Kamanda Mpinga aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, ambapo alibainisha kuwa vigogo hao wamekuwa wakiingilia utendaji kazi wa askari wake hasa wanapokamatwa ndugu zao kwa kukiuka sheria.
Dar es Salaam. Kamanda wa Kikosi cha
Usalama wa barabarani, Mohamed Mpinga amefunguka kwa kueleza
anavyokwazwa na baadhi ya viongozi wa juu wa Serikali, wanavyokwamisha
utendaji kazi wa askari wake.
Kamanda Mpinga aliyasema hayo hivi karibuni
alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, ambapo
alibainisha kuwa vigogo hao wamekuwa wakiingilia utendaji kazi wa askari
wake hasa wanapokamatwa ndugu zao kwa kukiuka sheria.
“Wapo wengi ambao husababisha Sheria za Usalama
Barabarani kuvunjwa kwa makusudi na ndugu, jamaa au rafiki zao kwa kuwa
watu hao mara wanapokamatwa, huwasiliana na vigogo hao kwa njia ya simu
ambapo vigogo hao huanza kuwatisha askari wangu, pamoja na kuwalazimisha
kutowachukulia hatua, “ alisema Mpinga.
Aliongeza:” Kwa kutambua hilo ndugu, jamaa na
marafiki wa vigogo hao, wamekuwa wakikiuka sheria husika kusudi. Yaani
mtu amegonga, unakuta kigogo anapiga simu kwamba asifunguliwe mashtaka,
kwa kweli ni vyema kuongoza nchi kwa msingi wa sheria,” alisema Kamanda
Mpinga huku akikunja uso kuonyesha kukerwa na jambo hilo.
Mpinga alisema hali hiyo ndiyo imesababisha
nidhamu wanayopaswa kuwa nayo madereva barabarani kushuka hata kuamua
kujiunga kwenye misafara ya viongozi mbalimbali, wakiwa na imani kwamba,
hawawezi kuchukuliwa hatua kwa kuwa watakingiwa kifua na vigogo hao.
“ Nimewaeleza trafiki wote kuwa makini zaidi
kwenye misafara, kwa sababu siku hizi hali imebadilika. Wawe
wanajiangalia jinsi wanavyosimamia au kuongoza misafara wakizingatia na
usalama wa maisha yao kwa jumla,” alisema Kamanda Mpinga.
“Hata hivyo, napenda kuwahakikishia kwamba
nitasimamia sheria katika utendaji wangu wa kazi, simu ikipigwa kwangu
sitoi ushirikiano wa aina hiyo. Nawasihi viongozi wenye tabia hizo
waache kuingilia utendaji kazi wa askari, mtu anapita taa nyekundu
inawaka akikamatwa lazima alipe faini,” alisema.
Aidha, alizungumzia kuhusu tuhuma zilizokuwa
zikielekezwa kwa askari wake za kuwa na vitabu bandia vya kuandika
adhabu, ambapo alieleza kuwa jambo hilo halina ukweli, huku akieleza
kwamba vitabu vinavyotumika vilichapwa vingi mwaka 2011.
“Nimesikia tuhuma hizi, lakini nawahakikishia
wananchi kwamba hazina ukweli kwa sababu baada ya kusikia nilifuatilia
nikabaini hofu yao inatokana na mwaka kwa kuwa vitabu vingi vina GN 2057
2011 vilitolewa makao makuu ya polisi,” alifafanua Kamanda Mpinga.

No comments:
Post a Comment