Sengerema. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema
kitendo kilichofanywa na uongozi wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba
cha kumfanya Mjumbe wa Bunge hilo, Zakia Meghji kupiga kura kama
Mzanzibar badala ya ‘Mtanzania Bara’ ni ‘uhuni’ unaotakiwa kuchukuliwa
hatua na wananchi.
Hayo yalisemwa juzi na viongozi wa Mabaraza ya
Wanawake na Vijana ya Chadema (Bawacha) na (Bavicha) katika mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi, Segerema mkoani
Mwanza.
Kauli hiyo wameitoa ikiwa ni saa 48 baada ya
gazeti hili kubainisha utata wa kura ya Meghji wakati wa kuipitisha
Katiba inayopendekezwa kupiga kama mjumbe kutoka Zanzibar badala ya
Tanzania bara kama alivyotakiwa.
Akihutubia mamia ya wananchi, Mwenyekiti mstaafu
wa Bavicha, John Heche alisema, “Kilichofanywa na Sitta (Mwenyekiti wa
Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta) cha kumbadilisha dakika za mwisho
Meghji kuhalalisha Katiba yao ni uhuni ambao Watanzania wanatakiwa
kuwawajibisha kupitia kura ya maoni.”
Aliongeza: “Hivi kweli inawezekanaje mtu katika
vikao vyote awe anahesabika kama mjumbe kutoka Tanzania Bara halafu
dakika za majeruhi baada ya kuona wanachokifanya hakitapata theluthi
mbili, hususani Zanzibar wampeleke huko….”?
Huku akishangiliwa na umati huo, Heche alisema
wajumbe wa CCM wameondoa tunu za taifa za uwazi na uadilifu baada ya
kuona zimewabana.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Bawacha, Hawa Mwaifunga
alisema wanawake wakiacha kutumika na CCM. hususani nyakati za chaguzi
zinapokaribia wataifanya nchi hii iliyokosa maendeleo kwa miaka 52 baada
ya uhuru kusonga mbele.
“Wanawake wenzangu nawaombeni mjitokeze kugombea
nafasi mbalimbali lakini pia kujiandikisha katika daftari la wapiga kura
na makazi ili muweze kushiriki kikamilifu katika chaguzi hizo,” alisema
Mwaifunga
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Bawacha, Grace
Tendega alisema,”Nawasihi wanawake wenzangu na vijana wenye sifa kwenda
kujiandikisha ili kuweza kuwa na sifa ya kuchagua na
kuchaguliwa...wanawake msiache kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi kwani tunaweza.”
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha,
Kunti Yusuph alisema nchi hii imefika hapa kutokana na kuwakumbatia
viongozi wasiotimiza wajibu wetu.
“Watanzania leo kupata huduma bora ni anasa,
kuapata huduma za afya, elimu na maji navyo ni anasa hivyo tuchukue
hatua kupitia uchaguzi wa serikaki za mitaa kubadili uongozi,” alisema
Yusuph

No comments:
Post a Comment