Gazeti la Mwananchi leo limerudi tena mitaani baada ya Serikali
kulifungia kwa wiki mbili. Kama wasomaji wetu na wananchi kwa jumla
wanavyokumbuka, Serikali kupitia Idara ya Habari (Maelezo) ililifungia
gazeti hili Septemba 27, 2013 kwa madai kwamba lilichapisha habari mbili
tofauti ambazo ilidai zilikuwa za uchochezi na kwamba zilikuwa na lengo
la kuwafanya wananchi waichukie pamoja na vyombo vyake vya ulinzi na
usalama.
Sio nia yetu hapa kueleza kwa undani maudhui ya
habari tulizozichapisha na Serikali kuzitumia kama nondo ya kulifungia
kwa muda huo mrefu. Hata hivyo, yafaa angalau kwa muhtasari tu kuweka
sawa kumbukumbu za hatua hiyo ya Serikali ambayo tunasema bila kutafuna
maneno kwamba ilikuwa ya uonevu na ya kiwango cha juu cha matumizi
mabaya ya madaraka.
Hata hivyo, huu hakika sio wakati wa kumtafuta
mchawi, kwa maana ya kutaka kujua nani hasa serikalini alitoa amri ya
kulifungia gazeti hili kwa sababu ambazo sisi tunaona hazikuwa na chembe
ya mashiko. Tulishangazwa kuona amri hiyo ya Serikali ikitolewa wakati
mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete akiwa nje ya nchi, tena akiwa katika
majukumu mazito ambayo dunia nzima ilikuwa ikiyafuatilia kwa shauku na
umakini mkubwa.
Kulifungia gazeti wakati huo hatuoni kama ilikuwa
kwa masilahi ya taifa kwa sababu hatua hiyo iliichafua taswira ya nchi
yetu na bila shaka Rais Kikwete alijikuta katika wakati mgumu kila
alipoulizwa kuhusu hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali yake.
Ni habari zipi zilizolipeleka gazeti hili
kifungoni? Habari ya kwanza ilikuwa juu ya waraka kuhusu mishahara mipya
ya watumishi wa Serikali ambayo tuliithibitisha pasipo kuacha shaka
yoyote kutoka katika vyanzo vyetu vya habari vya kuaminika katika
mamlaka za juu serikalini.
Tuliuchukulia kama taarifa muhimu sana kwa
watumishi wa Serikali na wananchi kwa jumla na hatukuona sababu ya
Serikali kutaka wananchi wafichwe kuhusu kuwapo kwa mishahara mipya kwa
watumishi wake.
Itakumbukwa kuwa, wiki chache kabla ya gazeti hili
halijachapisha habari hiyo, lilikuwa pia limechapisha habari kuhusu
mishahara mipya katika sekta binafsi kwa mujibu wa waraka wa Serikali
uliotolewa na Wizara ya Kazi na Ajira. Swali linalojitokeza hapa ni
hili: Inakuwaje mishahara mipya ya watumishi wa Serikali iwe siri na
mishahara mipya kwa sekta binafsi iwe kinyume chake?
Tunaamini kwamba utamaduni wa Serikali kuficha
habari na taarifa zenye manufaa kwa umma siyo utawala bora hata kidogo.
Ni hivi majuzi tu Rais Kikwete alipomwagiwa sifa na Rais Barrack Obama
kwa kutia saini mkataba wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi.
Habari ya pili iliyochapishwa Agosti 17 mwaka huu
na kusababisha gazeti hili kufungiwa ilihusu Serikali kuimarisha ulinzi
katika maeneo ya karibu na misikiti jijini Dar es Salaam jana yake
kufuatia kuwapo tetesi kwamba waumini wa Kiislamu siku hiyo
wangeandamana kupinga kitendo cha Jeshi la Polisi kumuweka mahabusu
Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa
Ponda. Baadhi ya waumini walikuwa wameonyesha kukasirishwa na kitendo
cha polisi kumwondoa Sheikh Ponda katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili
(Moi) na kumpeleka katika Gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam.
Habari hiyo yenye kichwa cha habari; ‘Waislamu
wasali chini ya ulinzi mkali wa polisi’ ilichapishwa ikiwa na mmoja wa
mbwa waliokuwa na polisi katika doria kutokana na hofu ya kuzuka vurugu
baada ya Swala ya Ijumaa, Agosti 16. Habari hiyo ilisema Waislamu
hawakuandamana na waliswali kwa amani na utulivu na kwamba polisi hao
waliokuwa na mbwa, huku wengine wakitumia pikipiki kufanya doria
walitanda katika mitaa mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ulinzi. Lakini
kwa mshangao wetu, Serikali katika kujaribu kuhalalisha kulifungia
gazeti hili ilitoa tafsiri ya uongo kwamba habari tuliyochapisha ilisema
kwamba mbwa walipelekwa katika maeneo ya ibada, wakati habari hiyo
haikuwa na kitu kama hicho. Serikali ilidai katika taarifa hiyo, kwamba
lengo la habari hiyo lilikuwa kuichonganisha na waumini wa Kiislamu ili
waichukie pamoja na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, kwani kwa
Waislamu mbwa ni haramu na picha hiyo iliudhalilisha Uislamu. Taarifa
hiyo potofu ya Serikali imetuthibitishia pasipo kuacha shaka kwamba
haikuwa na nia njema na gazeti hili.
Hatua ya kulifungia gazeti hili kwa sababu za
kufikirika imesababisha maumivu kwa watu wengi. Vijana (vendors)
waliokuwa wakiuza na kusambaza gazeti hili pamoja na familia
zinazowategemea wameumia. Waandishi wa kujitegemea wanaolipwa kutokana
na habari wanazotuma gazetini wameumia pamoja na familia zao. Hivyo
hivyo, watoa matangazo na wasomaji waliokuwa wakilitegemea gazeti hili
kwa habari za uhakika nao pia wameumia. Hasara ambayo MCL imepata
kutokana na hatua hiyo ya Serikali haitamkiki.
Pengine huu ni wakati mwafaka wa kuikumbusha
Serikali kwamba, gazeti hili pamoja na mengine yanayochapishwa na
Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), ni magazeti makini sana
yenye waandishi wa habari wanaoheshimu maadili ya taaluma yao. Hatusemi
kwamba hatuwezi kufanya makosa, kwani sisi ni binadamu.
Hata hivyo, inapotokea tukafanya makosa tunafanya masahihisho
stahiki haraka kwa lengo la kupunguza maumivu kwa yeyote tuliyemkosea.
Makosa ya makusudi kama kuandika habari za uongo hayavumiliki na kila
mwandishi wa kampuni yetu anatambua fika kwamba kufanya hivyo ni
kujitakia kiama.
MCL imeweka miongozo ya sera na malengo ya uhariri
kwa waandishi. Lengo ni kuhakikisha habari zinazochapishwa ni sahihi,
zinatenda haki na haziegemei upande wowote. Kwa maana hiyo, vyombo vyake
vya habari vinasimamia ukweli na haki na waandishi wake wana jukumu la
kuhakikisha wanakuwa na kiwango cha juu cha weledi na maadili ili
kuwawezesha kutoa habari kwa umma.
Tumetoka kifungoni tukiwa na somo muhimu. Kwamba
sheria kandamizi kama Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 haisimamii
masilahi ya taifa, bali kundi la watu wachache. Ni sheria kandamizi
ambayo kwa umoja wetu tunaweza kuifuta. Tungependa kuwashukuru wasomaji
wetu na wananchi kwa jumla kwa kuwa nasi katika kipindi kigumu
tulichokuwa kifungoni. Vilevile, tunavishukuru kwa namna ya pekee vyombo
vyote vya habari vya ndani na nje ambavyo vilisimama imara kupinga
hatua ya Serikali kufungia magazeti.
Tutakuwa watu wasio na shukurani kama hatutatambua
mshikamano mkubwa ulioonyeshwa na asasi za kiraia, mabalozi na watu
mbalimbali kupinga matumizi ya sheria hii kandamizi. Hatujakata tamaa,
bali tumetoka kifungoni tukiwa na hamasa kubwa kuendelea kuwapa habari
wananchi pasipo woga wala upendeleo.
Hatupambani na Serikali, lakini tutaendelea
kuikosoa pale inapofanya makosa na tutaipongeza pale inapotimiza wajibu
wake. Tunawaomba wasomaji wetu mwendelee kutuunga mkono.

No comments:
Post a Comment