Wednesday, 3 June 2015

Ukawa wawaponda waliotangaza nia CCM

Sumbawanga/Dar. Viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wameponda tabia ya makada wa CCM wanaotangaza nia ya kugombea urais kufanya hafla zinazotumia fedha nyingi kwenye jambo dogo.
Viongozi hao wamesema vitendo hivyo vinaonyesha kuwa chama hicho tawala hakichukii ufisadi na hivyo hakiwezi kuwa na mgombea safi.
Makada hao wamelipia muda wa matangazo ya moja kwa moja kwenye vituo vya redio na televisheni, kufanya maandalilizi ya gharama kubwa kwenye sehemu walizotangazia nia, kuandaa vipeperushi na mabango ya thamani huku baadhi wakituhumiwa kusafirisha watu kutoka sehemu mbalimbali kuhudhuria hafla hizo.
Akihutubia wakazi wa Sumbawanga mkoani Rukwa, katibu mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa alisema Serikali ya CCM ni kama ya watu wa ukoo mmoja wenye tabia zinazofanana.
Alisema Serikali imejaa tuhuma nyingi za rushwa na ufisadi na kwamba, kinachotakiwa ni kuinyima kura zote wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Katibu huyo alisema wale wote wanaojitokeza kutangaza nia ni ‘mafisadi’ ndio maana wanatumia nguvu ya fedha kuwanunua Watanzania, jambo ambalo alisema ni kinyume cha maadili.
“Ni hatari sana kuwachagua viongozi kwa fedha, hawa wanataka kuliangamiza Taifa,” alisema.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema anashangaa chama kilichoasisiwa na mjamaa Mwalimu Julius Nyerere, vijana wake wanafanya sherehe kubwa kwenye jambo dogo.
“Hata mwanasiasa mkongwe Kingunge (ngombare Mwiru) anakwenda kuwa mpambe kwenye shughuli inayokiuka taratibu,” alisema na kuongeza kuwa hiyo ni ishara mbaya.
Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi alihoji wanaotumia fedha nyingi kwenye jambo dogo, watazirudishaje.
Alisema kama makada hao walifanya kazi halali, hawawezi kuwa na fedha zinazoweza kugharimia sherehe kubwa kama hizo.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema mfumo mbaya wa CCM ndio unaonyesha chama hicho hakichukii mafisadi.“Kama chama kingekuwa kinachukia ufisadi, kingeandaa utaratibu wake ili watu wote wanaotangaza nia wawe na nguvu sawa,” alisema Mbatia.

Wednesday, 20 May 2015

Ufisadi huu sasa kiama

Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amewasilisha ripoti tano za ukaguzi wa fedha kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2014 akibainisha ufisadi wa zaidi ya Sh600 bilioni katika maeneo mbalimbali na matumizi ya fedha ambayo hayana maelezo ya kutosha.
Ukaguzi huo ulifanywa katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na ufanisi wa maeneo mbalimbali.
Ripoti hizo zinaonyesha jinsi watumishi hewa wa umma wanavyoendelea kulipwa mishahara, wakiwamo wa balozi za Tanzania waliostaafu, misamaha ya kodi na ukiukwaji wa ununuzi na matumizi yasiyoeleweka ya fedha katika Wizara ya Ujenzi na Kitengo cha Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Amina Mwidau na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Rajab Mbaruk Mohamed walizichambua ripoti hizo na kueleza jinsi watumishi wa Serikali wanavyotafuna mabilioni ya fedha.
Akizungumzia ripoti hiyo katika mkutano wa pamoja na CAG, Mwidau alisema imeonyesha jinsi Sh285 bilioni za Kitengo cha Maafa zilivyotafunwa licha ya kuwa zilitengwa kwa ajili ya kufanya shughuli maalumu.
Kuhusu Wizara ya Ujenzi, alisema ililidanganya Bunge baada ya kueleza kuwa Sh262 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara, kitu ambacho kimebainika kuwa siyo kweli.
“Ukaguzi unaonyesha kuwa fedha hizo zimetumika katika mambo mengine kabisa, yaani zimetumika tofauti na hakuna maelezo ya kuridhisha,” alisema Mwidau huku akifafanua kuwa wizara hiyo inadaiwa na makandarasi Sh800 bilioni.
Misamaha ya kodi
Profesa Assad alisema ofisi yake ilibaini kasoro katika mfumo wa ufuatiliaji wa misamaha ya kodi na kusababisha ukiukaji wa matumizi iliyotolewa kwa mafuta yanayotumika migodini.
Alisema mafuta yenye kodi ya Sh22.33 bilioni yaliyotakiwa kutumiwa na kampuni zilizosamehewa kodi, Geita Gold Mine na Resolute TZ Ltd, yalipelekwa kwa makandarasi wasiostahili msamaha na kusababisha hasara ya Sh22.33 bilioni,” alisema.
Alisema pia misamaha ya kodi kwa malengo tofauti na yaliyokusudiwa, ilitolewa na kusababisha upotevu wa Sh392.7 milioni katika Kampuni ya Kiliwarrior Expeditions Ltd ya Arusha iliyokuwa imesamehewa kodi Sh465.2 ili kuingiza magari 28.
Hata hivyo, alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kati ya hizo kukusanya Sh72.5 milioni.
Pia, alisema misamaha ya Sh53.4 milioni ilitolewa kwa Kampuni ya Kilemakyaro Mountain Lodge Limited kwa ajili ya mradi wa ujenzi na upanuzi hoteli katika Kijiji cha Changarawe wilayani Karatu, lakini kampuni iliagiza magari matatu kwa kutumia msamaha na mengine matano ‘kuchepushwa’.
“Hata hivyo, ukaguzi ulithibitisha ununuzi wa gari moja tu ya Hyundai Santa. Magari mengine matano aina ya BMW na Toyota Land Cruiser Prado hayakufahamika yalipo,” alisema. CAG aliishauri Serikali izibe mianya ya upotevu wa kodi kupitia misamaha ya kodi aliyobaini katika ukaguzi wa mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa misamaha ya kodi iliyotolewa.
Mashine za EFD
Alisema katika ukaguzi wa malipo na matumizi  ya mashine za kielektroniki (EFD), ofisi yake ilibaini kuwa kampuni binafsi hazitumii mashine hizo za kutolea stakabadhi.
Alisema hali hiyo imesababisha malipo ya Sh4.4 bilioni kutokuwa na stakabadhi za kielektroniki kwa taasisi za Serikali Kuu na Sh4.6 bilioni kwa sampuli  22 ya mamlaka za serikali za mitaa.
“Katika suala hili, TRA ilitoza faini Sh440.8 milioni kwa wafanyabiashara ambao walishindwa kutumia mashine za EFD ambapo jumla ya Sh72 milioni zililipwa sawa na asilimia 16 na hivyo kufanya bakaa ya Sh369 milioni ambayo haikulipwa,” alisema.
Alisema pia ukaguzi ulibaini upungufu katika usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali kama vile, malipo yasiyokuwa na nyaraka. Upungufu mwingine ni hati za malipo ambazo hazikuwasilishwa kwa ukaguzi, fedha zilizotumika nje ya bajeti, matumizi yasiyokuwa na manufaa na malipo ambayo hayakuidhinishwa na maofisa masuuli.
Alishauri taasisi za Serikali zisiendelee kanunua vifaa na huduma kwa wafanyabiashara wasiotumia mashine za EFD kutoa stakabadhi ya kukiri kupokea fedha.
“Hii iende sambamba na kuhakikisha kuwa maofisa masuuli wanaimarisha mfumo wa udhibiti wa ndani ikiwa pamoja na kuimarisha ukaguzi kabla ya malipo,” alisema.
Mishahara hewa
Alisema fedha zilizolipwa kwa watumishi hewa wa Serikali Kuu ni Sh141.4 milioni, “Hali hii inaendelea licha ya kuwa Serikali imewekeza kwenye mfumo wa Lawson kama njia mojawapo ya kudhibiti hali hiyo,” alisema. Hata hivyo, alisema suala hilo linazidi kupungua ikilinganishwa na mwaka jana. Lakini alisema Sh1.01 bilioni katika halmashauri 36 zililipwa kama mishahara kwa watumishi waliotoroka kazini, waliofariki, waliostaafu na kufukuzwa kazi.
Alisema kutokana na watumishi hewa, Sh845 milioni za halmashauri zililipwa kama makato ya taasisi mbalimbali kama vile mifuko ya pensheni, taasisi za fedha, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na TRA kwa ajili ya wafanyakazi hao hewa.
Katika balozi
CAG pia ameeleza jinsi Serikali ilivyolipa Sh543.7 milioni kutokana na kuwalipa watumishi wa balozi za Tanzania waliostaafu, waliokuwa wakifanya kazi bila kuwa na mikataba kutokana na changamoto za malipo ya kurejeshwa nyumbani.
Watumishi hao ni wa balozi za Tanzania Kinshasa (DRC), Maputo (Msumbiji), Ottawa (Canada) na Washington DC (Marekani).
Ripoti hiyo inaonyesha tarehe ambazo watumishi hao walistaafu, lakini Serikali iliendelea kuwalipa huku wakiwa katika maeneo yao ya kazi, zikijumuisha kodi za majengo huku baadhi ya watumishi hao wakifanya kazi licha ya kuwa mikataba yao kumalizika.
Ufisadi Tanesco
Ripoti hiyo pia ilibaini kuwapo kwa ununuzi wa Sh3.2 bilioni uliofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), bila kuzingatia kiasi kilichotengwa kwenye bajeti ya Sh400 milioni.
“Katika zabuni nyingine, Tanesco iliingia mkataba wa Sh340 milioni ambayo ni zaidi ya bajeti iliyotengwa ya Sh154 milioni. Ukaguzi haukuweza kupata ushahidi wa kuwapo kwa marejeo ya bajeti kwa kiasi kilichotumika nje ya makisio,” alisema
Vyama vya siasa
Kuhusu ukaguzi wa vyama vya siasa, CAG alisema hadi kufikia Juni, 2013 vyama 21 wakati vinakaguliwa, ni 12 tu ndivyo vilivyowasilisha taarifa za hesabu.Alisema kati ya vyama 12, tisa havikuwasilisha taarifa za hesabu ambavyo ni UPDP, Tadea, UDP, Demokrasia Makini, Chausta, DP, Jahazi Asilia, AFP na CCK.
Alisema katika ukaguzi huo, ilibainika kuwa vyama sita vya siasa vilipata hati ya shaka ambavyo ni CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na Chauma na vya vingine vilipata hati mbaya ambavyo ni NRD, UMD, ADC, APPT, NLD na SAU.
Alishauri Msajili wa Vyama vya Siasa akishirikiana na Mhasibu Mkuu wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), waandae mwongozo wa aina ya muundo wa taarifa za fedha utakaotumiwa na vyama vyote vya siasa.
Bajeti
Kuhusu bajeti, alisema tathmini waliyofanya kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, programu na shughuli nyingine za maendeleo katika baadhi ya halmashauri, imeonyesha kuwa hadi kufikia Juni 30, mwaka jana, halmashauri hizo zilikuwa na bakaa ya jumla ya Sh29.2 bilioni sawa na asilimia 28 ya jumla fedha zilizotolewa.
Alisema kubakia kwa kiasi kikubwa cha fedha bila kutumika katika utekelezaji wa miradi kunatokana na ucheleweshaji wa kutuma fedha katika halmashauri.
Deni la Serikali
Alisema hadi kufikia Juni 30, mwaka jana, deni la mifuko ya hifadhi ya jamii lilikuwa limefikia Sh1,699 milioni na Sh975.1 milioni zilipaswa kuwa zimereshwa, lakini hadi wakati wa kuandika ripoti hiyo zilikuwa bado hazijalipwa.
Alishauri mifuko na Serikali kuzingatia na kufuata mwongozo wa uwekezaji wa fedha za mifuko ambao pamoja na mambo mengine, unatoa ukomo wa aina za mali ambazo mifuko inaweza kuwekeza.

Monday, 18 May 2015

UCHAGUZI UPINZANI 2015: Anna Mghwira, Mwenyekiti ACT- Wazalendo

Historia yake
Anna Mghwira ni Mwenyekiti wa kitaifa wa chama kipya cha siasa, ACT – Wazalendo. Alizaliwa Januari 23, 1959 katika hospitali ya Mkoa wa Singida, Kata ya Mungumaji, Kitongoji cha Irao Manispaa ya Singida Mjini. (Januari mwaka huu alitimiza miaka 56).
Baba mzazi wa Anna alikuwa diwani na kiongozi wa Tanu kabla ya CCM hadi mwaka 1985, mama yake alijishughulisha na kilimo na ufugaji na wazazi hawa kwa ujumla walipata watoto tisa, akiwamo Anna.
Mgwira alianza safari ya kielimu katika Shule ya Msingi Nyerere Road mwaka 1968 – 1974 akaendelea na sekondari kwenye Shule ya Ufundi Ihanja kati ya mwaka 1975 – 1978 kabla ya kuhitimisha masomo ya juu ya sekondari (kidato cha V na VI) Lutheran Junior Seminary kati ya mwaka 1979 – 1981.
Aliendelea na masomo ya chuo kikuu mwaka 1982 baada ya kujiunga Chuo Kikuu cha Thiolojia (Chuo Kikuu cha Tumaini) na kuhitimu Shahada ya Thiolojia mwaka 1986.
Mwaka huohuo, alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea shahada ya Sheria.
Kati ya mwaka 1987 – 1998, aliendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa, akifanya kazi ndani na nje ya nchi na kupata uzoefu mkubwa.
Safari ya elimu ya Mghwira ilikamilikia Chuo Kikuu cha Essex, Uingereza ambako alianza Shahada ya Uzamili ya Sheria (LLM) mwaka 1999 na kutunukiwa mwaka 2000.
Licha ya kuwa mwanasheria na mtheologia aliyebobea, pia amefanya kazi za maendeleo kwa muda mrefu na ana uzoefu katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa, utumishi katika mashirika ya kimataifa, kitaifa na mashirika ya dini ambamo amejihusisha na masuala ya wanawake, watoto, wakimbizi, utawala na haki za binadamu.
Mghwira ana historia ya kupenda siasa, masuala ya jamii na michakato ya maendeleo kama inavyojidhihirisha katika maandiko yake mbalimbali katika majarida na magazeti ya hapa ndani ya nchi.
Alianza siasa tangu wakati wa Tanu akiwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu Youth League) na aliwahi kushinda tuzo mbalimbali kutokana na ushiriki wa juu katika Tanu lakini baadaye ilipoanzishwa CCM alipunguza ushiriki wake ili ajipe muda katika masomo na baadaye ndoa na malezi ya watoto.
Kwa kipindi kirefu, hakuwa anajihusisha na siasa hadi alivyoamua kujiunga na Chadema mwaka 2009 ambako alishika nafasi mbili tu za uenyekiti wa baraza la wanawake  ngazi ya wilaya na katibu wa baraza la wanawake mkoa.
Machi mwaka huu alijiunga rasmi na ACT – Wazalendo na katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa chama hicho, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa ACT.
Aliolewa na Shedrack Maghwiya tangu mwaka 1982 na walibahatika kupata watoto watatu wa kiume: Fadhili, Peter na Elisha. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, mumewe hivi sasa ni marehemu.
Mbio za ubunge
Mghwira alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza Januari 2012 baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki baada ya kifo cha Solomon Sumari.
Alishiriki kura ya maoni ndani ya Chadema akihitaji kupewa ridhaa. Hata hivyo, chama hicho kilimpitisha Joshua Nassari (Josh) na Mghwira alikuwa na kazi ya kuendelea kumuunga mkono hadi ushindi ulipotangazwa kwa chama hicho.
Pia, amewahi kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, kupitia Chadema japokuwa hakuchaguliwa kushikilia wadhifa huo.
Mbio za urais
Mghwira hajatangaza kuwa atagombea urais. Ila, tafiti kadhaa na maoni ya Watanzania zinaonyesha kuwa yeye ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa ambao wamejipambanua hivi karibuni na kuonyesha uwezo mkubwa katika uwanja wa kisiasa na hivyo anapewa nafasi kubwa kuwa anaweza kupewa majukumu makubwa na anaweza kuyahimili.
Nguvu yake
Jambo la kwanza linalompa nguvu mwanamama huyu ni umahiri katika elimu. Yeye ni msomi nguli wa masuala ya sheria lakini ana shahada tatu za vyuo vikuu. Nchi yoyote ingependa pamoja na sifa nyingine, iongozwe na Rais ambaye elimu si kikwazo kwake. Kwa nchi kama Tanzania ambayo mfumo dume umewakandamiza wanawake kwa kipindi kirefu, Mghwira anakuwa mmoja wa wanawake wachache wenye uwezo mkubwa.
Kwa sababu Mghwira ni mwanamke imara na anayepambana kwa muda mrefu sasa. Kitendo tu cha yeye kuwa mwanamke ni baraka tosha kwa siasa za kisasa ambazo zinaanza kuchangamkia, kukubali na kutafuta mchango wa wanawake katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Jinsia yake inampa fursa ya kuendelea kuaminiwa zaidi katika jamii ambayo inazidi kupoteza imani na uaminifu wa wanaume.
Lakini nguvu ya tatu ya Mghwira ni uthubutu. Ameniambia kuwa hata alipoingia katika ndoa bado alithubutu kujiendeleza kielimu bila kuchoka. Alipambana na changamoto za ndoa na shule. Wanawake wengi huchagua kufanya jambo moja na kuacha mengine, yeye alikwenda nayo yote na kuyakamilisha salama. Uwezo na uthubutu huu vinamfanya kuwa mwanamama imara anayeweza kukabidhiwa uongozi wa taasisi kubwa.
Mghwira ni mtu wa kuhoji kila jambo, si mwanamama “Ndiyo Mzee”. Wakati natafuta maoni ya watu waliowahi kufanya naye kazi katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, mtendaji mmoja aliniambia kuwa ukimpa Mghwira kazi ya harakati iliyo kwenye maandishi, hataondoka kwako hadi umpe taarifa za kina za kila jambo na atakuhoji hadi utachoka.
Hata mtaalamu mshauri wa chama hicho Profesa Kitila Mkumbo ameniambia kuwa wakati wanafanya marekebisho ya katiba ya chama cha ACT walikabidhi kazi hiyo kwa jopo maalumu la wataalamu akiwemo Mghwira.
Profesa Kitila ananiambia kuwa kwa kiasi kikubwa katika timu hiyo, Mghwira ndiye aliyehoji na kutoa mapendekezo ya masuala mengi kuliko hata wataalamu wengine wa sheria ambao walikuwa wanaume.
Nilipojaribu kumfikia Mghwira kwa ajili ya kupata taarifa zake za kina na maisha binafsi, nilijikuta nashushiwa maswali matano mfululizo kiasi kwamba nilirudi kujipanga na kumtafuta tena. Huyu ni mwanasiasa wa kisasa ambaye anahoji kila jambo lililoko mbele yake, sifa hii wanaikosa wakuu wengi wa nchi.
Pamoja na kuwa na elimu kubwa, uzoefu wa kutosha wa kukaa nje ya nchi na kufanya kazi na taasisi za kitaifa na kimataifa, Mghwira ni mwanamama wa kawaida sana. Watu wa karibu naye wanamtaja hivyo. Si mtu wa kupoteza muda na mambo yasiyo na tija, anapenda kuandika makala za kuelimisha jamii, kufanya kazi na jamii na kujitolea na kujichanganya na wananchi wasio na uwezo na wenye kuhitaji msaada. Sifa zote hizi ni nguvu muhimu kwa binadamu yeyote ambaye anahitaji uongozi mkubwa wa nchi.
Udhaifu wake
Udhaifu mkubwa nilioubaini na hata kujulishwa na watu wa karibu naye ni kuwa yeye ni mwanasiasa mpole sana. Nimeambiwa kuwa ni mpole kupita kiasi na mara nyingi huwa anakuwa msikilizaji mzuri kabla hajaanza kuhoji mambo mfululizo. Moja ya sifa muhimu za Rais ajaye ni uwezo wa kuwa mpole na mkali kutegemeana na mazingira.
Kiwango cha upole cha mwanamama huyu kinazidi kiwango cha ukali alionao na naliona kama ni jambo linalopaswa kufanyiwa kazi kwa sababu Taifa letu lilipofikishwa, mara kadhaa nimesisitiza kuwa tunahitaji kiongozi anayeweza kumudu hali zote mbili.
Lakini udhaifu wa pili mkubwa wa Mghwira ni kutojijenga kisiasa ndani ya nchi. Katika siasa, bado namuona kama mchanga, hajakomaa na kuwa na uwezo mkubwa kiasi cha kujipa jina kubwa kwa jamii.
Mchango wake katika jamii ni mkubwa kwa sababu amewahi kusimamia masuala mengi ya kijamii na kisheria yanayoonekana, lakini ninachokisema hapa ni kuwa, chama chochote kile kina jukumu la kusimamisha kiongozi ambaye anajulikana katika tasnia za siasa. Kutojijenga na kuwa juu tokea alipokuwa Chadema nakuchukulia kama udhaifu ambao anahitaji kuufanyia kazi.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Kama ACT - Wazalendo kitampitisha mwanamama huyu kuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, sababu ya kwanza ya kufanya hivyo inaweza kuwa ni ile dhana ya kumpa mwanamke nafasi.
Chama anachotoka ndicho peke yake kimeweza kumpa mwanamke nafasi ya juu ya uongozi, nadhani pia bado chama hicho kinaweza kumpa jukumu kubwa zaidi ya hilo kwa sababu tayari kimeshajijengea misingi ya kuwajenga kina mama.
Lakini ikiwa Mghwira atapitishwa, uzoefu wake kimataifa na katika masuala ya haki za binadamu na kushughulika na masuala ya kijamii kunaweza kuwa moja ya sababu.
Mwanamama huyu amefanya kazi mbalimbali za kitaaluma na kijamii hapa Tanzania, Sweden, Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Afrika. Amekuwa mwalimu wa vyuo vikuu hapa Tanzania na msimamizi wa miradi mbalimbali ya kitaifa ya mashirika ya ndani na nje ya nchi. Uwezo na uelewa wake vinampa fursa ya juu ya kuteuliwa kugombea urais na kuonyesha kuwa kina mama wanaweza ikiwa wanapewa fursa sawa na wanaume.
Nini kinaweza kumwangusha?
Dhana ileile ya kijinsia inayombeba, pia ndiyo inayoweza kumuangusha. Ikiwa ACT kitadhani kuwa vyama vingine washindani vitasimamisha wagombea wanaume imara ambao wanaungwa mkono na mfumo dume uliotawala nchi hii, chama hicho kinaweza kumuweka nje Mgwira na kutafuta mwanachama mwingine “mwanamume” ambaye atakuwa na fursa ya kupambana na wanaume wengine kutoka vyama vingine na kuangaliwa na jamii “ambayo kwa kiasi kikubwa bado inatawaliwa na wanaume”.
Lakini jambo la pili linaloweza kumwangusha ni ugeni wake katika masuala ya kisiasa. Kama nilivyoeleza, Mghwira hana uzoefu wa uongozi wa juu wa kisiasa katika vyama, nadhani nafasi aliyonayo ndani ya ACT - Wazalendo ndiyo inayompa uzoefu wa kwanza wa siasa za kitaifa.
Lakini uzoefu wa jumla unaonyesha kuwa vyama mbalimbali hapa Tanzania huteua wagombea urais wake miongoni mwa wanachama wazoefu au wale waliowahi kushika madaraka muhimu katika chama kwa muda mrefu. ACT ikipiga hesabu hizi inaweza kabisa kumuweka nje mwanamama huyu.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Ikiwa hatapewa fursa ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chake, anaweza kuwa na mipango mitatu mezani:
Mpango wa kwanza ni kugombea ubunge katika jimbo mojawapo Tanzania. Bahati nzuri nimejulishwa kuwa moja ya majimbo anayojipanga kugombea ni pale Singida. Ikiwa ndivyo basi, mpango huu unaweza kumfaa kwa maana ya kuzidi kujifunza na kupata uzoefu wa siasa za Tanzania kwa upana.
Lakini mpango wa pili ni kuendelea kufundisha vijana katika vyuo vikuu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri kwa wanafunzi na wa kisheria katika jamii. Katika masuala haya ana uzoefu mkubwa nayo na itakuwa tu ni kiasi cha kuendelea pale alipoishia.
Nadhani mpango wa tatu ni kuendelea kuongoza chama cha ACT - Wazalendo. Nimeambiwa kuwa uongozi (Uenyekiti wake) unapaswa kuisha Februari, 2020. Ikiwa ndivyo nadhani ana fursa njema ya kuendelea kufanya uongozi.
Hitimisho
Mgwira ni mwanasiasa na kiongozi wa chama kipya ambacho kimeanzishwa na wanachama wengi waliotoka Chadema. Safari yake kisiasa na hata ugombeaji wa nafasi nyingine kubwa za nchi kwa namna moja au nyingine, lazima utaathiriwa na ustawi au uzorotaji wa Chadema.
Ikiwa Chadema kitazidi kukubalika kwa Wwatanzania na kuwa chama kinachoimarika zaidi kuishinda ACT, ndiyo kusema kuwa yeye na wenzake watakuwa na wakati mgumu kujipambanua kisiasa na hivi ndivyo siasa za Afrika hutizamwa.
Pamoja na sintofahamu hizo, namuona Mgwira kama mmoja wanasiasa watulivu na wenye maono mapana katika Taifa hili. Kwa maneno yake yeye mwenyewe amenieleza kuwa “Natamani siku moja nchi hii iongozwe kwa misingi ya udugu na kusaidiana, kwa misingi ya malezi ya maadili bora kama alivyofanya Mwalimu Nyerere. Mimi nimekulia kwenye familia kubwa sana lakini wazazi wetu walitulea sote kama ndugu na tuliishi kwa furaha kubwa, nina ndoto kuwa Tanzania ijayo ipite katika njia hiyo.”
Ninachoweza kusema kwa sasa ni kumwombea mama huyu nguli wa upinzani na kumtakia safari njema katika nia zake za kisiasa ikiwamo hii ambayo ametajwa kwamba ana sifa za kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii; ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa (B.A) katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana kupitia +255787536759.

Urais wawagonganisha NCCR-Mageuzi, Chadema

Dar es Salaam. Chama cha NCCR-Mageuzi kimeponda kauli ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu kwamba Katibu mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani, Dk Willibrod Slaa ndiye atakayekuwa mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema mjini Moshi, hivi karibuni, Lissu alikaririwa akieleza kuwa Dk Slaa, ndiye atakayepitishwa na Ukawa kugombea nafasi hiyo.
Lakini Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi wa NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura aliliambia gazeti hili mwishoni mwa juma kuwa ni makosa kudhani kwamba Chadema ndicho chenye nafasi ya kusimamisha mgombea urais kupitia Ukawa, wakati bado mchakato wa kumpata mgombea haujafanyika.
Sungura ambaye pia ni miongoni mwa waasisi na mwanzilishi wa mageuzi nchini, alisema kati ya vyama vinne vilivyounda Ukawa, tayari Chadema imepewa majimbo mengi ya ubunge. “Fursa hiyo pekee imeshawapa uwezekano wa kutoa waziri mkuu kama upinzani utashinda”, alisema.
“Kwa kawaida chama chenye wabunge wengi ndicho kinachotoa waziri mkuu, sasa kwa namna yoyote Chadema ndiyo itakayotoa waziri mkuu, hivyo haiwezekani watoe na mgombea urais. Nawashauri wachague nafasi mojawapo,” alisema Sungura.
Sungura alisema kauli hiyo ya Lissu siyo sahihi na hailengi kujenga Ukawa, bali kuubomoa kwa kuwa haiwezekani chama kimoja kitoe rais, makamu wake na waziri mkuu. “Ni vizuri ikaeleweka mapema kwamba, haiwezekani chama kimoja kati ya vyama vinne washirika wa Ukawa, kikatoa mgombea urais, makamu na waziri mkuu,” alisema Sungura  na kuongeza:
“Kwa kuwa CUF kina nafasi kubwa ya kumtoa mgombea urais wa Zanzibar, vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na NLD, kimoja kati ya vyama hivyo kitamtoa ama rais au waziri mkuu au spika wa Bunge, kinyume chake ni tamaa inayoweza kuua Ukawa.”
Kwa mujibu wa Sungura, mageuzi chanya hayawezi kuletwa kwa ubinafsi, bali nia ya dhati ya Ukawa katika kuyatafuta.

Asimamishwa kazi kwa kumtumia JK ‘meseji

Moshi. Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa KCMC, Paul Mhumba amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kutuma ujumbe wa simu ya mkononi (sms) kwa Rais Jakaya Kikwete.
Kuvuja kwa ujumbe huo na nambari ya simu iliyotuma, kumeibua hisia tofauti kuhusu usiri wa ofisi ya Rais katika kushughulikia malalamiko nyeti ya wananchi na kuwaweka njiapanda watoa habari za siri.
Mhumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (Tughe) Tawi la KCMC anadaiwa  na Menejimenti ya KCMC kuwa ndiye aliyetuma ujumbe huo.
Katika barua yake ya Mei 5, yenye kumbukumbu PF.4515/22, KCMC ilidai uchunguzi umebaini kuwa Mhumba ndiye mtumaji wa ujumbe huo.
“Uongozi umepokea taarifa iliyotumwa mwishoni mwa Aprili na mwanzoni mwa Mei mwaka huu kwa njia ya ujumbe wa simu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete,” ilidai.
KCMC imedai katika barua hiyo, taarifa hiyo ya sms ilibeba ujumbe unaohusiana na matumizi mabaya ya fedha za hospitali hiyo unaofanywa na baadhi ya viongozi na Shirika la Msamaria Mwema (GSF).
Mbali na tuhuma hizo, lakini pia KCMC inadai taarifa hiyo ilimweleza Rais kuwa KCMC na GSF linalomiliki hospitali hiyo, zinajitosheleza kwa mapato, hivyo hakuna haja kwa Serikali kuendelea kuipatia ruzuku.
Pia, menejimenti imedai taarifa hiyo ilidai wafanyakazi wa KCMC wanatumikishwa kama watumwa, hivyo ni maombi yao (watumishi) Serikali ilegeze masharti ili ajira zao zichukuliwe na Serikali.
“Uchunguzi umeonyesha kuwa taarifa hiyo (kwa Rais), umeituma kwa kutumia simu ya kiganjani ambayo ulikabidhiwa kama mojawapo ya zana ya kuleta ufanisi katika majukumu yako,” imedai.
Mei 8, KCMC ilimwandikia barua Mhumba yenye kumbukumbu PF.4515/28 iliyotiwa saini na Profesa Raimos Olomi ikimjulisha kuwa amesimamishwa kazi kuanzia Mei 8 hadi Mei 14.
Katika barua hiyo, Profesa Olomi alidai menejimenti imepokea taarifa ya kutofanyika kwa kikao cha kamati ya nidhamu baada ya Mhumba kumkataa mwenyekiti kutokana na kukosa imani naye.
Pia, kikao hicho hakikufanyika baada ya Mhumba kuomba kamati hiyo iahirishwe kwa sababu mwakilishi wake hakuwapo na kikao kingine kupangwa Mei 15.
Hata hivyo, bado mhasibu huyo hajarejeshwa kazini na vikao vilikuwa vinaendelea kuhusu hatua za kinidhamu zinazostahili dhidi yake.
“Wakati hayo mambo mawili yanafanyiwa kazi, menejimenti imeamua kukusimamisha kazi. Kabla hujaondoka unatakiwa ukabidhi vitendea kazi pamoja na simu ya mkononi uliyokabidhiwa,” imedai.
Ofisa Uhusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo alipoulizwa kuhusu sakata hilo alisema kwa nafasi yake, hawezi kulizungumzia.
Mhumba alipotafutwa wiki iliyopita, alikiri kusimamishwa kazi kwa tuhuma za kumtumia Rais ujumbe wa simu ya mkononi, ingawa alikanusha kuhusika.
“Maudhui hayo kama ni kweli yalitumwa, hayana matatizo. Nimeongea na katibu mkuu kumuuliza kama alipokea sms kutoka kwa Rais na kuwapa KCMC na namba ya mtumaji amekanusha,” alidai.
Hata hivyo, alidai yeye akiwa mwenyekiti wa Tughe, amekuwa akionekana kama adui pale anapojaribu kutetea masilahi ya watumishi, likiwamo suala la kutopandishwa daraja tangu mwaka 2007 hadi 2015.
“Ni kweli, watumishi hawajapandishwa madaraja tangu 2007. Sisi (Tughe) tumekuwa tukilipigania kwa sababu linachangia wastaafu kulipwa pensheni ndogo,” alisema.
“Mimi kama kiongozi wa wafanyakazi, niko tayari kupeleka ushahidi kwa mambo ambayo Tughe tumekuwa tukipambana nayo, ikiwamo mahali zilipo fedha za mashine ya CT-Scan,” alisema Mhumba.
Tawi la Tughe KCMC, limemwandikia barua katibu mkuu wa Tughe, ikiomba Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama aingilie kati suala hilo ili haki itendeke.
Gama alipoulizwa kuhusu suala hilo, alikiri kupigiwa simu na Mhumba akimueleza lakini alimshauri aziandikie mamlaka husika.
Gama alisema akiwa mwakilishi wa Rais mkoani Kilimanjaro, atachunguza nini kimetokea baada ya kupata malalamiko rasmi kutoka kwa Mhumba au Tughe yenyewe.

Friday, 10 April 2015

Bakora sita za Ukawa kwa CCM

Dar es Salaam. Uhakika wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutamba katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utategemea umahiri wake katika kukabiliana na vikwazo sita vinaonekana kuwa mwiba kwake ambavyo upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unatarajiwa kuvitumia kama mtaji wake katika kampeni.
Vikwazo hivyo ni kuwapo kwa makundi ndani ya CCM yanayotokana na mitandao ya urais, hasira za wananchi juu ya mchakato wa Katiba Mpya, tuhuma za ufisadi ama kwa makada au Serikali yake, suala la Mahakama ya Kadhi, ahadi za Rais 2010 ambazo hazijatekelezeka na kuimarika kwa upinzani na muungano wake wa Ukawa.
Hata hivyo, baadhi ya makada wa chama hicho bado wanaona kuwa pamoja na vikwazo hivyo, chama hicho kitapenya katika uchaguzi huo na kuongoza tena Dola kwa kuwa kinao mtaji mkubwa wa wanachama na mtandao wake ni mpana kuliko chama chochote nchini.
Mgawanyiko na makundi
Kwa nyakati tofauti, viongozi wa CCM kupitia vikao vya ndani na mikutano ya hadhara, wamekuwa wakizungumzia jinsi ya kudhibiti mivutano ya makundi ya urais miongoni mwa wanachama wake, tatizo kubwa likiwa ni jinsi gani ya kuwaleta pamoja na kuponya makovu baada ya uteuzi.
Mathalani, tangu uchaguzi mkuu uliopita, viongozi wa CCM wamekuwa wakieleza mgawanyiko baada ya uteuzi kama sababu ya kuyakosa baadhi ya majimbo muhimu nchini na tatizo hilo linaweza kukikumba hata ngazi ya urais, kisipokuwa makini.
Makundi ya watia nia ya urais kwa sasa yamesambaa mikoani kimyakimya kutafuta uungwaji mkono na baadhi yake yamejijengea ushindani wa kihasama kati ya kundi moja na jingine hadi kutupiana maneno makali na tuhuma mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo linaweza kuhatarisha uimara wa chama na kukiathiri katika uchaguzi wa Oktoba.
Mchakato wa Katiba
Tangu ulipoanza mchakato huo hadi sintofahamu inayoendelea ya Kura ya Maoni, yametokea mambo mengi na kuzua hasira kwa baadhi ya Watanzania, hivyo kuwa miongoni mwa mambo yanayohofiwa kutumika kama bakora ya kuiadhibu CCM katika Uchaguzi Mkuu.
Hasira hiyo inatokana na jinsi wananchi walivyoipokea na kuiamini Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba na kuyakubali matokeo ya kazi yake lakini baadaye yakapinduliwa na Bunge la Katiba, kwa wingi wa kura za wajumbe wa CCM, ambazo hadi leo bado zinatia shaka.
Hata kitendo cha kushindikana kwa karata ya Serikali kuitisha Kura ya Maoni Aprili 30, ni kikwazo kingine kwa chama hicho, kwa kuwa hakuna namna nyingine ya kuonyesha kuungwa mkono na umma, ikiwa ni siku chache baada ya nguvu yake kuonekana kupungua katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Ufisadi 
Haitoshi, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Serikali imekuwa kwenye kipindi kigumu cha matukio ya ufisadi yaliyosababishwa na ama watendaji au makada wake. Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na sakata la Richmond ambavyo kwa vyovyote mwaka huu, litaibuka kwa kuwa linahusishwa na baadhi ya wagombea, sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow ambalo bado ni bichi, Epa ambayo baadhi ya watuhumiwa walisamehewa baada ya kurejesha fedha ambazo hazikuelezwa bayana zilikopelekwa na matukio yasiyokoma yanayoibuliwa katika ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Nguvu ya upinzani
Matokeo ya upinzani katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 nayo yanaonekana kujenga hofu kwa CCM kwa kuwa yameibua picha mpya kuwa vyama vya upinzani vinakubalika hadi vijijini ambako chama hicho kimekuwa kinazoa kura bila upinzani.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, ushindi wa CCM umepungua kutoka zaidi ya asilimia 91 za uchaguzi wa 2009 hadi asilimia 70 katika mitaa na vijiji mwaka jana, jambo ambalo lisipoangaliwa linaweza kukiathiri chama hicho.
Ahadi zisizokamilika
Mambo mengine mwiba kwa CCM kama chama tawala ni baadhi ya ahadi za 2010 ambazo hazijakamilika, zikiwamo za ilani ya uchaguzi na nyingine alizotoa Rais Jakaya Kikwete binafsi kadri alivyokuwa anaona mahitaji ya wananchi katika kampeni zake.
Baadhi ya ahadi hizo ni meli katika baadhi ya maziwa, barabara, vivuko, madaraja, hospitali na huduma nyingine mbalimbali.
Mahakama ya Kadhi
Pengine suala ambalo limeacha kovu kubwa katika uso wa CCM ni suala la Mahakama ya Kadhi. Suala hili liliingizwa katika ilani yake ya 2005 kuwa ikishinda itatafuta suluhisho ambalo hadi leo limeshindikana, badala yake likaweka ufa mkubwa katika utengamano wa Taifa.
Katika siku za karibuni, Waislamu walishuhudiwa wakidai ahadi hiyo iingizwe kwenye Katiba Mpya, lakini Serikali ikaomba isiwemo, ikisema itatungiwa sheria ambayo hata hivyo inapingwa na viongozi wa Kikristo wanaodai Serikali haina dini hivyo isijihusishe nayo. Muswada huo tayari umewasilishwa na kuondolewa bungeni mara mbili.
Maoni ya wachambuzi
Akizungumza vikwazo hivyo, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, aliungana na gazeti hili, akisema kashfa serikalini kwa vyovyote utakuwa ni mtaji mkubwa kwa Ukawa katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema suala la Katiba ni kesi inayojitegemea kwa Watanzania wengi wasiokubaliana na uamuzi wa Serikali kulazimisha muundo wa Serikali mbili ikiwa ni tofauti na maoni yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Warioba.
“Kuna athari za escrow ambazo zimeanza kuonekana tangu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hakuna aliyetegemea matokeo yale kwa upinzani, kwa hivyo hali siyo nzuri mpaka baadhi ya maeneo ya vijijini,” alisema na kuongeza:
“Hali ni mbaya katika tathmini inayoonekana kwa sasa na kama asingekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana chama hicho kisingekuwa na dalili za kurudi Ikulu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, Kinana ameiombea CCM msamaha na kwa kiwango fulani ameibeba.”
Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Emmanuel Mallya alisema vikwazo hivyo, haviwezi kuwa kipimo pekee cha kuikwamisha CCM kutokana na uzoefu uliopo.
“Kuna makundi matatu ninayoyajua, kuna Watanzania ambao huwezi kuwabadili kitu kwa CCM, wataichagua tu bila kujali changamoto hizo. Pili, kuna kundi la vijana ambao hufanya uamuzi dakika za mwisho, hawajulikani, kuna kundi la vijana la mabadiliko na kundi la kina mama wanaoangalia upepo wa utulivu, hawa hupiga kura kwenye utulivu wa chama,” alisema Dk Mallya.
Alisema Serikali bado inayo nafasi kubwa ya kutafuta maridhiano na taasisi, mashirika na makundi mbalimbali kwenye jamii ili kuondoa athari zinazoweza kujitokeza katika Uchaguzi Mkuu.
Dk Mallya alisema masuala ya Mahakama ya Kadhi na Mchakato wa Katiba yanaweza kuwa na athari kubwa kwa CCM kwa wananchi kupigia kura vyama vya upinzani.
“Serikali inaweza kurejesha imani ya Watanzania hata kwa muda uliobakia endapo itakubali kujadiliana, kukubaliana na taasisi, mashirika, viongozi wa dini na wadau,” alisema Dk Mallya.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama alisema suala la Katiba limewakatisha tamaa Watanzania wengi waliokuwa wameweka maoni yao na kuondolewa.
Profesa Penina alisema mchakato wa Katiba ulikuwa na matarajio mazuri kwa Watanzania lakini jinsi ulivyochakachuliwa, umewafanya wengi kugawanyika.
“Sasa siwezi kujua kama hatua hiyo inaweza kuwa ni hasira ya kuiadhibu CCM, hilo sijui, ila kwa kweli imewakatisha tamaa sana, labda tusubiri tuone,” alisema Profesa Mlama.
Kauli ya CCM 
Kupitia ziara zake za ujenzi wa chama, Kinana amekuwa akisema asilimia 90 ya ahadi za 2010 zimeshatekelezwa.
Siku chache zilizopita, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alilieleza gazeti hili kwamba, hata kama Ukawa wangeunganisha vyama vyote vya upinzani, bado CCM itakuwa na mtaji mkubwa wa kushinda Uchaguzi Mkuu.
Kauli ya Nape inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba aliyesema CCM haiteteleki kutokana na muungano wa Ukawa kwa kuwa ina mtaji wa wapigakura wengi.
“CCM tunajivunia kwa sababu Watanzania bado wana matumaini nasi, lakini hata kwa umoja wetu kama chama, tumefika vijijini tofauti na chama chochote, hao wapinzani wanakomea mjini tu,” alisema Simba.
Hata hivyo, mwenyekiti mstaafu wa UWT, Anna Abdallah alitoa maoni yake kwa tahadhari akisema kigezo pekee na muhimu kuliko vyote kitakachoifanya CCM kurejea madarakani ni uteuzi wa mgombea anayekubalika kwa wananchi, kwa kuwa huo ndiyo mtaji mkubwa kuliko vyote.
Alisema CCM imewahi kufanya makosa katika uteuzi wa majimbo kadhaa na kuchukuliwa upinzani.
“Kuchagua anayekubalika ni kigezo kikubwa kuliko vyote, kuhusu habari nyingine ya tuhuma au vigezo sita, sioni kama zina mashiko sana. Waswahili wanasema, “ukimpenda Mmakonde basi penda na ndonya yake”, alisema akimaanisha ukikipenda chama, penda na makandokando yake.

Mambo sita yaliyomshinda Rais Kikwete

Rais Jakaya Kikwete alitoa ahadi lukuki kwa makundi mbalimbali ya jamii katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wake kupitia kaulimbiu yake ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, lakini anaondoka madarakani mwaka huu akiwa ameshindwa kutekeleza ahadi nyingi  na zaidi ameacha manung’uniko na mgawanyiko.
Mwaka 2005, alipoingia madarakani aliahidi kuondoa uhasama wa kisiasa kati ya visiwa vya Unguja na Pemba, kuondoa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, kuwapatia wanahabari Sheria ya Habari, kupambana na ufisadi; na mwaka 2010 aliahidi kuwapa Waislamu Mahakama ya Kadhi na wananchi Katiba Mpya.
Mambo hayo sita yamekuwa mfupa mgumu kwa Rais Kikwete na anaondoka akiacha uhasama mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar, wakulima na wafugaji wakihasimiana, ufisadi ukiotesha mizizi, vyombo vya habari kufungiwa, nchi ikipasuka kuhusu Katiba Mpya na Mahakama ya Kadhi.
Sheria ya Habari
Rais Kikwete alijigamba kuruhusu uhuru wa vyombo vya habari na Serikali yake ilianza kuandaa muswada mwaka 2007 lakini haukufikishwa bungeni. Machi 30, 2012 Kikwete alipokuwa mgeni rasmi katika utoaji Tuzo za Umahiri katika Uandishi (EJAT), aliahidi mambo mengi mazuri likiwamo la kuwasilishwa Muswada wa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari katika Bunge la Oktoba.
Kuthibitisha kwamba Rais Kikwete hamaanishi anachokisema, Julai 30, 2012 yaani miezi minne tangu awape matumaini wanahabari, Serikali yake kupitia Idara ya Habari (Maelezo), ililifungia gazeti la MwanaHalisi, kwa muda usiojulikana. Halafu Septemba 27, 2013 gazeti  la Mtanzania lilifungiwa kwa muda wa siku 90 na Mwananchi kwa siku 14. Magazeti mengine yaliyowahi kufungiwa siku 90 ni Kulikoni (Januari 8, 2010) na MwanaHalisi (Oktoba 13, 2008).
Desemba 8, 2011 mwanasafu wa gazeti la Tanzania Daima, Samson Mwigamba; mhariri mtendaji wa gazeti hilo, Absalom Kibanda na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mwananchi Communications Ltd iliyochapisha gazeti hilo walifikishwa kortini wakikabiliwa na mashtaka ya uchochezi.
Septemba 2, 2012 aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi alipigwa na kufariki dunia akiwa mikononi mwa polisi alipokuwa akiripoti mkutano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa. Januari 23, 2015 Serikali yake imeamua kupiga marufuku usambazwaji wa gazeti la The EastAfrican nchini.
Katiba Mpya
Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 haikuwa na ahadi ya Katiba Mpya, lakini Novemba 8,      2010 siku alipozindua Bunge la 10, Kikwete alizungumzia umuhimu wa kuipa uhai Katiba iliyopo na Februari 2011 katika sherehe za CCM alisema atawapa Watanzania Katiba Mpya.
Kwa kuwa wazo hilo halikutokana na CCM, Kikwete alipata shida kulinadi ndani ya vyombo vya chama na Serikali na hata walipokubali, wasaidizi wake walidai ni marekebisho yeye akisema kuhuisha. Serikali ikatengeneza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,  akaunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu, Joseph Warioba ambayo ilifanya kazi ya kukusanya maoni na kutengeneza Rasimu ya Katiba. Mwaka 2014 akaunda Bunge Maalumu la Katiba (BMK) ambalo liliandika Katiba Inayopendekezwa.
Ukosoaji mkubwa aliofanya Rais Kikwete alipozindua BMK, uliwagawa wabunge katika makundi mawili ya kudumu; wanachama wa CCM upande mmoja na wapinzani upande wa pili. Pia, Tume ya Warioba ilipingana na BMK lililoongozwa na Samuel Sitta.
Aprili 16, wapinzani chini ya umoja wao Ukawa walisusia BMK, likawa pigo la kwanza. Pigo la pili na la mwisho ni Januari 23, 2015 Ukawa walipotangaza kususia Kura ya Maoni iliyopangwa Aprili 30. Kutokana na misuguano hiyo, na kwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi haikuwa imepewa fedha za kutosha zikiwamo za kununulia mashine za BVR kwa ajili ya kuandikisha wapigakura, Aprili 2, 2015 Kura ya Maoni ikafutwa hadi itakapotangazwa tena.
Mahakama ya Kadhi
Mwaka 2010, katika mazingira tata CCM iliingiza ahadi ya Mahakama ya Kadhi kwenye Ilani ya Uchaguzi. Lakini Serikali haikufanya juhudi kubwa kutengeneza mazingira ya kukubalika kwa mahakama hiyo; kwanza, kwa Waislamu wenyewe; pili, kwa Wakristo.
Kosa namba moja. Agosti 30, 2011 alipokuwa mgeni rasmi katika Baraza la Idi katika msikiti wa Gadaffi, Dodoma, Rais Kikwete aliwaambia Waislamu kwamba amezungumza na maaskofu na wamemwambia kuwa hawana shida na Mahakama ya Kadhi isipokuwa wanataka iundwe na kuhudumiwa na Waislamu wenyewe. Waislamu walilalamika mambo yao kujadiliwa kwanza na Wakristo ndipo waelezwe wao.
Kosa namba mbili. Serikali imekuwa ikikutana na uwakilishi mpana wa maaskofu kutoka madhehebu yote kupata maoni yao lakini imekuwa ikikutana na uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ambalo halikubaliwi na Waislamu wote.
Kosa namba tatu. Dalili zote zikionyesha hakuna uwezekano wa kukubalika kwa Mahakama ya Kadhi, Serikali ilitoa ahadi nzito ndani ya BMK na Waislamu waliporidhia, hazikuwepo juhudi za kuandaa semina za kuelimisha wadau kuhusu muundo na uendeshwaji wake hali iliyosababisha hata baadhi ya Waislamu kuikataa kwamba siyo kati ya nguzo tano za Uislamu. Vilevile, lilikuwepo shinikizo kutoka kwa maaskofu na hasa ulivyoligawa Taifa mapande mawili.
Mgogoro Zanzibar
Moja ya ahadi nzito iliyofurahiwa na Watanzania ni ile ya kumaliza uhasama wa kisiasa Zanzibar kati ya wanachama wa CCM wengi wao wakiwa Unguja na wenzao wa Chama cha Wananchi (CUF) ngome yao ikiwa Pemba. Ahadi hiyo iliianza kutekelezwa baada ya kuanzishwa mazungumzo baina ya viongozi wa CCM na CUF na hatimaye kufikia maridhiano na Katiba ikafanyiwa marekebisho kuruhusu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuongozwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pamoja na mafanikio hayo, uhasama wa kisiasa umerejea; CCM wakionekana kuwa vinara wa siasa za uhasama; wanawavizia na kuwapiga wafuasi wa CUF. Katika mikutano yao huhubiri ubaguzi kwa kuzingatia asili ya watu kwamba Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu wanatajwa kuwa ni vibaraka wenye lengo la kurudisha utawala Kisultani. Wanadai kwamba vibaraka hao wanataka kurudisha utawala wa Sultani aliyepinduliwa mwaka 1964,  Jamshid bin Abdullah Al Said, kizazi cha masultani kutoka Oman kilichotawala Zanzibar kuanzia mwaka 1832 hadi mwaka 1964.
Huu ni unafiki, ukweli ni kwamba Jamshid aliyetawala Zanzibar kuanzia Julai Mosi, 1963, baada ya kupinduliwa Januri 12, 1964 alikimbilia Uingereza. Salmin Amour, Rais wa awamu ya tano wa SMZ alitangaza kumpa uhuru Sultani huyo anayeishi Portsmouth, kurejea Zanzibar kama raia mwingine. Hajarudi.
Wakulima, wafugaji
Jambo jingine kubwa aliloahidi kushughulikia katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la Tisa Desemba 31, 2005 ni kulinda mazingira kwa kuhakikisha wakulima wanaachana na kilimo cha kuhamahama na wafugaji aliodai wanatembea umbali mrefu kusaka malisho wakiwa wamekonda na mifugo imekonda, kuwapa mbinu za ufugaji ili sekta ya ufugaji iwe ya kisasa.
Baada ya kuunda Serikali alitembelea Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, aliwaagiza watendaji: kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika pato la Taifa; kudhibiti uhamishaji holela wa mifugo; kuimarisha huduma za ugani; kufufua ranchi zilizopo na kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa; na kutoka katika uchungaji wa kuhamahama na kwenda katika ufugaji wa kisasa na wa kibiashara.
Vilevile, aliwaagiza kutafuta masoko ya nje ya kuuza mifugo na mazao yake; na kufikisha madawa na huduma za mifugo kwa wafugaji. Lakini miongoni mwa picha zilizojaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuanzia mwaka 2006 ni za maiti ya wakulima na wafugaji katika maeneo tofauti nchini.
Baadhi zikionyesha watu waliokatwa koo, waliopasuliwa vichwa na waliopigwa mishale na mikuki; nyingine zikionyesha nyumba au maboma yalivyochomwa moto, mifugo kuuawa. Hasira na uhasama vimetanda kila mahali.
Katika kipindi cha uongozi wake, imeshuhudiwa migogoro mingi ya ardhi kati ya masikini na matajiri, wakulima wazawa na wawekezaji na mbaya zaidi kati ya wakulima na wafugaji ambao wamechinjana Mbarali, Kilosa, Kiteto na kwingineko. Rais Kikwete anaondoka huku hali ikiwa mbaya kuliko alivyoikuta.
Vita ya ufisadi
Ahadi nyingine ya Rais Kikwete kwa Watanzania aliyoitoa katika hotuba yake ya Desemba 31, 2005 ni kuanzishwa kwa mapambano dhidi ya rushwa kubwa kubwa kwa vitendo na siyo lazima ushahidi uwepo kwa asilimia 100.
Alisema: “hata ukihisiwa umekula rushwa tutahakikisha tunachunguza na kushughulikia…” Lakini licha ya Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO) kutaja waliokula rushwa kupitia ununuzi wa rada ya kuongozea ndege, Serikali ilikataa kuwashughulikia.
Mafisadi wengine ambao hawakushughulikiwa na Serikali yake ni walionufaika kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa), walitoengeneza dili kupitia kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond/Dowans, walioiuzia vifaa hospitali ya Muhimbili kwa bei mbaya, waliochangisha fedha za kula tu baada ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini (2012) na sasa waliotengeneza mazingira ya kuchotwa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, Serikali imewanasa walimu na mahakimu na kuwafungulia mashtaka kwa madai ya kuchukua rushwa ndogondogo.

Friday, 27 March 2015

SHERIA: Sheria gharama za uchaguzi kung’ata zaidi

Dar es Salaam. Serikali inakusanya nguvu kuhakikisha Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010, inang’ata wagombea wote watakaojihusisha na rushwa katika harakati zao za kusaka uongozi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, watendaji kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wamesema, utekelezaji wa sheria hiyo ulikuwa na changamoto nyingi katika uchaguzi uliopita mwaka 2010.
Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ofisi yake ilikumbana na  changamoto nyingi zilizofanya ishindwe kuisimamia sheria hiyo ipasavyo.
“Mwaka 2010 changamoto zilikuwa nyingi lakini tumejifunza. Uchaguzi wa mwaka huu tumeshajipanga, tunajua jinsi gani ya kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo, tunajua tunahitaji ushirikiano wa karibu wa wadau ili kuweza kufanikisha jambo hilo,” alisema Nyahoza.
Nyahoza alitaja wadau ambao ofisi hiyo inatarajia kushirikiana nao katika kuisimamia sheria hiyo kuwa ni pamoja na vyama vyote vya siasa, asasi za kijamii, waandishi wa habari na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Ushirikiano huu unaanza kuimarishwa kabla ya uchaguzi. tumebaini kwamba wadau hawa wanatakiwa kupatiwa mafunzo ya namna wanavyoweza kushiriki kufanikisha utekelezaji wa sheria hii, pia kutakuwa na simu maalumu za kuripoti matukio yatakayokuwa kinyume,” alisema. 
Kauli ya Takukuru 
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alikiri kuwepo kwa mkakati wa kuunganisha nguvu hizo, licha ya kukabiliwa na changamoto ya rasilimaliwatu.
“Ni kweli hata sisi tumeona kuna umuhimu wa kushirikiana katika kufanikisha jambo hili, ingawa kuna changamoto ya rasilimali watu, tunaamini kazi zitafanyika kwa namna ambayo itadhihirisha dhana ya kuwapo kwa Takukuru,” alisema Dk Hoseah.
Dk Hoseah pia alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kuepuka kuuza haki zao za kuchagua viongozi bora kwa kudanganywa na zawadi za kanga, fulana, kofia na fedha. 
Sheria ikoje?
Ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wake wa 18, uliofanyika Januari 2010. Sheria hiyo  imeweka utaratibu wa kusimamia na kuratibu mapato, matumizi  na gharama za kampeni na uchaguzi wa vyama vya  siasa na wagombea.
Sheria hiyo ilisainiwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Machi 17, 2010 ili iweze kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, kwa lengo la   kukuza demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini.
Madhumuni ya kuwekwa Sheria hii ya Gharama za Uchaguzi ni kujenga mazingira yatakayowezesha kuwapo kwa uwazi zaidi katika matumizi ya fedha zitakazotengwa kwa ajili ya kampeni, pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa ndani ya vyama vya siasa katika uteuzi wa mgombea na uchaguzi wenyewe kwa ujumla.
Sheria hii imegawanyika katika sehemu nane. Sehemu ya Kwanza inaweka masharti kuhusu mambo ya utangulizi ambayo ni jina, tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria hii katika Tanzania Bara na Zanzibar  na vilevile inaweka tafsiri ya misamiati itakayotumika.
Sehemu ya pili inaorodhesha kazi za Msajili wa Vyama vya Siasa, ikiwemo mamlaka ya kusimamia na kukagua gharama za uchaguzi kwa vyama vya siasa  na mwenendo wa wasimamizi wa uchaguzi.
Sehemu ya  tatu inahusu masharti kuhusu fedha zitakazotumika kwa ajili ya uchaguzi, maana ya gharama za uchaguzi, uchaguzi ndani ya Vyama vya Siasa, gharama  ambazo vyama vya siasa vinapaswa kutumia wakati wa uchaguzi, masharti  kwa Vyama vya Siasa na wagombea kutoa taarifa kuhusu gharama zitakazotumika wakati wa uchaguzi.
Aidha, sehemu hii inatoa taarifa kuhusu michango au misaada inayotolewa na kupokewa na vyama vya siasa, kuzuia fedha kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kampeni za uchaguzi, matumizi ya gharama kwa vyama na taasisi za kiserikali  wakati wa kutoa elimu ya Kampeni na chaguzi za kisiasa.
Sehemu ya tano ya sheria hii inahusu masharti yanayokataza baadhi ya matumizi ya fedha kama gharama za kampeni na uchaguzi. Matumizi hayo ni yale yanayohusu  gharama kwa vitendo vinavyozuiwa  au kuwa haramu wakati wa kampeni na uchaguzi.
Sehemu ya sita ya sheria hii inapendekeza makosa ya  ujumla  pamoja na adhabu zinazoweza kutolewa kwa kukiuka masharti ya Sheria hii.
Sehemu ya saba inaweka masharti  kuhusu haki ya mgombea wa Ofisi ya Rais na Makamu wa Rais kutumia vyombo vya habari, wajibu wa Serikali na vyombo vya habari kumuwezesha kutumia  haki  hiyo.
Aidha, sehemu hii inaipa Serikali wajibu wa kutumia  vyombo vya ulinzi  na usalama ili kuhakikisha kwamba Vyama vya Siasa, wagombea wao na  wapiga kampeni wanafikia wapigakura bila ubaguzi wala  kupewa vitisho.
Sehemu ya nane ya sheria inafanya marekebisho katika Sheria ya vyama  vya siasa ili kuoanisha masharti  ya sheria hiyo. Marekebisho ya msingi ni kuongeza  kifungu cha 13A katika Sheria ya Vyama vya Siasa kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha Msajili wa Vyama vya Siasa kupata taarifa juu ya mgombea au chama cha siasa kinachojihusisha na vitendo vya ukiukaji wa masharti ya Sheria hii wakati wa kampeni za uchaguzi.

Urais Ukawa, hesabu zinalalia Chadema

Dar es Salaam. Wakati wenyeviti wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na kamati zake za kitaalamu wanakutana Zanzibar kutafuta suluhu kuhusu mgawanyo nafasi za kugombea katika uchaguzi mkuu ujao, kuna uwezekano mkubwa vyama hivyo kuteua mgombea urais kutoka Chadema.
Tovuti hii inaweza kuripoti kwa uhakika kuwa uwezekano huo unatokana na vigezo vinavyotumiwa na vyama hivyo kusimamisha mgombea mmoja kwa kila jimbo na kwenye nafasi ya urais ambavyo vinaipa Chadema nafasi hiyo dhidi ya vyama vingine katika umoja huo ambavyo ni CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Vigezo hivyo ni matokeo ya uchaguzi 2010, idadi ya madiwani kwa kila chama, matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Desemba mwaka jana, mtandao wa chama nchini na nguvu ya mgombea iwapo Chadema kitamsimamisha katibu mkuu wake, Dk Willibrod Slaa kwa mara ya pili.
Taarifa zilizolifikia Mwananchi kutoka ndani ya kamati ya ufundi ya Ukawa zinasema pamoja na kuwapo mvutano katika baadhi majimbo Tanzania Bara, kwa upande wa Zanzibar hakuna tatizo hilo, jambo linaloipa CUF nafasi ya moja kwa moja kwenye ubunge, uwakilishi na hata urais wa visiwa hivyo.
Kwa mujibu wa habari hizo, nafasi nzuri ya CUF kupita moja kwa moja Zanzibar bila ushindani ndani ya Ukawa, inatoa fursa kwa upande wa Bara, kwa vyama vilivyosalia kupitishwa kuwania urais wa Muungano.
Hata hivyo, kwa vigezo vilivyotajwa hapo juu, Chadema ndiyo inakuwa na nafasi isiyo na kipingamizi kutokana na rekodi vyama vilivyosalia Bara.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, Chadema kilimsimamisha Dk Slaa na aliibuka wa pili baada ya Rais Jakaya Kikwete akiwa na kura 2,271,941 (asilimia 26.34) akifuatiwa na Profesa Ibrahim Lipumba aliyepata kura 695,667 (asilimia 8.06) na Hashim Rungwe wa NCCR-Mageuzi aliyepata kura 26,388 (asilimia 0.31). NLD haikusimamisha mgombea urais.
Kwa upande wa majimbo yaliyotokana na uchaguzi wa 2010, Chadema kiliongoza kikiwa na wabunge 24 (wote kutoka Bara), CUF 23 (wawili kutoka Bara, 21 Zanzibar) na NCCR-Mageuzi wanne (wote wa Bara).
Katika rekodi za uchaguzi wa mitaa zilitolewa na Tamisemi kabla ya chaguzi za marudio, Chadema ilipata mitaa 980, ikifuatiwa na CUF (mitaa 266), NCCR Mageuzi  (28)  na NLD mtaa mmoja. Kwa upande wa vijiji, Chadema kilishinda vijiji 1,754, CUF (516), NCCR-Mageuzi (67) na NLD vijiji viwili.
Hata kwa upande wa vitongoji Chadema kiliviongoza vyama hivyo kwa kupata vijiji 9,145 kikifuatiwa na CUF (2,561), NCCR-Mageuzi (339) na NLD vitongoji viwili.
Tayari NCCR-Mageuzi kimeonyesha nia ya kumteua Dk George Kahangwa kuwania urais wakati Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alikaririwa na gazeti hili hivi karibuni akisema kuwa chama chake kimekwishamteua kuwania urais, hivyo jina lake litapelekwa Ukawa kushindanishwa.
Mvutano mkali
Hali ikiwa hivyo, wajumbe wa Ukawa leo watakumbana na wakati mgumu wa kufikia maridhiano ya kugawana majimbo 19 kutokana na taarifa za kuwapo mvutano mkali wa pande zote za vyama husika.
Wanaokutana leo ni wenyeviti wa vyama, makamu wenyeviti, makatibu na wajumbe wa sekretarieti kutoka vyama hivyo.
Kabla ya kuanza kikao cha leo, jana asubuhi wajumbe 16 wa Kamati ya Ufundi walikutana na baadaye jioni wenyeviti wa umoja huo wakawa na kikao cha awali, ikiwa ni sehemu ya vikao vya hatua za kugawana maeneo ya kuwania ili kutoa ushindani na hatimaye ushindi dhidi ya CCM.
Chanzo cha habari kutoka ndani kimelieleza Mwananchi kuwa NLD nayo imeongeza mvutano ikihitaji majimbo matano.
Wiki iliyopita, gazeti hili liliandika kuwa Ukawa ilikuwa imekamilisha kazi ya ugawaji wa majimbo 170 lakini ukawapo mvutano katika majimbo 19 ambayo vyama zaidi ya kimoja vilikuwa vinayataka.
Majimbo hayo ni Segerea, Kinondoni, Kigamboni na Ukonga ya Dar es Salaam, Morogoro Mjini na mengine ya mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Kagera.
“Mvutano ni kwamba, kuna vyama vinavyotaka uwakilishi tu wa majimbo hayo lakini kiukweli yanaweza kupotea bure tu endapo vitakabidhiwa. Wengine wanataka kuangalia zaidi ushawishi wa chama ndani ya jimbo husika ila wengine wanapinga, wakisema umoja huo hautakuwa na sababu kama watakosa uwakilishi,” kilieleza chanzo hicho.
“NLD wanahitaji majimbo matano, CUF na Chadema wanavutana zaidi, ila NCCR-Mageuzi wameonekana kushtushwa sana na hali hiyo,” kilisema chanzo kingine kutoka NCCR-Mageuzi.
Chanzo kingine kilieleza kuwa kamati ya wataalamu ilishakamilisha kazi yake ya uchambuzi wa majimbo hayo na kuwasilisha taarifa zake lakini kuna upinzani mkali ambao umeendelea kuibuliwa na wajumbe wa umoja huo.
“Kikao cha leo kinaashiria kuwa na mvutano, ninaamini kuna uwezekano wa kufikia mwafaka lakini ikishindikana kabisa kwa leo lazima vitaandaliwa vikao vingine,” kilieleza chanzo kingine.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu, Benson Kigaila (Chadema) alisita kuweka wazi juu ya mvutano uliopo huku akibainisha kuwa maridhiano yatapatikana.
Kigaila alisema kikao cha leo kina nafasi kubwa ya kumaliza mvutano huo na kueleza Watanzania juu ya mwelekeo wa safari yao.
Kigaila ambaye pia ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni ya Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chadema, alisema: “Kwa sasa siwezi kueleza chochote kwani vikao ndiyo vinafanyika kwa sasa, lakini naomba vikao vikishamalizika viongozi wetu watazunguza tu,” alisema.
Alipoulizwa juu ya NLD kuhitaji majimbo matano, Kigaila alikiri kuwa kweli wanataka mgawo wa majimbo lakini alikataa kutaja idadi yake.
“NLD wanayo haki kama vyama vingine, kwa nini wasipate? Watapata, lakini kuna taarifa sahihi zitakazoelezwa baada ya kikao cha leo.”
Jumanne wiki hii, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bara, Magdalena Sakaya alilieleza gazeti hili kuwa kikao hicho kitakuwa na ajenda ya kukusanya maoni na mapendekezo ya wanachama, kujadiliana kwa pamoja ili kufikia muafaka wa majimbo hayo.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema katika hatua za kutafuta maridhiano ya majimbo hayo, vyama vyote vinapaswa kutambua kila nafasi ya chama kilichoshiriki kwenye makubaliano ya Ukawa.
“Tukifuata kanuni, nadhani kuna vyama ambavyo havitakuwa na nafasi Ukawa na haitakuwa na maana ya kuungana, kwa hivyo lazima busara itumike zaidi. Haiwezekani chama fulani kilazimishe kuchukua majimbo mengi kuliko kingine,” alisema Nyambabe.
Alipoulizwa kuhusu utata katika mgawanyo wa majimbo, Dk Slaa alisisitiza kumalizika kwa mvutano kutokana na busara za viongozi wa vyama hivyo.

Thursday, 26 March 2015

Marufuku kuvuta sigara hadharani

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid amesisitiaza tamko la kupiga marufuku uvutaji wa sigara katika maeneo ya umma ili kuilinda jamii kutokana na madhara yatokanayo na moshi wa sigara.
Tamko la Waziri limekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani, moja ya magonjwa yanayosababishwa na uvutaji wa tumbaku.
Agizo hilo limezingatia Sheria ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121 TL, ya mwaka 2003, Kipengele cha 12(1) ambacho kinakataza matumizi ya bidhaa hiyo katika maeneo ya umma.
“Agizo hili linawataka wananchi wanaotumia bidhaa za tumbaku, kupunguza au kuacha kabisa, pia linaijumuisha jamii yote kujua madhara ya matumizi ya tumbaku na umuhimu wa kuzuia uvutaji katika maeneo ya umma,” alisema Waziri katika tamko lake.
Uvutaji sigara ulianza kupigwa marufuku kwa mara ya kwanza mwaka 1575 na Kanisa la Katoliki lakini katika karne ya 20 harakati dhidi ya uvutaji sigara zilipamba moto kwa sababu za kiafya.
Sababu kubwa ya kupiga marufuku ni ukweli kwamba uvutaji sigara ni hiari wakati kuvuta pumzi ni lazima, hivyo mtu anayetumia kilevi hicho hana budi kukaa mbali ili kuepusha uwezekano wa kupata magonjwa kama ya moyo na saratani kwa wasiotumia na ambao kuvuta pumzi ni lazima.
Msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamaja alisema nia ya marufuku hiyo ni kuhakikisha wizara inatimiza kwa vitendo sheria hiyo ya bidhaa za tumbaku kwa kupiga marufuku na kuchukua hatua za kisheria. “Jamii itusaidie kutoa elimu katika hili, kuna suala la kujenga maeneo maalum ya kuvuta sigara na elimu kwa wale wanaovuta,” alisema.
Sheria ya usimamizi wa bidhaa za tumbaku ya mwaka 2003, inaeleza kuwa nia ni kuwalinda vijana wenye umri wa chini ya miaka 18 na wale wasiovuta wasishawishike kuvuta.
Kuwalinda wasiovuta wasipate madhara, kuifahamisha jamii juu ya madhara ya tumbaku na madhara ya kuvuta moshi wa sigara inayovutwa na mwingine na kuhakikisha jamii haina wavutaji sigara.
Maeneo ambayo yamepigwa marufuku kuvuta sigara yametajwa katika tamko hilo kuwa ni katika ofisi zote za serikali na taasisi zake, hospitali za umma, vyuo vikuu na shule za umma, vituo vya usafiri wa anga, mabasi, bandari na treni, bustani, fukwe na katika maeneo ya kupumzika ya umma.
Pia tamko hilo la wizara limekataza uvutaji wa sigara katika mikutano yote ya kiserikali.
“Wizara inawataka wale wote ambao wanataka kuacha kabisa kuvuta sigara, wawatafute wataalamu wa afya ili wapate ushauri wa kitaalamu,” alisema waziri katika tamko hilo.
Kadhalika, agizo hilo limewataka wafanyakazi wa sekta ya afya na watumishi wa umma kuhakikisha wanafanyia kazi na wanasimamia agizo hili.
“Tunataka kila mmoja ashiriki katika agizo hili la kuzuia bidhaa za tumbaku, sekta binafsi, asasi za kidini na wadau wengine wa afya watusaidie katika kufanikisha hili,” alisema Waziri
Wakati wizara ikitoa tamko hilo, Kampuni ya Sigara (TCCL) imekuwa moja ya kampuni zilizoongoza kwa kulipa kodi mwaka jana.