Jumanne iliyopita tulichapisha habari
kuhusu ujio wa mwandishi wa Gazeti la Daily Mail la Uingereza, Martin
Fletcher, ambaye aliandika habari katika toleo la gazeti hilo la
Februari 9, mwaka huu kwamba Serikali ya Tanzania imeshindwa kukomesha
mauaji ya tembo na faru ambao wako katika hatari ya kutoweka,
akiwatuhumu baadhi ya maofisa wa Serikali na jamaa wa Rais kuwa sehemu
ya mtandao mkubwa wa ujangili.
Ujio huo umewashangaza wengi, kwani pamoja na
Serikali kukanusha kumwalika, mwandishi huyo amesema ziara yake nchini
imetokana na mwaliko wa Serikali. Hata hivyo, sisi hatuoni kama kualikwa
ama kutoalikwa na Serikali ni jambo linalostahili kujadiliwa kwa kuwa
sera ya uhariri ya magazeti yenye hadhi kama Daily Mail inawaelekeza na
kuwasisitizia waandishi kufuata maadili ya taaluma yao, ambayo ni
kuandika ukweli hata kama ukweli huo utawauma watu waliowafadhili ama
kuwawezesha kupata habari.
Hivyo, hatutazamii mwandishi Fletcher apindishe
habari au aandike habari za kuifurahisha Serikali kwa sababu tu ya
kufadhiliwa na kuruhusiwa kuingia katika sehemu nyeti ambazo hata
waandishi wazawa na wazalendo wa hapa nchini hawaruhusiwi. Kwa
kuzingatia utamaduni, maadili na weledi wa waandishi hao, utakuwa
muujiza kama mwandishi huyo atakubali ‘kununuliwa’ au kufadhiliwa na
Serikali ili taarifa atakazotoa baada ya ziara yake nchini ziisafishe
kutokana na taarifa za awali kwamba haifanyi juhudi za kutosha kuwalinda
wanyamapori.
Imeripotiwa kuwa mwandishi huyo pamoja na
mpigapicha wake wamepewa mapokezi mazuri nchini na kuingizwa katika
maeneo nyeti kama ghala za kuhifadhia shehena za meno ya tembo
yanayokamatwa, huku wakiwaacha maofisa katika Wizara ya Maliasili na
Utalii wakiwa vinywa wazi. Pia waliruhusiwa kupiga picha kinyume na
utaratibu na baadaye wakapelekwa Hifadhi ya Selous kwa ndege ya Idara ya
Wanyamapori.
Wizara ya Maliasili na Utalii imekiri kuwa ziara
ya mwandishi huyo imetokana na uamuzi wake wa kuweka uwazi suala hilo na
kwamba waandishi wengine wa BBC na CNN wameomba kufanya ziara kama
hiyo.
Ni wazi kuwa uamuzi huo ni jitihada za kujikwamua
na lawama za serikali kushindwa kukomesha vitendo vya ujangili na ndio
maana Rais Kikwete alikwenda katika vituo vya utangazaji vya BBC na CNN,
wakati waziri husika alikutana na wahariri wa magazeti ya Daily Mail na
Mail on Sunday kufafannua suala hilo.
Tumezungumzia ziara ya wageni hao kwa kirefu ili
kuonyesha jinsi Serikali inavyowatetemekea waandishi wa nje na kuwapuuza
wa ndani, kiasi cha kutotaka kwa makusudi kutoa habari kwa waandishi
wa ndani au kukutana nao kuzungumzia masuala muhimu ya nchi.
Tulitarajia viongozi wa juu wa serikali
wangekutana na vyombo vya habari vya ndani na kutoa ufafanuzi wa kina wa
suala hilo ili wananchi wapate picha halisi ya nini kilitokea kabla ya
kwenda nalo kwa waandishi wa nje.
Lakini juhudi kubwa ilielekezwa katika kutoa
ufafanuzi na ushirikiano kwa vyombo vya habari vya nje, akiwemo
mwandishi huyo wa Uingereza. Vyombo vya habari vya ndani vitasaidia
serikali pale tu itakapoamua kuwa ya uwazi na kutoa ushirikiano kwa
waandishi hasa katika masuala muhimu na nyeti yanayohusu mustakabali wa
taifa hili. Serikali inajidhalilisha kwa kudhani inawajibika kwa nchi
zinazotoa misaada badala ya wapigakura waliowapa uhalali wa kukaa
madarakani.

No comments:
Post a Comment