Monday, 29 July 2013

Tume ya Uchaguzi itasababisha vurugu

Uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata nne za Jimbo la Arusha Mjini ulifanyika juzi, ambapo Chadema kiliibuka mshindi katika kata zote nne za Themi, Kimandolu, Elerai na Kaloleni.
Kata hizo zilikuwa wazi tangu mwaka 2011 baada ya madiwani wake kutimuliwa uanachama na chama hicho kwa kwenda kinyume na msimamo wa chama chao kuhusu kutomtambua Meya wa Jiji la Arusha.
Kinyume na matarajio ya wengi, uchaguzi huo ulikuwa na idadi ndogo sana ya wapigakura kulinganisha na chaguzi zilizopita, kwani kati ya wapigakura zaidi ya 60,000 waliojiandikisha ni 11,042 tu waliojitokeza kupiga kura.
Kwa mfano, Kata ya Elerai inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wapigakura 23,885 lakini waliojitokeza kupiga kura juzi ni 3,824 tu.
Takwimu hizo zinaibua maswali magumu, hasa kuhusu hali inayoendelea kujitokeza ya kudidimia kwa demokrasia nchini.
Takwimu hizo zinatoa tahadhari ya kishindo kwamba huko tuendako sio salama na kwamba nchi yetu inakabiliwa na maangamizi makubwa iwapo Serikali haitaweka mazingira ya kuwawezesha wananchi kushiriki katika chaguzi mbalimbali pasipo kuhofia maisha yao.
Kutojitokeza kwa idadi kubwa ya wananchi kupiga kura katika uchaguzi wa Arusha juzi kumehusishwa na hofu iliyotokana na bomu lililorushwa katika mkutano wa kufunga kampeni za udiwani za Chadema mwezi uliopita ambapo watu wanne walikufa na wengine 60 kujeruhiwa, hivyo kusababisha kuahirishwa kwa uchaguzi katika kata hizo hadi juzi.
Lakini pia utendaji mbovu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Tec), katika chaguzi mbalimbali, ukiwamo wa juzi jijini Arusha pia umedhihirisha kwamba huko tuendako hapatakuwa salama iwapo tume hiyo haitafanyiwa mabadiliko makubwa.
Tunalazimika kusema hapa kwamba yafaa tutumie fursa tuliyonayo hivi sasa ya kuandika Katiba mpya kuhakikisha kwamba Katiba hiyo inatuzawadia Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyo huru na yenye uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu.
Uchaguzi wa juzi jijini Arusha umedhihirisha ulegelege na udhaifu mkubwa uliopo katika Tume hiyo. Pamoja na kuwa na uzoefu wa kutosha katika kusimamia chaguzi mbalimbali, Tume hiyo haionyeshi kubadilika wala kuwa na dira na mwelekeo wa kuiwezesha kwenda na wakati kuhakikisha chaguzi zinafanyika kwa mujibu wa sheria.
Kama tulivyoshuhudia katika uchaguzi wa Arusha juzi, kasoro ambazo zingeweza kuzuilika zimeendelea kujitokeza na nyingi zimekuwa zikijirudia kutokana na watendaji wa taasisi hiyo nyeti kufanya kazi kwa mazoea tu.
Pamoja na wananchi kuwa na shahada halali za kupigia kura na majina yao kubandikwa katika mbao za matangazo, baadhi yao walizuiwa kupiga kura kutokana na Daftari la Wapigakura kutokuwa na majina, maelezo na picha zao.
Baadhi ya majina ya wapigakura yalitokea zaidi ya mara moja wakiwa na namba tofauti, huku wataalamu wa mifumo ya kompyuta wakisuasua kurekebisha matatizo yaliyojitokeza.
Matatizo hayo, ikiwa ni pamoja na Tume kushindwa kuhakiki Daftari la Wapigakura mara kwa mara ni viashiria vya vurugu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kwani wananchi hawatakubali kuondoka vituoni pasipo kupiga kura kwa uzembe tu wa Tume hiyo.
Hii pengine inadhihirisha kwamba haitaweza hata kutumia teknolojia ya kisasa kuhesabu kura mwaka 2015. Matokeo yake ni vurugu zitakazotokana na kasoro hizo.

No comments: