Rais Jakaya Kikwete juzi alihutubia Bunge la 10 kwa lengo la
kuliaga na kulivunja rasmi kuashiria kuweka mazingira kwa ajili ya
Uchaguzi Mkuu ambao utatoa Bunge la kumi na moja.
Rais alitumia hotuba yake ya mwisho kwa chombo
hicho cha kutunga sheria kuelezea mafanikio ambayo Serikali ya Awamu ya
Nne imeyapata katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake, lakini pia
akawa muwazi kwa kueleza matatizo ambayo hakuweza kuyafikia, hasa suala
la bei ya mazao kwa wakulima na kushindwa kulifufua Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL).
Tunaungana na Watanzania wengine kumpongeza Rais
kwa jitihada ambazo Serikali yake imezifanya katika nyanja za uchumi,
siasa na jamii na hatuna shaka na takwimu alizozitoa kuelezea mafanikio
hayo.
Ni jambo lisilopingika kuwa alijitahidi kuimarisha
utawala bora, hasa baada ya kuruhusu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Serikali kuwasilishwa bungeni ambayo imesaidia kudhibiti ufisadi
kwenye vyombo vya umma, kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya
usafiri-barabara, bandari na viwanja vya ndege- huduma za afya,
ukusanyaji kodi, demokrasia na Muungano.
Kama alivyosema Rais, si rahisi kumaliza matatizo
yote katika awamu moja na hivyo atakayempokea kijiti ana wajibu wa
kuendeleza hayo atakayoyakuta hadi atakapoishia. Pamoja na kumpongea
Rais kwa hotuba hiyo na mafanikio ya Serikali ya awamu yake, tunadhani
kuna mambo ambayo hayakuwa na mafanikio makubwa au yalifanyiwa kazi
vizuri lakini yanaanza kuonekana kwenda mrama.
Suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar
(SUK) ni moja ya mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Nne, lakini
ni jambo linalosikitisha kwamba Rais Kikwete anaondoka wakati umoja huo
ukiwa na dalili za kumomonyoka.
Matukio ya hivi karibuni kwenye Baraza la
Wawakilishi ni ishara tosha kwamba mambo si shwari Zanzibar na hivyo
badala ya Rais kusifia mafanikio, angechukulia kuwa ni changamoto kubwa
kwa Serikali yake kushindwa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Pia, suala la Muungano halionekani kuwa linaachwa
salama kwa sababu kipindi hiki ndicho ambacho pande hizi mbili
zimerushiana maneno makali yanayoweka ishara mbaya kwa mustakabali wa
tunu hiyo muhimu kwa Taifa.
Ni dhahiri matukio yaliyojiri wakati wa Bunge la
Katiba yanatosha kuweka swali juu ya hatima ya Muungano, hasa baada ya
viongozi wa chombo hicho kushindwa kutafuta suluhu ili kuwa na
maridhiano ambayo yangejenga mazingira mazuri kwa Taifa kusonga mbele
likiwa kitu kimoja.
Pamoja na Rais kusema kuwa anaiacha nchi ikiwa
salama, bado kuna maswali mengi kuhusu usalama huo, amani na utulivu. Ni
kweli kwamba vitendo vya ujambazi vimepungua kulingana na hali
ilivyokuwa mwaka 2005 wakati akiingia madarakani, lakini hali inaonekana
si shwari kwa kuwa uhalifu huo sasa ni dhidi ya polisi na vituo vyao.
Uvamizi wa vituo vya polisi ambao jukumu lao ni
kulinda usalama wa raia, sasa umekuwa ukitokea kila mara, tishio la
ugaidi limeongezeka na vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi
wanapokuwa na madai yao vimeongezeka. Mambo hayo, ukichanganya na ukweli
kwamba takwimu zinazoashiria kukua kwa uchumi, hazionekani kwenye
maisha ya kila siku ya mwananchi wa kawaida, yanazidi kuiweka amani yetu
katika hali ya sintofahamu.
Tunadhani kuwa haya ni mambo ambayo inabidi
yawekwe bayana ili Taifa lijue kuwa pamoja na mafanikio mengine mengi
aliyoyataja mkuu wa nchi, bado tuna changamnoto hizo kubwa na hivyo hata
Rais anayekuja na Serikali yake, anapaswa kujua kuwa nchi ina mzigo
kiasi gani katika kudumisha Muungano, kuendeleza usalama wa raia na
kulinda muafaka uliofikiwa Zanzibar.

No comments:
Post a Comment