Wednesday, 6 November 2013

Nini kimemsibu Pinda kwenye uwaziri mkuu?

 
Dar es Salaam. Mwaka 2007 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu na nafasi yake, Mizengo Pinda aliyeshika nafasi yake alitarajiwa kuja na moto mkali zaidi.
Itakumbukwa kuwa Lowassa aliyeangushwa na kashfa ya mradi tata wa umeme wa Richmond, alishaanza kuonyesha machachari yake hasa katika suala la elimu ambapo alihamasisha ujenzi wa shule za sekondari za kata na miradi mingine.
Pinda aliingia akiwa amevaa ngozi ya kondoo, huku akijiita mtoto wa mkulima. Leo ni miaka sita imepita, tunamwona Pinda halisi alivyo. Kuna kila dalili kwamba amepwaya katika nafasi hiyo.
Tofauti na walivyokuwa mawaziri wakuu wengine, Pinda hajaonyesha ubunifu katika mambo na kuyasimamia. Badala yake amekuwa mtu wa kuonekana wakati wa matukio.
Kukitokea vurugu, wananchi wa Mtwara wameandamana, Waziri Mkuu Pinda anakwenda kutuliza, madaktari wamegoma, anakwenda kuzungumza nao, wenye malori na mabasi wamegoma, anakwenda kuwabembeleza.
Huu ni udhaifu, haiwezekani kiongozi ashughulikie matukio tu wakati anaweza kuboresha utendaji ili mambo yasiharibike.  Kutokana na udhaifu huo, hata mawaziri walio chini yake hawawajibiki ipasavyo. Ndiyo maana hivi karibuni, Wabunge wanaoendelea na kikao mjini Dodoma walimtaja kuwa mmoja kati ya mawaziri wanaopaswa kuwajibika kutokana na kushindwa kusimamia kazi zao.
Wabunge hao waliomba kujadili kwa dharura utekelezaji wa Operesheni Kimbunga na Operesheni Tokomeza, huku wengi wakiwataja wazi mawaziri kadhaa akiwemo yeye Pinda, Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), David Mathayo David (Mifugo na Uvuvi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).
Pinda analalamikiwa kwa kauli yake aliyoitoa bungeni katika mkutano uliopita akivitaka vyombo vya usalama kuwapiga wananchi wanaokiuka sheria.
Kutokana na usimamizi hafifu na kauli zake, kumekuwa na mauaji ya wananchi wasio na hatia kwenye operesheni ya ujangili wa meno ya tembo, kumekuwa na migogoro ya wakulima na wafugaji isiyokwisha, hali ya elimu imekuwa mbaya na mengineyo. Inawezekana nafasi ya uwaziri mkuu inakosa nguvu kwa sababu, Katiba inampa nafasi rais kama mtendaji.
Baadhi ya nchi hasa za kifalme, Waziri Mkuu ndiyo mwenye mamlaka ya mwisho, nyingine hazina cheo cha Waziri Mkuu, badala yake anakuwepo tu makamu wa rais.  Hiyo yote ni kuondoa migongano ya madaraka kwa sababu huwezi kuwa na rais mtendaji na waziri mkuu mtendaji kwa wakati mmoja, ni lazima mmoja atakuwa mtumwa wa mwenzake.
Hata hivyo, bado Pinda angeweza kutumia mamlaka aliyonayo kujijengea heshima kwa Taifa kiutendaji kama walivyofanya mawaziri wakuu wengine.

No comments: