Thursday, 14 March 2013
Tume ya Mizengo Pinda yaanza kuhoji wanafunzi, walimu

Mwenyekiti wa tume hiyo Profesa Sifuni Mchome, alisema jana kwamba shughuli hiyo imeanza katika Kanda ya Dar es Salaam ambapo wajumbe watatembelea shule 12.
“Tumeamua kuzungumza na wanafunzi waliopo shuleni na wale waliofanya mtihani huo watakaopatikana ili kujua ni nini kilichofanya wakapata alama hizo, pia itakuwa njia rahisi ya kupata watu wengi ikiwa ni pamoja na bodi za shule,” alisema Profesa Mchome:
“Kazi kwa Dar es Salaam ilianza Jumatatu na itaisha Ijumaa, kuna shule ambazo zimeainishwa. Tukifika kwenye hizo shule na kama zipo shule zingine jirani tutawaita waje kutoa maoni yao.” alisema.
Profesa Mchome alisema kuwa, ili kufanikisha shughuli hiyo wameteua kanda tano ikiwamo ya Dar es Salaam, Kusini, Mashariki, Kati na Kanda ya Magharibi ambayo itahusisha Mikoa ya Geita na Simiyu.
Profesa Mchome alieleza kuwa, ili kupata maoni ya wananchi wengi wamefungua tovuti inayoitwa www.tumek4.go.tz ili wengine watoe maoni huko.
Alisema kuwa, kanda hizo zimetengwa kwa kuzingatia hadidu za rejea zilizotolewa na Waziri Mkuu, ambapo wamechangua shule zilizofanya vibaya, zilizokuwa na ufaulu wa kati na zilizofanya vizuri ambazo ni zile za Serikali na zisizo za Serikali.
Alisema kuwa, tayari wameshazungumza na maofisa elimu pamoja na Muungano wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahosa).
Alisema kuwa, baada ya kutembelea shule hizo Dar es Salaam, juma lijalo timu hiyo itaenda katika kanda nyingine ambapo zitatembelewa shule 13.
Alisema kuwa, leo ratiba ya shughuli ya tume hiyo itawekwa katika tovuti yao.Profesa mchimo aliwataka wananchi watoe zaidi maoni yao kupitia tovuti hiyo, pamoja na vyombo vya habari ili waweze kukamilisha shughuli hiyo kwa kupata maoni ya watu wengi.
Papa mpya apatikana, achagua jina la Francis

Baada ya kuchaguliwa na makardinali wenzake 115, Kardinali Jorge Bergoglio (76) alichagua kufahamika kwa jina la Francis I.
Maelfu ya mahujaji, watalii na waumini wa Kanisa Katoliki waliokuwa wamejazana katika Viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Petro, Vatican kushuhudia moshi mweupe uliofuka saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kuashiria kuchaguliwa kwake, waliripuka kwa shangwe, nderemo na vifijo.
Muda mfupi baada ya moshi huo kutoka, kardinali mmoja alisimama katika ‘varanda’ ya Kanisa la Mtakatifu Petro na kutangaza “Habemus Papum” (tumepata papa mpya).
Papa Francis I alikuwa miongoni mwa waliokuwa wanawania nafasi hiyo na papa anayeondoka, Benedict XVI mwaka 2005, ambapo aliripotiwa kuibuka wa pili.
Kabla ya kuchaguliwa kwake, Papa Francis I ambaye kwa wadhifa wake pia anakwenda kuwa Askofu wa Roma, alikuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Buenos Aires, Argentine na kwa muda wote wa utumishi wa utumishi alikuwa huko huko nyumbani.
Anakuwa Papa wa 266 kuwahi kuongoza kanisa hilo lenye waumini zaidi ya bilioni 1.2 duniani.
Baada ya kutangazwa kwake, Papa Francis I alijitokeza kuzungumza kwa mara ya kwanza kama Askofu wa Roma.
Akiwa amechaguliwa katika awamu ya tano ya upigaji kura, inaelezwa kuwa alikuwa miongoni mwa mapapa waliochaguliwa kwa haraka baada ya muda mrefu, akiwa sawa na Benedict XVI (2005) na Pius XII aliyechaguliwa mwaka 1939.
Mshindi alitakiwa kupata kuta 77 au robo tatu ya makardinali 115 walioshiriki uchaguzi huo.
Papa Francis I anachukua nafasi iliyoachwa na Papa Benedict XVI aliyejiuzulu Februari 28, mwaka huu, ikiwa ni miaka 600 tangu Papa wa mwisho kujiuzulu.
Yeye ni nani
Papa Francis I, ni Papa wa kwanza kutoka Shirika la Jesuit ambaye ametumia muda wake mwingi wa utumishi nyumbani Argentina.
Anafahamika kwa utumishi uliotukuka kwa uangalizi wa kanisa na mapadri, mambo ambayo yanatajwa kuwa sifa kubwa ya kuchaguliwa kuwa Papa.
Papa huyo amedumu katika maisha ya kufundisha na kuongoza mapadri. Amefanya kazi Amerika ya Kusini ambako kuna Wakatoliki wengi. Kardinali Bergoglio anatambulika kwa kutamadunisha Kanisa la Argentina, lililokuwa miongoni mwa makanisa ya kihafidhina huko Amerika Kusini.
Amechagua jina la Papa Francis I, chini ya uangalizi wa Mtakatifu Francis wa Assisi.
Alizaliwa Buenos Aires katika familia ya mfanyakazi wa reli. Alipata upadrisho mwaka 1969.
Aprili 15, 2005, mwanasheria wa haki za binadamu alimfungulia mashtaka ya jinai kwa kushirikiana na maofisa wa jeshi kuwateka mapadri wawili wa Jesuit mwaka 1976, akiwa kiongozi wao aliwafukuza katika utumishi kutokana na migogoro katika jumuiya hiyo.
Msemaji wake alikanusha vikali tuhuma hizo na hakuna uthibitisho uliotolewa kumhusisha na madai hayo.
Kauli yake ya kwanza
Baada ya kutangazwa kuwa Papa wa 266, Kardinali Jorge Bergoglio (76) aliwataka waumini wa Kanisa Katoliki duniani kumwombea.
Papa huyo aliyechagua jina la Francis I, alisema: “Kama mnavyofahamu, kazi ya mkutano wa uchaguzi ilikuwa ni kuchagua Askofu wa Roma,” Francis I aliueleza umati uliokuwa unashangilia katika Viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Petro, huku akiwapungia mikono.
“Ni mimi hapa. Ninadhani makardinali wenzangu wamenichagua mimi kutoka mbali...Niko hapa. Ninapenda kuwashukuru kwa kunipokea.”
Akiwa kardinali alipambana na Serikali ya Argentina chini ya Rais Cristina Fernandez de Kirchner kuhusu msimamo wake dhidi ya ndoa za mashoga na utoaji bure wa huduma za uzazi wa mpango, ambazo zimekuwa zikipingwa na Kanisa Katoliki duniani kote.
Wednesday, 13 March 2013
Waislamu waonya kauli za uchochezi

Dar es Salaam. Wakati Kiongozi wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila akitiwa mbaroni kwa tuhuma za uchochezi wa kidini, viongozi wa Jumuiya ya Kiislamu Tanzania wametoa tamko na kusema kuwa baadhi ya kauli za viongozi wa Serikali na viongozi wa dini zina mwelekeo wa kukuza mfarakano wa kidini kuliko kuleta maelewano.
Wiki iliyopita Mchungaji Mtikila alikamatwa mkoani Rukwa akituhumiwa kuwahamasisha Wakristo wawavamie Waislamu.
Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema Mchungaji Mtikila alichochea uhasama kwa kuwaeleza viongozi wa Kikristo kuwa, wamekuwa wakionewa na Waislamu kutokana na matukio yanayoendelea kutokea hapa nchi.
Katika tamko lao, viongozi wa Kiislamu walisema kuwa mara nyingi kauli za viongozi wa dini na Serikali hazina nia njema bali zimekuwa za kibaguzi au za kiupendeleo.
“ Imekuwa ni kawaida kila anaposhambuliwa au kuuawa Padri baadhi ya viongozi wa Serikali, na wale wa Kikristo, vyombo vya habari, baadhi ya asasi na taasisi za kiraia wamekuwa wakiwanyooshea vidole na kuelekeza lawama zao kwa jamii ya Waislamu,” lilisema tamko hilo.
Katika tamko hilo Jumuiya ya Waislamu ilieleza kuwa Waislamu wamekuwa wakinyooshewa vidole kutokana na matukio hayo pasipo kuwa na ushahidi.
Iliongeza kuwa wamekuwa wakishutumiwa kuhusika katika matukio kabla hata ya uchunguzi wa vyombo vya usalama na polisi kufanyika.
Tamko hilo lilisema kuwa serikali kupitia waziri wa mambo ya ndani ilitoa kauli kuwa mauaji ya padri huyo ni matokeo ya kazi za ugaidi.
Tamko hilo lilisisitiza kuwa linaungana na wapenda amani wote kulaani mauaji, manyanyaso na udhalilishaji wa aina yoyote unaowalenga viongozi wa dini.
Jumuiya hiyo imewataka viongozi wa dini na Serikali kuhakikisha wanahimiza amani na mshikamano badala ya kuwa vyanzo vya kuchochea vurugu.
Wamesema hawatafumbia macho tabia ya kuendelea kunyoshewa vidole Waislamu kila linapotokea tukio la uvunjifu wa amani nchini na wamewataka Watazania wote kwa umoja wao kusimamia ushirikiano na kuiimba amani ili kulinusuru taifa na aina yoyote ya vurugu.
Benki Kuu yaingilia kati wizi wa ATM

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeingilia kati wizi wa fedha kwa kutumia mashine za kutolea fedha (ATM), ambao umeibua hofu kubwa katika sekta ya benki nchini.
Kutokana na wizi huo kukithiri katika baadhi ya benki, wafanyabiashara na wananchi wameanza kujipanga kuondoa fedha zao katika akaunti.
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu alizungumza kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki kwamba wameziagiza benki kuweka kifaa cha umeme (electronic chip) kwenye kadi zao za ATM ambazo si rahisi kughushi.
“Wizi kama huo unatokea wakati mtu anaweka namba za siri kwenye ATM kwani kuna watu huweka kamera ambazo husoma na namba hizo kufanikiwa kuzipata kisha kufanya wizi ,” alisema Profesa Ndullu.
Alisema kuwa kutokana na wizi kukithiri wamezitaka benki zote kuweka mifuniko katika eneo la namba za siri ili wezi wanaoweka kamera ili kuzinasa wakati mtu anatoa fedha washindwe kufanya hivyo.
Profesa Ndullu alisema wanafuatilia mfumo wa utendaji wa benki ili kuondokana na tatizo hilo ambalo hivi sasa limeibua mijadala na hofu kubwa miongoni mwa wananchi.
Benki kubwa nchini zimekumbwa na mtikisiko wa wizi wa fedha kwa kadi za ATM, ambao umeongezeka kwa kasi kiasi cha kufanya wananchi wengi kuhifadhi fedha zao kwenye mitandao ya makampuni mbalimbali ya simu za mikononi ambayo hata hivyo ripoti zimekuwa zikieleza kuwa nako usalama wake si wa kiwango cha juu.
Baadhi ya benki ambazo zimekumbwa na matukio hayo zimekuwa zikisita kutoa taarifa kueleza sababu za kushindwa kuzuia wizi huo na badala yake zimekaa kimya kuhofia kupoteza wateja.
Kukua kwa teknolojia za kifedha ambako kumerahisisha ufanisi wa matumizi na utunzaji wa fedha, sasa kunaonekana kugeuka na kuwa balaa kutokana na kuibuka kwa wizi mkubwa mahala zinakohifadhiwa kwenye akaunti za wateja kwa kutumia njia ya mtandao.
Taarifa za wizi huo zilianza kurindima mwezi Machi, 2010, ambako kiasi cha mabilioni ziliibwa kupitia katika mashine za ATM huku kati ya kiasi hicho jumla ya Sh360 milioni zikihusisha benki moja nchini.
Hata hivyo, mwaka huo watu wanne walikamatwa baada ya kuripotiwa wizi huo mkubwa. Sambamba na kukamatwa kwa watu hao, pia alikamatwa mfanyabiashara mmoja aliyekuwa akifanya jaribio la kuiba kimafia Sh221 milioni kutoka benki ya NBC.
Wimbi la wizi huo limeibuka tena katika kipindi cha Oktoba 2012 hadi Februari 2013 na inakadiriwa kuwa jumla ya kiasi cha Sh700 milioni kimeibwa katika benki mbalimbali kwa nyakati tofauti.
Hivi karibuni, Polisi mkoani Mwanza kwa kusaidiana na maofisa wa Benki ya NMB, iliwatia mbaroni watu watatu ambao walidaiwa kuiba kiasi cha Sh700 milioni kwa nyakati tofauti.
Watuhumiwa hao walinaswa baada ya kuwekewa mtego na maofisa wa benki pamoja na polisi usiku wa Februari 10, mwaka huu. Mtuhumiwa mmoja alinaswa akichukua fedha katika mashine ya ATM ya NMB kwenye Tawi la PPF Plaza.
Baada ya kunaswa kwa mtuhumiwa huyo, alisaidia kuwaelekeza polisi walipo wenzake, ambao walikutwa katika hoteli moja jijini Mwanza wakiwa wamejipumzisha.
Muargentina awa Baba Mtakatifu wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini,aitwa Francis I

Ni Baba Mtakatifu wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini. Kwenye hotuba yake ya kwanza amwombea Benedict, aomba Kanisa "litembee pamoja katika imani"
Jesuit Cardinal Jorge Bergoglio wa Buenos Aires amechaguliwa kuongoza Wakatoliki billioni moja kama Papa Francis I.
Ni Baba Mtakatifu wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini. Kwenye hotuba yake ya kwanza amwombea Benedict, aomba Kanisa "litembee pamoja katika imani".
Ametoa baraka yake ya kwanza ya umma saa nne unusu EAT. Awaomba waumini wamwombee.Wachambuzi wasema Francis ni Papa "mnyenyekevu."
Dk Slaa amkumbuka Sitta

Boniface Meena na Mussa Juma, Mwananchi
Kutokana na mvutano ambao umekuwapo mara kwa mara kati ya Chadema na Spika wa Bunge, Anne Makinda, chama hicho kimemkumbuka aliyekuwa Spika wa Bunge la 10, Samuel Sitta kikieleza kuwa alikuwa hapindishi sheria na kanuni za Bunge na ndiyo maana lilikuwa limetulia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu wabunge wa chama hicho kutakiwa kuhojiwa na Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema Spika Makinda amekuwa akipindisha kanuni na ndiyo maana kumekuwa hakuna utulivu bungeni.
“Spika Sitta aliyekuwepo kabla ya Makinda alikuwa hapindishi sheria na alikuwa anajirekebisha pale anapokosea na tulikuwa tukishauriana kwamba asijihusishe na mambo ya vyama,” alisema Dk Slaa.
Alisema Sitta, ambaye hivi sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki alikuwa hafuati mambo ya vyama kwa kuwa alitakiwa kuwa ni mtu ambaye hapendelei upande wowote. Sitta, ambaye alikuwa Spika kuanzia mwaka 2005-2010, alikuwa anajinadi kwa kuendesha Bunge kwa spidi na viwango.
“Makinda aachane na ushabiki wa CCM kwani anajua kabisa kanuni ya nane inamtaka Spika asifungamane na upande wowote hivyo aache kufanya hivyo,” alisema Dk Slaa.
Alisema ni muhimu Spika akawaeleza kimaandishi amepata wapi mamlaka ya kuruhusu kamati iendelee wakati zote zilivunjika rasmi katika Bunge lililopita.
“Spika kama hajui kanuni aende shule kujifunza kuliko kututia aibu, wanasheria, wabunge wamsaidie ili aweze kuelewa.”
Dk Slaa alisema katika mabunge ya kidemokrasia, kupongeza ni jambo halali na kuzomea pia ni jambo halali hivyo kitendo cha wabunge wao kuzomea ni sawa kwa kuwa ni njia yao ya kufikisha ujumbe. Akizungumzia suala la wabunge wake kuhojiwa na kamati hiyo ya Bunge, alisema hawatakwenda kuhojiwa na kamati hiyo na kama Bunge litaamua kuwafukuza lifanye hivyo ili wananchi waelewe.
“Hawawezi kwenda kuhojiwa na kamati ambayo haipo kisheria, nilipokuwepo bungeni nilishiriki kuandaa kanuni hizi za Bunge, Spika hana mamlaka anayojipa ya kuongeza muda wa kamati, hivyo aache kulidhoofisha Bunge na badala yake alisaidie,” alisema Dk Slaa.
Akizungumzia suala hilo, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema anashangazwa na Naibu Spika, Job Ndugai kusema kuwa kuna kamati ambazo huwa zinaendelea wakati nyingine zinapokuwa zimemaliza muda wake.
Lema aitisha maandamano
Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, ametangaza kuandaa maandamano makubwa yatakayoshirikisha wanawake na watoto katika Jiji la Arusha ili kushinikiza Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Arusha (AUWSA) kuwasambazia maji.
Akizungumza jana, Lema alisema ameamua kuandaa maandamano hayo ya kudai maji kwani kwa zaidi ya miezi sita sasa asilimia 70 ya wakazi wa Jiji la Arusha hawapati maji safi.
“Nimewaandikia barua AUWSA wiki mbili sasa nikiwataka wanipe mipango yao ya muda mfupi na mrefu ya kuondoa tatizo la maji Arusha, kwani mimi kama mbunge ninaweza kushirikiana nao kupunguza tatizo hili, lakini hawajajibu sasa tutawashinikiza kwa nguvu wa umma,” alisema Lema.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa AUWSA, Mhandisi Ruth Koya hakupatikana kuelezea kama amepokea barua hiyo baada ya kutopatikana ofisini, pia simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.
Monday, 11 March 2013
Ushindi wa Kenyatta wachambuliwa

Uhuru juzi alitangazwa kuwa Rais wa nne wa Kenya, baada ya kujipatia asilimia 50.07 ya kura zote zilizopigwa, dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga, aliyepata asilimia 43.28 ya kura hizo.
Kwa mujibu wa Katiba mpya ya Kenya, mgombea wa urais, ni lazima afikishe zaidi ya asilimia 50 ya kura, masharti ambayo Uhuru aliyatimiza japo kwa asilimia 0.07.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mhadhiri wa Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana, alisema siasa za ukabila ni saratani ambayo bado inaendeleao kuitafuna Kenya na kuwa jambo hilo si zuri kwa mustakabali wa nchi hiyo.
Alisema ukabila ni vigumu kuumaliza nchini humo, na imejionesha katika uchaguzi uliomalizika, jinsi wapigakura walivyokwenda kupiga kura zao kwa kumfuata mtu na si sera na itikadi za vyama.
Kauli hiyo pia imeungwa mkono na mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Audax Kweyamba, aliyesema kuwa Kenya bado inasumbuliwa na donda la ukabila.
“Nimefuatilia sana uchaguzi wa Kenya, hata ushindi unaonesha kabisa siasa za ukabila ni tatizo jambo ambalo si zuri kwa mustakabali wa nchi hiyo,” alisema.
Ushauri Bana alisema katika kutekeleza kauli yake ya kuunda Kenya moja, ni vema Uhuru aje Tanzania kujifunza msingi ya kujenga taifa kama alivyofanya Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere.
“Uhuru kama anataka kujenga nchi yenye umoja, aje kujifunza namna ya kujenga taifa, lakini hili hawezi kumaliza peke yake, isipokuwa kwa kusaidiwa na kambi ya Odinga na Wakenya kwa ujumla.
“Kinyume chake Wakikuyu (kabila la Uhuru) na Wakalenjini (kabila la Mgombea Mwenza, William Ruto), wataendelea kuongoza kwa sababu ndio wengi na wanajitokeza kupiga kura,” alisema Dk Bana. Kweyamba yeye alishauri Uhuru ateue viongozi au mawaziri, kulingana na uwezo wao na kuzingatia sura ya utaifa ili kuondoa picha ya ukabila iliyojengeka. Asilimia 0.07?
Akizungumzia ushindi mwembamba wa Uhuru, Dk Bana alisema haijalishi, ilimradi Katiba ya Kenya iliyopitishwa na wananchi wenyewe, inaruhusu mshindi kutangazwa akiwa amefikia zaidi ya asilimia 50 ya kura.
Hata hivyo, alisema ni vema nchi za Afrika ikiwemo Tanzania inayojiandaa kupata Katiba mpya, ziangalie suala hilo katika katiba zao.
Alipendekeza Katiba ziagize uundwaji wa Serikali ya Umoja ya Kitaifa, endapo kunakuwa na kuzidiana kwa kura chache, ili kuondoa manung’uniko kwa walioshindwa.
“Katika hali ya kawaida, ukishindwa kwa tofauti ndogo huamini matokeo, lakini hili linaweza kumalizwa kwa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kinyume chake kiongozi aliyeshinda, atatawala kwa nguvu ya dola kutokana na sehemu kubwa kumpinga,” alisema.
Naye Kweyamba alisema jambo la msingi ni hiyo asilimia 0.07 iliyompa Uhuru ushindi, iwe imetokana na Tume kuendesha uchaguzi huru na wa haki na imepatikana kihalali.
Wapigakura Kweyamba alisema Kenya imevunja rekodi ya idadi kubwa ya wapiga kura kujitokeza kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi, kwa kile kinachoonekana ni kuwa na matumaini mapya baada ya vurugu zilizotokea mwaka 2007.
“Tuombe Mungu, mambo yote yaishe salama na Kenya iwe salama, kwani endapo kutatokea machafuko, kuna hatari ya kushusha morali ya wananchi, ambao wamejitoa kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi,” alisema Kweyamba.
Alisema, Watanzania wanatakiwa kujifunza namna ya kutumia haki ya kuchagua vongozi, na kuachana na tabia ya kuona kuwa hawana haja ya kushiriki kwenye uchaguzi.
Alisema asilimia 42.8 zilizofikiwa mwaka 2010 haikuwa idadi nzuri. Naye Dk Bana alisema hiyo ni hatua nzuri, ambayo inaonekana imechangiwa na vyama siasa vya Kenya kutoa hamasa kwa wananchi na jinsi Serikali ilivyofanya kazi ya kutoa elimu ya uchaguzi kwa wananchi wake.
Mauaji ya albino yaichafua Tanzania

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim alisema jana jijini Dar es Salaam kwamba, licha ya Tanzania kuonyesha mafanikio katika utawala bora, bado maeneo hayo yanahitaji nguvu za ziada.
Mahadhi alisema hayo wakati wa kuadhimisha Siku ya APRM ikiwa ni miaka 10 tangu ilipoanzishwa.
“Ripoti ya APRM iliwasilishwa na Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wa wakuu wa nchi za Kiafrika na kusifiwa sana,” alisema.
Alisema kuna mambo machache yalijitokeza na yanayoharibu jina la Tanzania na watu wake.
Alisema kukithiri kwa rushwa ni sehemu ambayo ilitia doa katika ripoti hiyo na kwamba inahitaji kufanyiwa kazi.
“Tunahitaji kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Tume ya Maadili ya Viongozi ili kuondokana na kasoro hizo,” alisema Mahadhi.
Aidha alisema eneo la haki za binadamu nalo lilitia doa katika ripoti hiyo hasa mauaji ya walemavu wa ngozi (albino).
Uchaguzi Mkuu Kenya: Ghasia zaanza Kisumu

Nairobi: Polisi wa kutuliza ghasia juzi walilazimika kutumia mabomu ya machozi Mjini Kisumu kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakipinga kutangazwa kwa matokeo ya urais ambayo mgombea wao, Raila Odinga alianguka.
Vurugu hizo ziliibuka, baada ya kutangazwa kwa matokeo ya urais yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta.
Maelfu ya vijana wamekuwa wakirandaranda kwenye maeneo kadhaa ya Kisumu wakichoma majengo na kufunga barabara, huku wakiimba: “Bila Raila, hakuna amani.”
Vurugu hizo zilizoanza juzi jioni zimesababisha maduka kufungwa huku makundi ya vijana wenye hasira wakiendelea kurandaranda mitaani wakipambana na polisi ambao walifanya jitihada za kuwatuliza na kurejesha amani.
Ilielezwa kwamba, muda mfupi tu baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumtangaza Kenyatta kuwa mshindi, zaidi ya vijana 100 waliibuka na kuanza kuwarushia mawe polisi na muda mfupi baadaye idadi ya vijana hao iliongezeka na kusambaa katika maeneo karibu yote ya Kisumu.
Odinga ambaye alikuwa mgombea wa Muungano wa Cord, amewataka wafuasi wake kuwa watulivu kwa kuwa anahitaji kufuata mkondo wa sheria kupinga matokeo hayo.
Matokeo hayo yaliyotangazwa juzi, yalimpa ushindi Kenyatta aliyesimama kwa tiketi ya Muungano wa Jubilee, wa asilimia 50.07 dhidi ya asilimia 43 alizopata Raila.
Raila atinga mahakamani
Muungano wa Cord, leo utawasilisha vielelezo mahakamani kupinga ushindi wa Kenyatta.
Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Kenya, Amos Wako ametajwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa jopo la wanasheria watakaopinga ushindi wa Kenyatta.
Jopo hilo la wanasheria linaongozwa na mwanasheria mkongwe, George Oraro na baadhi ya mawaziri wakiwamo; Mutula Kilonzo, James Orengo na Ababu Namwamba ambao ni washauri wakuu wa jopo.
Oraro alimtetea aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Henry Kosgei wakati alipokabiliwa na kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC, The Hague.
Wengine wanaounda timu hiyo ni Gitobu Imanyara, Pheroze Nowrojee, Chacha Odera, Ambrose Rachier na Paul Mwangi.
Cord imepanga kufungua kesi ikitaka Mahakama itengue hatua ya kutangazwa kwa Kenyatta kuwa Rais wa Kenya kwa kuwa taratibu za ukusanyaji matokeo zilikiukwa.
Tangu juzi, jopo hilo la wanasheria lilikuwa na vikao mfululizo kuandaa ushahidi wa kesi hiyo ikiwamo kukusanya vielelezo watakavyosimamia katika kesi hiyo kwa mujibu wa Kifungu namba 163 cha Katiba ya Kenya.
Mfuasi wa Uhuru afariki
Shamrashamra za kushangilia ushindi wa Kenyatta ziliingia doa kwenye Mji wa Nyeri baada ya lori lililobeba mashabiki wa mgombea huyo kutumbukia kwenye korongo na kuua mtu mmoja. Katika ajali hiyo watu 30 walijeruhiwa lakini wakiwa katika hali mbaya.
Mwili wa mtu aliyefariki ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Nyeri wakati wengine waliojeruhiwa wamelazwa kwenye hospitali hiyo.
Lori hilo lilikuwa likienda maeneo ya Giakanja kwa ajili ya kukusanya mashabiki wengine na kuanza safari ya kuzunguka mitaa ya mji huo kushangilia ushindi. Kamanda wa Polisi Nyeri, Kirunya Limbitu alithibitisha ajali hiyo na kusema lori hilo lilikuwa kwenye mwendokasi na kupoteza mwelekeo kabla ya kutumbukia kwenye korongo na kupinduka.
Subscribe to:
Comments (Atom)