Tuesday, 7 May 2013

Sh 876.3 Bil kumaliza msongomano Jiji la Dar


Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge alitoa taarifa hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Abas Mtemvu (CCM).

Dodoma. Wizara ya Ujenzi inatekeleza miradi ya Sh. 876.336 bilioni katika Jiji la Dar es Salaam,yenye lengo la kutafutia ufumbuzi wa kupunguza msongamano wa magari katika Jiji hilo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge alitoa taarifa hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Abas Mtemvu (CCM).
Katika swali lake,mbunge huyo alitaka kujua mpango wa Serikali wa kulitafutia ufumbuzi tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam hasa katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Lwenge aliiitaja miradi hiyo kuwa ni Barabara ya Kimara- Kivukoni, Fire-Kariakoo na Magomeni hadi Morocco na ujenzi wa karakana na vituo vya mabasi yaendayo kwa haraka pamoja na kuhamisha nguzo za umeme.
“Barabara ya Mwenge-Tegeta, Barabara ya Kilwa Bendera Tatu-Mbagala Rangi Tatu, ujenzi wa daraja la Kigamboni, Flyover ya TAZARA, Barabara ya Gerezani, Barabara ya Mandela na Barabara ya Wazo Hill-Bagamoyo hadi Msata,’ alisema Lwenge.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka (RBT) kutoka Morocco kwenda Magomeni hadi Kivukoni na Kimara kutapunguza msongamano wa magari kati ya Oysterbay Polisi na Daraja la Salender.
Kuhusu mipango ya baadaye, alisema Serikali itaangalia uwezekano wa kujenga barabara ya juu pande zote za daraja la Salender, kupanua barabara kwenye maingilio ya daraja, kujenga lingine pembeni mwa daraja au kujenga mbadala kutokea Kenyata Drive kuunganisha na Ocean Road.

 

Serikali yataja changamoto ugatuaji madaraka nchini


Imetaja sababu hizo kuwa ni ushiriki mdogo wa jamii kwenye shughuli za jamii na maendeleo, mahudhurio hafifu ya wananchi katika vikao vya uamuzi, ukusanyaji na usimamizi dhaifu wa mapato yake.



Dodoma. Serikali imekiri kukabiliwa na changamoto kubwa zinazoikabili katika kutekeleza sera ya ugatuaji madaraka kwa wananchi wake.
Imetaja sababu hizo kuwa ni ushiriki mdogo wa jamii kwenye shughuli za jamii na maendeleo, mahudhurio hafifu ya wananchi katika vikao vya uamuzi, ukusanyaji na usimamizi dhaifu wa mapato yake.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri alisema ngazi ya mitaa na vijiji kumekuwa na tatizo kubwa la utunzaji wa vitabu vya hesabu, uandaaji taarifa za mapato na matumizi na taarifa za utekelezaji majukumu ya mitaa na vijiji.
Alikuwa akijibu swali la mbunge Viti Maalumu, Anastazia Wambura (CCM) ambaye alihoji Serikali inawezaje kuwahakikishia wananchi kwamba wenyeviti wa mtaa na vijiji wanajua wajibu wao kulingana na nafasi walizonazo.
Pia, mbunge huyo alitaka kujua Serikali jinsi inavyofuatilia fedha za uwezeshwaji na kujengewa uwezo, ambazo hutengwa kwa ajili ya kuwapa mafunzo viongozi hao ambazo hazifiki kwa wakati unaotakiwa.
Naibu Waziri alisema wenyeviti wa vijiji na mitaa wana wajibu wa kusimamia ulinzi na usalama maeneo yao, kuwakilisha wananchi katika vikao vya Kamati za Maendeleo ya Kata, wilaya na kuitisha na kuongoza mikutano.
“Kutokana na changamoto hizi, ni wazi kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwajengea uwezo wenyeviti wa vijiji na mitaa na watendaji wao ili kuhakikisha wanajua majukumu yao ipasavyo,” alisisitiza Mwanri.
Mwanri alisema Serikali imekuwa ikipeleka asilimia 40 ya fedha za kujenga uwezo katika vijiji na mitaa, asilimia 50 ya fedha hizo hutumika kuwajengea uwezo viongozi hao.

Grace Kihwelu alilia zao la kahawa



Dodoma..Mbunge wa Viti Maalum, Grace Kihwelu (Chadema) ameitaka Serikali kuja na mpango madhubuti wa kufufua kilimo cha kahawa katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Akiuliza swali bungeni jana,mbunge huyo alisema kwa miaka mingi zao hilo limekuwa tegemeo kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro,lakini kwa sasa kilimo hicho ni kama kimekufa.
“Je Serikali ina mpango gani madhubuti na mahsusi wa kufufua kilimo cha kahawa Kilimanjaro ambacho kwa miaka mingi kimekuwa tegemeo kwa wananchi wa Kilimanjaro na mhimili mkubwa kwa uchumi wa taifa?” Alihoji Kiwelu.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira alisema Serikali imeandaa mkakati wa kuendeleza tasnia ya kahawa kwa lengo la kuendeleza kilimo cha kahawa nchini kwa kuongeza tija na ubora wa kahawa kitaifa.
Aliyataja maeneo mahsusi ya mkakati huo ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa kahawa safi kutoka wastani wa sasa wa tani 50,000 kwa mwaka hadi tani 100,000 ifikapo mwaka 2022.
Nyingine ni kuongeza ubora wa kahawa ili kupata bei ya ziada katika masoko ya nje kutoka wastani wa asilimia 35 hadi kufikia wastani wa asilimia 70 ifikapo mwaka 2022,” alisema
Alisema maeneo muhimu katika mkakati huo ni pamoja na kuimarisha huduma za ugani ili wakulima wazingatie kanuni bora za kilimo cha kahawa na kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI) ili kuhakikisha upatikanaji wa miche bora ya kahawa.
Wassira alisema pia serikali inaendelea kuongeza matumizi ya viwanda vya kati vya kutayarisha kahawa ili kuongeza ubora wa zao hilo hivyo wakulima kunufaika na bei nzuri.

Kauli ya Kardinali imeacha maswali mengi kuliko majibu.



Jana nimebahatika kuisikiliza vyema taarifa fupi (KUNTU) iliyotolewa na mlezi wetu mkuu wa kiroho KARDINALI) ya kuujulisha umma ni nini kilichotokea kupitia chombo chake cha habari TUMAINI. Tunashukuru kwa taarifa yake hiyo ambayo kwa jinsi ilivyotolewa, nina hakika ilifanyiwa kazi ya kina kabla ya kuletwa hadharani.
Kwanza kabisa nashawishika kwa ukurasa wa awali kukubaliana na taarifa yake hiyo kutokana na imani yangu kuu kwake, na inavyojulikana kwa wachache kuwa kada ya UPAPA na UKARDINALI ni kada ambazo wanaozifikia pia wamepitia mambo ya kiintelijensia!
Tunashawishika kuamini hivyo kutokana na jinsi kiongozi huyu wa kiroho ambavyo ameweza kutoa ripoti yake ya kiintrijensia ndani ya chini ya masaa 24! Amesema suala hili lisihusishwe kwa aina yoyote ile na dini au itikadi ya uislamu bali waliofanya kitendo hicho ni WAKRISTO tena wa KANISANI hapo! Na kwa msisitizo akasema kuwa anao uhakika wa kile anachokisema!
Sasa inamaana kwa uweza wa kimungu ambao mtumishi huyu anao na ule wa uintelijensia alionao ameweza kuwasaidia hata polisi wetu kumaliza kazi ya upelelezi katika muda mfupi sana! Sasa kuna haja gani ya kuleta tena CIA? Na kama amesisitiza kuwa taarifa yake aliyoitoa ndiyo ya mwisho, kuna haja gani ya kuwashikilia hao watu wengine, si yeye apelike hiyo ripoti yake polisi ili kazi iwe fupi na amani irejee mioyoni mwa watu na kukata vilimilimi vya watu wengine ambao wanataka kupata umaarufu kupitia SAGA hilo?!

Lakini tukija katika upande wa pili, Je, hatuoni kuwa mtumishi wetu huyu amewahi sana kutoa ripoti yake hiyo ambayo inaonekana kama hitimisho la SAGA lenyewe?!

Na, Je, kama itatokea ikaja kuapatikina ripoti nyingine tofauti na hii tuliyoaminishwa na mtumishi wa mungu, Je, tutamwamini nani?
Maswali yapo mengi sana kuliko yale ya papo kwa papo ya Waziri mkuu, lakini katika hili nafikiri TAFAKARI ya kina ilitakiwa ichukuliwe kabla ya taarifa hii kutolewa.

Saturday, 20 April 2013

Trafiki: Vigogo serikalini wanatuvuruga


Kamanda Mpinga aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, ambapo alibainisha kuwa vigogo hao wamekuwa wakiingilia utendaji kazi wa askari wake hasa wanapokamatwa ndugu zao kwa kukiuka sheria.


Dar es Salaam. Kamanda wa Kikosi cha Usalama wa barabarani, Mohamed Mpinga amefunguka kwa kueleza anavyokwazwa na baadhi ya viongozi wa juu wa Serikali, wanavyokwamisha utendaji kazi wa askari wake.  
Kamanda Mpinga aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, ambapo alibainisha kuwa vigogo hao wamekuwa wakiingilia utendaji kazi wa askari wake hasa wanapokamatwa ndugu zao kwa kukiuka sheria.
“Wapo wengi ambao husababisha Sheria za Usalama Barabarani kuvunjwa kwa makusudi na ndugu, jamaa au rafiki zao kwa kuwa watu hao mara wanapokamatwa, huwasiliana na vigogo hao kwa njia ya simu ambapo vigogo hao huanza kuwatisha askari wangu, pamoja na kuwalazimisha kutowachukulia hatua, “ alisema Mpinga.
Aliongeza:” Kwa kutambua hilo ndugu, jamaa na marafiki wa vigogo hao, wamekuwa wakikiuka sheria husika kusudi. Yaani mtu amegonga, unakuta kigogo anapiga simu kwamba asifunguliwe mashtaka, kwa kweli ni vyema kuongoza nchi kwa msingi wa sheria,” alisema Kamanda Mpinga huku akikunja uso kuonyesha kukerwa na jambo hilo.
Mpinga alisema hali hiyo ndiyo imesababisha nidhamu wanayopaswa kuwa nayo madereva barabarani kushuka hata kuamua kujiunga kwenye misafara ya viongozi mbalimbali, wakiwa na imani kwamba, hawawezi kuchukuliwa hatua kwa kuwa watakingiwa kifua na vigogo hao.
“ Nimewaeleza trafiki wote kuwa makini zaidi kwenye misafara, kwa sababu siku hizi hali imebadilika. Wawe wanajiangalia jinsi wanavyosimamia au kuongoza misafara wakizingatia na usalama wa maisha yao kwa jumla,” alisema Kamanda Mpinga.
“Hata hivyo, napenda kuwahakikishia kwamba nitasimamia sheria katika utendaji wangu wa kazi, simu ikipigwa kwangu sitoi ushirikiano wa aina hiyo. Nawasihi viongozi wenye tabia hizo waache kuingilia utendaji kazi wa askari, mtu anapita taa nyekundu inawaka akikamatwa lazima alipe faini,” alisema.
Aidha, alizungumzia kuhusu tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwa askari wake za kuwa na vitabu bandia vya kuandika adhabu, ambapo alieleza kuwa jambo hilo halina ukweli, huku akieleza kwamba vitabu vinavyotumika vilichapwa vingi mwaka 2011.
“Nimesikia tuhuma hizi, lakini nawahakikishia wananchi kwamba hazina ukweli kwa sababu baada ya kusikia nilifuatilia nikabaini hofu yao inatokana na mwaka kwa kuwa vitabu vingi vina GN 2057 2011 vilitolewa makao makuu ya polisi,” alifafanua Kamanda Mpinga.

Chadema wamtangazia vita Spika Makinda

Wabunge waliofukuzwa na Naibu Spika, Job Ndugai juzi ni pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.


Dodoma. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema kuwa watakata rufaa katika Kamati ya Kanuni ya Bunge dhidi ya mwongozo wa Spika uliobariki adhabu ya kuwatimua kwa siku tano wabunge sita wa Chadema kwa kudharau mamlaka ya Spika.
Akitoa mwongozo wake jana, Spika Anne Makinda alibariki wabunge hao kutimuliwa akisema kuwa Kanuni za Bunge zilikiukwa.
Wabunge waliofukuzwa na Naibu Spika, Job Ndugai juzi ni pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Juzi Mbowe aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni ya 68 (7), akimtaka Spika aeleze naibu wake (Ndugai) alitumia kanuni gani ya Bunge, kuwasimamisha siku tano wabunge sita wa Chadema wasihudhurie vikao vya Bunge vinavyoendelea.
Mwongozo wa Makinda
Akitoa mwongozo huo jana, Spika Anne Makinda alisema kuwa kitendo kilichotokea hakiwezi kupuuzwa na wala kuvumiliwa na Bunge, pamoja na wananchi kwa kuwa ni utovu wa nidhamu ya Bunge na wananchi kwa jumla.
Alisema: “Kanuni ya 2(2) na 5(1), inampa mamlaka Spika ya kuleta amani bungeni.
Kanuni ya 2(2) inaeleza: “Iwapo jambo au shughuli yoyote haikuwekewa masharti katika kanuni hizi, Spika ataamua utaratibu wa kufuata katika jambo au shughuli hiyo, kwa kuzingatia Katiba, Sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge na mila na desturi za uendeshaji bora wa shughuli za Bunge na uamuzi huo utaingizwa katika kitabu cha maamuzi ili kuongoza mwenendo wa baadaye wa uendeshaji wa shughuli za Bunge.”
Kanuni ya 5(1) inaeleza: “Katika kutekeleza majukumu yake yaliyotajwa katika Ibara ya 84 ya Katiba, Spika ataongozwa na kanuni hizi na pale ambapo kanuni hazikutoa mwongozo, basi Spika atafanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa bunge la Tanzania.”
Makinda alisema kwa kutumia kanuni hizo mbili anakubaliana na uamuzi uliotolewa na Ndugai na kwamba suala hilo litaingizwa kwenye kitabu cha uamuzi wa Spika.
“Natumia Kanuni ya 2(2) na 5(1) kusema kuwa uamuzi uliofanywa na Ndugai ni halali na itaingizwa kwenye kitabu cha maamuzi ya Spika,” alisema Spika Makinda.
Kauli ya Mbowe
Mbowe jana alilieleza gazeti hili kuwa uamuzi wa Spika ulijielekeza katika jambo lisilo na kanuni inayolisimamia, tofauti na lile la kudharau mamlaka ya kiti cha Spika, lililotolewa maelekezo na Kanuni ya 74 (1).
Kanuni hiyo inasema: “Spika anaweza kutaja jina la mbunge kwamba amedharau mamlaka ya Spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge; ikiwa kwa maneno au vitendo mbunge huyo anaonyesha dharau kwa mamlaka ya Spika; au Mbunge huyo atafanya kitendo chochote cha makusudi cha kudharau shughuli ya Bunge au mbunge yeyote anayeongoza shughuli hiyo.”

Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema alisema kuwa majibu ya Spika ni ya bahati mbaya kwa sababu yameonyesha mwendelezo wa kupuuza Kanuni za Bunge.
Akieleza kiini cha tatizo, Mbowe alisema kuwa ni kuyumba kwa kiti, upendeleo wa wazi, kupanga mikakati na CCM na kumpuuza Mnadhimu wa Chadema. Alisema nidhamu bungeni haitapatikana kwa kuwatimua wabunge na kwamba wapo tayari kwa hilo, hata kama wataisha wote, hadi pale Kiti cha Spika kitakapoacha upendeleo.
“Tutaliheshimu Bunge kama taasisi huru, lakini si lilivyo sasa kama taasisi ya CCM,” alisema Mbowe na kufafanua kuwa: “..Nje ya Bunge wote tunaheshimiana, lakini mambo yanakuwa tofauti bungeni kwa sababu ya Kiti cha Spika kutotenda haki.”
Alifafanua kuwa katika tukio zima, mbali na kupuuza kanuni, adhabu yenyewe ilitolewa nje ya utaratibu, ikiwa ni pamoja na kuruhusu askari wasiokuwa na sare kuingia bungeni.
“Bungeni pale kukiwa na siwa ni mahali patakatifu, lakini Naibu Spika ‘alipaniki’ akaruhusu watu wakatoka kusikojulikana bila sare na huo ni ukiukwaji wa taratibu,” alisema na kuongeza:
“Pale hata Makamu wa Rais ili aruhusiwe kuingia, lazima kanuni itenguliwe, watumishi wa Bunge na askari wanaoruhusiwa ndani, lazima wawe na sare maalumu, lakini mara hii Kiti cha Spika kimeruhusu watu wasiohusika kuingia.”
Alisema kwamba, Ndugai aliyaacha kando mambo ya msingi, akabakia kusema Tundu Lissu amesimama mara nyingi na kusahau kuwa mbunge huyo ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, hivyo anaweza kusimama mara nyingi kadri ya mahitaji.
Alifafanua kuwa siku ya kufukuzwa kwa wabunge hao, Lissu alikuwa akitaka kuweka sawa kauli isiyokuwa sahihi ya Mwigulu Nchemba kuwa Dk Slaa hakufanya mkutano wa hadhara Singida wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, badala yake alifanya mkutano wa ndani ya viongozi wa dini.
Katika hatua nyingine, Frederick Katulanda, anaripoti kutoka Mwanza kuwa, wabunge watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliosimamishwa kuhudhuria vikao vitano vya Bunge watafanya ziara katika mikoa mitano kwa ajili ya kuwaeleza wapigakura wa majimbo yao hali ya Bunge na upendeleo wa Spika wa Bunge , wanaoamini umesababisha wao kutimuliwa.
Akielezea ziara yao katika majimbo yao Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje alisema kuwa wamefikia uamuzi huo ili kuwaeleza wananchi uonevu ndani ya Bunge na jinsi Spika na naibu wake wanavyoshindwa kusimamia kanuni kwa sababu ya kuwalinda CCM na Serikali.
Wenje alisema kwamba ratiba yao itaanzia katika Mkoa wa Mwanza, ambapo watafanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Sahara na kwamba wabunge wote watano watakuwapo kueleza yaliyowakuta bungeni.

Darasa la saba sasa kujiunga vyuo vikuu



Udahili huo utakaoanza mwaka huu wa masomo 2013/14, utakuwa ukiwahusisha wale ambao elimu yao imeishia darasa la saba na kuendelea, lakini walikosa sifa ya kuendelea na masomo kwa ngazi ya chuo kikuu.

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU), imepanga kuanza kuwadahili wanafunzi wa kujiunga na masomo ya vyuo vikuu kwa kutumia uzoefu wao.
Udahili huo utakaoanza mwaka huu wa masomo 2013/14, utakuwa ukiwahusisha wale ambao elimu yao imeishia darasa la saba na kuendelea, lakini walikosa sifa ya kuendelea na masomo kwa ngazi ya chuo kikuu.
Kupitia utaratibu huo mpya, mtahiniwa atajiunga na Chuo Kikuu kulingana na fani atakayoiomba na atatakiwa kufanya mitihani mitatu na kufaulu kwa wastani wa daraja B.
Mkurugenzi wa Ithibati na Ubora wa Elimu ya Juu kutoka TCU, Dk Savinus Maronga aliliambia gazeti hili kuwa baada ya kuona kuna watu wengi wanaopenda kuendelea na masomo ya elimu ya juu, lakini wameshindwa kutokana na kutokuwa na vigezo, TCU imeamua kuanzisha mitihani hiyo maalumu.
Alisema kuwa mfumo huo unaojulikana kama ‘Recognition of Prior Learning’ (RPL), utamwezesha mwombaji kudahiliwa vyuoni kupitia tume hiyo kama wanavyofanya watahiniwa wengine.
Sifa zinazotakiwa
Kuhusu sifa za kujiunga, Dk Maronga alisema kuwa mwombaji anatakiwa kuwa na umri kuanzia miaka 25 na kuendelea, sambamba na kuwa na elimu isiyopungua darasa la saba.
“Mwombaji anatakiwa kuwa na nia ya kujiunga na elimu ya chuo kikuu na uzoefu wa kile ambacho anakusudia kukisoma.
Awe na uwezo wa kuandika na kusoma Lugha ya Kiingereza, ambayo ndiyo inayotumika kufundishia vyuoni,”alisema Dk Maronga na kuongeza:
“Kuna watu wameishia darasa la saba, lakini wamefanya kazi katika eneo moja, mfano karani wa mahakama, mwandishi wa habari kwa muda mrefu. Hivyo mfumo huu utawawezesha kuendelea na masomo bila tatizo.”
Vigezo
Mkurugenzi huyo alisema, kutakuwa na mitihani ya masomo matatu, ambayo mtahiniwa ili apate nafasi ya kuendelea na masomo ni lazima afaulu kwa wastani wa daraja B.
Alisema daraja la kwanza linaloanza na alama A ni 75-100, daraja B+ ni 60-75, B ni 50-59, C ni 40-49, D ni 35-39 na daraja E ni 0-34.
“Katika mitihani mitatu atakayoifanya, atatakiwa kupata wastani wa daraja ‘B’ na somo husika la fani yake atatakiwa kupata alama B ili kuwa na vigezo vya kupata cheti kitakachomwezesha kuendelea na masomo yake,”alisema Dk Maronga.

Alibainisha kuwa mitihani itakayokuwa ikitumika kudahili watahiniwa itakuwa ni wa somo la Kiingereza na Hisabati utakaokuwa na alama 30.
Mtihani wa Pili utakuwa na alama 30 ambao ni mtihani wa Maarifa na wa tatu utakuwa na alama 40, utakaokuwa ukitokana na fani husika ya mwombaji.
“Mfano mtahimiwa anataka kusomea sheria au uandishi wa habari, atatakiwa kufaulu kwa asilimia 50 somo husika, hivyo endapo atakosa kupata asilimia 50 ya somo lake hatapata cheti kitakachomwezesha kuendelea na elimu ya juu,”alisema Dk Marango na kuongeza:
“Cheti tutakachompatia mtahiniwa kitakuwa halali kwa kipindi cha miaka mitatu na baada ya hapo mwombaji atatakiwa kufanya upya mitihani hiyo.”
Viambatanisho
Kutokana na maelezo ya TCU, mwombaji anatakiwa kuambatanisha cheti cha kuzaliwa au hati ya kusafiria,wasifu wake pamoja na vyeti vya ushiriki mzuri kutoka sehemu anayofanyia kazi.
Vingine ni nakala za vyeti vya taaluma, picha ndogo ‘passport size, nakala za vyeti vya taaluma za masomo ya hapo awali, ripoti ya tathmini ya utendaji kazi wake kazini kwa walioajiriwa kutoka kwa mwajiri na nakala ya kozi za awali alizokwishafanya.
Vituo vya Mitihani
Mkurugenzi huyo alisema mitihani itafanyika kati ya Mei na Juni mwaka huu katika vituo vinne vilivyoandaliwa katika vyuo.
Alisema kuwa chini ya mfumo huo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kitahusika na masuala ya Elimu huku Chuo Kikuu Tumaini Makumira cha Dar es Salaam (TUMADARCo) kikihusika na Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma.
Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA), kitahusika na Kilimo na Wanyamapori wakati Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU) kitahusika na masuala ya usimamizi na utawala,uhasibu, sheria na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).
“Kwa kuwa ndiyo tunaanza, tumeamua kutenga vituo vinne, lakini mwakani tunatarajia kuongeza viwe vingi ili kukidhi mahitaji ya wananchi walio wengi,”anasema Dk Maronga.

Monday, 15 April 2013

Raila, Kalonzo waenda Ikulu kwa Rais Uhuru










Lengo ni kufahamiana na kujadiliana kuhusu masuala ya nchi ya Kenya.
Nairobi. Vigogo wa Muungano wa Demokrasia na Mageuzi (Cord) wa Kenya, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wamerudi kutoka nchini Afrika Kusini na kumtembelea Rais Uhuru Kenyatta.
Ujio huo wa Odinga kwa mujibu wa msemaji wake, Dennis Onyango lengo lilikuwa  kufahamiana na kujadiliana masuala muhimu ya nchi.
Katika maongezi yao na Rais Kenyatta viongozi hao wa Muungano wa Cord walisema kwamba watahudhuria sherehe za kufunguliwa kwa Bunge la 11 nchini humo.
Akidhibitisha mbele ya waandishi wa habari taarifa za kuhudhuria sherehe hizo za kufunguliwa kwa Bunge hilo kwa viongozi hao Onyango alisema kwamba hayo ni makubaliano kati ya Uhuru na viongozi hao.
Alisema viongozi hao pia walijadiliana kuhusu namna  ya kukabili masuala yatakayowasilishwa bungeni kwa mtazamo wa kuridhiana.
Kwa sasa Muungano wa Jubilee unaounda serikali unamiliki mabunge yote mawili, huku maspika Justin Muturi na Ekwe Ethuro wa Bunge la Taifa na  la seneti mtawalia wakiwa wa Jubilee. Kwa hivyo, inatarajiwa kwamba ingawa Muungano wa Cord utakuwa upinzani kwa Serikali, hautakuwa na uwezo wa kupinga masuala muhimu.
Kwa upande wake Rais Kenyatta na Naibu wake  William Ruto waliahidi kuhakikisha kwamba upinzani unakua wa maana katika mabunge yote mawili na kwa Serikali kwa jumla.
“Walisema ni hamu yao kuona vyama vidogo vya upinzani vikitekeleza jukumu lao la kuiangalia Serikali ii isikiuke mipaka katika utendakazi wake,” alisema  Onyango.
Odinga alienda katika eneo Bunge la Khwisero kaunti ya Kakamega, ambapo alimwambia Rais Kenyatta asinunue wabunge wa Cord kuunga mkono upande wa Serikali.

Sh1 bilioni za kuzika viongozi zawakera wabunge




 Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola akichangia mjadala wa  Hotuba ya makadirio ya fedha katika Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2013/14 ambapo alitamka kutounga mkono makadirio hayo. Picha na Edwin Mjwahuzi 

Ni zilizotangazwa kutengwa kupitia Hotuba ya  Waziri Mkuu.
Dodoma. Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imelaumiwa kwa kutenga Sh1 bilioni kwa ajili ya maziko ya viongozi huku Watanzania wengi wakilia na umaskini mkubwa.
Shutuma hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki bungeni kwa nyakati tofauti wabunge akiwamo wa  Viti Maalumu Lucy Owenya (Chadema) na Kangi Lugola (Mwibara-CCM) wakati wakichangia hotuba ya makadirio ya bajeti katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/14.
Katika mchango wake Owenya alisema inatia aibu kuona kiasi kikubwa cha fedha kikitengwa kwa ajili ya maandalizi ya kuzika viongozi huku mambo muhimu na ambayo ni kipaumbele yakiachwa.
“Ni aibu na fedheha kubwa, hivi mmetenga kiasi hicho kwani mnajua nani atakufa na lini atakufa ndio maana mnajiandaa kumzika,” alihoji Owenya.
Mbunge huyo alikwenda mbele zaidi na kueleza kuwa Serikali imeshindwa kufikiri na hasa namna ya kuwaondolea umasikini na tabu wanazopata wananchi wake lakini inawaza habari za watu wanaojiandaa kufa.
Vile vile katika mchango wake Lugola ambaye alisema asingeunga mkono hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alihoji sababu za kutengwa kwa fedha hizo bila kujua nani atakufa lini.
Mbali na hilo, Owenya pia aliilaumu Ofisi ya Waziri kwa kushindwa kutumia mbinu mbadala za kuzuia matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi zinazotumiwa na wakuu wa mikoa kwa ajili ya kwenda Dodoma kufuatilia hotuba ya Waziri Mkuu.
Alimtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwatimua wakuu wa mikoa ili warudi mikoani kwao ili kuokoa fedha za walipa kodi zinazoteketea katika misafara yao mjini Dodoma.