Thursday, 28 February 2013

PSI: Tumezuia mimba milioni 1.2 zisizotarajiwa



Mtung’e alisema kifurushi hicho kitakuwa na vifaa vyote vitakavyohitajika kwa mjamzito kujifungua salama ambavyo alivitaja baadhi kuwa ni jozi mbili za glovu, nyuzi mbili, pamba, shuka kwa ajili ya matumizi ya mara moja, kitambaa cha joto cha mtoto, dawa ya kusafishia mikono, vidonge vitatu vya kuzuia mama kutokwa na damu nyingi.


SHIRIKA lisilo la kiserikali la PSI limesema kwamba limefanikiwa kuzuia mimba zisizotarajiwa 1.2 milioni mwaka uliopita.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, Mkurugenzi wa Afya ya Uzazi wa shirika hilo, Dk Nguke Mwakatundu alisema hiyo ilitokana na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa mkakati wake wa kutoa huduma za uzazi wa mpango nchini.

“Tumefanikiwa kutokana na kutoa huduma za uzazi zaidi ya matumizi ya kondomu. Ukiangalia tangu shirika lilipoanzishwa miaka 20 iliyopita, matumizi ya kondomu yalikuwa yakitumika zaidi. Lakini sasa njia hiyo imepita na nyingine kama lupu, vipandikizi, vidonge na sindano ambazo matumizi yake yameongezeka maradufu,” alisema.

Alisema katika mwaka wa jana, njia za muda mrefu za uzazi wa mpango zilitolewa kwa watu 102,772 ikilinganishwa na watu 48,518 mwaka uliotangulia ikiwa ni ongezeko la asilimia 92.
Alisema mafanikio hayo yametokana na mkakati wa shirika hilo kupanua wigo wake wa kusambaza huduma za afya katika maeneo ya mbali...

“Tumeongeza utoaji wa huduma katika sekta ya umma kwa asilimia 145. Kitu kikubwa tulichofanya ni kuongeza timu ya watoa huduma katika maeneo hayo kutoka tano hadi 10 na kila timu ina wauguzi wawili.”

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa PSI Tanzania, Romanus Mtung’e alisema katika kuhakikisha kwamba utoaji huo wa huduma unakuwa salama, shirika lake linaandaa Kifurushi Salama kwa ajili ya Kujifungua (Clean Delivery Pack), kitakachoanza kusambazwa Aprili mwaka huu.

Mtung’e alisema kifurushi hicho kitakuwa na vifaa vyote vitakavyohitajika kwa mjamzito kujifungua salama ambavyo alivitaja baadhi kuwa ni jozi mbili za glovu, nyuzi mbili, pamba, shuka kwa ajili ya matumizi ya mara moja, kitambaa cha joto cha mtoto, dawa ya kusafishia mikono, vidonge vitatu vya kuzuia mama kutokwa na damu nyingi.

Alisema lengo la shirika lake siyo kupunguza idadi ya watu kama ambavyo imekuwa ikitafsiriwa na wengi, bali kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili watu wapate watoto kwa mpangilio utakaowawezesha kuwatunza na kuwahudumia vyema na wao kupata fursa ya kushiriki katika masuala ya kiuchumi.

Ole Sendeka ahojiwa na timu ya Mangula





MBUNGE wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na vigogo kadhaa wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara, wamehojiwa na maofisa wa CCM, kuhusiana na malalamiko ya ukiukwaji wa taratibu katika uchaguzi wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa ya chama hicho (Nec) wa wilaya hiyo.


Hatua hiyo ni utekelezaji wa mikakati ya Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Phillip Mangula, ambaye aliahidi kushughulikia malalamiko yote ya chaguzi zilizopita na kuyatolea uamuzi. Mangula ndiye Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Maadili ya CCM.


Kuhojiwa kwa Sendeka na viongozi wengine wa Simanjiro, kumekuja siku chache baada ya kuhojiwa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary Nagu ambaye pia ushindi wake wa Nec Wilaya ya Hanang, ulilalamikiwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye akisema kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu na kanuni za uchaguzi wakati wa kinyang’anyiro hicho.


Katika uchaguzi wa Simanjiro, Sendeka alishinda kwa kupata kura 471 dhidi ya Diwani wa CCM Kata ya Mirerani, Justin Nyari ambaye alipata kura 126.


Maofisa hao kutoka Makao Makuu ya CCM, wakiongozwa na Mwanasheria wa CCM, Glorius Luoga waliwahoji Sendeka na Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Jamillah Mujungu, Nyari na viongozi wengine wa chama hicho.


Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika wikiendi iliyopita, zimebainisha kuwa Nyari na makada kadhaa wa CCM, wanalalamikia ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi huo, ikiwamo kufanyika kwa kampeni kinyume cha taratibu kama kutawaliwa na ukabila, pia baadhi ya wapigakura kutokuwa halali.


Hata hivyo, Luoga ambaye pia ni Mjumbe wa Nec anayetoka Songea Vijijini, alipotakiwa kuelezea hatma ya malalamiko hayo, hakutaka kufafanua kwa maelezo kuwa yupo Zanzibar.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Manyara, Ndekubali Ndeng’aso alikiri kufika kwa maofisa wa makao makuu ya chama hicho mkoani hapo na kuhojiana na walalamikaji na walilalamikiwa.


“Nadhani hizi ni taratibu za kawaida tu ndani ya chama, kuna ambao wamelalamika sasa chama kimeona ni busara kuwafuata na kujua malalamiko yao,” alisema Ndeng’aso.
Sendeka na Nyari hawakupatikana jana kuelezea kilichojiri katika mahojiano hayo kwani simu zao za mkononi ziliita bila ya kupokewa.


Hata hivyo, Mujungu licha ya kukiri kuhojiwa alisema wenye mamlaka ya kuzungumza ni maofisa hao wa makao makuu... “Hili jambo lipo ngazi za juu nadhani wao ndiyo wana majibu ya maswali yenu.”

Papa wawili katika mgongano wa kimadaraka




YAMETIMIA. Safari ya miaka saba ya Baba Mtakatifu Benedict XVI inakamilika leo pale atakapong’atuka rasmi katika uongozi wa Kanisa Katoliki, ifikapo saa 2:00 usiku kwa saa za Italia (saa 4:00 usiku kwa saa za Tanzania).


Kwa siku mbili, Papa amekuwa na shughuli nyingi katika makao yake, Gandolfo Castel, Vatican akijiandaa kimwili kuondoka, akiweka sawa nyaraka zake binafsi na zile za kanisa ambazo zitawekwa katika kumbukumbu.


Kwa upande mwingine Vatican, nchi ambayo ipo ndani ya Jiji la Rome iliyozungukwa na ukuta, ikiwa na ukubwa wa hekta 44 na wakazi 832 pekee, imekuwa katika hekaheka nyingi.
Jana, waumini zaidi ya 50,000 na wengine wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiwamo makardinali, maaskofu, mapadri na walei walialikwa kwa shughuli rasmi ya kumuaga kiongozi huyo.


Tofauti na kanuni yake, leo Benedict hatavaa viatu vyekundu kama ilivyozoeleka na badala yake amechagua viatu rahisi vya ngozi vilivyobuniwa Mexico. Alipewa viatu hivyo ikiwa ni zawadi wakati wa ziara nchini humo 2012.


Tangu alipotangaza uamuzi wake wa kung’atuka Februari 11, mwaka huu, utata umegubika nafasi yake katika maisha mapya ndani ya Vatican, akiitwa Papa Mstaafu.


Waumini, wataalamu na hata viongozi mbalimbali wa Kikatoliki wameanza kuhoji ni jinsi gani viongozi wawili (Papa) wataishi, huku wote wakivaa mavazi meupe wakiitwa Papa, wakiishi umbali mdogo kati yao, wakiwa na wasaidizi wengi wanaowahudumia.

Vatican
Nje ya Gandolfo Castel, ulinzi umeimarishwa na vibali vya kuingia Vatican vimesitishwa.
Juzi, Vatican ilitangaza kwamba Papa Benedict XVI atajulikana kama ‘Emeritus Pope’, yaani Papa Mstaafu mwenye cheo cha heshima, akiendelea kuitwa, ‘mtakatifu’ na ambaye ataendelea kuvaa nguo nyeupe.


Mavazi na hata jina lake jipya ni masuala ambayo yamezua uvumi mwingi, huku suala la mrithi wake mpya pia likiwa gumzo, kwani tukio kama hilo lilitokea miaka 600 iliyopita.
Ni uamuzi uliolishtua kanisa hilo lenye waumini 1.2 bilioni duniani na wengi wanasema awali, haikushauriwa Papa kustaafu kwani kwa kufanya hivyo kunaacha mizozo na minong’ono ya kuwania madaraka.


Hata hivyo, uongozi wa Vatican umesisitiza kuwa uamuzi huo wa Papa Benedict XVI ni wa kipekee na hakuna mzozo ambao utatokea baina yake na mrithi wake ambaye mchakato wa kumpata unatarajiwa kuanza ndani ya wiki mbili zijazo.


“Kulingana na mabadiliko katika kanisa letu, kuna Papa mmoja. Ni dhahiri kwamba katika hali ya sasa hakutakuwa na tatizo,” anasema Mhariri wa Gazeti la L’Oservatore Romano linalomilikiwa na Vatican, Giovanni Maria Vian.

Hofu iliyopo
Hata hivyo, wakosoaji wa mambo hawakubaliani na hoja hiyo na baadhi ya makardinali walioko Vatican kwa usiri mwingi, wanazungumzia suala hilo wakieleza kwamba litazua tatizo kubwa kwa Papa ajaye, hasa ikiwa mtangulizi wake, Benedict akiwa bado hai.


Mtaalamu wa tauhidi (theolojia), raia wa Uswisi, Hans Kueng ambaye amekuwa mtu wa karibu wa Papa Benedict XVI, ingawa kwa sasa ni mkosoaji wake amesema:
“Kwa sasa, Benedict XVI akiwa bado hai, kuna hatari ya kuwa na Papa kivuli, mwenye mamlaka kamili ambaye kwa chinichini anaweza kumshinikiza mrithi wake kufikia uamuzi.”
Hans Kueng alisema hayo alipozungumza na Gazeti la Der Spiegel la Ujerumani.


Msemaji wa Vatican, Padri Federico Lombardi alisema Papa Benedict XVI kwa upande wake aliamua aitwe Papa Mstaafu au ‘kiongozi mstaafu wa Roma.’ Anasema haelewi ni kwa nini ameamua kuacha jina lake la sasa la Askofu wa Rome.


Kwa wiki mbili zilizopita, maofisa mbalimbali wa Vatican wamekuwa wakifikiri kwamba Papa angeanza kuvaa mavazi meusi na kutumia jina la Askofu Mstaafu wa Rome ili kuepuka mkanganyiko na mrithi wake.
Mwingine ambaye amekuwa akizusha mkanganyiko ni Katibu wa Papa, Askofu Mkuu, George Gaenswein ambaye ataendelea kuwatumikia Papa wote wawili, yaani Benedict XVI kwenye Monasteri ndani ya Vatican na kazi yake ya kawaida ya kuwa kiranja katika nyumba ya Papa mpya.


Kwa upande wake, Papa Benedict XVI anasema anastaafu na sasa ataishi maisha ya sala na tafakuri ya kina, mbali na majukumu mengine ya kidunia.
Hata hivyo, bado atakuwapo kwenye nchi ndogo ya Vatican, mahali ambako makazi yake yatakuwa jirani na mnara wa kurushia matangazo wa Kituo cha Redio cha Vatican, akiliangalia vizuri Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.


Kwa upande wake, Kueng anasema ni kosa kwa Askofu Gaenswein kuwatumikia Papa wawili kwa wakati mmoja na pia Benedict XVI kubakia jirani na mahali hapo.
“Hakuna padri ambaye anapenda mtangulizi wake kuishi karibu naye na kufuatilia anayoyafanya.


Hata kama Askofu wa Rome, haipendezi kutenda kazi huku mtangulizi wako akiona na kufuatilia.”
Mbali na mitazamo hiyo, wengine wamedhani kuwa uamuzi wa Papa Benedict XVI unalenga kudumisha utamaduni wa watangulizi wake.


“Ninashangazwa kuona Papa Benedict XVI akiendelea kuitwa mbarikiwa na kuvaa nguo nyeupe,” anasema Padri James Martin, Mtawa wa Jesuit pia mwandishi na mhariri, lakini baadaye anajirudi na kusema:
“Lakini sioni ajabu, mbona marais wastaafu wa Marekani, bado wanaitwa Rais? ni alama ya heshima kwake.”


Katika mkanganyiko huo, wapo wanaoamini kwamba yanayotokea yanatokana na nguvu ya roho mtakatifu, huku wengine wakipiga upatu kwamba ni zamu ya Afrika kutoa Papa na wanatajwa Makardinali Peter Turkson wa Ghana na Francis Arinze wa Nigeria.

Mtanzania apewa uwaziri Rwanda

Sura nyingine mpya katika Baraza hilo ambalo liliapishwa juzi Ikulu ya Rwanda ni pamoja na Seraphine Mukantabana (Wakimbizi na

RAIS Paul Kagame wa Rwanda amemteua Mtanzania, Profesa Silas Rwakabamba kuwa Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika Jumatatu iliyopita.


Kabla ya uteuzi huo, Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda. Ni mmoja wa mawaziri wanaoingiza sura mpya katika Baraza la Rais Kagame ambalo amelifanyia mabadiliko kwa kuunda wizara nyingine mpya.


Sura nyingine mpya katika Baraza hilo ambalo liliapishwa juzi Ikulu ya Rwanda ni pamoja na Seraphine Mukantabana (Wakimbizi na Menejimenti ya Maafa) na Oda Gasinzigwa (Ofisi ya Waziri Mkuu- Familia na Jinsia).


Akizungumza kwa simu na mwandishi wetu jana, mdogo wa Profesa Rwakabamba, Timothy Rwamushaija anayeishi Dar es Salaam, alisema ndugu yake alizaliwa katika Kijiji cha Bushagara, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.


Alisema Profesa Rwakabamba alikuwa Mtanzania aliyeamua kuchukua uraia wa Rwanda na wote baba yao ni Mzee Titus Rwamushaija... “Huyu ni kaka yangu wa tumbo moja na kwa kweli tumefurahi sana kwa mafanikio yake sisi kama wanafamilia.”


Naibu Makamu Mkuu - Taaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Profesa Makenya Maboko alisema Profesa Rwakabamba alifanya kazi katika chuo hicho na aliondoka akiwa Mkuu wa Kitivo cha Uhandisi.


“Aliondoka wakati Kagame alipoingia madarakani na alikwenda kuongoza Taasisi ya Teknolojia ya Kigali (KIST) kabla ya kwenda katika Chuo Kikuu cha Kigali,” alisema Profesa Maboko.


Msomi huyo alikwenda Rwanda mwaka 1997, baada ya kuombwa na Rais Kagame ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya wahadhiri kwenda Kigali kufungua chuo kikuu katika taifa lake baada ya kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.


Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa kwanza wa KIST na kukifanya kuwa miongoni mwa vyuo bora barani Afrika kwa masuala ya teknolojia jambo lililomfurahisha Rais Kagame.


Baada ya mafanikio hayo, Rais Kagame alimteua kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda, Butare ambako pia alijizolea sifa baada ya kusimamia vyema ujenzi wa mabweni kwa wingi na kiongozi huyo alimtunukia uraia wa nchi hiyo kama zawadi.


Hata hivyo, Profesa Rwakabamba atakuwa amelazimika kuukana uraia wa Tanzania kwa kuwa katiba ya nchi hairuhusu uraia wa nchi mbili.
Profesa Rwakabamba alipata elimu ya msingi huko Muleba na akajiunga na Shule ya Sekondari ya Ihungo.


Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza na kupata Shahada ya Uhandisi mwaka 1971 na 1975 alipata Shahada ya Uzamivu katika fani hiyohiyo.


Wednesday, 27 February 2013

Pinda: Hatukukosea kuunda tume *Asema lengo ni kubaini kiini cha tatizo


WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amesema tume iliyoiunda ili kuchunguza matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa Februari 18 mwaka huu, itaanza kazi siku mbili au tatu zijazo.


Bw. Pinda aliyasema hayo Dar es salaam jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua ni lini
tume hiyo itaanza kazi na kuongeza kuwa, pamoja na watu
kuipinga, Serikali haikukosea kuiunda ili ifanye uchunguzi
wa kina kubaini kiini cha tatizo.

“Yanayosemwa ni mengi...wapo wanaosema tatizo linajulikana, jambo ambalo si kweli hivyo lazima tume ichunguze ili kujua mkweli na muongo,” alisema Bw. Pinda.

Aliongeza kuwa, tume hiyo pia itachunguza maeneo mengine
yenye utata mkubwa ili kuona jambo hilo halitokei tena.

Hivi karibuni, Bw. Pinda aliunda tume itakayochunguza sababu
ya matokeo mabaya kwa wanafunzi wengi waliofanya mtihani
wa kidato cha nne mwaka 2012.

Asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo walipata sifuri ambapo tume hiyo itajumuisha Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi, Chama cha Walimu nchini (CWT), Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari nchin

Waziri Muhongo akataa chakula hotelini aenda kwa mamalishe



Nipelekeni mahali nitakapopata chakula cha Kitanzania, ili tuwe sawa na Watanzania wenye hali ya chini kwani hizi fedha tunazokwenda kula huko ni jasho lao.”

Arusha
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amekataa chakula Hoteli ya Mount Meru na kwenda kula chakula cha Mamalishe.
Tukio hilo lililowashangaza watu 13 waliokuwa katika msafara wake lilitokea hivi karibu wakati

Profesa Muhongo alipokwenda Arusha kwenye mkutano wa wataalamu wa umeme wa nchi 11 za Afrika Mashariki, Kati na Kaskazini.

Waziri Muhongo aliandaliwa chakula hotelini hapo, lakini aliwashangaza wenyeji wake ambao ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na uongozi wa wizara yake.

Baada ya kufika katika mgahawa wa Pizza Point uliopo katikati ya mji wa Arusha, Waziri Muhongo aliagiza ugali na samaki kwa bei ya Sh7,000.

Tukio la waziri huyo kukataa kula chakula cha usiku katika hoteli hiyo ya kifahari, iliwashangaza hata wafanyakazi wa mgahawa huo baada ya kupata taarifa hiyo.
Ingawa haikufahamika mara moja sababu za waziri huyo kukataa kula katika hoteli hiyo kutokana na kuchukua uamuzi ghafla, lakini taarifa za ndani zinadai hakutaka kutumia fedha za walipa kodi kwa matumizi binafsi.

“Waziri aliandaliwa chakula katika Hoteli ya Mount Meru Arusha na mpaka tunatoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), ilijulikana tunakwenda kwenye hoteli hiyo lakini chakushangaza alipofika karibu na geti la kuingia hapo, akabadili uamuzi na kuamuru apelekwe mahali atakapopata chakula cha Kitanzania, huku akisema haoni sababu ya kula vyakula vya bei mbaya wakati kuna Watanzania hawana umeme,” alisema ofisa mmoja wa wizara hiyo ambaye hakutaka kutajwa na kumkariri Waziri Muhongo:

“Nipelekeni mahali nitakapopata chakula cha Kitanzania, ili tuwe sawa na Watanzania wenye hali ya chini kwani hizi fedha tunazokwenda kula huko ni jasho lao.”

Hata hivyo, Profesa Muhongo anadaiwa kuruhusu maofisa waliokuwa kwenye msafara wake ambao wangependa kula Mount Meru kuwashusha, ili akitoka kwa mamalishe awapitie kwa sababu kila mtu ana uamuzi wake.

Msafara wa waziri huyo ulikuwa na watu 13 akiwamo Msaidizi wake na Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud ambao wote walilazimika kula chakula katika banda la Pizza Point.

Mmiliki wa mgahawa huo, Grace Lyatuu alisema hakutarajia ujio wa waziri huyo na msafara wake, lakini baada ya kutambua kuwa ni Profesa Muhongo akamshukuru Mungu kwa kumfikisha hapo.

“Kwakweli ilikuwa ni usiku mgumu kwangu, kwani msafara ulikuwa mkubwa na wagafla, sikuwa na uhakika wa kupata vyakula vya kuwatosha lakini baada ya chakula kupatikana nikamshukuru Mungu kwani ilikuwa ni usiku na tulikuwa na maandalizi ya kufunga mgahawa,” alisema Lyatuu.

Profesa Muhongo alitumia Sh100,000 kwa chakula cha watu 13 na vinywaji na kuokoa zaidi ya Sh344,500.

Vigogo 10 wahusishwa mabilioni ya Uswisi


ZITTO ASISITIZA NYARAKA ZIPO, DK HOSEAH NDIYE ANAYEZIZUIA

VIGOGO 10 wametajwa kuhusika katika kashfa ya kuficha Sh303.7 bilioni katika benki mbalimbali nchini Uswisi.
Katika orodha hiyo inadaiwa kuwa yupo kiongozi mmoja mwandamizi mstaafu, maofisa watatu wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mawaziri wastaafu ambao baadhi yao bado ni wabunge na aliyewahi kuwa kiongozi mwandamizi wa Benki Kuu Tanzania (BoT).
Majina hayo ambayo mwandishi wetu amefanikiwa kuyaona, yamo katika orodha ya mchunguzi mmoja wa kimataifa wa masuala ya ufisadi (jina tunalo).
Juzi, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alimshukia Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah akimtuhumu kuandika barua Uswisi akisema Tanzania haina masilahi na mabilioni ya fedha yaliyofichwa katika benki zilizopo nchini humo. Hata hivyo, Dk Hoseah alikanusha madai hayo akisema hajawahi kufanya hivyo.
Akizungumza jana Zitto alisisitiza kauli yake akisema: “Sijawahi kumsema Dk Hoseah kwa lolote, kwa nini leo nimsingizie? Yeye mwenyewe anajua ushirikiano niliompa wakati wabunge wanapinga yeye asichunguze malipo ya posho mara mbili kwa wabunge.”
“Nilisimama kidete kusema Takukuru wapo sahihi na mimi nilikwenda mwenyewe kwao kuhojiwa na kuagiza wajumbe wa kamati yangu (Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma), waende kuhojiwa. Spika aliyestaafu (Samuel Sitta) akaizima kashfa ya wabunge kupokea posho mara mbilimbili. Mwulizeni amesahau? Sasa leo nimzushie ili iwe nini?.”
Alisema orodha ya Watanzania wenye fedha huko Uswisi, ipo na ameiona na nyaraka zinaweza kutolewa kwa taasisi za Serikali tu.
“Dk Hoseah kazuia nyaraka hizo. Akitaka nimwonyeshe mtu anayeweza kutoa nyaraka hizo, nipo tayari isipokuwa aahidi kuiweka wazi,” alisema Zitto.
Alisema katika orodha ambayo Waziri wa Fedha wa Ufaransa anayo, kuna Watanzania lakini akaituhumu Serikali akisema haitaki kufuata njia halali za kupata orodha hiyo kwa kuwa viongozi wengi na wafanyabiashara wakubwa wana akaunti katika benki za Uswisi.
Juni 26, mwaka huu gazeti hili lilichapisha habari kuhusu utoroshwaji wa fedha hizo na kueleza kuwa Polisi wa Kimataifa (Interpol) nchini kwa kushirikiana na Takukuru inachunguza suala hilo.
Kiasi hicho cha fedha kimedaiwa kuingizwa katika akaunti za Watanzania na kampuni moja ya uchimbaji mafuta na kampuni kadhaa za uchimbaji madini ambazo zinafanya kazi Tanzania.
Chanzo hicho kiliongeza kwamba kiasi hicho cha fedha kipo katika akaunti sita tofauti zinazomilikiwa na Watanzania wakiwamo wanasiasa wakubwa.
Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa tangu akaunti hizo zifunguliwe, wamiliki wake halali hawajawahi kuingiza hata shilingi.
“Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa fedha hizo zipo katika akaunti sita tofauti ambazo zinamilikiwa na wanasiasa wakubwa nchini na wenzetu wa Uswisi wameeleza fedha hizo zimeingizwa na kampuni kadhaa ambazo zinahusika na mafuta pamoja na madini hapa nchini,” kilidokeza chanzo hicho.
Kugundulika kwa kiasi hicho cha fedha katika benki za Uswisi ni kutokana na ripoti ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB) iliyotolewa mwaka huu.

Urais 2015: Utafiti wa Synovate wapondwa,wadau wadai una ajenda ya siri: Huko tuseme ni kuiogopa Cadema??




BAADHI ya wasomi nchini wameuponda utafiti uliofanywa na Shirika la Synovate huku miongoni mwao wakienda mbali zaidi kwa kusema: “Ulikuwa na ajenda ya siri.”


Utafiti huo pia umepondwa na wanasiasa akiwamo Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye amesema haziamini tafiti zinazotolewa na Syonovate akidai hazina ukweli wowote.


Licha ya matokeo ya utafiti huo wa Desemba mwaka jana kuonyesha kushuka kwa asilimia 25 kwa umaarufu wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa pamoja na chama chake, lakini unaweka wazi kwamba kiongozi huyu angechaguliwa kuwa Rais kama uchaguzi huo ungefanyika sasa.


Dk Slaa anaongoza kwa asilimia 17, akifuatiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.


Katika maoni yao, baadhi ya wasomi kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini walieleza wasiwasi wao kuhusu usahihi wa matokeo hayo na kuhoji mbinu zilizotumika wakisema inawezekana hazikuwa sahihi.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo ameuponda akisema haukufuata misingi ya sayansi ya siasa.


Dk Makulilo alisema alifanya utafiti kwa kampuni zinazofanya tafiti kama hizo kati ya mwaka 2010 hadi 2011 na kugundua udhaifu mkubwa katika kampuni hizo.


“Kwanza wanakosea, kwa mfano wanaposema kuwa utafiti huu ni mwendelezo wa ule uliofanyika Desemba 5 hadi 18, 2011. Ukichunguza utakuta data hizo hazipo. Zilizopo ni za Mei 2 hadi 19, 2011.”


“Kwa kawaida uelewa wa wananchi wa vijijini ni mdogo ukilinganisha na mijini kwa sababu mijini kuna vyombo vya habari. Kwa mfano, ukiangalia swali la nani anafaa kuwa Rais, mwaka 2011 walisema Dk Wilbrod Slaa alikuwa na asilimia 42, lakini sasa ana asilimia 17.


Vijijini wengi bado wanaikubali CCM kutokana na uelewa mdogo, iweje Dk Slaa ambaye chama chake hakina wafuasi wengi vijijini ashinde?” alihoji.


“Utafiti wa Synovate una dosari kubwa kisayansi, hauonyeshi tarehe wala wapi umefanyika. Waliohojiwa wameonyeshwa umri wao, lakini hawaelezwi maoni yao kulingana na umri, jinsia, wanatoka vijijini na mijini. Nilipofanya utafiti wangu niliwafuata wakakimbia…” alisema Dk Makulilo.


Mhadhiri mwingine wa UDSM, Profesa Gaudence Mpangala alisema nyakati za kuelekea Uchaguzi Mkuu, tafiti nyingi hufanyika zikiwa na malengo ya kubeba watu au chama fulani.


Hata hivyo, alisema kilichofanywa na Synovate ni utafiti hivyo kwa kuwa yeye hajafanya utafiti ni vigumu kuupinga moja kwa moja... “Ila kwa mtizamo wa kawaida unatia shaka.”

Alisema kitendo cha utafiti huo kuonyesha kuwa CCM inakubalika zaidi kuliko Chadema kwa sababu kwa siku za karibuni chama hicho kimekuwa kikizungumzia zaidi mambo ya kitaifa, pia kunampa shaka.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Dk Clavery Tungaraza alisema tafiti zinazofanywa na Synovate ni mara nyingi matokeo yake huwa hayaakisi uhalisia wa maisha.


Dk Tungaraza alisema utafiti wa Sayansi ya Jamii ndiyo wenye kuaminika zaidi kutokana na kutobadilikabadilika tofauti na tafiti za Synovate ambazo hutegemea mtu aliyehojiwa yuko katika hali gani kwa wakati huo.


Msomi huyo alieleza kushangazwa na tafiti za taasisi hiyo ambazo alidai kuwa mara nyingi hufanywa wakati nchi inapojiandaa kuingia kwenye uchaguzi akisema ingekuwa ni uungwana kama zingekuwa zinafanywa kila mwaka ili kujiridhisha na uhalali wa matokeo yake.


Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Baraka Nafari alisema ana shaka na utafiti huo na kudai kwamba inawezekana umefanywa kwa lengo la kumsafisha mtu fulani.


Alisema kwa kawaida matokeo ya utafiti uliofuata kanuni na taratibu zote, unatakiwa mwingine akiufanya mara 100, apate majibu kama yale ya utafiti wa awali mara 95.


“Hiyo inaitwa confidence level, (namna ya kujiaminisha, kuwa na imani na majibu). Kwa mfano, wanasema Watanzania hawaoni kuwa rushwa ni tatizo, wakati ukweli kwetu sisi rushwa ni janga, kuna shirika moja la kimataifa lilitaja nchi zenye rushwa Tanzania ikawa kwenye nafasi za juu sana,” alisema.


Kutokana na hali hiyo, alisema utafiti huo unaonekana kama chumba maalumu cha kuwasafisha baadhi ya watu na vyama vyao badala ya kusimamia kwenye ukweli... “Nautilia shaka kama uliandikwa kwa kuzingatia vigezo na siyo kwa lengo mahususi.”


Mhadhiri wa Chuo cha Mipango Dodoma, Dk Mark Msaki alisema kinachomtatiza ni kutoainishwa njia zilizotumika katika kufanya utafiti huo.


“Sikatai wala kukubali utafiti huu, lakini kwa kuwa ni jukumu la taasisi hizo kufanya tafiti nchini, zitekeleze hayo kwa kuzingatia haki kwa Watanzania wote na si vinginevyo,” alisema.


Dk Msaki pia alisema haridhishwi na taasisi za kisayansi kujikita katika kutafiti nani ana nafasi gani katika kupata urais wa Tanzania, huku nchi ikikabiliwa na changamoto nyingi zinazogusa moja kwa moja maendeleo ya jamii.


Alisema anaamini kuwa kitendo cha taasisi hizo kuibuka na tafiti zinazohusu urais, huku Uchaguzi Mkuu ukiwa bado takriban miaka miwili, ni ishara taasisi hizo kuhusika moja kwa moja katika kugeuza siasa ya Tanzania mchezo wa mpira wa miguu.

Wanasiasa wang’aka
Profesa Lipumba alisema: “Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Synovate walitoa utafiti ulioonyesha kwamba asilimia 94 ya Watanzania wako tayari kupiga kura lakini baadaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilitoa takwimu zake zilizoonyesha kuwa waliopiga kura walikuwa asilimia 42 tu.”


“Inawezekana hata hao waliotoa utafiti huo wakawa wanamtengenezea mtu fulani njia tu kwa mtindo wa kumpigia debe, binafsi siwaamini hasa baada ya makosa yale ya mwaka 2010.”
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema matokeo ya utafiti huo yanaacha maswali kwani hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu methodolojia na sampuli iliyotumika.
Alisema matokeo ya utafiti huo yanakinzana na ripoti nyingine za mwaka wa 2012 hasa ule wa Economic Intelligence Unit ambao unaonyesha kuwa Chadema kinazidi kupanda.


Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Sam Ruhuza alisema kati ya vinara tisa wa urais waliotajwa, hakuna hata mmoja anayeweza kuwa Rais wa Tanzania na kuongeza kuwa ushahidi wa hilo ni huko kupanda na kushuka kwa umaarufu wao kisiasa.


“Huko kushuka na kupanda, ni ishara kuwa hakuna Rais kati ya hao, haiwezekani mtu anayependwa na kuungwa mkono aporomoke kutoka asilimia 42 mpaka 17 na huu ni mwaka mmoja tu. Ikipita miaka miwili si wengine watabaki na asilimia moja au sifuri?”



RAILA ODINGA AMBWAGA UHURU KINYATTA KURA ZA MAONI

tr" style="text-align: left;" trbidi="on">

Matokeo ya utafiti wa Consumer Insight yanaonyesha kuwa Odinga hivi sasa anaungwa mkono na asilimia 46.8 ya wapigakura dhidi ya mwenzake, Kenyatta aliyepata asilimia 42.9. Mashabiki wa Mudavadi wamepungua kutoka asilimia 5.4 hadi 4.2.

WAGOMBEA urais wanaochuana vikali Kenya, Raila Odinga wa Muungano wa Cord na Uhuru Kenyatta wa Jubilee, wameendelea kukabana koo ikiwa ni siku tano kabla ya Uchaguzi Mkuu Jumatatu ijayo.

Tafiti tatu tofauti zilizodhaminiwa na Nation Media Group (NMG), ambazo matokeo yake yametoka jana, zimeonyesha kuwa wagombea hao wanatofautiana kwa asilimia zisizozidi 1.5, hali inayoonyesha kuwa lolote linaweza kutokea siku ya uchaguzi. Hata hivyo, Odinga ana nafasi zaidi katika uchaguzi wa marudio.

Matokeo yote hayo yamebainisha kuwa hakutakuwa na mshindi wa moja kwa moja, kwa kuwa wote hawatafikisha nusu ya kura zinazohitajika, huku utafiti ukibainisha kuwa katika mzunguko wa pili utakaofanyika ndani ya wiki tatu tangu kufanyika kwa uchaguzi wa awali, Odinga ana nafasi kubwa ya kushinda.

Matokeo ya Pollster Infotrack
Utafiti wa Kampuni ya Pollster Infotrack, unaonyesha kuwa kama uchaguzi ungefanyika leo, Odinga angeongoza kwa asilimia 46, Kenyatta angefuatia akiwa na asilimia 44.6, huku mgombea wa Amani, Musalia Mudavadi akiwafuata kwa mbali baada ya kupata asilimia 4.3.

Kwa mujibu wa matokeo hayo ya kura za mwisho za maoni, wote wawili, Odinga na Kenyatta wameongeza kura kwa asilimia moja kila mmoja, ikilinganishwa na matokeo ya wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa sheria za Kenya, si ruhusa kufanya wala kuchapisha kura za maoni siku tano kabla ya uchaguzi.

Kulingana na matokeo ya Infotrack Poll, Odinga anatazamiwa kushinda matokeo ya mzunguko wa pili kwa asilimia 49.2 huku mwenzake akiwa na asilimia 47.2.

Utafiti huo unaonyesha kuwa nusu ya wapiga kura wa Mudavadi watahamia kwa Odinga wakati Kenyatta atapata wale waliowapigia kura wagombea wengine, Martha Karua wa Narc, James Ole Kiyiapi (Restore and Build Kenya) na Peter Kenneth (Kenya National Social Congress).
Kwa upande wa makundi ya wagombea, Cord inaongoza kwa kuungwa mkono ikiwa na asilimia 45.8 ikifuatiwa na Jubilee (45.6%) na Amani ya Mudavadi ikiwa na asilimia 4.4.

Utafiti wa Consumer Insight
Matokeo ya utafiti wa Consumer Insight yanaonyesha kuwa Odinga hivi sasa anaungwa mkono na asilimia 46.8 ya wapigakura dhidi ya mwenzake, Kenyatta aliyepata asilimia 42.9. Mashabiki wa Mudavadi wamepungua kutoka asilimia 5.4 hadi 4.2.

Kampuni ya Consumer Insight imebaini kuwa iwapo uchaguzi utakwenda hadi marudio, Odinga atatangazwa mshindi kwa kufikisha asilimia 50.6 dhidi ya Kenyatta mwenye asilimia 46.3.
Utafiti huo wa Consumer Insight unaonyesha kuwa umaarufu wa Cord uko asilimia 47.8 wakati ule wa Jubilee ni asilimia 44.1.

Utafiti wa Strategic Pollster
Utafiti wa Strategic Pollster unaonyesha kuwa Odinga ataibuka mshindi kwa kupata asilimia 45.7 dhidi ya Kenyetta mwenye 43.8. Mudavadi bado ni wa tatu akiwa na asilimia 5.7.

Katika uchaguzi wa marudio, Strategic Pollster inasema Odinga ataibuka kidedea kwa asilimia 51.7 huku mwenzake Kenyetta akisimama kwenye asilimia 45.7.
Tafiti hizi zimetumia sampuli ya watu 2,600 wanaowakilisha wananchi 14,337,399 waliojiandikisha kupiga kura.

Wagombea urais walichuana vikali kwa mara ya pili juzi katika mdahalo, ambao ulikuwa fursa ya mwisho kupimwa na wapiga kura kabla ya uchaguzi utakaofanyika Jumatatu ijayo.
Kivuitu afariki dunia
Wakati huohuo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Kenya (ECK), Jaji Samuel Kivuitu amefariki dunia, siku tano kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Kivuitu (74) alifariki dunia saa nne usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya MP Shah ya Nairobi alikokuwa amepelekwa kutokana na mshtuko wa moyo.

Kivuitu anakumbukwa na mambo mawili makubwa na Watanzania. Matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya mwaka 2007 na pia kusoma Tanzania.

Alizua balaa Kenya baada ya kumtangaza katika mazingira ya kutatanisha Mwai Kibaki kama mshindi wa urais mwaka 2007 na kuzua vurugu za kikabila kutokana na mpinzani wake n Raila Odinga kuamini alipokonywa ushindi.

Alikuwa mmoja wa wanafunzi wa kwanza kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1961 na kumaliza mwaka 1965, akiwa katika Kitivo cha Sheria.

Familia ya marehemu Kivuitu imesema mazishi yatasubiri hadi Uchaguzi Mkuu umalizike Machi 4, mwaka huu

TCRA yafungia vituo viwili vya redio nchini

Felix
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano(TRCA)Walter Bugoya akitoa tamko la kuzifungia Redio Imani na Redio Kwa Neema kwa kipindi cha miezi 6 kutokana kutangaza matangazo yanayodaiwa kuwa ya kichochezi jijini Dar es Salaam jana.Kushoto ni Mkurungenzi wa Idara ya Habrio Maelezo Arthur Mwambene na Kaimu Mkurugenzi wav Utangazaji wa (TRCA)Andrew Kisaka.Picha na Fidellis
KAMATI ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa adhabu ya kuvifungia muda wa miezi sita vituo viwili vya redio za dini, Imani na Kwa Neema kwa kile kilichoelezwa ni kuendesha vipindi vya uchochezi.

Vilevile kamati hiyo imetoa adhabu ya faini ya Sh5 milioni kwa Kituo cha redio cha Clouds FM baada ya kubainika pia kukiuka taratibu za utangazaji kwa kurusha hewani kipindi kilichotafsiriwa kuwa ni cha uchochezi.


Kamati hiyo ya maudhui ilitangaza adhabu hizo jana jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari ikisisitiza kuwa lengo lao ni kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinazingatia maadili.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA,Walter Bugoya alisema TCRA imefikia hatua hiyo baada ya kuyafanyia uchunguzi wa kina malalamiko yaliyotolewa na wasikilizaji wa vituo hivyo vya redio.


Bugoya alisema redio hiyo ilitangazia wasikilizaji wake wasishiriki kwenye mkakati huo wa Sensa ya Taifa kwa kile walichodai kulingana na imani ya Kiislamu, wasingejua hatima ya mkakati huo.


Kuhusu Redio Kwa Neema inayorusha matangazo yake kutokea Geita, Bugoya alisema ilieneza uchochezi dhidi ya mtafaruku wa kidini uliozuka mkoani humo juu ya upande gani una haki ya kuchinja wanyama kwa ajili ya kitoweo.


Akizungumzia Kituo cha redio cha Clouds, Buyoga alisema kamati imeitaka kulipa fidia ya Sh5 milioni baada ya kubainika kuwa nacho kilienda kinyume cha maadili ya utangazaji kupitia kipindi chake cha Power Break Fast, cha Jicho la Ng’ombe walitoa kauli za uchochezi.