Pia azimio la tano ni mamlaka husika za kifedha na
za kiuchunguzi kuitaja Benki ya Stanbic na benki nyingine yoyote
itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi,
kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya
Escrow, kuwa taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
Azimio la sita alilitaja Zitto kuwa ni kuiomba Serikali iandae
na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda Takukuru kwa
lengo la kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia, kupambana na
kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi
zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisasa.
Alisema azimio la saba la Bunge ni kuitaka
Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na
kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.
Katika azimio lake la nane Bunge liliazimia kwamba
Serikali itekeleze azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa
vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge la Bajeti
Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya
umeme.
Wakichangia mapendekezo hayo mapya yaliyosomwa na
Zitto, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe alisema
wamekubaliana na mapendekezo hayo mapya manane yanayotosha kufikisha
ujumbe.
Alisema ni muhimu viongozi wa Serikali wakalinda
rasilimali za nchi kwa kutekeleza wajibu wao wakijua Watanzania wengi
masikini wanawategemea wao kuwatoa kwenye umaskini.
“Niombe tu Waziri Mkuu awe mkali ili tusifike
kwenye mshike mshike kama huu tuliofikia kwa sasa,” alisema Mbowe na
kuongeza: “Waziri Mkuu uwe mkali kwa kweli.”
Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe ambaye ni
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) alilishukuru
Bunge kwa kufanya kazi yake akieleza kuwa limeweka maslahi ya nchi kwa
kushikana pamoja.
“Kumekuwa na makosa yamefanyika kwenye baadhi ya maeneo, hivyo hatua zimechukuliwa,” alisema Filikunjombe.
Alisema anafurahi kwamba hatua stahiki zimechukuliwa kwa waliohusika.
“Sasa hatua stahiki zitachukuliwa kwa kila mmoja kwa nafasi yake,” alisema.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira alisema juzi hali ilikuwa mbaya,
lakini wameweza kuridhiana kwa kuwa wote ni binadamu.
Alisema mtafaruku uliotokea umewafundisha kwamba wanaweza kukubaliana wakijadiliana.
“Kazi haikuwa rahisi, lakini tumeelewana na
aliyosema Zitto ndiyo tuliyokubaliana kwa kuwa CCM haina sera ya
kukubali jambo lolote ambalo linaminya maendeleo ya wananchi,” alisema.
Alisema Serikali ina wajibu wa kutekeleza maazimio
ya Bunge hivyo yanayowagusa wenzao ndani ya Serikali watawajibika kwa
kuwa ndiyo wajibu.
“Sasa hivi kila mhimili umeguswa hivyo tutatekeleza,” alisema Wasira.
Spika Anne Makinda aliwaonya wabunge kuachana na
watu wenye fedha wanaotoa kwa lengo la kuwahonga, kwani zitawaweke
pabaya kwa kuwa hawana kinga za makosa ya jinai.
Bunge laendelea jana asubuhi
Baada ya juzi Spika Makinda kuahirisha Bunge kwa
kushindwa kufikia mwafaka, jana Bunge liliendelea asubuhi, lakini baada
ya wabunge kuingia Spika alitangaza kuahirisha Bunge hadi saa tano
asubuhi ili vyama vikafanye vikao kwa ajili ya kutafuta suluhu ni maneno
gani yatumike katika mapendekezo ya Kamati ya PAC yanayotaka kuwang’oa
vigogo wote wa Serikali wanaotuhumiwa kuhusika na sakata hilo.
Wakati Spika akitoa maelekezo hayo tayari asubuhi
na mapema wabunge wa Kambi ya Upinzani walioungana wote walikuwa
wameshakutana kwenye Ukumbi wa Msekwa kuweka msimamo kuhusu mapendekezo
hayo.
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini na
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) Mchungaji Peter Msigwa walisema kuwa
kikao chao kiliamua kuwa wasimamie mapendekezo yote yaliyopendekezwa na
kamati kama yalivyo na lisibadilishwe hata moja.
Selasini alisema wabunge wa CCM wanachotaka
kufanya ni kuwaokoa watuhumiwa, lakini wao wanaingia bungeni na msimamo
mmoja wa kutaka mapendekezo yote ya PAC yapite kama yalivyo.
“Wakikataa tutamalizana pale ndani,” alisema
Selasini huku Msigwa akisema, “Wanataka kutufanyia uhuni, sisi tunataka
mapendekezo yote ya kamati yapite kama yalivyo.”
Wakati upinzani ukiwa na msimamo huo na kuendelea
na shughuli zao Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi alionekana akizunguka kuwaomba wabunge wa CCM
waelekee White House (Makao Makuu ya CCM Dodoma) kwa ajili ya kikao
chao.
Hata hivyo, wabunge wengine wa CCM walionekana kutojali kikao
hicho huku wakiendelea mazungumzo na wabunge wa upinzani huku
wakipongezana na wengine wakikandiana kutokana na jambo lililotokea
juzi.
Bunge larejea saa tano na kuahirishwa
Kikao cha Bunge kilirejea jana saa tano baada ya
kuahirishwa asubuhi na Spika alimpa nafasi Lukuvi ambaye alitoa hoja ya
kuomba Bunge liridhie kuongeza muda wa saa moja kwa ajili ya pande zote
mbili kufanya mashauriano na kurudi na kauli moja kama Bunge. “Nilikuwa
naomba tuahirishe Bunge kwa saa moja ili tuendelee na mashauriano na
kuja na kauli moja,” alisema Lukuvi.
Hoja hiyo ilipingwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema),
John Mnyika aliyesema kuwa haiwezekani wakatoka nje kwenda kwenye
mashauriano ya kukubaliana na msimamo wa CCM na kusema ni kauli moja ya
Bunge. “Haiwezekani tukatoka na kauli moja kwa kuweka msimamo wa
misimamo ya kichama,” alisema Mnyika.
Lukuvi alisimama tena na kusema; “Tumeomba saa
moja tuendelee na mashauriano ili tutoke pamoja na siyo suala la vyama
hapa. Tunataka tushauriane kama Bunge.”
Baada ya Lukuvi kumaliza, Spika Makinda alisema
anatoa muda hadi saa kumi jioni ili viongozi wa upinzani na CCM wakakae
ili kushauriana jinsi gani ya kuweza kuja na maneno yanayofaa kwenye
mapendekezo yanayofuatia.
Hoja hiyo ilionekana kupingwa na wabunge wakieleza
kwamba saa kumi jioni ni mbali hivyo Mbunge wa Kigoma Kaskazini
(Chadema), Zitto Kabwe alisimama na kusema kuwa masaa mawili yanatosha
kwa mashauriano lakini siyo saa moja kama Serikali ilivyoomba.
Spika alimpa nafasi Mbunge wa Kuteuliwa, James
Mbatia ambaye yeye alipendekeza masaa matatu ili kamati ikae na kuona
jinsi gani wataweza kufikia mashauriano yao.
Spika Makinda alisema ni lazima wabunge waelewe
kwamba mabunge ya kisasa yakifikia katika hali kama ya jana na juzi,
lazima wakutane pande zote na kufanya mashauriano.
“Tuwe Bunge la kisasa lazima tushauriane
tunapofika kwenye suala kama hili na hivyo mkutane wote na kukubaliana.
Hivyo tukubaliane wakija na kauli moja tunapitisha,” alisema Spika
Makinda.
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka
aligomea kauli hiyo ya Spika na kueleza kuwa anakubali pande zote kutoa
watu, lakini hakubaliani kwamba wakija na kauli moja ndiyo ipitishwe.
Kabla Ole Sendeka hajakaa Mbunge wa Nyamagana
(Chadema), Ezekiel Wenje alisimama na kusema watu wapewe muda wa
kushauriana, hivyo timu iundwe na ikae kwa muda mrefu ili wengine ambao
hawatakuwa kwenye kamati hiyo wapate nafasi ya kutaarifiwa juu ya nini
kinachoendelea
“Kwa hiyo Spika mimi nakubali turudi saa kumi ili hiyo timu
ikakae na sisi kwenye vikao vyetu tupewe taarifa tukifika hapa baadaye
tumalizane tu,” alisema Wenje na hoja yake iliungwa mkono na wabunge
hivyo Spika Makinda akasema viongozi wote wakae na kuja na kauli moja.
Pia, akitaka Zitto awe na wawakilishi kwa kuwa
ndiye mwenye hoja, lakini wale wanaotuhumiwa wasiingie kwenye kamati
hiyo. Hivyo akaahirisha Bunge.
Bunge laahirishwa tena saa kumi
Bunge lilirejea tena saa kumi jioni na kuahirishwa
baada ya Spika kupewa taarifa kwamba kamati iliyoteuliwa kwa ajili ya
mashauriano haijamaliza kazi.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Jenister Muhagama alisimama kwa upande wa CCM na kumweleza Spika kuwa
corcus yao imeambiwa kwamba bado majadiliano yanaendelea.
“Spika sisi tulituma wawakilishi sita na mpaka
sasa tumeambiwa kazi inaendelea lakini sijui kwa wenzetu imekuwaje
lakini hadi sasa bado,” alisema Muhagama.
Spika Makinda alipokea taarifa hiyo na kuhoji
upande wa upinzani una taarifa gani ambapo Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
alisimama na kusema, “Na sisi tumeelezwa kwamba bado.”
Kwa kauli hiyo Spika Makinda aliamua kuahirisha
Bunge hadi saa moja jioni na kuwaeleza wabunge kwamba suala hilo lazima
limalizike ifikapo saa mbili na robo usiku.
Wabunge walitoka nje na kuendelea na shughuli zao
huku wengine wakijikusanya vikundi vikundi wakijadiliana. Wengine
waliamua kukaa Kanteen ya Bunge kusikiliza hotuba ya Rais Jakaya Kikwete
ambaye amerejea nchini jana akitokea nchini Marekani alikokuwa kwa
matibabu ya tezi dume.
Kilichotokea juzi usiku
Juzi Spika Makinda alilazimika kuahirisha Bunge
kutokana na wabunge wa Kambi ya Upinzani kugoma kukubali marekebisho ya
Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge kwamba uamuzi wa
kumng’oa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo uachiwe
mamlaka iliyomteua.
Chenge alifanya marekebisho akieleza pendekezo la
kumng’oa Profesa Muhongo lisomeke kama lile la Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Eliakim Maswi ambalo Bunge lilipitisha kwamba: “Bunge
linaazimia kulifikisha suala hili kwa mamlaka ya uteuzi kwa hatua
zaidi.”
Kipengele hicho kilikataliwa na upinzani na kuamua kusimama
wakitaka Profesa Muhongo achukuliwe hatua lakini CCM waligoma ndipo
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliposimama na
kusema kuwa haiwezekani kamati imependekeza mambo halafu Bunge linataka
kuwalinda watuhumiwa.
Mbowe alisema kama Bunge linaamua hivyo wao
hawawezi kuwa upande wa uamuzi huo kauli iliyowanyanyua wabunge wote wa
upinzani vitini kutaka waondoke, ingawa Spika alimsihi Mbowe kuwatuliza,
ilishindikana na Spika kuamua kisitisha Bunge hadi jana.
Jitihada kubwa zilifanyika kuwasihi wabunge wa
upinzani kutulia lakini walianza kupiga kelele wakieleza kuwa hawawezi
kulinda wezi.
Spika Makinda kabla ya kuahirisha aliwaeleza
wabunge kuwa anapata wakati mgumu kwa kuwa Bunge limekuwa likiingilia
shughuli za mihimili mingine na kwamba tayari ana kesi mahakamani
kutokana na kuelezwa kuingilia shughuli za mahakama hivyo aliwaomba
wabunge waache kutoa maamuzi ambayo yanaingilia mhimili wa Serikali.
“Tayari mimi nina kesi huko katika mhimili
mwingine sasa mnataka nigombane tena na Executive (Serikali) itakuwaje
jamani naomba tutafute maneno ya kutokuingilia mhimili mwingine,”
alisema Spika Makinda.
Maneno yake hayo yalionekana kupuuzwa na wabunge
wa upinzani na wengine wa CCM huku wakipiga kelele kuwa ni lazima
watuhumiwa waliohusika kwenye sakata la escrow washughulikiwe kama
ilivyokuwa kwenye sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili.