Saturday, 20 April 2013

Darasa la saba sasa kujiunga vyuo vikuu



Udahili huo utakaoanza mwaka huu wa masomo 2013/14, utakuwa ukiwahusisha wale ambao elimu yao imeishia darasa la saba na kuendelea, lakini walikosa sifa ya kuendelea na masomo kwa ngazi ya chuo kikuu.

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU), imepanga kuanza kuwadahili wanafunzi wa kujiunga na masomo ya vyuo vikuu kwa kutumia uzoefu wao.
Udahili huo utakaoanza mwaka huu wa masomo 2013/14, utakuwa ukiwahusisha wale ambao elimu yao imeishia darasa la saba na kuendelea, lakini walikosa sifa ya kuendelea na masomo kwa ngazi ya chuo kikuu.
Kupitia utaratibu huo mpya, mtahiniwa atajiunga na Chuo Kikuu kulingana na fani atakayoiomba na atatakiwa kufanya mitihani mitatu na kufaulu kwa wastani wa daraja B.
Mkurugenzi wa Ithibati na Ubora wa Elimu ya Juu kutoka TCU, Dk Savinus Maronga aliliambia gazeti hili kuwa baada ya kuona kuna watu wengi wanaopenda kuendelea na masomo ya elimu ya juu, lakini wameshindwa kutokana na kutokuwa na vigezo, TCU imeamua kuanzisha mitihani hiyo maalumu.
Alisema kuwa mfumo huo unaojulikana kama ‘Recognition of Prior Learning’ (RPL), utamwezesha mwombaji kudahiliwa vyuoni kupitia tume hiyo kama wanavyofanya watahiniwa wengine.
Sifa zinazotakiwa
Kuhusu sifa za kujiunga, Dk Maronga alisema kuwa mwombaji anatakiwa kuwa na umri kuanzia miaka 25 na kuendelea, sambamba na kuwa na elimu isiyopungua darasa la saba.
“Mwombaji anatakiwa kuwa na nia ya kujiunga na elimu ya chuo kikuu na uzoefu wa kile ambacho anakusudia kukisoma.
Awe na uwezo wa kuandika na kusoma Lugha ya Kiingereza, ambayo ndiyo inayotumika kufundishia vyuoni,”alisema Dk Maronga na kuongeza:
“Kuna watu wameishia darasa la saba, lakini wamefanya kazi katika eneo moja, mfano karani wa mahakama, mwandishi wa habari kwa muda mrefu. Hivyo mfumo huu utawawezesha kuendelea na masomo bila tatizo.”
Vigezo
Mkurugenzi huyo alisema, kutakuwa na mitihani ya masomo matatu, ambayo mtahiniwa ili apate nafasi ya kuendelea na masomo ni lazima afaulu kwa wastani wa daraja B.
Alisema daraja la kwanza linaloanza na alama A ni 75-100, daraja B+ ni 60-75, B ni 50-59, C ni 40-49, D ni 35-39 na daraja E ni 0-34.
“Katika mitihani mitatu atakayoifanya, atatakiwa kupata wastani wa daraja ‘B’ na somo husika la fani yake atatakiwa kupata alama B ili kuwa na vigezo vya kupata cheti kitakachomwezesha kuendelea na masomo yake,”alisema Dk Maronga.

Alibainisha kuwa mitihani itakayokuwa ikitumika kudahili watahiniwa itakuwa ni wa somo la Kiingereza na Hisabati utakaokuwa na alama 30.
Mtihani wa Pili utakuwa na alama 30 ambao ni mtihani wa Maarifa na wa tatu utakuwa na alama 40, utakaokuwa ukitokana na fani husika ya mwombaji.
“Mfano mtahimiwa anataka kusomea sheria au uandishi wa habari, atatakiwa kufaulu kwa asilimia 50 somo husika, hivyo endapo atakosa kupata asilimia 50 ya somo lake hatapata cheti kitakachomwezesha kuendelea na elimu ya juu,”alisema Dk Marango na kuongeza:
“Cheti tutakachompatia mtahiniwa kitakuwa halali kwa kipindi cha miaka mitatu na baada ya hapo mwombaji atatakiwa kufanya upya mitihani hiyo.”
Viambatanisho
Kutokana na maelezo ya TCU, mwombaji anatakiwa kuambatanisha cheti cha kuzaliwa au hati ya kusafiria,wasifu wake pamoja na vyeti vya ushiriki mzuri kutoka sehemu anayofanyia kazi.
Vingine ni nakala za vyeti vya taaluma, picha ndogo ‘passport size, nakala za vyeti vya taaluma za masomo ya hapo awali, ripoti ya tathmini ya utendaji kazi wake kazini kwa walioajiriwa kutoka kwa mwajiri na nakala ya kozi za awali alizokwishafanya.
Vituo vya Mitihani
Mkurugenzi huyo alisema mitihani itafanyika kati ya Mei na Juni mwaka huu katika vituo vinne vilivyoandaliwa katika vyuo.
Alisema kuwa chini ya mfumo huo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kitahusika na masuala ya Elimu huku Chuo Kikuu Tumaini Makumira cha Dar es Salaam (TUMADARCo) kikihusika na Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma.
Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA), kitahusika na Kilimo na Wanyamapori wakati Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU) kitahusika na masuala ya usimamizi na utawala,uhasibu, sheria na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).
“Kwa kuwa ndiyo tunaanza, tumeamua kutenga vituo vinne, lakini mwakani tunatarajia kuongeza viwe vingi ili kukidhi mahitaji ya wananchi walio wengi,”anasema Dk Maronga.

Monday, 15 April 2013

Raila, Kalonzo waenda Ikulu kwa Rais Uhuru










Lengo ni kufahamiana na kujadiliana kuhusu masuala ya nchi ya Kenya.
Nairobi. Vigogo wa Muungano wa Demokrasia na Mageuzi (Cord) wa Kenya, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wamerudi kutoka nchini Afrika Kusini na kumtembelea Rais Uhuru Kenyatta.
Ujio huo wa Odinga kwa mujibu wa msemaji wake, Dennis Onyango lengo lilikuwa  kufahamiana na kujadiliana masuala muhimu ya nchi.
Katika maongezi yao na Rais Kenyatta viongozi hao wa Muungano wa Cord walisema kwamba watahudhuria sherehe za kufunguliwa kwa Bunge la 11 nchini humo.
Akidhibitisha mbele ya waandishi wa habari taarifa za kuhudhuria sherehe hizo za kufunguliwa kwa Bunge hilo kwa viongozi hao Onyango alisema kwamba hayo ni makubaliano kati ya Uhuru na viongozi hao.
Alisema viongozi hao pia walijadiliana kuhusu namna  ya kukabili masuala yatakayowasilishwa bungeni kwa mtazamo wa kuridhiana.
Kwa sasa Muungano wa Jubilee unaounda serikali unamiliki mabunge yote mawili, huku maspika Justin Muturi na Ekwe Ethuro wa Bunge la Taifa na  la seneti mtawalia wakiwa wa Jubilee. Kwa hivyo, inatarajiwa kwamba ingawa Muungano wa Cord utakuwa upinzani kwa Serikali, hautakuwa na uwezo wa kupinga masuala muhimu.
Kwa upande wake Rais Kenyatta na Naibu wake  William Ruto waliahidi kuhakikisha kwamba upinzani unakua wa maana katika mabunge yote mawili na kwa Serikali kwa jumla.
“Walisema ni hamu yao kuona vyama vidogo vya upinzani vikitekeleza jukumu lao la kuiangalia Serikali ii isikiuke mipaka katika utendakazi wake,” alisema  Onyango.
Odinga alienda katika eneo Bunge la Khwisero kaunti ya Kakamega, ambapo alimwambia Rais Kenyatta asinunue wabunge wa Cord kuunga mkono upande wa Serikali.

Sh1 bilioni za kuzika viongozi zawakera wabunge




 Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola akichangia mjadala wa  Hotuba ya makadirio ya fedha katika Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2013/14 ambapo alitamka kutounga mkono makadirio hayo. Picha na Edwin Mjwahuzi 

Ni zilizotangazwa kutengwa kupitia Hotuba ya  Waziri Mkuu.
Dodoma. Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imelaumiwa kwa kutenga Sh1 bilioni kwa ajili ya maziko ya viongozi huku Watanzania wengi wakilia na umaskini mkubwa.
Shutuma hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki bungeni kwa nyakati tofauti wabunge akiwamo wa  Viti Maalumu Lucy Owenya (Chadema) na Kangi Lugola (Mwibara-CCM) wakati wakichangia hotuba ya makadirio ya bajeti katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/14.
Katika mchango wake Owenya alisema inatia aibu kuona kiasi kikubwa cha fedha kikitengwa kwa ajili ya maandalizi ya kuzika viongozi huku mambo muhimu na ambayo ni kipaumbele yakiachwa.
“Ni aibu na fedheha kubwa, hivi mmetenga kiasi hicho kwani mnajua nani atakufa na lini atakufa ndio maana mnajiandaa kumzika,” alihoji Owenya.
Mbunge huyo alikwenda mbele zaidi na kueleza kuwa Serikali imeshindwa kufikiri na hasa namna ya kuwaondolea umasikini na tabu wanazopata wananchi wake lakini inawaza habari za watu wanaojiandaa kufa.
Vile vile katika mchango wake Lugola ambaye alisema asingeunga mkono hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alihoji sababu za kutengwa kwa fedha hizo bila kujua nani atakufa lini.
Mbali na hilo, Owenya pia aliilaumu Ofisi ya Waziri kwa kushindwa kutumia mbinu mbadala za kuzuia matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi zinazotumiwa na wakuu wa mikoa kwa ajili ya kwenda Dodoma kufuatilia hotuba ya Waziri Mkuu.
Alimtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwatimua wakuu wa mikoa ili warudi mikoani kwao ili kuokoa fedha za walipa kodi zinazoteketea katika misafara yao mjini Dodoma.

Sunday, 14 April 2013

Spika asipuuze ushauri wa CAG



SPIKA wa Bunge, Anne Makinda hivi karibuni alizifanyia mabadiliko kamati za kudumu za Bunge, huku Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ikiunganishwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Ikumbukwe kuwa kamati hizi za uangalizi wa mashirika ya umma ziliundwa wakati wa uongozi wa Spika Samuel Sitta na kuwapa wapinzani waziongoze.
Kwa kipindi chote cha uhai wa kamati hizo, kwa kweli zilijitahidi kufanya kazi ya kufuatilia kwa ukaribu fedha za serikali ambazo zimekuwa zikifujwa hovyo bila utaratibu wa wazi.
Katika hatua ambayo haikutarajiwa, Spika Makinda alibadili utaratibu wa mtangulizi wake Sitta na hivyo akazivunja baadhi ya kamati na kuunda nyingine huku akiziunganisha POAC na PAC.
Lengo la Sitta lilikuwa ni kuongeza uwajibikaji wa serikali na ndiyo maana Bunge liliridhia kamati hizo tatu yaani Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC), Kamati ya Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ziongozwe na upinzani.
Uamuzi wa Spika Makinda kuziunganisha kamati za POAC na PAC umelalamikiwa na wengi akiwemo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Uttouh wakidai kila moja ilikuwa na majukumu makubwa ambayo hata hivyo hawakuyakamilisha, hivyo kuziunganisha ni kuwatishwa majukumu wajumbe wake.
Hata hivyo, wapo wanaoutazama uamuzi huo kama msukumo wa kisiasa wa Serikali ya CCM kujaribu kukibana chama kikuu cha upinzani bungeni na hivyo kutengeneza utaratibu huo kuwapunguzia madaraka.
Hivi karibuni CAG ameweka bayana kuwa kamati mpya ya PAC inahitaji muujiza wa Mungu kukamilisha kazi zake. Kwamba haiwezi kufikia nusu ya kazi zake za mwaka.
Alisema kabla ya kamati hizo kuunganishwa, POAC ilikuwa na mzigo mzito na sasa umeongezwa, ambapo katika hali ya kawaida itashindwa kufanya kazi ya kuisimamia serikali.
Hatupaswi kupuuza ushauri wa CAG. Huyu ni mtaalamu anayejua masuala ya fedha yalivyo na ugumu wake, hivyo kupendekeza kwake Kamati ya POAC irejeshwe kuna mantiki.
Ni wazi kuwa Spika wa Bunge alikurupuka pasipo kusikiliza mawazo ya wabunge katika uundwaji wa kamati mpya, vinginevyo kusingekuwa na manung’uniko haya tunayoyasikia leo.
Kosa hili la kuifuta kamati muhimu kama POAC kwa malengo ya kisiasa tu, ni tafsiri kwamba viongozi wetu hawajali maslahi ya watu na taifa kwa ujumla.
Tunaamini kuwa Spika wa Bunge kwa mamlaka aliyonayo ataufanyia kazi ushauri wa CAG kwa manufaa ya taifa letu ili kuokoa fedha za umma zisipotee holela.

Saturday, 13 April 2013

Muuza dawa za kulevya aliyeishia kukatwa mkono, mguu



Hata baada ya kuhamia Uswis bado maisha yanaendelea kuwa magumu.Alijikuta akiandamwa na majanga zaidi.
Mbembele anaendelea na simulizi yake, anasema mwishoni mwa mwaka 1999 alifanikiwa kuhamia nchini Uswizi, alijiandikisha kama mkimbizi kutoka Msumbiji.
Hali ilivyokuwa nchini Uswizi
“Nilivyofika Uswizi, nilipelekwa moja kwa moja kwenye kambi ya wakimbizi iliyokuwapo jimbo la Debendorf katika Jiji la Zurich, nilijitambulisha kama John ‘Chuma’ Fernando kutoka Msumbiji.
Alipokelewa vizuri na maofisa wa uhamiaji na kupewa chumba kilichokuwa na mahitaji muhimu ya maisha ya mtu wa kawaida.
“Nilianza maisha mapya katika kambi hiyo, nilikutana na wazamiaji wengi kutoka nchi za Afrika mashariki na kati kama Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Demokrasia ya Kongo,” anasema na kuongeza.
“Maisha yalikuwa mazuri kwa sababu tulikuwa tunapewa kiasi cha dola 600 kila mwezi pamoja na mahitaji na huduma nyingine kama za michezo na cha kufurahisha zaidi tulikuwa huru kufanya mambo yetu”.
“Baada ya maisha ya miaka mitatu kambini pale ilitokea kampeni ya kuwarudisha watu waliokuwa na mazingira mazuri nchini mwao kutokana na kuporomoka kwa uchumi katika nchi za Ulaya”
“Kiongozi wa kambi yetu ‘Shefa’ alisikia taarifa halisi za uraia wangu kuwa ni Mtanzania na akaamua kufikisha taarifa hizo kwa maofisa wa uhamiaji ambao walinipeleka kwa Balozi wa Msumbiji kwa mahojiano,” anabainisha na kuongeza;“Nilifikishwa kwa Balozi wa Msumbiji, nilifanya naye mahojiano kuhusu uraia wangu, baadaye alinishtukia kutokana na kutokuongea vizuri kireno”
Anasema baada kushtukiwa na balozi alimueleza kuwa yeye ni Mmakonde wa Msumbiji ambaye hakubahatika kwenda shule ndiyo maana hakuweza kuongea Kireno kwa Ufasaha.
“Nilimwambia natokea Mweda mji wa Msumbiji unaopakana na Tanzania ambapo watu wake walikuwa wanaongea Kimakonde mchanganyiko na Kireno kama mimi”
Mbembele anaongea kwa kuonyesha ushujaa wa kumshinda balozi katika maongezi kwa kumdanganya “Balozi alinibembeleza nirudi msumbiji lakini nilikataa kwa kudai kuwa sababu nilizoondokea kule bado hazikutatuliwa”.
“Baada ya maongezi, balozi alishindwa kutafuta sababu ya kuniruidisha Msumbiji hivyo nikaendelea na maisha ya ukimbizi pale Dubendorf,”anasimulia kuwa wakati akishangilia ushindi wa kumdanganya balozi kumbe alikuwa ameshawekwa katika kitabu cha watu watukutu na wenye makosa.
Matukio ya ushirikina na jaribio la kutolewa sadaka
Baada ya kushinda jaribio la kurudishwa nyumbani Mbembele anasema chuki ilizidi baina yake na baadhi ya raia wa Kenya waliokuwapo kambini hapo na kumtengenezea mazingira magumu ya kuishi.
“Nilikosa rafiki, nilihisi kila mtu ni adui yangu. Sikuwa na chakufanya zaidi ya kumuomba Mungu na kuendelea na maisha kwa kuwa raia wengi walikuwa wanarudishwa makwao kwa wingi”.

Anasema siku moja akiwa matembezini alikutana na wazungu watatu ambao walikuwa wanaelekea katika sherehe kubwa ya utamaduni wa Waswizi ambayo hujumuisha toleo la sadaka ya damu ya binadamu.
“Kule Uswizi tarehe 1 Agosti kila mwaka huazimishwa sherehe ya nchi nzima, baadhi ya wenyeji husherekea na kutoa sadaka ya damu kwa miungu na mizimu yao,” anabainisha Mbembele na kuongeza;
“Wale watu watatu walinibembeleza tukashirikiane nao katika sherehe hizo mpaka nikakubali kuandamana nao huku tukitembea taratibu kuelekea katika msitu mkali uliopo ndani ya milima iliyopo pembezoni mwa mji”
Huku akionyesha dalili za kusisitiza uwepo wa uchawi uliopitiliza huko Uswizi, Mbembele anasema “Wanasema Tanzania kuna uchawi, aaah uchawi Ulaya bwana”
“Tulipoingia katikati ya poli tukielekea katika viwanja maalumu vya sherehe hizo, mtu mmoja kati ya wale watatu alibadilika ghafla akawa kama sokwe mkubwa mwenye meno ya kutisha kiasi cha kunitisha na kufanya niishiwe nguvu” anasema na kuongeza kuwa jambo hilo lilimtisha mno na kumkosesha raha.

KONA YA SHERIA:Unachotakiwa kufahamu kuhusu ndoa kisheria



Kutokana na sheria ya ndoa ya Mwaka 1971, ndoa inatafsiriwa kuwa ni muungano wa hiari baina ya mwanaume na mwanamke, muungano unaokusudiwa kudumu kwa muda wote wa maisha yao.
Kutokana na tafsiri hiyo kuna mambo makuu matatu yanayotiliwa mkazo na tafsiri hiyo. Kwanza muungano huo lazima uwe wa hiari yaani usitokane na kushurutishwa ama na mzazi au mtu yeyote yule.
Ikiwa wawili hao watakuwa wamelazimishwa kufunga ndoa, basi ndoa hiyo haitakuwa ndoa kwa mujibu wa tafsiri ya ndoa katika sheria ya ndoa ya mwaka 1971.
Wapo ambao wakati mwingine unaweza kuona kwa mfano mzazi au mlezi anamlazimisha kuoana na fulani kwa sababu zake, ndoa kama hiyo kisheria sio haki na mwenye kulazimishwa anaweza kuamua akipenda kuachana na aina hiyo ya ndoa. Jambo la msingi ni kuhakikisha anayelalamika anakuwa ana ushahidi kwa kile ambacho analalamikia, kwa mfano anaweza kueleza namna alivyolazimishwa.
Ni kweli inawezekana fulani anafaa kuwa na mwanao, kisheria inashauriwa kutomlazimisha, badala yake lililo la msingi ni kushauri, kisha mtu mwenyewe aamue.
Pili ndoa lazima iwe muungano wa watu wawili na ni lazima watu hao wawe wa jinsia mbili tofauti yaani mwanaume na mwanamke. Kwa maana hiyo ndoa ya watu wa jinsia moja yaani mwanaume na mwanaume au mwanamke na mwanamke haitambuliki katika sheria ya ndoa ya mwaka 1971.
Siku hizi kuna watu wameanza kuja na mambo ya ndoa za jinsia moja, hizo ni aina ya ndoa ambazo kwa mujibu wa sheria za Tanzania hazikubaliki.
Tatu ni uhusiano huo uwe wenye kukusudiwa kudumu kwa muda wote. Lengo la kufunga ndoa ni ndoa hiyo idumu kwa kwa kipindi chote cha maisha ya wanandoa. Ndio kusema kwamba hakuna ndoa za mikataba, ya kusema labda mtaishi kwa muda fulani, kwa mfano mwaka mmoja.
Ndoa inayofungwa ikiwa na lengo ya kuvunjwa baada ya kipindi fulani si ndoa halali kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971.
Ndoa itavunjwa ikiwa kutabainika/kutajitokeza mambo yanayoweza kupelekea ndoa kuvunjika kama inavyobainishwa kwenye sheria ya ndoa na si vinginevyo.
Kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakikaa tu bila kuangalia namna gani wanaweza kuzingatia sheria za ndoa.Kwa mfano wapo watu ambao wamekuwa wakiishi tu, huku wao wakifikiri kwamba kuishi kwao kunatosha kuifanya ifahamike kama ndoa.
Kisheria ni kwamba kuna taratibu zake za kuzingatiwa ili watu wafahamike kama wanandoa.Kukubali kuishi tu bila kuzingatia taratibu za kisheria kunaondoa maana halisi ya ndoa hasa kwa mfano watu wenyewe wanapokuwa hawako tayari kuzifuata taratibu hizo.
Aina Za Ndoa
Kutokana na sheria ya ndoa ya mwaka 1971, ndoa zimemegawanyika katika aina mbili ambazo ndoa ya mke mmoja ambapo huhusisha mume mmoja na mke mmoja.
Aina ya pili ni ndoa ya wake wengi ambayo mume mmoja anakuwa na wake zaidi ya mmoja, waweza kuwa wawili ama zaidi kulingana na vile ambayo wahusika wenyewe wataona inafaa au kulingana na imani zao za dini, hata hivyo ni lazima kuwepo na makubaliano.

Chadema yatishia kujitoa mchakato wa Katiba Mpya

Dodoma na Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitajitoa katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo muhimu mawili hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu.

Wakati Chadema wakisema hayo, Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limesema uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba uliomalizika siku tatu zilizopita katika maeneo mbalimbali nchini haukuwa huru na ni batili, huku likipendekeza urudiwe katika maeneo yote yaliyokumbwa na kasoro.

Katika hoja zake, Chadema kimesema kinataka kufutwa kwa uteuzi/uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata na badala yake wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na Kamati za Maendeleo za Kata (WDC).
Msimamo huo ulitolewa na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati akisoma hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/14 huku akiitaka Serikali kuwasilisha muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ili maeneo kadhaa yafanyiwe marekebisho.

“Katika Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba tunataka marekebisho ya vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi katika Bunge Maalumu la Katiba wa taasisi zilizoainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Pia vifungu vyote vinavyohusu ushiriki wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Zanzibar katika mijadala inayohusu mambo yasiyokuwa ya Muungano.”

Jukwaa la Katiba
Kwa upande wake, Jukwaa la Katiba limesema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa kubadili mwenendo wake kuanzia katika utaratibu wa kuwapata wajumbe hao hadi uundwaji wa Bunge la Katiba na wananchi kupiga kura za maoni. Limesema isiporekebisha utaratibu huo, litakwenda mahakamani kusitisha mchakato mzima wa Katiba.

Kumalizika kwa uchaguzi huo kunaashiria kuanza kwa mabaraza ya Katiba Mei mwaka huu, ambayo yatakuwa yakijadili rasimu ya Katiba ambayo imetokana na maoni mbalimbali yaliyotolewa na wananchi.

Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba alisema uchaguzi huo ulikuwa na kasoro zaidi ya 15, ambazo ni itikadi za vyama na udini, rushwa, uchakachuaji, upendeleo, ubaguzi wa makundi ya watu wenye ulemavu na kukosekana kwa mwongozo timilifu wa uchaguzi huo.

Baadhi ya mikoa iliyokumbwa na kasoro hizo ni Dar es Salaam, Arusha, Mara, Singida na Dodoma. “Pia kulikuwa na vurugu katika uchaguzi huu, kukataliwa kwa barua za maombi za baadhi ya waombaji, kutokuwa na tarehe rasmi ya uchaguzi, uandikishaji bandia wa wapigakura, kukosekana kwa orodha ya majina ya wagombea katika mitaa na vijiji.”

Je hii ndiyo njia ya kujenga ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu?

Serikali imekataa ushauri wa wabunge na kusema kuwa itaendelea kuwaajiri wastaafu mbalimbali nchini hadi hapo soko la ajira litakapojitosheleza.
Mbali na hilo, jana Serikali ilitangaza bungeni kuwa kazi za wakuu wa mikoa siyo ajira rasmi, bali ni ajira za kisiasa ambazo hazipaswi kuhesabiwa.
Akijibu swali bungeni jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) Celina Kombani, alikiri kuwa bado Serikali inaendelea kutoa ajira kwa watu ambao wamestaafu na kuwa itaendelea kufanya hivyo kwa siku za usoni.
Alikuwa akijibu swali la Vicent Nyerere (Musoma-Chadema) ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kusitisha kutoa mikataba kwa wastaafu ili wahitimu wanaotoka vyuoni wapate ajira na kujenga nchi yao.
Mbunge huyo pia alihoji nafasi za wakuu wa mikoa nchini ambao wengi hufanya kazi wakiwa katika umri mkubwa, huku baadhi wakiwa wamestaafu utumishi wa umma. Waziri alisema ni kweli kuwa wako wataalamu wengi wanaohitimu vyuo vikuu hapa nchini ambao wanahitaji kuingia katika soko la ajira, lakini hupatiwa ajira kulingana na uwezo na bajeti ya Serikali.
Kuhusu wastaafu kuendelea kupewa ajira, alisema “Hilo linatokana na utaalamu walionao ambao ni vigumu kuziba nafasi zao kwa kipindi cha haraka.”
Kombani alizitaja kada ambazo Serikali inatoa mikataba kwa wastaafu kuwa ni walimu, waganga, wahandisi na wahadhiri wa vyuo ambao

Tuesday, 9 April 2013

Hatua za dharura kutumika kudhibiti dawa za kulevya Zanzibar













Zanzibar. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Serikali italazimika kuchukua hatua za dharura katika kukabiliana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini.
Alisema wafanyabiashara hao wamekuwa wakiwatumia vijana kwa ajili ya kununua na kusambaza dawa za kulevya, bila ya kuzingatia athari zitokanazo na biashara hiyo haramu ambayo pia huzorotesha maendeleo ya kiuchumi kwa taifa.
Maalim Seif alieleza jhayo jana ana katika hafla ya ufunguzi wa kampeni ya kupunguza matumizi ya dawa za kulevya na athari zake shuleni, iliyofanyika Shule ya Sekondari ya Lumumba.
Alisema hatua za dharura ni lazima zitumike katika kuwashughulikia wafanyabiashara hao, vyenginevyo taifa litaendelea kuangamia kutokana na matumizi makubwa ya dawa za kulevya.
Alifahamisha kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wamekuwa wakijali zaidi maslahi yao, na kuamua kuwatumia vijana kuendeleza biashara na matumizi ya dawa hizo, jambo ambalo halikubaliki kwa mustakbali wa Zanzibar.
Aliwahadharisha vijana kuwa makini na wafanyabiashara hao na kutokubali kutumiwa katika biashara hiyo. Ufunguzi wa kampeni hiyo iliyoandaliwa na “Sober Houses” chini ya ufadhili wa Hoteli ya “Double Tree Tanzania”, ulikwenda sambamba na uzinduzi wa chapisho maalum la kitabu ambacho kitatumika kufundishia shulen