Tuesday, 2 April 2013

Jamii:Kwanini Tanzania haiendelei haraka

Ombaomba wa India wanafanya jambo kukushawishi kumsaidia.Kwa mfano nikiwa katika mitaa ya New Delhi, nilikutana na ombaomba, walianza kunichezea muziki na michezo mingine, kabla ya kunisogelea na kuomba

 
New Delhi, India. Hivi karibuni nilikuwa nchini India, ni baada ya kuwa nimechaguliwa kati ya waandishi pekee wawili kutoka Tanzania, kuungana na waandishi wengine 16 kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa ajili ya mafunzo na pia kuripoti mkutano baina ya India na nchi za Afrika, uliofanyika Jijini New Delhi.
Zaidi ya New Delhi, nilitembelea pia miji mingine kama vile Noida, Agra, Mumbai na kadhalika. Ninachoweza kusema ni kuwa kuna mambo mengi ambayo Tanzania inapaswa kujifunza kutoka India. India ni taifa linalokua haraka, wapo ombaomba lakini hata ukizungumza nao unakuta ‘wanafikiri  tofauti’ na sisi;wana tofauti kubwa na wa hapa nchini.
Tofauti ya ombaomba wa Tanzania na India
Ombaomba wa India wanafanya jambo kukushawishi kumsaidia.Kwa mfano nikiwa katika mitaa ya New Delhi, nilikutana na ombaomba, walianza kunichezea muziki na michezo mingine, kabla ya kunisogelea na kuomba.
Mtoto mwenye mmoja mwenye umri wa miaka nane hivi, alijichora uso kama paka usoni, hakika utatamani kumwangia maana anachekesha. Japo si wote wanaofanya kitu kabla ya kuomba, wengi ni wabunifu.
Hata nilipotembelea katika miji mingine, ikiwemo Mumbai bado niliendelea kubaini ubunifu wa watu hawa, kule nilikutana kwa mfano na dada mmoja aliniita akanifunga ua mkono wa kulia, nikawa nafikiri ni kama ‘karibu mgeni’…kule alikuwa ni ombaomba, baadae alianza kuniomba fedha.Haina maana kwamba ombaomba ni kazi nzuri, ninachotaka kukieleza hapa ni kwamba ni kuonyesha namna gani wenzetu wana ubunifu.
Hata wafanyakazi nchini, unakuta wengi sawa wanakuwa ofisini lakini wapo ambao ni wazembe, wengine wako bize na mitandao ya kijamii, badala ya kufanya mambo ya maana, mwisho wa mwezi ndio wa kwanza kuuliza kama mshahara umeshatoka au bado.
Baadhi ya wanandoa, ni mafisadi, anatumia fedha kuhonga, kulewa badala ya kuimarisha nyumba yake. Ulioa au kuolewa kwanini kama unashindwa kutulia na familia yako? Wengi wazuri wa kulalamika wanapata fedha ndogo, je unakitumiaje kidogo unachokipata?
Wengine wanahonga zaidi kuliko kufanya maendeleo, japo wachumi wanashauri kwamba ukitaka kuwa na maendeleo hakikisha angalau unaweka akiba asilimia 15 ya kipato chako, ili mwisho wa mwaka ufanyie kitu fulani kikubwa.
Wapo wanaoweza kuuliza aaah kipato chenyewe kidogo nitaweza kuwekeza hiyo asilimia 15? Jiulize je, kipato chako kingepungua au mwajiri wako angepunguza mshahara kwa asilimia 15 ungefanyaje?
Kama ungeishi, maana yake ni kwamba unapaswa kuishi na kufumbia macho hiyo asilimia 15 kwa kuiweka akiba ili hatimaye mwisho wa siku ufungue mradi au kuendeleza shughuli zako, hii ndio siri muhimu ya kufanikiwa katika maisha.Fanya kama hiyo asilimia 15 haiko, tafuta njia zingine za kuishi.
Mojawapo ya sababu ya kutokua haraka kwa maendeleo hapa nchini, ni tatizo la ubunifu na uwezo wa kuthubutu.Wengi wa Watanzania ni maarufu wa kulalamika, badala ya kuchukua hatua.Muda mwingi unapotea.
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma India na Tanzania
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi na Watumishi wa Umma Tanzania ina maswali mengi hasa namna inavyofanya kazi zake. Ni kama iko tu kufurahisha wakubwa, sio kusaidia kweli taifa, ndivyo watu wengi wanavyoona.
Kwa mfano mwisho wa viongozi kujaza fomu za kueleza mali zao na kuzirudisha kwenye sekretarieti hiyo ilikuwa Disemba 31 mwaka jana. Hata hivyo wale ambao hawajatangaza mali, hakuna hatua za kisheria wanazochukuliwa.

No comments: