Monday, 6 January 2014

Mkono atoboa siri za Zitto

Dar es Salaam.Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono ametoa ufafanuzi juu ya uhusiano wake na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe.
Hatua hiyo ya Mkono imekuja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kumtuhumu kuwa aliwahi kumpa Zitto magari mawili.
Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Mkono alisema kuna magari mawili yanayohusishwa na Zitto na kuyataja kuwa ni Toyota Land Cruiser na Nissan Patrol.
“Sijawahi kumpatia Zitto magari, isipokuwa kuhusu hiyo Land Cruiser, nilitoa msaada wa kuwanusuru Zitto na Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe), kule Tarime kwenye msiba wa marehemu Chacha Wangwe (aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Chadema), kwani walikuwa wakitishiwa kupigwa.”
Alisema alitoa gari hilo lililokuwa na Bendera ya Bunge liwachukue Mbowe na Zitto na kuwapeleka Mwanza... “Walipofika Mwanza, Zitto aliwasiliana na mimi kuhusu ununuzi wa gari hilo na kupitia wakala wangu nilimuuzia,” alisema Mkono.
Kuhusu Nissan Patrol, Mkono alisema lilikodishwa kwa Zitto na mpaka sasa bado analipa gharama za kulikodisha...
“Hata nyaraka za umiliki wa gari hili ninazo mimi mwenyewe kama mmiliki halali. Ninamiliki magari mengi tu hata wewe mwandishi ukitaka Vogue (aina ya gari) nitakukodisha tu,” alisema Mkono.
Alisema wanafahamiana kwa siku nyingi hata kabla ya Zitto kuwa mbunge na kwamba aliwahi kufanya mazoezi kwa vitendo katika ofisi yake (Mkono), alipokuwa mwanafunzi.
Kuhusu tuhuma kwamba anawahonga wapinzani wake wajitoe katika uchaguzi ili apite bila kupingwa alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, 2005 na 2010 alipita bila kupingwa kutokana na uchapakazi wake wa kiwango kikubwa.
Mkono pia alijibu tuhuma zilizotolewa na Zitto jana kwamba Mbowe alipewa mamilioni ya fedha na Mkono kwa nyakati tofauti na kusema hajawahi kutoa fedha zozote kusaidia Chadema.
Zitto akana
Katika hatua nyingine, Zitto ameitaka Chadema kumwandikia mashtaka mapya yaliyoibuliwa na Lissu ili aweze kujitetea.
“Mashtaka yangu ni yale tu ya waraka na kugombea uenyekiti na shtaka moja la masuala ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Kwa kuwa hawakuniandikia mashtaka hayo kinachobakia ni majungu tu, masuala ya kuhongwa magari ni tuhuma zinazorudiwarudiwa bila ushahidi wowote,” alisema na kuongeza:
“Mkono ananihonga ili nimpe nini? Yeye mbunge na mimi ni mbunge pia. Hiyo hongo tunabadilishana na nini? Katika kumaliza Shahada yangu ya Uzamili ya Sheria na Biashara nilifanya `internship’ (mafunzo kwa vitendo) kwa Mkono na hivyo kuna uhusiano wa kikazi wa baba na mtoto.”
Zitto alisema kuwa Mkono ni kama mzee wake na suala la kumpa chochote kile si hoja.
Kitila amruka Slaa
Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk Kitila Mkumbo amesema kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa kuwa alikiri kwamba Zitto alikuwa akiujua waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013, ni za kutunga.
Juzi, wakati akieleza uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kuwafukuza uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Dk Kitila, Dk Slaa alisema wakati akihojiwa na Kamati Kuu, Dk Kitila alisema Zitto alikuwa akiujua waraka huo.
“Siyo kweli. Hata siku moja sijawahi kukiri kwamba Zitto alikuwa akiufahamu waraka, kilichosemwa na Dk Slaa ni uongo.”
Mwigamba afafanua
Mwigamba alisema hakuhojiwa na Kamati Kuu kwa sababu yeye ni Msabato na Siku ya Sabato, hairuhusiwi kufanya jambo lolote zaidi ya kumwomba Mungu.
“Waliniita Ijumaa (Januari 3) ili nihojiwe lakini mpaka saa 12 jioni sikuwa nimehojiwa na niliwaeleza kuwa jua likizama sitakubali kuhojiwa kwa sababu itakuwa imeanza Siku ya Sabato,” alisema.
Alisema kikao cha Kamati Kuu kiliendelea Januari 4, mwaka huu, pia hakuweza kwenda kuhojiwa kwa sababu ilikuwa Sabato, pia alikuwa kanisani, “Niliwaambia kuwa nipo tayari kuhojiwa Jumapili, hawakunijulisha kama wameridhia.”

Thursday, 2 January 2014

Friday, 27 December 2013

Viatu hatari kwa afya ya miguu ya wanawake

‘Mchuchumio’ ama viatu vyenye visigino virefu, ni mojawapo ya vitu vinavyopendwa na baadhi ya wanawake mbalimbali, si katika Tanzania bali dunia nzima.
Wataalamu wanaeleza kuwa viatu hivi huharibu pingili za uti wa mgongo na huvunjavunja mifupa ya visigino.
Wanawake wenye maumbo ya kati, ambao si wanene wala wembamba wamekuwa wakipendelea viatu virefu.
Kwa kiasi kikubwa wasichana wafupi, wamekuwa wakipendelea kuvaa viatu virefu ili angalau na wao waonekane warefu.
Ashura Mgweno, mfanyakazi wa Kampuni ya Usafi jijini Dar es Salaam, anasema: “Nimetumia viatu kwa muda mrefu, lakini sasa sitaki kusikia viatu virefu. Mimi ni mfupi, nilikuwa navaa sana, lakini sasa sitaki hata kuviona jinsi vilivyonitesa,” anasema.
Anasema kuwa viatu virefu muda wake ni miaka mitatu, inaharibu visigino na misuli ya miguu na kutengeneza vigimbi ambavyo baadaye husababisha maumivu makali.
Akizungumzia hili, Ruth Erasto ambaye anafanya kazi katika ofisi moja jijini Dar es Salaam, anasema aliacha kuvaa ‘mchuchumio’ kwa maagizo ya daktari.
“Niligawa viatu vyangu vyote virefu baada ya kupatwa na maumivu ya mgongo. Viatu virefu havilinganishi mwili wakati wa kutembea na niliagizwa na daktari kuachana na viatu virefu...hiyo ilitokana na mimi kuanza kupatwa na matatizo ya mgongo,” anasema.
Anasema kuwa alipatwa na matatizo hayo bila kufahamu, lakini baada ya kuchunguzwa, ndipo ikabainika kupatwa na matatizo hayo.
Mwanamama mwingine aliyepatwa na matatizo hayo, Victoria, anasema kuwa inamlazimu kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kila mara kwa ajili ya kuangaliwa maendeleo ya mgongo baada ya kuvaa viatu virefu kwa muda mrefu na kumletea athari hizo.
Victoria ambaye ni mfupi na mnene kiasi kwa umbile, anasema kuwa pamoja na kupenda kuvaa viatu hivyo, hataki kusikia habari zake.
“Nakuambia sina hamu na viatu hivi, acha kabisa, nimekoma...nimekwenda Muhimbili hadi nimechoka, maumivu kuanzia kiuno hadi mgongo,” anasema. 
Jozi mbili
Hakika, wapo wanawake wanaofahamu madhara ya kuvaa viatu hivyo, lakini wengine wanafahamu, lakini wanapuuza. Baadhi ya wanaopuuza ni kutaka kuonekana wa kisasa zaidi, licha ya kuwa wanahisi maumivu makali wanapovaa.
Mara kwa mara, wengi wa wanawake hulazimika kubeba viatu jozi zaidi ya moja, vile vya chini (flat shoes) kwa ajili ya kubadilisha pindi mambo yanapokuwa magumu.
Christina Mdete, Mkazi wa Yombo Buza, Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam anasema amekuwa akibeba jozi mbili za viatu anapotoka nyumbani na kuvaa viatu virefu anapoingia ofisini. “Hata ninapokuwa ofisini, navua kisha navaa ‘flat’...ah! siwezi wewe, kutwa nzima, vinaumiza halafu hauko na raha ukivaa muda wote.
Anasema hata wanaokwenda kwenye sherehe, hutumia muda mfupi kuvaa, kwani ni pale wanapokwenda kutoa zawadi na baada ya hapo, vinavuliwa na kuvaliwa viatu vya chini.
Wasichana wengi wanafahamu ‘mchuchumio’ husababisha maumivu makali lakini je, ndiyo kutimiza usemi wa ukitaka uzuri shurti udhurike? Kwa kawaida, urembo hauwezi kusababisha maumivu, lakini kuvaa viatu virefu kuna athari kubwa.
Utafiti mbalimbali wa hivi karibuni unaonyesha kuwa viatu virefu havifai hata kidogo. Kimsingi, uvaaji wa viatu virefu husababisha maumivu makali ya misuli ya miguu pamoja na nyama za nyuma kwenye maungio ya magoti na enka.
Uharibifu ni mkubwa pia huweza kutokea ndani ya magoti kwa kuhamisha maungio (dislocate). Kwa jinsi mhusika anapovaa viatu virefu kwa muda mrefu, ndipo inaposababisha madhara ya muda mrefu.
Mbali na hayo, vilevile, husababisha mwili kukosa usawa wakati wa kutembea, misuli ya miguu kubana, kupoteza mwelekeo wa mwendo halisi na wakati mwingine husababisha mhusika kuanguka na kumsababishia maumivu makali.
Madaktari wanashauri kuvaa viatu virefu kuwe kwa muda maalumu kwa shughuli maalumu na visizidi urefu wa inchi mbili.
Kama mtu alizoea kuvaa viatu virefu kwa muda mrefu, inashauriwa kuacha taratibu badala ya kubadilika haraka kwenda kwenye viatu. Kama viatu virefu vitavaliwa kazini, ni vizuri kuwepo na viatu vingine vya kubadilisha.
Utafiti mwingine unaonyesha kuwa viatu virefu husababisha maumivu makali ya dole gumba la mguu, kuzuia ukuaji wa kucha na matatizo mengine. Watafiti hao wa Chuo Kikuu cha Griffith kwenye mji wa Queensland, Australia wakiongozwa na Dk Neil Cronin, katika utafiti wao, waliliambia gazeti la New York Times kwamba wanaendelea kufanya utafiti kuona madhara zaidi yanayoweza kupatika.
Katika uchunguzi uliochapishwa kwenye jarida la Journal of Applied Physiology, Dk Cronin anasema wanawake wengi waliofanyiwa utafiti wamebainika kutokuwa imara katika miguu yao, kupatwa na maumivu makali na kuharibiwa misuli na enka ya mguu.
Naye Dk Orly Avitzur, Mganga Mshauri kwenye kitongoji cha Tarrytown, New York, Marekani anasema kuwa alifanya utafiti kwa wanawake wa zaidi ya miaka 40 kuwa hawawezi kuvaa viatu virefu kwa kuwa miguu yao tayari imeharibiwa.
“Kama ni miaka 20 sawa, ni kitu kingine,” Avitzur anasema. “Kama ikiwa ni zaidi ya miaka 40 ni tatizo na itakuwa suala lingine mtu akivaa viatu hivyo, lakini chini ya hapo haina shida sana.”
Mtaalamu wa Mifupa katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam, Dk Edemeza Machange anasema kuwa matatizo ni makubwa kwa mtumiaji wa viatu virefu na athari zaidi huwakumba wanawake wanene.
“Ni mbaya sana...kwa wanawake wanene haishauriwi watumie viatu virefu kwa kuwa vitawaletea matatizo mengi katika miili yao,” anasema.
Kama walivyosema wataalamu waliotangulia, Machange anasema kuwa kubwa linaloumiza wanawake wengi ni kuvaa viatu virefu kwa kipindi kirefu na matokeo yake ni kuumwa mgongo kwani uharibu mpangilio wa pingili za uti wa mgongo.
“Kwa kawaida mtu anapoteza mwendo halisi, sasa kutotembea kwa mpangilio, huharibu mfumo wa pingili za mgongo, hata kiuno na kusababisha maumivu makali...tumekataza wengi kuvaa viatu virefu baada ya kupatwa na matatizo ya mgongo.”
Anawashauri kinamama hasa wasichana, wafahamu kuwa pamoja na kutaka urembo, lazima wajali afya zao kwa kuvaa viatu virefu katika kipindi kifupi na zaidi ni kuangalia madhara kwa baadaye kuliko kukimbilia kuvaa viatu virefu kwa ajili ya urembo.

Makamba ajipigia debe la urais kiaina

Mwanza. Katika kile kinachoonekana kama kujipigia debe katika kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amewaambia viongozi wa dini Kanda ya Ziwa kwamba vijana wanapofika kuomba ridhaa yao, muwaangalie, msiwabeze.
Huku akikataa kuweka bayana nia yake ya kuwania urais kwa maelezo kwamba muda wa kufanya hivyo haujawadia, Makamba aliwaambia viongozi hao wa dini kwamba wagombea hao wanapopita wawasomee sifa za uongozi katika Biblia na kusema kumekuwapo mjadala wa sifa za uongozi kuhusu kijana na kusema amekuwa akitoa mwito kwa vijana wasiokuwa na makandokando kushiriki na kujitokeza katika kusaidia nchi ipone.
Akizungumza juzi usiku mjini hapa katika chakula cha pamoja na maaskofu na wachungaji kutoka Umoja wa Makanisa ya Kikristo wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Makamba ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli (CCM), alisema: “Huu ni wakati wa kila mmoja kutafakari hatima ya nchi yetu. Ndugu zangu… nadhani tuzungumze machache yanayohusu nchi yetu na Taifa letu, kwa sababu sote ni Watanzania na wote tuna hamu ya kujua na kutafakari mustakabali wa nchi yetu, umoja wetu, amani yetu na utulivu wetu.”
Alisema vijana wengi wamekuwa waoga kwa madai kwamba hawana fedha, uzoefu lakini akasema maaskofu na wachungaji wanapaswa kuwa mashahidi kupitia vitabu kwani katika Yeremia imeelezwa jinsi Mungu alivyompatia unabii Yeremia ambaye alidai yeye bado mdogo.
“Yeremia alipopewa unabii alilalamika mimi mdogo mimi siwezi, lakini Mungu alimwambiaje, ngoja nisome, (Yeremia 1: 4-10) …. Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako nilikujua, kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalumu, nilikuweka uwe nabii kwa mataifa,” alisema na kuongeza:
“Bwana alimwambia usiseme, mimi ni mtoto mdogo. Utakwenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza, usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe.”
Alisema Tanzania inapita katika kipindi kigumu, hivyo viongozi wa dini wanapaswa kuongoza maombi yatakayoiwezesha kupata kiongozi mwenye sifa ya kuivusha katika kipindi hicho.
Makamba amesema nchi inakabiliwa na nyufa kama vile rushwa, udini, ukabila, Uzanzibari na Uzanzibara, huku akirejea hotuba ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya Machi 1995, ambayo aliyataja mambo hayo kuwa nyufa zinazoweza kuliangamiza taifa.
Alisema Tanzania inahitaji uponyaji na ikibidi kuanza upya kwa maana ya aina ya uongozi unaohitajika hivi sasa na kwamba ili kutimiza lengo hilo, viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kutafakari na kuielekeza nchi njia sahihi ya kufuata.
“Shughuli za siasa zimeingiliwa na matapeli, lakini hata shughuli yenu pia imeingiliwa na matapeli. Sasa tunapotafuta uponywaji wa nchi yetu ninyi mna nafasi kubwa kwani uponyaji tunaouzungumzia ni wa maovu ya kiroho, uongo, ubakaji na vitu kama hivyo, ninyi mna nafasi kubwa sana,” alisema.
Alisema viongozi wa kisiasa pia wanayo nafasi yao katika kuponya taifa lakini lazima wanapofanya kazi hiyo wawe wasafi.Alisema askofu au mchungaji akihubiri anapaswa kuwa msafi na hata katika uongozi wa siasa anaposimama mtu na kusema yeye ni jawabu la matatizo ya wananchi ni vizuri kumtazama sura yake kama ameacha (maovu) 
“Tunapoomba uongozi wa kisiasa zipo sifa kwani tunaomba kuongoza watu wa Mungu ambao ni walewale wanaokuja kanisani ndiyo wanaokuja katika siasa, kuongoza watu wa Mungu siyo kitu kidogo…… hivyo lazima vigezo vya kuongoza watu hawa viwe vikubwa sana,” alisema
Rasilimali za nchi
Alisema Tanzania hivi sasa inakabiliwa na changamoto zinazoweza kuitwa kuwa ni za kidunia na za kibinadamu zinazojumuisha masuala kama vile upatikanaji wa huduma za afya, maji na elimu.
“Tunagawanyika ingawa migawanyiko hiyo si ya kidini, rangi na kikabila... iko ya namna gani, watu wachache wananufaika na keki (rasilimali) ya taifa kuliko wengine,” alisema Makamba na kuongeza:
“Sasa Serikali, hili kwetu ni muhimu sana…. hakuna kitu muhimu kama kuendelea kujenga umoja wa taifa letu, migawanyiko hii ndiyo changamoto. Elimu anayoipata mtoto wangu ndiyo anaipata mtoto wa Rwamgasa, Kwimba na Nyarugusu?”
Alisema usawa katika elimu pamoja na huduma nyingine kama afya na nyingine muhimu, ndiyo msingi wa ujenzi wa taifa lenye amani na umoja kwani kila mmoja atajihisi kunufaika na rasilimali za nchi.
Naibu Waziri huyo alisema changamoto nyingine zinazoikabili nchi ni vitendo vya rushwa, ubadhirifu na wizi wa mali ya umma, ubakaji, utapeli na kuporomoka kwa maadili.
Alisema taifa halipaswi kusubiri adhabu kutoka kwa Mungu kama inavyosomeka katika vitabu vitakatifu ambako kuna ushahidi kuhusu gharika wakati wa Nuhu, pia moto wakati wa Sodoma na Gomora, huku akiwapa changamoto viongozi wa dini kukabiliana uovu unaoshika kasi.
“Sasa taifa letu lina miaka 52 ya Uhuru wa Tanganyika na mwakani tunaadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Zanzibar. Miaka 50 ni mingi kwa binadamu, lakini ukweli ni kwamba kazi ya kulijenga taifa letu ndiyo inaanza.”
Shinikizo la maaskofu
Baada ya hotuba yake, baadhi ya maaskofu na wachungaji walisikika wakimshinikiza Makamba atangaze nia ya kugombea urais lakini alisema atafanya hivyo wakati mwafaka ukiwadia.
Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa hayo ya Kikristo, Askofu Charles Sekelwa alisema: “Viongozi wa dini tukubaliane kuwa walezi na tusimkatae mtu kwa dini yake wala kabila lake. Wakijitokeza vijana huko mbele tuwaunge mkono, hayo maneno ni ya mtu mwenye hekima”.Askofu Jacob Lutabija alisema amepokea ujumbe mzito ambao atakwenda kuutangaza kwa waumini wake wa Musoma akisema kwa watu wenye hekima zao wametambua nini wanapaswa kufan



Kuundwa Tume Huru ya Uchaguzi kunasubiri kuwapo machafuko?

Kama kuna jambo ambalo limewafanya wananchi wengi kukuna vichwa kwa muda mrefu pasipo kupata majibu, ni kutoundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia chaguzi mbalimbali na mchakato wa kupata Katiba Mpya katika ngazi zote zilizosalia, baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kumaliza kazi yake rasmi wiki ijayo.

Kwa maana hiyo, mchakato wa Katiba Mpya unaingia katika awamu ya pili kwa Tume hiyo ya Warioba kukabidhi kijiti cha mbio za mchakato huo kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ambayo majukumu yake sasa ni pamoja na kusimamia mambo muhimu mwakani ambayo ni pamoja na: Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura; Kura ya Maoni kuhusu Rasimu ya Tatu ya Katiba Mpya; Utoaji wa Elimu ya Uraia kuhusu upigaji wa kura hiyo na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Nec pia ndiyo itasimamia na kuendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Majukumu hayo hakika ni mazito mno kutekelezwa na Nec, ambayo imekuwa na udhaifu mkubwa kiasi cha kupoteza mwelekeo na imani kwa wananchi. Tangu kuanzishwa kwake na Sheria ya Bunge mwaka 1977, Tume hiyo imedhihirisha kwamba siyo huru hata kidogo kutokana na kuonekana machoni mwa wananchi kwamba imo mfukoni mwa Serikali na chama tawala, kwani yamejitokeza matukio mengi ya aibu katika uhai wake wa miaka 36, ikiwa ni pamoja na kuegemea upande wa watawala.
Ndiyo maana siyo wananchi wengi walioshangazwa na kauli ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Damian Lubuva alipokiri miezi michache iliyopita wakati akitoa maoni ya Tume yake mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa, Tume yake siyo huru. Alishauri kwamba katika mazingira ya sasa ya kuwapo mchakato wa kupata Katiba Mpya, iundwe Tume Huru ya Uchaguzi ili chombo hicho kipate mwafaka wa kitaifa ili kiweze kusimamia mchakato mzima kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, chini ya Katiba Mpya.
Kauli ya Jaji Lubuva imethibitisha pasipo kuacha chembe ya shaka kwamba hoja za muda mrefu za vyama vya upinzani na asasi zisizo za kiserikali kwamba Tume hiyo siyo huru zina mashiko. Tafsiri sahihi ya hoja hizo ni kuwa, siyo tu kwamba Tume hiyo siyo huru, bali pia chombo hicho hakina uwezo wa kusimamia majukumu yake kwa ufanisi kutokana na matatizo ya kisera na kimfumo. Kukosekana kwa utashi wa kisiasa pia kumechangia mno katika kudumaza Tume hiyo, ambayo kwa mujibu wa Katiba iliyopo wajumbe wake wanateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, ambaye ni kada namba moja wa chama tawala.
Kitendawili kinachoshindikana kuteguliwa hadi sasa ni sababu za mamlaka husika kutoona umuhimu wa kuwapo mfumo wa kupata Tume Huru ya Uchaguzi ili uende sambamba na kupatikana kwa Katiba Mpya. Lazima tukubali ukweli kwamba Tume iliyopo sasa haikubaliki katika mazingira tuliyomo na ya baadaye. Kama Tume hiyo imekataa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa miaka mingi sasa, kwa mfano, tutegemee nini zaidi ya vurugu, machafuko na umwagaji damu huko tuendako?





Sunday, 22 December 2013

Wabunge wa CCM wamgomea Waziri Mkuu Pinda

Dodoma. Wabunge wa CCM jana mchana walimgomea Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge (Party Cocas) ya chama hicho, Mizengo Pinda na kushinikiza mawaziri watatu ambao wizara zao zimetajwa kushindwa kusimamia vyema Operesheni Tokomeza Ujangili wajiuzulu.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa mawaziri walioshinikizwa kujiuzulu wenyewe ni pamoja na Balozi Khamisi Kagasheki ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii,  Dk Emmanuel Nchimbi (Waziri wa Mambo ya Ndani)  na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa bungeni jana kiliitishwa na Pinda ambaye pia ni Waziri Mkuu kwa lengo lililoelezwa ni kuwapoza wabunge.
Chanzo cha habari kutoka katika kikao hicho kilisema kuwa wabunge hao walitaka mawaziri hao kujiuzulu wenyewe ili kukinusuru chama  mbele ya wananchi.
“Tumemtaka Waziri Mkuu akakae na wenzake na kutuambia kama wanajiuzulu au la na kutupa jibu kabla ya kuahirishwa kwa Bunge, mtasikia wenyewe baadaye ndani ya Bunge,”kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, baada ya kukamilika kwa kikao hicho na wabunge kurejea bungeni, Pinda hakurejea bungeni, badala yake ilidaiwa kwamba alikuwa na kikao katika ofisi zake zilizopo bungeni.
Hadi  saa 11.25 alasiri  wakati kikao cha Bunge kikiendelea Waziri Mkuu alikuwa hajarejea bungeni, huku ikielezwa kwamba katika kikao alichokuwepo hakikuwahusisha mawaziri wanne waliokuwa katika shinikizo la kujiuzulu.


Malipo ya fidia yawatoa machozi wananchi Dar

Dar es Saalam. Wananchi wa Mji Mpya Majohe, Guluka Kwalala na Ulongoni katika Manispaa ya Ilala  wameiomba Serikali kuingilia kati na kumwamuru mwekezaji wa ujenzi wa njia ya umeme wa  kilovoti 220 kutoka Somanga Mtama  mpaka Kinyerezi, Kilwa Enegy kuwalipa gharama zinazoendana na hali ya maisha ya sasa.
Ombi hilo walilitoa  jana walipokuwa wakijadili kuhusu  dodoso la uhakiki wa mali zao na malipo, walilopewa lilivyokuwa na  upungufu, mapunjo ya mali zao hasa thamani  za nyumba kuwa kidogo  tofauti na gharama  za ujenzi na ununuzi wa kiwanja walizotumia.
Utathmini wa mali na nyumba za wananchi unadaiwa kufanywa na kampuni binafsi iliyofahamika kwa jina la Joransa, ambapo tathmini katika maeneo hayo ilifanyika mwaka 2011 na kutolewa ahadi kuwa malipo ya fidia yangeanza kulipwa baada ya miezi mitatu .
.Baruani Kanoze  akilalamikia kulipwa  fedha kidogo tofauti na thamani ya mali zake, alisema mwekezaji huyo awali aliwahi kusema kuwa atawalipa kwa kiwango kinachoendana na gharama za maisha zilivyo kwa wakati husika jambo ambalo limewashangaza sana. hasa kulingana na kiwango cha malipo kilichotolewa.
‘Ni jambo ambalo haliingii akilini baada ya kuangalia karatasi za tathmini na kukuta gharama zilivyowekwa za viwanja na kupangisha nyumba, kiwanja umewekewa Sh1 milioni na gharama ya kupanga nyumba eti Sh20,000 kwa mwezi, sijui unakwenda kupanga wapi nyumba’ alisema mkazi wa Guluka Kwalala ambaye hakutaka kutajwa gazetini.
 Alisema yeye anamiliki nyumba ya vyumba  vitano, yenye umeme, choo bora pamoja na  kisima cha maji alivyovijenga   kwa zaidi ya Sh40 milioni,  kwenye dodoso la uhakiki wa mali  anaambiwa thamani ya nyumba yake ni Sh6 milioni.
Aidha, walishauri kuliko Serikali kujiingiza katika maafa kwa kukubali mradi huo utekelezwe wakati wananchi hawajaridhika na fidia ao, ni vyema ikafanyika tathmini nyingine ambayo itakuwa ya haki .
Hata hivyo, uongozi wa Kilwa Energy ulipotafutwa kufafanua malipo hayo ya wananchi, simu zao hazikuweza kupatikana.

Kufutwa kodi ya simu, Bunge aibu tupu

Hatua ya Rais Jakaya Kikwete kutia saini hati ya dharura ili Muswada wa Fedha wa mwaka 2013 ufanyiwe marekebisho na kuondoa tozo ya kodi kwa laini za simu imeliacha Bunge katika fadhaa na fedheha kubwa.
Bunge la Bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2013 lilishuhudia wabunge wa chama tawala wakitumia wingi wao bungeni kupitisha kodi hiyo ambayo iliamsha hasira na vilio kutoka kwa wananchi kutoka kila kona ya nchi.
Tunasema hatua hiyo ya Rais imeleta fadhaa na fedheha kwa Bunge kutokana na kuwapo matukio mengi ya aina hiyo katika kipindi kifupi, ambapo Bunge limekuwa likipitisha miswada mingi muhimu kwa ushabiki wa kisiasa badala ya kuangalia masilahi mapana ya taifa. Rais kwa kuwasitiri  wabunge wa chama chake amekuwa akitia saini miswada hiyo na kuwa sheria, lakini baadaye amekuwa akisikiliza hoja za wapinzani na kulazimika kurudisha sheria hizo bungeni ili zifanyiwe marekebisho.
Siyo nia yetu hata kidogo kuorodhesha hapa sheria zote ambazo Rais amezirudisha bungeni kufanyiwa marekebisho katika miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo, wasomaji wetu watakumbuka kuwa, moja ya sheria nyeti zilizorudishwa bungeni ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ndiyo hasa iliyoanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya yapata miezi 18 iliyopita. Kama tulivyosema hapo juu, muswada wa sheria hiyo na miswada mingine mingi muhimu ilipitishwa na Bunge kwa ushabiki wa kisiasa na kiitikadi, kwa maana ya hoja za wabunge wa upinzani kuzimwa au kujadiliwa kwa kejeli, vijembe na matusi na hatimaye kupuuzwa.
Ni katika muktadha huo, Sheria ya Fedha ya mwaka 2013 iliyoanzisha tozo ya kodi kwa laini za simu inapaswa kuangaliwa. Bunge kwa staili hiyohiyo ya ushabiki wa kisiasa na kiitikadi lilipitisha muswada wa sheria hiyo, huku wabunge wa upinzani wakipinga na kuainisha athari zake kwa wananchi na uchumi wa taifa. Ni kweli Rais alisaini muswada huo na kuwa sheria, lakini kutokana na athari zake kwa uchumi na wananchi kwa jumla, sasa  ameirudisha bungeni kwa hati ya dharura akitaka ifanyiwe marekebisho na kuifuta kodi hiyo mara moja.
Ni aibu kwa Bunge, Serikali na Kamati ya Bajeti iliyobuni tozo hiyo kutoona mapema madhara ambayo yangesababishwa na kodi hiyo ya Sh1,000 (kwa kila laini ya simu kila mwezi) kwa wananchi maskini ambao  wanahangaika kupata mlo mmoja kwa siku. Spika wa Bunge, Anne Makinda na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kutojua hali halisi ilivyo, hasa vijijini walikaririwa bungeni wakitetea kwa nguvu hoja ya kuwekwa kwa tozo hiyo,  wakidai kila mwananchi anao uwezo wa kuilipa kila mwezi.
Kutokana na utata uliosababishwa na tozo hiyo, kodi hiyo ilikuwa haijaanza kulipwa mpaka sasa, licha ya Bunge kupitisha muswada huo Julai, mwaka huu. Rais Kikwete baadaye aliingilia kati kwa kuagiza mamlaka zote husika  kukutana mara moja kumaliza mvutano wa kodi hiyo kwa kutafuta vyanzo mbadala vya kodi ili kuziba pengo la Sh178 bilioni ambazo zingetokana na kodi kwenye laini za simu. Ni matarajio yetu kwamba Bunge letu litakuwa limepata somo la kutosha, hivyo litakuwa makini siku zijazo kwa kuhakikisha linapitisha miswada pasipo hila wala ushabiki wa kisiasa.

Wednesday, 18 December 2013

Wabunge waliokwepa safari watakiwa kurejesha posho

Dodoma.Sakata la wabunge waliochukua posho kwa ajili ya safari za mafunzo nje ya nchi na kuacha kusafiri, limeingia hatua mpya baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwataka wazirudishe.
Katika orodha ya wabunge wanaotajwa katika sakata hilo, wamo baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha NCCR-Mageuzi.
Sakata hilo liliibuliwa bungeni wiki iliyopita mjini Dodoma na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM) wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac).
Keissy alisema baadhi ya wabunge wanapaswa kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kuchukua posho za safari za nje ya nchi lakini hawakwenda safari hizo.
Mbunge huyo alifafanua kuwa mbali na kutokwenda kabisa safari hizo, lakini wapo ambao walikwenda na hawakukaa siku zote zilizopangwa.
“Tunawajua na wapo humu ndani,” alisema huku baadhi ya wabunge wakipaza sauti wakitaka awataje, lakini yeye akasema siyo jukumu lake kuwataja kwani Ofisi ya Bunge inawajibika kufanya hivyo.
Mbunge huyo alienda mbali na kudai mbunge mmoja alikatisha safari ya kwenda Marekani na kuamua kwenda Dubai kwa safari binafsi ambayo haikuwepo katika ratiba ya ziara hiyo ya mafunzo.
Habari za uhakika zilizopatikana jana zilisema wabunge wanane walichukua posho ya safari ya kati ya Sh5 milioni na Sh6 na Spika amewaandikia barua akiwataka warudishe fedha hizo.
Majina ya wabunge hao tunayo, lakini kwa sababu za maadili ya uandishi wa habari, gazeti hili halitaweza kuwataja kwa kuwa hawakupatikana ili kujibu tuhuma hizo kama maadili yanavyoelekeza.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake bungeni mjini Dodoma jana, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema kuwa Spika ameshaliona jambo hilo na kulichukulia hatua za kiutawala.
“Spika amewaandikia barua akiwataka kurejesha fedha zote za safari ambazo hawakwenda. Ni lazima wazirudishe hakuna namna,” alisema Joel ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge.
Alipoulizwa kuhusiana na majina yao na kiasi walichochukua, Joel alisema hilo ni jambo la kiutawala na kwamba Spika ndiyehuarifiwa na kamati kuhusiana na wabunge ambao hawakusafiri.
“Spika ndiye anayearifiwa na wenyeviti wa kamati husika juu ya wabunge waliosafiri na wasiosafiri kwa sababu wao ndiyo wanapanga safari na sisi tunawapa posho,” alisema.
Akizungumzia malalamiko ya wabunge juu ya baadhi ya wabunge wasiofika bungeni kusaini ili wapate posho ya kikao, Joel alisema tatizo hilo limepungua kwa kiasi kikubwa.
“Lilikuwepo lakini limepungua kwa kiasi kikubwa baada ya kugundua wakifika kwenye malipo majina yao waliosainiwa yamekatwa,” alisema Joel.
Alipoulizwa kuhusiana na tatizo hilo la kupokea posho za safari za nje ya nchi bila kwenda, Mnadhimu wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu alisema kuwa bado hajapata taarifa hizo.
“Lakini muhimu hapa ni Bunge kuandaa utaratibu wa kurejesha mrejesho wa jinsi walivyozitumia na hapo ndipo watagundulika wabunge wanaosafiri kweli na muda waliokaa mahali husika,” alisema Lissu.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) ambaye anatajwa kuwemo kwenye orodha ya wabunge waliopokea posho bila kusafiri, alikiri na tayari alishamuandikia barua Katibu wa Bunge akimueleza kwamba hakusafiri na kuomba utaratibu wa kurejesha fedha hizo.
Nasari alisema yeye alikuwa Jimboni kwake kwa shughuli za wananchi wake, hivyo hakuweza kusafiri na suala hilo alilifikisha mapema kwa Katibu ili ampe maelekezo namna ya kurejesha fedha hizo.