Thursday, 28 February 2013

PSI: Tumezuia mimba milioni 1.2 zisizotarajiwa



Mtung’e alisema kifurushi hicho kitakuwa na vifaa vyote vitakavyohitajika kwa mjamzito kujifungua salama ambavyo alivitaja baadhi kuwa ni jozi mbili za glovu, nyuzi mbili, pamba, shuka kwa ajili ya matumizi ya mara moja, kitambaa cha joto cha mtoto, dawa ya kusafishia mikono, vidonge vitatu vya kuzuia mama kutokwa na damu nyingi.


SHIRIKA lisilo la kiserikali la PSI limesema kwamba limefanikiwa kuzuia mimba zisizotarajiwa 1.2 milioni mwaka uliopita.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, Mkurugenzi wa Afya ya Uzazi wa shirika hilo, Dk Nguke Mwakatundu alisema hiyo ilitokana na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa mkakati wake wa kutoa huduma za uzazi wa mpango nchini.

“Tumefanikiwa kutokana na kutoa huduma za uzazi zaidi ya matumizi ya kondomu. Ukiangalia tangu shirika lilipoanzishwa miaka 20 iliyopita, matumizi ya kondomu yalikuwa yakitumika zaidi. Lakini sasa njia hiyo imepita na nyingine kama lupu, vipandikizi, vidonge na sindano ambazo matumizi yake yameongezeka maradufu,” alisema.

Alisema katika mwaka wa jana, njia za muda mrefu za uzazi wa mpango zilitolewa kwa watu 102,772 ikilinganishwa na watu 48,518 mwaka uliotangulia ikiwa ni ongezeko la asilimia 92.
Alisema mafanikio hayo yametokana na mkakati wa shirika hilo kupanua wigo wake wa kusambaza huduma za afya katika maeneo ya mbali...

“Tumeongeza utoaji wa huduma katika sekta ya umma kwa asilimia 145. Kitu kikubwa tulichofanya ni kuongeza timu ya watoa huduma katika maeneo hayo kutoka tano hadi 10 na kila timu ina wauguzi wawili.”

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa PSI Tanzania, Romanus Mtung’e alisema katika kuhakikisha kwamba utoaji huo wa huduma unakuwa salama, shirika lake linaandaa Kifurushi Salama kwa ajili ya Kujifungua (Clean Delivery Pack), kitakachoanza kusambazwa Aprili mwaka huu.

Mtung’e alisema kifurushi hicho kitakuwa na vifaa vyote vitakavyohitajika kwa mjamzito kujifungua salama ambavyo alivitaja baadhi kuwa ni jozi mbili za glovu, nyuzi mbili, pamba, shuka kwa ajili ya matumizi ya mara moja, kitambaa cha joto cha mtoto, dawa ya kusafishia mikono, vidonge vitatu vya kuzuia mama kutokwa na damu nyingi.

Alisema lengo la shirika lake siyo kupunguza idadi ya watu kama ambavyo imekuwa ikitafsiriwa na wengi, bali kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili watu wapate watoto kwa mpangilio utakaowawezesha kuwatunza na kuwahudumia vyema na wao kupata fursa ya kushiriki katika masuala ya kiuchumi.

No comments: