Saturday, 13 September 2014

Cheyo awavaa Ukawa bungeni



Dodoma. Mwenyekiti wa Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD), John Cheyo amewavaa viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akieleza kuwa walichokubaliana katika kikao chao na Rais Jakaya Kikwete ni kwamba Bunge liahirishwe Oktoba 4 na si kama wanavyodai wakiwa nje.
Akizungumza bungeni mjini Dodoma jana, Cheyo alisema hakuna makubaliano ya kutaka Bunge lisitishwe kabla ya kukamilisha kazi zake Oktoba 4, ikiwamo kutoa Katiba itakayopendekezwa kwa wananchi.
“Mojawapo tulilokubaliana ni Bunge hili lipate Katiba itayopendekezwa kwa wananchi,” alisema Cheyo huku akipigiwa makofi na kelele kutoka kwa baadhi ya wajumbe.
“Pia tulikubaliana kwa hali halisi ya muda tulionao, haiwezekani mchakato mzima ukamalizika na maana ya kumalizika mchakato ni kura ya maoni ya wananchi na ndiyo wenye Katiba.”
“Tukasema kama inabidi tufike mpaka kule (kura ya maoni) inatubidi tuahirishe uchaguzi wa 2015 jambo ambalo sisi wote hatuliafiki na mheshimiwa Rais alisema msinitwishe mzigo huu,” alisisitiza Cheyo.
Cheyo alisema Rais katika mazungumzo hayo alitaka utaratibu wa kufanya uchaguzi kila Oktoba ya mwisho wa kipindi cha miaka mitano uendelee ili wananchi wenyewe watoe ridhaa kupitia uchaguzi wa viongozi.
“Bunge hili haliendeshwi kwa amri ya mtu ambaye yuko barabarani. Bunge hili linaendeshwa kwa mujibu wa Sheria na sheria tuliyokuwa nayo kwa sasa ni GN 254 (tangazo la Serikali) ambayo inasema uhai wa Bunge ni mpaka Oktoba 4,”alisema Cheyo.
Cheyo alisema haiwezekani Rais akasimama mara baada ya makubaliano na kutangaza kuwa siku inayofuata Bunge lisitishe shughuli zake.
“Watu tumekubaliana na kuna video ambayo kila mmoja aliyekuwa akizungumza alirekodiwa. Kweli mnataka tumuombe sasa mheshimiwa Rais tutengenezewe kipindi maalumu kila mmoja aonekane anasema nini?” alihoji.
“Tuwe waungwana. Itoshe mimi kusema yale niliyotangaza hayo ndiyo makubaliano.

Hii nayo ni sanaa ya kimataifa

Utamaduni wa Mtanzania, katika sekta ya burudani, unaweza ukapotea kama waongeaji tusipotumia majukwaa yetu ya kuongelea na kuliongelea hili angalau kwa uchache.
Uchunguzi wa jarida hili umegundua hili na nachukua wasaa huu kama mshikadau wa burudani hapa nchini kuwaambia wandaaji, tuangalie upya aina za burudani tunazotoa na watu tunaowapelekea.
Kiukweli tunaanguka na kwa kuanguka sisi tutajikuta siku moja tukiangusha maadili ya kijana wa kitanzania pia na burudani ni ajira kwa vijana wetu sasa tukisababisha itumike ndivyo sivyo, kutakuwa na hatari ya kuliletea hasara taifa katika siku za usoni.
...Nina maana yangu kusema hivi.
Katika miezi sita ya nyuma nimeshuhudia matamasha mengi ambayo majina yake hayaendani na kinachofanyika kwenye tamasha hilo, hali inayosababisha watu makini wa tasnia ya burudani kuanza kushindwa kabisa kuwaelewa waandaaji, wamekuwa kama wadanganyifu hivi sifa ambayo si nzuri kwa mfanyabiashara aliyedhamiria kukaa kwenye tasnia kwa muda mrefu.
Tamasha linaitwa la kimataifa, lakini kinachopatikana kwenye tamasha hilo utakuta ni kama tamasha la Dar es Salaam hivi, sasa sijui ni kutokana na bajeti au ni kutokana na ufinyu wa fikra ama ni kutokana na uroho wa kipato au ni kuhisi kwamba wale unaowapelekea burudani hawana akili?
Unapomwambia mtu naleta kitu cha kimataifa, halafu zinaonekana sura za hapahapa unataka kusema kwamba sisi ni wa kimataifa?
...tangu lini?
Basi kuwe na angalau na uwakilishi wa nchi mbili tatu...
Hamna!
Tunamdanganya nani sasa?
Tunajidanganya wenyewe kwa taarifa maana mwisho wa siku Watanzania si wajinga tena, wanajua mambo mazuri na mabaya, ..unaona bwana? Mwisho wa siku wakishajua wewe si mkweli kwenye kazi zako watakukimbia na wakikukimbia utataka kumtafuta mchawi, kumbe umejiloga mwenyewe.
Kuna haja ya kuwa makini katika hili ndugu zangu wadau, kuna watu wana akili zao wamekaa tu wanaangalia haya mambo, wanachambua tu na mwishowe watatoa hoja zao na unaweza kuhisi unaonewa, kumbe ndiyo stahili yako.
Ukisema kitu ni cha kimataifa, kiwe cha kimataifa kweli, kikiwa kitu cha kiasili kiwe cha kiasili kweli na wasanii jamani wapo wengi, siyo kila siku wale wale tu tutoe nafasi kwa kizazi kilichopo mtaani kuonyesha uwezo wake tusiangalie tu walio karibu yetu.

Jaji Warioba: Namshangaa Sitta

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema anashangazwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta kung’ang’ania kuendelea na Bunge hilo licha ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia lifikie kikomo Oktoba 4 mwaka huu.
Hivi karibuni, Rais Kikwete alikutana na viongozi wa vyama vya siasa vilivyo chini ya Kituo cha Demokrasia (TCD) na kukubaliana kusitisha mchakato wa Katiba hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Akizungumza katika mahojiano maalumu wiki hii jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba alisema ameshangazwa na uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba kuendelea na vikao wakati uwezekano wa kukamilisha mchakato haupo.
“Hivi kuna haraka gani ya kuwa na rasimu katika Bunge hili? Mimi nilivyoelewa makubaliano ya Rais na TCD ni kama walikuwa wanasema kwa ustaarabu hebu twende polepole. Nimeambiwa kuwa Rais alitoa muda mpaka Oktoba 4, lakini uongozi wa Bunge ukapanga mpaka mwisho wa Oktoba,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Mimi nafikiri makubaliano kati ya Rais na viongozi wa vyama ni kukataa kuongeza muda. Hiyo kwangu ni lugha ya kistaarabu kwa Bunge kwamba hamwezi kumaliza kazi hii kwa kipindi hiki,” alisema Jaji Warioba.
Alimtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Sitta kukubali kukosolewa kama yeye anavyokubali kukosolewa kuhusu Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume yake, badala ya kujihami.
“Nilipoanza wakati ule mengi yalisemwa, lakini nilijua, ukipewa kazi maalumu lazima upate maoni ya watu ya kila aina. Kuna wale ambao watakusifu na wengine watakusema vibaya. Nilisemwa mengi sana. Lakini kwa kuwa nimefanya kazi ya Taifa siwezi kuhangaika na mtu mmoja mmoja,” alisema na kuongeza:
“Sitta asikilize wale wanaosema kuwa ana kasoro, asije akafikiri kuwa hana kasoro.”
Aliongeza: “Nashangaa sana mambo yanavyoendelea kwenye Bunge, hata siku hizi siangalii tena. Ni wakati fulani mtu anaweza kunipigia simu, hebu angalia wanavyosema....”
Alisema hatua ya uongozi wa Bunge kung’ang’ania kuendelea na mchakato ni kupingana na Rais Kikwete.
“Lakini mimi inanishangaza ilikuwaje Rais anatoa nyongeza ya hadi Oktoba 4, uongozi wa Bunge unaongeza hadi mwisho wa mwezi? Rais anasema hivi na Bunge linasema hivi. Mimi naomba uongozi wa Bunge utafakari tena,” alisema na kuongeza:
“Kinachofanywa na uongozi wa Bunge la Katiba hakina shinikizo la CCM , bali ni uamuzi ambao unatokana na matakwa yao
“Kama ni makubaliano ya viongozi wa vyama vya siasa na CCM walikuwapo, sasa kama chama kimeona hatuwezi kupata Katiba bora kwa nini tena uendelee?”
“Sheria ilisema Bunge lile litapewa siku 70, lisipomaliza litapewa nyingine 20, wakafanya tafsiri zao, kwani hizo siku 90 hazijaisha? Walipofikia wakati wakasema sasa tunakutana na Bunge la Bajeti tuahirishe, wakaahirisha. Kama mara ya kwanza liliwafanya wasitishe, nini kinawazuia kwa sasa?”
Alisema mbali ya tamko hilo, uongozi wa Bunge hilo umetangaza kuendelea na mchakato wakisema kuwa rasimu itakuwa tayari mwisho wa mwezi huu.
“Nasikia wanaendelea, nasikia wanasema rasimu itakuwa tayari mwisho wa mwezi huu. Hivi katika hali hii wanaweza?” alihoji Jaji Warioba huku akionyesha sura ya mshangao.
Warioba ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya pili ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alisema ahadi iliyotolewa na Sitta ya kupatikana kwa rasimu ndani ya Septemba haitekelezeki.
“Sina tatizo na kuahirisha Bunge Maalumu la Katiba, kwa kuwa waliona haiwezekani kupata Katiba kabla ya uchaguzi, lakini sioni uwezekano wa kumaliza kazi zote kwa wakati huu,” alisema na kuongeza:
“Sioni kama wana muda wa kamati kuandika rasimu mpya ya kupigia kura, kwa sababu suala siyo kupiga kura tu, kuna mambo ambayo lazima kuwe na maridhiano na itachukua muda.”
Akitoa mfano wa suala la Muungano, Warioba alisema ni kati ya mambo yanayohitaji maridhiano badala ya kuishia kwenye kupiga kura tu.
“Kwa mfano suala la muungano halitakwisha hivihivi bila maridhiano. Kuna mengine, nimesikia wanajadili Mahakama ya Kadhi, limejitokeza sana. Litakapofika kwenye uamuzi, lazima kuwe na maridhiano. Wasipokuwa na maridhiano inawezekana wakaleta rasimu ambayo haina Mahakama ya Kadhi. Je, wale wanaoitaka wakikataa una uhakika wa kupata theluthi mbili? Wale wanaopinga wakikubali utapata theluthi mbili?” alihoji.
Kupiga kura
Akizungumzia kauli ya Sitta ya kuwasiliana na balozi za nje ili kuhakikisha wajumbe waliosafiri huko wapige kura hukohuko, Warioba alisema kupiga kura peke yake hakutoshi kutoa uhalali wa Katiba bali maridhiano ndiyo msingi.
Aliongeza: “Mimi sielewi uongozi wa Bunge unafanya nini! Kwa sababu ukipitisha kitu kwa siri, hata kabla ya kufika kwenye kura ya maoni kikakataliwa na wananchi. Ni vizuri kutulia na kushauriana, wasiwe na haraka.”
Amewashauri viongozi wa Bunge hilo kutafakari upya uamuzi wa kuendelea na vikao wakati Rais ameonyesha nia ya kuvisitisha.
Misimamo ya vyama imeharibu
Akieleza sababu za Bunge hilo kuyumba, Jaji Warioba alisema licha ya Tume yake kuwapa viongozi wa vyama vya siasa na wajumbe wengine nyaraka 10, lakini wameingiza misimamo ya vyama vyao:
“Mchakato ulipoanza kwa wale ambao tulikabidhiwa kazi hii, tuliamini tunaelekea kupata Katiba bora itakayotokana na maoni ya wananchi. Sisi kwenye Tume hilo ndilo lilikuwa lengo letu. Tulijipanga tulivyoweza mpaka tukatoa rasimu ambayo kwa kiwango kikubwa ilizingatia maoni ya wananchi,” alisema.
Jaji Warioba alisema mwanzo wa Bunge waliamini kuwa maoni ya wananchi yatazingatiwa, lakini baadaye walishangaa kuona maoni ya vyama ndiyo yanazingatiwa badala ya wananchi.
“Lazima nikiri kwamba mwanzo wa Bunge hilo haukuwa mzuri. Sisi tuliamini kwamba chochote kinachokuja kitaangalia tulichofanya kwa msingi wa kuona wananchi wamesema nini….
“Lakini walivyoanza ikabidilika kabisa ikawa ni kwa msimamo wa vyama. Tukatoka kwenye msingi wa maoni ya wananchi tukaingia kwenye maoni ya vyama.”
Aliendelea kusisitza kuwa misimamo ya vyama ndiyo imeua matumaini ya kupata Katiba Mpya licha ya Tume hiyo kutoa nyaraka 10 za randama zinazoonyesha maoni ya wananchi na sababu ya mapendekezo ya rasimu hiyo.
“Nimewasikiliza kwa kirefu wajumbe wa Bunge la Katiba, inaonekana wengi hawakusoma taarifa tulizowapelekea. Tuliwapelekea nyaraka 10. Tuliwapelekea Rasimu, Randama inayoelezea kila ibara, maoni ya wananchi kisha sababu za mapendekezo,” alisema na kuongeza:
“Baada ya hapo kuna vitabu vikubwa viwili vinavyoeleza maoni ya wananchi. Kuna kitabu kingine cha maoni ya mabaraza. Kuna kile cha takwimu na kitabu cha utafiti. Sasa pamoja na vitabu vyote hivyo, bado watu wanazungumza bila kuzingatia yaliyoandikwa.”
Alisisitiza kuwa wajumbe wengi hawakusoma vitabu hivyo kwa sababu walikwenda bungeni na misimamo ya vyama vyao.
“CCM wana misimamo yao, Chadema yao, CUF na NCCR-Mageuzi nao wana yao.”
Kufutwa kwa vipengele muhimu
Akizungumzia kuhusu kuondolewa kwa mambo muhimu katika rasimu hiyo ya Katiba, Warioba alisema hali hiyo inatishia kupatikana kwa Katiba Mpya kama ilivyokusudiwa.
Alisema baada ya kuondolewa kwa vipengele muhimu katika Rasimu ya Katiba ni wazi kwamba Katiba itakayopatikana haitakuwa tofauti na iliyopo sasa.
“Katiba Mpya siyo kuandika waraka mpya, ni kuona kuna tofauti gani kati ya katiba hiyo na ile ya zamani. Kuna maeneo fulani ambayo ndiyo yaliyofanyiwa mabadiliko. Lakini kutokana na mambo yanavyokwenda yale mabadiliko makubwa hayapo tena,” alisema.
Aliyataja maeneo makubwa yaliyobadilishwa katika rasimu hiyo ni suala la maadili akisema kuwa wananchi walisisitiza kuporomoka kwake na kupendekeza njia za kudhibiti.
“Wananchi walikuwa wanataka lazima tuwe na mwongozo kwenye Katiba utakaowezesha kujenga utamaduni na maadili. Kwa hiyo katika rasimu tukaona kwenye utangulizi unaobeba misingi mikuu ya utaifa. Tukaona lazima kuimarisha misingi mikuu,” alisema.
Alisema katiba ya sasa inasema misingi mikuu ni uhuru, haki, udugu na amani na kwamba wananchi walitaka yaimarishwe hayo.
Jaji Warioba alisema wananchi walisema huwezi kuzungumzia haki bila usawa, huwezi kuzungumzia amani bila umoja na katika umoja lazima kuwe na mshikamano.
“Lakini wakasema msingi wa kwanza ni utu, kwa hiyo Tume ikazingatia misingi yote ya utu na maadili ikafika misingi minane badala ya minne.”
Alisema eneo lingine lililofanyiwa mabadiliko ni tunu ya taifa, akieleza kuwa wananchi walitaka ziwekwe kwenye Katiba kutokana na maelezo kwamba ndizo zinazojenga utamaduni wa Taifa.
Maadili ya Viongozi
Kuhusu maadili kwa viongozi, alisema walipendekeza, madaraka ya viongozi yawe ni dhamana, hivyo yawekewe kanuni, lakini Bunge badala ya kuheshimu maoni ya wananchi yamefanyiwa mabadiliko

Alisema Tume yake iliangalia sheria ya maadili wakaona haina nguvu sana na inategemea kiongozi mmoja.
Jaji Warioba alitoa mfano wa nchi ambazo hazikuwa na maadili ya viongozi madhubuti na kujikuta zipo katika matatizo makubwa kuwa ni Ufilipino.
Alisema katika nchi hiyo maadili ya viongozi yalikuwa yameshuka sana, rushwa imezidi, hivyo walipomwondoa madarakani rais wa nchi hiyo, Ferdnand Marcos, maadili ya viongozi wakayaweka kwenye katiba.
Alitaja nchi nyingine ambazo zimeweka maadili ya viongozi kwenye katiba ni Afrika Kusini, Namibia na Kenya.
Aliendelea kusema kuwa hata zawadi wanazopewa viongozi zinapaswa kuwa za Taifa ili kuepusha kuchanganya masilahi ya Taifa na masilahi yao binafsi hasa pale viongozi wanapopewa zawadi wakati wa kutia saini kwenye mikataba ya Serikali.
“Kwanza wananchi walisema zawadi anayopewa kiongozi inakuwa ni mali ya Taifa. Wakasema viongozi wanaingia mikataba na wanajifikiria wenyewe.
Pili, katika kuimarisha maadili kwa viongozi Tume ilipendekeza kiongozi asiwe na akaunti nje kinyume cha sheria.
Tatu, iwe ni wajibu wa kiongozi kutangaza mali zake, kiongozi lazima atofautishe kati ya masilahi yake na masilahi ya umma, na kiongozi aepuke kutumia mali ya umma kwa masiahi yake.
Hata hivyo, alisema mwelekeo wa Katiba Mpya umebadilika hasa baada ya mambo hayo kuondolewa na kuyafanya kuwa sheria za kawaida.
“Wenzetu yaliwashinda wakayaweka kwenye katiba, sisi tunayaondoa. Nimeshangaa hata waliposema uwazi na uwajibikaji siyo tunu. Lakini katika nchi yoyote lazima uzingatie uwazi na uwajibikaji ili kuepuka ufisadi na wizi,” alisema.
Kuhusu madaraka ya wananchi katika Katiba alifafanua haja ya wananchi kuwawajibisha viongozi wao wakiwamo wabunge akisema kuwa mamlaka hayo yameporwa na kupewa vyama vya siasa.
“Wananchi walisema sisi ndiyo wenye madaraka ya katiba, sasa tunataka mbunge wetu asiwe waziri. Pili tunataka ubunge uwe na kikomo.
“Uchaguzi siku hizi siyo kitu ni kama mnada tu. Walisema kama mbunge ameshindwa tuwe na madaraka ya kumwondoa hata kama muda haujafika, kwa sasa hawawezi kuwaondoa kwa sababu ya rushwa,” alisema na kuongeza:
“Lakini wamesema haiwezekani kumwondoa mbunge na watu watafanya mbinu za kuwaondoa wabunge. Lakini vyama vya siasa vimepewa mamlaka ya kuwaondoa wabunge na vimefanya hivyo. Wananchi wanaomchagua wanasema italeta matatizo.”
Kuhusu wabunge kutokuwa mawaziri, alisema walifanya utafiti na kuona ugumu wa kutenganisha madaraka ya Serikali na madaraka ya Bunge kwa sababu Serikali iko ndani ya Bunge.
Alisema kwa mabadiliko waliyopendekeza wao rais aondolewe bungeni abaki kuwa mtendaji na amiri jeshi mkuu na mawaziri wake wasiwe wabunge.
Alisema hata hivyo mapendekezo hayo yamekataliwa kwa madai kuwa mfumo wa sasa waliouzoea ni wa kibunge ambao Waziri Mkuu anakuwa mbunge na anakaa bungeni.
“Kuna nchi zenye mfumo huo kama vile Uingereza, Canada, Australia, ni nchi za Jumuiya ya Madola, mkuu wa nchi siyo mtendaji mkuu, bali waziri mkuu ndiyo anakuwa mbunge. Lakini hapa unakuwa na rais katika Bunge ambaye haingii bungeni. Kunakuwa na mkanganyiko,” alisema na kuongeza:
“Kinachofanyika ni Serikali inalibana Bunge ama Bunge linaingia katika mambo ya Serikali,” alisema.
Muungano
Kuhusu suala la muungano alisema Bunge la Katiba limekuwa likijadili udhaifu wa Serikali tatu badala ya kuangalia udhaifu wa Serikali mbili, huku wakipanga kupunguza mambo ya muungano.
“Sasa hivi nasikia wanataka kuondoa mambo mengi zaidi ya muungano. Sisi tuliyaondoa kwa kuwa na Serikali tatu. Lakini kwa sasa watayaondoa bila kuweka utaratibu,” alisema na kuongeza:
“Serikali ya muungano inashughulikia tu mambo ya Bara. Huoni Waziri wa muungano akivuka maji na kwenda kufanya kazi Zanzibar. Hiyo imeleta matatizo makubwa. Kwa kuwa Serikali ya Muungano inashughulikia zaidi mambo ya Bara,” alisema.
Alitoa mfano wa mikopo akisema kuwa Zanzibar haiwezi kukopa kwa kuwa haitambuliki kama nchi kimataifa bali ni lazima ije bara na ipate dhamana.
Huku akitoa mifano ya dira na mikakati ya maendeleo, Warioba aliendelea kufafanua kasoro za muungano.
“Chukua mfano wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 ni ya Bara maana Zanzibar wao wana Dira ya Maendeleo ya 2020. Mikakati ya maendeleo kama Mkukuta ni wa Bara, Zanzibar kuna Mkuza. Kama ni hivyo, Wazanzibari wanakuja Bara kufanya nini? Kwa nini wanakuja kushiriki katika maamuzi ya bara? Hilo limekuwa ni tatizo la kisiasa na yamekuwapo malalamiko ya muda mrefu.”
Aliongeza suala la kuwapo kwa migongano ya Katiba ya Muungano na ile ya Zanzibar huku moja ikisema nchi ni moja na nyingine ikisema nchi mbili zilizoungana.
Jaji Warioba alisema kutokana na mabadiliko muhimu yaliyopendekezwa na Tume yao kuondolewa, huenda kukawa na Katiba yenye mabadiliko kidogo.
“Wamechukulia yale mambo ya uongozi tu, uwe na muundo mpya wa Tume ya uchaguzi, uchaguzi wa rais, Rais achaguliwe kwa asilimia 50 na zaidi, uchaguzi wa rais unaweza kuhojiwa mahakamani. Lakini yale ya wananchi yameachwa.
Haki za binadamu
Kuhusu haki za binadamu, Warioba alisema kuwa wananchi walitaka vikwazo vilivyokuwapo viondolewe, hivyo tume ilifanya marekebisho ikiwamo kuweka mgombea binafsi.
Baada ya uchaguzi Katiba itapatikana?
Kuhusu suala la kuahirisha mchakato hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, Jaji Warioba alisema rais ajaye atalazimika kufuata sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kumalizia mchakato huo.
“Sheria ipo, sidhani kwamba akija atapingana nayo. Tumekusanya maoni, tumekwenda bungeni na tunangoja kura za maoni, kwa nini avunje sheria? Labda kwa kuwa sheria inasema wajumbe wa Bunge la Katiba ni pamoja na wabunge wa muungano, sasa kama hawakurudi sijui atafanyaje? Je, waendelee hao hao au wateuliwe wengine?” Alihoji.
Ardhi na Maliasili
Jaji Warioba pia ameshangazwa na Bunge hilo kuingiza masuala ya ardhi, maliasili na Serikali za Mitaa kwa siri akisema huko ni kuvuruga mchakato.
Alisema mambo hayo si ya Muungano na yanahitaji na yalipaswa kutolewa hadharani ili wananchi waone kwanza.
“Kuna mambo ambayo Bunge limeyafanya kwa siri. Wameingiza sura mpya kwenye rasimu, kuhusu ardhi na maliasili na Serikali za Mitaa,” alisema .
Alisema kuziingiza kwenye rasimu lazima muwe na uhakika kwamba yatatumika pande zote, na kwamba bara wana utaratibu wao wa Serikali za Mitaa na Zanzibar wana utaratibu wao wa ardhi na maliasili ambao ni tofauti kabisa na ule wa Bara.
Alisema kuweka kwenye Katiba ya Muungano mambo hayo ni kuvuruga. Huku akitoa angalizo kuhusu umiliki wa ardhi na rasilimali zake, Warioba alisema kuwa hilo ni suala linalopaswa kujadiliwa na kila upande wa muungano:
“Sisi tuliliona suala la ardhi na maliasili, lakini kwa kuwa siyo suala la muungano tukaliacha. Wananchi walisema Serikali haithamini ardhi yao, mtu anahamishwa kwa lengo zuri tu la kujenga shule au barabara, lakini fidia anayopewa hailingani na thamani ya ardhi yake. Wanahesabu miti tu, hatuwezi kumletea maisha mtu huyu,” alisema na kuongeza:
“Wanasema kama Serikali inapendelea wawekezaji wa nje na wa ndani. Hata hapa mjini matatizo yanatokea, watu wanahamishwa mtu mwenye uwezo akishatokea. Kwa mfano, mahali kuna madini wanaondolewa anapewa mwekezaji, mwananchi anaendelea kuwa masikini. Ilitakiwa kuwe na utaratibu ambao mwananchi mwenye ardhi awe anapewa asilimia tano, Serikali za Mitaa asilimia 10 na Serikali Kuu asilimia 25, wanataka wafaidi. Ndiyo siri ya mambo ya Mtwara.”
Jaji Warioba ambaye amewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Tume ya kuchunguza rushwa ya mwaka 1996, alisema kuwa anafarijika kuona kuwa anaaminiwa na Serikali na matokeo ya kazi zake yanafanyiwa kazi ndani na nje ya nchi.
Alimtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba kukubali kukosolewa kama yeye anavyokubali kukosolewa katika kazi zake.
“Nilipoanza wakati ule mengi yalisemwa, lakini nilijua, ukipewa kazi maalumu lazima upate mrejesho wa kila aina. Kuna wale ambao watakusifu na wengine watakusema na nilisemwa mengi sana. Lakini kwa kuwa nimefanya kazi ya Taifa siwezi kuhangaika na mtu mmoja mmoja.
“Alivyosema Sitta nakubaliana naye, kazi ya binadamu haikosi kasoro na sisi hatukuamini kwamba kazi yetu haikuwa na kasoro. Ilikuwa nazo, kulikuwa na mambo labda tulipitiwa. Ningefikiri, hayo anayosema angeyatumia na kwake, asifanye mambo kama hivi anavyofanya… Asikilize wale wanaosema kuwa ana kasoro, asije akafikiri kuwa hana kasoro.
Lakini mimi nashangaa sana mambo yanavyoendelea kwenye Bunge, hata siku hizi siangalii… ni kweli.
“Ni wakati fulani fulani mtu anaweza kunipigia simu, hebu angalia wanavyosema. Bado nina matumaini, wananchi hawa wametoa mawazo ya msingi, tukiyazingatia tutapata Katiba bora, tusipoyazingatia tutapata Katiba itakayoanzisha mgogoro,” alisema Jaji Warioba.
.

Sunday, 24 August 2014

Rasimu ya Warioba ‘yachanwachanwa’

Dodoma. Kuna kila dalili kwamba mabadiliko mengi yaliyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba yakigusa miundo ya taasisi nyeti za umma yatawekwa kando na huenda Bunge Maalumu likatoa Katiba isiyokuwa na mabadiliko makubwa kama ilivyotarajiwa.
Gazeti hili limebaini kuwa kamati nyingi za Bunge hilo zimebadili mapendekezo mengi hasa yanayowagusa viongozi na taasisi nyeti kama Bunge, tofauti na ilivyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Jaji Joseph Warioba.
Miongoni mwa mambo ambayo yamependekezwa kurejeshwa kama yalivyokuwa ni muundo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo kwa mujibu taarifa kutoka kwenye kamati mbalimbali, ni kuendelea na muundo wa sasa unaowajumuisha wabunge kutoka Zanzibar.
Katika maelezo yake, Jaji Warioba alisema moja ya kero za muungano katika eneo la Bunge ni malalamiko kwamba wabunge kutoka Zanzibar wamekuwa wakishiriki katika Bunge la Muungano na kushiriki kujadili mambo yanayohusu Tanzania Bara.
Kupitia mfumo wa Serikali tatu, Rasimu ilikuwa na mapendekezo ya kuwapo kwa Bunge la Muungano lenye wabunge 75, lakini mapendekezo hayo pia yamefutwa katika kamati karibu zote na kurejesha mfumo wa sasa pamoja na uwapo wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano, Hamad Rashid Mohamed alisema jana kuwa suala la muundo wa Bunge lilisababisha mvutano mkubwa katika kamati yake na baadhi ya wajumbe walikuwa wakihoji uwakilishi mkubwa wa wabunge wa Zanzibar katika Bunge la Muungano hata kwa mambo ya Tanzania Bara.
Hata hivyo, alitetea hali hiyo akisema uwapo wa wabunge kutoka Zanzibar ni moja ya masharti yaliyowekwa na Katiba. “Hata Katiba ya sasa imeweka sharti la idadi ya wabunge wa Zanzibar, hilo nalo ni sharti la Katiba huwezi kuliondoa, kama unataka kuliondoa unapotunga Katiba maana yake ni lazima uvunje muungano.”
Alisema mwaka 1964 mambo yote ya Tanganyika yaliingizwa kwenye Serikali ya Muungano... “Kwa hiyo ni lazima ukafumue Muungano, useme haya ni ya Tanganyika na haya ni ya Muungano,” alisema.
Hamad alisema katika hadidu ya rejea, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikatazwa kugusa mambo ya Muungano. “Hivi wabunge 70 wanaokuja kutoka Zanzibar wakazungumzia mambo ya Bara, hivi kuna dhambi gani, sioni kosa kabisa.” Mwenyekiti huyo alisema kamati yake imebaini kwamba Rasimu ya Warioba ina upungufu mwingi kwani hata baadhi ya kero zilizotajwa zilishafanyiwa kazi na Serikali.
Hoja ya ushiriki wa Wazanzibari katika masuala ya Tanzania Bara iliripotiwa kuibuka katika Kamati Namba Moja ambako mmoja wa wajumbe, Ally Keissy alinikuliwa akihoji sababu za wajumbe wa Zanzibar kushiriki mambo ambayo wao siyo sehemu yake.
Mbali na muundo wa Bunge, kamati nyingi pia zimefuta mapendekezo kadhaa yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo ni pamoja na wabunge kutokuwa mawaziri, ukomo wa ubunge kwa vipindi vitatu vya miaka mitano mitano, wabunge kuwajibishwa na wananchi, kupunguzwa kwa madaraka na kinga ya rais.
Katika Kamati Namba Tano, Hamad alisema suala la wananchi kumuondoa mbunge lilikataliwa. “Hivi ni kigezo gani ambacho kinaonyesha mbunge hakuweza kuwaletea wananchi maendeleo. Nini utatumia cha kupima ufanisi wa huyu mbunge?”
Alisema kuliweka jambo hilo katika Katiba ni kuleta matatizo na kwamba wameliacha suala hilo mikononi mwa vyama vya siasa kuangalia kama mbunge anafanya kazi ya ilani zao au la.
Mgawanyiko mpya
Habari zaidi zinasema kuwekwa kando kwa mapendekezo mengi yaliyolenga kurekebisha mifumo ya uongozi na utawala, kumesababisha mgawanyiko hasa miongoni mwa wajumbe watetezi wa muungano wa serikali mbili, ambao awali, waliahidiwa kwamba muundo huo usingekuwa na sura yake ya sasa, bali ungeboreshwa.
Mmoja wa wabunge wa CCM alisema jana kwamba: “Tutawapa wapinzani sifa maana umma utaamini kwamba bila wao hakuna kinachoweza kubadilika, sasa kama tunarejesha kila kitu ambacho kiko kwenye Katiba tuliyonayo kuna maana gani ya kuwa na mchakato?”
Mmoja wa wenyeviti wa kamati za Bunge Maalumu naye alisema kinachoendelea ndani ya kamati nyingi ni kufuta mapendekezo ya Rasimu na kuleta mapendekezo mapya ambayo ni sawa na yaliyomo kwenye Katiba ya sasa.
“Ndani ya chama (CCM) tuliamua kupinga mapendekezo ya serikali tatu baada ya kuahidiwa kwamba tutakuja na muundo wa serikali mbili zilizoboreshwa, lakini hata hizo hatuzioni. Kwa hiyo wananchi wataamini kwamba kilichosemwa na Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi), ni cha kweli,” alisema mwenyekiti huyo.
Utata wa akidi
Mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu, Dk Francis Michael aliamua kuahirisha kikao jana saa tano asubuhi kutokana na kile alichokiita kuwa ni kuwapa muda wajumbe waende kusoma zaidi sura ya tisa ambayo inahusu muundo wa Bunge.
Hata hivyo, habari ambazo zilikuwa zimelifikia gazeti hili mapema zinasema kuahirishwa kwa kikao hicho kulitokana na akidi kutotimia, taarifa ambazo Dk Michael alizikanusha kwa kuonyesha idadi ya wajumbe ambao walikuwa wamesaini karatasi ya mahudhurio.
Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo alikiri kwamba hadi ilipotimu saa 4:00 asubuhi jana kamati yake ilikuwa ikikabiliwa na upungufu wa wajumbe wanne, hivyo waliwapigia simu na kubaini kwamba walikuwa katika shughuli nyingine ikiwamo kumpokea Rais Jakaya Kikwete.
“Baadhi ya wajumbe ni mawaziri kwa hiyo baada ya kukamilisha majukumu yao walifika na saa tano hivi akidi ilikuwa imetimia,” alisema Dk Michael.

Profesa Mbilinyi afichua siri nzito

Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Profesa Simon Mbilinyi amefichua siri na kueleza kwamba wakati alipochaguliwa kuiongoza wizara hiyo nchi ilikuwa imefilisika.
Hata hivyo, alisema kuwa kwa ushirikiano na rais wa wakati huo, aliweza kuimarisha uchumi ndani ya siku 365 alizofanya kazi.
Profesa Mbilinyi aliyeshika wadhifa huo katika Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Rais Benjamin William Mkapa, alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Upanga, Dar es Salaam, ambapo alieleza hali ya uchumi ilivyo sasa ikilinganishwa na miaka 19 iliyopita.
Alisema wakati alipopewa jukumu la kuiongoza wizara hiyo mwaka 1995 na Rais Benjamin Mkapa, alikuta uchumi umetetereka kwa kiasi kikubwa, hata taifa kushindwa kukubalika na taasisi za fedha za kimataifa na wafadhili waliosusa kutoa misaada wala kuikopesha fedha.
“Mkapa aliniteua kuwa waziri wake wa fedha, lakini wakati ananikabidhi ofisi hiyo, hali ya uchumi ilikuwa ni mbaya sana. Nilikuta uchumi umetetereka, sababu hatukulipa madeni ya kimataifa, wakasusa. Kimsingi nchi ilifilisika, lakini hatukuweza kusema mbele ya wananchi,”alisema Profesa Mbilinyi na kuongeza:
“Nilikubali na kuanza kufanya kazi kama waziri tukishirikaina naye (Mkapa), katika mambo mbalimbali ili kuweka uchumi katika hali nzuri. Uhusiano baina ya Serikali na taasisi hizo za kimataifa pia nchi wafadhili haukuwa mzuri, kwa hiyo tukajitahidi kurudisha heshima yetu. Tulirudisha heshima na kukubali masharti machache ya msingi ya Shirika la Fedha Duniani(IMF) na Benki ya Dunia, ikiwamo suala la uanachama, uchumi ukaanza kufufuka.”
“Kwa kipindi hicho hatukuingia kwenye makubaliano mengine ya mikopo hadi baadaye sana. Kwa hiyo ndiyo ilikuwa njia ya kurudi kwa IMF na WB kwa kuzingatia hayo,”alifafanua Profesa Mbilinyi.
Baada ya muda kiasi alisema wakaanza tena kufanya makubaliano ya baina ya nchi mbili na kuanza tena kupata misaada hasa kutoka Korea Kaskazini, India, Japan na Urusi na baadaye uchumi ukaanza kuonekana unaweza kufufuka ndipo Benki ya Dunia ikarejea na makubaliano ya kawaida.
“Hata hivyo, sikukaa hapo muda mrefu. Nilifanya kazi zote ndani ya mwaka mmoja nikamaliza. Hapo tulishainua uchumi hadi ukakaa sawa, tulikuwa kwenye nafasi nzuri kiuchumi kama nchini nyingine wanachama wa Benki ya Dunia,”alisema.
Kiongozi huyo mkongwe wa masuala ya uchumi alisema, licha ya kuwa alifanya kazi kwa juhudi na bidii kwa ajili ya masilahi ya taifa katika Wizara ya Fedha, baadhi wa watu hawakuona jema katika hilo.
“Licha ya kuwa mambo yalienda vizuri, kipindi hicho cha mwaka mmoja nilijenga uadui na watu wengi kwani niliwazibia mianya ya ulaji. Hata hivyo, jambo hilo ndilo lililosababisha kuachia nafasi hiyo na kumwambia Mkapa:“Naenda kuendelea na ubunge wangu, mchague mwingine akusaidie katika masuala ya fedha,”alisema Mbilinyi na kuongeza kuwa hilo ni moja kati ya mambo yaliyoweka historia katika maisha yake ya kulitumikia taifa la Tanzania.
Profesa Mbilinyi ambaye pia amewahi kuwa mashauri wa kiuchumi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alisema baada ya uamuzi huo aliamua kujikita kwenye ubunge pekee.
“Wakati Mkapa aliponiteua kuwa waziri wake wa fedha nilikuwa mbunge wa Peramiho, hivyo baada ya mwaka mmoja na kama mwezi mmoja hivi nilipoamua kuachia wadhafa huo, nikawa mbunge kwa jimbo langu kwa miaka kumi, kabla ya kuacha kujihusisha na masuala ya kisiasa. Huo ndiyo ukawa mwisho na siasa zangu. Ilikuwa mwaka 2005,” alisema Profesa Mbilinyi.
Akilinganisha hali ya uchumi wakati alipokuwa waziri na sasa, Profesa Mbilinyi ambaye sasa anafanya shughuli za mshauri wa uchumi akiwa pia mkulima na mfugaji alisema kuwa kwa mtazamo wake mwenendo wa uchumi ni mzuri.
“Sasa hivi nadhani una matatizo ya kawaida, lakini tunaendelea vizuri. Kwa mwendo huu, nadhani tutafikia malengo ya kuwa kati ya mataifa yenye uchumi wa kati duniani ifikapo mwaka 2025, kama tukiendelea hivi ,” alisema Profesa Mbilinyi na kuongeza:
“Kwa gesi iliyogunduliwa, uwezekano wa kupatikana mafuta na madini, inatia imani kwamba tunaweza kufika mbali. Rais Kikwete awe wa mwisho kuiongoza Tanzania ikiwa katika hali ya umasikini. Lakini pia nampongeza Rais Kikwete kwa kufikisha uchumi wa nchi ulipo sasa.”
Kuteuliwa na Nyerere
Akizungumzia kuteuliwa kwake na Nyerere alisema: “Alikuwa mwalimu wangu nilipokuwa nasoma Shule ya Sekondari Pugu. Wakati anaondoka kwenda kuanza siasa mwaka 1955 alituacha pale. Nilimaliza shule 1956 nikawa nafanya kazi ya kuuza mafuta Sheli BP, Pugu.
Lakini wakati huo nilikuwa namsaidia Mwalimu kufundisha makada wa TANU ambao ni vijana.
Niliwafundisha hesabu na Kiingereza wakati wa usiku katika Mtaa wa Lumumba kwa sababu wakati ule watumishi wa Serikali walikuwa hawaruhusiwi kuingia kwenye siasa” alisema Profesa Mbilinyi.
Aliongeza: “Alipokuwa rais akakumbuka kuwa Mbilinyi yupo Chuo Kikuu na kwa vile nilikuwa nafundisha vijana wa TANU, basi akaniita mimi pamoja na Justine Rweyemamu tumsaidie kumsomea makaratasi yake ya uchumi.
Alikuwa anasema kuwa uchumi wake ni wa kisiasa, hivyo tukawa wasaidizi wake wa masuala ya uchumi pamoja na vijana wengine kama saba hivi.”
Alielezea kuwa alifanya kazi na Mwalimu Nyerere kwa maika minane na kwamba anamkumbuka kwa mambo mengi.

Kesi yafunguliwa Bunge la Katiba, Kesi ya kuhoji uhalali wake yafunguliwa

Dar es Salaam/Dodoma. Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma kwa sasa liko katika hatihati ya kuendelea baada ya kufunguliwa kesi ya kuhoji madaraka yake.
Kesi hiyo ilifunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana na Mwandishi wa Habari Saidi Kubenea, kupitia kwa wakili wake Peter Kibatala, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika kesi hiyo iliyopewa usajili wa namba  28 ya mwaka 2014, Kubenea anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba. Kubenea amefungua kesi hiyo akiomba mahakama itoe tafsiri hiyo, chini ya  vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya Marekebisho ya Katiba namba Namba 83 ya mwaka  2011.
Sambamba na kesi hiyo ya kuomba tafsiri ya mamlaka ya Bunge  hilo, pia Kubenea amewasilisha maombi mahakamani hapo akiiomba mahakama itoe zuio la muda la kusimamisha Bunge hilo ili kusubiri uamuzi wa maombi ya tafsiri hiyo.
Maombi hayo ya kusimamisha Bunge hilo kwa muda yaliyopewa usajili wa namba 29 ya mwaka 2014, pamoja na maombi ya msingi ya tafsiri ya mamlaka ya Bunge yote yalifunguliwa mahakamani hapo jana chini ya Hati ya Dharura.
Katika kesi hiyo ya msingi anaiomba Mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya masharti ya vifungu hivyo vya sheria hiyo na pia itamke kama Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.
Kwa mujibu wa hati ya madai, Kubenea anadai kuwa msingi wa kesi hiyo unatokana na uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Desemba Mosi, 2011, lililopitisha  Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Anasema sheria hiyo ilikuwa na lengo la kuratibu mchakato wa kutungwa kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Anaendelea kusema kuwa kutokana na sheria hiyo,  Rais aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na mambo mengine vilevile kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mapendekezo ya Katiba Mpya na kwamba kwa msingi huo Tume hiyo iliandaa Rasimu ya Katiba.
Anadai kuwa baada ya Tume hiyo kuundwa iliendelea kukusanya maoni ya wananchi yaliyotolewa katika mikutano ya hadhara na katika miundo tofauti ikiwamo mabaraza ya Katiba yaliyoanzishwa kila wilaya kwa lengo hilo.
Hati hiyo inaendelea kueleza kuwa kwa mujibu wa takwimu halisi za tume hiyo,  jumla ya watu 333,537 walitoa maoni yao katika nyanja tofauti, tofauti za mapendekezo ya Katiba, ambayo ndiyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyatumia kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya.
Inaendelea kueleza hati hiyo kuwa baada ya Rais kukabidhiwa rasimu ya mwisho Desemba 8, 2013, kwa mujibu wa vifungu vingine vya sheria hiyo, aliunda Bunge la Katiba kwa lengo la kujadili Rasimu ya Katiba na hatimaye kupata Katiba Mpya.
Hata hivyo, kwa mujibu wa hati hiyo baada ya Bunge la Katiba kuundwa, mjadala uliibuka ndani na nje  ya  misingi ya kisheria kuhusu mamlaka yake, kama Bunge linaweza kwenda kinyume na Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na tume hiyo.
Inaendelea hati hiyo kubainisha kuwa mjadala huu pia uliibuka ndani ya Bunge la Katiba lenyewe kuhusiana na mamlaka yake katika utekelezaji wa majukumu yake kama lina mipaka au la kwa mujibu wa vifungu hivyo 25 (1) na 25 (2) vya sheria hiyo.
Katika kusisitiza mjadala kuhusu mamlaka ya bunge hilo, hati hiyo inatoa mfano wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika mkutano wake wa mwaka, ambacho kilisema kuwa vifungu hivyo havilipi bunge hilo mamlaka ya kubadili rasimu hiyo.
Hati hiyo inaongeza kuwa wakati TLS wakitoa msimamo huo, kuna wataalamu wengine wa sheria wanadai kuwa  Bunge hilo linaweza kubadilisha na kuongeza ibara kadri itakavyoona inafaa bila kujali rasimu hiyo.
Kwa mujibu wa hati hiyo, mvutano huo ndani ya Bunge hilo ulisababisha baadhi ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje na kususia vikao, wakidai kuwa  rasimu hiyo haiwezi kubadilishwa. Msimamo huo wa wajumbe wa Ukawa, kwa mujibu wa hati hiyo ni  tofauti na wajumbe wengine waliobaki wanaodai kuwa Bunge hilo lina mamlaka ya kubadili vifungu vya rasimu.
Kwa mujibu wa hati hiyo, utungaji wa Katiba ni jambo la kitaifa ambalo si tu kwamba linabeba matumaini ya Watanzania bali pia linabeba mustakabali na ustawi wa nchi.
Hivyo, hati hiyo inaeleza kuwa tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge la Katiba dhidi ya Rasimu ya Katiba ni jambo  muhimu sana katika kuongoza mchakato huo ili kuhakikisha kuwa unakwenda kwa mujibu wa sheria zinazohusika.
Katika hati ya maombi, Kubenea anaomba mahakama itoe amri ya kusimamisha kwa muda vikao vya Bunge la Katiba vinavyoendelea Dodoma, kusubiri uamuzi wa  Mahakama kuhusu mamlaka yake.
Katika hati ya kiapo chake aliyoiambatanisha na kesi na maombi hayo, Kubenea anadai kuwa hata baada ya Wajumbe wa Ukawa kutoka nje, wajumbe waliobaki wanaendelea kujadili rasimu hiyo.
Hati hiyo ya kiapo inaeleza kuwa kufunguliwa kwa kesi hiyo sambamba na maombi hayo ya kusimamisha kwa muda Bunge la Katiba si tu kunalenga kupata tafsiri ya Kimahakama kuhusu mamlaka ya Bunge la Katiba.
Rafu Kamati za Bunge Maalumu
Wakati kesi hiyo ikifunguliwa, kumekuwa na taarifa ndani ya kamati za Bunge zinazoendelea kuchambua rasimu hiyo zinazoeleza kuchezwa rafu ili kuwezesha upatikanaji wa akidi kwa ajili ya hatua ya kupiga kura kupitisha ibara za rasimu hiyo katika baadhi ya kamati.
Hivi sasa kamati nyingi ziko katika hatua ya kupiga kura ili kupitisha ibara za Rasimu ya Katiba, kazi ambayo inahitaji theluthi mbili ya wajumbe kutoka pande za muungano kwa mujibu wa kanuni za Bunge Maalumu.

 Ili kutimiza matakwa hayo, gazeti hili limebaini kuwa rafu zimeanza kuchezwa hasa katika kamati ambazo zimeshindwa kutimiza sharti hilo. Moja ya rafu hizo ni ile ya mjumbe wa Kamati namba tano, Maida Hamad Abdallah kuhamishiwa kinyemela katika Kamati namba 8, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kuwezesha upatikanaji wa akidi katika kamati aliyohamia.
 Habari zinasema mjumbe huyo kutoka Zanzibar alishiriki kupiga kura juzi mchana na wajumbe wa kamati hiyo walielezwa kuwa amepelekwa ili kuziba nafasi ya Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum ambaye hawezi kushiriki vikao hivyo kutokana na kwamba ni mgonjwa.
 Hata hivyo, suala hilo lilizua mvutano kiasi baada ya baadhi ya wajumbe kuhoji uhalali wa uhamisho huo ambao ni kinyume cha kanuni za Bunge Maalumu, hasa ikizingatiwa kwamba alipigia kura mambo ambayo hakushiriki kuyajadili na kuyafanyia uamuzi.
Mwenyekiti wa Kamati namba tano, Hamad Rashid Mohamed alithibitisha Abdallah kuhamia kamati namba nane inayoongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Muungano, Job Ndugai kwa maelezo kwamba aliomba mwenyewe.
“Ni jambo ambalo ameomba mwenyewe kuhamia huko na ameruhusiwa maana hilo ni jambo la kawaida kama ambavyo wajumbe wengine kama kina Mbowe (Freeman) waliwahi kuomba, siyo jambo geni,” alisema Rashid.
 Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema hakuwa na taarifa za uhamisho huo. Alipoulizwa kuhusu iwapo Kanuni zinaruhusu alisema suala la kupanga ujumbe wa kamati liko chini ya mamlaka ya mwenyekiti wa Bunge hilo.
 “Kwa kweli sifahamu na wala sina taarifa hiyo, hilo suala la kanuni pengine hebu zisome ili ufahamu zinasemaje kuhusu mjumbe kuhama kutoka kwenye kamati moja kwenda kamati nyingine,” alisema Hamad.
 Wajumbe wa Bunge Maalumu waliokwisharipoti wanakaribia 450, idadi ambayo ni zaidi ya theluthi mbili ya akidi inayotakiwa, lakini hali ni tofauti kwenye kamati kutokana na sababu mbalimbali, utoro ikiwa mojawapo.
 Kutokana na mwenendo huo na wajumbe wengi kutoingia kwenye vikao licha ya kuripoti, kuna wasiwasi iwapo akidi itapatikana wakati wa kupitisha rasimu hiyo wakati Bunge Maalumu litakapoanza kukutana kwa umoja Septemba 2 mwaka huu.
Matakwa ya kanuni
Kanuni ya 55 (1) ya Kanuni za Bunge Maalumu Toleo la 2014 inasema: “Kamati zinaundwa na mwenyekiti kwa namna ambayo itawezesha kila mjumbe kuteuliwa kuwa mjumbe wa kamati mojawapo.”
Fasili ya pili ya kanuni inasema wakati wa kufanya uteuzi wa wajumbe hao, mwenyekiti atazingatia kwa kadri inavyowezekana idadi ya wajumbe inalingana kwa kila kamati na uwiano kutoka pande zote za muungano.
Kadhalika kanuni hiyo inasema katika uteuzi wake mwenyekiti atazingatia idadi ya kila aina ya wajumbe ilivyo katika Bunge Maalumu, jinsia, wajumbe wenye mahitaji maalumu na uwepo wa wajumbe wenye utaalamu wa sheria.
Kanuni hiyo iko kimya kuhusu uhamishaji wa wajumbe na fasili yake ya nne inasema: “Ujumbe katika kamati utadumu kwa kipindi chote cha maisha ya Bunge Maalum.”
Waraka wa uchambuzi wa mgawanyo wa wajumbe katika kamati unaonyesha kuwa Kamati namba tano alikotoka Maida ina wajumbe 52 na kati yao 34 wanatoka Tanzania Bara na 18 Zanzibar wakati kamati alikohamia pia ina wajumbe 52; 35 kutoka Tanzania Bara na 17 kutoka Zanzibar.
Kwa maana hiyo hata kama uhamisho wa Maida ungekuwa na lengo la kuimarisha uwiano kwa maana ya pande za muungano, ni dhahiri kwamba unaathiri kwa maana ya idadi wajumbe kutoka Zanzibar katika kamati namba tano.
Gazeti hili lilimtafuta Ndugai kwa lengo la kupata maelezo jinsi alivyompokea mjumbe huyo, lakini kutwa nzima ya jana simu yake ilikuwa ikiita bila majibu. Kadhalika Maida naye alitafutwa lakini simu yake ilikuwa imezimwa wakati wote. Maida hakuwamo kwenye kamati yake ya awali namba nne ilipokutana jana mchana baada ya kuwa wamepumzika asubuhi kupitia sura za nyongeza.
Kupitisha uamuzi
Kanuni hizo pia zinaelekeza kwamba wakati wa kupitisha uamuzi lazima wajumbe wawe wamefikia theluthi mbili kwa pande zote za muungano, jambo ambalo limekuwa gumu kutokana na mahudhurio hafifu kwenye kamati husika.

Pinda abadili upepo urais CCM

Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameingia rasmi katika mbio za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), hatua ambayo imebadili mwelekeo wa kinyang’anyiro cha nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015.
 Gazeti hili limethibitisha kwamba Pinda tayari ameamua kujitosa kuwania nafasi hiyo kupitia CCM ambayo tayari inawaniwa na makada wa chama hicho wasiopungua 15 na baadhi yao wameishatangaza nia zao kwa nyakati tofauti.
Habari kutoka ndani ya CCM zinasema uamuzi wa Pinda kuwania urais mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwakani, umesababisha kiwewe miongoni mwa wagombea na kunakifanya kinyang’anyiro hicho kuchukua sura mpya.
Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM aliliambia gazeti hili siku chache zilizopita mjini Dodoma kuwa: “Na sisi tumesikia kwamba PM (Waziri Mkuu) amejitosa na kama ni kweli atawasumbua wagombea wengi kutokana na rekodi yake hasa katika uadilifu.”
“Yeye (Pinda) ana faida tatu kubwa; kwanza hana kundi katika chama, anaelewana na watu wote, pili nafasi yake ya uwaziri mkuu inampa nafasi ya kufahamika kwa watu wengi na tatu rekodi yake ya uadilifu, hana kashfa za ovyoovyo, labda kama ataharibu dakika hizi za mwisho,” alisema kiongozi huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Wengine ambao wamekuwa wakitajwa kuwania uraia kupitia CCM ni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na mtangulizi wake katika nafasi hiyo, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
 Wegine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta. Wengine wanaotajwa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Katiba, Asha-Rose Migiro.
 Pia wamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige na aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Balozi Ali Karume.
Wasomi
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema wingi wa wanaojitokeza kutaka kuwania urais ni njia ya kuunda mtandao utakaomwezesha mtu fulani au mmoja kunyakua tiketi hiyo.
“Watu wanapiga kampeni katika harambee kwa njia ya kutengeneza mitandao, kwani ukifika wakati wa chama kumpitisha mgombea, asiposhinda ataibuka na kuwaeleza kuwa mnaoniunga mkono mimi muungeni fulani,” alisema.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema kujitokeza kwa idadi kubwa ya wanaowania nafasi ya urais, kutatoa fursa ya wananchi kutambua udhaifu wa kila mmoja jambo litakalowezesha kupatikana kwa mtu sahihi wa kupeperusha bendera ya chama hicho.

“Wakiwa wengi, kila mmoja atataka kuonyesha umahiri wake na sisi ambao ni wananchi watawaliwa tutaweza kutambua upungufu wa kila mmoja, jambo litakalosaidia kupatikana kwa mtu sahihi,” alisema Mbunda
Kambi ya Pinda 
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa siku kadhaa mjini Dodoma ambako vikao vya Bunge Maalumu vinaendelea umebaini kuwa kambi ya Pinda inaongozwa na Mwenyekiti wa Mamlaka za Mitaa Tanzania (ALAT) ambaye pia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi.
 Inadhaniwa kuwa Dk Masaburi atatumia ushawishi wake kwa viongozi wa mamlaka za miji na wilaya zinazoongozwa na wenyeviti wa halmashauri na mameya wa miji, manispaa na majiji kumuunga mkono mgombea huyo ambaye pia hivi sasa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ziko chini ya ofisi yake.
Wiki hii kundi la wafuasi wa Pinda likiongozwa na Dk Masaburi lilikuwa mjini Dodoma likijaribu kutafuta kuungwa mkono na makada viongozi wa CCM ambao walikuwa wakishiriki kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho pamoja na wale walioko katika Bunge Maalumu.  Habari zinasema mbali na Dodoma, tayari kambi hiyo imeshafanya vikao kadhaa jijini Dar es Salaam na Visiwani Zanzibar lengo likiwa ni kutafuta kuungwa mkono na makada wa CCM katika sehemu hizo. Hivi sasa nguvu za Pinda zinaelekezwa katika mikoa mingine nchini kwa lengo hilohilo. Kutokana na kasi ya kambi yake, wafuasi wa baadhi ya wagombea wameanza kufuatilia mwenendo wao kwa lengo la kukusanya ushahidi wa kile wanachokiita ‘rafu’ zinazochezwa ili kupata ushahidi unaoweza kutumika dhidi ya mgombea huyo wakati mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM utakapoanza mapema mwakani.
Itakumbukwa kwamba makada watano wa chama hicho ambao ni Lowassa, Membe, Makamba, Wassira na Ngeleja wanatumikia adhabu na wapo chini ya uangalizi wa chama hicho baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni za urais kabla ya muda kutangazwa. 
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema hivi sasa ni mapema mno kusema ni lini mchakato wa kupata wagombea wa nafasi za uongozi ndani ya chama hicho utaanza na kwamba wakati mwafaka ukiwadia wananchi watafahamishwa.
Uwezo, udhaifu wake
Hata hivyo wakosoaji wake wanasema Pinda akiwa Waziri Mkuu hana cha kujivunia na kwamba amekuwa mzito kufanya uamuzi mara kadhaa kiasi cha kusababisha baadhi ya mambo muhimu ya nchi kukwama na kwamba kwa maana hiyo hastahili kuwa rais.
“Ni kitu gani ambacho nchi inakikumbuka kuhusu huyu bwana ambacho alikifanya katika miaka yake ya uwaziri mkuu, kama alikuwa kwenye nafasi kubwa kiasi hicho na hakuna alichofanya, atawezaje kumudu madaraka ya mkuu wa nchi?” alihoji mmoja wa makada wakongwe wa CCM.
Waziri mmoja wa sasa (jina tumelihifadhi), alisema Pinda hana uwezo wa kuongoza nchi, kwani wao wakiwa mawaziri ameshindwa kuwasaidia katika kero mbalimbali walizokuwa wakimfikishia kama kiongozi wao.
 “Muulize waziri yeyote kuhusu uwezo wa jamaa, kila kukicha tunampelekea mambo tunayokutana nayo, lakini hakuna kinachowezekana kwake, atakwambia subiri leo, subiri kesho na hatimaye jambo linaishia hivyohivyo,” alisema.
Kwa upande mwingine, watetezi wake wanasema Pinda wanayemnadi ni yule aliyepata kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – Tamisemi) kiasi cha kuonekana anafaa kuwa Waziri Mkuu.
 Wanasema kushindwa kwake kufanya kazi ipasavyo ni matokeo ya sababu zilizomfanya mtangulizi wake, Lowassa kung’oka katika nafasi yake.

Friday, 1 August 2014

AJIRA: Watu 6,740 kuwania nafasi 47 za kazi TBS

Dar es Salaam. Watu 6,740 leo wanatarajia kufanyiwa usaili wa kuwania nafasi 47 zilizotangazwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Aprili, mwaka huu.
Usaili huo unataka kufanana na ule wa Idara ya Uhamiaji ambao ulihusisha waombaji 10,000 waliokuwa wakiwania nafasi 70, utafanyika leo na kesho katika Ukumbi wa Yombo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Ili kuepuka kuchaguliwa kwa waombaji wenye uhusiano na wafanyakazi wa shirika hilo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake, Joseph Masikitiko aliliambia gazeti hili jana kuwa kazi ya usaili itafanywa na taasisi nyingine na TBS itapelekewa majina 47 ya watakao kuwa wamekidhi vigezo.
Masikitiko alisema ili kuepuka upendeleo pia, wameamua kujivua kusimamia mchakato huo na utafanywa na taasisi mbalimbali, na akiitaja moja ya taasisi hizo kuwa ni ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua).
“Kuna taasisi tumezichagua zisimamie usaili huo, wao watasimamia na wakikamilisha watatuletea majina hayo,” alisema.
Alisema wameamua kufanya hivyo ili kuepuka yale yaliyowakumba wenzao wa Idara ya Uhamiaji.
Aliongeza: “Hata hizo taasisi tulizoomba zinapaswa zitende haki na ziepuke kutumiwa na baadhi ya watu ambao siyo waaminifu, tunahitaji wafanyakazi watakaopatikana wawe wenye sifa zinazotakiwa.”
Usaili wa Uhamiaji uliofanyika katika Uwanja wa Taifa Dar es Salasam, ulihusisha zaidi ya watu 6,000 kati ya watu 10,000 walioomba nafasi hizo.
Baada ya usaili wa watu 6,115, walipatikana 1,681 ambao waliingia katika kinyang’ayiro cha kusaka watumishi 70.
Hata hivyo, Serikali ilisitisha ajira hizo 70 baada ya kuzuka kwa tuhuma za upendeleo uliokithiri wakati wa usaili.
Kati ya nafasi za kazi 22 zilizoombwa, nafasi iliyoombwa na watu wachache ni ya ofisa maabara msaidizi ambayo imeombwa na watu 61 na anatakiwa mtu mmoja.
Katika nafasi ya mhasibu msaidizi, wameomba watu 1,360, lakini wanaotakiwa kuajiriwa ni watu watatu tu.
Nafasi zilizotangazwa na shirika hilo na idadi ya walioziomba katika mabano ni ya mhasibu msaidizi (1,350), mkaguzi msaidizi wa ndani (266), msaidizi wa mahesabu (305), ofisa rasilimali watu (857), Ofisa viwango (211), maofisa ubora wa viwango (752) na wataalamu wa hali ya hewa (117).
Wengine ni mhandisi wa mitambo (89), fundi mchundo (88), ofisa maabara msaidizi (61), msaidizi wa maabara (141), Mtaalam wa mifumo ya kompyuta (307), katibu muhtasi (247) na ofisa uhusiano wa kampuni na umma (342).
Pia kuna nafasi ya dereva (408), wahariri (71), mwanasheria (140), mkutubi (80), msimamizi msaidizi wa kumbukumbu namba moja (230), msimamizi msaidizi wa kumbukumbu namba mbili (501) na ofisa masoko mwandamizi (167).

Malecela: Wakati utafika wasomi watabaki kwenye taaluma zao

Katika toleo la jana Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela alizungumzia historia yake katika siasa na mchakato wa Katiba Mpya. Katika sehemu ya pili ya mahojiano na gazeti hili, anaeleza pamoja na mambo mengine, ubinafsishaji, ajira na ushiriki wa wasomi kwenye siasa.
Swali: Kuna taarifa kwamba uliwahi kuwekwa ndani kutokana na ushiriki wako katika harakati za ukombozi kupitia Tanu. Hili likoje?
Malecela: Sikuwekwa ndani kwasababu ya harakati za Tanu, hapana. Wakati narudi kutoka India baada ya kumaliza masomo yangu ya shahada ya kwanza, nilipita njia ya Mombasa, kutoka Mombasa nikaja Arusha. Arusha pale alikuwepo Nsilo Swai ambaye alikuwa mwalimu wangu Mazengo halafu India tukasoma wote, kwa hiyo alikuwa pale kama Katibu Mkuu wa Meru Cooperative Union. Nikaona nipite kwake nikae pale siku mbili, tatu hivi, kutoka Arusha nikaja Dodoma. Nilipofika tu nikaitwa kituo cha polisi. Nilipofika pale wakapekua mizigo yangu sasa wakanikuta na kitabu kimoja cha George Padimo ambacho kilikuwa kinaitwa Pan Africanism or Communism, wale wapekuzi kwa bahati mbaya hawakuwa Wazungu walikuwa ni weusi wenzangu.
Basi wakasema huyu mtu ana chembe-chembe za ukomunisti huyu ngoja tumweke ndani. Nililala mahabusu pale siku mbili aliyekuja kunitoa alikuwa ni Mzungu. Wakati huo wa Waingereza kila siku lazima mkuu wa polisi aende akaripoti kwa Mkuu wa Wilaya akieleza kwake ana watu wangapi mahabusu na makosa yao.
Sasa alipokwenda kuripoti kwamba kwenye mahabusu wana kijana ametoka India na wanafikiri kwamba ni mkomunisti, akawaambia kwamba mleteni. Mkuu wa Wilaya huyo alikuwa anaitwa Eyas, nikaenda ofisini kwake bahati yule Eyas alikuwa ni raia wa Ireland. Sasa nilipofika ofisini kwake akaagiza chai tukawa tunakunywa, akasema Waingereza hawa wabaya ndio maana sisi tunapigana nao we kijana angalia usifanye ovyoovyo.
Wakati huo ulikuwa mwaka 1959. Basi akanihubiria hapo, baada ya hapo akawaambia wale polisi ujinga huo, huyu hawezi kuwa mkomunisti, huyu ni Mgogo mwacheni arudi kwao. Na kweli yule Mkuu wa Wilaya alifurahi kuona kuwa mimi nimetoka kijijini huko akanipeleka mpaka nyumbani Mvumi kwa gari yake.
Swali: Hapa tulipo kuna tatizo kubwa la ajira na wengi wamelizungumzia, wewe unalizungumzia vipi?
Malecela: Kwanza nataka muelewe huku tulikotoka chama kilikuwa kinasema nini. Chama kilikuwa kinawakilisha siasa ya ujamaa na kujitegemea ndio maana katika miongozo mingi ya Tanu na baadaye Chama Cha Mapinduzi, ilikuwa kila siku inaomba watu wajiunge pamoja katika vikundi ili kuzalisha. Nitawapa ushahidi wakati nikiwa kwenye Baraza la Mawaziri.
Mara tu tulipopata uhuru Nsilo Swali alikuwa ndio Waziri wa Mipango wakalizungumzia hilo la ajira ya vijana Dar es Salaam. Wakasema si tunayo mashamba ya sukari Kilombero, basi wakachukua vijana pale zaidi ya 3,000 wakakaa nao, nakumbuka walisindikizwa na treni la kwenda Kidatu kuwapeleka vijana waende wakafanye kazi na walipewa mishahara kama ya miezi miwili na vifaa vyote vya kwenda kukata miwa. Hiyo yote ilikuwa ni nguvu za kuwapa vijana ajira.
Wakaenda kule miezi mitatu baadaye hakuna hata mmoja aliyebaki. Niwape ushuhuda wa karibuni wakati Mama Kunambi (Bernadetha, DC wa Dar es Salaam) aliwahi kuja na wazo lilelile, mimi nikamwambia wazo hili huko nyuma tulijaribu, lakini baada ya miezi mitatu wote wakawa wamerudi hapa. Kwanza tukapita kwenye mashamba ya mkonge tukatafuta vibarua, sio ya wasomi hapana, ni ya vijana kufanya kazi kwa mikono. Mama Kunambi akahesabu vijana wake 3,000, hizi rekodi sijui kama Ilala wanazo, tukahangaika, tukawapeleka hawa vijana kwamba waende wakafanye kazi huko na wao wakakubali.
Tukawapa mishahara miezi miwili kabla hata hawajafika huko. Baada ya miezi mitatu minne wote wakawa wamesharudi Dar es Salaam. Sijui kwa nini tukianza kusema ajira mimi nahisi mara nyingine sisi Watanzania tunaanza kujiona Serikali yetu haifanyi chochote, ndio maana tunakuwa na matatizo haya tunasahau hili ni tatizo la ulimwengu mzima.
Ni kweli wenzetu walioendelea tatizo hili linakuwa tofauti, kwa mfano Uingereza utakuta vijana wasiokuwa na ajira ni wengi, lakini kule mara nyingine ni kwa sababu ya kuchagua kazi ambayo ni sawa na huku ambako watu wanafikiri kuwa bado wanaweza kupata kazi ya kufagia ofisini na siyo kwenda kukata mkonge.
Kwa hiyo hili tatizo la vijana tunalo, lakini sisi kama Tanzania tunachotakiwa kufanya ni vitu viwili ambavyo kweli tuvifanye kwa juhudi kubwa kabisa maana yake ndio urithi ambao baba wa taifa ametuachia wa kukabiliana na matatizo yetu. Kama tunaweza kuboresha maisha ya vijijini kweli huwezi kupata wamachinga Dar es Salaam. Jamani kwa sababu ninyi ni watu wa habari naomba muende mkachunguze Dar es Salaam, muone hawa watu wa Lushoto, Wasambaa nenda kahesabu hawa watu kama utamkuta Msambaa Dar, hakuna, kwanini?
Mimi nimekwenda Lushoto unakuta kijana ana eka yake ya nyanya, anailima vizuri kweli kweli na kiutaalamu. Ukiilima eka moja vizuri, inakupa zaidi ya tani mia moja za nyanya na kule wanalima mara tatu kwa mwaka.
Kwa hiyo kule Lushoto hupati vijana wa kuja kuwa wamachinga, hapana.
Swali: Viwanda vingi vilibinafsishwa haiwezi kuwa sababu ya tatizo la ajira?
Malecela: Mimi sisemi kuwa viwanda vingi vimebinafsishwa ndio tatizo la ajira, hapana. Ninachosema kuna wakati katika miaka ya 1970 Tanzania ilikuwa na viwanda vingi vya nguo. Kiwanda cha Urafiki kilikuwa kimeajiri zaidi ya vijana 3,000, Ufi (Kiwanda cha zana za kilimo) kiliajiri watu 1,000 na Tanita (cha kubangua korosho) kiliajiri wafanyakazi 2,000.
Sasa vyote hivyo akaja mtu akutuambia ohhh kuendeshwa na Serikali haifai, hivi vinatakiwa viende binafsi. Tulivyosema hivyo viendeshwe na watu binafsi, Wahindi wakaja kwanza wakapandisha bei ya korosho. Korosho kilo moja Sh800.
Viwanda vyetu vikakosa korosho kwa hiyo vikasimama na hii imetokea juzi juzi hapa bei ya korosho imeanguka kutoka Sh800 kwa kilo hadi Sh120. Walipoona viwanda vimedorora havifanyi kazi na vyama vya ushirika vimekufa kwa sababu vilikuwa vikiendeshwa na hii biashara ya korosho, wakapunguza bei.
Nenda Morogoro yaani unajua vitu vingine tunasema tu, lakini mimi ambaye niliona viwanda vikifanya kazi leo napita Morogoro unaweza kuona ni mji unaokufa, lakini vilipokuwa vinafanya kazi pita pale saa 10:00 jioni unaona watu wanatoka kule kwenye viwanda sasa wanakuja mjini we mwenyewe unashangaa hivi hii ni Tanzania.
Kwa viwanda tukadanganywa ohh vitu vinavyoendeshwa na serikali haviendi, vibinafsishwe tukasahau kwamba vingine watu wale wanakuja na nia kabisa anakinunua kiwanda palepale anakifunga.
Nenda Mwanza mfano mzuri na huu ndio huwa unanisikitisha kweli kweli, ukiwa unakwenda uwanja wa ndege mkono wako wa kushoto utaona magofu makubwa, yale magofu yalikuwa majengo ya kiwanda kikubwa cha ngozi.
Akaja mtu akabinafsisha akachukua mitambo yote kauza Kenya sasa ukienda pale unalikuta jumba tu tupu.
Swali. Kwa hiyo kwa kifupi ubinasfisishaji haukuwa kitu kizuri?
Malecela: Kwanza binafsi nisingependa kuhukumu kuhusu ubinafsishaji. Mimi ninasema kila kitu mnapokifanya jamani mkifanye hatua kwa hatua. Siku za nyuma tulikuwa hatuna haja ya kuleta hizi juisi kutoka nje ya nchi, tulikuwa na kiwanda cha kutengeneza juisi ya machungwa lakini hata kilivyokufa sijui. Tulikuwa na kiwanda cha betri Matshushita. Unajua Matshushita kilivyokufa? Tajiri mmoja aliingiza betri za matshushita kutoka Indonesia akauza, Matshushita wakaja serikalini wakasema kama hivi tutafunga, wakafunga.
Barabara ya Pugu (Nyerere) ilikuwa mahali ambapo ikifika jioni watu wanatoka kazini unaangalia unajua kweli tuna viwanda, lakini vingi vimefungwa. Pale Dar es Salaam tulikuwa na viwanda vya nguo tulikuwa na Sungura Textile, tulikuwa na Tasini, tulikuwa na kama viwanda vinne vya kutengeneza nguo. Arusha General Tyre, tulikuwa na viwanda viwili vya nguo hiki A-Z kilifikia wakati hadi kinatengeneza nguo za ndani wakiziweka lebo ya mark Spencer, unatoka hapa unakwenda kununua vest Uingereza kumbe inatengenezwa Arusha.
Swali: Kuna wimbi sasa kila mtu anagombea ubunge, maprofesa, madaktari wanaacha kazi zao wanagombea ubunge. Unafikiri ni kwanini?
Malecela: Nadhani hasa kwa wasomi mimi nasema Mungu anisamehe kama ninawasingizia, wengi walifikiri nikiwa mbunge nitakuwa waziri. Kwa huko nyuma maprofesa wachache walipata uwaziri kweli. Walipoanza kuja kwa fujo na kwa wingi ikawa haiwezekani tena, halafu wengine hata ufanisi wao ulikuwa mdogo.
Swali; Pamoja na hapo kuna wimbi hili la watoto wa viongozi nalo linakuja kwa kasi!
Malecela; Mimi nataka kuwaambia kwa kweli hilo la kusema watoto wa wanasiasa mnawaonea. Unamkuta mzee yeye mfua vyuma, anatengeneza visu amekaa na mfuko wake. Mtoto anakaa pembeni anaona baba yake anapopuliza moto, anaona mpaka chuma kinavyokuwa chekundu. Anamwona baba yake anavyokwenda kukigongagonga hadi kinakuwa kisu, ama kama jembe na kadhalika.
Sasa mbona watoto wa walimu wakichukua ualimu hatusemi? Watoto wa madereva wakiwa madereva hatusemi, ila watoto wa viongozi wakiwa wanasiasa mnasema. Sisi tuna msemo kwamba; ukimwangalia ng’ombe mguu wa mbele utakapokanyaga na huu wa nyuma utakuja kukanyaga hapohapo.
Kwa hiyo hawa watoto wa wanasiasa bwana wakati mwingine wanaongozana na baba anapokwenda mahali, mara nyingine haendi kwa sababu anavutiwa na mkutano hapana, yeye anakwenda tu ili apande gari la baba. Kwa hiyo anakwenda pale baba anahutubia pale anaona, sasa watakuwa wajinga sana kama hawajifunzi. Kwa hiyo mimi nasema watoto wa viongozi tuwahukumu kwa utendaji wao.
Kweli kama mtu akianza kutumia jina la baba yake ohh mimi mtoto wa fulaniatashindwa.
Swali: Unatoa ushauri gani kwenye hili wimbi la wasomi maprofesa na madaktari kukimbilia kwenye siasa?
Malecela: Mimi sina ushauri wowote. Ni kama nguo, zilikuja watu wakaanza kulalamika jamani wasichana lakini baadaye ni mtindo ulipita. Hata hivi sasa wengi watakwenda kwenye siasa lakini muda ukifika watagundua kuwa kwenda kwenye siasa ni kupoteza muda.
Swali.Ukiwa Waziri Mkuu, ulikuwa ndio msimamizi wa shughuli zote za Bunge. Kuna kipindi Bunge lilikuwa moto na hasa wakati wa G 55 unaweza kulizungumzia hili?
Malecela: Siwezi kulizungumzia sana kwa sababu kipindi hicho kilipita. Ni kweli kulikuwa na kundi la G 55 ambao walikuwa wanataka Tanganyika. Katika Muungano Tanganyika nayo ionekane iwe Serikali ya Tanganyika ya Zanzibar halafu Muungano. Ilikwenda ilivyokwenda lakini mwisho ikaishia kwenye chama ambacho kilipeleka kwa wanachama basi mambo yakamalizika.
Swali: Ukiwa Waziri Mkuu changamoto uliyoipata unaizungumziaje?
Malecela: Changamoto huwezi kuizungumzia kwa sababu hizi ndizo zinazokujenga kwa wakati huo kwamba ukisikia jina Malecela unalinganisha na hiki na hiki; vizuri na vibaya.
Swali: Ukiwa Waziri Mkuu, uliwahi kujionyesha hadharani kuwa wewe ni mpenzi wa timu ya mpira ya Simba Sports Club, uliwahi kukacha safari yako moja kwa ajili ya kwenda kushuhudia Simba ikifanya vitu vyake uwanjani. Sijui kwa sasa hali yako ikoje kimichezo?
Malecela: Mechi zote ambazo nimewahi kuwa mgeni rasmi Simba inacheza, ilishinda. Ngojeni niwape historia kidogo, mimi wakati nikisoma Shule ya Sekondari Minaki, Dar es Salaam kulikuwa na timu tatu. Kulikuwa na timu ya Wazungu, timu ya Wahindi, Magoha na Waarabu na timu ya Waafrika.
Nendeni kwenye historia mchele walikuwa wanakula Wahindi, Wasomali na wengine Mwafrika ulikuwa huruhusiwi kununua mchele mpaka upate kibali. Sasa hata kama ukiwa mchezaji namna gani, timu ya wazungu ilikuwa ikiitwa Sunderland sasa hata uwe nani ilimradi wewe ni mweusi huwezi kuichezea timu hiyo.
Hii ya wahindi, magoha na waarabu ilikuwa ikiitwa Cosmo Club hata uwe nani huwezi kujiunga na kama sio wa jamii hizo.
Kwa watu weusi ilikuwa Yanga Africans, sasa wewe hata utake kucheza mpira wa namna gani lazima ukawe Yanga. Kwa hiyo hakukuwa na chaguo hivyo mtu ukiwa mpenzi wa mpira lazima tu uwe mwana Yanga.
Kwa hiyo wazungu walipoanza kuondoka ile Sunderland ikaanza kupungukiwa nguvu wakajitahidi kujiunga na Cosmo.
Nao walipoanza kuondoka na kuhama ndio baadaye wakaanza, jamani tuwachukue na wenzetu. Wakawachukua na waafrika na mwenyekiti wa kwanza na ndio akaleta na jina la Simba alikuwa Amon Nsekela. Karume alikuwa Yanga kwa sababu wakati ule hakuwa na chaguo.
Swali: Hadi sasa bado wewe ni shabiki wa Simba?
Malecela: Mimi napenda mpira mzuri tu. Kuna wakati nilikuwa nafikiri hii vita ya Yanga na Simba ilikuwa inadumaza mpira. Nilipokuwa Waziri wa Kilimo kwa kweli nilijitahidi nikaunda timu ikaenda kucheza na hizi timu kubwa zikaenda droo. Baada ya hapo wachezaji wangu wakachukuliwa mmoja mmoja na mtu wa kilimo akafanywa kuwa Mwenyekiti wa Yanga na timu yetu ya Kilimo ikafa.

Swali Kuna jambo ambalo ungependa lifahamike kwa wananchi?
Malecela: Ningependa wananchi wafahamu kwamba maendeleo ni hatua. Mimi nimekwenda Nigeria nimeendesha gari kutoka Abuja kwa barabara mpaka Port Harcourt jamani, umaskini niliouona kule ni wa kupindukia, huwezi kuulinganisha na wetu hata kidogo.
Mimi nilipokwenda kuripoti Tukuyu ilinichukua siku mbili kufika. Siku ya kwanza niliondoka Dodoma na basi nikalala Iringa. Kutoka pale kesho yake nikalala Mbeya ndio nikafika Tukuyu. Lakini sasa ukitoka Dodoma saa 12:00 asubuhi Mbeya saa tisa umeshafika.
Hapa ilikuwa safari ya hapa (Dodoma) hadi Iringa ilikuwa ni maili 240 ilikuwa ni ya kutwa nzima. Unaondoka hapa asubuhi na mabasi haya ya Urafiki unafika kule jioni, lakini sasa hivi unaondoka Iringa saa 12:00 asubuhi saa 4:00 asubuhi uko Dodoma.
Kinyago
Katika sebule ya Mzee Malecela mjini Dodoma ameweka kinyango kikubwa mfano wa mti ambao umebeba watu wakiwa wamebeba vitu mbalimbali.
Malecela anakizungumzia kinyago hicho kilimgharimu sh 300,000 wakati akiwa Waziri Mkuu miaka ya tisini na kilichongwa kwa muda wa miezi miwili.
Kama hiyo haitoshi anasema mchongaji wa kinyago hicho ambaye sasa ni marehemu alikuwa akiifanya kazi hiyo tu kwa kipindi cha miezi miwili ambapo ilimlazimu kumuwekea wafanyakazi kwa ajili ya kumfulia, kumpikia na kumfanyia vitu vingine ili atumie muda mwingi kuchonga kinyago hicho.
Anasema kinyago hicho kimetengenezwa kwa kutumia shina la mti aina ya mpingo na hata kuingia katika sebule yake ilimlazimu kuvunja moja ya dirisha kutokana na ukubwa wa kinyago hicho ambacho ilishindikana kupita mlangoni.
Twende kwenye elimu, nimekuwa Chancellor (Mkuu wa Chuo) wa Open University (Kikuu Huria) kwa miaka 20 tumekuwa na mikutano ya ‘machancellors’. Bado Tanzania tuna vyuo vikuu vingi kuliko jirani zetu Kenya, Uganda na sasa ukishakuwa kuliko Kenya na Uganda sembuse Rwanda na Burundi. Hata Zambia, hata Msumbiji hawajafika hivyo mimi nasema kuwa hili jambo la Watanzania kunung’unika kila siku kwamba hatuna hiki hatujafanya hivi, ni kana kwamba hatujafanya maendeleo nasikitika sana tunajitukana.
Wengine wanaosema hivyo hawajatoka waende wakaone na mahali pengine palivyo. Nenda Horohoro mpaka wa Tanzania na Kenya, ukija kwetu unaona watu, vijiji na nyumba za bati, palepale unapita mpaka unaenda Kenya, utaona tofauti.
Ukiangalia ukubwa wa nchi ukichukua Kenya na Uganda ukaziweka pamoja bado Tanzania ni kubwa kuliko nchi hizo kwa zaidi ya maili 6,000. Kwa hiyo wenzetu wakijenga barabara ya lami zaidi ya km 150 wameshafika kwenye mpaka wa nchi, lakini sisi kujenga barabara kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma ni zaidi ya Km 1000.
Nafikiri kwa nyinyi watu wa habari ukianza kuzungumzia vitu vizuri ambavyo Serikali imefanya wataanza kutukana huyo amekuwa CCM number two au CCM B .
Swali.Sasa hivi tunaona vyuo vyote vinatoa shahada, hata vyuo vya kutoa vyeti au stashahada vinabadilishwa, unalizungumziaje hili?
Malecela: Na hilo ni kosa kubwa sana unapokuwa na mhandisi lazima huku chini uwe na watu wa kukuunga mkono, sasa hao ndio tulikuwa tunawatoa mafundi, Mbeya, Dar Technical ni kweli ulivyosema.
CBE sasa imekuwa chuo kikuu. Chuo cha Mipango kilijengwa kwa lengo la kusaidia maendeleo vijijini, malengo ya Mwalimu (Nyerere) kila kijiji kiwe na mtu ambaye anaweza akasaidia mipango ya maendeleo sasa ni chuo kikuu.
Mimi nilipokuwa India, nimeona mtu na shahada ya uzamili lakini ni kondakta wa daladala, kwa nini? Kwa sababu Chuo Kikuu cha Bombay kilikuwa kinapokea zaidi ya wanafunzi 60,000 kila mwaka.Ndio nakwambia sasa tuna viwanda vya kutengeneza mabomu.

JOTO 2015: Mrema asema yuko tayari kumkabili Mbatia

Moshi. Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema (TLP) amesema amejiandaa kuingia ‘vitani’ na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye ametangaza kuwania ubunge katika jimbo hilo, mwaka 2015.
“Siogopi mtu yeyote. Nimejiandaa vilivyo kwa mpambano huu. Najivunia rekodi yangu nzuri ya utendaji wala sitishiki na wananchi wangu nimewauliza wameniambia nisihofu,” alisema Mrema.
Kwa mujibu wa Mrema, anaamini rekodi yake nzuri ya utendaji ndiyo itakayomuuza mwaka 2015 na kwamba, ni rekodi hiyo nzuri ndiyo iliyowafanya wananchi wa jimbo hilo wakamchagua mwaka 2010.
“Umesahau nilikuwa mbunge wa Moshi Vijijini wakati huo ikiwa ni pamoja na Vunjo? Rekodi yangu nilipokuwa naibu waziri mkuu inajieleza. Yeye (Mbatia) aje nimejiandaa kwa mpambano,” alisema.
Juzi, Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa, alisema kwa sasa ameelemewa na maombi ya makundi mbalimbali ya jamii yakimtaka agombee ubunge katika jimbo hilo mwakani.
“Nimefuatwa mara kadhaa na viongozi wa dini wakiniomba nigombee tena 2015. Wapo wananchi wamenifuata hadi bungeni. Simu yangu imejaa meseji nyingi za kuniomba,” alisema Mbatia.
Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliwahi pia kuwa mbunge wa kwanza wa jimbo hilo chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1995 hadi mwaka 2000.
“Hayo maombi ya wananchi siwezi kusema nawakatalia, mimi ni nani nikatae kuwatumikia Watanzania wenzangu? Niko tayari kuwatumikia ila wajue kwa sasa kuna mbunge,” alisema.
Mbatia aliongeza, “Natarajia kwenda Vunjo wakati wowote kuanzia leo ili nitoe jibu rasmi mbele ya Wanavunjo. Nashukuru kwa heshima hii waliyonipa. Naahidi sitawaangusha.”
Wiki iliyopita, baadhi ya wananchi waliodai kuwawakilisha wenzao kutoka kata zote za jimbo hilo, walitoa tamko lililosomwa na Mathew Temu wakimtaka Mbatia agombee ubunge kupitia vyama vya NCCR, Chadema na CUF vinavyounda Ukawa. Katika tamko hilo, wananchi hao walisema rekodi ya Mbatia alipokuwa mbunge haijawahi kuvunjwa.