Saturday, 13 April 2013

Muuza dawa za kulevya aliyeishia kukatwa mkono, mguu



Hata baada ya kuhamia Uswis bado maisha yanaendelea kuwa magumu.Alijikuta akiandamwa na majanga zaidi.
Mbembele anaendelea na simulizi yake, anasema mwishoni mwa mwaka 1999 alifanikiwa kuhamia nchini Uswizi, alijiandikisha kama mkimbizi kutoka Msumbiji.
Hali ilivyokuwa nchini Uswizi
“Nilivyofika Uswizi, nilipelekwa moja kwa moja kwenye kambi ya wakimbizi iliyokuwapo jimbo la Debendorf katika Jiji la Zurich, nilijitambulisha kama John ‘Chuma’ Fernando kutoka Msumbiji.
Alipokelewa vizuri na maofisa wa uhamiaji na kupewa chumba kilichokuwa na mahitaji muhimu ya maisha ya mtu wa kawaida.
“Nilianza maisha mapya katika kambi hiyo, nilikutana na wazamiaji wengi kutoka nchi za Afrika mashariki na kati kama Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Demokrasia ya Kongo,” anasema na kuongeza.
“Maisha yalikuwa mazuri kwa sababu tulikuwa tunapewa kiasi cha dola 600 kila mwezi pamoja na mahitaji na huduma nyingine kama za michezo na cha kufurahisha zaidi tulikuwa huru kufanya mambo yetu”.
“Baada ya maisha ya miaka mitatu kambini pale ilitokea kampeni ya kuwarudisha watu waliokuwa na mazingira mazuri nchini mwao kutokana na kuporomoka kwa uchumi katika nchi za Ulaya”
“Kiongozi wa kambi yetu ‘Shefa’ alisikia taarifa halisi za uraia wangu kuwa ni Mtanzania na akaamua kufikisha taarifa hizo kwa maofisa wa uhamiaji ambao walinipeleka kwa Balozi wa Msumbiji kwa mahojiano,” anabainisha na kuongeza;“Nilifikishwa kwa Balozi wa Msumbiji, nilifanya naye mahojiano kuhusu uraia wangu, baadaye alinishtukia kutokana na kutokuongea vizuri kireno”
Anasema baada kushtukiwa na balozi alimueleza kuwa yeye ni Mmakonde wa Msumbiji ambaye hakubahatika kwenda shule ndiyo maana hakuweza kuongea Kireno kwa Ufasaha.
“Nilimwambia natokea Mweda mji wa Msumbiji unaopakana na Tanzania ambapo watu wake walikuwa wanaongea Kimakonde mchanganyiko na Kireno kama mimi”
Mbembele anaongea kwa kuonyesha ushujaa wa kumshinda balozi katika maongezi kwa kumdanganya “Balozi alinibembeleza nirudi msumbiji lakini nilikataa kwa kudai kuwa sababu nilizoondokea kule bado hazikutatuliwa”.
“Baada ya maongezi, balozi alishindwa kutafuta sababu ya kuniruidisha Msumbiji hivyo nikaendelea na maisha ya ukimbizi pale Dubendorf,”anasimulia kuwa wakati akishangilia ushindi wa kumdanganya balozi kumbe alikuwa ameshawekwa katika kitabu cha watu watukutu na wenye makosa.
Matukio ya ushirikina na jaribio la kutolewa sadaka
Baada ya kushinda jaribio la kurudishwa nyumbani Mbembele anasema chuki ilizidi baina yake na baadhi ya raia wa Kenya waliokuwapo kambini hapo na kumtengenezea mazingira magumu ya kuishi.
“Nilikosa rafiki, nilihisi kila mtu ni adui yangu. Sikuwa na chakufanya zaidi ya kumuomba Mungu na kuendelea na maisha kwa kuwa raia wengi walikuwa wanarudishwa makwao kwa wingi”.

Anasema siku moja akiwa matembezini alikutana na wazungu watatu ambao walikuwa wanaelekea katika sherehe kubwa ya utamaduni wa Waswizi ambayo hujumuisha toleo la sadaka ya damu ya binadamu.
“Kule Uswizi tarehe 1 Agosti kila mwaka huazimishwa sherehe ya nchi nzima, baadhi ya wenyeji husherekea na kutoa sadaka ya damu kwa miungu na mizimu yao,” anabainisha Mbembele na kuongeza;
“Wale watu watatu walinibembeleza tukashirikiane nao katika sherehe hizo mpaka nikakubali kuandamana nao huku tukitembea taratibu kuelekea katika msitu mkali uliopo ndani ya milima iliyopo pembezoni mwa mji”
Huku akionyesha dalili za kusisitiza uwepo wa uchawi uliopitiliza huko Uswizi, Mbembele anasema “Wanasema Tanzania kuna uchawi, aaah uchawi Ulaya bwana”
“Tulipoingia katikati ya poli tukielekea katika viwanja maalumu vya sherehe hizo, mtu mmoja kati ya wale watatu alibadilika ghafla akawa kama sokwe mkubwa mwenye meno ya kutisha kiasi cha kunitisha na kufanya niishiwe nguvu” anasema na kuongeza kuwa jambo hilo lilimtisha mno na kumkosesha raha.

No comments: