Bado tunazungumzia habari za mwaka mpya mpaka labda tutakapoingia mwezi wa pili. Mwaka mpya, mambo mapya au siyo?
Mwaka mpya umeanza, kila mtu sasa anazungumzia
mipango yake kwa mwaka huu, huku wengine wakiwa na viporo vya mwaka
jana, hata hivyo siyo ishu kwa kuwa huu ni mwaka mwingine na una mambo
yake.
Ni mipango mizuri kuitamka na mitamu kuisikiliza,
lakini je, huu ni uhalisia au tunatekeleza wajibu wetu kwa kuwa ndiyo
maongezi yaliyotawala vinywa vyetu mwezi huu.
“Ninataka kubadilika, mwaka huu pombe no, situmii pesa ovyo, lazima nijenge, nitapunguza uzito, naacha sigara n.k,” hii ni baadhi tu ya misemo inayotawala mwezi huu.
Ni mitamu kweli kweli kuitamka na hata usikilizapo
huleta raha. Kwa mhusika huenda inampa picha nzuri mbeleni kwani
ikifanikiwa itakuwa bao la kisigino.
Cha kujiuliza hapa hivi ni kweli lazima tusubiri
Januari mosi kuanza kutafuta mabadiliko katika maisha yetu, yaani
ninaweza kuwa mtu tofauti Desemba 31, halafu nikaamka Januari mosi na
kuwa mwingine.
Usiku wa mwaka mpya unalala ukiwa njwii kwa ulevi wa pombe, lakini ukiwa na matarajio ya kuacha ulevi kesho yake.
Kama ulikuwa hufahamu basi
huu ndiyo ukweli, ni asilimia nane tu ya watu wote duniani ndio
hufanikiwa kwa kutegemea mwaka mpya kubadilika, wengine wakijitahidi
sana ni wiki moja tu baada ya hapo wanarudia maisha yao ya zamani.
Ni kujidanganya kudhani kuwa ifikapo tarehe fulani, unaweza kuiondoa tabia iliyojizoesha kwa miaka mingi.
Kisaikolojia unapojipangia tarehe za kubadilika
katika kitu fulani, unakuwa unajiwekea ugumu kwani inatakiwa pale
unapogundua tatizo uanze kulifanyia kazi na si kulipangia tarehe.
Maneno matupu hayavunji mfupa. Kupanga nitafanya hivi siku fulani ni sawa na usemi huo kwani hayo ni maneno matupu.
Kwa wenye tabia hii ni rahisi kusahau ulijipangia nini mara itakapingia Februari, pengine utaanza kuikumbuka mipango yako pale watu watakapoanza kuzungumza habari za mwaka kwisha.
Ikishafika Oktoba au Novemba kauli za ‘mwaka umeisha huu’ huanza
kutawala maongezi yetu, hapo ndipo unaweza kukumbuka ulichojipangia kwa
mwaka huu, lakini kwa kuwa ni mtu wa mwaka mpya basi utaona isiwe shida nitaaanza tena mwakani.
Kama unatamani mabadiliko basi usisubiri mwaka
mpya, unapogundua kitu ndani yako ambacho ungependa kibadilike basi
kifanyie kazi mara moja.
Mabadiliko hayaji mara moja bali kwa hatua ndogondogo, chukua hatua pale unapoona unapaswa kuanza.
Kuna matatizo mengine unapoyachelewesha ndipo
yanapokuwa makubwa zaidi, badala ya kutumia muda mfupi kuyatatua unaweza
kujikuta unatumia nguvu na pesa nyingi.
Mwaka mpya uwe wa kusherehekea sikukuu na mfanikio
ambayo kwa uchache umeyafanikisha. Usisubiri mwaka mpya kuanza kufanya
kitu fulani.

No comments:
Post a Comment