Tuesday, 7 May 2013

Sh 876.3 Bil kumaliza msongomano Jiji la Dar


Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge alitoa taarifa hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Abas Mtemvu (CCM).

Dodoma. Wizara ya Ujenzi inatekeleza miradi ya Sh. 876.336 bilioni katika Jiji la Dar es Salaam,yenye lengo la kutafutia ufumbuzi wa kupunguza msongamano wa magari katika Jiji hilo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge alitoa taarifa hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Abas Mtemvu (CCM).
Katika swali lake,mbunge huyo alitaka kujua mpango wa Serikali wa kulitafutia ufumbuzi tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam hasa katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Lwenge aliiitaja miradi hiyo kuwa ni Barabara ya Kimara- Kivukoni, Fire-Kariakoo na Magomeni hadi Morocco na ujenzi wa karakana na vituo vya mabasi yaendayo kwa haraka pamoja na kuhamisha nguzo za umeme.
“Barabara ya Mwenge-Tegeta, Barabara ya Kilwa Bendera Tatu-Mbagala Rangi Tatu, ujenzi wa daraja la Kigamboni, Flyover ya TAZARA, Barabara ya Gerezani, Barabara ya Mandela na Barabara ya Wazo Hill-Bagamoyo hadi Msata,’ alisema Lwenge.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka (RBT) kutoka Morocco kwenda Magomeni hadi Kivukoni na Kimara kutapunguza msongamano wa magari kati ya Oysterbay Polisi na Daraja la Salender.
Kuhusu mipango ya baadaye, alisema Serikali itaangalia uwezekano wa kujenga barabara ya juu pande zote za daraja la Salender, kupanua barabara kwenye maingilio ya daraja, kujenga lingine pembeni mwa daraja au kujenga mbadala kutokea Kenyata Drive kuunganisha na Ocean Road.

 

No comments: