Tuesday, 2 April 2013

Maghorofa 100 Dar feki, Serikali ina kigugumizi

 Kwanini Serikali haichukui hatua kwa majengo hayo 100 yaliyobainika kuwa hayajajengwa kwa kuzingatia viwango? Wenye akili timamu wanaweza kuendelea kujiuliza maswali mengi zaidi na kujibu wanavyoweza.


Dar es Salaam.
Kuporomoka jengo lililopo Mtaa wa Indira Gandhi Jijini Dar es Salaam, huenda ikawa mwanzo tu wa kuporomoka majengo mengine zaidi hasa kufuatia matokeo ya tume iliyoundwa mwaka 2006 iliyobaini zaidi ya majengo 100 Jijini Dar es Salaam yamejengwa bila kuzingatia viwango.
Kwanini Serikali haichukui hatua kwa majengo hayo 100 yaliyobainika kuwa hayajajengwa kwa kuzingatia viwango? Wenye akili timamu wanaweza kuendelea kujiuliza maswali mengi zaidi na kujibu wanavyoweza.
Wapo wanaoweza kusema rushwa ndio inasababisha mambo mengi kutofanyiwa kazi kwa ufasaha, lakini mbele ya sheria utaombwa utoe ushahidi, hapo bila shaka patafanya wengi kubadili maneno kwamba aaah labda Serikali inaendelea kufanya mchakato, mpango mkakati, mkakati yakinifu nk dhidi ya majengo hayo.
Kubomoa jengo lenye ghorofa 16 au hata chini au zaidi ya hapo baada ya kulibaini halijazingatia viwango, ni lazima uwe na uso mgumu. Baadhi ya wananchi wanasema wenye majengo bila shaka hawawezi kutulia wakisubiri sheria ifanye inachotakiwa kufanya, hapo ndipo ugumu unapoanzia.
Pinda analo na kujibu
Baadhi ya watu wanafikiri kuondolewa madarakani kwa viongozi walio katika wizara husika na sakata hili akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye ofisi yake ilichunguza na kubaini maghorofa zaidi 100 kuwa ni feki, kunaweza kuwa ni mojawapo ya mambo muhimu kwa sasa.
Mke na watoto wafukiwa
Licha kwamba jengo hilo liliporomoka saa 2.30 asubuhi, baadhi ya watu waliofukiwa na kifusi cha jengo hilo walikuwa wakiwasiliana na jamaa zao kwa njia ya simu na wengine wakipiga kelele za kuomba msaada.
Idd Baka ambaye alikuwa akiwasiliana na mkewe ambaye aliegesha gari huku ndani kukiwa na watoto wake wawili alikwenda dukani kununua bidhaa, mara jengo hilo likaporomoka, alikuwa akiwasiliana nae hadi majira ya mchana simu ya mke wake haikuwa inapatikana.
Vifaa duni
Ni dhahiri kwamba endapo kungekuwapo na vifaa vya kutosha katika zoezi la uokoaji lingewezaa kufanikiwa kwa  muda mfupi na kwa kiasi kikubwa hivyo kuwapata majeruhi wakiwa hai.  
Katapila latumika
Cha  ajabu na aibu kwa taifa kutokuwa tayari kwa kuwa na vifaa vya kuokolea kwani tangu saa 2:30 hadi ilipofika saa 4.30 ndipo lilipatikana katapila moja ambalo nalo halikuwa na tija kutokana na kuwapo kwa uwezekano wa kuwakandamiza au kuwajeruhi zaidi  watu waliofukiwa na kifusi hicho.
Kutokana na kutokuwepo na vifaa vya kukatia nongo waokoaji iliwachukua takribani dakika 15 kukata nondo zilizokuwa zimemkandamiza.
Umati wa watu ulivamia kifusi na kuanza kukisomba kwa mikono  ili hali jambo hili lilikuwa kama mchezo wa kuigiza ambao umegharimu uhai wa watu zaidi ya 35 pamoja na kuharibu magari yaliyobondwa na kuwa kama chapati takribani matano.
Mashuhuda
Ali Mparang’ombe mmoja wa mafundi wa jengo hilo anasema kudondoka kwa jengo hilo ni mtiririko wa majengo mengine kutokuwa katika viwango vinavyotakiwa.


“Ndugu yangu mimi ni fundi nilikuwa nimeingia ndani, lakini nilitoka kwenda upande wa pili kutafuta chai kwani leo (Ijumaa iliyopita) ni sikukuu mama lishe hawakuwepo wengi hapa”anasimulia Mparang’ombe na kuongeza:
“Ndipo kwa kule nilisikia kishindo kikubwa, kuja kuangalia ni jengo nililotoka takribani dakika 15 tu limeanguka, nimepoteza watu muhimu sana ambao tulikuwa tukifanya sote kazi, sasa sijui itakuwaje”.
Mparang’ombe anasema jengo hilo lilikuwa likijengwa chini ya viwango kwani katika ndoo 12 za mchanga walikuwa wakichanganya saruji mfuko mmoja.
Majengo mengi feki
“Hapa kama kama ndoo 12 mfuko mmoja wa saruji unategemea nini, na ni majengo mengi hapa mjini ambayo yamejengwa kwa aina hii, hivyo ni kudra za Mwenyezi  Mungu zinahitajika”anasema Mparang’ombe.
“Jengo hili lilipofika ghorofa ya 12 lilisimamishwa kujengwa na ghorofa ya 15 lilisimamishwa tena lakini hatujui alikuwa anatumia njia gani hadi akawa anaruhusiwa kuendelea na ujenzi,” anasema.
Kibali cha jengo lililoanguka
Naibu Meya wa Halmashauri ya Ilala, Kheri Kessy alisema mwaka 2007 walitoa kibali kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kushirikiana na ‘Aliraza Investment Limited’ kujenga jengo la ghorofa 10.
Alipotakiwa kueleza kwa nini hawakuchukua hatua baada ya kuendelea kujengwa hadi kufikia ghorofa zaidi ya 10,  alisema hawahusiki, ila kuna taasisi zingine za Serikali zinazosimamia majengo zinatakiwa kuulizwa.
Matokeo ya tume yanapuuzwa
Mwaka 2006 Tume iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa ilibaini kuwa zaidi ya maghorofa 100 yaliyopo jijini Dar es Salaam yalikuwa chini ya viwango.
Idadi hiyo ni tone tu la maghorofa yaliyo chini ya viwango nchi nzima ambayo bila shaka kuyabomoa ugumu unakuja pale wamiliki wake kuwa vigogo na wafanyabiashara mashuhuri.
Hali kadhalika akiwa bungeni wakati wa majumuisho ya Ofisi yake Bungeni mwaka 2008/09, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema ofisi yake ingechukua hatua za makusudi dhidi ya majengo ili kuzuia vifo kama hivi visivyo vya lazima. Kufumbia macho mambo ndiko leo kumesababisha watu zaidi ya 35 kuuawa, achilia mbali mali zingine yakiwemo magari.

Jamii:Kwanini Tanzania haiendelei haraka

Ombaomba wa India wanafanya jambo kukushawishi kumsaidia.Kwa mfano nikiwa katika mitaa ya New Delhi, nilikutana na ombaomba, walianza kunichezea muziki na michezo mingine, kabla ya kunisogelea na kuomba

 
New Delhi, India. Hivi karibuni nilikuwa nchini India, ni baada ya kuwa nimechaguliwa kati ya waandishi pekee wawili kutoka Tanzania, kuungana na waandishi wengine 16 kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa ajili ya mafunzo na pia kuripoti mkutano baina ya India na nchi za Afrika, uliofanyika Jijini New Delhi.
Zaidi ya New Delhi, nilitembelea pia miji mingine kama vile Noida, Agra, Mumbai na kadhalika. Ninachoweza kusema ni kuwa kuna mambo mengi ambayo Tanzania inapaswa kujifunza kutoka India. India ni taifa linalokua haraka, wapo ombaomba lakini hata ukizungumza nao unakuta ‘wanafikiri  tofauti’ na sisi;wana tofauti kubwa na wa hapa nchini.
Tofauti ya ombaomba wa Tanzania na India
Ombaomba wa India wanafanya jambo kukushawishi kumsaidia.Kwa mfano nikiwa katika mitaa ya New Delhi, nilikutana na ombaomba, walianza kunichezea muziki na michezo mingine, kabla ya kunisogelea na kuomba.
Mtoto mwenye mmoja mwenye umri wa miaka nane hivi, alijichora uso kama paka usoni, hakika utatamani kumwangia maana anachekesha. Japo si wote wanaofanya kitu kabla ya kuomba, wengi ni wabunifu.
Hata nilipotembelea katika miji mingine, ikiwemo Mumbai bado niliendelea kubaini ubunifu wa watu hawa, kule nilikutana kwa mfano na dada mmoja aliniita akanifunga ua mkono wa kulia, nikawa nafikiri ni kama ‘karibu mgeni’…kule alikuwa ni ombaomba, baadae alianza kuniomba fedha.Haina maana kwamba ombaomba ni kazi nzuri, ninachotaka kukieleza hapa ni kwamba ni kuonyesha namna gani wenzetu wana ubunifu.
Hata wafanyakazi nchini, unakuta wengi sawa wanakuwa ofisini lakini wapo ambao ni wazembe, wengine wako bize na mitandao ya kijamii, badala ya kufanya mambo ya maana, mwisho wa mwezi ndio wa kwanza kuuliza kama mshahara umeshatoka au bado.
Baadhi ya wanandoa, ni mafisadi, anatumia fedha kuhonga, kulewa badala ya kuimarisha nyumba yake. Ulioa au kuolewa kwanini kama unashindwa kutulia na familia yako? Wengi wazuri wa kulalamika wanapata fedha ndogo, je unakitumiaje kidogo unachokipata?
Wengine wanahonga zaidi kuliko kufanya maendeleo, japo wachumi wanashauri kwamba ukitaka kuwa na maendeleo hakikisha angalau unaweka akiba asilimia 15 ya kipato chako, ili mwisho wa mwaka ufanyie kitu fulani kikubwa.
Wapo wanaoweza kuuliza aaah kipato chenyewe kidogo nitaweza kuwekeza hiyo asilimia 15? Jiulize je, kipato chako kingepungua au mwajiri wako angepunguza mshahara kwa asilimia 15 ungefanyaje?
Kama ungeishi, maana yake ni kwamba unapaswa kuishi na kufumbia macho hiyo asilimia 15 kwa kuiweka akiba ili hatimaye mwisho wa siku ufungue mradi au kuendeleza shughuli zako, hii ndio siri muhimu ya kufanikiwa katika maisha.Fanya kama hiyo asilimia 15 haiko, tafuta njia zingine za kuishi.
Mojawapo ya sababu ya kutokua haraka kwa maendeleo hapa nchini, ni tatizo la ubunifu na uwezo wa kuthubutu.Wengi wa Watanzania ni maarufu wa kulalamika, badala ya kuchukua hatua.Muda mwingi unapotea.
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma India na Tanzania
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi na Watumishi wa Umma Tanzania ina maswali mengi hasa namna inavyofanya kazi zake. Ni kama iko tu kufurahisha wakubwa, sio kusaidia kweli taifa, ndivyo watu wengi wanavyoona.
Kwa mfano mwisho wa viongozi kujaza fomu za kueleza mali zao na kuzirudisha kwenye sekretarieti hiyo ilikuwa Disemba 31 mwaka jana. Hata hivyo wale ambao hawajatangaza mali, hakuna hatua za kisheria wanazochukuliwa.

Saturday, 30 March 2013

Odinga akwaa kisiki tena



Nairobi.Mahakama ya Juu ya Kenya imemthibitisha Uhuru Kenyetta kuwa Rais halali mteule wa nchi hiyo pamoja na mgombea mwenza wake, William Ruto.


Mahakama hiyo iliwathibitisha Kenyatta na Ruto jana katika uamuzi wa kesi ya kupinga matokeo uliowapa ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Machi 4, 2013, iliyofunguliwa na mpinzani wao mkuu katika kinyang’anyiro hicho, Waziri Mkuu, Raila Odinga.


Odinga katika kesi hiyo aliituhumu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya nchi hiyo kuwa ilihujumu matokeo ya uchaguzi ili kumpa ushindi, Kenyatta.Hata hivyo, katika uamuzi wake jana Mahakama hiyo ilisema kwamba Kenyatta na Ruto walichaguliwa kihalali katika uchaguzi huo mkuu.

Maaskofu waijia juu Serikali



Dodoma. Wakristo wamesema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imeshindwa kuwasaidia ili waishi kwa amani na utulivu katika nchi yao.


Kauli hiyo ilitolewa jana na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu, wakati akisoma tamko la Maaskofu wa madhehebu ya Kikristo Tanzania katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa lililopo eneo la Jamatini.

Katika tamko hilo alilolisoma kwa niaba ya Maaskofu wote, Kinyunyu alisema kuwa umefika wakati ambao Wakristo wamechoka na vitendo wanavyofanyiwa na baadhi ya waumini wa dini zingine.


“Tatizo ni kuwa Serikali inashindwa kuchukua hatua mapema, makanisa yanachomwa, migogoro inazidi, lakini hakuna hatua zozote ambazo Serikali inachukua katika kunusuru hali hiyo, tumechoka,” alisema.


“ Serikali imeshindwa kuchukua hatua kwa muda mwafaka kwa kila jambo ambalo linatokea kwa Wakristo na hata inapoonyesha kuwa imechukua hatua haionyeshi sana kujali juu ya yale wanayofanyiwa Wakristo. Askofu huyo alisema kuwa matokeo yanayotokea Zanzibar mathalan, Wakristo wanaoishi huko yamewasababishia hofu hivyo wengi kuanza kuvikimbia visiwa hivyo na kukimbilia Tanzania Bara.


Kwa mujibu wa Askofu Kinyunyu, suala la uchomaji wa makanisa hadi sasa limeshindwa kupatiwa ufumbuzi na kila kukicha bado makanisa yanaendelea kuchomwa moto akahoji Serikali kukaa kimya maana yake nini.

Aidha, tamko hilo limeitaka Serikali kuweka utaratibu mzuri na ufafanuzi wa kina kuhusu uchinjaji wa nyama ambao umekuwa ni tatizo kubwa hapa nchini. “Hapa litolewe tamko kila mtu kwa imani yake achinje mwenyewe siyo kuanza kulaumiana au kumpa haki mmoja akachinja na mwingine akaachwa. Tunaomba sana ufafanuzi wa kina juu ya suala hilo ili kuondoa mgogoro baina yetu na wenzetu.”
wamekuwa wakifanyiwa, lakini akasisitiza kuwa wanatakiwa kupigana kwa maombi na ndiyo silaha kubwa ya ushindi.


Katika hatua nyingine, wakati Wakristo wakiwa na hofu ya kusherehekea Sikukuu ya Pasaka watu wasiofahamika wamevamia makanisa matatu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini na kuvunja ofisi za wachungaji na wainjilisti.

Serikali yatwishwa zigo migogoro ya kidini nchini


“Baada ya kufa kwa Azimio la Arusha nchi ilipoteza itikadi imara ya kitaifa, kukosekana kwa itikadi hii ndiyo kumesababisha nchi kuongozwa bila kuwa na mfumo unaoeleweka. Mambo hayo ndiyo yanayosababisha migogoro…,” alisema Profesa Mpangala.

lakini walifumbiwa macho na kutochukuliwa hatua yoyote, sasa tabia hiyo imeota mizizi.
Juzi maaskofu hao walitoa tamko hilo katika ibada ya Ijumaa Kuu mjini Dodoma, kusema umefika wakati ambao Wakristo wamechoka na vitendo wanavyofanyiwa na baadhi ya waumini wa dini zingine.


“Tatizo ni kuwa Serikali inashindwa kuchukua hatua mapema, makanisa yanachomwa moto visiwani Zanzibar, migogoro inazidi, lakini hakuna hatua zozote ambazo Serikali inachukua katika kunusuru hali hiyo, tumechoka,” ilisema taarifa ya maaskofu.


Wakati maaskofu hao wakieleza hayo, jana Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum aliliambia Mwananchi Jumapili kwamba Serikali inatakiwa kuwakutanisha masheikh na maaskofu ili kumaliza tofauti zilizopo.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen-Kijo Bisimba alisema Serikali ilitakiwa kuchukua hatua miaka mingi iliyopita kwa kuwa mgogoro huu haukuanza leo.


“Migogoro ya kidini ilianza siku nyingi lakini Serikali ilikuwa kimya, wapo watu waliokamatwa kwa tuhuma za kukashifu dini za wenzao lakini hawajachukuliwa hatua yoyote,” alisema Bisimba.


Akizungumzia hali hiyo Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema migogoro hiyo ilianza kuchipua miaka michache baada ya kufa kwa Azimio la Arusha.


“Baada ya kufa kwa Azimio la Arusha nchi ilipoteza itikadi imara ya kitaifa, kukosekana kwa itikadi hii ndiyo kumesababisha nchi kuongozwa bila kuwa na mfumo unaoeleweka. Mambo hayo ndiyo yanayosababisha migogoro…,” alisema Profesa Mpangala.

Alisema jambo jingine ni kufa kwa Siasa za Ujamaa na Kujitegemea, ongezeko la umaskini na watu kukosa ajira, hivyo kuwa wepesi kushawishika kujiingiza katika migogoro ya kidini.

“Nadhani umefikia wakati wa Serikali kufuata sheria ili kumaliza hali hii, ikiwa ni pamoja na kukutana na pande zenye migogoro,” alisema Mpangala.

Mhadhiri mwingine wa Chuo hicho, Dk Kitila Mkumbo alisema Serikali inatakiwa kufanya mambo mawili ili kumaliza tatizo hilo. Jambo la kwanza ni kuzikutanisha pande zote mbili huku yenyewe ikiwa katikati na kutoegemea upande wowote.


Katika maelezo yake, Sheikh Mussa alisema, “Serikali ndiyo mlinzi wa amani hivyo inatakiwa kuhakikisha inawakutanisha watu wa pande zinazosigana kiitikadi, lakini Watanzania pia tunatakiwa kutambua thamani ya amani yetu hivyo tunatakiwa kuisaidia Serikali katika jambo hili.”

Katika tamko la maaskofu hao lililosomwa na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu alisema, “Serikali imeshindwa kuchukua hatua kwa muda mwafaka, pindi inapotokea migogoro au dini moja kutishiwa amani.”

“Matokeo yanayotokea Zanzibar mathalan, Wakristo wanaoishi huko yamewasababishia hofu, hivyo wengi kuanza kuvikimbia visiwa hivyo na kukimbiliaTanzania Bara.”

Kwa mujibu wa Askofu Kinyunyu, suala la uchomaji wa makanisa hadi sasa limeshindwa kupatiwa ufumbuzi na kila kukicha bado makanisa yanaendelea kuchomwa moto akahoji Serikali kukaa kimya maana yake nini?

Ni simanzi, taharuki zatawala D’Salaam


Zoezi la kutafuta miili iliyokwama katika vifusi inaendelea, zaidi ya maiti 22 zapatikana.
Dar es Salaam. Idadi ya watu waliokufa kutokana na kufukiwa na kifusi cha jengo la ghorofa 16 lililoporomoka juzi asubuhi jijini Dar es Salaam, imefikia 22.


Habari zilizopatikana kutoka eneo la uokoaji na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova zinaeleza kuwa miili iliyopatikana imepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.


Jengo hilo lililokuwa likijengwa mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi na Kampuni ya Lucky Construction Limited liliporomoka saa 2.30 asubuhi wakati mafundi na vibarua wakiendelea na ujenzi huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.

Rais Kikwete
Rais Jakaya Kikwete ambaye jana pia alifika katika eneo la tukio, kama ilivyokuwa juzi, alipata taarifa fupi ya maendeleo ya uokoaji kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadik na Kamanda Kova.


Baada ya kupewa taarifa hiyo, Rais Kikwete alimwagiza Kamanda Kova kuhakikisha wahusika wanakamatwa akiwamo Mkadiriaji Majengo (Quantity surveyor), mchora ramani za majengo (Architecturer), Mhandisi Mshauri (Consultant) na Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam. Juzi baada ya kutembelea eneo la tukio, Rais Kikwete aliagiza wahusika wote wa ujenzi huo wachukuliwe hatua kali.


Habari zilizopatikana jana zilidai kuwa Diwani wa Kata ya Goba, Wilaya Kinondoni, Ibrahim Kisoka ambaye ndiye mmiliki wa kampuni ya ujenzi, na Mhandisi Mshauri kwa pamoja wamejisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi na hadi saa 8:00 jana mchana walikuwa wakihojiwa.


Awali Kamanda Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa amemtaka mmiliki wa Kampuni ya Lucky Construction Limited ambaye ni Diwani wa Kata ya Goba, Kisoka na wahusika wengine kujisamilisha kituo cha polisi, kabla hawajaamua kutumia nguvu kumtafuta.

Pinda atembelea eneo la tukio
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifika eneo hilo saa 3:41 asubuhi, kujionea hali ilivyo, lakini hakutoa tamko lolote. “Sina la kusema,” alisema Waziri Mkuu alipoulizwa na waandishi wa habari kutoa kauli ya serikali kuhusiana na tukio hilo.


Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi aliyefuatana na Pinda, alisikika akimwagiza Kamanda Kova kuhakikisha mchora ramani wa jengo hilo naye anatiwa nguvuni kwa kuwa jengo hilo lilikuwa la ghorofa 10, lakini likajengwa hadi 16. Mtu mwingine ambaye anatafutwa na jeshi la polisi kukamatwa ni Mhandisi Mshauri.


Lukuvi alimwagiza Kova kuwa watu waliokuwa karibu na jengo jingine la ghorofa 15 lililojengwa na mkandarasi huyo, kuhama mara moja na ubomoaji ufanyike bila kuleta madhara.

Mwenyekiti wa CUF
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alitumia fursa hiyo kuitaka Serikali kuwabana makandarasi wasio na sifa kwani wanahatarisha maisha ya watu.
“Huu ni uzembe, wahandisi wa jiji walikuwa wapi? Wasimamizi na washauri walikuwa wapi hadi jengo linafikia ghorofa 16?” Alihoji Profesa Lipumba.


Profesa Lipumba aliitaka Bodi ya Makandarasi (CRB) kufuta leseni ya kampuni hiyo, kwani imeonyesha kuwa haiwezi kusimamia ujenzi na hivyo kusababisha vifo.

Huzuni, vilio na simanzi
Vilio na huzuni viliendelea kutanda jana katika eneo hilo ambapo waokoaji walikuwa wakijitahidi kufukua vifusi na kuzingirwa na watu waliokuwa wakisubiri ndugu zao waliofukiwa na kifusi kutolewa.


Watu wengi tangu asubuhi walikuwa wamesimama karibu na eneo hilo huku wengi nyuso zao zikiwa zimegubikwa na simanzi na wengine wakilia. Mama mmoja aliyekuwa akilia mapema asubuhi katika Mtaa wa Mshihiri, alisema mwanawe ni fundi na jana hakurudi, lakini pamoja na kilio, alisema bado haamini kama mwanawe amepoteza maisha.


Mwingine aliyekuwa ameshikiliwa na wenzake, alisikika akisema miongoni mwa waliopotea ni mume wake aliyemuaga asubuhi kuwa anakwenda kibaruani lakini hadi usiku wa manane hakurudi hivyo ilibidi afike eneo hilo.


Mama mwingine wa jamii ya Kihindu aliyekuwa akilia, alizirai kabla ya kuzinduka baada ya kupatiwa huduma ya kwanza. Mama huyo alisema mtoto wake ni miongoni mwa waliokwama kwenye kifusi hicho.

Barabara zafungwa
Mbali ya watu hao barabara zote zinazoingia katika eneo hilo zimefungwa.
Barabara hizo ni Mshihiri na Morogoro, Hazrat Abbas, Mali -Asia, Mali-Zanaki, Mtaa wa Zanaki, India na Indira Ghandhi.

Wachina walishangaa ‘zege’
Wachina wa Kampuni za ujenzi za China zilizopo nchini, Beijing Construction Engineering Group, BCEG iliyojenga Uwanja wa Taifa, na ile ya China Civil Engineering Construction Company (CCECC) inayojipanga kwa ujenzi wa Daraja la Kigamboni, ni miongoni mwa waliofika kusaidia uokoaji.

0
inShare


Mmoja wa Wachina hao alichukua kipande cha zege kilichotoka kwenye jengo hilo, na kukisaga kwa kutumia mkono, kikapukutika.


“Hii mchanga mingi..., hakuna zege kama hii,” alisema Mchina huyo kutoka Kampuni ya CCECC ambaye hata hivyo alikataa kutaja jina lake.
Wachina hao walitoa kijiko ambacho ndicho kilichosaidia kwa kiasi kikubwa katika uokoaji huo.

Huduma za kijamii
Mashirika mbalimbali ya hisani, yalikuwa na kazi ya kuleta vyakula, maji na vitu vingine kwa waokoaji ili kazi iendelee bila kusimama.


Malori ya Kampuni ya Strabag yanayotumika kwa ujenzi wa Barabara ya Morogoro kwa mabasi yaendayo kasi, yalishiriki kikamilifu saa 24 kuzoa kifusi hicho kilichokuwa kimejaa nondo za kila saizi.


Vikosi vya uokoaji pamoja na manesi wa Hospitali ya Mwananyamala, Hospitali ya Ibrahim Hajj na Chama cha Msalaba mwekundu, wameweka kambi wakiwa na dawa, dripu, na vitu mbalimbali vya huduma ya kwanza.

Matukio mengine
Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu jengo kuanguka, kwani Februari jengo la ghorofa nne lilianguka maeneo ya Kijitonyama Mpakani jijini Dar es Salaam na kusababisha kifo cha mtoto wa miaka 9.


Licha ya ujenzi wa jengo hilo kusimamishwa miaka 10 iliyopita, familia ya marehemu iliendelea kuishi katika jengo hilo.


Juni 21, 2008 jengo la ghorofa 10 lilikuwa likiendelea kujengwa na Kampuni ya NK Decorators katika Mtaa wa Mtendeni Kisutu jijini Dar es Salaam liliporomoka na kuua mtu mmoja.


Mwaka 2006 jengo la ghorofa lilianguka eneo la Chang’ombe Village Inn na kuua mtu mmoja, baada ya tukio hilo aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa aliunda tume kuchunguza tukio hilo ambayo ilibaini kuwa zaidi ya maghorofa 100 jijini Dar es Salaam yalikuwa yamejengwa kinyume na taratibu za ujenzi.

Saturday, 23 March 2013

Wanyamapori 15,000 wauawa nchini



Moshi. Zaidi ya wanyamapori 15,220 wameuawa na majangili katika hifadhi mbalimbali zilizopo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) katika kipindi cha miaka minne iliyopita wakiwamo tembo 419.


Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alipendekeza kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kuchunguza kuimarika kwa mtandao wa ujangili nchini.

“Ni mtandao wa kimafia ambao hata baadhi ya watendaji serikalini wanaujua, lakini wanauogopa sasa. Katika mazingira haya ni vyema Bunge likachunguza ni kina nani hawa ambao wanaogopwa,” alisema.


Kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa Tanapa, Mtango Mtahico, baadhi ya wanyama waliouawa kwa ajili ya kitoweo walikaushwa na kusafirishwa nje ya nchi zikiwamo nchi za Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan.


Mtahico alisema katika wanyamapori hao 15,220 waliouawa na majangili kati ya mwaka 2009 na 2012, kwa ajili ya kitoweo wamo nyumbu, mbogo, nyamera, pofu, pundamilia, swala na wanyama wengine.


Mhifadhi huyo alitoa taarifa hiyo juzi katika kikao cha wadau wa uhifadhi Kanda ya Kaskazini kilichohudhuriwa na wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge na wakurugenzi wa halmashauri.


“Ujangili huu wa wanyama ambao unaongezeka nchini unachochewa na mahitaji ya kitoweo na pia mahitaji ya kibiashara kama ya pembe za ndovu na faru duniani”alisema Mhifadhi Mkuu huyo.

Mtahico alisema katika miaka ya hivi karibuni, mitandao ya ujangili imekuwa ikijiimarisha na kutumia silaha za kivita, sumu na nyaya ambazo mpaka sasa hazijulikani zinatoka maeneo gani ya nchi.“Utafiti unaendelea kujua hizi nyaya zinatoka wapi maana zinakamatwa nyingi, lakini hazipungui na hizi hazichagui zikishategeshwa zinaweza kuua hata nyumbu 100 kwa mara moja,” alisema Mtahico.


Akizungumza katika mkutano huo wa siku mbili, mbunge wa Karatu, Israel Natse alilalamikia unyama unaofanywa na askari wa Tanapa wanaodhibidi ujangili akitaka wabadili mtazamo wa utendaji kazi.


“Rangers (askari) ni wanyama mno, vitendo wanavyofanya utadhani ni vitendo vile vilivyokuwa vikifanywa na Makaburu,” alisema Natse akilalamikia pia fidia ndogo kwa watu wanauawa na wanyama.


Kauli hiyo iliungwa mkono pia na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari ambaye alisema kuna udhalilishaji mkubwa wanaofanyiwa wananchi wanaokutwa wakiwa ndani ya hifadhi hizo.

Xi Jinping kusaini mkataba ujenzi wa Bandari Bagamoyo



Dar es Salaam. Rais wa China, Xi Jinping anatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ziara ya siku moja, ambapo pamoja na mambo mengine atasaini mikataba 17, kati ya nchi hiyo na Tanzania, ukiwamo wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani.


Ujenzi huo utakaofanywa na Kampuni ya Merchants Holding ya China, utakwenda sambamba na ujenzi wa barabara inayounganisha bandari hiyo na Reli ya Kati na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).


Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema ujio wa rais huyo aliyechaguliwa wiki mbili zilizopita, utakuwa wa manufaa makubwa kwa Tanzania.


“Mbali na mkataba huo pia tutasaini mikataba wa kidiplomasia. Vilevile, China imefungua soko la Watanzania kuuza tumbaku nchini humo na mkataba wa kuliendeleza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC),” alisema Membe.


Waziri huyo alisema kiongozi huyo wa China pia atafungua jengo la kisasa la mikutano la Mwalimu Nyerere.


“Kwa kuwa anakuja Afrika kwa mara ya kwanza huku Tanzania ikiwa nchi ya kwanza, Jinping pia atatoa hotuba yake juu ya msimamo wa China kwa Tanzania na Afrika kwa jumla,” alisena Membe.

Waziri Sitta awaanika wabunge wa Afrika Mashariki kuhusu posho




Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amewajibu wabunge wa Afrika Mashariki akisema wengi hawahudhurii vikao vya kupewa mwongozo kuhusu bunge hilo kwa kuwa “wanataka kulipwa posho”.

Kauli hiyo ya Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, imekuja siku moja tangu wabunge hao waichongee wizara hiyo kwa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, kwamba imeshindwa kuwapa mwongozo pale wanapokwenda kwenye vikao vya Bunge la Afrika Mashariki.

Akizungumza katika kikao cha kamati hiyo jana, Sitta alisema wabunge hao wamekuwa vinara wa kuomba posho kila wanapotakiwa kuhudhuria kwenye mikutano ya wizara yake.

Katika maelezo yake Sitta alimeshutumu Katibu wa Wabunge hao, Shyrose Bhanji kuwa ndiye anayeongoza kwa kutoa udhuru mara kadhaa, hivyo kutoudhuria vikao vinavyoitishwa na wizara hiyo.

“ Wizara imejiwekea utaratibu mzuri wa kukutana na wabunge hao, lakini nafikiri katibu wao ndiye anayeongoza kwa kutohudhuria,” alisema Sitta na kuongeza:

“Nadhani amekuwa na shughuli nyingi sana, tuna utaratibu wa kukutana kila baada ya miezi mitatu, lakini ndiye aliyeongoza pia kutoa malalamiko hayo yasiyo na ukweli.”

Waziri Sitta katika majibu yake alifafanua kwamba wizara hiyo bado haijapewa majukumu rasmi ya kutoa mwongozo kwa wabunge hao.

Mbali na Sitta, naibu wake, Abdullah Juma Saddallah naye alieleza tabia za wabunge hao huku akisisitiza kuwa posho kwao ndiyo jambo la umuhimu zaidi.

Saddallah alisema malalamiko hayo ni ya ajabu na yamewashtua kwa sababu hayana ukweli, lakini wamekuwa wakijikuta kwenye mtihani kwani kuna baadhi ya wabunge hao wakiitwa kuudhuria vikao utambulia kuuliza posho.

“Wizara haina fungu la kuwahudumia wabunge hao, hili limekiwishajadiliwa katika vikao vya kamati vilivyopita na ilikubalika kuwa ofisi ya bunge itaangalia uwezekano wa kuwapatia ofisi na vitendea kazi vingine,” alisema Saddallah.

Alisema pia kabla ya kuteuliwa wabunge hao wizara hiyo kwa kushirikiana na ofisi ya Bunge ilifanya uchambuzi na kuandaa mwongozo utakaowezesha ushirikiano na uwajibikaji baina ya Bunge la Tanzania na wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

“Mwongozo huu umewezesha kuundwa kwa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo awali ilitarajiwa kuwa Kamati ya Bunge ya Afrika Mashariki inayotoa nafasi ya kutoa taarifa za utekelezaji na kupata mwongozo,” alisema Naibu Waziri huyo.

Aliongeza kuwa “Wizara kwa kushirikiana na Bunge iliandaa semina kwa wabunge hawa mara baada ya kuteuliwa kwao ili kuwajengea uelewa wao kuhusu jumuiya kabla hawajaanza kazi zao, semina hii ilifanyika Mei 2012,” alisema.

Naibu Waziri huyo alisema katika semina waliyopewa wabunge hao mbala na kutolewa kwa mada mbalimbali kuhusu mfumo wa utendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pia wabunge

walipewa vitabu ambavyo vinaonyesha ni taratibu, misingi na hatua za Mtangamano.

Naibu Waziri huyo alibainisha zaidi kuwa wabunge hao wa EALA wamekuwa wakishirikishwa katika shughuli mbalimbali za wizara, akitoa mfano kuwa mwenyekiti wao hualikwa katika uwasilishaji wa hotuba ya Bajeti na uzinduzi wa shuhghuli mbalimbali za wizara hiyo.

Katika madai yake juzi Bhanji alidai kuwa wanashindwa kujadili maslahi ya wananchi katika Bunge la Afrika Mashariki kutokana na kutengwa na wizara, huku mwenzake Abdalah Mwinyi akisema kuwa, mpaka sasa serikali haina sera ya mtangamano ambao utawaweka pamoja wabunge wa Tanzania.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mussa Zungu alisema kamati imeridhika na maelezo yaliyotolewa na wizara hiyo, ikiwa ni pamoja na hatua ambazo imezichukua katika kuhakikisha sera inakuwepo.