Monday, 11 March 2013

Mauaji ya albino yaichafua Tanzania


Mpango wa Afrika wa Kutathmini Utawala Bora (APRM), umebaini kwamba rushwa na ukiukaji wa haki za binadamu ni tatizo kubwa nchini linalohitaji kufanyiwa kazi ili kuimarisha utawala bora.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim alisema jana jijini Dar es Salaam kwamba, licha ya Tanzania kuonyesha mafanikio katika utawala bora, bado maeneo hayo yanahitaji nguvu za ziada.

Mahadhi alisema hayo wakati wa kuadhimisha Siku ya APRM ikiwa ni miaka 10 tangu ilipoanzishwa.

“Ripoti ya APRM iliwasilishwa na Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wa wakuu wa nchi za Kiafrika na kusifiwa sana,” alisema.

Alisema kuna mambo machache yalijitokeza na yanayoharibu jina la Tanzania na watu wake.
Alisema kukithiri kwa rushwa ni sehemu ambayo ilitia doa katika ripoti hiyo na kwamba inahitaji kufanyiwa kazi.

“Tunahitaji kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Tume ya Maadili ya Viongozi ili kuondokana na kasoro hizo,” alisema Mahadhi.
Aidha alisema eneo la haki za binadamu nalo lilitia doa katika ripoti hiyo hasa mauaji ya walemavu wa ngozi (albino).

No comments: