Baada ya wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU),
kutumia mabilioni ya fedha za walipakodi wa nchi zao kufanya kampeni
ulimwengu mzima kwa lengo la kuwanusuru Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na
makamu wake, William Ruto wasishtakiwe katika Mahakama ya Uhalifu (ICC),
hatua ya Baraza la Usalama kulikataa Azimio hilo wiki iliyopita bila
shaka itakuwa imeufedhehesha na kuufadhaisha Umoja huo mbele ya jumuiya
ya kimataifa.
Rais Kenyatta, Ruto na mtangazaji Joshua arap Sang
walifunguliwa mashtaka ICC kwa kuhusishwa na vurugu zilizotokea Kenya
baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2007, ambapo zaidi ya watu 1,500 walipoteza
maisha, huku maelfu wakiachwa bila makazi. Katika hatua ya kushangaza,
viongozi hao wa AU waliamua kuinunua kesi hiyo kwa kutishia kwamba
wangezitoa nchi zao katika Mkataba wa Roma ulioanzisha ICC iwapo
mashtaka hayo yasingefutwa.
Baada ya mkakati huo kukwama walikuja na kitu
kipya. Kwamba ICC imekuwa na sera za kibaguzi dhidi ya viongozi weusi
barani Afrika na kusema ndiyo maana inawalenga viongozi hao pekee. Lengo
lilikuwa kuwachochea raia wa nchi zao barani Afrika waione ICC kama
chombo cha kikoloni na chenye ubaguzi dhidi yao na viongozi wao, hivyo
wazishinikize serikali zao kujitoa uanachama wa Mahakama hiyo. Viongozi
hao walitegemea raia wa nchi zao wafanye maandamano na kuilaani ICC na
mataifa yote yanayoiunga mkono.
Kinyume chake, vyombo vya habari na asasi za
kiraia barani humo viliwaelimisha na kuwahamasisha wananchi ili watambue
njama za viongozi wa nchi zao zenye lengo la kuitenga ICC ili
kuendeleza ubabe na utawala wa mabavu, ukandamizaji, uvunjaji wa haki za
binadamu na mauaji ya raia wasio na hatia.
Hata hivyo, hata baada ya njama hizo kugundulika,
viongozi hao kupitia AU walibadili mbinu na kuitaka ICC ihamishie kesi
hiyo barani Afrika, hasa nchini Kenya au Tanzania kwa maelezo kwamba
Afrika ina uwezo wa kujiamulia mambo yake yenyewe. Mbinu hiyo pia
ilishindwa, kwani ICC iligundua kwamba Afrika haina mfumo wa kimahakama
ulio imara wa kuwawajibisha viongozi wa nchi wanaokiuka haki za
binadamu.
Pamoja na AU kuwachochea washtakiwa wasihudhurie
kesi zao ICC, wao walisema watahudhuria, pengine kwa kutambua athari na
madhara ya kutokufanya hivyo. Ruto tayari amehudhuria kesi yake na Rais
Kenyatta atafanya hivyo Februari 2014. Hapo ndipo AU ilipolazimika
kutupa karata ya mwisho kwa kuandaa Azimio na kuliwasilisha katika
Baraza la Usalama la UN, ikitaka kesi za kina Kenyatta ziahirishwe kwa
mwaka mmoja ili viongozi hao wakabiliane na tishio la usalama nchini
Kenya kutokana na tukio la kigaidi lililotokea jijini Nairobi hivi
karibuni.
Hata hivyo, mbinu hiyo pia imeshindwa, baada ya
Baraza la Usalama kulikataa Azimio hilo wiki iliyopita. Ni aibu iliyoje
kwa viongozi wa Afrika kuwakingia kifua watawala wenzao, pasipo kujali
waathirika wa ghasia za mwaka 2007, ambao wamesubiri kwa muda mrefu
kupata haki zao pasipo mafanikio. Sisi tunasema uamuzi wa Baraza la
Usalama ni ushindi kwa wana wa Afrika, wakiwamo wananchi wa Kenya ambao
theluthi mbili walisema kupitia kura ya maoni wiki iliyopita kwamba kesi
dhidi ya Rais Kenyatta na wenzake ziendelee kusikilizwa ICC.

No comments:
Post a Comment