Thursday, 13 March 2014

Mbatia: Katiba itapatikana kwa maridhiano

Dodoma. Jina la mwanasiasa James  Mbatia si geni sana miongoni mwa Watanzania na amejizolea sifa ya kutanguliza masilahi ya taifa tangu mchakato wa kupata Katiba Mpya ulivyoanza.
Mbatia, ambaye alishiriki katika harakati za kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi miaka ya 1990,  mara nyingi amejitokeza kusaka mwafaka pale inapotokea sintofahamu kwenye vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Busara aliyoitumia wakati wa upitishaji wa muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, ndiyo aliyoirudia katika Bunge Maalumu la Katiba.
“Dalili za kutopatikana kwa Katiba Mpya zimeanza kuonekana, ni vizuri ikatumika busara na hekima katika kuvuka kikwazo hiki na njia pekee ni maridhiano,” alisema Mbatia, Septemba,  mwaka jana.
Mbatia aliyotoa maneno hayo baada ya wabunge wote kutoka kambi ya upinzani isipokuwa Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema wa TLP kususia upitishaji wa muswada kupinga ubabe wa CCM.
“Sisi siyo tutakaoifanya Tanzania isitawalike bali CCM. Tunafanya haya kwa nia njema kabisa hatutaki damu ya Watanzania imwagike kwa jambo linaloepukika,” alisema Mbatia katika kipindi hicho.
Katika kipindi hiki cha Bunge la Katiba,  busara hiyo ndiyo imetumika ili kusawazisha mambo wakati yalipokuwa yanakwenda vibaya kwenye semina ya kujadili Rasimu ya Kanuni.
Bunge hilo lilikuwa katika hati hati ya kuvunjika katika siku za awali tu za utungaji wa Katiba pale lilipojikuta likiwa njia panda kuhusu kuamua aina ya kura itumike kuamua vifungu vya Rasimu.
Kwanini Mbatia anaamini falsafa ya Katiba ni tendo la maridhiano?
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Mbatia anasema Katiba siku zote ni tendo la maridhiano na kutoa mfano wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.
 “Mwezi Aprili  22, mwaka 1964, Rais Nyerere (Julius) alikaa na Rais Karume (Abeid) wa Zanzibar wakakubaliana kuwa nchi hizi ziungane, hili lilikuwa tendo la maridhiano,” anasema Mbatia.
“Kwa hiyo Aprili 24, mwaka 1964 Bunge la Tanganyika lilikaa na kutunga sheria ya maridhiano hayo na baadaye Aprili 26, mwaka huo, Muungano ukazaa nchi inayoitwa Tanzania,” anasema Mbatia.
Kwa msingi huo, Mbatia ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, anasema siku zote maridhiano yanaanza kwanza na watu wakishaafikiana ndio wanayatungia sheria.
“Tuna mfano mwingine wa kujifunza kule Zanzibar,  Seif Shariff Hamad (Katibu Mkuu CUF) na Rais Amani Karume walijifungia Ikulu Novemba mwaka 2009 na wakafanya tendo la maridhiano,” anasema.
“Walikaa wao wawili tu wakaridhiana kuwa watafute mwafaka na baada ya kuridhiana Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, likaitwa na kufanya mabadiliko ya 10 ya Katiba ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa,”anasema Mbatia.
Mbatia anasema maridhiano hayo ndiyo yaliyowafanya Watanzania na watu wengi duniani washuhudie Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2010 ukifanyika  bila tone la damu ya Mzanzibari kumwagika.
“Tume ya Jaji Warioba (Joseph) imekusanya maoni ya Wanzania na kupendekeza muundo wa Serikali tatu kuwa ndiyo chaguo la Watanzania lakini leo CCM wanatilia shaka uadilifu wa Jaji Warioba.
“Nawashauri rafiki zangu wa CCM wasianze kuhoji leo uadilifu wa Jaji Warioba. Yeye na mzee Butiku (Joseph) ni wafuasi wa karibu sana wa Nyerere lakini wameheshimu maoni ya Watanzania,” anaonya Mbatia.
Mbatia anasema ni vizuri wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wakaiboresha Rasimu ya Katiba na kwamba kama kuna hoja mpya za kujenga ziingizwe lakini si kwa vitisho na ubabe.
“Kulazimisha mambo yenye mwelekeo wa kupatikana kwa Katiba yenye masilahi mapana ya CCM, litakuwa jambo la kutowatendea haki Watanzania na hicho kitakuwa ndiyo chanzo cha machafuko,” anaeleza Mbatia.
Mbatia anasema ni katika msingi huo huo wa kutaka Tanzania isiingie kwenye machafuko, ndiyo maana alipendekeza kuundwa kwa Kamati ya Maridhiano baada ya kujitokeza kwa dalili mbaya.
“Tulikuwa tumekwama katika njiapanda…CCM wameng’ang’ania kura ya wazi wakati wanajua si matakwa ya kidemokrasia, sasa mimi nikaona hapana hebu turudi kwenye maridhiano,” anasema Mbatia.
Mbatia anasema kwa moyo huo huo wa maridhiano alioupendekeza, ndio ulisaidia kupatikana kwa mwafaka juu ya kanuni ya 37 na 38 ya Bunge Maalumu la Katiba na kuongeza;
“Bila kuundwa kwa kamati ya maridhiano nina hakika Bunge hili lingekuwa limeshasambaratika lakini bado ‘spirit’ (moyo) ipo na hali hii ndiyo tunataka iendelee kwa sababu bado tuna shughuli pevu.
Mbatia anasema kutaibuka mvutano katika vifungu hivyo pale watakapofikia hatua ya kupitisha ibara za Katiba na kuwataka CCM wasome alama za nyakati na kutazama matakwa ya Watanzania.
“CCM waelewe kuwa Watanzania wanatutazama, leo wanapolazimisha kura ya wazi kupitisha Katiba halafu tukienda kwenye kura ya maoni Katiba hiyo hiyo ipigiwe kura ya siri, hakuna atakayewaelewa.”
Mbatia aliongeza kusema; ”Hakuna ubishi kuwa mabadiliko ya 10 ya Zanzibar yalikiuka Katiba ya Muungano na Watanzania wanalifahamu hilo lakini hoja ya msingi hapa ni maridhiano.”
Mabadiliko hayo ndio yaliyotamka kuwa Zanzibar ni nchi yenye mipaka yake, ina Katiba yake, ina bendera yake na ina wimbo wake wa Taifa, kitendo kinachotafsiriwa kuwa ni uhaini kwa mujibu wa Katiba ya Muungano.
Mbatia ni nani hasa?
Mbatia ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuteuliwa na Rais,  Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi na amesoma fani ya uhandisi wa majengo.

No comments: