Kigali.
Rais Paul Kagame wa Rwanda ameonya kwamba yeyote atakayewasaliti
Wanyarwanda na Serikali yake anastahili kuchukuliwa hatua kali na kwamba
amejitolea maisha yake kuijenga na kuhakikisha Rwanda inakuwa salama
dhidi ya wote wasio na mapenzi mema.
Akizungumza katika ibada maalumu ya kuliombea
taifa juzi, Kagame aliwataka Wanyarwanda wote kuungana katika kusimamia
misingi sahihi na msimamo wao kama taifa, bila kujali tetesi zinazotoka
katika mataifa ya nje kuhusu wale waliotangaza kuisaliti Serikali yake.
Japokuwa hakutaja moja kwa moja kuhusu tuhuma
zinazoikabili Serikali yake kuhusiana na mauaji ya aliyewahi kuwa Mkuu
wake wa Ujasusi aliyeuawa Januari mosi akiwa hotelini huko Afrika
Kusini, Patrick Karegeya, alisema wale wote wanaoigeuka nchi yao na
kuchagua kuua raia wasio na hatia kwa sababu zao binafsi wanastahili
kushughulikiwa ipasavyo.
“Sitakuwa na huruma na watu ambao wanasahau namna
Rwanda ilivyowatengeneza na kuwa hapo walipo na hatimaye wanaamua
kuisaliti kwa kuua raia wa Rwanda wasio na hatia, wakiwemo kinamama na
watoto,” aliongeza.
Alisema Rwanda haina sababu ya kuhusishwa au
kuwajibishwa kwa ajili ya wale walioamua kuchukua njia zaidi na kufanya
mambo yao kwa nia ya kuharibu yale yaliyofanyika kwa ajili ya
kuliimarisha taifa la Rwanda.
Aliwataka viongozi wa Rwanda kutokusumbuliwa kwa
yanayowakuta ‘maadui wa taifa’ kwa kuwa Mungu aliwapa nguvu ya kujenga
na pia kukilinda kile walichokijenga, hivyo wale wanaosahau kwamba wana
dhamana kwa Wanyarwanda na kuamua kutenda mambo mabaya dhidi ya taifa
lao ni hakika kwamba wamesahau kuwa hawataweza kuwa juu ya watu wao.
“Mliponiapisha kuwa kiongozi wenu mliniagiza kwamba wakati wote niilinde nchi hii, kwa maana ya kusimama kwa ajili ya watu wake.
Lakini kila mmoja miongoni mwenu ana wajibu,
aidha kwa njia ya kuhubiri au kukanusha tuhuma zozote za uongo kuhusu
Rwanda,” alisema Kagame kama alivyokaririwa na gazeti la New Times la
Rwanda.
Alisema watu wa mataifa ya nje ambao wamekuwa wakiinyooshea kidole Kigali wamekuwa wakifanya hivyo mara 1000 zaidi kwa ajili ya kulinda nchi zao.
Hakusita kukumbusha kwamba wapo baadhi ya watu
ambao wamekuwa wakitishia wazi hadharani kutaka kuipindua Serikali na
wamekuwa wakishiriki katika mikakati ya ulipuaji wa mabomu
yaliyosababisha mauaji ya raia kwenye Mji wa Kigali.
Tutapambana
Mtandao wa Chimreports.com uliripoti kwamba Kagame
alionekana ‘mwenye hasira’ aliposema: “Kwa wale waliotengenezwa na kuwa
juu na Rwanda kisha kutugeuka kama taifa tutapambana nao. Yeyote
anayeidharau Rwanda atashughulikiwa ipasavyo popote alipo.”
Serikali ya Afrika Kusini
Msemaji wa Wiara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini,
Clayson Monyela alisema hajapata taarifa zozote kuhusu kauli hizo za
Kagame na hata hivyo hawezi kusungumzia suala hilo kwa kuwa liko nje ua
uhusiano wa kidiplomasia baina ya Rwanda na nchi yake.
Hiyo ni kwa sababu Kagame hakutaja nchi yoyote
katika hotuba yake hiyo ya jumapili na Afrika Kusini haiwezi kuchukua
hatua ya kujihisi kwamba labda ndiyo inayohusika.
“Tukio lililotokea Johannesburg liko chini ya
uchunguzi wa polisi na wote tunasubiri matokeo ya uchunguzi huo. Hatuna
sababu ya kuanza kumhisi mkuu yeyote wa nchi, hatuendeshi diplomasia
yetu kwa mtindo huo,” alisistiza.
Kejeli
Jumamosi iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Rwanda,
Jenerali James Kabarebe alikaririwa na mtandao wa AFP akizungumzia
yaliyomkuta Karegeya aliyeuawa huko Afrika Kusini akisema: Unapochagua
kuishi kama mbwa, utakufa kama mbwa.”
Alikaririwa akisema, “Msipoteze muda wenu kwenye
ripoti kwamba fulani aliuawa kwa kutumia kamba katika gorofa ya saba
kwenye nchi fulani. Unapochagua kuwa mbwa, utakufa kama mbwa, na wafanya
usafi watasafisha na kutupa kwenye pipa la taka ili usiwachafue.
“Kimsingi hayo ni mambo yanayowapata waliochagua
kupitia njia hiyo. Hatuna la kufanya juu yao, na hatuwezi kulaumiwa kwa
ajili ya yanayowakuta,” alisema.
Mauaji ya Karegeya
Mwili wa Patrick Karegeya aliyekuwa mshirika wa
Rais Kagame kisha kutofautiana na kukimbilia uhamishoni nchini Afrika
Kusini ulikutwa ukiwa kwenye chumba cha hoteli mjini Johannesburg huku
kukiwa na kitambaa chenye damu na kamba kando yake.
Baada ya polisi kueleza kwamba Karegeya aliuawa
kwa kunyongwa, wasaidizi wake waliituhumu Serikali ya Rwanda kwa
kuhusika na mauaji hayo.
Karegeya alikuwa mkuu wa usalama wa taifa
akihusika na usalama wa nje wa Serikali ya Rais Kagame. Mwaka 2004
alishushwa cheo kisha kukamatwa na kuswekwa jela kwa miezi 18 kwa madai
ya kwenda kinyume na mkuu wake wa kazi. Alikimbia nchini Rwanda mwaka
2007.
Pamoja na wapinzani wa Kagame kumtuhumu moja kwa moja kuhusika na mauaji hayo, Serikali yake haikuwahi kukubali au kukanisha moja kwa moja, lakini kwa kauli yake alisema juzi kwamba ‘Hahitaji kuomba ruhusua kwa yeyote anaposimamia ulinzi wa taifa lake.”
Pamoja na wapinzani wa Kagame kumtuhumu moja kwa moja kuhusika na mauaji hayo, Serikali yake haikuwahi kukubali au kukanisha moja kwa moja, lakini kwa kauli yake alisema juzi kwamba ‘Hahitaji kuomba ruhusua kwa yeyote anaposimamia ulinzi wa taifa lake.”

No comments:
Post a Comment