Hivi karibuni Serikali ilizindua mpango ujulikanao kwa jina la
‘’Matokeo Makubwa Sasa’’, uliohusu sekta mbalimbali zenye changamoto
zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.
Sekta zilizoainishwa chini ya mpango huo ni elimu, miundombinu, madini na nishati, uchumi na fedha pamoja na sekta ya maji.
Katika sekta ya elimu, wataalamu kutoka ndani na
nje ya vyombo vya Serikali vinavyoshughulikia elimu, walikutana na
kuandaa mikakati tisa ya kunusuru sekta ya elimu nchini, hasa elimu ya
msingi na ile ya sekondari.
Pamoja na mambo mengine, mikakati hiyo inalenga
kwa kiwango kikubwa kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa ngazi
hizo muhimu katika mfumo wa elimu nchini.
Makala haya yanadurusu kwa kina maelezo ya
mwongozo wa namna mikakati hiyo itakavyotekelezwa ndani ya kipindi cha
miaka mitatu ya mpango.
Ujenzi wa miundombinu muhimu shuleni
Shughuli za ujenzi zilizobainishwa kutekelezwa
katika mpango huu ni pamoja na ujenzi, ukarabati na ukamilishaji
majengo kama madarasa, maabara, vyoo, utoaji wa maji safi na kuweka
umeme kupitia gridi ya Taifa au umeme wa mwanga wa jua.
Serikali imepanga kuwezesha utekelezaji wa haraka
wa mradi wa awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari
(MMES II) katika ujenzi wa miundombinu ya msingi kwa shule 1,200 ifikapo
mwaka 2014.
Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa shule hizi
katika awamu tatu: awamu ya kwanza itakamilika Septemba 2013 ambapo
shule za sekondari 264 zitajengwa.
Awamu ya pili itakamilika Machi 2014 ambapo shule
za sekondari 528 zitahusika na awamu ya tatu itakamilika Septemba 2014
ambapo shule za sekondari 408 zitajengwa au kukarabatiwa.
Mgawanyo wa shule kimkoa katika awamu kwanza
unahusisha Arusha (14), Dodoma (12), Dar es Salaam (6), Geita (6),
Iringa (8), Kagera (14), Katavi (4), Kigoma (8), Kilimanjaro (14), Lindi
(12), Manyara (12), Mara (12) Mbeya (16), Morogoro (12), Mtwara(12),
Mwanza (11), Njombe (8), Pwani (14), Rukwa (6) Ruvuma (10), Shinyanga
(8), Simiyu (7), Singida (8), Tabora (12) na Tanga (18).
Ruzuku ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia:
Katika kutekeleza mpango, Serikali inatoa ruzuku ya vifaa vya
kufundishia na kujifunzia kwa kuzipa shule uwezo wa kununua vitabu na
vifaa vingine na kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa shule.
Kiwango cha ruzuku kilicholengwa kwa mwaka ni Sh
25,000 kwa kila mwanafunzi wa elimu ya sekondari na shilingi 10,000 kwa
mwanafunzi wa elimu ya msingi.
Aidha, Serikali imepanga kuinua ufaulu katika
shule kwa kuboresha upatikanaji wa vitabu vya kiada na vifaa vya
kufundishia na kujifunzia shuleni, na kuhakikisha vifaa vya kufundishia
na kujifunzia vinafika shuleni na kutumika.
Upangaji wa shule kuzingatia matokeo
Serikali imeanza kuzipanga shule kitaifa kwa
kuzingatia matokeo, kwa lengo la kuongeza uwajibikaji na ushiriki wa
jamii katika usimamizi wa utoaji wa elimu bora. Uwajibikaji ni kati ya
changamoto kubwa zinazoukabili mfumo wa elimu kwa sasa.
Shule zitapangwa kwa ubora wa matokeo katika
mitihani na kisha kutangazwa kwa umma, ili iwe chachu ya kuandaa jamii
kuwajibika na kuleta uelewa mpana.
Faida za upangaji wa shule ni pamoja na kuziamsha
shule kufanya vizuri, itasaidia shule kujitathmini, itawahamasisha
walimu na wanafunzi kufanya kazi kwa bidii na kuzitambua shule
zilizofanya vizuri zaidi.
Shule zitakazofanya vibaya zitafuatiliwa na kupewa
msaada kulingana na upungufu uliojitokeza. Shule zitakazoonyesha
maendeleo chanya kwa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka uliopita
zitapewa tuzo.
Utaratibu wa kutoa tuzo kwa shule utatoa motisha
kwa shule kuongeza bidii na kutoa matokeo bora zaidi. Tuzo hii itaanzia
katika matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na sekondari.
Aidha, tuzo za fedha taslimu na nyinginezo
zitatolewa katika makundi mawili ya shule, ambayo ni shule
zilizoonyesha maendeleo ya juu na shule zilizofanya vizuri. Nafasi za
ushindi zitagawanywa katika mikoa yote ili kupata msambao wa utoaji wa
tuzo hizo.
Pia shule zitapanga utaratibu wa kugawana tuzo kwa
uwazi na ushirikishwaji. Tuzo zitakazotolewa kuanzia mwaka huu
zitajumuisha fedha, vyeti, vifaa mbalimbali, ngao na vikombe.
Motisha kwa walimu
Katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji, Serikali imeandaa
mkakati wa kuwatambua walimu wanaofanya kazi vizuri kwa kuwapa tuzo,
kuhakikisha madeni yote ya walimu yanalipwa kwa wakati na kuandaa mpango
wa motisha kwa walimu wanaofanya kazi katika maeneo yenye mazingira
magumu.
Motisha kwa walimu ni muhimu kwa kuwa kazi ya
ualimu ni kazi yenye jukumu la kumwandaa Mtanzania atakayesheheni
maarifa, ujuzi na stadi za kukabiliana na changamoto za kimaendeleo.
Aidha, walimu wanakabiliwa na changamoto nyingi
ikiwemo madai mbalimbali kutoshughulikiwa kwa , hali inayosababisha
walimu wengi kukata tamaa.
Katika kutekeleza mkakati huu wa motisha kwa
walimu, kuanzia Julai 2011 hadi sasa Serikali imelipa madai ya
malimbikizo ya mishahara ya walimu 31,779 yenye thamani ya Sh 28.5
bilioni, ambapo Sh 28,544,743,604.06 zimelipwa kupitia mishahara ya
watumishi husika.
Pia kutoka Januari 2012 hadi Juni, 2013, Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imelipa madai yasiyo ya mishahara ya
walimu 2,825 yenye jumla ya Sh.2.6 bilioni kati ya shilingi 3.3 bilioni
ya fedha kutoka Hazina. Lakini pia Serikali kwa sasa inaendelea na
majadiliano na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kuhusu kuboresha zaidi
maslahi ya walimu.
Kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi
Programu ya kujenga uwezo wa walimu na wanafunzi
katika ujifunzaji na ufundishaji imeanzishwa ili kutatua changamoto ya
msongamano wa wanafunzi darasani ambao husababisha wanafunzi wenye
kuhitaji msaada katika ujifunzaji kushindwa kusaidiwa.
Pia kuna changamoto ya baadhi ya walimu kutokuwa
na nyenzo muhimu za kufundisha kwa ufanisi, kama vile kushindwa kuandaa
maandalio ya somo na kutokuwepo kwa utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi
katika maeneo yenye changamoto za uelewa kwa baadhi ya shule.
Katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza
katika ufundishaji na ujifunzaji, Serikali itaendesha mitihani ya
majaribio kwa ajili ya kuwabaini wanafunzi wenye mahitaji ya ziada
katika kujifunza, kutoa mafunzo kwa walimu kwa ajili ya utekelezaji na
kutoa mafunzo rekebishi kwa wanafunzi kwa kuzingatia maeneo yenye
changamoto za kuelewa.
Programu hii inawalenga walimu wa masomo ya
Bayolojia, Hisabati, Kiswahili na Kiingereza katika ngazi ya sekondari
na walimu Hisabati, Kiswahili na Kiingereza kutoka shule za msingi.
Walengwa wengine ni wanafunzi wa darasa la saba na kidato cha nne
kuanzia mwaka 2013 hadi 2015.
No comments:
Post a Comment