Thursday, 16 July 2015

Mtoto wa bwana shamba awa kinara kitaifa

Dar es Salaam. Wakati Ramadhani Gembe (pichani) anafanya mtihani wa Taifa wa kidato cha sita miezi miwili iliyopita, hakuwahi kufikiri angeshika namba moja kwa ufaulu kitaifa licha ya jitihada zake za kujituma.
Lakini siku zote Mungu hamtupi mja wake. Kama jina lake linavyosadifu mwezi mtukufu unaomalizika siku mbili zijazo, Ramadhani ambaye amehitimu Shule ya Wavulana ya Feza jijini Dar es Salaam, ameibuka mwanafunzi bora nchini kati ya waliofanya mtihani huo wa kujiandaa kwa masomo ya elimu ya juu.
“Nilitegemea ningefaulu lakini siyo kwa kiwango hicho… hii ni ‘surprise’ (shtukizo),” alisema Gembe alipohojiwa na Mwananchi baada ya matokeo ya kidato cha sita kutangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa.
“Nawashukuru wazazi, walimu, ndugu na wanafunzi wenzangu kwa kunipa ushirikiano. Nilikuwa nafanya sana ibada hivyo haya matokeo ni juhudi binafsi na majibu ya Mungu,” alisema Ramadhani aliyesoma mchepuo wa fizikia, kemia na baiolojia (PCB).
Historia ya Ramadhani darasani si haba kwani mwaka 2008 alikuwa ni mwanafunzi pekee aliyejiunga na shule ya vipaji maalumu ya Ilboru, Arusha akitokea shule ya Msingi Mombo na alipata daraja la kwanza akiwa na pointi 11 katika matokeo ya kidato cha nne.
“Siku zote kilichonifanya niongeze juhudi katika masomo yangu ni malengo ya baadaye... mimi nataka kuwa daktari wa binadamu hivyo sikutaka kulegalega kusoma. Pia, wazazi wangu pamoja na hali ngumu walijitahidi kunisaidia kimawazo, kirasilimali na kimaadili…naomba na wazazi wengine wawafanyie hivyo watoto wao,” alisema.
Baba azungumza
Nurdin Gembe, ambaye ni mzazi wa Ramadhani, alisema familia imepokea kwa furaha matokeo hayo na kwamba alikuwa akiyategemea kuwa mazuri kutokana historia ya kijana wake katika madarasa ya nyuma.
“Huyu mtoto namlea kawaida japo zamani alikuwa mtundu sana… ilibidi nimpe mafundisho mengi sana ya kidini bila kupoteza ratiba ya kusoma shuleni. Nashukuru kuwa alizingatia na amefika hapo alipofika,” alieleza Gembe ambaye ni bwana shamba kitaaluma.
Mwanafunzi wa tisa
Kwa upande wake Yonazi Senkondo, aliyeshika nafasi ya tisa kitaifa, alisema matokeo hayo ni majibu ya maombi kwa Mungu na juhudi zake kusoma na ushirika na wanafunzi wenzie.
“Siku zote nilikuwa naombea niingie 10 bora, najua leo Mungu amejibu maombi yangu. Nilikuwa nafanya mijadala na wanafunzi wenzangu hasa huyo aliyeshika namba moja. Sishangai yeye kuwa katika ngazi hiyo.
“Siku zote naamini maombi na nidhamu ndiyo msingi wa yote kwa sababu unaweza kukesha unasoma, lakini matokeo yakaja tofauti,” alisema Yonazi aliyekuwa akisoma fizikia, kemia na bailojia (PCB) katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Feza, jijini Dar es Salaam.
Mama yake, Jeanette Senkondo alisema matokeo ya kuingia 10 bora ni kama shtukizo kwa kuwa alikuwa anajua mwanaye ana uwezo wa kufaulu ila siyo kwa kiwango hicho na kwamba ni mafanikio ya sala, juhudi na mipango, ushirikiano, nidhamu na malezi bora ya mwanafunzi.
“Tangu chekechea alikuwa na juhudi za masomo na siku zote akipanga kitu lazima akitimizie… pia huwa anasali na kufunga hata mimi wakati wa majuma mawili ya mtihani nilifunga kumuombea. Bila shaka Mungu amejibu maombi,” alisema Senkondo ambaye ni mhadhili wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hurbert Kairuki.
Mkuu wa Feza alonga
Makamu Mkuu wa Shule ya Wavulana ya Feza, Ali Nungo alisema kitendo cha kuingiza wanafunzi 10 bora ni changamoto wanayotakiwa kuliendeleza siku zote kwani hawajawahi kufanya kwa kiasi hicho.
“Vijana hawajatuangusha, tulitegema watafanya vizuri ila siyo kiwango hicho. Sisi kama walimu na uongozi wa shule tumefanya tuwezalo kuwawezesha kwa kuwafundisha na kuwapa ushirikiano lakini lazima wazazi watambue kumleta mtoto tu Feza si kwamba anakuwa bora, lazima kuwe na ushirikiano mzuri baina ya pande zote,” alisema.

Wednesday, 15 July 2015

Nani Mgombea urais wa UKAWA?

 Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA vimetangaza rasmi kufikia makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Akitangaza makubaliano hayo mara baada ya kumalizika kwa kikao kirefu kilichokuwa kikijadili mustakabali wa kumpata mgombea urais pamoja na ugawanaji wa majimbo mapya, mwenyekiti mweza wa UKAWA James Mbatia amesema kuwa umoja huo umemteua mgombea ambaye ni chaguo la watanzania.
“Mgombea tutakayemtaja ndiye chaguo la watanzania” Amesema Mbatia
Mbatia amegoma kutaja jina la mgombea aliyepitishwa na umoja huo na kusema kuwa atatangazwa siku chache zijazo kwa madai kuwa anaandaliwa utambulisho maalum utakaoambatana na shamra shamra.
“Tayari jina tunalo lakini tutaliweka hadharani baada ya siku mbili tatu hivi, na tutamtoa kwa kimasomaso”
Katika kikao hicho kilichomalizika majira ya saa 3:30 usiku kikihusisha wenyeviti wa vyama hivyo pamoja na kamati ya ufundi ya UKAWA, mwenyekiti mwenza wa UKAWA kutoka chama cha wananchi CUF Prof Ibrahim Lipumba hakuweza kuhudhuria.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka CUF, chama hicho kilimuagiza Naibu Katibu Mkuu wa CUF Magdalena Sakaya kuiwakilisha, lakini baadaye Sakaya aliondoka katika kikao hicho bila maelezo yoyote.
Kwa upande wake Magdalena Sakaya alipoulizwa kuhusu kukosekana kwake katika kikao hiho, alisema kuwa ndani vyama bado kuna migogoro kwahiyo ni vema kumaliza kwanza migogoro ya ndani ya vyama na ndipo wajadili hatma ya wagombea wa UKAWA.
Mkurugenzi wa mawasisliano wa chama hicho bwana Abdul Kambaya alipoulizwa kuhusiana na hilo akasema kuwa hakuna mwakilishi yeyote wa CUF aliyekuwepo kikaoni hapo hadi kikao hicho kikimalizika.
Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohammed alipoulizwa kuhusiana na kukosekana kwa Prof Lipumba kikaoni hapo amedai kuwa Prof Lipumba ni mgonjwa, na hali yake ya kiafya haimruhusu kuhudhuria kikao hicho.
“Mwenyekiti wetu ni mgonjwa, alikuwa safarini kutoka Kigoma, amerejea lakini hali yake si nzuri, ameshikwa na Malaria kali sana na miguu pia inamsumbua” Amesema Rajab Mbarouk.
Viongozi waliokuwepo wakati wa mazungumzo na waandishi wa habari ni James Mbatia, Freeman Mbowe, Tundu Lissu, John Mnyika, Emmanuel Makaidi, Dkt Wilbroad Slaa, Mosena Nyambabe, Dkt George Kahangwa (mgombea urais kupitia NCCR) na mtu anayetajwa kuwa mwakilishi kutoka chama cha CUF.
Licha ya kushindwa kutaja jina la mgombea urais kupitia UKAWA, baadhi ya vyanzo vya ndani vinaonesha kuwa mgombea urais aliyepitishwa na UKAWA ni Dkt. Wilbroad Slaa ambaye ni Katibu Mkuu CHADEMA.
Katika hatua nyingine, afisa habari wa CHADEMA Tumaini Makene aliwaambia waandishi wa habari kuwa tayari vyama hivyo vimekamilisha kazi ya kugawana majimbo mapya 26 kazi iliyofanyika leo katika kikao hicho.
Kuhusiana na mgombea wa CCM Dkt John Magufuli, viongozi hao wamesema kuwa hawatishiki naye, na wala hawamfikirii, na kusisitiza kuwa mgombea ambaye ni chaguo la watanzania atatoka UKAWA na atatangazwa siku chache zijazo.

Saturday, 11 July 2015

Hongera Rais Kikwete, changamoto bado nyingi

Rais Jakaya Kikwete juzi alihutubia Bunge la 10 kwa lengo la kuliaga na kulivunja rasmi kuashiria kuweka mazingira kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ambao utatoa Bunge la kumi na moja.
Rais alitumia hotuba yake ya mwisho kwa chombo hicho cha kutunga sheria kuelezea mafanikio ambayo Serikali ya Awamu ya Nne imeyapata katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake, lakini pia akawa muwazi kwa kueleza matatizo ambayo hakuweza kuyafikia, hasa suala la bei ya mazao kwa wakulima na kushindwa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Tunaungana na Watanzania wengine kumpongeza Rais kwa jitihada ambazo Serikali yake imezifanya katika nyanja za uchumi, siasa na jamii na hatuna shaka na takwimu alizozitoa kuelezea mafanikio hayo.
Ni jambo lisilopingika kuwa alijitahidi kuimarisha utawala bora, hasa baada ya kuruhusu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuwasilishwa bungeni ambayo imesaidia kudhibiti ufisadi kwenye vyombo vya umma, kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya usafiri-barabara, bandari na viwanja vya ndege- huduma za afya, ukusanyaji kodi, demokrasia na Muungano.
Kama alivyosema Rais, si rahisi kumaliza matatizo yote katika awamu moja na hivyo atakayempokea kijiti ana wajibu wa kuendeleza hayo atakayoyakuta hadi atakapoishia. Pamoja na kumpongea Rais kwa hotuba hiyo na mafanikio ya Serikali ya awamu yake, tunadhani kuna mambo ambayo hayakuwa na mafanikio makubwa au yalifanyiwa kazi vizuri lakini yanaanza kuonekana kwenda mrama.
Suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) ni moja ya mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Nne, lakini ni jambo linalosikitisha kwamba Rais Kikwete anaondoka wakati umoja huo ukiwa na dalili za kumomonyoka.
Matukio ya hivi karibuni kwenye Baraza la Wawakilishi ni ishara tosha kwamba mambo si shwari Zanzibar na hivyo badala ya Rais kusifia mafanikio, angechukulia kuwa ni changamoto kubwa kwa Serikali yake kushindwa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Pia, suala la Muungano halionekani kuwa linaachwa salama kwa sababu kipindi hiki ndicho ambacho pande hizi mbili zimerushiana maneno makali yanayoweka ishara mbaya kwa mustakabali wa tunu hiyo muhimu kwa Taifa.
Ni dhahiri matukio yaliyojiri wakati wa Bunge la Katiba yanatosha kuweka swali juu ya hatima ya Muungano, hasa baada ya viongozi wa chombo hicho kushindwa kutafuta suluhu ili kuwa na maridhiano ambayo yangejenga mazingira mazuri kwa Taifa kusonga mbele likiwa kitu kimoja.
Pamoja na Rais kusema kuwa anaiacha nchi ikiwa salama, bado kuna maswali mengi kuhusu usalama huo, amani na utulivu. Ni kweli kwamba vitendo vya ujambazi vimepungua kulingana na hali ilivyokuwa mwaka 2005 wakati akiingia madarakani, lakini hali inaonekana si shwari kwa kuwa uhalifu huo sasa ni dhidi ya polisi na vituo vyao.
Uvamizi wa vituo vya polisi ambao jukumu lao ni kulinda usalama wa raia, sasa umekuwa ukitokea kila mara, tishio la ugaidi limeongezeka na vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi wanapokuwa na madai yao vimeongezeka. Mambo hayo, ukichanganya na ukweli kwamba takwimu zinazoashiria kukua kwa uchumi, hazionekani kwenye maisha ya kila siku ya mwananchi wa kawaida, yanazidi kuiweka amani yetu katika hali ya sintofahamu.
Tunadhani kuwa haya ni mambo ambayo inabidi yawekwe bayana ili Taifa lijue kuwa pamoja na mafanikio mengine mengi aliyoyataja mkuu wa nchi, bado tuna changamnoto hizo kubwa na hivyo hata Rais anayekuja na Serikali yake, anapaswa kujua kuwa nchi ina mzigo kiasi gani katika kudumisha Muungano, kuendeleza usalama wa raia na kulinda muafaka uliofikiwa Zanzibar.

MCHAKATO URAIS CCM: Lowassa akatwa

Dodoma. “Anakatwa, hakatwi” ndilo swali lililokuwa linaulizwa nchi nzima jana, lakini hatimaye Kamati Kuu ya CCM iliyokutana hadi usiku wa manane iliibuka na jibu kwamba Edward Lowassa amekatwa, huku kukiwa na wingu zito baada ya wajumbe watatu kupingana na uamuzi huo.
Muda mfupi baada ya kikao hicho, pamoja na kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikataa kutaja majina yaliyopitishwa, akaunti ya Twitter ya CCM, iliwataja waliopitishwa kuwa ni Bernard Membe, Dk John Magufuli, Dk Asha Rose Migiro, January Makamba na Amina Salum Ali na kuwatupa wengine 33 akiwamo Lowassa.
“Kikao cha Kamati Kuu kimeisha salama. Kesho (leo) Halmashauri Kuu itakutana kuanzia saa 4:00 asubuhi,” alisema Nape baada ya kikao hicho.
Alipotakiwa kutaja majina ya makada watano waliopitishwa, Nape alisema: “Nimeambiwa mchakato bado unaendelea na kesho (leo) Halmashauri Kuu itakutana kuendelea na kazi. Kwa hiyo nawakaribisha kesho kuanzia saa 4:00 asubuhi mje mchukue picha, habari, karibu sana.” Mkutano Mkuu utafanyika saa nane mchana leo.”
Dakika chache baada ya kikao hicho kumalizika, wajumbe watatu wa Kamati Kuu, wakiongozwa na mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa wanapinga uamuzi huo ambao hawakuutaja, wakidai kuwa si majina yote yaliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo.
Dk Nchimbi, akiongozana na mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa na mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sofia Simba waliwaeleza waandishi wa habari mara tu baada ya mkutano wa Kamati Kuu kuwa kikao hicho hakikufuata kanuni kwa kuwa majina machache yaliwasilishwa na hayakuhusisha mgombea anayekubalika.
Ingawa hawakumtaja mgombea huyo waliyesema anatajwa na wengi, wajumbe hao wanafahamika kuwa wanamuunga mkono Lowassa.
Baada ya kikao hicho taarifa za wagombea hao zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii na mijadala ya wazi ilianza kuhusu uamuzi wa kumtosa Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Mmoja wa makada watano waliopitishwa kwenye mchujo huo aliithibitishia Mwananchi kuwa jina lake limepita, lakini akasema hataki akaririwe na badala yake akamshauri mwandishi aangalie akaunti ya twitter ya CCM baada ya nusu saa.
Habari za jina la Lowassa kukatwa zilizagaa tangu jana asubuhi, ilipoelezwa kuwa CCM ilifanya majadiliano na wadau mbalimbali kuangalia jinsi ya kudhibiti watu wanaounga mkono baada ya kupata taarifa kuwa ameenguliwa.
Lowassa azua mjadala
Awali wakati Kamati Kuu ya CCM ikikutana jana usiku kupitisha majina ya makada watano walioomba kuwania urais, jina la Edward Lowassa ndilo lililotawala mijadala mingi kwenye mitandao ya kijamii, likiambatana na swali moja; amekatwa, hajakatwa?
Hali hiyo iliendelea zaidi jana usiku wakati CCM ilipotangaza mabadiliko ya tatu ya ratiba za vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.
Watu wengi walikuwa wamefurika kwenye jengo la makao makuu ya CCM mjini hapa, maarufu kama White House na walioruhusiwa kuingia walikuwa waandishi wa habari na wajumbe wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu, ambao walikuwa wakifuata makabrasha na vitambulisho.
Mapema jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari kuwa kikao cha Kamati ya Maadili na Usalama ingekutana kuanzia saa 4:00 asubuhi na kufuatiwa na Kamati Kuu saa 8:00 mchana, lakini baadaye akatangaza mabadiliko mengine ambayo yalionyesha kuwa Kamati Kuu ingekutana kuanzia saa 10:00 jioni na Halmashauri Kuu baada ya futari.
Majira ya saa 2:00 usiku, Nape alitangaza kuwa kikao cha Kamati Kuu kingeanza muda huo na kwamba kingechukua muda mrefu na hivyo Halmashauri Kuu itakutana leo kuanzia saa 4:00 asubuhi na orodha ya makada watano waliopita kwenye mchujo itatangazwa muda huo.
Wakati Nape anawaambia waandishi wa habari jana asubuhi kuhusu sababu za kuahirishwa kwa vikao, tayari kulikuwa na habari kuwa Lowassa ameenguliwa baada ya vikao vya maridhiano kabla ya vikao hivyo vya juu kuhusu namna ya kudhibiti wanachama wanaomuunga mkono.
Habari hiyo ndiyo iliyokuwa mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii. “Amekatwa au hajakatwa?” ndilo swali lililoulizwa na wengi kwenye mitandao hiyo kutaka kujua kama kada huyo, aliyeonyesha kuungwa mkono na wengi wakati wa kusaka wadhamini.
Akizungumza na waandishi jana asubuhi, Nape alisema kuahirishwa kwa vikao hivyo muhimu kulitokana na mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kuwa na vikao na watu mbalimbali kupata ushauri kuhusu namna ya kumaliza mchujo kwa usalama.
“Mwenyekiti alikuwa na vikao mbalimbali vya consultation (mashauriano) na wadau ili kuhakikisha vikao vinakwenda salama,” alisema Nape na kuongeza kuwa hiyo ndiyo ilisababisha ratiba ya vikao kubadilishwa.
Hata hivyo, Nape hakuelezea vikao vya mashauriano kati ya Rais Kikwete na Serikali vilihusisha makundi gani.
Nape alisema mabadiliko hayo pia yalitokana na shughuli za kiserikali na kichama ambazo Kikwete alikuwa nazo mjini Dodoma, ambako Julai 9 mwenyekiti huyo wa CCM alifanya kazi mbili za kuzindua jengo jipya la mikutano la chama hicho na baadaye kulihutubia kwa mara ya mwisho Bunge la 10, siku ambayo alitakiwa kuongoza kikao cha Kamati Kuu.
Awali Kamati ya Usalama na Maadili, ambayo inachambua wagombea na kutoa mapendekezo ya kila mmoja, ilipangwa kukutana Julai 8, na kufuatiwa na Kamati Kuu (Julai 9), Halmashauri Kuu ya Taifa (Julai 10) na Mkutano Mkuu ambao ungefanyika Julai 11-12.
Lowassa ndiye anayeonekana kuwa kinara miongoni mwa makada 38 walioomba kugombea urais kwa tiketi ya CCM, akionekana kuwa na wafuasi wengi ndani na nje ya chama, hali ambayo aliionyesha kwenye harakati za kutafuta wadhamini.
Mbunge huyo wa Monduli aliungwa mkono na takriban wenyeviti 15 wa mikoa, wabunge kadhaa waliojitokeza bayana kueleza misimamo yao kwake na wajumbe kadhaa wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu.
Jana, baada ya kusogezwa mbele kwa kikao cha Halmashauri Kuu, watu wengi waliondoka kwenye viwanja vya makao makuu ya CCM, na hakukuwapo na makada wanaowania kugombea urais kwenye eneo hilo ambako Kamati Kuu ilikuwa ikiendelea na kikao chake.
Kwa kawaida Kamati Kuu hupitisha majina matano kwa makubaliano licha ya kwamba katiba ya CCM inaruhusu maamuzi kufikiwa kwa kupiga kura.
“Mara nyingi hakuna upigaji kura kwenye vikao vya Kamati Kuu,” alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya alipoongea na Mwananchi nje ya jengo hilo jana saa 2:40 usiku baada ya kuarifiwa kuwa kikao cha Halmashauri Kuu kimeahirishwa hadi leo.
“Mara nyingi uamuzi huwa ni kwa maridhiano licha ya Katiba kuruhusu upinzani kura pale mnaposhindwa kukubaliana,” alisema Profesa Mwandosya ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu.

Monday, 29 June 2015

Sifa 10 za mgombea urais bora wa upinzani 2015

Ni jana tu nimemaliza uchambuzi wa watu wanaotajwa au waliojitokeza kugombea urais au wale ambao hawajajitangaza na hawana nia lakini jamii ndani na nje ya vyama vyao inawataja kama watu wenye sifa, uwezo na hata vigezo vya kuiongoza nchi yetu, kutoka vyama vya upinzani.
Lengo la uchambuzi huu ni kuwafanya Watanzania waanze kuwafahamu viongozi wao wajao na hata aina ya sifa wanazoweza kuwa nazo. Inawezekana kabisa kuwa wagombea waliochambuliwa asitokee mmoja wao kugombea au la, lakini hapa ninachoangalia ni kwamba tayari wananchi watakuwa “wamesogezwa karibu na ajenda ya uchaguzi” na hata akiletwa mgombea kutoka wapi, walau wananchi watakuwa wanajua wafanye uamuzi wa namna gani.
Leo nahitimisha hoja ya wagombea wa upinzani kwa kutoa sifa 10 za mgombea urais bora kutoka upinzani ambaye anaweza kupigiwa kura nyingi na Watanzania na hatimaye kuwa rais mpya wa Tanzania:
1. Mwenye umaarufu/umashuhuri na anayekubalika
Sifa hii ni muhimu, unapokuwa nje ya dola na nje ya chama tawala siyo rahisi kukishinda chama kinachoongoza Serikali. Umaarufu, umashuhuri na kukubalika ni mambo ya lazima. Ukitizama historia ya dunia na hata Afrika, vyama vikongwe vilipoondolewa madarakani waliofanya hivyo walikuwa wapinzani mashuhuri. Umuhimu wa sifa hii ni kuwa walau mtu maarufu na mashuhuri au anayekubalika, tayari amewekeza “mbegu” kwenye mioyo ya wananchi, wanaweza kumwamini ili waondoe hatima ya nchi mikononi mwa chama kilichowaongoza kwa miaka 50 na kuiweka mikononi mwa watu wapya. Wananchi wasipomwamini kiongozi wa upinzani anayekuja kwa sababu wanamkubali, ndipo huzuka ile kasumba ya “tupige kura kwenye zimwi likujualo”.
Hatari ya sifa hii
Umaarufu, umashuhuri na kukubalika vitaweza kufanya kazi kwa upinzani ikiwa mgombea husika hatatumia mwanya wa kukubalika kwake kujenga kiburi na hatimaye kuwasaliti wananchi. Ndiyo kusema kuwa vyama vya upinzani vitapaswa kuchagua mtu bora ambaye atatimiza matakwa ya wananchi “hata kama ni maarufu kuliko jua”.
2. Atakayebeba ajenda bora na kuifafanua vizuri
Kubeba ajenda bora na kuwa na uwezo wa kuifafanua kwa lugha rahisi ni jambo la muhimu kwa mtarajiwa kutoka upinzani. Moja kati ya makosa makubwa ya vyama vya upinzani katika bara la Afrika ni kutaka kubeba ajenda nyingi na kumrundikia mgombea urais, nakubali kuwa Afrika ina matatizo katika kila sekta ya maisha ya mwanadamu, lakini lazima iwe na vipaumbele vinavyowaumiza wananchi. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa na ajenda bora kuliko ile ya CCM na atapaswa kuwa na uwezo wa kuifafanua akaeleweka na mipango ya utekelezaji wake ikawa siyo ya “kusadikika”.
Hatari ya sifa hii
Ni pale inapotokea kuwa mgombea bora wa urais kutoka upinzani anazunguka nchi na ajenda iliyo bora kabisa lakini utekelezaji wake ukifanana au kushabihiana moja kwa moja na ule wa mgombea wa CCM. Wananchi wakiona upinzani unahubiri mipango na mbinu zilezile za CCM wataamua pia kuchagua “shetani wanayemjua” ili kujiweka kwenye mazingira ya usalama zaidi. Hivyo, ajenda ya mgombea bora wa upinzani na utekelezaji wake vinapaswa kuwa “vya kipekee”.
3. Mwenye uzoefu na rekodi ya uchapakazi
Uzoefu wa uongozi na uchapakazi unaofahamika ni jambo la msingi kwa mgombea bora wa urais kutoka upinzani. Vyama vya upinzani haviwezi kushinda uchaguzi na mgombea bora vitakayekuwa naye ikiwa mtu huyo si mzoefu na mchapakazi anayefahamika, mtu mwenye kujali wengine katika kazi lakini ambaye wananchi wataamini kuwa huyu atasimama pamoja na sisi usiku na mchana kuleta mabadiliko ya nchi.
Katika siasa, wananchi hupaswa kwanza kuamini na kisha hufanya uamuzi. Ikiwa mgombea bora wa urais wa upinzani hatakuwa na rekodi za uzoefu wa utumishi (katika taasisi za dini, serikali, vyama vya siasa na nyinginezo) si rahisi kumuuza kwa wananchi. Pia, ni lazima awe ni mtu ambaye rekodi zake zinatajwa kuwahi kuleta mabadiliko makubwa mahali alipofanya kazi.
Hatari ya sifa hii
Sifa hii hupaswa kuelezewa na kufahamika kwa wananchi kutoka kwa timu za kampeni za wagombea, wakati mwingine wapambe wa wagombea huchukua muda mwingi kutaja elimu ya mgombea wakidhani wananchi wanachagua elimu, kumbe elimu ni jambo moja tu kati ya sifa 100 za kiongozi. Ikiwa sifa hii muhimu haielezwi kwa uwazi kwa wananchi na hasa kwa kutaja rekodi bora za mgombea wa upinzani, wananchi wanaweza kumpa kisogo.
4. Mwenye uadilifu usio na shaka
Mgombea bora wa upinzani katika uchaguzi, anapaswa kuwa na uadilifu uliotukuka, usio na madoa wala shaka. Hapa nina maana kuwa, awe ni mtu ambaye uadilifu wake unatambulika kwa wananchi na kwa Taifa zima. Awe na rekodi za uadilifu kumshinda mgombea wa CCM, nina maana kuwa, wananchi wakimpima huyu wa upinzani na yule wa CCM – haraka haraka wasimame na kusema, “…naam! Huyu wa upinzani ni mwadilifu zaidi”. Marais wengi walioingia madarakani hasa hapa Afrika na hata Ulaya na Marekani kwa kuviondoa vyama vilivyokuwa madarakani, walipimwa kwa sifa hii.
Hatari ya sifa hii
Kigezo hiki hupata shida kubwa katika nchi ambazo uelewa wa wananchi vijijini na hata mjini si mkubwa. Wagombea waadilifu nao huweza kuchafuliwa ndani ya siku moja tu. Katika nchi ambayo si ajabu mgombea akawa hata na uwezo wa “kuhonga” chombo cha habari ili kimchafue mwenzake, sifa za mgombea bora zinaweza kuingizwa katika tope. Vyama vya upinzani vitapaswa kuwa na mfumo sahihi wa kuhakikisha uadilifu wa mgombea wake unazungumzwa kama ulivyo na haubadilishwi na propaganda za CCM.
5. Mwenye uwezo wa kusimamia, kuinua uchumi
Moja ya matatizo ambayo hayana dawa hapa Tanzania ni usimamizi wa uchumi. Nchi yetu inayumba kila mara na tunashindwa kutekeleza mipango yetu kwa sababu ya uchumi dhaifu, unaobadilika kila dakika na ambao hauna dira. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa na uwezo wa kusimamia na kuinua uchumi wa nchi. Awe ni mtu ambaye akisimama na kuweka ajenda ya uchumi mezani, Watanzania wote wanamwelewa, kwamba “naam, huyu ana uwezo wa kusimamia uchumi na kuondoa umaskini wa nchi”.
Hatari ya sifa hii
Ni pale mgombea wa upinzani atazunguka na mipango kabambe ya uchumi lakini yenye shaka kubwa kwenye utekelezaji au kuondoa umaskini, lakini pia ni pale mipango hiyo haitakuwa ya muda mfupi. Katika nchi maskini, wananchi wanahitaji matokeo haraka, vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la kuwa na mipango ya mfano ya muda mfupi ili kuwahakikishia wananchi kuwa ile ya muda mrefu pia itaweza kutekelezeka kwa wakati.
6. Kuongoza mapambano dhidi ya rushwa
Rushwa ni adui wa haki na ni tatizo kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Afrika. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa mtu wa kipekee ambaye moja ya sifa zake kuu ni mapambano dhidi ya rushwa, ndogo na kubwa. Awe ni Mtanzania ambaye si tu kwamba anapiga vita rushwa, bali anawachukia wala rushwa kama “kifo” na ni mtu ambaye yuko mbali kabisa na wala “rushwa”. Ndani ya CCM kwenyewe nadhani watatafuta mgombea wa namna hii ili kulinda hadhi yao, vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la kutafuta mpinga rushwa mahiri kuliko yule wa CCM, kwamba ukiwaweka pamoja hawa wawili – wananchi wenyewe waseme “…naam huyu wa upinzani anaweza mapambano haya zaidi kuliko huyu wa CCM”
Hatari ya sifa hii
Ikiwa upinzani utakuwa na mtu mashuhuri katika mapambano ya rushwa lakini ukawa hauna mipango ya kuhuisha haraka mifumo inayoleta mianya ya rushwa ndani ya nchi. Ndiyo kusema kuwa moja ya mipango ya upinzani inapaswa kuwa ni pamoja na kuweka wazi mifumo mipya ya usimamizi wa mapambano dhidi ya rushwa na hata kueleza watu watakaokuwa na sifa za kufanya kazi na mifumo hiyo.
7. Asiyependa kulipiza visasi na atakayefuata sheria
Jambo hili si dogo katika siasa. Rais ajaye kutoka upinzani anapaswa kuwa na sifa hii. Kwamba afahamike na kujulikana kwa kutokuwa na tabia ya kulipiza visasi lakini ambaye atazingatia matakwa ya sheria katika utendaji na awe na rekodi hizo. Unajua, kuna mambo ya kisheria ambayo ni lazima rais yeyote yule akiingia lazima ayafuate, mfano, wizi wa pesa za umma, hata kama umefanywa mwaka 1960 na ushahidi upo, lazima watuhumiwa wachukuliwe hatua leo, “jinai haifi wala kupotea”. Lakini kuna masuala mengine mengi tu ya kawaida ambayo yalikuwa yanatendwa na uongozi uliopita kwa sababu “za kipuuzi” na zisizo na maana, hayana haja ya kuwa kichwani kwa rais anayekuja.
Hatari ya sifa hii
Wananchi wengi huhofia masuala ya usalama iwapo vyama vipya vitaingia madarakani, hasa Afrika na moja ya masuala ambayo hupoteza usalama ni “kulipiza visasi”. Ndiyo maana vyama vya upinzani vinawajibika kuwa na mgombea ambaye hatalipiza visasi kwa makosa ya nyuma ya kiutendaji, ila atafanya hivyo kwa yale yaliyokosewa kwa makusudi na kwa kutofuata sheria.
8. Uwezo wa kubadilisha mfumo wa nchi
Tangu tumepata uhuru, nchi yetu imekuwa inasifika kwa kuwa na mifumo mibovu na isiyo na tija katika kila sekta. Hili ni janga kubwa. Rais bora ajaye kutoka upinzani ana kazi kubwa ya kubadilisha mfumo wa sasa wa nchi katika kila eneo ili mifumo ifanye kazi kwa mbio na kwa tija kubwa zaidi. Leo kuna watu walishtakiwa miaka ya 1990 na bado wako gerezani bila kuhukumiwa, kuna Kiwanda cha Sukari Kilombero na huko bei ya sukari ni kubwa kuliko Dar es Salaam. Haya ni matatizo makubwa ya kimfumo. Wananchi watahitaji kuwa na kiongozi ambaye atakuja kubadilisha kabisa mifumo ya utendaji kazi katika nchi. Kwa bahati nzuri, upinzani unaweza kuwa na hoja kama hii kwani vyama hivyo havikuwahi kuongoza Serikali na vimekuwa “waathirika” wa mfumo uliopo.
Hatari ya sifa hii
Ubadilishaji wa mifumo ukifanywa haraka na kwa pupa, utaingilia na kuvunja hata mifumo ambayo ilikuwa imeanza kukua na kukomaa kwa upande chanya. Ni jukumu la mgombea bora wa upinzani na timu zake kutambua mifumo yote ya utendaji katika sekta za jamii na kubainisha tangu wakati wa kampeni, ipi itavunjwa na ipi itarekebishwa ili kutoleta hofu yoyote kwa wapiga kura.
9. Msimamo unaoeleweka juu ya Katiba
Suala la katiba mpya ni ajenda muhimu katika uchaguzi wa mwaka huu. Mgombea bora wa upinzani atapaswa, yeye mwenyewe kuwa na busara za kutosha na msimamo thabiti juu ya masuala ya kikatiba na hasa mchakato wa Katiba Mpya. Naona kuna Watanzania wengi watapiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu kwa chama au mgombea ambaye atakuwa na misimamo ya wananchi katika suala la katiba. Hadi sasa hatuelewi kama katiba itapitishwa au la na hatuelewi kama wananchi wanaikubali au wanaikataa. Nani atatuvusha na kwa utaratibu gani? Majibu atakuwa nayo mgombea bora wa urais kutoka upinzani.
Hatari za sifa hii
Msimamo wowote ule wa mgombea urais wa upinzani katika jambo hili unaweza kuwa na athari chanya au hasi kulingana na namna wananchi wanavyolitazama suala la katiba. Kama mgombea huyu atakuwa na msimamo katika kuikataa Katiba Inayopendekezwa na kwamba ataanzisha mchakato mpya na ikiwa hayo ndiyo matakwa ya wananchi walio wengi, jambo hili peke yake litamuongezea kura za kutosha. La ikiwa kinyume chake, litakuwa na athari ya kiwango hichohicho bila kujali kama athari yenyewe ni chanya au hasi.
10. Uzoefu wa masuala ya kimataifa
Moja ya kazi kubwa za mkuu wa nchi ni kuliwakilisha Taifa katika masuala ya kimataifa. Rais bora kutoka upinzani hakwepi kuwa na rekodi imara ya masuala ya kimataifa, si kuishi Ulaya na Marekani, lakini kuwe na ushahidi wa kutosha kuwa amewahi kushiriki katika baadhi ya shughuli muhimu za kimataifa na kwamba huenda hata kimataifa yeye ni mtu bora. Nadhani CCM inaweza kuwa na mgombea mwenye sifa hii pia, ni jukumu la upinzani pia kuwa na mtu ambaye amejipanga vyema kimataifa na mambo aliyoyasimamia kimataifa pia yanajulikana, si lazima yawe ya kiserikali, yanaweza kuwa ya kijamii, ya kitaasisi au ya kitaaluma.
Hatari ya sifa hii
Sifa hii inaweza kufanywa moja ya propaganda za kuisaidia CCM, kwamba ndicho chama pekee chenye watu waliofanya kazi za kimataifa na wataifanya Tanzania ikubalike kimataifa. Vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la kupambana na propaganda hii kwa kuwa na mgombea ambaye tayari wananchi wanatambua kuwa ana uzoefu wa kimataifa usio na shaka ili kusiwe na tabu ya kuanza kumwelezea muda mrefu kwa wapigakura juu ya eneo hili.
HITIMISHO
Andiko hili peke yake haliwezi kujadili sifa zote muhimu za kiongozi bora kutoka vyama vya upinzani anayeweza kulivusha Taifa. Nimechokoza mjadala wa masuala muhimu tu. Tukumbuke kuwa, kazi ya kuongoza Serikali si nyepesi, inataka kujipanga kila idara na kuwathibitishia wapigakura kuwa mnaweza bila shaka. Tabia ya wapigakura huwa ni kutafuta namna gani watawaamini watu wanaowapa madaraka. Bahati nzuri vyama vya upinzani katika Taifa letu vimekwishafanya kazi ya kupigiwa mfano inayothibitisha, uzalendo, uadilifu, uzoefu uwajibikaji na utendaji kazi bora.
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii; ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa (B.A) katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana kupitia +255787536759.
Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni yake binafsi.

Lowassa amweka Kikwete kitanzini

Dar es Salaam. Ndivyo alivyosema na bila shaka ndivyo anavyoamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini kauli ambazo amekuwa akizitoa tangu kuanza kwa mbio za urais zinamuweka katika hali ngumu Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Lowassa alirudia moja ya kauli hizo juzi alipokuwa Dar es Salaam kuendelea na kazi ya kutafuta wadhamini aliposisitiza kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa “Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje,” akisisitiza kuwa yeye ndiye anayeweza kuleta mabadiliko hayo.
Mbunge huyo wa Monduli ametoa kauli hizo kabla ya vikao vya juu vya kufanya uamuzi wa mgombea urais wa CCM vitakavyoongozwa na Rais Kikwete. Vikao hivyo vitaanza Julai 8.
Tayari makada 42 wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya chama hicho kikongwe kugombea urais na kutoa ahadi mbalimbali, lakini Lowassa, ambaye amekuwa akipata wadhamini wengi kuliko makada wengine, ndiye ambaye ametoa kauli zinazomuweka Kikwete kwenye hali ngumu.
Tangu alipoanza kuzungumzia urais kwenye kikao cha kwanza na wahariri Mei 25 mjini Dodoma, Lowassa amekuwa akitoa kauli kadhaa katika mikoa mbalimbali nchini, akianzia Arusha ambako alitangaza nia ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM na baadaye kwenye harakati za kusaka wadhamini.
Asiyenipenda ahame CCM
Akijibu swali kwamba anaweza kuhama chama iwapo jina lake litakatwa kwenye mchakato wa ndani ya CCM, Lowassa alieleza jinsi alivyokitumikia chama na imani yake.
“Sina mpango wa kuhama chama changu, sina Plan B. Mimi ni Plan A tu. Tangu nimalize chuo kikuu mwaka 1977, nimekuwa mwana-CCM. Sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha. Maisha yangu yote ni CCM,” alisema Lowassa.
“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiyo ahame, siyo mimi.”
Safari hii JK ataniunga mkono
Akihutubia maelfu ya wananchi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mei 30 wakati akitiania, Lowassa alielezea tukio la kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya CCM kuwania urais mwaka 1995 wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Kikwete, ambaye pia alichukua fomu hizo.
“Wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Pamoja tulikwenda kuchukua fomu na baadaye kwa pamoja tukazungumza na waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati yetu, mwenzake ambaye hangefanikiwa angemuunga mkono mwingine,” alisema Lowassa na kuongeza kuwa wakati ule alimuunga mkono Kikwete...“Natarajia safari hii, Kikwete ataniunga mkono.”
Mwaka huo, Kikwete alishindwa na Benjamin Mkapa ambaye baadaye akawa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Mwaka 2005, Lowassa hakuchukua fomu na badala yake alimuunga mkono Kikwete aliyeshinda na mbunge huyo wa Monduli kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Pengine kauli hiyo ya Lowassa kutaka amuunge mkono ndiyo iliyosababisha Rais Kikwete kutupiwa swali na mwanadiplomasia wa Marekani Juni 9 wakati akizungumza na Jumuiya ya Watanzania waishio Uholanzi katika hoteli ya Chawnie Plaza. Rais Kikwete alijibu kuwa hana mtu wake na kwamba wote ni wagombea wake, na kama ni suala la kuchagua, ana kura moja tu kama wajumbe wengine.
Mabadiliko aliyotabiri Nyerere
Akiwa mjini Iringa Juni 20, Lowassa alitumia kauli hiyo ya Nyerere kuhusu mabadiliko ndani na nje ya CCM.
“Baba wa Taifa alisema kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” alisema Lowassa.
“Huu ni wakati wa mabadiliko. CCM ikijipanga inaweza kuleta mabadiliko na mtu wa kuleta mabadiliko hayo ni mimi,” alisema Lowassa kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa.
Pia aliwaambia wahariri mjini Dodoma kuwa hawezi kuondoka CCM na kama kuna watu wanadhani hivyo, waondoke wao. Alikuwa akijibu swali kama atakuwa tayari kuondoka CCM iwapo ataenguliwa kwenye mchujo wa wagombea urais.
Hakuna wa kumkata jina
Juni 22, akizungumza mara baada ya kuwasili mkoani Ruvuma alisema hatarajii jina lake kukatwa katika vikao vya CCM vitakavyoketi kumteua mwanasiasa atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais.
“Nimekuwa mwanaCCM tangu mwaka 1977 nilipomaliza chuo kikuu, sijawahi kufanya kazi nje ya CCM hivyo nakijua chama na hakuna mgombea atakayeweza kuvunja rekodi ya utendaji wangu katika chama, sasa leo anayetaka kukata jina langu anatoka wapi? Anakata kwa sababu gani? Sioni kosa la kukatwa jina na Watanzania hawaoni, kwa hiyo msiwe na wasiwasi jina litarudi tu,” alisema Lowassa.
Anayemtuhumu kwa ufisadi amtaje
Siku ya kuchukua fomu Juni 5, Lowassa alijibu kwa kifupi maswali ya wanahabari na kusema kama kuna mtu ana ushahidi wa tuhuma za ufisadi dhidi yake amtaje jina.
“Kama hawakunitaja hawakunihusisha… Mtu anayejiamini aseme na anitaje. Nachoka na siasa za tuhuma, hatupimi viongozi kwa rekodi za matusi ila tu zijengwe hoja.
CCM ikijipanga itashinda
Juni 25, akiwa mjini Babati kutafuta wadhamini, Lowassa alisema iwapo CCM itajipanga vizuri, ikamaliza migogoro na kujiamini, itashinda mapema katika uchaguzi.
“Tukijipanga vizuri, tukajiamini tukaacha magomvi katika umoja wetu huu, tutashinda uchaguzi mapema dhidi ya watani wetu.”
Kwa kujipanga, Lowassa alikuwa akimaanisha kumteua yeye kugombea urais kwa tiketi ya CCM, akisema kufanya hivyo kutamaliza uchaguzi mapema.
Alichokisema Dar
Akiwa Dar es Salaam juzi kusaka wadhamini alirejea kauli ya Mwalimu Nyerere ya mwaka 1995 kwamba mabadiliko yasipopatikana ndani ya CCM, yatatafutwa nje ya chama hicho.
Kutokana na kauli hizo ni wazi kuwa rais Kikwete atakuwa katika mtihani mzito wakati atakapokuwa akiendesha vikao vya chama hicho vya kupata mgombea urais.
Kwa mujibu wa ratiba za CCM, kikao kitakachoanza kitakuwa na Usalama na Maadili kitakachofanyika Julai 8 na kufuatiwa na Kamati Kuu Julai 9 ambayo itawachuja wagombea hao 42 na kubaki watano ambao majina yao yatawasilishwa Halmashauri Kuu (NEC) Julai 10 kuchuja wagombea hao na kubaki watatu watakaopigiwa kura na mkutano mkuu kumpata mmoja. Mkutano mkuu utafanyika Julai 11 na 12.
Vikao vyote isipokuwa cha Usalama na Maadili vitaongozwa na Rais Kikwete.
Jambo jingine linaloonekana kukitesa chama hicho katika kupitisha mgombea ni idadi kubwa ya wana-CCM wanaojitokeza kumdhamini waziri mkuu huyo wa zamani.
Kwa mujibu wa taratibu za chama hicho kila mgombea urais anatakiwa kudhaminiwa na wanachama 30 katika mikoa 15 nchini ili kufikisha idadi ya wadhamini 450, lakini Lowassa amekuwa akipata wanachama hadi 50,000 wanaotaka kumdhamini katika baadhi ya mikoa.
Makada, wasomi wazungumzia kauli
Pius Msekwa alisema chama kikongwe kama CCM hakiwezi kutishika kwa kauli kama hizo ambazo zinaweza kuwa na tafsiri tofauti kwa wananchi wa kawaida ambao hawafahamu taratibu za chama wanaoweza kuamini kuna watu wanaonewa.
Alisema kwa taratibu za chama, mgombea anatakiwa kueleza sera zake atakachowafanyia wananchi, lakini akiwa anatoa kauli za vitisho anakuwa kero kwa wanaomsikiliza kwani haziwasaidii.
“Sidhani kama ni kauli nzuri, kinachotakiwa wagombea wanadi sera zao na wasubiri kupitishwa na kamati itakayokaa kwa ajili hiyo badala ya kutamka kauli zisizokuwa na tija wala faida kwa mwananchi wa kawaida, ”alisema Msekwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Frank Tilya alisema ameshangazwa na tabia hiyo ya wagombea wa CCM iliyoibuka kabla ya taratibu za uchaguzi kutangazwa kwani huko nyuma haikuwapo.
Alisema anachofahamu CCM ina taratibu zake za kupata wagombea kwa kuwachuja, hivyo kauli hizo zinaonyesha kuingilia mamlaka hizo na wanaozisimamia.
Alisema ameshangazwa na kinachojitokeza katika uchaguzi wa mwaka huu wagombea wa CCM badala ya kutangaza nia na kuomba wadhamini wao wanafanya kampeni kabisa utafikiri wameshapitishwa.
“Hii ni hatari kwa siasa, watu kufanya mambo kwa kutokuzingatia taratibu siyo jambo jema, nahisi kuna kitu hakipo sawa huko, wanapaswa wajichunguze na kuacha wahusika wafanye kazi yao badala ya wao kuwa majaji,” alisema Dk Tily.
Mhadhiri wa UDSM, Dk Benson Bana alisema anayachukulia hayo kama majigambo ya wanachama kutafuta nguvu na kujiamini na kwamba haoni kama kuna shida, kwa sababu mwisho wa siku watajulikana nani anabaki na nani anaondoka katika kinyang’anyiro hicho.
“Ninachoomba kifanyike hapa ni kamati kufanya kazi yake bila kupindapinda wala kumuogopa mtu, kwani inaonekana wazi kuna ambao wanajinadi wakiwa na lengo la kutafuta nafasi huko mbele ya safari ili wasiachwe na atakayeshinda, kutengeneza historia katika maisha yao, pia wapo wenye nia ya kweli,” alisema Dk Bana.

Saturday, 20 June 2015

CCM imejali fedha za wagombea siyo demokrasia

Tangu Chama cha Mapinduzi (CCM) kilipofungua milango kwa makada wake wanaojiona wana sifa ya kuwania urais wakachukue fomu, wananchi wameshuhudia msururu mrefu wa makada hao wakitangaza nia kwenye mikutano ya hadhara na pili wakichukua fomu za udhamini.
Waliochukua fomu za udhamini hadi sasa wamefikia 38 na wanapita mikoani kutekeleza sharti la kudhaminiwa na wanachama 450 kutoka katika mikoa 15.
Upande mmoja ni jambo linalofurahisha kuona makada hao wakitumia haki yao ya kikatiba na kidemokrasia kushiriki katika mbio za kuwania urais. Pia kinadharia, ni jambo lenye afya kwamba kamati za uteuzi zitapata wigo mpana wa kuwachuja hadi kumpata anayefaa, kwa kuzingatia sifa zinazohitajika, kwa nafasi hiyo nyeti.
Upande wa pili, utitiri wa wagombea hao, ni ushahidi kwamba chama hakina tena mfumo wa kuandaa viongozi wake ila kinasubiri wazuke tu na kuifanyia sitihizai nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini.
CCM inajua kuwa nafasi ya urais ni nyeti lakini miongoni mwa waliotozwa Sh1 milioni na kupewa fomu ni wanaokosa sifa kabisa kama kada ambaye elimu yake ni ya msingi tu wakati kiwango cha elimu kinachohitajika ni shahada, na mwingine mwenye umri ulio chini ya miaka 40 inayotakiwa kikatiba.
Hata kama, makada hao wanatimiza haki yao kidemokrasia, CCM wanapokeaje fedha za fomu kutoka kwa makada ambao kimsingi hawana sifa ya urais? Hapa CCM imejali zaidi fedha na siyo demokrasia. Ikiwa katika jambo lililowazi kiasi hiki CCM imevurunda, si itavurugwa na utitiri wa wagombea hao wakati wa kumpata kada anayefaa kuwania urais?
Makada wengine waliopewa fomu ili waingie kwenye mchujo ni naibu mawaziri na mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Nne; baadhi yao wameteuliwa hivi karibuni na hawajafanya kitu cha maana na wengine wamekuwa mizigo. Mbali ya hao, wapo waliotajwa wazi katika kashfa kubwa za ufisadi.
Hao wote wanapita mikoani kuomba udhamini wakiikosoa Serikali ilivyoshindwa kupambana na rushwa na kukusanya kodi na ilivyoshindwa kuboresha huduma za jamii kama elimu, afya na kuwapa ajira vijana. Baadhi yao wanajipigia debe kuwa hakuna mwingine anayefaa isipokuwa wao.
Vilevile, baadhi ya wagombea wanatumia wapambe kuhonga wanachama ili wafurike kwa wingi kudanganya umma kuwa wanadhaminiwa na wengi kwa madai wanapendwa; baadhi ya wagombea wamefanyiwa fujo hadi mmoja kupigwa na vijana wa tawi la ulinzi la chama hicho maarufu kama Green Guards.
Yanapofumbiwa macho, mambo haya ambayo yanakidhalilisha peupe chama hicho kikongwe tena na makada wake, ni ishara mbaya kuelekea kumpata mgombea atakayekuwa na uwezo wa kuunganisha kambi zinazopingana ndani ya chama, kujitenga na matajiri na kuongoza nchi kwa utulivu.
Tunapenda kuwakumbusha viongozi wa CCM kwamba wakati Mwalimu Julius Nyerere anastaafu alisema; “Bila CCM imara nchi itayumba.” Na kwa kuwasaidia wakati wa uteuzi wa mgombea urais mwaka 1995 alipendekeza wote waliotajwa katika vyombo vya habari kuwa wanahusika na kashfa za kisiasa au za rushwa waondolewe ili wabaki walio safi tu, na pia mgombea wa CCM asiwe mwenye kukumbatia matajiri.
Leo ni tofauti, tunachokiona ndani ya CCM kinatia shaka kwani licha ya utitiri huo mrefu wa wagombea urais tunadhani chama hicho kilipaswa kujua sifa za awali za wagombea wake kabla ya kuchukua fedha.Mathalani jambo la umri na elimu ni sifa ambazo zipo wazi, je kulikuwa na sababu gani ya kuchukua fedha kutoka kwa wagombea ambao tayari wanaonekana kukosa hata sifa za msingi kabisa.

Thursday, 18 June 2015

Prof Lipumba, Zitto DK Slaa, kuvaana kwenye mdahalo

Dar es Salaam. Umoja wa watendaji wakuu wa kampuni wa CEO RoundTable (CEOrt) umeandaa mdahalo wa kuzungumzia mbio za urais utakaowahusisha viongozi wa vyama vya upinzani, Profesa Ibrahim Lipumba, Dk Willibrod Slaa, Zitto Kabwe na Emmanuel Makaidi, lakini Chadema imesema itakuwa tayari kwa midahalo baada ya mchakato wa ndani kukamilika.
Kauli hiyo ya Chadema inaweza kuwa kikwazo kingine kwa CEOrt kuendesha midahalo hiyo baada ya wa kwanza uliokuwa uhusishe makada 10 wa CCM wanaoomba ridhaa ya chama hicho kuwania urais, kushindwa kufanyika kutokana na viongozi wa sekretarieti kutoa kauli tofauti siku moja kabla.
Kiongozi wa CEO, Ali Mufuruki alisema jana kuwa Dk Slaa, Profesa Lipumba, Makaidi na Zitto, ambaye ni kiongozi mkuu wa ACT-Wazalendo, wamethibitisha kushiriki kwenye mdahalo huo utakaofanyika kesho kuanzia saa 1:00 jioni jijini Dar es Salaam.
Lakini Dk Slaa aliiambia Mwananchi jana kuwa Chadema itakuwa tayari kushiriki kwenye midahalo baada ya kumaliza mchakato wa kupata mgombea wake na kukamilisha Ilani ya Uchaguzi, mambo ambayo alisema hupitishwa na vikao vya juu.
“Kamanda, sijui kama ni kongamano au mdahalo: 1. Chadema inaendeshwa kwa katiba, kanuni na taratibu zake. Hadi siku ya leo taratibu zetu hazijafikia kupata aspirants (watangazania),” alisema katibu huyo mkuu wa Chadema katika ujumbe wake mfupi wa simu.
“2. Kama kuna waliopata aspirants, Chadema bado mchakato wetu unaendelea. 3. Midahalo inafanywa kwa msingi wa ilani. Chadema ilani yetu haijafika bado mbele ya vikao vya maamuzi, yaani Baraza Kuu na Mkutano Mkuu. Hivyo tukienda mdahalo tutakuwa tunazungumzia ilani ipi?
“Hivyo tuko tayari kwa midahalo yote baada ya mchakato wetu wa ndani kukamilika.”
Mufuruku alikuwa ametuma taarifa hiyo kwenye ukurasa wake wa facebook na alipopigiwa simu na Mwananchi, alithibitisha kuwapo kwa mdahalo huo ambao alisema utaonyeshwa moja kwa moja na vituo vya televisheni, redio na intaneti.
Kuhusu ushiriki wa Zitto, ambaye atagombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Mufuruki alisema CEOrt imemualika kwa kuwa ni kiongozi wa chama ambacho kinaweza kusimamisha mgombea wa urais.
“Kushiriki si lazima uwe unachukua fomu za kugombea urais. Yeye ni kiongozi wa chama ana mawazo yanayoweza kutoa mchango kwenye mdahalo,” alisema Mufuruki.
CEOrt imepanga kufanya midahalo kadhaa mwezi huu na Juni 25 itaendesha mdahalo utakaoshirikisha wagombea kutoka CCM baada ya kada mmoja tu, Balozi Amina Salum Ali, kujitokeza kwenye mdahalo wa kwanza na hivyo kusababisha uahirishwe.
Profesa Lipumba, ambaye amechukua fomu za kuomba ridhaa ya CUF kupitishwa kugombea urais kwa mara ya tano iwapo jina lake litapitishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliiambia Mwananchi jana kuwa atashiriki kwenye mdahalo huo, kama ilivyo kwa Makaidi ambaye amepitishwa na NLD kuwania nafasi hiyo.zi wa sekretarieti kutoa kauli tofauti siku moja kabla. NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD vimepanga kusimamisha mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vyote, lakini kila chama kitalazimika kupata mgombea wake ambaye jina lake litapelekwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya kupitishwa kabla ya kuteua mmoja ambaye atawakilisha vyama hivyo kwenye Uchaguzi Mkuu.
ridhaa ya chama hicho kuwania urais, kushindwa kufanyika kutokana na viongozi wa sekretarieti kutoa kauli tofauti siku moja kabla.
Kiongozi wa CEOrt, Ali Mufuruki alisema jana kuwa Dk Slaa, Profesa Lipumba, Makaidi na Zitto, ambaye ni kiongozi mkuu wa ACT-Wazalendo, wamethibitisha kushiriki kwenye mdahalo huo utakaofanyika kesho kuanzia saa 1:00 jioni jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Dk Slaa aliliambia gazeti hili jana kuwa, Chadema itakuwa tayari kushiriki kwenye midahalo baada ya kumaliza mchakato wa kupata mgombea wake na kukamilisha ilani ya uchaguzi, mambo ambayo alisema hupitishwa na vikao vya juu.
“Kamanda, sijui kama ni kongamano au mdahalo: 1. Chadema inaendeshwa kwa katiba, kanuni na taratibu zake. Hadi siku ya leo taratibu zetu hazijafikia kupata aspirants (watangazania),” alisema katibu huyo mkuu wa Chadema katika ujumbe wake mfupi wa simu.
“2. Kama kuna waliopata aspirants (watiania), Chadema bado mchakato wetu unaendelea. 3. Midahalo inafanywa kwa msingi wa ilani. Chadema ilani yetu haijafika bado mbele ya vikao vya maamuzi, yaani Baraza Kuu na Mkutano Mkuu. Hivyo tukienda mdahalo tutakuwa tunazungumzia ilani ipi?
“Hivyo tuko tayari kwa midahalo yote baada ya mchakato wetu wa ndani kukamilika.”
Mufuruki alikuwa ametuma taarifa hiyo kwenye ukurasa wake wa facebook na alipopigiwa simu na Mwananchi, alithibitisha kuwapo kwa mdahalo huo ambao alisema utaonyeshwa moja kwa moja na vituo vya televisheni, redio na intaneti.
Kuhusu ushiriki wa Zitto, ambaye atagombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Mufuruki alisema CEOrt imemualika kwa kuwa ni kiongozi wa chama ambacho kinaweza kusimamisha mgombea wa urais.
“Kushiriki si lazima uwe unachukua fomu za kugombea urais. Yeye ni kiongozi wa chama ana mawazo yanayoweza kutoa mchango kwenye mdahalo,” alisema Mufuruki.
CEOrt imepanga kufanya midahalo kadhaa mwezi huu na Juni 25 itaendesha mdahalo utakaoshirikisha wagombea kutoka CCM baada ya kada mmoja, Balozi Amina Salum Ali, kujitokeza kwenye mdahalo wa kwanza na hivyo kusababisha uahirishwe.
Profesa Lipumba, ambaye amechukua fomu za kuomba ridhaa ya CUF kupitishwa kugombea urais kwa mara ya tano iwapo jina lake litapitishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliiambia Mwananchi jana kuwa atashiriki kwenye mdahalo huo, kama ilivyo kwa Makaidi ambaye amepitishwa na NLD kuwania nafasi hiyo.
NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD vimepanga kusimamisha mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vyote, lakini kila chama kitalazimika kupata mgombea wake ambaye jina lake litapelekwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya kupitishwa kabla ya kuteua mmoja ambaye atawakilisha vyama hivyo kwenye Uchaguzi Mkuu.
Imeandikwa na Goodluck Eliona na Kelvin

Wema Sepetu sasa rasmi katika siasa

Dar es Salaam. Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu (pichani kushoto akiwa na mama yake), ametangaza rasmi nia yake ya kutaka kugombea ubunge wa Viti Maalumu Singida Mjini, kupitia tiketi ya CCM.
Wema alisema kwa muda mrefu marehemu baba yake Balozi Issac Sepetu, alikuwa akimshauri aingie kwenye siasa na sasa ametimiza ndoto za wazazi wake.
Miaka mitano iliyopita, Wema anayekubalika na mashabiki wengi, aliwahi kuweka wazi kuwa yeye ni mkereketwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na mshabiki wa klabu ya soka ya Yanga na kwamba hiyo ndiyo sababu ya yeye kupendelea rangi za njano na kijani.
Akizungumza na kipindi cha redio cha Ala za Roho kwa njia ya simu, usiku wa kuamkia jana, Wema alisema yupo mkoani Singida kwa muda sasa akiendelea na kampeni ili kujitayarisha kuchukua fomu ifikapo Julai 15 mwaka huu.
Alisema anaamini nguvu za Mungu, Watanzania na watu wa Singida watamwamini na kumpa kura zao kwa kuwa sasa ni wakati wa vijana kujipambanua na kusaidia jamii yao.
“Nipo Singida kuhamasisha vijana wajitokeze kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Kupiga Kura, pia huku mimi ni nyumbani na nimejiandikisha tayari, ili ifikapo Julai 15 nichukue fomu. Ninachotafuta ni kuungwa mkono na Watanzania,” alisema Wema.
Alibainisha kuwa anajiamini na hakuna kitakachomshinda, kwani alipoingia katika mashindano ya ‘Miss Tanzania hakutegemea kama ataweza, lakini alifanikiwa, hata alipojitosa kwenye uigizaji akafanikiwa.
“Sasa naingia katika siasa, najua kwamba nitaweza. Mimi ni binadamu, nina mambo yangu, ila naamini hakuna linaloshindikana. Nitagombea ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Inshallah tuombe uzima,” alisema.
Wema alisema kwamba tayari ana kikundi chake cha kampeni akiwamo meneja wake Martin Kadinda sanjari na Petitman Wakuache.
“Nimeshafanya mengi kuhusu kujiandaa na uchaguzi hata kampeni, nilikuwa nazungumza na uongozi wangu ambao yupo Martin Kadinda pia yumo Petiman, huyu anahusika na kampeni yangu kwa hiyo Watanzania wajue tu kwamba nitachukua fomu ya kugombea ubunge wa Viti Maalumu na tutaona huko mbele itakavyokuwa kwa sababu hiki ni kinyang’anyiro,” alisema Wema.
Wema alisema kwamba kwa sasa ni kama anaingia kwenye mapambano yaliyo sawa na vita hivyo kuna kupata na kukosa.
“Lakini sifikirii kukosa kwa sababu mtu ukifikiri kukosa unajiweka kwenye ‘negative side’, lakini najua kwa nguvu za Watanzania na kwa nguvu za wananchi wa Singida, wataniamini na kunipa kura zao,”alisema.
Wema alifafanua kwamba licha ya kuungwa mkono na wanaume wengi mkoani humo, kinamama wa Singida pia wanamuunga mkono kwani wanamfahamu vizuri na sera zake wanazijua, hivyo ahofii kelele za watu wa pembeni.
“Nitaingia bungeni kwa ajili ya maslahi ya wananchi na kutetea haki za wananchi wangu, si kingine. Wamejitokeza watu wengi kwa ajili ya kugombea, kwa nini amejitokeza Wema Sepetu na watu wameanza kuzungumza mambo mengi?” alihoji.
Katika mahojiano hayo Diva alimuuliza Wema Sepetu kuhusu taarifa ya kuwa na uhusiano na rafiki wa kiume wa Linah alisema:
“Huwezi kuamini, habari hizo siyo za kweli kwa sababu tulikuwa tunafanyakazi naye tu, ila nimeshangazwa kuona kwa nini Linah ameenda hewani kwenye kipindi na kuzungumza hizo habari, naomba watu waelewe kwamba si kweli.”

Serikali yatangaza nafasi za kazi 1,100

Serikali kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi za kazi 1,134 katika sekta mbalimbali za ofisi za umma.
Kwa mujibu wa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi nafasi hizo za kazi ambazo zinapatikana katika tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ya www.ajira.go.tz ni kwa ajili ya waajiri mbalimbali wa ofisi za umma.
Katibu alifafanua kuwa nafasi 949 ni kwa ajili ya waajiri walioainishwa katika ofisi za wizara, halmashauri na nyingine 185 ni za taasisi na wakala mbalimbali za Serikali.
Aidha, amewataka waombaji wote wa fursa za ajira kufungua matangazo yote mawili ya kazi na kuzingatia masharti ya Matangazo yote kama yalivyo katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili kabla ya kutuma maombi yao Aprili 9, 2013.
Daudi alifafanua kuwa waajiri ambao watatoa ajira hizo ni makatibu wakuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Maendeleo Jinsia na Watoto, Wizara ya Kazi na Ajira na Ofisa Mtendaji Mkuu Wakala wa Vipimo.
Wengine ni Makatibu wakuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi, Wizara ya Maji na Katibu Ofisi ya Rais Maadili.
Wengine ni Makatibu Tawala wa Mikoa ya Kagera, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Mwanza, Shinyanga, Manyara, Dar es Salaam, Morogoro, Geita, Pwani, Mara, Kilimanjaro, Lindi, Singida, Tabora, Tanga, Katavi na Arusha; pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za majiji na manispaa Mwanza, Iringa, Songea, Shinyanga, Morogoro, Singida, Kigoma/ Ujiji na Temeke.
Nafasi nyingine ni kwa ajili ya wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya Mufindi, Kyela, Rungwe, Mbeya, Chunya, Biharamulo, Bukoba, Muleba, Namtumbo, Songea, Morogoro, Makete, Mkuranga, Mbinga, Tunduru, Ukerewe, Sengerema, Ilemela, Busega, Maswa na Meatu.
Nyingine ni Wilaya za Shinyanga, Kishapu, Kilosa, Msalala, Rufiji, Rorya, Ruangwa, Lushoto, Mkinga, Mpanda, Monduli, Ngorongoro, Kigoma, Nachingwea, Rombo, Same, Singida, Urambo, Tabora, Babati, Mbulu, Simanjiro na Kiteto.
Pia zimo Wilaya za Handeni, Pangani, Kibondo, Chamwino Mtwara, Nanyumbu, Mpwapwa, Kongwa na Tandahimba pamoja na halmashauri za miji ya Njombe na Kibaha. Nafasi nyingine ni za Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) na Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa).
Nafasi hizo zilizotangazwa zimegawanyika katika kada zifuatazo; Mchambuzi Mifumo ya Kompyuta daraja la II – (nafasi 10), Ofisa Vipimo II – nafasi 6, Mpima Ardhi, daraja la II (nafasi 26), Mhandisi daraja la II – Ufundi Umeme – Nafasi 9, Ofisa Mipango Miji daraja la II– nafasi 13 na Mhandisi daraja la II - Ujenzi (Nafasi 16).
Pia wanahitajika wahandisi daraja la II - Maji (Nafasi 13), Ofisa Misitu daraja la II (nafasi 7), Ofisa wa Sheria daraja la II – nafasi 3, Mtakwimu daraja la II – nafasi 8 na nyingine mbalimbali.