Sunday, 10 March 2013

Haki za Binadamu nao watoa tamko



Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu ambao ni mkusanyiko wa asasi zaidi ya 70 za kiraia zinazotetea haki za binadamu (THRD-Coalition) , kwa kushirikiana na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC),vimeelezea kulaani vikali shambulio la kinyama alilofanyiwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda.

Uchunguzi tulioufanya bado haujatujapatia habari za undani zaidi na uhakika wa tukio hilo, lakini kwa taarifa za awali kwa asilimia kubwa linahusiana na kazi yake ya utetezi wa haki za binadamu kupitia taaluma yake ya uandishi wa habari.

"Tunasema hivyo kwa sababu vitisho dhidi ya wanahabari na watetezi wengine wa haki za binadamu,vinataka kuzoeleka sasa hapa nchini jambo ambalo halikuwapo katika miaka ya nyuma.

"Takribani ndani ya miezi 10 sasa, zaidi ya watetezi wa haki za binadamu 10 wakiwamo waandishi wa habari wameshajeruhiwa, wamepata vitisho au kuuawa."

Ilisema taarifa hiyo iliyosainiwa na Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Mtandao huo kuwa matukio hayo yanaashiria lengo la kutaka kuzima sauti za watetezi wa wanyonge kwa visingizio mbalimbali na wakati mwingine matukio haya yakipewa sura tofauti ikiwamo uhalifu wa kawaida, visa vya kudhulumiana na visasi vya kimapenzi.

"Hatupendi kuingilia wala kukwamisha utendaji kazi wa jeshi hilo, lakini pia hatupendi wanahabari na watetezi wengine wafanye kazi yao katika mazingira ya woga. Tunaamini kwamba zipo njia muafaka zaidi za kushughulikia masuala yanayohusu taaluma ya habari," ilisema taarifa hiyo.

Mtandao huo umewataka watu wote wanaotumika au wanaoendeleza wimbi la mashambulizi kwa wanahabari na watetezi wote wa haki za binadamu kwa ujumla, waache kufanya hivyo kwani wataliingiza nchi katika machafuko makubwa pamoja na kuisihi Polisi na Serikali kubeba jukumu lao la kuhakikisha usalama wa watetezi wa haki za binadamu, na raia wote.

No comments: