Watu hao wanaondolewa maeneo yao huku ikielezwa kuwa zoezi hilo
ni endelevu, viongozi wa Manispaa za jiji hilo nao wamekuwa wakitoa
elimu juu ya usafi kwa wafanyabiashara wa hoteli pia.
Acha hilo, katikati ya wiki hii nyakati za jioni
lilikatiza gari katikati ya jiji hilo likipuliza dawa ya kuua mbu na
kuwafanya watu waliokuwa wamesimama kando ya barabara wakisubiri usafiri
kukohoa hovyo, kupiga chafya na kutafuta sehemu ya kujificha kukwepa
adha hiyo.
Hayo yote yanafanyika ili Rais Barack Obama wa
Marekani atakapowasili nchini na msafara wake alione Jiji la Dar es
Salaam likiwa safi na kila njia inafanywa kuhakikisha jiji hilo
linakluwa safi. Duh, usafi kwa ajili ya ujio wa wageni tu? Aibu gani
hii. Natambua wazi kwamba ugeni mkubwa wa viongozi wa zaidi ya nchi 14
umekuja nchini kwa mkutano wa Majadaliano ya Kiuchumi, pamoja na ziara
ya Rais Obama wa Marekani ni heshima kubwa kwa taifa letu. Pia,
natambua kwamba ugeni huu utakuwa na manufaa kwa wafanyabiashara wetu wa
hoteli, migahawa, huduma za usafiri na hata wafanyabiashara ndogondogo
kwani watapata fursa ya kuingiza kipato.
Sina tatizo na ujio wa viongozi hao, lakini
kinachonishangaza ni kuanza kwa operesheni ya usafi uliyoshindikana
miaka nenda rudi kwa sababu tu ya ujio wa viongozi hao, huku watendaji
wakidai ni zoezi endelevu. Nchi yetu inawajali wageni kuliko wenyeji,
ipo tayari kuhakikisha wageni hawang’atwi na mbu, hawasumbuliwi na
wafanyabiashara na ombamba waliotapakaa maeneo ya mjini wala kusikia
harufu chafu ya takataka zilizotelekezwa katika maroli, aibu gani hii!
Kila kukicha tumekuwa tukishuhudia takataka
zikitapakaa maeneo mbalimbali ya jiji na karibu kila kona kuna chupa za
maji yaliyotumika, mifuko ya plastiki na taka nyinginezo.
Kama hiyo haitoshi, kuna matela yaliyojaa
takataka, yametelekezwa katika sehemu mbalimbali za masoko au maeneo ya
makazi ya watu. Mifereji ya kupitisha majitaka, mingi imeziba, jambo
ambalo husababisha maji yanayotokana na mvua kusambaza uchafu, unaobebwa
kwenye maeneo ya makazi au barabarani.
Taka hizi husambaa na kuziba njia za waenda kwa miguu, hivyo kuwapa watumiaji hao wa barabara ugumu wakati wanapotembea.
Katika mitaa mbalimbali kuna madimbwi
yaliyosahauliwa na mamlaka husika, madimbwi ambayo yanawasitiri mbu na
kuwa mahala pao kuzaliana na kueneza magonjwa ikiwamo Malaria.
Kwa miaka nenda rudi Jiji la Dar es Salaam,
ambalo ndilo kioo cha taifa letu, limekuwa likiongoza kwa kuupalilia
ugonjwa wa kipindupindu, ambao chanzo chake kikuu ni uchafu. Karibu kila
mwaka uongozi wa Hospitali za Jiji hilo hupokea wagonjwa wa
Kipindupindu.
Operesheni hii ya usafi inayofanyika sasa
ilitakiwa kuanza miaka mingi iliyopita, siyo tu katika usafi wa
mazingira bali ingekwenda hadi katika kusimamia miundombinu na ujenzi
holela wa makazi usiozingatia mipango miji kwani ujenzi huo husababisha
uchafu kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya maji taka.
Takataka kila mahali, harufu za vinyesi, maji
taka, magari mabovu, biashara kila kona hadi makaburini. Mitaro
imefurika , chupa za mikojo na mifuko ya plastiki imezagaa hadi
barabarani mingine ikiwa na kinyesi, hiyo ndiyo Dar es Salaam.
Lakini hivi sasa, ujio wa wageni hawa umewaamsha
wahusika, wanafanya usafi kila kona kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda
sawa na siyo ajabu kuona kila kitu kimelala baada ya viongozi hao
kuondoka.
Usafi katika Jiji la Dar es Salaam unahitaji utafiti wa kina
na njia za kitaalamu zaidi katika kuhakikisha masuala ya usafi na
mazingira yanafanikiwa.
Nasema hivi kwa sababu mipango na miundo mbinu ya
miji huo ni ya zamani tangu enzi ya mkoloni ambapo idadi ya wakazi
likuwa ndogo ukilinganishwa na sasa. Natambua kuwa jukumu la usafi ni la
watu wote, ila kwa upande wa Serikali inatakiwa kuja na mikakati mipya
na endelevu itakayolitoa jiji hili katika hali ya uchafu kwa kutumia
fedha zitokanazo na ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali
na siyo kusubiri ujio wa viongozi.
Wafanyabiashara kupanga bidhaa, barabarani na
mbele ya majengo ya Ofizi za Serikali, kushamiri kwa gereji bubu
mitaani, kumbi za burudani zinazopiga muziki usiku kucha, ni moja ya
kero zilizowashinda watendaji wa mamlaka husika.
Mamlaka husika zimeshindwa hata kudhibiti mfumuko
wa vilabu vya pombe, kiasi kwamba hata shule za msingi na sekondari za
jijini Dar es Salaam zimezungukwa na Baa na nyumba za kulala wageni.
Karibu Rais Obama kwani ujio wako umewakumbusha
wahusika kulifanyia usafi Jiji la Dar es Salaam ikiwa ni baada ya muda
mrefu kupita tangu wafanye hivyo, pengine watakumbuka tena kufanya usafi
siku atakayokuja Malkia Elizabeth wa Uingereza.
No comments:
Post a Comment