SPIKA wa Bunge, Anne Makinda hivi karibuni alizifanyia mabadiliko kamati za kudumu za Bunge, huku Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ikiunganishwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Ikumbukwe kuwa kamati hizi za uangalizi wa mashirika ya umma ziliundwa wakati wa uongozi wa Spika Samuel Sitta na kuwapa wapinzani waziongoze.
Kwa kipindi chote cha uhai wa kamati hizo, kwa kweli zilijitahidi kufanya kazi ya kufuatilia kwa ukaribu fedha za serikali ambazo zimekuwa zikifujwa hovyo bila utaratibu wa wazi.
Katika hatua ambayo haikutarajiwa, Spika Makinda alibadili utaratibu wa mtangulizi wake Sitta na hivyo akazivunja baadhi ya kamati na kuunda nyingine huku akiziunganisha POAC na PAC.
Lengo la Sitta lilikuwa ni kuongeza uwajibikaji wa serikali na ndiyo maana Bunge liliridhia kamati hizo tatu yaani Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC), Kamati ya Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ziongozwe na upinzani.
Uamuzi wa Spika Makinda kuziunganisha kamati za POAC na PAC umelalamikiwa na wengi akiwemo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Uttouh wakidai kila moja ilikuwa na majukumu makubwa ambayo hata hivyo hawakuyakamilisha, hivyo kuziunganisha ni kuwatishwa majukumu wajumbe wake.
Hata hivyo, wapo wanaoutazama uamuzi huo kama msukumo wa kisiasa wa Serikali ya CCM kujaribu kukibana chama kikuu cha upinzani bungeni na hivyo kutengeneza utaratibu huo kuwapunguzia madaraka.
Hivi karibuni CAG ameweka bayana kuwa kamati mpya ya PAC inahitaji muujiza wa Mungu kukamilisha kazi zake. Kwamba haiwezi kufikia nusu ya kazi zake za mwaka.
Alisema kabla ya kamati hizo kuunganishwa, POAC ilikuwa na mzigo mzito na sasa umeongezwa, ambapo katika hali ya kawaida itashindwa kufanya kazi ya kuisimamia serikali.
Hatupaswi kupuuza ushauri wa CAG. Huyu ni mtaalamu anayejua masuala ya fedha yalivyo na ugumu wake, hivyo kupendekeza kwake Kamati ya POAC irejeshwe kuna mantiki.
Ni wazi kuwa Spika wa Bunge alikurupuka pasipo kusikiliza mawazo ya wabunge katika uundwaji wa kamati mpya, vinginevyo kusingekuwa na manung’uniko haya tunayoyasikia leo.
Kosa hili la kuifuta kamati muhimu kama POAC kwa malengo ya kisiasa tu, ni tafsiri kwamba viongozi wetu hawajali maslahi ya watu na taifa kwa ujumla.
Tunaamini kuwa Spika wa Bunge kwa mamlaka aliyonayo ataufanyia kazi ushauri wa CAG kwa manufaa ya taifa letu ili kuokoa fedha za umma zisipotee holela.

No comments:
Post a Comment