Monday, 30 June 2014

Msekwa aeleza sababu ya wasomi kukimbilia siasa

Dar es Salaam. Kwa nini siasa imegeuka kimbilio la wengi, wakiwamo wasomi Tanzania?
Ni swali aliloulizwa Spika mstaafu, Pius Msekwa katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni.
Akijibu swali hilo, Msekwa alieleza kwa ufupi sababu za wasomi kuacha taaluma zao na kuwekeza nguvu na akili zao katika siasa akisema inalipa kwa haraka na kwa njia nyingi zikiwamo mishahara minono, posho na marupurupu kuliko zilivyo taaluma nyingine.
Msekwa ambaye amewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akitokea kwenye Chama cha Tanu na baadaye kurejea kwenye siasa, alisema malipo manono yamewafanya wasomi wengi, wakiwamo maprofesa, madaktari na wengineo kuifanya kimbilio.
Alisema pia uhuru wa watu kuchagua kazi nyepesi za kufanya katika maisha yao umefanya waione siasa kama kimbilio rahisi kuliko kutoka jasho kwenye taaluma, zikiwamo za utafiti, tiba, upasuaji, ualimu na nyinginezo. “Siasa imegeuka kimbilio kwa kuwa ina posho na marupurupu mengi zaidi,” alisema Msekwa na kuongeza kuwa wanasiasa wanajipitishia posho ambazo haziwezi kutolewa kwingineko.
“Mpe mtu choice (chaguo), acha aende kokote hata katika siasa, lakini ni vyema taaluma pia ikaheshimika,” alisema na kuongeza kuwa jambo hilo lilianzia  kwenye awamu zilizopita ambako wasomi, ama walioteuliwa au kuchaguliwa waliamua kushiriki siasa na hivyo kuziacha taaluma zao. Msekwa alimtaja msomi mmoja, Profesa Mazengo ambaye aligombea ubunge baadaye akautelekeza baada ya kushindwa kutimiza dhamira yake.
“Kulikuwa na mtu anaitwa Profesa Mazengo, yeye alikimbilia kwenye siasa akilenga kupata uwaziri. Ubunge alishinda lakini alipokosa uwaziri akautelekeza ubunge wake, hata jimboni hakwenda, hakuwakilisha wananchi na wapigakura wake, hivyo hakurudi baada ya miaka mitano,” alisema.
Kwa siku za karibuni, siasa na hasa ubunge, unaonekana kuwa na masilahi na fursa zaidi kuliko nafasi nyingine katika jamii na ndiyo maana wasomi wamekimbilia huko kwa matarajio ya kupata fursa za kupitisha mambo yao. Baadhi yao (wasomi), ubunge siyo tija, wamejikita zaidi kwenye nafasi katika serikali, zikiwamo za mitaa ili kufanikisha biashara zao au kuwa karibu wananchi wa ngazi ya chini.
Kwa mfano, orodha ya wabunge kwenye Bunge la sasa, inaonyesha wasomi wengi wakiwamo maprofesa, madaktari wa falsafa, madaktari wa tiba au wahandisi.
Msekwa alipoulizwa anadhani ni kwa nini Serikali haiboreshi masilahi ya wasomi katika taaluma zao, alicheka kisha akasema uwezo wa nchi ni mdogo, haiwezi kuboresha masilahi ya watumishi wote lakini inaweza tu kwa wabunge.

No comments: