Dar es Salaam.
Tanzania inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, mwaka huu. Baadhi ya
wananchi hasa vijana waliofikisha miaka 18 hivi karibuni hawajawahi kushiriki
kwenye uchaguzi wowote na uchaguzi huu ni wa kwanza kwao.
Saa 1: Wananchi wanatakiwa kufika vituoni kuanzia saa
moja asubuhi wakiwa na vitambulisho vyao vya kupigia kura.
04:Jambo la nne, mwananchi akimaliza kupiga kura aende
nyumbani kusubiri matokeo kutangazwa.
53:Kwa mujibu wa kifungu cha 53 cha Sheria ya
Uchaguzi, wagombea urais na wagombea wenza wanayo haki ya kutumia vituo vya
redio na televisheni vya Serikali wakati wa muda rasmi wa kampeni.
Peter Elias, Mwananchi
Dar es Salaam. Tanzania inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, mwaka huu. Baadhi ya
wananchi hasa vijana waliofikisha miaka 18 hivi karibuni hawajawahi kushiriki
kwenye uchaguzi wowote na uchaguzi huu ni wa kwanza kwao.
Vijana hawa na
watu wengine, wanahitaji kujifunza au kukumbushwa juu ya mambo ya kufanya siku
ya uchaguzi ili kufanya zoezi la upigaji kura kuwa lenye mafanikio na kuepusha
uvunjifu wa sheria unaoweza kumweka mtu matatani.
Kwa bahati
mbaya, elimu kwa mpigakura haitolewi mara kwa mara kwa wananchi mpaka nyakati
za uchaguzi. Hata wakati huo ukifika, baadhi ya watu hasa wale wa hali ya
chini, hawafikiwi na elimu hiyo.
Elimu kwa mpiga
kura bado inahitajika ili kila mwananchi afahamu haki na wajibu wake katika
mchakato mzima wa uchaguzi. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ndiyo yenye jukumu
la kutoa elimu hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine.
Hata hivyo,
zoezi hili linakabiliwa na changamoto ya uhaba wa rasilimali za kufanikisha
utoaji wa elimu kwa wapigakura. Vilevile, hakuna chombo maalumu cha kuratibu na
kusimamia utoaji wa elimu ya uraia.
Mwenyekiti wa
Nec, Jaji Damian Lubuva anasema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni pamoja
na uhaba wa Asasi za kiraia zinazotoa elimu kwa wapigakura na kuwafikia wananchi
wote nchi nzima.
Jaji Lubuva
anasema Tume imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba elimu inawafikia wapigakura
nchi nzima. Anasema watatumia vyombo vya habari vikiwamo vinavyomilikiwa na
taasisi za dini ili kuwafikia wananchi haraka zaidi.
Zingatia haya
siku ya uchaguzi
Mkurugenzi wa
uchaguzi – Nec, Kailima Kombwey anafafanua mambo muhimu ambayo mpigakura
anatakiwa kufanya siku ya uchaguzi bila kuathiri masharti ya sheria za uchaguzi
na kanuni zake.
Wahi kituoni
Anasema jambo
la kwanzana la msingi ni kuwahi asubuhi katika kituo cha kupigia kura.
Kombey anasema wananchi wanatakiwa kufika vituoni kuanzia saa moja asubuhi
wakiwa na vitambulisho vyao vya kupigia kura.
Anasema kila
mpigakura anatakiwa kujua kituo atakachopigia kura na kuhakiki kama jina lake
lipo kwenye orodha ya wapigakura kwenye kituo husika.
Panga foleni
Kombey
anabainisha kuwa watu watapanga foleni kuingia chumba cha kupigia kura na vituo
vitafungwa kuanzia saa 10 jioni. Anasema watakaokuwa kwenye mstari baada ya
muda huo wataruhusiwa kuendelea kupiga kura mpaka watakapomaliza.
“Tunasisitiza
wananchi wajitokeze kwa wingi ili wawachague viongozi wao. Kupiga kura ni jambo
la muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu. Wasipojitokeza basi wasilaumu kiongozi
atakayechaguliwa na wengine,” alisema Kombwey.
Mkurugenzi huyo
anasema katika uchaguzi wa mwaka 2010, waliandikisha watu milioni 20 lakini
waliojitokeza kupiga kura walikuwa chini ya milioni 10. Kwa hiyo, anasisitiza
zaidi kujitokeza kupiga kura siku hiyo.
Usivae sare za
chama
Jambo la pili,
mpigakura asivae nguo yenye nembo au alama yoyote ya chama cha siasa kwenye
kituo cha kupigia kura. Kufanya hivyo ni kukiuka taratibu za uchaguzi na
mtuhumiwa anaweza kushitakiwa kwa kuhujumu mchakato wa upigaji kura.
Kombey
anafananisha jambo hilo na akufanya kampeni siku ya kupiga kura, jambo ni
kinyume na kanuni. Kwa hiyo, fulana, kofia, bendera au kanga au nguo yoyote
inayovaliwa na chama chochote haitakiwi kwenye eneo la kupigia kura.
“Tunatoa muda
wa kampeni ili wanasiasa na vyama vyao wajinadi kadri wanavyotaka lakini siku
ya uchaguzi siyo siku ya kufanya kampeni, ni kinyume cha kanuni za uchaguzi,”
anasema mkurugenzi huyo.
Anaendelea
kubainisha kuwa Tume kupitia kifungu cha 124 (a) cha sheria ya taifa ya
uchaguzi ya mwaka 1985 ilianda maadili ya uchaguzi ambayo yamefanyiwa
mabadiliko madogo mwaka huu na kukubaliwa na vyama vyote.
Wahusika wakuu
katika maadili haya ni Tume ya Uchaguzi, Serikali, wagombea na wanachama wote
wa vyama vya siasa. Kombwey anasema wadau hawa kwa pamoja wana wajibu wa
kufanya uchaguzi huru na wa haki.
Usilete
ushabiki
Jambo la tatu,
wapigakura wasilete ushabiki kwenye vituo vya kupigia kura. Mambo ya ushabiki
ni pamoja na kuongelea matokeo ya uchaguzi kabla hayajatangazwa na mamlaka
husika zilizokasimiwa jukumu hilo.
Mkurugenzi huyo
anafafanua kwamba jambo hilo linajenga hisia tofauti miongoni mwa wapiga kura
na linaweza kusababisha vurugu endapo matokeo yatakuwa kinyume chake.
Anabainisha kuwa kura ni siri ya mpigakura mwenyewe.
“Sitarajii
kuona watu wakitengeneza makundi ya kujadili mwenendo wa uchaguzi kwenye vituo.
Hiyo ni sawa na kampeni siku ya uchaguzi, hatutaacha ufanyike kwa sababu
utaharibu mchakato wa uchaguzi,” anasema.
Ukipiga kura
nenda nyumbani
Jambo la nne,
mwananchi akimaliza kupiga kura aende nyumbani kusubiri matokeo kutangazwa.
Kuendelea kukaa kwenye vituo vya kupigia kura kunasababisha msongamano usio wa
lazima.
Kombwey anasema
hakuna haja ya kukaa kwenye vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kulinda kura
kwa sababu tayari mawakala wa vyama vya siasa wapo kwa ajili ya kuangalia
mwenendo mzima wa uchaguzi.
“Ile dhana ya
kutaka kulinda kura zisiibiwe ndiyo inayosababisha vurugu kwenye vituo. Hizo ni
hisia tu, hakuna wa kuiba kura kwa sababu kuna mawakala wanaowakilisha vyama
vyao,” anasema.
Tume ina jukumu la kutangaza matokeo
Anasema jukumu la kutangaza matokeo ya urais ni la
Tume ya uchaguzi. Tume pia imekasimisha jukumu la kutangaza matokeo ngazi ya
kata kwa msimamizi msaidizi wa kata na ngazi ya jimbo kwa msimamizi wa
halmashauri.
Kombwey anasema kuna baadhi ya watu wanatishia
kutangaza matokeo endapo Tume itachelewa kufanya hivyo. Anasisitiza kuwa
kufanya hivyo ni kinyume cha utaratibu kwa sababu hakuna mtu mwenye jukumu hilo
zaidi ya Nec.
Anasema Nec imejipanga kutangaza matokeo ya
urais ndani ya siku tatu kwa sababu watatumia Mfumo wa Kusimamia Matokeo (RMS)
ambao utawawezesha kupokea, kujumlisha na kutangaza matokeo.
Licha ya kutakiwa kisheria kutangaza matokeo hayo
ndani ya siku saba, Nec imebainisha kwamba mfumo huo utasaidia kuongeza kasi ya
ukusanyaji wa matokeo kutoka sehemu mbalimbli nchini.
Mabadiliko ya sheria
Jaji Lubuva anasema mabadiliko makubwa ya sheria ya
uchaguzi yalifanyika mwaka 2010, mwaka huu sheria hiyo haijafanyiwa marekebisho
isipokuwa kanuni za uchaguzi zimerekebishwa ili kuleta ufanisi katika uchaguzi
ujao.







