Dar es Salaam. Siku moja baada ya maudhui ya Ripoti ya Tume
iliyoundwa kuchunguza matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana kuwekwa
wazi, wadau wa elimu wamekiri na kusema kuwa mfumo wa elimu ya Tanzania
upo katika hali mbaya.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mbunge wa
kuteuliwa na Rais, James Mbatia alisema matokeo ya tume hiyo yanaonyesha
udhaifu wa hali ya juu katika sekta ya elimu jambo ambalo alishawahi
kulisema katika hoja maalumu bungeni.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi,
alisema alishawahi kuishauri Serikali kuufumua mfumo wa elimu nchini na
kuanza upya ili kunusuru taifa la kesho ambalo ndilo linaloathirika na
rasilimali watu zisizo na ubora.
Matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana
yalionyesha kuwa asilimia 60.6 ya wanafunzi Tanzania walipata alama
sifuri na wanafunzi 23,520 sawa na asilimia tano ndiyo waliofaulu jambo
ambalo lilisababisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuunda tume ya kuchunguza
matokeo hayo.
Baadaye, mitihani hiyo ilisahihishwa upya na Pinda kukabidhiwa matokeo Juni, mwaka huu.
“Nilishasema katika hoja yangu bungeni Januari 31
na Februari 1, mwaka huu nikamwomba waziri anionyeshe mitaala ya elimu
ya sasa, lakini hakuitoa,” alisema Mbatia.
Mbatia alisema ili taifa hili liondokane na janga
la elimu lililopo halina budi kukubali kuwa ni kweli Tanzania ipo katika
janga la elimu na kuunda dira ya elimu itakayotuongoza katika safari ya
elimu nchini.
Mbatia aliongeza kuwa elimu ya Tanzania ipo
mahututi na kuwa kila mwaka wanafunzi wanaomaliza katika shule
mbalimbali hawana sifa za kutosha za kuweza kushindana katika masoko ya
kimataifa.
“Tumeshaanza kuona taifa linaangamia kwa sababu ya
ubovu wa elimu, ni lazima tukiri hilo kwa sababu hata Rais alikiri na
kuikubali hoja yangu Aprili 30 mwaka huu alipokuwa mkoani Mbeya” alisema
Mbatia
Mbunge huyu ambaye awali aliteuliwa kuwa miongoni
mwa wajumbe wa tume ya uchunguzi wa matokeo haya na kukataa kushiriki
alisema, ili Serikali iondokane na janga hili haina budi kuunda Kamati
ya Bunge ambayo itaisimamia Serikali na kutoa mawazo mapana kuhusu
elimu.
Mbatia alishauri Bunge lisiegemee itikadi za vyama
au porojo za kutaka sifa za kisiasa na badala yake suala la elimu
lijadiliwe kwa maslahi ya taifa.
Mdau mwingine wa elimu, Dk Method Samwel, ambaye
ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(DUSE), alisema tatizo la elimu hapa nchini lielekezwe zaidi kwenye
mfumo uliopo kuliko laumu taasisi au mtu mmoja mmoja
Dk Samwel alisema tangu zamani mfumo wa elimu umekuwa ni wa
kudorora na haya ni matokeo ya mfumo huo ambao haukuwa na misingi imara
kwa muda mrefu.
Alitolea mfano wanaokwenda kusomea ualimu wengi ni
wale waliofeli kwa kupata daraja la nne, jambo ambalo linasababisha
wataalamu wa kada hiyo kuwa ni wale waliofeli pekee.
“Yapo mambo mengi yanayotakiwa kufanyiwa kazi
katika sekta ya elimu Tanzania, suala la kudai kuwa Baraza la Mitihani
na Taasisi kuwa ndizo taasisi zenye makosa, hazina ukweli,” alisema.
Hata hivyo, Dk Samwel alisema, tume hiyo bado ina
maswali mengi ya kujibu kulingana na walichokisema katika sehemu ya
ripoti yao.
“Nashindwa kuelewa kwa sababu kila nikisoma majibu
ya tume hiyo napata maswali mengi zaidi. Kwa mfano, walimu waliofanya
mtihani wakafeli walipewa muda wa kujiandaa? “ alihoji na kuongeza:
“Na kuhusu mitihani ya Tanzania kuonekana kuwa ni
migumu zaidi, Je waliwapa mitihani ya Tanzania wanafunzi wa nchi
nyingine au walitumia mbinu gani kupata matokeo hayo?”
Hata hivyo, Mkuu wa Kitivo cha Elimu wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo, alipinga ripoti ya tume hiyo na
kusema kuwa wamepotosha taarifa kwani tatizo halikuwa katika mtihani
bali ni wanafunzi wenyewe wamefeli.
Dk Mkumbo amesema tatizo si la walimu, wala
baraza, wala mitihani yenyewe bali ukweli utabaki kuwa wanafunzi
walifeli mtihani wa Kidato cha Nne kwa sababu ya mfumo mbovu wa elimu.
Mhadhiri huyo alihoji tena kuwa tume hiyo ilitumia
njia gani kujua kuwa mtihani wa Sayansi ulihitaji saa sita kuufanya na
ni kwa mbinu gani waliupima mtihani wa Tanzania na kujua kuwa ni mgumu
kuliko mitihani mingine.
“Nilipata ripoti fulani iliyoonyesha kuwa mitihani
ya Tanzania ni mizuri na haina matatizo, ripoti ilionyesha kuwa haina
chembe ya mashaka na inatungwa kwa ustadi. Tusitafute sababu, tatizo si
mitihani ni wanafunzi wenyewe wamefeli,” alisema.
Pia, Dk Mkumbo alisema kuwa ni dharau kubwa kusema
kuwa baadhi ya wasahihishaji hawakuwa na sifa kwani hilo ni tusi kubwa
kwa walimu kwani wao ndiyo wamekuwa wakisahihisha kila siku.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule
Binafsi nchini,(Tamongsco), Albert Katagira alisema si kweli kuwa
mtihani ulikuwa mgumu bali tatizo lipo katika uandaaji wa wanafunzi.
“Mtihani ulikuwan sahihi kabisa, mbona wanafunzi wengine
walifaulu. Ni wanafunzi wenyewe, ambao nao hatuwezi kuwalaumu moja kwa
moja,” alisema Katagira.
Alisema taifa bado lina tatizo katika mfumo wa
elimu na kuweka mkazo katika masomo ya sayansi na hisabati ambayo
yanaonekana kuwa magumu kwa wanafunzi wengi.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mafinga,
Mustapha Mambea alisema, mtihani wa Fizikia na Kemia haikuwa migumu,
lakini kuna mada kadhaa ambazo hawakufundishwa.
Profesa Mchome aongea
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alisema kuwa wameshindwa kuiweka hadharani
ripoti hiyo kwa kuwa bado inafanyiwa kazi serikalini.
Profesa Mchome, ambaye ndio aliongoza tume hiyo,
alisema kuwa ripoti hiyo inatakiwa kupelekwa kwenye kikao cha Baraza la
Mawaziri kwa ajili ya kujadiliwa.
Alidokeza, hata hivyo, tayari walikuwa wameanza
kufanyia kazi baadhi ya vitu vinavyotakiwa kufanyiwa kazi haraka kwenye
ripoti hiyo.
Katibu Mkuu wa Necta, Dk Joyce Ndalichako, ambaye
ameomba likizo ya muda mrefu ikitafsiriwa pengine ndio mwanzo wa
utekelezaji wa ripoti hiyo.