.
Mwanri alisema Serikali imekuwa ikipeleka asilimia
40 ya fedha za kujenga uwezo katika vijiji na mitaa, asilimia 50 ya
fedha hizo hutumika kuwajengea uwezo viongozi hao.

No comments:
Post a Comment