Friday, 11 October 2013

Serikali yatangaza nafasi za kazi 1,100

Serikali kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi za kazi 1,134 katika sekta mbalimbali za ofisi za umma.
Kwa mujibu wa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi nafasi hizo za kazi ambazo zinapatikana katika tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ya www.ajira.go.tz ni kwa ajili ya waajiri mbalimbali wa ofisi za umma.
Katibu alifafanua kuwa nafasi 949 ni kwa ajili ya waajiri walioainishwa katika ofisi za wizara, halmashauri na nyingine 185 ni za taasisi na wakala mbalimbali za Serikali.
Aidha, amewataka waombaji wote wa fursa za ajira kufungua matangazo yote mawili ya kazi na kuzingatia masharti ya Matangazo yote kama yalivyo katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili kabla ya kutuma maombi yao Aprili 9, 2013.
Daudi alifafanua kuwa waajiri ambao watatoa ajira hizo ni makatibu wakuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Maendeleo Jinsia na Watoto, Wizara ya Kazi na Ajira na Ofisa Mtendaji Mkuu Wakala wa Vipimo.
Wengine ni Makatibu wakuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi, Wizara ya Maji na Katibu Ofisi ya Rais Maadili.
Wengine ni Makatibu Tawala wa Mikoa ya Kagera, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Mwanza, Shinyanga, Manyara, Dar es Salaam, Morogoro, Geita, Pwani, Mara, Kilimanjaro, Lindi, Singida, Tabora, Tanga, Katavi na Arusha; pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za majiji na manispaa Mwanza, Iringa, Songea, Shinyanga, Morogoro, Singida, Kigoma/ Ujiji na Temeke.
Nafasi nyingine ni kwa ajili ya wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya Mufindi, Kyela, Rungwe, Mbeya, Chunya, Biharamulo, Bukoba, Muleba, Namtumbo, Songea, Morogoro, Makete, Mkuranga, Mbinga, Tunduru, Ukerewe, Sengerema, Ilemela, Busega, Maswa na Meatu.
Nyingine ni Wilaya za Shinyanga, Kishapu, Kilosa, Msalala, Rufiji, Rorya, Ruangwa, Lushoto, Mkinga, Mpanda, Monduli, Ngorongoro, Kigoma, Nachingwea, Rombo, Same, Singida, Urambo, Tabora, Babati, Mbulu, Simanjiro na Kiteto.
Pia zimo Wilaya za Handeni, Pangani, Kibondo, Chamwino Mtwara, Nanyumbu, Mpwapwa, Kongwa na Tandahimba pamoja na halmashauri za miji ya Njombe na Kibaha. Nafasi nyingine ni za Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) na Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa).
Nafasi hizo zilizotangazwa zimegawanyika katika kada zifuatazo; Mchambuzi Mifumo ya Kompyuta daraja la II – (nafasi 10), Ofisa Vipimo II – nafasi 6, Mpima Ardhi, daraja la II (nafasi 26), Mhandisi daraja la II – Ufundi Umeme – Nafasi 9, Ofisa Mipango Miji daraja la II– nafasi 13 na Mhandisi daraja la II - Ujenzi (Nafasi 16).
Pia wanahitajika wahandisi daraja la II - Maji (Nafasi 13), Ofisa Misitu daraja la II (nafasi 7), Ofisa wa Sheria daraja la II – nafasi 3, Mtakwimu daraja la II – nafasi 8 na nyingine mbalimbali.

Pinda atengua amri ya Magufuli

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana amefuta agizo lililotolewa na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli la kuwataka wamiliki wa magari makubwa ya mizigo, kutozwa asilimia tano kwa kila gari litakalozidisha uzito na kuagiza kurudiwa kwa utaratibu wa zamani wa msamaha wa asilimia tano ya tozo hiyo.
Pinda pia ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Wizara ya Ujenzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Uchukuzi na Ofisi ya Waziri Mkuu kukutana na Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa),Chama cha Wamiliki wa
Malori (Tatoa) ili kukubaliana kwa pamoja kuhusu tozo hiyo. Agizo hilo la Magufuli alilolitoa takribani siku nne zilizopita, liliathiri kasi ya upakuaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam kutokana na mgomo huo wa malori.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Pinda alisema, katika mazingira yaliyopo sasa, ushirikiano kati ya Serikali na wadau unahitajika. “Ni lazima wadau washirikishwe ili kusiwe na malalamiko na mambo yaende vizuri,” alishauri Pinda.
Alisema, awali utaratibu uliokuwa unatumika ulipewa baraka na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu (sasa Ujenzi), Basil Mramba ambaye baada ya wadau wa usafirishaji kulalamika kuhusu ubovu wa barabara na mizani, alitoa unafuu wa kupunguza asilimia tano ya uzito utakaosomwa katika mizani (utakaozidi).
“Lengo lake ilikuwa ni kufidia matatizo ya upungufu wa mizani kutoweza kupima kwa usahihi uzito wa magari yanayopimwa katika vituo mbalimbali vya mizani nchini, lakini hivi sasa mizani yetu ni mizuri na ya kisasa,” alisema na kuongeza:
“Lakini ikumbukwe kuwa agizo hilo lilikuwa kinyume na Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 toleo la 2002 na kanuni zake za mwaka 2001, ambayo inazuia malori kuzidisha uzito. Mramba aliamua vile ili kumaliza hali iliyokuwa imejitokeza wakati akiwa Wizara ya Miundombinu,” aliongeza Pinda. Alisema kati ya kanuni hizo, kanuni ya 7(3) inatoa sharti la kama lori likibainika kuzidisha mzigo,sharti ni ama kupanga upya mzigo ili kupunguza uzito,kuushusha mzigo uliozidi au kupigwa faini mara nne ya faini ya kawaida. Pinda alisema baada ya kuibuka kwa mgomo huo alikutana na wadau wa usafirishaji na mawaziri wa wizara zenye dhamana na ujenzi na usafirishaji, kubaini kuwa kulikuwa na ulazima wa wizara hizo kukutana na wadau ili wakubaliane.
Bandari walia na mgomo
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA),imeeleza kuwa wananchi ndiyo wataumia kwa kulazimika kulipa hasara iliyotokana na mgomo huo.
Kaimu Meneja Mawasiliano wa Bandari hiyo, Janeth Ruzangi alisema hali hiyo itatokana na wafanyabiashara kulazimika kupandisha bei ya bidhaa mbalimbali zilizokwama kwa siku kadhaa bandarini hapo ili kufidia gharama walizotozwa na wamiliki wa meli.

Tumetoka kifungoni na hamasa kubwa

Gazeti la Mwananchi leo limerudi tena mitaani baada ya Serikali kulifungia kwa wiki mbili. Kama wasomaji wetu na wananchi kwa jumla wanavyokumbuka, Serikali kupitia Idara ya Habari (Maelezo) ililifungia gazeti hili Septemba 27, 2013 kwa madai kwamba lilichapisha habari mbili tofauti ambazo ilidai zilikuwa za uchochezi na kwamba zilikuwa na lengo la kuwafanya wananchi waichukie pamoja na vyombo vyake vya ulinzi na usalama.
Sio nia yetu hapa kueleza kwa undani maudhui ya habari tulizozichapisha na Serikali kuzitumia kama nondo ya kulifungia kwa muda huo mrefu. Hata hivyo, yafaa angalau kwa muhtasari tu kuweka sawa kumbukumbu za hatua hiyo ya Serikali ambayo tunasema bila kutafuna maneno kwamba ilikuwa ya uonevu na ya kiwango cha juu cha matumizi mabaya ya madaraka.
Hata hivyo, huu hakika sio wakati wa kumtafuta mchawi, kwa maana ya kutaka kujua nani hasa serikalini alitoa amri ya kulifungia gazeti hili kwa sababu ambazo sisi tunaona hazikuwa na chembe ya mashiko. Tulishangazwa kuona amri hiyo ya Serikali ikitolewa wakati mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete akiwa nje ya nchi, tena akiwa katika majukumu mazito ambayo dunia nzima ilikuwa ikiyafuatilia kwa shauku na umakini mkubwa.
Kulifungia gazeti wakati huo hatuoni kama ilikuwa kwa masilahi ya taifa kwa sababu hatua hiyo iliichafua taswira ya nchi yetu na bila shaka Rais Kikwete alijikuta katika wakati mgumu kila alipoulizwa kuhusu hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali yake.
Ni habari zipi zilizolipeleka gazeti hili kifungoni? Habari ya kwanza ilikuwa juu ya waraka kuhusu mishahara mipya ya watumishi wa Serikali ambayo tuliithibitisha pasipo kuacha shaka yoyote kutoka katika vyanzo vyetu vya habari vya kuaminika katika mamlaka za juu serikalini.
Tuliuchukulia kama taarifa muhimu sana kwa watumishi wa Serikali na wananchi kwa jumla na hatukuona sababu ya Serikali kutaka wananchi wafichwe kuhusu kuwapo kwa mishahara mipya kwa watumishi wake.
Itakumbukwa kuwa, wiki chache kabla ya gazeti hili halijachapisha habari hiyo, lilikuwa pia limechapisha habari kuhusu mishahara mipya katika sekta binafsi kwa mujibu wa waraka wa Serikali uliotolewa na Wizara ya Kazi na Ajira. Swali linalojitokeza hapa ni hili: Inakuwaje mishahara mipya ya watumishi wa Serikali iwe siri na mishahara mipya kwa sekta binafsi iwe kinyume chake?
Tunaamini kwamba utamaduni wa Serikali kuficha habari na taarifa zenye manufaa kwa umma siyo utawala bora hata kidogo. Ni hivi majuzi tu Rais Kikwete alipomwagiwa sifa na Rais Barrack Obama kwa kutia saini mkataba wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi.
Habari ya pili iliyochapishwa Agosti 17 mwaka huu na kusababisha gazeti hili kufungiwa ilihusu Serikali kuimarisha ulinzi katika maeneo ya karibu na misikiti jijini Dar es Salaam jana yake kufuatia kuwapo tetesi kwamba waumini wa Kiislamu siku hiyo wangeandamana kupinga kitendo cha Jeshi la Polisi kumuweka mahabusu Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda. Baadhi ya waumini walikuwa wameonyesha kukasirishwa na kitendo cha polisi kumwondoa Sheikh Ponda katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) na kumpeleka katika Gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam.
Habari hiyo yenye kichwa cha habari; ‘Waislamu wasali chini ya ulinzi mkali wa polisi’ ilichapishwa ikiwa na mmoja wa mbwa waliokuwa na polisi katika doria kutokana na hofu ya kuzuka vurugu baada ya Swala ya Ijumaa, Agosti 16. Habari hiyo ilisema Waislamu hawakuandamana na waliswali kwa amani na utulivu na kwamba polisi hao waliokuwa na mbwa, huku wengine wakitumia pikipiki kufanya doria walitanda katika mitaa mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ulinzi. Lakini kwa mshangao wetu, Serikali katika kujaribu kuhalalisha kulifungia gazeti hili ilitoa tafsiri ya uongo kwamba habari tuliyochapisha ilisema kwamba mbwa walipelekwa katika maeneo ya ibada, wakati habari hiyo haikuwa na kitu kama hicho. Serikali ilidai katika taarifa hiyo, kwamba lengo la habari hiyo lilikuwa kuichonganisha na waumini wa Kiislamu ili waichukie pamoja na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, kwani kwa Waislamu mbwa ni haramu na picha hiyo iliudhalilisha Uislamu. Taarifa hiyo potofu ya Serikali imetuthibitishia pasipo kuacha shaka kwamba haikuwa na nia njema na gazeti hili.
Hatua ya kulifungia gazeti hili kwa sababu za kufikirika imesababisha maumivu kwa watu wengi. Vijana (vendors) waliokuwa wakiuza na kusambaza gazeti hili pamoja na familia zinazowategemea wameumia. Waandishi wa kujitegemea wanaolipwa kutokana na habari wanazotuma gazetini wameumia pamoja na familia zao. Hivyo hivyo, watoa matangazo na wasomaji waliokuwa wakilitegemea gazeti hili kwa habari za uhakika nao pia wameumia. Hasara ambayo MCL imepata kutokana na hatua hiyo ya Serikali haitamkiki.
Pengine huu ni wakati mwafaka wa kuikumbusha Serikali kwamba, gazeti hili pamoja na mengine yanayochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), ni magazeti makini sana yenye waandishi wa habari wanaoheshimu maadili ya taaluma yao. Hatusemi kwamba hatuwezi kufanya makosa, kwani sisi ni binadamu.
Hata hivyo, inapotokea tukafanya makosa tunafanya masahihisho stahiki haraka kwa lengo la kupunguza maumivu kwa yeyote tuliyemkosea. Makosa ya makusudi kama kuandika habari za uongo hayavumiliki na kila mwandishi wa kampuni yetu anatambua fika kwamba kufanya hivyo ni kujitakia kiama.
MCL imeweka miongozo ya sera na malengo ya uhariri kwa waandishi. Lengo ni kuhakikisha habari zinazochapishwa ni sahihi, zinatenda haki na haziegemei upande wowote. Kwa maana hiyo, vyombo vyake vya habari vinasimamia ukweli na haki na waandishi wake wana jukumu la kuhakikisha wanakuwa na kiwango cha juu cha weledi na maadili ili kuwawezesha kutoa habari kwa umma.
Tumetoka kifungoni tukiwa na somo muhimu. Kwamba sheria kandamizi kama Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 haisimamii masilahi ya taifa, bali kundi la watu wachache. Ni sheria kandamizi ambayo kwa umoja wetu tunaweza kuifuta. Tungependa kuwashukuru wasomaji wetu na wananchi kwa jumla kwa kuwa nasi katika kipindi kigumu tulichokuwa kifungoni. Vilevile, tunavishukuru kwa namna ya pekee vyombo vyote vya habari vya ndani na nje ambavyo vilisimama imara kupinga hatua ya Serikali kufungia magazeti.
Tutakuwa watu wasio na shukurani kama hatutatambua mshikamano mkubwa ulioonyeshwa na asasi za kiraia, mabalozi na watu mbalimbali kupinga matumizi ya sheria hii kandamizi. Hatujakata tamaa, bali tumetoka kifungoni tukiwa na hamasa kubwa kuendelea kuwapa habari wananchi pasipo woga wala upendeleo.
Hatupambani na Serikali, lakini tutaendelea kuikosoa pale inapofanya makosa na tutaipongeza pale inapotimiza wajibu wake. Tunawaomba wasomaji wetu mwendelee kutuunga mkono.

Friday, 4 October 2013

HOTUBA YA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WANANCHI, TAREHE 4 OKTOBA-2013.

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 4 OKTOBA, 2013
Ndugu Wananchi;
Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza mwezi Septemba salama na kuwasiliana kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri. Naomba radhi kuzungumza nanyi siku ya leo kwa sababu nilikuwa safari na nilirejea jioni ya tarehe 30 Septemba, 2013. Awali nilifikiria nisiseme, nisubiri mwisho wa mwezi wa Oktoba. Lakini, baada ya kupata taarifa ya yaliyojiri, nimeshauriwa na nimekubali angalau niyasemee baadhi ya mambo huenda itasaidia. Niwieni radhi nisipoyasemea baadhi ya mambo siyo kwa kuyapuuza, bali kwa kuepuka hotuba kuwa ndefu mno. Nitayatafutia mahali pengine pa kuyasemea.
Uhusiano na Rwanda
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Julai, nilizungumzia hali ya uhusiano wetu na Rwanda kutokuwa mzuri na tatizo la ujambazi na wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera. Nafurahi kusema kuwa kwa yote mawili kuna maendeleo ya kutia moyo.(P.T)

Tarehe 5 Septemba, 2013, nilikutana na kuzungumza na Mheshimiwa Rais Paul Kagame wa Rwanda mjini Kampala. Tuliitumia fursa ya ushiriki wetu katika Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu kuzungumzia uhusiano baina yetu na nchi zetu. 
Mazungumzo yalikuwa mazuri na sote tulikubaliana kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Kwa sababu hiyo tulielewana kuwa tutengeneze mazingira yatakayosaidia kutuliza hali na kurudisha nchi zetu katika uhusiano mwema kama ilivyokuwa siku zote. Nawaomba ndugu zangu hususan wanasiasa, watumishi wa umma, wanahabari na wenye mitandao ya kijamii na blog na wananchi kwa ujumla tusaidie kuimarisha uhusiano mwema baina ya Rwanda na Tanzania na watu wake.
Majambazi na Wahamiaji Haramu
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba hiyo pia nilisema kuwa tutachukua hatua thabiti dhidi ya majambazi na wageni wanaoishi nchini bila ya kuzingatia taratibu zinazohusika. Niliwataka majambazi wajisalimishe wao na silaha zao kwa hiari. Wale wanaoishi nchini bila ya kuwa na kibali halali wahalalishe ukaazi wao au warejee makwao. Nilitoa siku 14 kuanzia tarehe 29 Agosti, 2013 wafanye hivyo kwani baada ya hapo tungeanzisha operesheni maalum ya kushughulika na watu wa makundi yote mawili.
Ndugu Wananchi;
Kumekuwepo na mafanikio ya kutia moyo. Kwa upande wa wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha sheria watu wapatao 21,254 waliondoka kwa hiari. Hali kadhalika zaidi ya ng'ombe 8,000 waliondolewa na silaha 102 zilisalimishwa. Baada ya operesheni kuanza tarehe 6 Septemba, 2013 na kumalizika tarehe 20 Septemba, 2013, wahamiaji haramu 12,828 walirejeshwa makwao na watuhumiwa 279 wa unyang'anyi wa kutumia silaha walikamatwa. Aidha, mabomu 10 ya kutupa kwa mkono (offensive hand grenades), silaha 80, risasi 780 na mitambo 2 ya kutengeneza magobole vilikamatwa. Pia, ng'ombe 8,226 walikamatwa wakichungwa katika mapori ya hifadhi. Kwa upande wa mazao ya misitu, mbao 2,105 zilikamatwa pamoja na nyara mbalimbali za Serikali.
Ndugu Wananchi;
Agizo la kuwataka watu wanaoishi nchini isivyo halali wahalalishe ukaazi wao au waondoke kwa hiari au wataondolewa lilipotoshwa hasa na vyombo vya habari vya nje ya Tanzania. Walikuwa wanadai eti Tanzania ilikuwa inafukuza wakimbizi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo. Hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2013 wakimbizi 68,711 walikuwepo kwenye Kambi ya Nyarugusu, Mkoani Kigoma. Hakuna mkimbizi ye yote aliyetakiwa kuondoka. Ukweli ni kwamba hakuna mtu ye yote kati ya wale watu walioondoka kwa hiari au kusaidiwa kuondoka wakati wa operesheni ambaye ni mkimbizi. Kama ingekuwa hivyo, wa kwanza kulalamika wangekuwa wenzetu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Bahati nzuri jambo hilo halikutokea.
Ndugu Wananchi;
Yalikuwepo pia madai kwamba tunawaonea na kuwatesa watu walioishi nchini miaka mingi. Ati iweje sasa ndiyo waambiwe kuwa siyo raia. Siku zote Serikali ilikuwa wapi? Uraia haupatikani kwa kuishi nchi ya kigeni kwa miaka mingi. Unapatikana kwa kutimiza masharti ya kuomba na kupewa uraia. Kama mtu hakufanya hivyo anabaki kuwa raia wa nchi aliyotoka au walikotoka wazazi wake. Ipo mifano ya watu mashuhuri ambao walilazimika kuachia nyadhifa zao baada ya kugundulika kuwa siyo raia. Hawakuwa wanaonewa, ndiyo matakwa ya Katiba na Sheria za nchi yetu.
Ndugu Wananchi;
Katika kutekeleza operesheni hii niliagiza kuwa wale watu ambao wameishi hapa nchini miaka mingi ambao wana nyumba, mashamba au mali mbalimbali au wameoa au kuolewa na wana watoto au hata wajukuu waelekezwe kuhalalisha ukaazi wao. Iwapo watakataa kufanya hivyo basi wasaidiwe kurejea kwao. Pia niliagiza watu wasiporwe mali zao wala kudhulumiwa. Sijapata taarifa ya kufanyika kinyume na maelekezo yangu. Lakini kama wapo watu waliotendewa tofauti, taarifa itolewe kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa au hata Ofisi ya Rais ili hatua zipasazo zichukuliwe. Hatutaki watu wadhulumiwe au kuonewa.
Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi kwa uongozi wao mzuri katika zoezi hili. Pia, nawapongeza Makamanda na askari wa JWTZ na Polisi pamoja na maafisa wa Idara ya Uhamiaji, Idara ya Mifugo, Idara ya Wanyamapori, Idara ya Misitu na Idara nyinginezo za Serikali kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Najua awamu ya kwanza imeisha tarehe 20 Septemba, 2013 na kama nilivyosema kuwa safari hii operesheni itakuwa endelevu, muda si mrefu awamu ya pili itafuata. Nawaomba waendelee kuchapa kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu ya hali ya juu.
Ziara ya Canada na Marekani
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 17 na 28 Septemba, 2013 nilifanya ziara ya kikazi katika nchi za Canada na Marekani. Nchini Canada nilitembelea Chuo Kikuu cha Guelph ambapo nilitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu kwa kutambua jitihada zetu tuzifanyazo kujiletea maendeleo na mafanikio ya kutia moyo tunayoendelea kupata licha ya changamoto zinazotukabili. Katika mazungumzo yangu na uongozi wa chuo hicho wamekubali kuwa na ushirikiano wa karibu na Wizara zinazohusika na Elimu, Kilimo na Mifugo pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma. Nimewataka Mawaziri wa Wizara hizo na viongozi wa vyuo hivyo kuchangamkia fursa hiyo bila kuchelewa.
Ndugu Wananchi;
Nchini Marekani nilikutana na kuzungumza na maafisa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya nchi hiyo wakiwemo Rais Barack Obama na baadhi ya Wabunge wa Bunge la Marekani. Mazungumzo yetu yalilenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zetu na mambo yalienda vizuri. Wote walituhakikishia kuwa mambo tuliyoyazungumza na kukubaliana na Rais Barack Obama wakati wa ziara yake nchini yanaendelea kufanyiwa kazi. Miongoni mwa hayo maombi yetu ya kupatiwa vitabu milioni 2.4 vya sayansi na hisabati yamekubaliwa na utekelezaji umeanza. Upatikanaji wa vitabu hivyo utamwezesha kila mwanafunzi wa sekondari kuwa na kitabu chake.
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine kubwa na la faraja kwetu ni kuwa mapendekezo yetu ya miradi ya umeme na barabara za vijijini za kugharamiwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika lao la Changamoto za Milenia yamepokelewa vizuri. Kinachosubiriwa ni miradi ipi itakubaliwa na Bodi ya MCC na kiasi gani cha fedha kitatengwa na Bunge la Marekani kwa ajili hiyo.
Tuzo ya Uhifadhi
Jambo lingine muhimu katika safari yangu ya Marekani ni kutunukiwa tuzo na "International Congressional Conservation Foundation" kwa kutambua juhudi zetu katika kuhifadhi wanyama pori na mafanikio tuliyoyapata. Licha ya changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo, tuzo hii imetupa moyo wa kuongeza nguvu katika jitihada tunazozifanya sasa kupambana na ujangili na matatizo mengine ya uhifadhi wa wanyama na misitu.
Ndugu Wananchi;
Kilichotupa moyo zaidi ni kauli za utayari wa kutusaidia katika mapambano hayo zilizotolewa wakati wa kupewa tuzo na katika mkutano wa mfuko wa Maendeleo wa Clinton na katika mkutano maalum wa kupambana na ujangili na biashara ya meno ya tembo duniani.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Ndugu Wananchi;
Shabaha kuu ya safari yangu ya Marekani ilikuwa kuhudhuria Mkutano wa 68 wa Umoja wa Mataifa unaoendelea jijini New York mpaka Desemba, 2013. Mada kuu ya mkutano wa mwaka huu ni kuandaa agenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 yaani: Post 2015 Development Agenda: Setting the Stage. Kama mtakavyokumbuka Malengo ya Milenia yaliyoamuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2000, yanafikia ukomo wa utekelezaji wake mwaka 2015.
Katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu mjadala umehusu nini kifanyike baada ya mwaka 2015. Hata hivyo, mjadala huo unaanza kwa kufanya tathmini ya utekelezaji wa yale Malengo Manane ya Milenia ya mwaka 2000 umefikia wapi mpaka sasa na utafikia wapi mwaka 2015 kwa kila nchi na kwa dunia kwa ujumla. Tathmini ya jumla inaonesha kuwa kumekuwepo na jitihada kubwa ya kutekeleza malengo haya katika kila nchi. Yapo malengo ambayo utekelezaji wake umefikia shabaha hivi sasa na yapo ambayo upo uwezekano wa shabaha kufikiwa ifikapo mwaka 2015. Vile vile yapo ambayo shabaha haitafikiwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu, Tanzania, tumefikia shabaha katika mambo yafuatayo:
(1) Lengo la Milenia namba 2 kuhusu uandikishaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule ya msingi;
(2) Lengo la Milenia namba 3 hasa kuhusu usawa wa kijinsia katika Shule za Msingi na Sekondari. Ukweli ni kwamba, wasichana wanaanza kuwa wengi kuliko wavulana. Hatujafikia shabaha kwa upande wa usawa wa kijinsia katika elimu ya juu na ni vigumu kulifikia ifikapo 2015. Pia hatujafikia lengo kwa upande wa usawa wa Wabunge wanawake na wanaume. Hata hivyo, kwa kutumia mchakato wa Katiba unaoendelea sasa tunaweza kufikia lengo katika uchaguzi wa 2015 iwapo tutaamua iwe hivyo;
(3) Lengo la Milenia namba 4 kuhusu kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga na wale wenye umri chini ya miaka mitano;
(4) Tumefikia shabaha kwa Lengo la Milenia Namba 6 kuhusu kupunguza maambukizi ya UKIMWI; na
(5) Kwa upande wa lengo namba 7 kuhusu mazingira, tumefikia shabaha kwa upande wa upatikanaji wa maji mijini. Bado tuko nyuma kwa maji vijijini ingawaje tunaweza kufikia lengo ifikapo mwaka 2015 kama tutaendeleza uwekezaji tulioamua kufanya katika bajeti ya mwaka huu. Lakini, hatutaweza kufikia shabaha kwa upande wa usafi wa mazingira mijini na vijijini ifikapo mwaka 2015. Safari bado ndefu sana.
Ndugu Wananchi;
Malengo ya Milenia namba 1 na namba 5 ambayo bado tuko nyuma sana ya shabaha hatutafikia lengo ifikapo 2015. Tumeendelea kutekeleza lengo la Milenia namba 1 kuhusu kupunguza umaskini na njaa kwa zaidi ya nusu kutoka kiwango cha mwaka 2000. Hatua tunazochukua kuleta mageuzi katika kilimo zina lengo la kuhakikisha usalama wa chakula na kuongeza mapato ya wakulima. Mafanikio yanaanza kuonekana lakini si ya kiwango cha kutufikisha kwenye lengo ifikapo mwaka 2015. Tunao, pia, mpango wa kupanua programu ya TASAF ya Conditional Cash Transfer ili tuwafikie watu wengi maskini. Hata kama tutafanikiwa kuutekeleza mapema mpango huu utatusogeza sana mbele lakini bado tutakuwa chini ya lengo kwa upande wa kupunguza umaskini ifikapo 2015.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Lengo la Milenia namba 5, kuhusu afya ya kina mama wajawazito bado tuko nyuma katika kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na kuongeza idadi ya wajawazito wanaojifungua chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya. Hatutaweza kufikia shabaha ifikapo mwaka 2015. Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (2007 – 2017) una nia ya kukabiliana na matatizo haya. Tumeongeza ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, tumeboresha upatikanaji wa dawa na tumepanua sana mafunzo ya madaktari, wauguzi na wakunga mambo ambayo yamesaidia kutufikisha hatua tuliyopiga mpaka sasa. Naamini juhudi zetu tukiziendeleza zitatusogeza mbele zaidi ingawaje bado tutakuwa chini ya lengo. Miaka michache ijayo, tatizo hili nalo litakuwa historia.
Ndugu Wananchi;
Lengo la Milenia namba 8 linazihusu nchi tajiri kuongeza michango yao kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza Malengo ya Milenia. Bahati mbaya sana mataifa tajiri hayajafikia viwango wanavyotarajiwa kutoa na hata vile wanavyoahidi wenyewe kutoa katika majukwaa mbalimbali. Kama wangetimiza ahadi zao, sura ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia ingekuwa tofauti kabisa.
Ndugu Wananchi;
Hiyo ndiyo hali ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia hapa nchini. Hakuna nchi ye yote duniani iliyofanikiwa kutekeleza shabaha za malengo yote kwa ukamilifu. Ushauri wa viongozi wote waliozungumza ulitaka mataifa yaliyoendelea yatimize ahadi zao za kuchangia utekelezaji wa Malengo ya Milenia. Ilionekana suala la upatikanaji wa fedha halina budi kuangaliwa kwa makini sasa na baada ya mwaka 2015. Bila ya hivyo ufanisi utakuwa mdogo katika kuongeza kasi ya utekelezaji kwa pale paliposalia kufikia malengo ya 2015 na hata kwa Malengo ya baada ya mwaka 2015.
Mashambulizi ya Kigaidi ya Westgate, Nairobi
Ndugu Wananchi;
Wakati nikiwa safarini, tarehe 21 Septemba, 2013 kulitokea shambulilizi la kigaidi katika Jengo la Biashara la Westgate, huko Nairobi, Kenya. Watu 67 walipoteza maisha na zaidi ya 200 walijeruhiwa. Nilituma salamu za pole na rambirambi kwa Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta na wananchi wa Kenya na kuwahakikishia kuwa tupo pamoja nao katika wakati huu wa majonzi.
Nafahamu kuwa baada ya tukio hilo watu wengi hapa nchini wameingiwa na hofu kuhusu usalama wetu. Ni hofu ya msingi kwani tarehe 8 Agosti, 1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na magaidi na ndugu zetu 11 wasio na hatia walipoteza maisha.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwafahamisha kuwa tangu shambulio la mwaka 1998, Serikali imekuwa inajenga uwezo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kupambana na ugaidi katika nyanja mbalimbali. Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku hadi siku. JWTZ, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili hiyo. Juhudi zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa.
Baada ya tukio la Kenya, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu. Pamoja na kujizatiti kwetu huko hatuwezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea nchini. Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa makubwa na tajiri yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari na wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe zaidi.
Hali kadhalika, tumewataka watu wote wenye shughuli zinazokusanya watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa n.k. waweke kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo yao. Pia waangalie uwezekano wa kuweka vifaa vya upekuzi (metal detectors and x-rays). Najua watu wanaweza kulalamikia usumbufu au gharama, lakini gharama na hasara ya kushambuliwa ni kubwa zaidi kuliko ya usumbufu huo.
Ndugu Wananchi;
Nawaomba muendelee kufanya shughuli zenu bila ya hofu ingawaje msiache kuwa makini na kuchukua tahadhari. Watu watoe taarifa kwa vyombo vya usalama wanapoona mtu au watu au kitu cha kutilia shaka. Ni muhimu kwa usalama wake, wa kila mtu, jamii na taifa. Maafisa husika wa vyombo vya ulinzi na usalama wataendelea kuelimisha umma kuhusu hatua mbalimbali za tahadhari za kuchukua. Sisi Serikalini tumejipanga kuchukua hatua zaidi kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu na watu wake.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
Kama mtakavyokumbuka, Bunge lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Novemba, 2011. Sheria hii imeweka mchakato mzima wa kupata Katiba hiyo na kuunda taasisi zake. Mwezi Mei, 2012, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa na imekamilisha hatua tatu muhimu katika mchakato huo. Hatua hizo ni kupokea maoni ya wananchi, kutayarisha rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya na kupokea maoni ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ya taasisi. Hivi sasa Tume inaandaa mapendekezo ya Rasimu ya Pili ya Katiba itakayopelekwa kwenye Bunge Maalum. Baada ya tafakuri zake, Bunge Maalum litatoa rasimu ya mwisho ya Katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni. Baada ya hatua hiyo, ndipo tutakapokuwa tumepata Katiba Mpya.
Ndugu Wananchi;
Baada ya Bunge la Novemba, 2011 kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kulikuwepo na madai ya kutaka sheria hiyo iboreshwe kutoka vyama vyote vya siasa vikiwemo vyama vya upinzani na Chama tawala. Majadiliano yalifanyika baina ya Serikali na vyama hivyo pamoja na shirikisho la asasi za kiraia. Makubaliano yalifikiwa kuwa marekebisho yafanyike kwa awamu. Awamu ya kwanza ihusishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba kisha hapo yafanyike marekebisho yanayohusu Bunge Maalum na mwisho Kura ya Maoni.
Kama ilivyokuwa kwa mabadiliko yaliyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba, safari hii nayo vyama vya siasa vilitoa mapendekezo yao. Yalifanyika mazungumzo kati yao na Serikali na maelewano kufikiwa kuhusu maeneo ya kufanyiwa marekebisho. Serikali ilitayarisha rasimu ya Muswada na kuuwasilisha kwa wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ndugu Wananchi;
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa mapendekezo yake na ushauri kwenye maeneo mawili. Kwanza kwamba uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar. Pili walishauri kwamba kama Bunge Maalum litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa, liweze kuongezwa muda hadi kufikia siku 90. Maeneo mengine ya Muswada waliafikiana nayo.
Ndugu Wananchi;
Kwa kuzingatia utaratibu wa kutunga Sheria, Serikali ilifikisha Muswada kwa Spika wa Bunge ambaye nae aliuwasilisha kwenye Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala. Kama ilivyo ada, Kamati hiyo ilifanya vikao na wadau na kupokea maoni yao kuhusu Muswada. Nimeambiwa kulikuwa na mjadala wa kina na mapendekezo mazuri yalitolewa na wadau. Kisha hapo Wajumbe wa Kamati walikaa wenyewe kujadili Muswada walikuwepo pia Wabunge ambao si Wajumbe wa Kamati walioshiriki kwa vile Kanuni zinaruhusu. Nimeambiwa pia kwamba mjadala ulikuwa mpana na wa kina zaidi. Mapendekezo kadhaa yalitolewa na Wajumbe kuhusu vifungu mbalimbali vya Muswada.
Ndugu Wananchi;
Nimefahamishwa kuwa Wabunge wa vyama vyote walichangia na kwamba baadhi ya nyakati mambo yalipokuwa ugumu mawazo mazuri ya baadhi ya Wabunge wa upinzani yalisaidia kupata ufumbuzi. Nimeambiwa pia kwamba Wajumbe wa Kamati na upande wa Serikali walikubaliana kwa maeneo mengi isipokuwa machache ambayo walikubaliana kwa pamoja wayapeleke Bungeni ili Wabunge nao wayajadili na kuyapatia ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Baada ya Kamati kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mathias Chikawe aliwasilisha Muswada Bungeni. Akafuatiwa na Mheshimiwa Gosbert Blandes kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kutoa maoni ya Kamati. Baadaye Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Tundu Lissu alitoa maoni yake.
Ndugu Zangu;
Baada ya watu hao watatu kutoa maoni yao ilitarajiwa kuwa Wabunge wangeanza kujadili Muswada. Naambiwa mambo hayakuwa hivyo. Badala yake kukazuka malumbano baina ya Spika na baadhi ya Wabunge wa Upinzani wakitaka Muswada usijadiliwe. Ilifikia wakati hoja hiyo ikabidi iamuliwe kwa kura ambapo ilishindwa. Katika hali isiyotarajiwa, Wabunge wote wa upinzani wakatoka nje ya Bunge isipokuwa wawili. Kitendo hicho kimewanyima Wabunge wengi wa upinzani fursa ya kutetea hoja zao walizozitoa kupitia hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani. Pia wamejinyima nafasi ya kusema mambo mengine wakati wa mjadala na Kamati ya Bunge zima.
Wabunge waliokuwepo waliendelea kuujadili Muswada na kutoa hoja na mapendekezo ya kuuboresha. Walifanya hivyo wakati wa mjadala na wakati wa kupitia kifungu kwa kifungu. Baadhi ya hoja na mapendekezo yalikubaliwa na mengine yalikataliwa. Miongoni mwa yaliyokubaliwa na Wabunge, kwa mfano, ni kuhusu elimu ya mtu atakayekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum na lile la ukomo wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Kwa maoni yangu madai ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata baadhi yangeweza kukubalika kama Wabunge wake wangekuwepo Bungeni na kushiriki mchakato wote wa kujadili na kupitisha Miswada Bungeni. Bahati mbaya hawakuwepo, hivyo hapakuwepo na mtu wa kusema mawazo yao. Baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana. Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na kuamuliwa Bungeni na si vinginevyo. Kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria kama Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hii. Naamini na wao wanautambua ukweli huo.
Ndugu Wananchi;
Kuna msemo wa wahenga kuwa "historia hujirudia". Naomba hekima ziwaongoze viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia utaratibu tulioutumia mwaka 2012. Kulipotokea mazingira kama haya pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi. Baada ya kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo.
Ndugu Wananchi;
Kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu. Tutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tukikataa kufanya hayo Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu. Watakuwa na haki ya kuuliza nia ni hii yetu sote ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria au tuna dhamira nyingine iliyojifisha?
Kama dhamira yetu ni kutaka kupata Katiba mpya kwa mujibu wa Katiba na Sheria, ushauri wangu na rai kwa ndugu zetu wa CHADEMA, CUF na NCCR-Maguezi ni kuwa waachane na mipango ya maandamano na kufanya ghasia. Badala yake watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na kisheria kujenga hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa kuboresha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga badala ya kubomoa. Tutaliponya taifa. Sisi katika Serikali tuko tayari.
Ndugu Wananchi;
Napenda pia kuzisemea baadhi ya hoja zilizotolewa na Kambi ya Upinzani. Kwanza kabisa nasema kuwa nimesikitishwa sana na madai na tuhuma za uongo eti katika uteuzi wa Tume ya Katiba sikuheshimu mapendekezo ya TEC, CCT na walemavu.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Siyo tu kauli hiyo ya Mheshimiwa Tundu Lissu ni uzushi na uongo mtupu bali pia ni ya unafiki, fitina na uzandiki wa hali ya juu. Nasema hivyo kwa sababu, sipendi kuamini kuwa Mheshimiwa Mbunge amesema yale kwa kutokufahamu ukweli au kwa bahati mbaya. Amesema yale kwa makusudi mazima ya kupotosha ukweli ili pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wale Wajumbe 166 wa Bunge Maalum.
Napenda ieleweke kuwa siishabikii kazi hiyo, lakini kwa kutimiza wajibu na maslahi ya taifa nikiagizwa na Sheria za nchi nitafanya. Nasema hivyo kwa sababu nafahamu ni kazi ngumu. Kama kazi ya uteuzi wa Wajumbe 30 wa Tume haikuwa rahisi hata kidogo, hii ya uteuzi wa watu 166 itakuwa ngumu zaidi. Ile ya Tume ilikuwa ngumu kwa namna mbili. Kwanza, kwamba taasisi zilizoomba na waombaji walikuwa wengi mno kuliko nafasi za kujaza yaani 15 Zanzibar na 15 Bara. Zanzibar ziliomba taasisi zaidi ya 60 na waombaji walikuwa zaidi ya 200 wakati Bara kulikuwa na taasisi zaidi ya 170 zikiwa na waombaji zaidi ya 500. Kupata watu 30 kutoka orodha kubwa kiasi hicho si mtihani mdogo. Pili kwamba tulitakiwa kuunda Tume inayoasili sura ya taifa, yaani watu wa nchi yetu kwa maeneo, vyama vya siasa, dini, wanawake, vijana, walemavu, wafanyakazi, wasomi, Wabunge, Wawakilishi, wanasheria, wafanyabiashara, wakulima, asasi za kiraia n.k.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na changamoto hizo, lakini tulifanikiwa kuunda Tume iliyopokelewa vizuri na jamii na kufanya watu wengi hata wale ambao hawakuteuliwa wahisi kuwakilishwa. Tulifanyaje? Kwanza kabisa tulihakikisha kuwa tunapata wawakilishi wa vyama vya siasa vyenye wawakilishi Bungeni na kwenye Baraza la Wawakilishi na tunapata wawakilishi wa mashirika ya dini zetu kubwa yaani, TEC, CCT na BAKWATA. Ndiyo maana nikasema kuwa kwa Mheshimiwa Tundu Lisu kudai kuwa mapendekezo ya TEC na CCT hayakuheshimiwa ni uongo wa mchana usiokuwa na kichwa wala miguu.
Baada ya hapo ndipo tukaangalia waombaji wa makundi na taasisi nyingine. Tulijitahidi sana kupata watu ambao wanawakilisha kundi zaidi ya moja. Tulifikiria hivyo kwa sababu ni ukweli ulio wazi kuwa si kila taasisi iliyoomba itapata mwakilishi kwani hata tungependa iwe hivyo nafasi hazikuwepo. Kwa kutumia utaratibu huu makundi mengi yamepata uwakilishi kutokana na watu waliopendekezwa na makundi mengi. Tumefanya kazi kubwa sana ya kuwianisha mambo na makundi ya maslahi mbalimbali nchini.
Ndiyo maana naiona mantiki ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishirikiana na Rais wa Zanzibar wa kuwateua Wajumbe wa Bunge Maalum. Dhana kuwa kila kikundi kiteue chenyewe watu ingefaa sana kama kungekuwepo na nafasi za kutosha kila kundi nchini. Hilo haliwezekani, labda tuwe na Bunge Maalum lisilokuwa na ukomo wa wajumbe.
Ndugu Wananchi;
Mimi na Rais wa Zanzibar tumekuwa tunajiuliza baada ya kazi ngumu na nzuri tuliyoifanya na iliyopongezwa na wengi ya kuteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba nini kilichoharibika sasa hata tuonekane hatuaminiki kuteua hawa 166? Kama ni kwa sababu za Mheshimiwa Tundu Lissu, nimeshasema hazina ukweli wowote. Ninapojiuliza kwa nini aseme uongo nashindwa kupata jibu linaloingia akilini. Wakati mwingine nafikiria kuwa ni hiana. Lakini nadhani ni hila za kisiasa zenye nia ya kutaka kupata watu wa kutetea maslahi ya chama chake. Kama hiyo ndiyo shabaha basi amekosea sana.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Hatutengenezi Katiba ya Chama fulani bali Katiba ya nchi, Katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama ambao ndiyo wengi kuliko wote. Lazima tuongozwe na ukweli huo na tuwe na msimamo huo wakati wote. Lazima tukumbuke kuwa si watu wote wanaostahili au kuwa na sifa ambao wataomba na kupata nafasi ya kuwa Wajumbe, hivyo wale wachache watakao bahatika lazima wawasemee wote. Wanatakiwa kusikiliza na kuwakilisha mawazo ya wote hata wale wasiokuwa wa Chama chao au kundi lao.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri hii ndiyo sifa kubwa iliyooneshwa na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Wamewasimamia na kuwasemea watu wote bila ya kubagua. Natambua kuwepo kwa baadhi ya watu ambao hawafurahii msimamo huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao kuwalaumu Wajumbe wa Tume kwa ajili hiyo ni kuwaonea na kutowatendea haki. Tunataka watakaokuwa Wajumbe wa Bunge Maalum nao waige mfano huu mzuri. Wajali maslahi mapana ya taifa letu na watu wake badala ya kujali yale ya taasisi zao au makundi yao.
Zanzibar Kutokushirikishwa
Ndugu Wanachi;
Nimeambiwa pia kuliwepo madai ya Zanzibar kutokushirikishwa ipasavyo. Nimeeleza kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika Muswada. Hivyo basi napata tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa msingi wake nini! Labda kuna kitu sikuambiwa!
Nimeulizia kuhusu hoja ya Kamati kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar. Nimeambiwa kuwa Kanuni za Bunge hazina sharti hilo hivyo Kamati haistahili kulaumiwa. Kama hivyo, nashauri kuwa suala hili lirudishwe Bungeni ili Wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka. Vinginevyo watu wataendelea kulauminiana isivyostahili. Hivyo basi, kuligeuza jambo hili kuwa ni suala la kukataa Muswada au kususia vikao vya Bunge au kufanya maandamano sidhani kama ni sawa.
Ndugu Wananchi;
Nimeambiwa pia kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya Wajumbe wa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sababu ya idadi ya Wajumbe wa Tume kuwa sawa inatokana na utaratibu wao wa kufikia uamuzi. Ni kwa maelewano ya wote (consensus) na siyo kwa kupiga kura. Ndiyo maana idadi imewekwa sawa ili sauti za pande zote zisikike sawia. Bunge Maalum lina sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi mbili ya kura za kila upande kukubali. Bila ya hivyo hakuna uamuzi.
Hivyo basi, katika Bunge Maalum nguvu si uwingi wa kura ambazo upande fulani unaweza kupata bali ni ulinganifu sawa wa kura za kila upande peke yake. Huu ndiyo msingi unaotumika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa kwa lengo la kulinda maslahi ya Zanzibar. Zanzibar ina Majimbo 50 ya uchaguzi na Tanzania Bara ina Majimbo 189, hivyo ukiamua kwa wingi kila wakati Wazanzibari watashindwa. Lakini, hapajakuwepo madai ya Zanzibar nao kutaka kuwa na idadi sawa ya majimbo kama Bara au kupunguza majimbo ya Bara yawe sawa na ya Zanzibar kwa sababu wingi si hoja. Msingi unaotumika ni kutoa nguvu sawa za uamuzi kwa kila upande wa Muungano wakati wa kuamua masuala ya Katiba. Hakuna mdogo wala mkubwa, wote wako sawa. Hakuna mdogo kumezwa na mkubwa. Ndiyo msingi unaopendekezwa kutumika kwenye Bunge Maalum hivyo hakuna kitakachoharibika kwa idadi ya Wajumbe kutokukulingana. Nadhani inafaa ibaki ilivyo. Lakini kama Wabunge wataamua waongeze idadi itakuwa kwa sababu nyingine siyo hii ya mfano wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Katika orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani lipo suala la uhai wa Tume ya Katiba. Wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalum bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato. Nimeulizia ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya Serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Limetokana na pendekezo la Mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na Wabunge wengi. Kwa hiyo kuilaumu Serikali si haki. Serikali inaweza kuwa mshirika katika hoja hii.
Nami naiona hoja ya Wajumbe wa Tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume. Je ushiriki huo uwe vipi? Je ni Wajumbe wote au baadhi yao ni jambo linaloweza kujadiliwa.
Ndugu Wananchi;
Naomba nimalizie kwa kuwasihi viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kuongozwa na hekima iliyotumika wakati tulipokuwa na tatizo linalofana na hili kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mimi naamini kama iliwezekana kufanikisha mambo wakati ule inaweza kufanya hivyo hata safari hii. Itatufikisha pale tunapopataka salama salimini bila maandamano, kushupaliana au uvunjifu wa amani. Kupanga ni kuchagua, naomba sote, mmoja mmoja na kwa umoja wetu tuchague njia ya mazungumzo na maelewano kwani itaihakikishia nchi yetu amani, usalama na utulivu. Tukifanya hivyo historia itatuhukumu kwa wema.
Mungu Ibariki Tanzania. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.

Friday, 20 September 2013

Bagamoyo na maeneo ya kihistoria yasiyojulikana

Siku chache zilizopita nilitembelea Kitongoji cha Magomeni, mjini Bagamoyo, katika kitongoji hicho nilipiga picha vipande vya nguzo ambayo ni mabaki ya lango la mji huo.
Dereva wa bodaboda aliyenipeleka hapo nilimuuliza kama anaelewa chochote kuhusu kuta hizo mbili, lakini cha ajabu alisema hajui licha ya kuishi  Bagamoyo miaka mingi.
Baada ya hapo nilikutana na dada ambaye anasema amezaliwa na kuishi eneo la Magomeni, lakini hajui maana ya kuta hizo. Nilimwambia kijana kwamba enzi hizo, Bagamoyo ilipokuwa chini ya Wakoloni wa Kiarabu, eneo hilo palikuwa na lango likionyesha mtu anaingia mjini na kwa wenye nchi.
Misafara ya watumwa, wamisionari na wavumbuzi, wafanyabiashara, walipita katika lango hilo. Kuta  nyingine zilizokuwa upande mwingine wa barabara, zimepotea. Kuta nilizopiga picha ziko kwenye uwanja wa mtu. Zinaweza kupotea kwa kuharibiwa wakati wowote.
Pia kulikuwa na nguzo nyingine pale ‘top life bar’ lakini sasa imebaki moja, nyingine imepotea. Nilielezwa na wahifadhi kwamba eneo linalozunguka Caravan Serai, katika soko, na kule kituo cha mabasi kipya lilitumika kujenga kambi za watumwa. Lakini hakuna anayefahamu hilo.
Katika Idara ya Mambo ya Kale, inayoshughulikia masuala ya historia, hakuna maelezo yanayoonyesha eneo hilo kulikuwa na lango hilo. Hakuna kumbukumbu yoyote.
Nimekwenda Bagamoyo mara kadhaa, kila unapotembelea moja ya kivutio cha historia utapata habari tofauti, aidha itatofautiana na ya zamani, au itapotoshwa kidogo. Inafika mahali unashindwa kuelewa ukweli ni upi.
Baada ya kusoma kitabu cha Henry Morton Stanley anaeleza walipoanza safari walipumzika kwenye shamba la mama mmoja, Gonera wa Kihindi, nje ya Bagamoyo. Lakini safari hii niliambiwa Gonera alikuwa ni askari mlinzi aliyejengewa nguzo pale eneo la Mji Mkongwe na von Wisman mwaka 1898.
 Inaonekana Bagamoyo ina maeneo mengi ya kihistoria ambayo hayajawekwa katika historia kuu. Na hili ni kosa la idara husika.

Hakimu achomwa kisu mahakamani

Shinyanga. Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo iliyopo eneo la Nguzo Nane, Kata ya Kambarage Mjini Shinyanga, Satto Nyangoha amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu katika shavu lake la kushoto baada ya kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa baiskeli.
Kitendo hicho kinadaiwa kufanywa na mlalamikaji katika kesi hiyo, Emmanuel Izengo (28), mkazi wa Tambukareli, Shinyanga baada ya kutokuridhishwa na hukumu iliyotolewa bila ya mshtakiwa, Daniel Makelezia, mkazi wa Lubaga Shinyanga na mdhamini wake, Marko Nkelezia kuwepo mahakamani.
Katika hukumu yake, Hakimu Nyangoha alisema mshtakiwa atakapopatikana atatumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa baiskeli hiyo aina ya Neria yenye thamani ya Sh150,000.
Awali, ilielezwa kwamba baada ya tukio hilo la wizi lililotokea Agosti Mosi, mwaka huu katika eneo la Nguzo Nane, mshtakiwa alikamatwa na kuwekwa mahabusu na kufunguliwa kesi namba 460 ya 2013 kabla ya kuachiwa kwa dhamana Agosti 23, mwaka huu huku kesi yake ikiendelea na pande zote mbili zilitoa maelezo.
Hata hivyo, baada ya kutoa maelezo, si mshtakiwa wala mdhamini wake aliyehudhuria mahakamani hapo licha ya kesi hiyo kusikilizwa mara mbili bila ya taarifa yoyote kabla ya hakimu huyo kutoa hukumu hiyo jana.
Kushambuliwa
Baada ya hukumu hiyo mlalamikaji alitoa shukrani na kuwashika mikono wote waliokuwamo mahakamani humo na kutoka nje.
Ilidaiwa kuwa baada ya dakika 15, Izengo alirudi mahakamani hapo na kudai kuwa ameleta risiti ya kumwonyesha hakimu thamani ya baiskeli yake alipoingia ndani ndipo kelele za Mshauri wa Baraza, Mary Wamba zikaanza kusikika akisema: ‘Njooni jamani hakimu kavamiwa anapigwa’.
Baada ya watu waliokuwa karibu kuingia katika ofisi ya Mahakama hiyo walikuta hakimu ameshacwhomwa kisu katika shavu la upande wa kushoto huku akivuja damu nyingi huku mtuhumiwa huyo akiendelea kumshambulia. Baada ya tukio hilo, wasamaria wema walimpeleka hakimu huyo katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambako alilazwa kwa matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema mtuhumiwa alikamatwa mara baada ya tukio hilo kusubiri hatua za kisheria dhidi yake.

Monday, 16 September 2013

Kisumo: Ndugai, Mbowe wote wana makosa

Moshi. Mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo amezungumzia vurugu zilizotokea bungeni akisema Naibu Spika, Job Ndugai na Kiongozi wa Upinzani, Freeman Mbowe, wote wana makosa.
Kisumo ambaye ni mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Wadhamini wa CCM, alisema ameanza kupata wasiwasi kuhusu mhimili wa Bunge hususan kiti cha Spika hasa katika suala la Mbowe.
Mwanasiasa huyo aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili jana ku tokana na vurugu zilizotokea Bungeni wiki iliyopita baada ya Naibu Spika kuamuru kutolewa nje kwa nguvu kwa Mbowe.
Kisumo alisema alichopaswa kufanya Ndugai baada ya Mbowe kukaidi amri ya kutoka nje ni kumwita mpambe wa Bunge (Sergeant at Arm) na kama ataendelea kukaidi alitakiwa kuahirisha Bunge.
“Mbowe alitolewa na Polisi nadhani Naibu Spika alikosea…Mpambe ndiye alipaswa amtoe na akishindwa alipaswa aahirishe Bunge halafu amshtaki kwenye kamati husika,” alisema Kisumo.
Kisumo alisema kitendo cha Ndugai kuamuru Polisi kuingia ndani ya Bunge ambao wamefunzwa kutumia nguvu, kilikuwa ni makosa makubwa na kusisitiza katika hilo Ndugai alikosea.
Hata hivyo alisema hata Mbowe, naye alikuwa na makosa pale alipokataa kutii maagizo ya kiti (Naibu Spika).
“Mbowe na chama chake kisichukulie ubabe wao katika mikutano ya hadhara ambayo haina lugha ya kibunge na kuzipeleka bungeni haya ni makosa makubwa,” alisema.
Kisumo alisema binafsi anapenda vyama vingi lakini hapendi aibu ya kupigana mahali patakatifu kama bungeni na kuutaka upinzani pamoja na uchache wao Bungeni, kushindana kwa hoja zenye nguvu.
“Vyama vya upinzani haviwezi kushinda hoja yoyote bungeni itakayoamuliwa kwa njia ya kura kwa sababu ya uchache wao… Wao waendelee kutoa hoja na mwisho wa siku umma utawaelewa,”alisema.
Kisumo alisisitiza kuwa Chadema wasichukulie mambo yao ya majukwaani yaliyojaa kile alichodai tamaa ya madaraka kuongoza nchi wakayapeleka bungeni ambako kuna kanuni na taratibu.

Kashfa mpya dawa za kulevya

Dar es Salaam/Nairobi. Raia wa Nigeria aliyefukuzwa Kenya miezi minne iliyopita kwa kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya, amekamatwa tena nchini humo akiwa na pakiti 425 za heroin, akiaminika kwamba alipitia Tanzania.
Mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Enobemhe Emmanuel Peter inaaminika alishukia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, akitokea Nigeria na kisha kwenda Kenya kwa barabara, kupitia mpaka wa Namanga mkoani Arusha.
Peter alikamatwa pamoja na mwanamke ambaye ni raia wa Kenya, usiku wa Ijumaa iliyopita jijini Nairobi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.
Raia huyo wa Nigeria ni kati ya wageni waliofukuzwa nchini humo Juni mwaka huu kwa agizo la Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliyeamuru raia wa kigeni wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya wafukuzwe nchini humo.
Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Kenya, Dk Hamisi Massa alisema uchunguzi zaidi wa dawa hizo utafanyika kabla mtuhumiwa huyo kufikishwa mahakamani.
“Ni kati ya watu waliokuwa wamefukuzwa nchini katika nyumba aliyokamatiwa kulikutwa pia na pakiti 425 za heroin,” alisema Dk Massa.
Mtu huyo amekamatwa kutokana na kuwapo kwa taarifa zilizoonyesha kuwa, watu wengi waliofukuzwa Kenya kutokana na kujihusisha na biashara hiyo sasa wamerejea tena.
Julai 9 mwaka huu, Ofisa Uhamiaji wa nchi hiyo, Edward Kabiu Njau alifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kumruhusu Anaeke Chimenze, aliyefukuzwa nchini humo, kurejea tena.
Chimenze ambaye ni raia wa Nigeria mwenye pasi ya kusafiria namba 02743350, pia anadaiwa kurudi nchini humo kupitia mpaka wa Namanga.
Uhamiaji Tanzania
Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna, Abbas Irovya alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yupo nje ya ofisi. “Mtafute Tatu ndiye mtu wa habari zaidi, kama atakuwa amepata hizo taarifa atakueleza,” alisema.
Mwananchi ilipomtafuta Tatu Iddi alisema hajapata taarifa hizo na kutaka mwandishi amtumie barua pepe ikiwa na maelezo ya mtu huyo aliyekamatwa ili aweze kutafuta taarifa zaidi.

Naye Kaimu Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Mbaraka Batenga alisema hayuko kwenye nafasi nzuri ya kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hakuwa ofisini kutokana na kuugua.
Hata hivyo, alisema kwa kawaida mtu akifukuzwa kwenye nchi moja isitafsiriwe kuwa haruhusiwi kwenda nchi nyingine.
“Naomba nikusaidie kitu kimoja kama kwa ajili ya kuelewa zaidi mambo haya, mtu akifukuzwa kwenye nchi moja haina maana kuwa hawezi kwenda kwenye nchi nyingine,  sisi tukimfukuza mtu itakuwa kosa kama atarudi tena Tanzania,”alisema na kuongeza:
“Kwa hiyo kama huyo mtu alifanya kosa huko Kenya na akafukuzwa Kenya ni kosa kurudi Kenya, hapo hata ofisa aliyemruhusu kurudi huko itabidi akamatwe,” alisema Batenga.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema mtu akifukuzwa nchi moja haimaanishi kuwa haruhusiwi kwenda nchi nyingine.
Alisema kama kikosi cha kupambana na dawa za kulevya cha Kenya kingekuwa kinashirikiana na kile cha Tanzania, ingekuwa rahisi kuwadhibiti watu hao.
“Wenzetu wangekuwa wanafanya kazi kwa ushirikiano na sisi ingesaidia sana, wakimkamata mtu wanatuambia. Huyo mtu alipita tu Tanzania,” aliongeza Nzowa.
Nzowa alitahadharisha kuwa kumfukuza sio kigezo cha kumzuia mtu kupita Tanzania kwani haijulikani alifukuzwa kwa kosa lipi huko Kenya. 

Mbowe, Lipumba, Mbatia wambana JK

Dar es Salaam. Mshikamano wa vyama vya upinzani katika kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 umehamia nje ya Bunge na sasa vyama hivyo vimetangaza kuanza kampeni ya kuuhamasisha umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.
Jana wenyeviti wa vyama hivyo; James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) walikutana na waandishi wa habari na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutosaini muswada huo kuwa sheria, hadi pale kutakapokuwa na maridhiano ya pande zote husika.
Walisema muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha umma wa Watanzania kufanya uamuzi wa kunusuru walichokiita “utekaji madaraka na mamlaka ya nchi kutoka kwa wananchi” hivyo wanaitaka Serikali kurekebisha kasoro zinazojitokeza katika mchakato huo.
Akitoa tamko la pamoja kwa niaba ya viongozi wenzake, Profesa Lipumba alisema wanachopigania ni kuurejesha mchakato wa Katiba Mpya mikononi mwa umma, kwa maelezo kwamba suala hilo kwa sasa limehodhiwa na CCM.
“Rais Kikwete asisaini muswada huu, aurejeshe bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuaminiana na mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Hatutakwenda kumwona ila aurejeshe bungeni,”alisema Lipumba na kuongeza:
“Mchakato huu unahitaji uvumilivu, staha na hekima na usitawaliwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa kutoka kwa watawala. Misingi hii ikipuuzwa mchakato mzima unaweza kutumbukiza taifa letu katika mpasuko, migogoro na hata machafuko.”
Mwenyekiti huyo wa CUF alisema nchi ni mali ya watu, hivyo mchakato huo haupaswi kuhodhiwa na chama kimoja, badala yake  unapaswa kuwa shirikishi na jumuishi ili kuwezesha kuandikwa kwa Katiba katika msingi wa maridhiano.
Kuna madai kwamba muswada ulipitishwa ukiwa na marekebisho ambayo yalifanyika kinyume na maoni ya wadau na kinyume hata na makubaliano ya awali ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu mamlaka ya Rais kuteua wajumbe Bunge Maalumu la Katiba.
Madai mengine ni kwamba wabunge wa CCM waliongeza baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho, hivyo kutoa mwanya kwa Serikali inayoongozwa na chama hicho kupitia kwa Rais kuwa na mamlaka zaidi ya uteuzi wa wajumbe husika.
Itakumbukwa kuwa Septemba 6 mwaka huu, wabunge wa CCM walitumia wingi wao kupitisha muswada huo katika mkutano wa Bunge ambao ulisababisha tafrani kiasi cha Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi kutolewa nje ya Bunge kwa amri ya Naibu Spika, Job Ndugai.
Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.
Mbowe na Mbatia
Kwa upande wake, Mbowe alisema: “Amani itavurugwa kama mchakato wa Katiba Mpya utahodhiwa na chama kimoja cha siasa, ikiwa hivyo sisi hatutakubali kuwa kondoo. Wanaohubiri amani watambue kuwa kuna misingi ya kuipata amani ni lazima haki iwepo.”
Alisema fursa ya kupata Katiba Mpya inapotezwa na watu wachache ndani ya CCM, na kwamba wapinzani watatumia kila aina ya mbinu kuwaelewesha Watanzania kinachoendelea, ili washiriki katika kuidai Katiba iliyotokana na mawazo yao.
Mbowe alisema wapinzani hawatarudi nyuma na hawatakubali nchi kurejeshwa chini ya uongozi wa Katiba ya sasa.
“Mwalimu Nyerere aliwahi kuandika katika kitabu chake kwamba, ‘kuna siku wananchi watachagua kifo kama viongozi hawatakuwa makini’. Amani itaharibiwa na wale wenye dola, sio vyama vya upinzani” alisema Mbowe.
Kwa upande wake,  Mbatia alisema: “CCM ndio nini… Wanatakiwa kujua kuwa Tanzania kwanza vyama baadaye, vyama vya siasa vilivyokuwa vikitawala nchini Kenya, Zambia vimekufa, lakini nchi hizo bado zipo.  CCM inaweza kufa, lakini Tanzania itaendelea kubaki.”
“CCM wakisema wapinzani tunafanya vurugu wanakosea, katika taifa hili Watanzania hawajawahi kuandika Katiba iliyotokana na mawazo yao. Katiba Mpya ni tendo la maridhiano na kisiasa sio kisheria, sisi tuna tofauti, lakini tumeziweka pembeni.”
Mbatia alimtaka Rais Kikwete kusimamia kikamilifu mchakato wa Katiba ili historia isije ikamhukumu. “Yeye ndio ameanzisha mchakato huu wa kupata Katiba Mpya, aweke masilahi ya taifa mbele sio masilahi ya chama chake cha siasa, CCM haiwezi kuwa juu ya dola na Serikali, asisaini marekebisho ya Katiba yaliyofanyika bungeni,”alisema Mbatia na kuongeza: “Mkono wa Rais usilitumbukize taifa la Tanzania katika machafuko, kwanza hagombei tena urais wala uongozi ndani ya chama chake,  sasa anamwogopa nani.”
Vyama hivyo pia vimetangaza kuanza rasmi mikutano nchi nzima kwa lengo la kuushawishi umma kupinga kile walichokiita kuwa ni ‘hujuma dhidi ya upatikaji wa Katiba Mpya’.
Mikutano hiyo itaanzia Septemba 21 mwaka huu, katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam na baadaye viongozi hao watakutana na makundi mbalimbali yakiwamo asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa, wasomi na taasisi za elimu.
Makundi mengine ni pamoja na vyama vya wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji, wavuvi, sekta binafsi, watu wenye ulemavu, jumuiya za wanawake, vijana na wastaafu.

Hivi ndivyo raia wa Ujerumani walivyoshibishwa demokrasia

Bado siku sita raia wa nchi hiyo kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu ambapo kitaifa itakuwa ni Septemba  22, mwaka huu. 
Raia wa Ujerumani wamebakiza siku sita kushiriki katika uchaguzi mkuu nchini humo huku kila chama kikiwa na Itikadi zake.
Hakuna utawala wowote wa kisiasa duniani usiojigamba kwamba ni wa kidemokrasia, hata zile nchi ambazo waziwazi unaziona ni za kidikteta.
Hata pale Wajerumani wanaposema demokrasia yao ni sawa kabisa na tafsiri asilia ya neno hilo utawala ambao chimbuko lake ni matakwa ya wananchi lakini hivyo sivyo asilimia mia moja katika utekelezaji.
Katika miji ya Uyunani ya kale, ambako neno demokrasia lilianzia, wanaume waliokuwa huru walikusanyika masokoni na kuamua juu ya sheria za kutumiwa katika miji yao.
Hata hivyo, katika miji mikubwa ya kisasa duniani, jambo kama hilo ni muhali kutekelezeka. Wananchi wanaweza tu kuelezea maoni yao kupitia wawakilishi wao waliowachagua. Siasa ni ushindani wa kuwania madaraka. Hivyo ndivyo ilivyo pia kwa nchi ya Ujerumani. Katika siku ya uchaguzi wapiga kura huamua vipi mamlaka ya Serikali yagawiwe katika kipindi cha miaka minne ijayo ya bunge.
Vyama vya kisiasa na wanasiasa baada ya kuchaguliwa hutakiwa kutilia maanani mkondo wa hisia, maoni na matakwa ya wananchi unavyokwenda kabla ya kufikia maamuzi.
Hali hii inafanya kila Serikali, ambayo wananchi wanaweza kuiondoa kutoka madarakani, ijitahidi kuhakikisha wananchi wanaridhika nayo.
Ni wazi kwamba pale Serikali yeyote inapohisi haiwezi kuondolewa kutoka madarakani na wananchi basi inakuwa haijali na hujifanyia mambo inavyotaka.
Uchaguzi hutoa nafasi kwa upinzani kuingia madarakani pale wananchi wanapoamua wanataka mabadiliko.
Raia ndio wenye kuamua juu ya namna ya kugawa madaraka ya kisiasa na ni ndiyo wenye kuhalalilsha mgawo huo.
Hata raia wasiokwenda kupiga kura nao wana ushawishi juu ya Serikali ijayo. Wingi wa wapiga kura unaathiri matokeo ya uchaguzi na sura ya Serikali ijayo.
Msingi wa demokrasia ni wengi wape. Programu ya kundi liliopata kura nyingi ndio inayotekelezwa, bila ya shaka kutilia maanani pia maoni ya walio wachache.
Demokrasia haisemi kwamba walio wengi ndio wana haki ya kila kitu, haitaki kuweko udikteta wa walio wengi, lakini inataka upinzani usikilizwe na upewe nafasi huru ya kuwashawishi walio wengi wabadilishe mawazo yao, kama inawezekana.
Nchini humo upinzani hukaa chonjo kusubiri kuingia madarakani pale wananchi wanapotaka yafanyike mabadiliko.
Raia wote wa Ujerumani wana haki ya kupiga na kupigiwa kura bila ya kujali dini, kiwango cha elimu, jinsia, kipato na kazi gani ambayo  anaifanya.
Shuruti ni kwamba mpiga kura asiwe chini ya umri wa miaka 18, japokuwa baadhi ya mikoa inaruhusu wenye umri wa miaka 16 kushiriki katika chaguzi za mabunge ya mikoa.
Tangu mwaka 1992  ulipotiwa saini Mkataba wa Maastricht raia wa nchi za Umoja wa Ulaya wanaweza kupiga kura katika chaguzi za Serikali za mitaa.
Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani ni demokrasia inayotegemea vyama ambavyo hupigania kuungwa mkono programu zao.
Wajerumani wanapopiga kura hutilia maanani sana programu za vyama, viongozi wa vyama hivyo, na kwa kiwango kidogo wagombea wa vyama hivyo.
Christian Democratic, CDU, chama kinachoongozwa na Kansela wa  sasa, Angela Merkel, kwa muda wa miaka 41 kimekuwa kikishiriki katika Serikali mbalimbali za mseto.
Kansela wa kwanza wa Ujerumani na wa kutoka Chama hicho, Konrad Adenauer ( 1949-1963),  alikuwa alama ya kuifungamanisha Ujerumani na Jumuiya ya Kujihami ya Magharibi, NATO, na Umoja wa Ulaya.
Pia Kansela wa kutoka Chama hicho, Helmut Kohl (1973-1998) anatajwa kuwa ni muasisi wa Umoja wa Ujerumani. Angela Merkel ndiye sasa mgombea wa ukansela wa chama hicho
Social Democratic, SPD, kutokana na programu yake ya Godesberg ya mwaka 1959, kiliachana na wito wa kutaka kuweko mapambano ya kitabaka na kikakubali kuweko uchumi wa masoko, lakini wenye kutilia maanani maslahi ya watu wasiojiweza.
 Mwishowe kilikubali nchi hii ifungamanishwe na kambi ya Magharibi. SPD imeunda Serikali za mseto na vyama tofauti.
Mwenyekiti wake ni Sigmar Gabriel, lakini mgombea wake wa ukansela hivi sasa ni Peer Steinbrueck.
Christian Social ni chama ndugu na CDU, lakini kinafanya shughuli zake tu katika mkoa wa kusini wa Bayern, ambako huko CDU haiko.
Tangu mwaka 1957  Waziri kiongozi wa Mkoa wa Bayern alitokea chama hicho. Kiongozi wake hivi sasa ni Horst Seehofer. CSU hakina mgombea wa ukansela, lakini kinamuunga mkono Angela Merkel.
Chama cha kiliberali cha Free Democratic kwa muda kimekuwa kikishiriki katika serikali za mseto. Kinataka Ujerumani ibakie imefungamana na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya NATO,  na kuweko nchini uchumi wa masoko huru. Kiongozi wake hivi sasa ni Philipp Rösler, ambaye pia ni waziri wa uchumi. Hakina mgombea wa ukansela.
Chama cha Kijani, kilichoundwa mwaka 1980, kinapigania ulinzi wa mazingira na usawa wa kijinsia katika nyadifa za kisiasa na serikalini. Hakina mgombea wa ukansela. Viongozi wake wenza ni Claudia Roth na Cem Ozdemir.
Die Linke, chama cha  mrengo wa shoto, kinapinga Ujerumani kuwemo katika Jumuiya ya kijeshi ya NATO na hakiitaki sarafu ya Ulaya ya Euro.
Katika uchaguzi wa mwaka 2009 chama hicho kilijipatia asilimia 11.9. Kinapinga jeshi la Ujerumani kujiingiza katika nchi za nje.
Mafanikio au kuhindwa kwa chama chochote kati ya hivyo ndiko kutakoamua Serikali ya namna gani wanayostahili kuwa nayo Wajerumani baada ya Septemba 22.