Wednesday, 23 October 2013

Elimu ya Tanzania iko mahututi’

Dar es Salaam. Siku moja baada ya maudhui ya Ripoti ya Tume iliyoundwa kuchunguza matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana kuwekwa wazi, wadau wa elimu wamekiri na kusema kuwa mfumo wa elimu ya Tanzania upo katika hali mbaya.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mbunge wa kuteuliwa na Rais, James Mbatia alisema matokeo ya tume hiyo yanaonyesha udhaifu wa hali ya juu katika sekta ya elimu jambo ambalo alishawahi kulisema katika hoja maalumu bungeni.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, alisema alishawahi kuishauri Serikali kuufumua mfumo wa elimu nchini na kuanza upya ili kunusuru taifa la kesho ambalo ndilo linaloathirika na rasilimali watu zisizo na ubora.
Matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana yalionyesha kuwa asilimia 60.6 ya wanafunzi Tanzania walipata alama sifuri na wanafunzi 23,520 sawa na asilimia tano ndiyo waliofaulu jambo ambalo lilisababisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuunda tume ya kuchunguza matokeo hayo.
Baadaye, mitihani hiyo ilisahihishwa upya na Pinda kukabidhiwa matokeo Juni, mwaka huu.
“Nilishasema katika hoja yangu bungeni Januari 31 na Februari 1, mwaka huu nikamwomba waziri anionyeshe mitaala ya elimu ya sasa, lakini hakuitoa,” alisema Mbatia.
Mbatia alisema ili taifa hili liondokane na janga la elimu lililopo halina budi kukubali kuwa ni kweli Tanzania ipo katika janga la elimu na kuunda dira ya elimu itakayotuongoza katika safari ya elimu nchini.
Mbatia aliongeza kuwa elimu ya Tanzania ipo mahututi na kuwa kila mwaka wanafunzi wanaomaliza katika shule mbalimbali hawana sifa za kutosha za kuweza kushindana katika masoko ya kimataifa.
“Tumeshaanza kuona taifa linaangamia kwa sababu ya ubovu wa elimu, ni lazima tukiri hilo kwa sababu hata Rais alikiri na kuikubali hoja yangu Aprili 30 mwaka huu alipokuwa mkoani Mbeya” alisema Mbatia
Mbunge huyu ambaye awali aliteuliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa tume ya uchunguzi wa matokeo haya na kukataa kushiriki alisema, ili Serikali iondokane na janga hili haina budi kuunda Kamati ya Bunge ambayo itaisimamia Serikali na kutoa mawazo mapana kuhusu elimu.
Mbatia alishauri Bunge lisiegemee itikadi za vyama au porojo za kutaka sifa za kisiasa na badala yake suala la elimu lijadiliwe kwa maslahi ya taifa.
Mdau mwingine wa elimu, Dk Method Samwel, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUSE), alisema tatizo la elimu hapa nchini lielekezwe zaidi kwenye mfumo uliopo kuliko laumu taasisi au mtu mmoja mmoja

Dk Samwel alisema tangu zamani mfumo wa elimu umekuwa ni wa kudorora na haya ni matokeo ya mfumo huo ambao haukuwa na misingi imara kwa muda mrefu.
Alitolea mfano wanaokwenda kusomea ualimu wengi ni wale waliofeli kwa kupata daraja la nne, jambo ambalo linasababisha wataalamu wa kada hiyo kuwa ni wale waliofeli pekee.
“Yapo mambo mengi yanayotakiwa kufanyiwa kazi katika sekta ya elimu Tanzania, suala la kudai kuwa Baraza la Mitihani na Taasisi kuwa ndizo taasisi zenye makosa, hazina ukweli,” alisema.
Hata hivyo, Dk Samwel alisema, tume hiyo bado ina maswali mengi ya kujibu kulingana na walichokisema katika sehemu ya ripoti yao.
“Nashindwa kuelewa kwa sababu kila nikisoma majibu ya tume hiyo napata maswali mengi zaidi. Kwa mfano, walimu waliofanya mtihani wakafeli walipewa muda wa kujiandaa? “ alihoji na kuongeza:
“Na kuhusu mitihani ya Tanzania kuonekana kuwa ni migumu zaidi, Je waliwapa mitihani ya Tanzania wanafunzi wa nchi nyingine au walitumia mbinu gani kupata matokeo hayo?”
Hata hivyo, Mkuu wa Kitivo cha Elimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo, alipinga ripoti ya tume hiyo na kusema kuwa wamepotosha taarifa kwani tatizo halikuwa katika mtihani bali ni wanafunzi wenyewe wamefeli.
Dk Mkumbo amesema tatizo si la walimu, wala baraza, wala mitihani yenyewe bali ukweli utabaki kuwa wanafunzi walifeli mtihani wa Kidato cha Nne kwa sababu ya mfumo mbovu wa elimu.
Mhadhiri huyo alihoji tena kuwa tume hiyo ilitumia njia gani kujua kuwa mtihani wa Sayansi ulihitaji saa sita kuufanya na ni kwa mbinu gani waliupima mtihani wa Tanzania na kujua kuwa ni mgumu kuliko mitihani mingine.
“Nilipata ripoti fulani iliyoonyesha kuwa mitihani ya Tanzania ni mizuri na haina matatizo, ripoti ilionyesha kuwa haina chembe ya mashaka na inatungwa kwa ustadi. Tusitafute sababu, tatizo si mitihani ni wanafunzi wenyewe wamefeli,” alisema.
Pia, Dk Mkumbo alisema kuwa ni dharau kubwa kusema kuwa baadhi ya wasahihishaji hawakuwa na sifa kwani hilo ni tusi kubwa kwa walimu kwani wao ndiyo wamekuwa wakisahihisha kila siku.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi nchini,(Tamongsco), Albert Katagira alisema si kweli kuwa mtihani ulikuwa mgumu bali tatizo lipo katika uandaaji wa wanafunzi.
 “Mtihani ulikuwan sahihi kabisa, mbona wanafunzi wengine walifaulu. Ni wanafunzi wenyewe, ambao nao hatuwezi kuwalaumu moja kwa moja,” alisema Katagira.
Alisema taifa bado lina tatizo katika mfumo wa elimu na kuweka mkazo katika masomo ya sayansi na hisabati ambayo yanaonekana kuwa magumu kwa wanafunzi wengi.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mafinga, Mustapha Mambea alisema, mtihani wa Fizikia na Kemia haikuwa migumu, lakini kuna mada kadhaa ambazo hawakufundishwa.
Profesa Mchome aongea
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alisema kuwa wameshindwa kuiweka hadharani ripoti hiyo kwa kuwa bado inafanyiwa kazi serikalini.
Profesa Mchome, ambaye ndio aliongoza tume hiyo, alisema kuwa ripoti hiyo inatakiwa kupelekwa kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kujadiliwa.
Alidokeza, hata hivyo, tayari walikuwa wameanza kufanyia kazi baadhi ya vitu vinavyotakiwa kufanyiwa kazi haraka kwenye ripoti hiyo.
Katibu Mkuu wa Necta, Dk Joyce Ndalichako, ambaye ameomba likizo ya muda mrefu ikitafsiriwa pengine ndio mwanzo wa utekelezaji wa ripoti hiyo.

Friday, 18 October 2013

Ubabe wa Dk Magufuli unaumiza uchumi wa nchi


Tumeshuhudia mvutano kati ya Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) ambao wanapinga sheria ya tozo ya asilimia tano kwa wasafirishaji wanaozidisha mizigo na kusababisha uharibifu wa barabara.
Mbali na Tatoa, Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) pia wanapinga sheria hiyo ya barabara namba 30 ya mwaka 1973 na marekebisho yake ya mwaka 2001.
Waziri Magufuli alisema anasimamia sheria hiyo ili kuhakikisha barabara haziharibiwi na watu wachache wenye nia ya kujinufaisha binafsi bila kujali masilahi ya Taifa.
Hata hivyo wamiliki hao kupitia Tatoa walisema Waziri huyo amerudisha tozo ya asilimia tano kwa maslahi yake na amekuwa mtu ambaye haambiliki, hashirikiani na wadau pamoja na kujichukulia sheria mkononi.
Wakizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam wamiliki hao walieleza kuwa sheria hiyo iliyotangazwa na Magufuli ilianza kutumika Oktoba Mosi na kupatiwa barua Oktoba 2, mwaka huu ya kueleza kwamba tozo hiyo imeondolewa jambo ambalo lilisababisha msongamano. Hata hivyo Waziri Mkuu, Mizengo Pinga aliumaliza mgogoro huo na kuruhusu wamiliki wa magari hayo kuendelea na safari zao kwa mwezi mmoja wakati jitihada nyingine zikiendelea.
Pinda alisema kutokana na sakata hilo, amelazimika kuunda kamati ambayo itakutana na wadau, Tatoa na Taboa ili kupata ufumbuzi wa mgogoro uliojitokeza. Athari zilizojitokeza ni pamoja na kusimama kwa upakuaji na upakiaji wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, kukwama kwa usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi na kukwamisha biashara na huduma za jamii kwa wananchi.
Kutokana na mvutano huo ni wazi kwamba usingekuwa na tija kwa Serikali wala Tatoa na Taboa, bali ungeleta maumivu makubwa kwa wananchi.
Pamoja na ushupavu wake Dk Magufuli katika kusimamia sheria, mimi naona wakati mwingine atumie pia busara, kwani wakati mwingine sheria pekee hazitatui matatizo.
Ni kweli kwamba Dk Magufuli anasimamia sheria halali, lakini ajue kwamba sheria hizo hutungwa na Bunge linalowawakilisha wananchi. Dk Magufuli akitoa tamko lake anasema wasafirishaji wengi nchini ni wanasiasa, kama wanaona kuondolewa kwa ofa ya uzito uliozidi wa asalimia tano wapeleke hoja bungeni ipitishwe rasmi.
Dk Magufuli akaendelea kusema kuwa, wanaogomea ni matajiri hivyo waende mahakamani.
Ubabe huu hauna tija yoyote, badala yake anashiriki kwa namna moja au nyingine kuhujumu uchumi wa nchi.
Nchi yetu inapaswa kuondoa vikwazo hivyo ili kuimarisha biashara za ndani na nje ya mipaka yake. Nchi yetu hii ina bandari ambayo inategemewa na nchi kama vile Zambia, Zimbabwe, Rwanda, Burundi, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Anachotakiwa kufanya Dk Magufuli ni kuimarisha utengenezaji wa barabara kwa kuongeza kiwango cha ubora ili magari yachukue uzito mkubwa zaidi

Kwa upande mwingine, Serikali ichukue changamoto hii kama nafasi ya kufufua Mashirika ya Reli ya TRC na Tazara badala ya kuachia tu malori yasafirishe mizigo. Wakati sasa umefika mizigo isafirishwe kwa reli ili kuepuka msongamano wa magari, uharibifu wa barabara na kuharakisha mizigo inafika kwa wateja kwa wakati.
Kazi ya Waziri Mkuu Pinda isiwe kusubiri migogoro tu, bali aisimamie Serikali ifufue njia mbadala za usafiri. Ni aibu kwa nchi yetu yenye zaidi ya miaka 50 ya uhuru, inashindwa kuendesha mashirika ya usafirishaji kwa mfano shirika la reli na ndege ambayo yaliyoachwa na wakoloni.

Mfumo wa kupanga alama kidato cha 4 na 6 kubadilishwa

Ikiwa yamebaki majuma machache wanafunzi wa kidato cha nne waanze mtihani wa wa taifa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iko kwenye mchakato wa kubadilisha mfumo wa upangaji za mitihani ya sekondari na matumizi wa alama za maendeleo ya mwanafunzi (Continuous Assessment (CA).
Mfumo huo ambao unatarajiwa kuanza kutumika kwenye Mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka huu, unakuja ikiwa ni miezi michache tangu Tume ya Waziri Mkuu iliyoundwa kuchunguza chanzo cha kufeli kwa maelfu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012.
Akizungumzia mchakato huo, Kamishna wa Elimu Profesa Eustella Bhalalusesa alisema kwamba hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni sehemu ya kuboresha elimu na kuwa haina uhusiano na taarifa ya tume iliyoundwa na Waziri Mkuu ambayo mpaka sasa haijawekwa hadharani.
“Mambo yanakwenda yanabadilika hata binadamu yeyote anabadilika kila siku, mfumo unaotumika sasa hivi ni wa siku nyingi,” alisema.
Alisema kuwa, ili kuweza kuboresha vyema mfumo huo wameshirikisha wadau mbalimbali zikiwamo shule za sekondari.
“Kama unataka kuboresha lazima upate maoni, lengo letu ni kushirikisha shule zote za sekondari za Tanzania, ila siwezi kukuhakikishia kama zote zitashiriki kwa kuwa tunawatumia zaidi maofisa elimu mkoa na wilaya. Tumeweka pia dodoso kwenye mdandao ili watu zaidi washiriki.
Kuhusu tume ya Pinda hapa haihusiki kabisa, ile ilikuwa na mambo yake, hata bila ile tume sisi hii tungefanya tu,” alisema Profesa Bhalalusesa.
Alisema kuwa, mpaka sasa wameshapokea zaidi ya asilimia 60 ya maoni hayo kutokana na lengo walilo jiwekea.
Dodoso hilo ambalo pia Mwananchi imefanikiwa kuliona, linasema kuwa serikali inakusanya maoni ya wadau wa elimu kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama (Grade Ranges) katika mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na cha sita pamoja na matumizi ya ‘Alama Endelevu ya Mwanafunzi [Continuous Assessment (CA)].
“Serikali imeamua kukusanya maoni haya kwa sababu kwa muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika katika mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na kidato cha sita havifanani pamoja na kwamba mitihani hiyo yote ni ya elimu ya sekondari.
Pia mfumo wa elimu ya sekondari umekuwa na miundo tofauti ikiwemo ule unaotumika shuleni na ule wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta),” sehemu ya dodoso inasema.
Dodoso hilo linafafanua kuwa, muundo wa kwanza ni ule wa shule ambao alama mgando (Fixed Grade Ranges) ambao alama zinazotumika kupanga madaraja: A = 81 – 100; B = 61 – 80; C = 41 – 60; D = 21 – 40 na F = 0 – 20.
Muundo wa pili ulioidhinishwa kutumiwa na Necta kuanzia mwaka 2012 ni Upangaji wa Alama Mgando usiobadilika (Fixed Grade Range).
Kwa kidato cha nne alama zilizotumika ni A = 80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49 na F = 0 – 34.
Kwa upande wa kidato cha sita alama zilizotumika ni A = 80 – 100; B = 75 - 79; C = 65 – 74; D = 55 – 64; E = 45 – 54; S = 40 – 44 na F = 0 – 39.
Kwa mujibu wa dodoso hilo, alama zinazopendekezwa ni A = 81 – 100, B = 61 – 80, C = 41 – 60, D = 21 – 40 naF = 0 - 20.

Wasomi watoa tahadhari majadiliano ya JK, wapinzani

Dar es Salaam. Wasomi wameonyesha wasiwasi wao juu ya mazungumzo kati ya Rais Jakaya Kikwete na vyama vya siasa vya upinzani vyenye wabunge, kuhusu tofauti zilizojitokeza katika Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Wasomi hao licha ya kuunga mkono mazungumzo, wamesema wanasiasa wana kawaida ya kuwa na agenda za siri jambo ambalo baadaye huzusha tena mzozo, huku wakirejea kwamba si mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kufanya mkutano wa aina hiyo.
Kauli hizo zimetokana na Rais Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya siasa; CCM, Chadema, CUF, NCCR Mageuzi, TLP na UDP kukubaliana kuweka pembeni tofauti za kiitikadi na kutanguliza masilahi ya taifa katika mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya.
Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Azavery Lwaitama alisema uamuzi wa Rais Kikwete ni mzuri lakini unaweza ukawa umechezwa kwa karata ya kisiasa.
Alifafanua, “Inaweza kuwa karata ya kisiasa kwa sababu bado Bunge lina wabunge wengi wa CCM, pia marekebisho yatasimamiwa na Waziri wa Katiba na Sheria, (Mathias Chikawe) sijui kutakuwa na jipya gani.”
Lwaitama alisema ili mambo yaende sawa, Rais Kikwete anatakiwa kuhakikisha kuwa marekebisho hayo yatakayofanywa nje ya Bunge, hayabadilishwi tena bungeni. “Ahakikishe kuwa wabunge wanapitisha tu yale ambayo yamerekebishwa nje ya Bunge.”
Naye Profesa Gaudence Mpangala wa UDSM alisema: “Tutajua kama hili jambo limetulia ama la, kama Bunge likipitisha mapendekezo mapya, kama ikiwa hivyo mambo yatakwenda vizuri.”
Hata hivyo, Profesa Mpangala alionyesha wasiwasi wake kama wabunge wataamua kuyapinga mabadiliko hayo, huku akishauri itumike njia ambayo itawafanya wabunge kukubaliana na kile kilichojadiliwa nje ya Bunge.
Alisema Katiba nzuri ni lazima itokane na mwafaka wa pamoja na kwamba nia ya Rais Kikwete inapaswa kuendelezwa hadi bungeni.
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Bashiru Ally alisema: “Siku zote mtu asiyejua anapokwenda hawezi kupotea njia, mchakato wa Katiba Mpya una mgongano wa mtazamo kuna maswali mengi kuhusu mchakato huu kuwa wa kisiasa na kisheria.
Alisema kuwa mchakato huo sasa haujulikani unaendeshwa kwa masilahi ya nani, kwa sababu kila malalamiko mengi yanayotolewa yamebebwa na vyama vya siasa.
“Tupo njiapanda, binafsi sina imani kubwa na mchakato huu, vyama vimeweka masilahi yao zaidi mbele,” alisema Bashiru.
Aliyekuwa Mbunge wa Monduli na Mkuu wa wilaya, Lepilal Ole Moloimet alisema mtindo wa Rais Kikwete wa kuzungumza na wapinzani ni mzuri kwa sababu unasaidia kuweka mazingira ya utulivu na maelewano nchini.
Alisema utaratibu huo ni mzuri katika kuondoa manung’uniko, hasa kwa wale ambao hawaridhiki na hali halisi ya mambo yanavyokwenda nchini.
Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema atakuwa kwenye mazingira mazuri ya kuchambua mpango wa Rais Kikwete kukutana na vyama vya upinzani, pindi mchakato ukikamilika.
“Bado ni mapema sana. Mazungumzo bado hayajamalizika. Tusubiri yamalizike ndipo nitakapokuwa na nafasi nzuri ya kuyazungumzia,” alisema Nape.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Ntatiro alisema kwamba wanatarajia kutoa taarifa kuhusu mazungumzo hayo na Rais Kikwete.
Alisema mpaka sasa chama hicho bado hakina uhakika kama kweli kilichoandikwa kwenye vyombo vya habari jana ndicho kilichoafikiwa kwenye mazungumzo hayo.
Kwa upande wake Chadema kupitia kwa Ofisa wake wa Habari, Tumaini Makene nao walisema watatoa taarifa yao baadaye.
Makubaliano ya mkutano
Taarifa ya Ikulu juzi, ilisema Rais Kikwete na viongozi hao walikubaliana vyama vyote vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha sheria hiyo, viwasilishe mapendekezo yao haraka serikalini ili itafutwe namna ya kuyashirikisha katika marekebisho ya sheria hiyo.
Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni Wenyeviti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Chadema, Freeman Mbowe, NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.
Katika hoja zao, wapinzani wanataka kuangaliwa upya kwa idadi ya wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba, utaratibu wa
kupitisha Katiba Mpya kwenye Bunge Maalumu wakisisitiza kwamba kuwapo haki sawa kwa kila upande wa Muungano
Hoja nyingine ni ukomo wa Tume ya Mabaraza ya Katiba ambapo viongozi hao walipendekeza kwa rais kuwa tume iendelee kuwapo hadi Katiba Mpya itakapopatikana badala ya kuvunjwa mapema kabla ya Katiba Mpya.
Hoja nyingine kuingizwa kwa mambo ambayo hayakujadiliwa wala kupitishwa na Bunge kwenye muswada huo, wakitoa mfano wa
kifungu kipya kinachompa Katibu wa Bunge na yule wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, mamlaka ya kusimamia mchakato wa kumchagua mwenyekiti wa muda wa Bunge.
Walisema pendekezo hilo ni jipya na kwamba halikuwepo kwenye muswada uliotolewa maoni na wadau.

Kesi ya Pinda kuunguruma leo

Dar es Salaam. Kesi ya Kikatiba inayomkabili Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), inaanza kuunguruma leo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilifunguliwa kwa ushirikiano wa Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Katika kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013, LHRC na TLS, wanadai kuwa Pinda alivunja katiba kwa kauli aliyoitoa Bungeni kuhusu polisi kuwapiga raia wanaokaidi amri.
Walalamikaji hao wanadai kuwa kauli hiyo ni amri kwa vyombo vya dola kutekeleza sheria ya kuwapiga wananchi, wakati wa vurugu.
Hata hivyo Pinda na AG katika majibu yao, wamewasilisha pingamizi la awaliambalo pamoja na mambo mengine wanadai kuwa walalamikaji na watu waliorodheshwa katika kesi hiyo, hawana mamlaka kisheria kufungua kesi hiyo.
Pingamizi hilo limepangwa kusikilizwa leo na jopo la majaji linaloongozwa na Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu.

Wednesday, 16 October 2013

Zitto asimamisha ruzuku za mwezi kwa vyama vya siasa

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac),Zitto Kabwe amevilipua vyama vya siasa kwa uvunjaji wa sheria na kusimamisha ruzuku ya kila mwezi hadi vitakapowasilisha taarifa za ukaguzi wa fedha za umma tangu mwaka 2009 kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Pia kamati hiyo itawaweka kitimoto makatibu wakuu wa vyama vya siasa vinavyopata ruzuku ili wajieleze ni kwa nini hawajawasilisha taarifa hiyo hadi sasa.
Alisema hayo jana wakati kamati hiyo ilipokutana na Msajili wa Vyama vya Siasa katika Ofisi ndogo za Bunge.
Zitto alisema tangu mwaka 2009 vyama tisa vya siasa vinavyopewa ruzuku na Serikali vilipata jumla ya Sh67.7 bilioni lakini havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa ruzuku kwa msajili kama vinavyopaswa kufanya hivyo kisheria.
“Ninaagiza msajili kuanzia sasa ruzuku isitolewe kwa chama chochote cha siasa hadi hapo kitakapowasilisha ripoti ya ukaguzi wa hesabu tangu mwaka 2009 hadi sasa na makatibu wataitwa ili wajieleze kwa nini hawajafanya hivyo,” alisema.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye alipoulizwa jana alisema: “Ninahitaji muda kuangalia kama kweli taarifa hiyo haijawasilishwa na sheria inasemaje kuhusu suala hilo,” alisema.
Alisema baada ya siku mbili za kazi atakuwa na majibu ya kuridhisha kuhusiana na suala hilo.
Viongozi wengine wa vyama vya siasa vinavyopata ruzuku, hawakupatikana kuelezea hali hiyo. Zitto aliongeza,“ Hivi ni vyama vya siasa ambavyo wakati ukifika vinaweza kuja kuongoza Serikali, lakini inashangaza ni kwa nini vinatumia fedha za walipakodi bila kukaguliwa, huu ni uvunjaji wa sheria.”
Kwa mujibu wa Zitto, vyama hivyo na fedha za ruzuku walizopata kwenye mabano tangu mwaka 2009 ni CCM (Sh50.9 bilioni), Chadema (Sh9.2 bilioni) na CUF (Sh 6 bilioni).
Vingine ni NCCR-Mageuzi(Sh677 milioni),UDP (Sh333 milioni), TLP (Sh217 milioni), APPT-Maendeleo (Sh217 milioni), DP (Sh3.3 milioni) na Chausta (Sh2.2 milioni).
Zitto alisema ingawa jukumu la ukaguzi wa fedha za umma ni la ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali lakini hakufanya hivyo kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.
Alisema vyama vya siasa viliagizwa kufanya ukaguzi kwa kutumia kampuni binafsi kama vilivyokuwa vikifanya zamani hadi hapo ofisi ya CAG itakapopata fedha.
Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa msajili kuviagiza vyama vya siasa kutenga sehemu ya fedha za ruzuku kwa ajili ya ukaguzi.
Alisema viongozi hao waone kwamba suala la ukaguzi wa fedha za ruzuku ni muhimu ili kuleta uwazi katika matumizi ya fedha za umma.
“Sasa kamati imeshindwa kuendelea na kazi kwa sababu hakuna hesabu zilizokaguliwa, nendeni tutawaita siku nyingine,” alisema.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alisema vyama hivyo vimekuwa vikidai kwamba havina ruzuku ya kufanya ukaguzi kwa kutumia kampuni binafsi.
“Kwa hiyo siwezi kuchukua fedha nikavipa vyama vya siasa kwaajili ya ukaguzi wakati hazijatengwa katika bajeti,” alisema.
Hata hivyo,Zitto alimwelekeza Mutungi kwamba fedha za ukaguzi ziko kwenye ruzuku wanazopewa na kwamba hiyo siyo sababu ya kuhalalishwa kutokaguliwa kwa hesabu zao.

Tuesday, 15 October 2013

Kisumo: CCM inaweza kung’oka madarakani

Dar es Salaam. Mwanasiasa na kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Kisumo ameonya kuwa chama hicho kinaweza kuondolewa madarakani kutokana na kunyamazia vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma vinavyotokea nchini.
Mzee Kisumo alitoa onyo hilo wiki iliyopita katika mazungumzo maalumu aliyofanya na Mwananchi nyumbani kwake Dar es Salaam kuhusu kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere inayoadhimishwa leo.
Alisema tatizo kubwa la chama hicho ni kwamba kimemeendelea kuwa chama dola kikikaa mbali na wananchi, huku kikishindwa kuidhibiti rushwa na kuwajibisha wahusika wa vitendo hivyo.
“Chama kimebaki kuwa cha walalamikaji, kila mtu amekuwa mlalamikaji. Hata Waziri Mkuu amegeuka mlalamikaji. Sijaona watu wanaowajibishwa kwa ufisadi,” alisema Kisumo na kuongeza:
“CCM haiwezi kujivunia ufisadi unaoonekana nchini. Siwezi kusema imeukumbatia, lakini nasema imekuwa CCM bubu, hata kuukemea ufisadi haiwezi. Utamaduni huu enzi za Mwalimu Nyerere haukuwapo.”
Alisema kutokana na udhaifu huo wa CCM, kuna uwezekano mkubwa wa chama cha upinzani, na hasa Chadema kutumia mwanya huo kuwashawishi wananchi na kushinda uchaguzi.
Kisumo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa CCM, alisema ingawa Chadema haijaonyesha wazi mambo kinayoyapigania, kinaweza kutumia agenda ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma kuwavutia wananchi na kuchaguliwa.
Alitoa mfano wa tuhuma za baadhi ya viongozi wa Serikali kuficha mabilioni ya shilingi kwenye benki za Uswisi, kuwa zinaweza kuwa kete muhimu ya kuwaingiza Chadema madarakani, iwapo Serikali ya sasa haitawashughulikia wahusika.
“Wakijitokeza na kuwataja majina wahusika, wakasema fulani na fulani ndiyo wenye mabilioni haya Uswisi, na Serikali ikasita kuwachukilia hatua, wakasema tukiingia madarakani tutawakamata, wananchi wanaweza kuwaamini na kuwachagua,” alisema na kuongeza: “Wakishinda uchaguzi hata kwa viti vichache tu, watakosa nguvu bungeni, lakini kwa wananchi watakuwa na nguvu sana.
Hii inaweza kuwasaidia kwa miaka mitano ya kwanza. Wanaweza kupata ushindi mkubwa zaidi kwa mara ya pili na wakiingia madarakani watawafunga viongozi wa zamani kweli.”
Mzee Kisumo anasistiza, “Hili linawezekana. Anayesema uwezekano wa CCM kushindwa haupo, anajikana mwenyewe. CCM inabidi ijihami na majibu ya jinsi inavyotumia rasilimali za nchi.”
Alionya kuwa si vizuri kuishia kujinadi kwa mambo mengi mazuri iliyofanya huko nyuma, akitolea mfano kuwa hiyo ni sawa na nguo nyeupe ambao ikiingia doa moja tu inakuwa haitamaniki tena.

“Sisemi kwamba hawajafanya kitu, yapo mengi mazuri waliyoyafanya, lakini ufisadi ni sawa na doa kwenye shati jeupe ambalo huwa linaonekana kuliko weupe na ung’avu wa shati hilo,”alisema Kisumo.
Alisema katika siku za karibuni ufisadi umekuwa jambo la kawaida, hadi umegeuzwa kuwa wa kitaasisi, ambapo aligusia hata Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ulioanzishwa na Bunge kuwa ni sehemu ya ufisadi.
Alihoji iweje fedha za umma zitumike kumsadia mtu mmoja kujiimarisha kisiasa, akisema hiyo ni ‘Built in Corruption’.
Mzee Kisumo pia alizungumzia mvutano ambao umekuwa ukijitokeza kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwamba msingi wa mvutano huo ni kuwapo tabaka la wahalifu wasioweza kuguswa na sheria.
“Unapokuwa na mvutano huo una maana mbili, kwanza ni hali kwamba huyo mmoja anajua sabababu za watuhumiwa kutochukuliwa hatua, lakini pili ni kwamba huenda tuna watu wawili katika nafasi hizi, lakini wana nia mbili tofauti,”alisema Kisumo na kuongeza:
“Ni hatari sana unapokuwa na mfumo kwenye nchi ambao unawalinda baadhi ya wahalifu, unakuwa na wahalifu wanaoguswa na wengine hawaguswi, watu wanasubiri pengine itokee siku waone mtu wasiyemtarajia anafikishwa mahakamani na hapo watajua kwamba kweli nchi imeamua kupambana na rushwa na ufisadi.”
…Aonya Zanzibar
Mzee Kisumo pia alizungumzia mchakato wa mabadiliko ya Katiba Mpya na kwamba mvutano kuhusu muundo wa Muungano ni matokeo ya upande wa Zanzibar kuachiwa kufanya vitendo vingi vinavyoashiria kutafuta uhuru kamili kama nchi nje ya Muungano huo.
Vitendo hivyo kwa mujibu wa kada huyo ni mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar ambayo yalitamka kuwa Zanzibar ni nchi, kurejesha bendera yake, wimbo wake wa taifa na mambo mengine.
“Katika hatua sasa Zanzibar wanajiona kwamba wamekaribia kutimiza azma yao, kuelekea katika ‘uhuru’ kamili, nasema whoever (yeyote) aliyefumbia macho vitendo hivi akiwa Rais, alifanya makosa makubwa,”alisema Mzee Kisumo na kuongeza:
“Ukitafakari hali hiyo, kama tukiwa na mfumo wa Serikali Tatu, ni kitu gani kitawazuia Tanganyika nao wasidai kuwa na Katiba sawa na ile ya upande wa pili? Ikifika hapo mimi sioni Muungano kuwapo.”
Hata hivyo, alionya kuwa masuala yote yanayohusu Muungano ikiwa ni pamoja na lile la mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar, yanapaswa kufanyiwa uamuzi wa busara kwani historia inaonyesha kuwa kuvunja Muungano wowote ule lazima damu imwagike.

“Muungano wa States (nchi) za Marekani uligharimu umwagaji damu, United Kingdom (Uingereza) pia damu ilimwagika, kwa hiyo lazima tujifunze kwamba ikiwa tutafikia hatua ya kuvunja Muungano wetu, hatuwezi kupita salama katika hili,” alisema.
Alisema kinachotokea sasa kuhusu Zanzibar kuwa na mwelekeo wa kujitenga, ilianza katika chaguzi zilizopita, pale ambapo Mzanzibari aliyekaa nje ya visiwa hivyo kwa zaidi ya miaka mitano anakosa haki ya kupiga kura kwa kukosa sifa ya ukaazi.
“Hili nalo ni tatizo kubwa, Mzanzibari ambaye ameamua kuishi Moshi, Morogoro au kwingineko nchini uhalali wake wa kuwa Mzanzibari unawekwa shakani, kwani hawezi kupiga kura kama hajaishi Zanzibar mfululizo kwa kipindi hicho,” alisema Mzee Kisumo na kuongeza:
“Ukiangalia kwa Mtanzania wa Bara, hakutani na kadhia hii, yeye ataishi popote hata kama nje ya nchi kwa muda wowote, lakini akirudi nyumbani haambiwi eti si mkaazi, kama ni Tabora atakwenda kwao au Mbeya”.
Mzee Kisumo alisema kutokana na hali hiyo kuna kundi kubwa la Wazanzibari ambalo linajikuta katika hatari ya kukosa haki zao na kwamba ikiwa kutakuwa na mfumo wa Serikali Tatu na upande wa Tanzania Bara kuanzisha utaratibu kama wa Zanzibar, watajikuta kwenye utata wa uraia wao.
“Tukiwa na Tanzania moja iliyoungana, ambayo watu wake hawana mwelekeo wa kuangalia masilahi yao zaidi, haya mambo hayawezi kutokea. Kimsingi mtu yeyote ambaye ni raia wa Tanzania anapaswa kujivunia uraia wake kama Mtanzania na hapaswi kuishi kwa vikwazo vya aina hii,”alisema Kisumo na kuongeza:
“Kwa hiyo mimi nasema haya mambo lazima… Lazima tuyatizame kwa upana wake….Maana hawa watu wapo wanaathirika, sihitaji kutaja majina ya watu hapa, lakini wapo, wanafahamika na wengine ni wafanyabiashara wakubwa sana nchini, wametoka Zanzibar na wameishi Tanzania Bara kwa miaka mingi.”
Kisumo alionekana kukerwa zaidi na pendekezo la kuwapo kwa Serikali ya mkataba na kusisitiza kuwa wanaotoa mawazo ya aina hiyo wanakusudia kuvunja Muungano kwa masilahi yao binafsi.
... Asema Nyerere alijaa katika mioyo ya Watanzania
Wakati taifa leo linatimiza miaka 14 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Kisumo anasema kuwa kiongozi hiyo alikuwa na sifa nyingi ambazo zilimfanya kujaa mioyoni mwa wa Watanzania.
Akizungumzia sifa za Nyerere kabla na baada ya uhuru wa Tanganyika iliyokuja kuwa Tanzania baadaye , Kisumo anaeleza kiongozi huyo alikuwa na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yake na Bara la Afrika kwa jumla.
Kisumo, ambaye alifanya kazi na kiongozi huyo kabla na baada ya uhuru, alisema sifa nyingine ya Mwalimu Nyerere ilikuwa uwezo wake wa kushawishi na kuongoza.

“Nyerere pia aliamini katika umoja wa taifa na uongozi wa pamoja na ndio maana alifanikiwa katika nyanja nyingi,” anasimulia Kisumo, ambaye alianza siasa kupitia kwenye vyama vya wafanyakazi akiwa na Waziri Mkuu wa zamani, Rashid Kawawa na Marehemu Michael Kamaliza katika miaka ya 1950.
Kisumo anasema bila ya kificho kuwa marais waliomfuatia Nyerere wameshindwa kufikia sifa ya Mwalimu hasa linapokuja suala zima la sifa za uongozi.
Alitoa mfano kitendo cha Nyerere kwa kutumia lugha ya Kiswahili na kuunganisha watu wa Tanganyika kupigania uhuru bila ya kumwaga damu kutoka kwa Waingereza.
“Alipigania uhuru bila ya kuwa na jeshi au silaha unaweza mwenyewe ukamfikiria mwenyewe Mwalimu alikuwa ni kiongozi wa aina gani?
“Nyerere aliunganisha machifu waliokuwa na nguvu sana katika kipindi kile ingawa alipingwa na baadhi yao kama Chifu Thomas Marealle wa Moshi.
“Huyu Chifu Marealle alikwenda mbali zaidi na hata kwenda kwenye Umoja wa Mataifa nchini Marekani na kueleza kuwa Tanganyika haikuwa tayari kujitawala, lakini alishindwa kwa hoja za Mwalimu,” aliongeza Kisumo, ambaye alishika nyadhifa mbalimbali wakati wa uongozi wa Nyerere zikiwamo za Uwaziri na Ukuu wa Mkoa.
Kisumo anaeleza kuwa Mwalimu aliwazidi kete Waingereza kwani alipenya katika asasi mbalimbali za Watanganyika.
“Mwalimu alitumia michezo kudai uhuru, alikuwa karibu sana na klabu ya Yanga pia hata vikundi vya muziki wa dansi na taarabu,” aliongeza Kisumo.
Kisumo anasimulia kuwa baada ya Tanganyika kupata uhuru bado Nyerere alisaidia mataifa mengine katika harakati zao za kupigania uhuru wao na alitaka Umoja wa Afrika na ndio maana akaasisi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.
Ukombozi wa Afrika
Alisema Nyerere alikubali Kamati ya Ukombozi ya iliyokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) iweke makao makuu yake jijini Dar es Salaam.
“Kilikuwa kitendo cha hatari kwani mataifa mengi wakati ule hayakukubali kupokea wapigania uhuru kwa kuhofia usalama wa nchi zao.

“Vyama mbalimbali kutoka nchi za Afrika Kusini, Angola, Msumbiji na Namibia vilileta watu wao kwa mafunzo ya kijeshi, jambo ambalo lilitutisha wakati ule,” anaongeza Kisumo.
Kisumo alisimulia kuwa Nyerere alisimamia umoja na ukombozi wa Bara la Afrika na kumfanya ajizolee sifa sawa na marais wengine kama Gamal Abdel Nasser wa Misri, Ben Bella wa Algeria na Kwame Nkrumah wa Ghana.
Kisumo alisema kuwa Mwalimu hakuishia kuunga mkono wapigania uhuru wa Afrika pia aliunga mkono harakati za Wapalestina kujikomboa kutoka kwa Israel, ambayo katika miaka ya mwanzo wa Uhuru ilikuwa kati ya wafadhili wakubwa wa Tanzania.
“Nakumbuka Kiongozi wa Chama cha Ukombozi cha Palestina (PLO), Yasser Arafat alialikwa katika moja ya mikutano ya chama cha TANU iliyofanyika jijini Dar es Salaam,” anaongeza Kisumo.
Sera za uchumi
Kisumo anasema kuwa Nyerere alikuwa anaamini kuwa Tanzania itaendelea kiuchumi kama itawekeza vya kutosha katika kilimo.
“Ndio maana katika miaka ya mwanzo baada ya uhuru tulikuwa na sera ya `Siasa ni Kilimo’ na baadaye `Kilimo cha Kufa na Kupona’,” alisema Kisumo.
Kisumo alisema kuwa baada ya kampeni ya kilimo, Nyerere aliona umuhimu wa kujenga viwanda ili kutumia malighafi iliyotoka katika kilimo.
“Ndio maana ukaona tukajenga viwanda vya nguo katika Miji ya Dar es Salaam, Arusha, Musoma na Mwanza pia kiwanda cha nyuzi pale Tabora,” alisema.
Pia Kisumo alisema kuwa Mwalimu aliweka mkazo katika elimu ya kujitegemea ili kumwandaa kijana wa Kitanzania.
“Hivi majuzi nilisikitika sana baada ya kusikia ikiwa shule moja huko Kigoma imepokea msaada wa vyoo vya shimo kutoka kwa Wachina! Hivi kweli imefika mahali wanafunzi wetu wanashindwa kuchimba vyoo?” alihoji Kisumo kwa masikitiko.
Kisumo alisema kuwa mambo yalibadilika katika miaka ya 1990 wakati Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Margareth Thatcher alipoanzisha sera za ubinafsishaji na utandawazi.
“Hapo ndio yakabadilika ambapo mataifa makubwa yakazidi kuzikandamizia nchi changa kupitia misaada ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF),” alisema Kisumo.
Kisumo alisema Mwalimu alipambana na mataifa hayo makubwa na kutaka kuacha kukandamiza nchi changa. Alipambana na mataifa kupitia Tume ya Kusini 1986, taasisi ambayo ilitokana na uliokuwa Umoja wa Nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM).

Zitto sasa aanika mshahara wa Rais

Igunga. Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe amesema sababu ya kutaja mishahara ya viongozi wakuu wa nchi ni kuzuia mianya ya watu wachache kuiibia nchi kutokana na usiri wa jambo hilo.
Zitto alitoa kauli hiyo jana mjini Igunga, wakati akitangaza mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mujibu wa Zitto, kwa mwaka kiongozi huyo wa nchi analipwa Sh384 milioni ambazo ni wastani wa Sh32 milioni kwa mwezi bila kukatwa kodi.
Hatua ya Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC), kutaja mshahara wa rais inakuja wiki moja baada ya kutaja mshahara wa Waziri mkuu kuwa ni Sh26 milioni kwa mwezi pasipo kukatwa kodi
Zitto alisema hoja ya msingi si kiasi wanancholipwa viongozi hao walioajiriwa na wananchi bali ni usiri unaofanywa juu ya kiwango hicho. Alisemaha ni jambo la kusikitisha kuona mwalimu anayelipwa mshahara wa Sh200,000 kwa mwezi ukikatwa kodi huku viongozi wa kuchaguliwa wakiwa wanapokea mishahara mikubwa pasipo kukatwa kodi.
Alisema katiba ya sasa Ibara ya 43(1), inaeleza kuwa rais atalipwa mshahara na malipo mengine huku ibara hiyo hiyo kifungu cha pili ikizuia mshahara na marupu rupu kupunguzwa, hali aliyoelezea kuwa ni muhimu katiba mpya ikabadilisha sheria hizo kwa manufaa ya nchi.
“Kwa hiyo hata kesho kama Dk Slaa akiwa Rais na akataka kupunguza mshahara wake kwa katiba hii hawezi na hili jambo si sahihi kwani viongozi wa ngazi hizi wanapata kila kitu bure kutoka Serikalini,” alisema Zitto.
Zitto alisema kuwa kitendo cha Serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania, hakikuzingatiwa kulingana na uwazi uliowekwa kwa kuandika uwazi wa viwango vya mishahara.
Alisema kuwa waziri aliyehusika kufunguia magazeti hayo hakufikiria kwa makini kutokana na kuwa na uelewa mdogo na kuongeza kuwa hakuna kosa lolote linalopelekea kufungiwa magazeti hayo kutokana na ukweli ulioandikwa

Kikwete: Tumeshinda maadui zetu

Dar/Iringa. Rais Jakaya Kikwete amesema maadui wote ambao walitaka kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi wamedhibitiwa .
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake itaendelea kulinda amani ya nchi na maadui wote wanaohusika na kutaka kuvuruga nchi watachukuliwa hatua kali za kisheria. “Kulikuwapo na upepo mbaya, lakini kwa sasa Tanzania ni shwari na tumemshinda adui,” alisema Rais Kikwete jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere yaliyoandamana na sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru, mkoani Iringa.
Alisema katika siku za hivi karibuni, maadui wasioitakia mema Tanzania walikuwa na mkakati wa kuvuruga amani ya nchi, lakini Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dola vimewadhibiti na nchi iko salama.
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa amani kwa sababu inajua wazi kwamba nchi ikiingia kwenye mgawanyiko, mshikamano utavurugika na shughuli za maendeleo zitasimama.
Katiba Mpya
Rais Kikwete alisema mwaka 2014 ni mwaka wa kipekee kwa nchi kwa kuwa utakuwa na mambo makubwa matatu yatakayofanywa.
Rais Kikwete alisisitiza kwamba Katiba Mpya ni lazima ikamilike mwakani kama mambo yatakwenda kama ilivyopangwa.
Vilevile, alisema mwakani Tanzania itasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa udhalimu na kuwarudishia Wazanzibari heshima ya mwanadamu na utu wake.
“Pia tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wetu. Nawaomba Watanzania wajiandae kuyafanikisha vizuri mambo hayo ili historia mpya ifunguliwe nchini.
“Wazanzibari waanze miaka mingine baada ya miaka hamsini ya uhuru wao, muungano uanze miaka mingine baada ya miaka hamsini na Katiba Mpya itupeleke miaka mingine tukiwa wamoja,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete alionya kuwa asingependa mchakato wa kupata Katiba Mpya uligawe taifa na kuleta mfarakano utakaovunja umoja wa kitaifa badala ya kuuimarisha.
“Tunataka tuwe na Katiba itakayojenga, siyo kubomoa, kutugawa kwa misingi ya kiitikadi,” alionya Rais Kikwete.

Alisema kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa kwa mwaka huu ni kusisitiza mshikamano wa kitaifa unaopinga mbinu zozote za kuligawa taifa. “Kaulimbiu ya mwaka huu; Tanzania ni wamoja, tusigawanywe kwa misingi ya tofauti zetu za dini, itikadi, rangi au rasilimali,” alisema Rais Kikwete.
Alisisitiza kuwa amekusudia mabadiliko ya Katiba ambayo mchakato wake unaendelea yawe ya kulipeleka mbele taifa kimaendeleo kwa zaidi ya miaka 50 ijayo.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alisema atapendelea kuona Katiba Mpya inazinduliwa Aprili 13, mwakani, siku ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa Baba wa Taifa.
Alisema kitendo hicho kitaienzi zaidi siku hiyo na kuandamana na mpango wa kubadilisha maadhimisho ya kitaifa ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere kutoka Oktoba 14 siku aliyofariki na kuwa Aprili 13, siku aliyozaliwa.
..ataka kuvuruga Mwenge
Maadhimisho ya Mwenge nusura yaingie dosari baada ya mwanamume kujichomeka katika kundi la wanahabari akiwa na lengo la kumdhuru kiongozi wa Mbio za Mwenge.
Kitendo hicho kilifanyika wakati Rais Kikwete akiwa tayari ameshuka chini katika jukwaa dogo akisubiri kukabidhiwa mwenge huo, mtu huyo alichomoka kutoka katika kundi la waandishi wa habari na kujaribu kumvamia kiongozi wa Mbio za Mwenge, Juma Ali Sima aliyekuwa ameshikilia Mwenge huo.
Hata hivyo, jitihada za mtu huyo za kutaka kumvamia kiongozi wa Mwenge zilikwama baada ya kudhibitiwa vikali na askari waliokuwa wakilinda amani uwanjani hapo.
Katika kipindi hicho, Rais Kikwete pamoja na wasaidizi wake wengine walikuwa mita kama tisa kutoka katika eneo la tukio akisubiri kukabidhiwa Mwenge huo.
Rais Kikwete alisema kilele cha maadhimisho ya Mbio za Mwenge kimefanywa kuwa pia siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere tangu afariki miaka 14 iliyopita.
Alisema Watanzania wote bila kujali vyama vyao wana wajibu wa kuyakumbuka mema yote ya Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni pamoja na mafundisho yake.
Rais pia alisema ili kumkumbuka zaidi Mwalimu Nyerere alipendekeza siku yake ya kuzaliwa ndiyo iitwe Nyerere Day na ianze kusherehekewa kwa mbwembwe, iwe na mijadala ya kazi zake na itumiwe kufanya shughuli mbalimbali za kujenga taifa kwa lengo la kumuenzi.
Kuhusu dawa za kulevya
Katika maadhimisho hayo, Rais Kikwete alizungumzia mkakati wa Serikali yake wa kupambana na dawa za kulevya kwamba kitaanzishwa chombo maalumu kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema kazi ya kupambana na dawa za kulevya ni ngumu na hatari kutokana na wanaofanya kazi hiyo kuwa na fedha nyingi, lakini Serikali itawalinda wote

Friday, 11 October 2013

Museveni, Dk Besigye wakutana ana kwa ana

Kampala. Wapinzani wawili wa kisiasa, Rais Yoweri Museveni na mpinzani wake mkuu, Dk Kizza Besigye wamekutana ana kwa ana kwenye sherehe za Uhuru huko Rukungiri, siku moja baada ya Rais Museveni kumrushia vijembe Besigye.
Wawili hao wanakutana baada ya Museveni kumtaka Besigye na Meya wa Jiji la Kampala, Erias Lukwago kuacha kuchochea machafuko kwenye mji huo kwa nia ya kutaka kuiingiza nchi hiyo kwenye vurugu kama ilivyo Misri kwa sasa.
Pia aliwataka kuacha kuingia katika mapambano ambayo hayana faida kwao kwa kuwa mara zote wamekuwa wakishindwa hivyo ni vyema wakirejea kwenye chama tawala, ambako watapokelewa kwa heshima.
Maoni hayo yaliibua mvutano wa maeneo kutoka kwa Dk Besigye ambaye amewahi kuwa daktari wa Museveni ambapo alikaririwa na gazeti la Daily Monitor akihoji “Niombe samahani kwa lipi? Yeye amejifanya kuwa jaji na hilo ndilo tunapambania,” alisema.
Katika maadhimisho ya leo, dhima kuu ni ‘Kuimarisha fursa za uwekezaji’ ambapo Rais Museveni ndiye mgeni rasmi na Dk Besigye akihudhuria kwa mwaliko rasmi wa Ikulu.