Friday, 1 August 2014

Uongozi mbaya wa shule chanzo cha ugonjwa wa watoto kupagawa

Mara nyingi tumekuwa tukishuhudia wasichana wengi hasa wakiwa shuleni wakipata matatizo ya kuweweseka, kupiga kelele na kuchanganyikiwa kiasi cha kushindwa kuendelea na masomo.
Ingawa watu wa jinsia zote, wakubwa kwa wadogo wanaweza kupata tatizo hili, wanaoathirika zaidi ni wanawake hasa wasichana wa umri kati ya miaka 12 na18.
Matukio ya wanafunzi kupagawa, kuweweseka na kupiga kelele yametokea jijini Dar es Salaam katika shule kadhaa za msingi. Agosti 2005, wanafunzi 24 wa Shule ya Msingi ya Uwanja wa Ndege walipata tatizo hilo na Novemba 2006, wanafunzi 15 wa darasa la tano katika Shule ya Msingi ya Mbuyuni.
Matukio kama yayo yametokea katika mikoa mingine kama tukio la Machi 2007 kwenye Shule ya Msingi ya Lewa wilayani Korogwe, Tanga, Mei  2008 lilipotokea kwa wanafunzi 50 na mwalimu wao mkoani Dodoma na wanafunzi 30 wa Shule ya Msingi ya Mang’ula mkoani Morogoro mwaka 2009.
Hali hii imekuwa ikipokewa kwa hisia tofauti na watu mbalimbali katika jamii. Wengine huihusisha na imani za kishirikina, kupagawa na pepo au kudhuriwa na mizimu.
Ingawa jamii ina maoni tofauti kuhusu tatizo hili, wanasayansi wanaamini kuwa hali hii inatokana na matatizo ya afya ya akili yanayojulikana kama hysteria.
Kihistoria ugonjwa huu ulianza zamani hata kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Jina la ugonjwa huu lilitokana na mawazo ya madaktari wa zamani wa Kigiriki waliokuwa wanafikiria kwamba chanzo cha ugonjwa huu ni matatizo katika mfuko au mji wa mimba wa mwanamke, ambao kwa Kigiriki unaitwa hystera.
Madaktari wa Kigiriki walidhani kuwa huu ni ugonjwa unaowapata wanawake pekee. Hii ilitokana na idadi kubwa ya wagonjwa wa tatizo hili kuwa wanawake, na hata pale wanaume walipokuwa na dalili za tatizo la hysteria ilidhaniwa kuwa wana tatizo jingine kwa vile hawakuwa na mfuko au mji wa mimba.
Dhana ya madaktari wa kipindi hicho juu ya ugonjwa huu ilikuwa kwamba mfuko wa kizazi (mji wa mimba) unabana na kukauka kutokana na kutokufanya ngono kwa muda mrefu au kuzidiwa na hamu ya ngono.  Matibabu ya enzi hizo yalihusisha kumtekenya mwanamke katika sehemu zake za siri ili apate kumaliza hamu ya ngono, lakini matibabu hayo yalikuwa hayatoi matokeo ya uponaji yaliyotarajiwa.
Hata hivyo, sayansi ya tiba ya binadamu imethibitisha kuwa hysteria ni ugonjwa wa akili unaotokana na msongo mkali wa mawazo na hisia.
Linaonekana ni tatizo zaidi la afya ya akili na kisaikolojia.
Tatizo hili hutokea pale mtu anapopata msongo wa kihisia maishani zaidi ya vile alivyojiandaa au anavyoweza kukabiliana nao. Mara nyingi msongo huu hutokana na hisia au mgogoro wa fikra, kutokuwa na uhakika wa usalama katika siku za usoni, kutengwa na jamii au kutosikilizwa kwa upendo. Tamaa kali ya kutaka kupendwa kuliko kawaida isipotimizwa, pia huleta tatizo hili.
Wakati mwingine hisia na fikra hutokana na matatizo ya kawaida, lakini akili huyakuza sana na mhusika akajiona hawezi kuyakabili, hafai na hathaminiwi.
Mgonjwa anaweza kujilaumu na kupata hisia za kupoteza ulinzi au kupata kumbukumbu isiyonyamazishwa ya tukio la kinyama alilotendewa kama vile kubakwa, kunyanyaswa au ukatili  wa kijinsia.
Watu wanaopata ugonjwa wa hysteria huwa na matatizo ya kihisia ambayo mara nyingi hawapendi kuyazungumzia na kwa sababu hiyo, matatizo hayo huwaelemea sana.
Katika utafiti uliofanywa na Altamura AC na wenzake nchini Malawi, iligundulika kuwa wanawake wengi, hasa wasichana hupata msongo mkali sana wa mawazo, kujilaumu na kushuka sana moyo pale wasiporidhishwa na hali ya maisha waliyo nayo. 
Mwanasaikolojia Mareesa Dannielle wa New Zealand, katika utafiti wake mwaka 2007, alibaini kuwa uongozi mbaya wa watu unaweza kuchangia kwa namna moja ama nyingine kutokea kwa tatizo hilo.
Kaimu mganga mkuu wa Wilaya ya Ulanga,  Eddy Mjungu anasema: “Hii inaweza kuwa watoto kutolelewa vizuri, uhusiano wao na wazazi, walimu na hata migogoro ya kimapenzi.”
Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu mmoja pekee lakini pia unaweza kusambaa kwa wengine katika kundi la watu wanaokabiliwa na msongo wa kisaikolojia unaofanana na wanaokaa au kufanya kazi katika mazingira yanayofanana.
Hysteria inayosambaa huanza na mtu mmoja na anapoonyesha dalili, wengine nao huanza kujenga hofu na hisia za kuathirika baada ya kumwona mwenzao.
Mara nyingi dalili za hysteria inayosambaa hazionyeshi chanzo bayana na hazitafasiriki sawasawa lakini zinaenea kwa haraka miongoni mwa walioona mgonjwa wa kwanza aliyepata tatizo.
Hofu huongezeka zaidi na tatizo husambaa zaidi pale linapoanza kuhusishwa na imani za kishirikina, mambo ya kimizimu na kupagawa na majini au pepo wabaya.
Hofu huzidi pale timu ya wataalamu wa uchunguzi wa vyanzo vya magonjwa wanaposhindwa kubaini chanzo bayana cha tatizo.
Hysteria ingawa ni tatizo la  afya ya akili, pia hudhuru afya ya mwili kwa kiwango kikubwa. Hofu, woga na wasiwasi husababisha mapigo ya moyo wa mgonjwa kwenda haraka, kutapika, kupata kichefuchefu, mwili kuishiwa nguvu na maumivu ya kichwa.
Matatizo mengine ni pamoja na miguu kufa ganzi, kushindwa kutembea, kupiga kelele au kucheka sana bila sababu za msingi na  kupata degedege.
Wagonjwa wengine hupoteza hamu ya chakula, kutokupata choo kabisa au kuharisha na wengine hutokwa jasho jingi, kutetemeka, kupumua kwa shida au kushindwa kupumua vizuri kiasi kwamba hewa chafu ya ukaa haitolewi mwilini kwa kiwango cha kutosha.

Ukawa, CCM kucheza kete ya mwisho leo

Ni katika kikao cha maridhiano chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa
Dar es Salaam. Kete ya mwisho ya kuamua iwapo wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) watarejea katika Bunge la Katiba au la itachezwa leo katika kikao cha maridhiano baina ya umoja huo na CCM, chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
Kikao hicho kinafanyika siku nne kabla Bunge hilo kuendelea na vikao vyake Jumanne ijayo licha ya msimamo wa Ukawa wa kuendelea kuvisusia.
Kikao hicho kinachovikutanisha vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na CCM ni cha mwisho baada ya kile cha kwanza kilichofanyika wiki moja iliyopita kumalizika bila mwafaka wowote.
Akizungumza na waandishi wa habari jana akiwa na wenyeviti wenzake, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema hadi jana msimamo wao ni kutohudhuria vikao vya Bunge hilo labda ikitokea miujiza katika kikao cha leo.
Mbowe alisema ni miujiza kwa sababu kwa madai ya Ukawa, ni lazima mjadala huo ujikite kwenye Rasimu ya Katiba, ambayo imebeba mapendekezo ya wananchi na kutaka wajumbe wenzao, hasa kutoka CCM, kuacha kujenga hoja kwa kutumia kejeli, matusi na mizaha ambayo si rahisi wenzao kuyakubali.
Moja ya ajenda ya kikao hicho ambacho leo kitakuwa na wajumbe 20 kutoka kila chama, ni kuwashawishi Ukawa kurejea bungeni ili kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.
Ukawa walisusia vikao vya Bunge la Katiba hilo Aprili 16 wakipinga kubadilishwa Rasimu ya Katiba na wajumbe wa CCM kwa maelezo kuwa ni kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Mbowe alisema ni jambo la kushangaza kuona Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta wakitoa kauli za kuwashutumu Ukawa wakati wakijua wazi kuwa kuna mazungumzo kati ya vyama vya siasa na Jaji Mutungi vinaendelea.
Juzi pia, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), liliisihi Ukawa kurudi bungeni ili kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya, lakini likasema mjadala huo uzingatie Rasimu ya Katiba.
“Hata viongozi wa dini nao wametoa matamko wakitaka Ukawa turejee bungeni, tunashukuru maoni yao. Ila wanatakiwa kujua sababu zilizotufanya mpaka tukasusia. Wanatakiwa kuwaonya CCM wanaokwenda kinyume na mchakato huo,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Wakati tupo katika mazungumzo, Sitta anaanzisha kikao chake na kutoa tamko kuwa Bunge litaendelea wakati akijua Ukawa wapo katika kikao pamoja na viongozi wa chama chake cha CCM. Kauli hizi zinazokosa umoja zinaonyesha Serikali na timu nzima haiko tayari kutafuta mwafaka wa suala hili.”
Profesa Lipumba
Akieleza sababu nyingine za Ukawa kususia vikao vya Bunge la Katiba, Profesa Lipumba aliwataka viongozi wa dini kutambua kuwa CCM ndiyo chanzo cha mchakato huo kuingia dosari, kwamba wanatakiwa kukionya chama hicho kiheshimu maoni ya wananchi.
“Tuliondoka bungeni kwa sababu Sitta alishindwa kuwadhibiti wajumbe wa Bunge la Katiba waliokuwa wakizungumza lugha za matusi, kejeli, uchochezi na ubaguzi, alivunja kanuni za Bunge kwa kuruhusu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni kabla ya Bunge kusikiliza hotuba ya ufunguzi ya Rais Jakaya Kikwete.”
Alitaja sababu nyingine kuwa ni kauli ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kueleza kanisani kuwa nchi itaingia vitani iwapo muundo wa serikali tatu utapita, kwamba Zanzibar inataka serikali tatu ili kurejesha Waarabu visiwani humo.
“Lukuvi aliyasema hayo kanisani akimwakilisha Waziri Mkuu Pinda. Licha ya kutoa maneno ya uchochezi hakuna mamlaka iliyo juu ya Lukuvi iliyoomba radhi kwa kauli yake,” alisema.
Mbatia
Mbatia alisema rasimu inayotakiwa kujadiliwa ni ile iliyopendekezwa na Tume ya Warioba yenye muundo wa Serikali tatu.
“Hata kuhusu Tunu za Taifa zilizotajwa katika rasimu; yaani utu, uzalendo, uadilifu, uwazi, umoja, uwajibikaji na lugha ya taifa wenzetu wa CCM wameyakataa. Sasa sijui wanataka kulipeleka wapi hili taifa. Tutaendeleaje kujadili?” alihoji.
Hofu ya wajumbe
Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo wamesema kutorejea bungeni kwa Ukawa kutaathiri upatikanaji wa Katiba Mpya yenye maridhiano.
Mmoja wa wajumbe hao, Charles Mwijage alipendekeza kusitishwa kwa mchakato huo kwa kuwa maridhiano ni jambo muhimu katika kutengeneza Katiba.
“Kukosekana kwa Ukawa bungeni kutaathiri upatikanaji wa Katiba Mpya kwa sababu suala hili linahitaji zaidi maridhiano ya pande zinazotofautiana kiitikadi,” alisema Mwijage ambaye pia ni Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM).
“Ningekuwa na uwezo, ningeamua mchakato huu wa  Katiba usitishwe na tuendelee kutumia Katiba iliyopo kwa sababu suala hili linahitaji zaidi maridhiano,” alisema.
Mbunge huyo alisema, “Ukawa wanataka kujenga mazingira ya kuja kuikataa Katiba itakayopatikana ili watusababishie vurugu na mapigano.”
Alisema Rais aliona kwamba kundi la wajumbe 629 likikaa pamoja linaweza kutengeneza Katiba Mpya kwa maridhiano, lakini kama kuna kundi linajitoa ni wazi kwamba kutakuwa na dosari katika utengenezaji.
Mjumbe mwingine, Ezekiah Oluoch alisema iwapo wajumbe wa CUF kutoka Zanzibar ambao wanaunda Ukawa hawatarejea bungeni, Katiba Mpya haiwezi kupatikana kwa sababu theluthi mbili haziwezi kupatikana.
“Katiba haipatikani kwa ubabe au wengi-wape, bali inapatikana kwa maridhiano na mwafaka bila kujali idadi ya wingi wa wajumbe,” alisema Oluoch ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Alisema Bunge hilo litatumia fedha nyingi za walipa kodi bila kupata Katiba Mpya, hivyo akashauri mchakato huo usogezwe mbele hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Lackson Mwanjali alisema kitendo cha Ukawa kukataa kurejea bungeni ni pigo katika mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu inatengenezwa kwa majadiliano na kufikia mwafaka.
“Tunapokuwa bungeni watu kutoka vyama na itikadi tofauti tunajadiliana, tunabishana na baadaye kufikia mwafaka na kufanya maridhiano, sasa wenzetu hawapo ni tatizo kubwa,” alisema.
Mwanjale alisema ingawa wanakwenda kwenye Bunge Maalumu la Katiba itakuwa vigumu kupata Katiba bora.
Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Diana Chilolo alisema wangependa Ukawa warejee bungeni lakini kama hawaendi watawakilishwa na wenzao.
“Wapo watu kutoka katika vyama vya upinzani pale ambao watawawakilisha. Yupo Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema na Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo watawawakilisha na tutapata Katiba bora,” alisema Chilolo.
Mbunge wa Sikonge (CCM), Saidi Mkumba alisema Katiba inayotafutwa ni ya Watanzania wote hivyo kundi la Ukawa kukataa kurudi bungeni hakuwezi kusimamisha mchakato huo.
Mambo sita ya kuzingatia
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Khoti Kamanga amebainisha mambo sita yanayotakiwa kufanyiwa kazi kabla ya Bunge hilo kuanza vikao vyake Agosti 5.
Akizungumza katika kilele cha Siku ya Wanawake Afrika iliyoandaliwa na Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WilDAF), Dk Kamanga alisema:
“Mosi, huu utaratibu wa wengi-wape ni mzuri lakini tusiung’ang’anie ingawa demokrasia inaruhusu na kinachotakiwa ni kuweka mbele masilahi ya taifa.”
“Kuna wachache wanakuwa na hoja za kutosha lakini kutokana na uchache wao demokrasia inawatupa. Katika suala la Katiba maridhiano ni jambo la muhimu na suala la wengi-wape liwekwe kando.”
Pili, alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa kufanyiwa marekebisho hasa Kifungu cha 36 (5) kilichobainisha kuwa endapo mwafaka hautapatikana Katiba ya mwaka 1977 itaendelea kutumika.
“Unapoanza safari huwezi kushindwa na ukarudi nyuma, kwa kuwa kila mmoja amekiri kwamba Katiba ya sasa ina viraka 14 ambavyo ni vingi sana,” alisema.
Jambo la tatu, Dk Kamanga alisema kunahitajika ujasiri katika kubaini na kukubali ni wapi mchakato wa Katiba ulipojikwaa. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa kuheshimiwa na si kukiukwa.
Jambo la nne ni kuwa, Bunge linatakiwa kujadili rasimu na kutokwenda kinyume na sheria ilivyo kama ilivyoandaliwa na Tume ya Katiba  kwa mujibu wa sheria.
“Rasimu iliyopo ya Desemba 2013 iliandaliwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokusanya maoni ya wananchi, hivyo sheria haitakiwi kuvunjwa, pia Bunge linatakiwa kuizingatia,” alisema.
“Tano, tunatakiwa kusoma rasimu ili unapochangia au kuona mtu akichangia uwe unajua anachokisema na jambo la mwisho ni ngumu kwa vyama kuweka kando masilahi yao lakini kwa jambo hili wanatakiwa kutanguliza mbele masilahi ya taifa,” alisema Dk Kamanga.

Monday, 30 June 2014

Msekwa aeleza sababu ya wasomi kukimbilia siasa

Dar es Salaam. Kwa nini siasa imegeuka kimbilio la wengi, wakiwamo wasomi Tanzania?
Ni swali aliloulizwa Spika mstaafu, Pius Msekwa katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni.
Akijibu swali hilo, Msekwa alieleza kwa ufupi sababu za wasomi kuacha taaluma zao na kuwekeza nguvu na akili zao katika siasa akisema inalipa kwa haraka na kwa njia nyingi zikiwamo mishahara minono, posho na marupurupu kuliko zilivyo taaluma nyingine.
Msekwa ambaye amewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akitokea kwenye Chama cha Tanu na baadaye kurejea kwenye siasa, alisema malipo manono yamewafanya wasomi wengi, wakiwamo maprofesa, madaktari na wengineo kuifanya kimbilio.
Alisema pia uhuru wa watu kuchagua kazi nyepesi za kufanya katika maisha yao umefanya waione siasa kama kimbilio rahisi kuliko kutoka jasho kwenye taaluma, zikiwamo za utafiti, tiba, upasuaji, ualimu na nyinginezo. “Siasa imegeuka kimbilio kwa kuwa ina posho na marupurupu mengi zaidi,” alisema Msekwa na kuongeza kuwa wanasiasa wanajipitishia posho ambazo haziwezi kutolewa kwingineko.
“Mpe mtu choice (chaguo), acha aende kokote hata katika siasa, lakini ni vyema taaluma pia ikaheshimika,” alisema na kuongeza kuwa jambo hilo lilianzia  kwenye awamu zilizopita ambako wasomi, ama walioteuliwa au kuchaguliwa waliamua kushiriki siasa na hivyo kuziacha taaluma zao. Msekwa alimtaja msomi mmoja, Profesa Mazengo ambaye aligombea ubunge baadaye akautelekeza baada ya kushindwa kutimiza dhamira yake.
“Kulikuwa na mtu anaitwa Profesa Mazengo, yeye alikimbilia kwenye siasa akilenga kupata uwaziri. Ubunge alishinda lakini alipokosa uwaziri akautelekeza ubunge wake, hata jimboni hakwenda, hakuwakilisha wananchi na wapigakura wake, hivyo hakurudi baada ya miaka mitano,” alisema.
Kwa siku za karibuni, siasa na hasa ubunge, unaonekana kuwa na masilahi na fursa zaidi kuliko nafasi nyingine katika jamii na ndiyo maana wasomi wamekimbilia huko kwa matarajio ya kupata fursa za kupitisha mambo yao. Baadhi yao (wasomi), ubunge siyo tija, wamejikita zaidi kwenye nafasi katika serikali, zikiwamo za mitaa ili kufanikisha biashara zao au kuwa karibu wananchi wa ngazi ya chini.
Kwa mfano, orodha ya wabunge kwenye Bunge la sasa, inaonyesha wasomi wengi wakiwamo maprofesa, madaktari wa falsafa, madaktari wa tiba au wahandisi.
Msekwa alipoulizwa anadhani ni kwa nini Serikali haiboreshi masilahi ya wasomi katika taaluma zao, alicheka kisha akasema uwezo wa nchi ni mdogo, haiwezi kuboresha masilahi ya watumishi wote lakini inaweza tu kwa wabunge.

Dk Salim afichua siri ya JK na Tume ya Warioba

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim amesema hakutarajia kusikia kauli za Rais Jakaya Kikwete alizozitoa bungeni kukosoa Rasimu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa sababu walikuwa wanampa taarifa kwa kila hatua waliyokuwa wanafikia kabla ya kutoa rasimu hiyo.
Dk Salim alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam wiki iliyopita.
“Hatukutarajia kama hali ingefikia hatua iliyofikia,” alisema Dk Salim na kuongeza: “Lakini Rais ana uamuzi wake na anazingatia mambo mengine mengi.”
Akilihutubia Bunge maalumu la Katiba Machi 21, mwaka huu Rais Kikwete aligusia mambo saba ya msingi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani kutekelezeka. Miongoni mwa mambo hayo ni muundo wa Serikali. Alipinga waziwazi pendekezo la serikali tatu lililopendekezwa na Tume na kuegemea katika muundo wa serikali mbili na idadi ya watu walioupendekeza akionyesha kuwa ilikuwa ni ndogo.
Pia alisema ni vigumu kutenganisha uwaziri na ubunge kama ilivyokuwa imependekezwa na Tume kwa maelezo kuwa mawaziri wanatakiwa kuwepo bungeni ili kujibu hoja za Serikali.
Jambo lingine alilokosoa katika Rasimu ni pendekezo la mtu kupoteza ubunge kwa sababu ya kuugua kwa miezi sita mfululizo huku akisema baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi ambayo hayapaswi kuwamo katika Katiba, bali katika sheria zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Katika mahojiano hayo maalumu, Dk Salim alisema baada ya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume aliacha kuhudhuria vikao vya chama chake ili aweze kufanya kazi hiyo kwa usahihi na alimtaarifu Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais na katibu mkuu wake na walimwelewa.
Alipoulizwa anaitazama vipi Tanzania iwapo Katiba Mpya haitapatikana, Dk Salim alisema ana wasiwasi kwa kuwa suala hilo limeingizwa siasa na Bunge Maalumu limegeuka la kisiasa hivyo linaweza kuleta matatizo.
“Tuko katika hali ambayo si nzuri inayohitaji uongozi thabiti, viongozi wote watambue umuhimu wa zoezi hili kwa lengo la kulinda amani na utulivu wa nchi yetu,” alisema.
Alisema kunahitajika ufumbuzi wa kudumu na hicho ndicho kipimo cha uongozi kwa CCM, Chadema na wengine kwa kutafakari masilahi ya Watanzania wa leo, kesho na keshokutwa.
Nini kifanyike?
Dk Salim alisema jambo muhimu sasa ni pande mbili zinazoshindana kuhusu idadi ya Serikali kutumia mwezi ujao wa Julai kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao ili Bunge la Katiba liendelee bila misuguano.
“Mwezi huu wa Julai ni muhimu sana, ni mwezi pekee uliobaki wa kuwaweka pamoja wanaotofautiana. Kila jitihada zinatakiwa kufanyika ili kuhakikisha Bunge Maalumu linakutana tena Agosti na wapinzani waliosusa wanarejea ili kumaliza kazi hiyo kabla ya kutoa rasimu ya tatu kwa ajili ya kura za maoni,” alisema na kuonya kuwa kuendelea na katiba ya sasa kunaweza kuleta matatizo.
Neno ‘wasaliti wa Mwalimu Nyerere’ lamchefua
Aidha, Dk Salim ameeleza kusikitishwa na kukatishwa tamaa na kauli za baadhi ya wanasiasa dhidi yake na wajumbe wenzake wa Tume kwa kuwaita wasaliti na hasa kitendo cha kutilia shaka uzalendo wao.
“Inakatisha tamaa sana. Mimi nina umri wa miaka 72, kati yake zaidi ya miaka 30 nimeitumikia nchi yangu, haiingii akilini katika umri huu wa mwisho nianze kuisaliti nchi yangu, inasikitisha sana kusikia eti hawa wasaliti wa Mwalimu Nyerere,” alisema.
Dk Salim ambaye ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF), alisisitiza kuwa wajumbe hao wamekuwa wakishutumiwa na watu wenye malengo yao, akitolea mfano kuwa hata Dk Mwesiga Baregu aliwahi kushutumiwa na chama chake na kutakiwa ajitoe kwenye tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Itakumbukwa kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekuwa ikishutumiwa na wanasiasa hasa kutoka CCM kutokana na mapendekezo yake ya mfumo wa Muungano wa serikali tatu badala ya mbili zinazoungwa mkono na chama hicho.
Kutokana na tofauti hiyo, wajumbe walio wengi wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka CCM waliamua kubadili baadhi ya vifungu vya rasimu.
“Ni bahati mbaya sana binadamu unapotukanwa, unatupiwa madongo, tunaonekana wapuuzi kwa kazi ya kukusanya maoni ya wananchi, inaumiza sana,” alisema.
Kama ambavyo Jaji Warioba amesema mara nyingi, Dk Salim aliitetea Rasimu ya Katiba, akisema kilichopendekezwa ndiyo picha halisi ya maoni ya Watanzania.
Alisema Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi yenye hoja nzito yakieleza hasa matatizo yao katika nyanja mbalimbali kama afya, elimu, ardhi na mengine, ingawa hoja kuhusu muundo wa Serikali ndizo zinaonekana kushikiwa bango na wanasiasa.
Alisema ushahidi wa watu waliohojiwa upo katika maandishi, sauti na picha za video na idadi yao inatosha kuwakilisha Watanzania wote.
“Wanasema hatukuhoji watu wengi, waliohojiwa ni representative sample (sampuli), huwezi kuhoji Watanzania wote milioni 45,” alisema Dk Salim.
Alisema ni jambo la kushangaza kuwa mchakato umetekwa nyara na wanasiasa lakini Katiba inastahili kuwa ya kitaifa ya Watanzania wote, wenye vyama na wasio na vyama vya siasa.
Alisema hata kwenye tume, walikuwapo wajumbe zaidi ya 12 ambao hawatokani na CCM, wakitoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na wote walikuwa na mawazo tofauti lakini waliamua kuyaweka kando na kutoa rasimu inayotoa taswira ya mawazo na masilahi ya wananchi.

Monday, 23 June 2014

Wabunge saba watikisa Bunge

Dodoma. Wabunge saba wamelitikisa Bunge tangu mkutano wa Bunge la Bajeti ulipoanza kutokana na michango yao binafsi.
Mwandishi wetu ambaye amekuwa bungeni tangu Mkutano wa Bajeti ulipoanza ametoa tathmini yake kuhusu michango ya wabunge iliyosisimua katika mjadala na kuibuka na orodha ya wabunge hao saba. Hata hivyo, katika tathmini hiyo, majina ya wabunge ambao walichangia kwa niaba ya kamati au kutokana na nafasi zao za uwaziri au uwaziri kivuli hajayaingizwa katika orodha hiyo.
Tathmini hiyo imefanyika huku leo mjadala wa Bajeti ya Serikali ya 2014/15 ukihitimishwa tayari kwa kupigiwa kura na wabunge kesho, baada ya kukamilisha mfululizo wa mijadala ya bajeti za wizara zote za Serikali tangu Bunge hilo lilipoanza Mei 6, mwaka huu. Hoja zilizoibuliwa na wabunge hao kwa nyakati tofauti ziliitikisa Serikali na kusababisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kiti cha Spika au aliyekuwa akikaimu nafasi ya Waziri Mkuu bungeni, Profesa Mark Mwandosya ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) kusimama kutoa ufafanuzi.
Waliotikisa
Wabunge waliotikisa Serikali katika michango yao ni Ally Keissy (Nkasi Kaskazini - CCM), David Kafulila (Kigoma Kusini - NCCR-Mageuzi), Kangi Lugola (Mwibara - CCM), Dk Faustine Ndugulile (Kigamboni - CCM), Tundu Lissu (Singida Mashariki - Chadema), Abbas Mtemvu (Temeke –CCM) na Cecilia Paresso (Mbunge wa Viti Maalumu-Chadema) .
Kafulila
Siku mbili baada ya Bunge kuanza Mei 8 mwaka huu, wakati wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kafulila aliibuka na sakata la kuchotwa kwa Dola za Marekani 122 milioni (Sh200 bilioni) akidai ni ufisadi uliofanywa na vigogo sita wa Serikali.
Aliwataja kwa majina vigogo hao na kusisitiza kuwa wamehusika na ufisadi wa fedha hizo zilizokuwa zimewekwa katika akaunti ya Baraza la Usuluhishi la Migogoro ya Kibiashara (Escrow), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Akaunti hiyo ilifunguliwa kutokana na mgogoro wa kibiashara kati ya IPTL na Tanesco na Tanesco ilipeleka shauri hilo mahakamani kulalamikia gharama kubwa za uwekezaji wanazotozwa na IPTL, hivyo kuamuliwa fedha hizo ziwekwe humo hadi shauri litakapoamuliwa, lakini baadaye zilichotwa katika mazingira ya kutatanisha.
Lugola
Lugola aliibuka Mei 10, mwaka huu katika mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na kusema kuwa Serikali ya CCM ambayo yeye ni mbunge wake, inaendeshwa kisanii huku akishangaa waziri mwenye dhamana ya kilimo, Christopher Chizza kuendelea kuwa waziri wakati hotuba yake imejaa blaablaa.
Pia alimgeukia Naibu Waziri, Godfrey Zambi na kumwambia amejisahau kwamba naye alikuwa akikaa kiti cha nyuma bungeni akipaza sauti, baada ya kupata madaraka amewageuka wenzake na kushirikiana na waziri.
Akizungumza kwa sauti ya ukali ambayo mara nyingi haitarajiwi kwa wabunge wa CCM, Lugola alihoji inakuwaje wakulima wanapelekewa pembejeo feki, dawa feki na skimu za umwagiliaji zinachakachuliwa na bado Chizza anaendelea kubaki kama waziri?
Keissy
Mei 27, mwaka huu ilikuwa zamu ya Keissy, mbunge machachari wa Nkasi Kaskazini pale alipozua sokomoko wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Mambo ya Nje. Kauli yake kuwa Zanzibar haichangii katika Muungano hivyo haina haki ya kuhoji mambo ya upande wa pili wa Muungano na kwamba hata umeme hailipi nusura imponze.
Alisema Zanzibar ina asilimia 2.8 ya watu wote wa Tanzania na kwamba kwa idadi hiyo, wananchi wa jimbo moja wanaweza kukusanyika eneo moja kwa kuitwa na mlio wa filimbi tu, kauli iliyosababisha wabunge kutoka Zanzibar kutaka kumpiga ‘kavukavu’.
Abass Mtemvu
Juni 5, Mtemvu naye aliibua mpya baada ya kumlipua Mbunge wa Urambo Magharibi (CCM), Profesa Juma Kapuya kuwa anafahamu uuzaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) ambalo alidai limeuzwa kwa Sh280 milioni.
Mtemvu alisema kulifanyika ujanjaujanja kati ya Kampuni ya Simon Group na Meya wa Jiji Dar es Salaam, Didas Masaburi kukopa benki na taasisi nyingine kwa ajili ya kununua shirika hilo, kauli ambayo ilipingwa na Kapuya huku suala la Uda likiendelea kukamata mjadala hadi Mwendeshaji wa Uda kuitwa bungeni.
Faustin Ndungulile
Mei 29 mwaka huu, Dk Ndugulile alimweka katika wakati mgumu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka wakati wa mjadala wa bajeti ya wizara hiyo na kuwa Serikali haijashirikisha wadau katika mradi wa Kigamboni utakaogharimu Sh11.7 trilioni.
Sakata hilo liliingiliwa na Waziri Mkuu ambaye alisema kuwa tatizo la mradi huo ni elimu kutotolewa kwa umma na kuomba wabunge waiachie Serikali suala hilo.
Tundu Lissu
Juni 2, Lissu aliwalipua Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Binilith Mahenge kwamba wanatumia vibaya nafasi zao kwa kuweka fedha nyingi za miradi ya maji katika maeneo wanakotoka, huku sehemu zenye matatizo ya huduma hiyo zikitengewa fedha kiduchu.
Lissu alisema Profesa Maghembe ambaye ni Mbunge wa Mwanga, Kilimanjaro, wizara yake imetenga Sh1.4 bilioni kwa ajili ya miradi ya maji, ambazo ni zaidi ya mara saba ya Sh190 milioni zilizotengwa kwa ajili hiyo katika Wilaya ya Ikungi, Singida.
Mawaziri hao waliokolewa na Profesa Mwandosya akisema kuwa miradi hiyo katika wilaya za Same, Mwanga na Korogwe ilianza wakati yeye akiwa Waziri wa Maji, hivyo hawakujipendelea.
Cecilia Paresso
Mbunge huyu aliichachafya Serikali na kuungwa mkono na wabunge 13 wanawake wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakitaka iongezewe fedha ili kukabiliana na vifo vya kinamama na watoto.
Paresso alisema wizara hiyo imetengewa Sh622 bilioni, ikiwa ni pungufu ya Sh131 bilioni ya bajeti ya wizara hiyo mwaka 2013/14 ilipotengewa Sh753 bilioni.
Hoja hiyo iliwanyanyua Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid na Naibu Mawaziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Adam Malima kutoa ufafanuzi. Wote hao walishindwa kumshawishi Paresso na wenzake, hadi Serikali ilipoahidi kuongeza fedha za wizara hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa Sh87 bilioni kwa ajili ya kulipa deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Friday, 20 June 2014

Kiasi kingine kikubwa cha gesi chagunduliwa nchini. Je wananchi wanafaidikaje na gesi hiyo?

Dar es Salaam. Kampuni ya Statoil ya Norway na mshirika wake ExxonMobil wamegundua kiasi kingine kikubwa cha gesi katika Bahari ya Hindi nchini Tanzania.
Kiwango hicho kinakadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni mbili mpaka tatu (sawa na lita trilioni 56.6 hadi trilioni 84.9).
Ugunduzi huu unafanya jumla ya ujazo wa gesi iliyogunduliwa na washirika hao kufikia takriban futi za ujazo trilioni 20 (lita trilioni 566.25) kwenye Kitalu Namba 2, ambako washirika hao wanafanya shughuli za utafiti na uchimbaji.
‘’Tangu mwaka 2012 tumekuwa tukipata mafanikio ya asilimia 100 nchini Tanzania na eneo hilo limekuwa kitovu cha utafiti ndani ya muda mfupi. Ni kwa haraka tulitoka kwenye kuchimba kisima kimoja hadi kuwa na mkakati wa kuchimba visima vingi,’’ alisema Makamu wa Rais wa Shughuli za Utafiti za Statoil Ukanda wa Magharibi, Nick Maden.
Ugunduzi huo mpya katika Kisima Piri-1 umefanyika katika eneo lenye kiwango kidogo cha mawe ya mchanga kama ilivyokuwa wakati ilipogunduliwa gesi katika Kisima cha Zafarani-1 mwaka 2012.
Ugunduzi katika kisima hicho unakuwa wa sita katika Kitalu Namba 2.
Uchimbaji wa gesi katika kisima hicho ulifanywa na meli ya Discoverer Americas, usawa wa mita 2,360 za kina cha maji. Meli hiyo sasa inachimba kisima kingine cha Binzari katika Kitalu namba 2.
“Eneo lingine la utafiti limeshaandaliwa na litajaribiwa ndani ya mwaka 2014 na 2015. Tunatarajia kuchimba visima zaidi na tunatumaini kuwa matokeo ya visima hivi yataongeza kiasi cha ujazo wa gesi kwa ajili ya miundombinu ya mradi mkubwa wa gesi hapo baadaye,’’ alisema Maden.
Statoil ambayo imekuwapo nchini tangu 2007, inatafiti na kuchimba gesi katika kitalu namba mbili kwa niaba ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ikiwa na hisa ya asilimia 65 katika kitalu hicho wakati ExxonMobil Exploration and Production Tanzania Limited ina asilimia 35.

Lissu ailipua tena Serikali

Dar/Dodoma. Serikali imeumbuliwa bungeni ikidaiwa kuwasilisha taarifa za uongo kupitia Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu ugawaji wa madawati yaliyonunuliwa kwa ‘chenji ya rada’.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alitoa tuhuma hizo jana, wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014, akisema Serikali imewadanganya wabunge kwa kuwa hakuna kitu kilichofanyika.
Alisema katika majibu ya Serikali kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kwa kuwa imetangaza kununua madawati 93,740 na kuyagawa katika halmashauri mbalimbali nchini wakati siyo kweli.
Alisema kwa mtindo huo, Serikali imelidanganya Bunge pamoja na Watanzania kwa kuwa imetangaza madawati hewa ambayo hayapo.
“Wabunge kama kweli mnatimiza majukumu yenu na hampo hapa kwa masilahi yenu tu, hebu hojini halmashauri zetu zimepelekewa haya madawati 93,000 yanayozungumzwa humu au mnapiga makofi tu? Serikali inadanganya tunatakiwa tuihoji tuiwajibishe,” alisema.
Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alitoa mfano wa mgawo huo kwenye Halmashauri ya Ikungi, Singida kwamba ilitangazwa kupelekewa madawati 508 lakini amekwenda jimboni na hakukuta dawati hata moja.
Alisema uchunguzi wake umebaini kuwa hata katika wilaya mbalimbali ikiwamo ya Iringa, hakuna kitu kama hicho.
“Jana sikuwa hapa bungeni nilikwenda kwenye halmashauri yangu, hakuna dawati hata moja. Hata Halmashauri ya Iringa kwa Mchungaji Msigwa (Peter) hapa ananiambia hakuna dawati hata moja, mnatudanganya ili iweje?” Aliwashauri wabunge wengine kufanya utafiti katika maeneo yao iwapo kuna madawati ambayo yamepelekwa kutokana na fedha zilizorejeshwa na Serikali kama chenji ya rada.
Lissu alisema ni maneno matupu ambayo yamekuwa yakiwahadaa wabunge na kuwafanya wasahau wajibu wao wa kuisimamia Serikali na kujikuta ni washangiliaji wakati wote. Lissu alisema kinyume na taarifa hizo za Waziri Mkuu, Bunge jana lilikuwa limeelezwa na Naibu Waziri (hakumtaja) kuwa madawati hayo hayajagawanywa.
Katika kipindi cha maswali na majibu, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Kassim Majaliwa akijibu swali la nyongeza la Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe - CUF), kuhusu madawati hayo, alisema kwa kuwa madawati hayo bado yanagawanywa, watakaa na kuangalia utaratibu mzuri wa kuyafikisha Zanzibar.
Lissu pia alisema fedha ambazo zilitajwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo kuwa ni pato la Watanzania ni uongo kwa kuwa ni mali ya wamiliki wa migodi.
Alisema takwimu za waziri zimesababisha Watanzania kuamini kuwa wameingiza fedha nyingi ilihali kiasi kilichoingia hakifikii hata asilimia 10 ya pato la wawekezaji.
Awali, akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhanga Mpina alielezea hofu yake kuhusu maendeleo ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwamba inaweza kufa kutokana na Serikali kutokuilipa madeni yake.
“Mifuko ya hifadhi ya jamii itakufa kutokana na kuidai Serikali madeni mengi makubwa. Kuna haja ya kuangalia jinsi ambavyo tunaweza kuishauri Serikali kwa suala hili,” alisema Mpina.
Mbunge huyo alielezea kukerwa kwake na matumizi ya Dola ya Marekani badala ya Shilingi katika malipo mbalimbali, jambo ambalo linazidi kushusha thamani ya Shilingi.
“Watu wanakuja na Dola wanatumia na wanaondoka nazo bila hata kuzibadilisha, basi ni vyema kama tunaona fedha yetu haifai tuiondoe tutumie hizo Dola,” alisema Mpina.
Aliikosoa Serikali akisema haijawahi kufanya mdahalo wa kina kujadili jinsi matumizi ya Dola yanavyoiathiri Shilingi ya Tanzania.
Majaliwa
Hata hivyo, Majaliwa akizungumza na gazeti hili jana jioni alisema inawezekana Lissu hakumwelewa au amefanya makusudi kupotosha kile ambacho yeye alikizungumza ili kujipatia sifa kwa umma.
“Nilichokisema hakitofautiani na kile kilichomo kwenye jedwali la hotuba ya Waziri Mkuu, nimesema kwamba hadi sasa tunaendelea kugawa madawati ya plastiki katika halmashauri za wilaya 41 na hivi ninavyozungumza halmashauri ya mwisho inayopelekewa madawati leo (jana) ni Temeke,” alisema Majaliwa na kuongeza:
“Kwa upande wa madawati ya mbao, ambayo yeye (Lissu) ameyaita ya chuma, nayo yanaanza kusambazwa katika halmashauri zilizobaki 123, na kazi hiyo itaendelea na ifikapo Agosti 15 mwaka huu kila halmashauri itakuwa imepata mgawo wake.”
Alisema tayari Serikali imetangaza zabuni ya utengenezaji wa madawati awamu ya pili ambayo itafunguliwa Jumatatu ijayo na kwamba baada ya taratibu kukamilika utengenezaji huo utaanza na kukamilika katika muda wa miezi miwili.
Alisema katika awamu ya kwanza, kila halmashauri inatarajiwa kupata madawati 756, sawa na madawati 123, 984.
“Kama unakumbuka awali tulipanga madawati haya yapelekwe kwenye wilaya kama sita nadhani, lakini wabunge walishauri kwamba kila wilaya inufaike na ndicho tulichokifanya,” alisema.

Suala la mgombea binafsi halina mjadala tena

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu imeandika historia katika nchi yetu, baada ya kutoa hukumu iliyohitimisha safari ndefu ya wananchi kutaka wagombea binafsi waruhusiwe katika chaguzi za serikali za mitaa, ubunge na urais. Tunasema mahakama hiyo imeandika historia kutokana na suala hilo kukataliwa na Serikali yapata zaidi ya miongo minne sasa, hata pale mahakama za juu nchini zilipotamka kwamba kuwapo kwa mgombea binafsi ni haki ya kila raia kikatiba.
Pengine wananchi wengi hawajui kwamba nchi yetu iliwahi kuwa na wagombea binafsi. Katika Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi wa mwaka 1960, chama tawala cha TANU kilipoteza kiti cha ubunge katika Jimbo la Mbulu, baada ya Herman Elias Sarwatt aliyegombea kiti hicho kama mgombea binafsi kushinda.
Ushindi huo na mwingine wa baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani ulikishtua chama hicho tawala na ndipo kilipotumia wingi wa wabunge wake bungeni kubadilisha Katiba na kufuta vyama vya upinzani na wagombea binafsi, hivyo kuifanya Tanganyika nchi ya utawala wa chama kimoja.
Hivyo kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kuliibua suala la mgombea binafsi. Serikali iliendelea kumkataa mgombea binafsi, ikisema lazima kila mgombea awe mwanachama wa chama cha siasa. Ndipo mwaka 1993 Mchungaji Christopher Mtikila alipofungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma iliyosikilizwa na Jaji Kawha Lugakingira ambaye alikubaliana na hoja zake, kwamba kugombea kama mtu binafsi ni haki ya kila raia kwa mujibu wa Katiba, kwa maana ya haki ya kuchagua viongozi na haki ya kugombea uongozi.
Lakini katika hali ya kushangaza mwaka 1994, Serikali kwa kutumia wingi wa wabunge wake bungeni ilihakikisha chombo hicho kinafanya mabadiliko ya 11 ya Katiba katika Ibara ya 34 kwa kuzuia wagombea binafsi. Ndipo mwaka 2005, Mchungaji Mtikila alifungua kesi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam akipinga marekebisho hayo ya Katiba. Hatimaye, jopo la majaji watatu chini ya Jaji Kiongozi, Amiri Manento lilikubali hoja za Mchungaji Mtikila na kuruhusu mgombea binafsi.
Iliwashangaza wengi mwaka 2010 kuona Serikali ikikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa. Majaji saba wa mahakama hiyo walisikiliza kesi hiyo chini ya aliyekuwa Jaji Mkuu Augustino Ramadhani. Serikali ilidai katika rufaa yake kwamba hakuna mahakama yoyote nchini yenye uwezo kisheria kusikiliza kesi inayotaka mgombea binafsi na kwamba mahakama za chini zilijipachika madaraka ya kibunge ya kutunga sheria badala ya kuzitafsiri. Katika hukumu iliyokosolewa na wengi, mahakama hiyo, pamoja na kukubaliana na hoja ya haki ya kila raia kuchagua au kuchaguliwa bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa, ilisema siyo jukumu la mahakama kujielekeza katika masuala ya kisiasa.
Ndipo Mchungaji Mtikila alikata rufaa katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu iliyoko Arusha na Juni mwaka jana, mahakama hiyo ilitoa ushindi kwa mrufani na kuitaka Serikali ya Tanzania kutoa taarifa ndani ya miezi sita kuhusu namna inavyotekeleza hukumu hiyo.
Ni jambo jema sasa kwamba Serikali imesema imo katika mchakato wa kisheria utakaoruhusu mgombea binafsi. Sisi tumetiwa moyo na hali hiyo na tunaitaka Serikali itambue kwamba suala hilo halina mjadala tena.

Thursday, 19 June 2014

Lowassa: Bomu la ajira kwa vijana kulipuka muda wowote

Dodoma. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema vijana 10,500 waliojitokeza hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kufanya usaili wa nafasi 70 za kazi katika Idara ya Uhamiaji, ni ishara kuwa bomu la ajira litalipuka muda wowote.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya Viwanja vya Bunge, Lowassa alisema Serikali ni lazima ihakikishe inatengeneza ajira kwa kuwa kila mwaka zaidi ya vijana 30,000 wanahitimu katika vyuo mbalimbali nchini.
Wasomi hao wa fani mbalimbali walijitokeza katika uwanja huo Ijumaa iliyopita, kuanzia saa 12 asubuhi wakisubiri kufanyiwa usaili huo.
Lowassa ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008, amenukuliwa mara nyingi akiitaka Serikali kuchukua hatua kukabiliana na tatizo la ajira na akisema ni bomu linalosubiri kulipuka.
Mbunge huyo wa Monduli kupitia CCM, aliwahi kuingia kwenye malumbano makali na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka kuhusiana na suala la ajira kwa vijana.
Kabaka akiwa bungeni, Machi 21, 2012 alitoa takwimu za namna Serikali ilivyokuwa inatengeneza ajira kwa nia ya kumjibu Lowassa, ambaye alikuwa ameeleza tatizo la ajira linavyowaathiri vijana.
Jana, Lowassa kuongezeka kwa makundi ya vijana wanaopora watu katika maeneo mbalimbali nchini ni ishara ya ukosefu wa ajira. “Watanzania sasa tupo milioni 48 na kila mwaka vijana zaidi ya 30,000 wanahitimu vyuo vikuu na kazi hakuna, pamoja na hilo hatuambiwi ni vijana wangapi ambao hawana kazi,” alisema Lowassa.
Alisema lazima Serikali itengeneze ajira kwa wananchi wake, huku akimtolea mfano Rais wa Marekani, Barack Obama kwamba alishinda awamu ya pili kwa sababu ya kutengeneza ajira.
“Mfano mzuri ni katika uanzishwaji wa viwanda. Tunapofikiria kuanzisha kiwanda cha pamba kwanza lazima tuangalie tutatengeneza ajira ngapi,” alisema.
Katika kuonyesha kuwa ajira sasa ni tatizo nchini, juzi jioni wakati wa mjadala wa Bajeti Kuu, Naibu Spika Job Ndugai alisema Mtanzania mwenye nia ya kugombea urais mwaka 2015 ili aweze kuelekewa kwa wananchi ni lazima aeleze mikakati ya kuwasaidia vijana kupata ajira.
“Ajira ni tatizo kubwa na lazima lishughulikiwe. Kuna vijana hawaendi shule lazima watazamwe. Kuna wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne, cha sita na vyuo vikuu. Nazungumza kutoka moyoni kabisa. Hizi ni dakika za mwisho za Serikali ya awamu ya nne, wale wanaojipanga kwa awamu ya tano kama hawataongelea ajira basi waandike wameumia.”
Ndugai alisema vijana wasio na kazi ndiyo wapigakura wakubwa na kusisitiza kuwa mgombea yeyote makini ni lazima afikirie suala la ajira kwa vijana.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema: “Vijana 10,500 kufanya usaili wa nafasi 70 ni janga la taifa. Yupo kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM aliwahi kulizungumza hili lakini akapondwa kwamba anazungumza mambo kwa kuzua. Sasa huu ndiyo ukweli wenyewe.”

Bajeti ya elimu 2014/15: Serikali imesikiliza kilio cha wananchi?

Pamoja na changamoto za viwango duni vya ubora, ufaulu hafifu, uhaba wa miundombinu, mazingira yasiyoridhisha ya kujifunza na kufundishia; sekta ya elimu imeendelea kukumbwa na matatizo ya miongozo duni inayosababisha ikose mwelekeo.
Matatizo haya ni kama vile kuanzishwa kwa utaratibu wa kuweka kivuli (OMR) kwa shule za msingi, kupanga upya viwango vya alama za ufaulu elimu ya sekondari (angalia matokeo ya kidato cha nne 2012).
Mengine ni kufutwa kwa daraja sifuri na kuanzishwa kwa daraja la tano (dalili ya kuficha aibu ya ongezeko la daraja sifuri), kurejeshwa na kubatilishwa tena kwa sharti la ufaulu kidato cha pili na kuanza kutumika kwa viwango vipya vya ufaulu vilivyokataliwa na Bunge mwaka 2013.
Kimsingi matatizo haya sehemu tu ya matukio yanayotoa picha ya mkanganyiko uliopo katika mfumo unaoongoza elimu.
Taswira inayojitokeza hapa ni kuwa serikali inatumia nguvu nyingi kuipamba sura ya elimu kwa kurekebisha matokeo na kurahisisha ufaulu huku kwa ndani imeficha udhaifu mkubwa katika ufundishaji, ujifunzaji, usimamizi wa shule, uwajibikaji na ubovu wa elimu inayotolewa.
Hakuna haja ya kulumbana, kila Mtanzania anaguswa na hali ya kuporomoka kwa kiwango cha elimu nchini. Umefika wakati Serikali ichukue hadhari na kuachana na tabia ya kupuuza ushauri unaotolewa na wadau wa elimu wanaosisitiza mambo ya msingi ya kufanyia kazi ili kuboresha elimu.
Kwa mfano, kufaulisha wanafunzi ambao hawakufundishwa kikamilifu ni kutengeneza kansa nyingine ambayo italitafuna taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Huu si uzalendo.
Tukemee tabia ya serikali kufanya amuzi wa mzaha katika elimu na kuitaka isikilize vilio vya wananchi na kuwataka watendaji kutanguliza mbele maslahi ya taifa.
Tunaitaka serikali na wabunge kuzingatia mambo muhimu yafuatayo katika bajeti ya elimu ya mwaka 2014/15.
Masilahi ya walimu
Kwa mujibu wa Takwimu za Chama cha Walimu (CWT), hadi kufikia Desemba 2013 madai ya walimu ambayo hayakulipwa yalifikia Sh 61bilioni. Ombi la CWT kwa serikali kuongeza mishahara ya walimu kwa asilimia 50 limekataliwa na walimu wameendelea kupuuzwa.
Wakati huohuo serikali inatumia asilimia 43 tu ya fedha za mishahara ya watumishi wa umma kuwalipa walimu ambao idadi yao ni asilimia 67 ya wafanyakazi wote wa umma. Lakini serikali ilitumia asilimia 57 ya fungu la mishahara ya umma kuwalipa wafanyakazi wa sekta nyingine ambao ni asilimia 33 tu ya watumishi wote wa umma.
Serikali kupitia Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, imeahidi kuwa italipa madai haya ya walimu katika mwaka wa fedha 2014/15.
Hata hivyo, tunakumbusha kuwa haya ni madai ya muda mrefu na ahadi kama hizi zimekuwa zikitolewa mara kwa mara pasina utekelezaji.
Serikali itambue msemo usemao; “Uzuri wa mfumo wa elimu unategemea ubora wa walimu wake”. Kwa mantiki hii haina budi kuwathamini walimu kama kweli inakusudia kuboresha elimu.
Walimu wamekata tamaa na tusipokuwa makini hali hii itaambukizwa kwa watoto wetu, familia zao na hatimaye sehemu kubwa ya jamii pia itakata tamaa.
Uwekezaji katika elimu
Katika makubaliano ya mpango wa Elimu Kwa Wote (EFA - 1990), ambayo Tanzania imeridhia, iliazimiwa kuwa uwekezaji katika elimu katika kila nchi mwanachama ufikie walau asilimia 20 ya bajeti nzima au asilimia sita ya pato la nchi husika.
Hata hivyo, hali imekuwa tofauti katika nchi yetu. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita uwekezaji umekuwa ukishuka badala ya kuongezeka.
Kwa mfano, mwaka 2008/09 bajeti ya sekta ilifikia asilimia 20, lakini ikashuka mpaka asilimiua 18 mwaka 2010/11. Na baadaye mwaka 2013/14 ikashuka hadi asilimia 17.3.
Tunazidi kuikumbusha serikali katika kipindi hiki wanachoelekea kupanga na kupitisha bajeti, izingatie makubaliano haya ambayo kwa hiyari ilitia saini na kuridhia kuwa itajitahidi kupanga walau asilimia 20 ya bajeti yake kuu katika sekta ya elimu.
Upungufu wa ruzuku shuleni
Tanzania iliporidhia kutekeleza mipango ya maendeleo ya elimu ya msingi na sekondari, lengo lilikuwa kuziwezesha shule za umma kuwa na uwezo wa kujiendesha na kusimamia utoaji wa elimu katika kiwango kinachostahili.
Utoaji wa ruzuku (Sh 10,000 kwa wanafunzi wa msingi na 25,000 kwa sekondari) ulikuwa sehemu ya maazimio ya utekelezaji wa makubaliano hayo.
Jambo la ajabu ni kuwa, taarifa za utekelezaji wa mpango na azimio hili la utoaji ruzuku zinaonyesha kuwa kiasi ambacho kimekuwa kikifika shuleni ni pungufu ya kilichopangwa.
Mathalani, katika awamu ya kwanza ya mpango wa elimu ya msingi, wastani wa Sh 6,497 tu ndizo zilizofika shuleni badala ya Sh10,000, huku wastani wa Sh 5,500 tu ndio ukifika shuleni wakati wa utekelezaji wa awamu ya pili.
Hali hii inaendelea hata katika utekelezaji wa awamu ya tatu. Wastani wa kiwango kilichofika shuleni mwaka 2012/13 ni Sh 3,580 badala ya Sh 10,000.
Hali hii inazikumba pia shule za sekondari ambazo nazo zinapokea wastani wa Sh 16,384 badala ya 25, 000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi.
Ikumbukwe tu hapa kuwa viwango hivi ni wastani tu wa hali ya utoaji ruzuku shuleni, lakini katika hali halisi ziko shule nyingi ambazo hupata chini ya wastani wa 1,500 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi.
Bajeti ya elimu ya awali
Kwa kutambua umuhimu wa elimu ya awali katika makuzi na maendeleo ya mtoto kitaaluma na kijamii, serikali imeazimia katika mipango yake mbalimbali kufanya uwekezaji stahili katika eneo hili.
Sera ya Elimu ya 1995, mtaalaa wa elimu ya awali wa 2007, Dira ya Taifa 2025, Mpango wa Maendeleo Elimu ya Msingi (MMEM), Mkukuta ni miongoni mwa mipango ambayo inaakisi azimio la serikali kukuza elimu ya awali.
Pamoja na maazimio haya serikali imeshindwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano haya. Mathalani uwiano kati ya wanafunzi wa awali na darasa umebaki kuwa 1:115 badala ya 1:25, uwiano kati ya mwanafunzi kwa mwalimu pia ni 1:124 badala ya 1:25. (BEST 2013).
Tutakumbuka kuwa elimu ya awali haikugusiwa kabisa katika mpango wa ruzuku katika awamu ya kwanza ya Mpango wa Maendeleo Elimu ya Msingi (MMEM ). Na hata ilipogusiwa katika awamu ya pili, fedha kwa ajili ya ruzuku elimu ya awali hazikutoka kabisa.
Katika awamu ya tatu, elimu ya awali imejumuishwa katika bajeti ya ruzuku kwa shule za msingi. Hata hivyo, taarifa za utekelezaji mipango zinaonyesha fedha kwa ajili ya elimu ya awali hazijumuishwi katika fedha ya ruzuku inayokwenda shuleni.
Kuimarisha ukaguzi 
Hali ya ukaguzi bado ni mbaya, uwezo wa serikali kukagua shule hauridhishi. Takribani asilimia 19.1 tu ya shule zote za msingi ndizo zinazokaguliwa kwa mwaka na asilimia 21.4 kwa shule za sekondari.
Wizara husika ijitahidi kuongeza bajeti ya ukaguzi wa shule angalau idara iweze kukagua asilimia 50 ya shule zote za msingi na sekondari kwa mwaka.
Kama bajeti ya ukaguzi itaongezwa tuna imani shule zetu zitakaguliwa. Hivyo viwango vya ubora vitafahamika, upungufu utafanyiwa kazi ili hatimaye tuweze kuwa na elimu bora.
Wakati tukiitaka serikali kuongeza bajeti ya ukaguzi, tunasisitiza pia umuhimu wa kuwa na Wakala ya Ukaguzi wa Elimu kama zilivyo sekta nyingine. Hii ndio njia pekee na sahihi ya kuboresha ufanisi katika suala la ukaguzi.
Mazungumzo ya mchakato huu yamekuwepo kwa taribani miaka mitatu sasa lakini mafanikio yake hayaonekani. Itaendelea wiki ijayo