Graf, ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi
nchini, alisema kuwa hivi karibuni Serikali ya Uswisi ilisaini mkataba
wa kimataifa wa kubadilishana taarifa kuhusu masuala ya fedha, ambao
unajulikana kwa lugha ya Kiingereza kama `Convention on Mutual
Administrative Assistance in Tax Matters’.
Alisema ikisaini mkataba huo ina maana itasaidiwa na Serikali ya Uswisi kupata fedha zilizofichwa na Watanzania.
“Serikali ya Tanzania inatakiwa kuweka mkakati wa
kisheria utakaotengeneza mazingira ya kubadilishana taarifa za fedha na
mataifa mengine. Kwa jambo hilo hata Serikali ya Uswisi inaweza kusaidia
katika kupatikana kwa fedha zilizofichwa,” alisema Graf, ambaye
anaongoza Serikali ya Uswisi kwani kwa kawaida Rais wa Bunge ndiye pia
kiongozi wa taifa hilo.
Graf alisema kwa sasa itakuwa ngumu kwa Tanzania
kupata fedha hizo kwani haijasaini mkataba wa kimataifa wa kubadilishana
taarifa za fedha na mataifa mengine.
Alieleza pia katika miaka ya karibuni Serikali ya
Uswisi imeandaa muswada wa sheria wa kubana fedha zilizopatikana kwa
njia za kifisadi na kufichwa katika benki za Uswisi. Graf alisema sheria
hiyo ikipita itaruhusu Serikali ya nchi hiyo kutaifisha fedha ambazo
zimepatikana kwa njia haramu na kufichwa katika benki za huko.
Muswada huo unaoitwa kwa lugha ya Kiingereza
`Freezing and Restitution of Assets of Politically Exposed Persons
obtained by Unlawful Means Bill’ ulisomwa kwa mara ya kwanza kwenye
Bunge la nchi hiyo mwezi Mei, mwaka huu.
Graf alisema faida nyingine ya Tanzania kusaini mkataba huo ni kuwa, itaweza kuwatoza kodi Watanzania hao walioweka fedha huko.
Alifafanua kuwa siyo fedha zote zinazowekwa kwenye
benki za Uswisi kuwa ni haramu kwani kuna nyingine zimepatikana
kihalali, lakini zinaweza kutozwa kodi.
“Tanzania inakosa kodi kutokana na fedha
zilizohifadhiwa na Watanzania wenye akaunti kwenye benki za Uswisi,”
aliongeza Graf, ambaye alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo Novemba 26,
2012 na kutakiwa kukaa madarakani kwa mwaka mmoja.
Graf alisema pia fedha za kodi zingeisaidia Tanzania kugharimia sekta mbalimbali za maendeleo.
Zito aitupia lawama Serikali
Naye Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, ambaye yuko nchini
Uswisi akifuatilia masuala ya utoroshaji fedha na kufichwa kwenye benki
za huko, alisema kuwa wakati shinikizo la dunia sasa limeelekea kumaliza
tatizo la ukwepaji kodi na utoroshaji wa fedha kutoka nchi za Afrika,
lakini Serikali ya Tanzania inasuasua juu ya kupambana na jambo hilo.
Zitto alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari kuwa moja ya njia ya Serikali za nchi maskini kupata taarifa za
kampuni kubwa za kimataifa yanayokwepa kodi ni mfumo wa kupashana
taarifa unaoitwa kwa lugha ya Kiingereza `automatic exchange of tax
information’.
“Kutokana na shinikizo la nchi mbalimbali, hivi
sasa nchi zinazoitwa `tax havens’ (nchi zinazohifadhi fedha kwa siri)
fedha zimeanza kuweka sahihi makubaliano ya kutoa taarifa,” alisema
Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema).
Alisema kuwa Tanzania mpaka sasa haijaweka saini
na Serikali haijatoa taarifa yoyote kwa umma juu ya sababu ya
kutokufanya hivyo. “Ghana, Afrika Kusini na Nigeria nchi zinazotegemea
sana rasilimali kama Tanzania zimeweka saini mkataba huu tayari,”
aliongeza Zitto.Alisema asilimia 44 ya fedha za kigeni inazopata
Serikali ya Tanzania zinatokana na mauzo ya madini nje. Kampuni za
madini ndizo zinazoongoza kukwepa kodi.
Alisema Tanzania inapoteza jumla ya Dola 500
milioni (Sh783 milioni) na Dola 1.25 bilioni (Sh2 trilioni) kwa mwaka
kutokana na kampuni kubwa za kimataifa kukwepa kodi.
“Hii ni sawa na kusema Tanzania inapoteza Dola2 milioni (Sh3.1 bilioni) kila siku kwa uporaji huu,” alisema Zitto.
Zitto alisema Serikali lazima ichukue hatua mara moja kuhakikisha Tanzania inaingia makubaliano ya kupashana taarifa za kikodi.
Jaji Werema agoma kujibu
Alipoulizwa juu ya Tanzania kutokusaini mikataba
ya kimataifa ya kubadilishana taarifa za utoroshaji fedha na mambo au
kodi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema hawezi
kujibu suala hilo.
“Muulize huyo aliyekwambia kuwa Tanzania
haijasaini mikataba ya kubadilishana taarifa za utoroshaji fedha na
masuala ya kodi. Naomba uniache nifanye kazi zangu,” alijibu Jaji Werema
kwa mkato na kukata simu.
Mahojiano kamili na Rais wa Uswisi, soma Mwananchi Jumapili.

No comments:
Post a Comment