Katika ushabiki wa kisasa tunaweza kufikia hatua ya kuchapana makonde mpaka kupelekana mahakamani, lakini tunaposikia ‘Bit’ kabla ya mashairi, taratibu kila mtu utamwona anaanza kujiachia bila kujali amekutana na hasimu wake wa kisiasa.
Hatua hiyo inatokana na nguvu iliyopo ndani ya
muziki hususan ule uliongia katika karne hii ya 21, kwa staili mpya za
kubana pua(R&B) na kufoka foka(Hip Hop).
Hata hivyo wakati hali hiyo ikijitokeza, kumekuwa na mtazamo, dhana na hofu juu ya wasanii wanaojihusisha kwa karibu na shughuli za kisiasa kwamba wanaweza kupoteza nguvu katika soko lao kimuziki.
Baadhi ya mashabiki waliozungumza na Starehe,
wanasema hatua hiyo inaweza kusababisha idadi kubwa ya vijana ambao ni
mashabiki wa Bongo Fleva, huku wakiwa wamejikita zaidi katika ushabiki na mivutano ya kisiasa.
Kutokana na mtazamo huo kwa mashabiki, Starehe
imefanikiwa pia kuzungumza na baadhi ya wasanii wahusika ambao wako
kwenye siasa pamoja na mameneja ambao husimamia soko la muziki huo hapa
nchini.
Akizungumza na Starehe siku chache
baada ya mvutano wa mbunge wa Kigoma Kaskazin Zitto Kabwe na Chama
chake, Sunday Mangu ambaye ni kiongozi wa kundi la wasanii kutoka Mkoa
wa Kigoma (KAS), anasema ni hatari kwa msanii kujihusisha moja kwa moja
katika mgogoro na ushabiki wa kisiasa.
“Msanii hutakiwi kuwa sehemu ya ushabiki ila
hatukatazwi kutoa ‘sapoti’ za kisiasa. Kwa mfano Zitto tumekuwa naye
bega kwa bega kwenye mgogoro huo kama kijana mwenzetu ambaye amekutana
na changamoto katika nafasi yake ya kisiasa,” anasema na kuongeza;
“Endapo msanii atafanya hivyo anaweza kujitenga na
kundi fulani kwenye jamii hatua ambayo siyo sahihi, msanii hana kundi
wala hatakiwi kuwa kwenye itikadi zozote za ushabiki.
Hata hivyo kwa upande wake Profesa Jay anafafanua
akisema kuwa msanii kutumiwa kwenye kampeni za kisiasa haimaanishi kuwa
yeye ni sehemu ya chama kile.
Jay anasema kwa msanii ambaye anatumika tu kwenye
kampeni za siasa haoni kama inaweza kuathiri kazi zake na kwamba
anachoangalia ni maslahi ya kazi yake.
“Msanii anatumiwa kwa pesa huwezi kusikia msanii
anafanya kampeni bila malipo, mimi sijawahi kufanya kampeni na siwezi
kujua moja kwa moja zimewaathiri vipi lakini sijawahi kuona kama kuna
msanii yeyote aliyetumika kisiasa na akaathirika kimuziki,” anasema Jay.
Hata hivyo Jay anaongeza kuwa msanii pia ni
binadamu kama wengine ambao wana haki ya kuwa na hisia katika ushabiki
wa mambo wanayoyapenda katika jamii.
Akitoa mfano, Jay anasema msanii kabla ya kuwa msanii
inawezekana alikuwa ni shabiki wa Simba, hivyo hawezi kuacha ushabiki
wake kwa sababu ya muziki, kutokana na hofu ya kuathiri soko lake kwa
mashabiki wa Yanga.
“Msanii kuwa na Kadi ya CCM au Chadema siyo dhambi
pia japokuwa inaweza kuwa mbaya zaidi pale atakapojiingiza zaidi kwenye
ushabiki wa kisiasa, binafsi sioni kama kuna tatizo ila mashabiki
wanapaswa kujua msanii anapofanya hivyo ni sehemu ya kazi yake,” anasema
Jay.Mbali na Jay, Afande Sele anasisitiza kuwa athari zinaweza
kujitokeza katika upande wa wadau wa muziki.
“Wadau wa muziki wanaweza kuwa wamegawanyika
katika makundi ya kisiasa kwa hivyo msanii unaweza kuwa chama fulani
wakati mdau ambaye anatakiwa ‘kukusapoti’ bila kujua kumbe ana hisia na
chama kingine cha siasa. Kwa mazingira hayo msanii unaweza kukosa msaada
kwake,” anasema Sele.
Sele anasema pamoja na hofu hiyo lakini hakuna shabiki yeyote ambaye anaweza kumsaliti msanii kutokana na itikadi za kisiasa.
Anaongeza kuwa shabiki ambaye anaweza kuwa na dhana ya kumsaliti msanii kwa sababu za kisiasa, atakuwa hajamtendea haki.
“Mimi hakuna ambaye hajui kwa sasa ni mwanachama
wa Chadema, lakini bado ninapopanda jukwaani nashangiliwa na mashabiki
wangu wote wakiwamo hata wa vyama vingine. Hapo siasa inakuwa pembeni
kabisa,” anasema Sele na kuongeza;
Kinachofanya msanii aendelee kukubalika kwa mashabiki wa aina zote ni kutokana na aina ya mashairi na ubora wa kazi zake.
Anasema shabiki mwenye mapenzi ya dhati kwa
msanii, hawezi kubadilishwa mtazamo na mapenzi yake kwa itikadi hizo za
kisiasa na badala yake mapenzi yataongeza kutokana na mwendelezo wa
harakati.
“Kama mashairi yangu yalikuwa ni kugusa ukweli
halisi wa maisha na udhaifu wa viongozi, naamini kuingia kwenye siasa
itakuwa ni ushawishi zaidi kwa watu wanaohitaji mabadiliko,” anasema
Sele.
Mameneja wanasemaje?
Meneja maarufu wa kundi la Tip Top Connection, Diamond,
Shaa na wasanii wengine kadhaa anayejulikana kwa jina la Babu Tale,
kwanza anasema ifahamike wazi kuwa msanii hana dini wala chama chochote
anachokitumikia kupitia muziki wake.
Tale anasema msanii ni kama mfanyakazi yeyote mwingine ambaye yuko tayari kufanya kazi kwa ajili ya kuangalia masilahi yake.
“Kesho unaweza kumwona amevaa tisheti za CCM, lakini baada ya siku kadhaa utamwona Chadema endapo watapanda dau zuri. Hilo ni jambo muhimu sana kwa mashabiki kuelewa kabla ya kuyumbishwa na dhana za kisiasa,” anasema Tale na kuongeza;
Katika uchaguzi wa mwaka 2010 alitumika kwenye
kampeni za Rais Kikwete akiwa na wasanii wake mbalimbali anaowasimamia.
“Tulikubaliana kufanya shoo zile kwa sababu za kimasilahi, inawezekana
siku nyingine ukawaona wasanii hao hao wakapanda kwenye jukwaa za vyama
vingine.
Kwa upande wake Meneja wa kundi la Wanaume
family(TMK), Said Fela anaongeza akisema changamoto kubwa iliyopo ni
mashabiki ambao hawaelewi nini ambacho msanii anazingatia katika kazi
zake.
Anasema kinachojitokeza ni mtazamo usiosahihi kwa
mashibiki na kutokuelewa kama msanii anaweza kufanya shoo yoyote kama
sehemu ya kazi zake kimuziki.
“Mashabiki wetu siwezi kuwahukumu kwani hawana
ubaguzi hata kidogo, hawawezi kubadilishwa mapenzi yao kwa msanii kwa
sababu za kisiasa, hatujafikia hatua ya kuwa na siasa au mashabiki wa
aina hiyo,” anasema Fela.
Akitoa mfano Fela anasema msanii wa Hip Hop, Joseph Mbilinyi ambaye kwa sasa ni mbunge wa Mbeya Mjini, bado hajaathiriwa na siasa katika soko lake la muziki.
“Kama wasanii kujihusisha na siasa ingekuwa na athari basi
‘Sugu’ leo hii asingeweza kufanya shoo ambayo inaweza kuchanganya
mashabiki wa aina zote bila kujali itikadi za vyama vyao,” anasema Fela
na kuongeza;
Kwa hivyo mimi nadhani huo ni mtazamo ambao siyo
sahihi kabisa, muziki wetu bado haujawa na tatizo kama hilo na siamini
kama linaweza kujitokeza katika siku za mbele.

No comments:
Post a Comment