Dar es Salaam. Baadhi ya wanafamilia wa
waliopoteza ndugu kwenye shambulio la ugaidi katika Ubalozi wa Marekani
jijini Dar es Salaam mwaka 1998, wameelezea kufarijika kutokana na
malipo ya fidia, licha ya kwamba hayawezi kurejesha uhai wa waliokufa.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti,
ndugu hao walisema, licha ya mahakama nchini Marekani kuwapa fidia
lakini pengo la jamaa zao halitazibika.
Wiki iliyopita, Mahakama Kuu ya Marekani, ilitoa
amri ya kuwalipa fidia ya dola za Marekani 957 milioni (Sh1.555
trilioni) waathirika 23 wa shambulio hilo.
Jaji Thomas Bates katika hukumu yake alisema kati
ya fedha hizo, Dola za Marekani 420 milioni (Sh670 bilioni) watapewa
ndugu wa marehemu watano na waathirika wanne wa Tanzania wakati kitita
kilichobaki kitakwenda kwa waathirika ambao ni Wamarekani.
Jaji Bates alisema Serikali za Iran na Sudan
zitawajibika kulipa fidia hizo kutokana na kuhusika na mashambulio hayo
mabaya kuwahi kutokea Afrika Mashariki.
Mmoja wa jamaa waliopoteza maisha katika tukio
hilo, Kulwa Ramadhan alisema anasubiri kuletewa taarifa zaidi kuhusu
taratibu za kupata fidia hiyo.
“Huwezi kuwa umeridhika na fidia kwa kuwa
tumepoteza ndugu zetu lakini pia hata hicho kilichopatikana
hatukukitarajia kupata,” alisema Ramadhan.
Alisema kuna baadhi ya jamaa wa marehemu watano
hawakuingizwa kwenye idadi ya watakaopata fidia kutokana na kuchelewa
kujiandikisha katika kesi hiyo.
“Baada ya tukio uongozi wa Ubalozi wa Marekani
ulituambia tutoe taarifa zetu zote za mawasiliano na kwamba
tusibadilishe namba za simu kwa ajili ya kuwasiliana kinachojiri.
“Lakini kuna baadhi ya jamaa walibadilisha namba
zao na kufanya mawasiliano kuwa magumu hivyo kushindwa kuingizwa katika
idadi ya wadai katika kesi hiyo,” alisema.
Ramadhan aliyempoteza pacha wake, Dotto Ramadhani
alisema baadhi ya jamaa walijitokeza baadaye baada ya hatua muhimu za
kesi kufanyika kitendo ambacho kiliwazuia kushiriki katika kesi.
Waathirika wengine
Naye Judith Mwila aliyempoteza mume wake kwenye tukio hilo,
alisema anashukuru Ubalozi wa Marekani pamoja na mawakili waliowasaidia
kufanikisha kesi hiyo.
“Binafsi nimepata taarifa kamili jana (juzi)
kutoka kwenye gazeti la Mwananchi na sikutarajia kama tungeshinda kesi
hiyo na tukapewa fidia ya fedha kiasi hicho. Hata hivyo tunaendelea
kusubiri taarifa za mawakili wetu kuhusu taratibu zinazofuata kupata
fedha hizo,” alisema.
Aliongeza kuwa iwapo atapata sehemu ya fedha hizo
atashauriana na watoto wake jambo la kufanya ikiwamo kufanya biashara
kubwa. Mwila ana watoto watatu alioachiwa na marehemu mume wake.
Alisema kuwa tangu mchakato wa kesi ulipoanza
mwanzoni mwa mwaka 2001, Ubalozi wa Marekani na mawakili wao,
walimpeleka Marekani mara mbili.
“Kesi hii imedumu muda mrefu. Mara ya kwanza
nilikwenda 2001 kutoa ushahidi na mara ya mwisho ni 2010 na tangu wakati
huo tulikuwa tukipewa tu taarifa juu ya maendeleo ya kesi,” alisema
Mwila.
Kwa upande wake, Grace Paulo ambaye alifiwa na
mumewe Elisha Paulo alisema: “Ninamshukuru Mungu kwa sisi kushinda kesi
hii na hivyo tunasubiri mawasiliano na wahusika kufahamu jinsi ya kupata
fedha hizo.
“Tumekuwa tukiishi kwa shida sana, hivyo hizo
fedha zitatusaidia kujikwamua na matatizo yanayonikabili na mwanangu,”
alisema Paulo ambaye aliachiwa mtoto mmoja aitwaye Mary Paulo.
Kwa mujibu wa waathirika hao, Serikali ya Marekani
kupitia Shirika la Misaada la Marekani (Usaid) liliwapa msaada wa
kuwasomesha watoto pamoja na makazi ili kupunguza makali ya maisha.
Hata hivyo, wengi wao wanaendelea kufanya biashara
ndogondogo kutokana na misaada hiyo kuwekwa katika eneo maalumu la ada
za watoto.
“Kwa sasa ninafanya biashara ya kuuza nguo za
mitumba na nilishaondoka Dar es Salaam mara tu baada ya msiba mwaka 1998
kutokana na maisha ya mjini kuwa magumu.
“Baadaye Ubalozi kupitia taasisi za kiraia
walinitafuta hadi wilayani Mpwapwa ndipo waliponijengea nyumba
ninayoishi sasa,” aliongeza Paulo anayeishi mkoani Dodoma.
Jamaa hao pia walisema kuwa gharama halisi za kesi
hiyo hawazifahamu kutokana na kesi nzima kusimamiwa na Serikali ya
Marekani na mawakili wao.
Hata hivyo, uhakika wa kupata fedha hizo unabaki mikononi mwa
wakili wa jamaa hao, Thomas Fortune Fay ambaye baada ya hukumu hiyo
alisema anafuatilia jinsi ya kupata fedha kwa Serikali za Sudan na Iran.
Alisema ataangalia jinsi ya kutaifisha baadhi ya mali za nchi hizo ili kupata fedha za kuwalipa waathirika hao.

No comments:
Post a Comment